About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Thursday, September 22, 2011

Maskini mtoto IVVO PONERA anavyoteseka baada ya kuungua moto shambani baada ya kibanda alimukuwepo kuungua moto


 
 Mtoto IVVO PONERA mwenye umri wa mwaka mmoja akiwa amelazwa katika Hospital ya mkoa wa Songea baada ya kufikishwa Hospital hapo akitokea kijijini kwao Mchomolo Wilayani Namtumbo,

Mama wa mtoto huyo Paulina Lwambo akizungumza na mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ katika hospital hiyo alisema kuwa IVVO alikuwa analelewa kwenye kibanda shambani na kaka yake aitwaye Jackson Ponera wakati yeye anaendelea na shughuli za kuvuna mahindi

Alisema kuwa katika kibanda hicho alikuwa amepika chakula ili waweze kujipatia mlo baada ya kumaliza kuvuna,ghafla akasikia mwanaye Jackson anamwita huku akisema kibanda kinaungua moto

"Niliacha kuvuna na kukimbilia kwenye kibanda na kukuta kibanda kinaungua na mtoto IVVO yupo ndani,nilichanganyikiwa lakini nilifanikiwa kumuokoa akiwa ameharibika mwili wake kwa kuungua"alisema Lwambo

Alieleza zaidi kuwa nilimchukua kwa umakini mkubwa na kumleta hapa Hospital kwa ajili ya matibabu na anaendelea vizuri na matibabu

MTOTO AZALIWA NA UVIMBE KICHWANI,WENGI WANASEMA HUENDA ANA VICHWA VIWILI

Na Stephano Mango ,Songea

Martina Nombo (27) mkazi wa kijiji cha Lulambo Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma amejifungua Mtoto wa kike ambaye anadaiwa kuwa na vichwa viwili ameomba msaada kwa watu wenye uwezo wamsaidie wakiwemo wataalam wa upasuaji wa Kichwa wamsaidie kuhokoa maisha ya Mwanaye.

Akizungumza na mtandao huu wa www.stephanomango.blogspot.com  katika wodi namba tano  ambapo amelazwa na Mwanaye huyo hospitali ya Mkoa wa Ruvuma jana mara baada ya  kupata rufaa kutoka hospitali ya  Mbuyula iliyopo Wilaya ya Mbinga

 Mama wa Mtoto huyo amesema, alijifungua salama  kwa njia ya kawaida mapema  9 juni mwaka huu katika hospitali ya Mbuyula ambapo mara baada ya kukabidhiwa mwanaye na wauguzi aligundua kuwepo kwa tatizo hilo na aliwaarifu nao walimweleza kuwa aendelee kuwa na subira.

Amesema, tangu alipojifungua katika hospitali ya Mbuyula kichwa cha mtoto waki kilizidi kukua na kutengeneza kitu kama uvimbe ambapo mtoto  aliendelea kutibiwa hospitalini hapo hadi madaktari walipompatia rufaa ya kumwamishia  katika hospitali ya mkoa jana  kwa ajili ya matibabu zaidi.

Kwa upande Daktari Bingwa wa upasuaji wa hospitali hiyo Hassan Lumbe amesema, picha ya  X-ray imeonyesha kuwa ndani ya kichwa kuna shimo ambalo linasababisha ubongo utoke na kuingia kwenye  uvimbe ,pia mifupa ya kichwa aijajiunga vizuri.

Amesema,upasuaji wa mtoto huyo katika hospitali hiyo hauwezi kufanyika  kutokana na kutokuwa na vifaa  na utaalamu walionao hawakidhi viwango vya kutoa tiba kwa mtoto huyo hivyo wanamrufaa kwenda muhimbili .

Amesema,kesi kama hizo ni chache kuripotiwa katika Hospital hiyo na kwamba wao walimpokea  baada ya kupewa rufaa toka katika hospitali aliyozaliwa ya  Mbinga  nao wanatarajia kumpatia rufaa kwenda hospitali ya taifa ya  Mhubili kwani wamefanya vipimo na vimeonyesha kuwa opelesheni hiyo haiwezi kufanywa hapo na wanachofanya ni kuandaa rufaa pamoja na fedha kidogo ya kumsaidia kumsafirisha Mama huyo na Mwanaye.

Mwisho.



WATATU WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUITAPELI BENKI YA NMB

Na Gideon Mwakanosya, Songea
WATU watatu wamefikishwa Mahakamani  kwa kosa la kula njama na kutenda kosa la jinai  la kufanya udanganyifu  na kujipatia mkopo wa fedha toka  katika Benki ya NMB tawi la Songea Mkoani Ruvuma .

Wakisomewa shitaka hilo jana na  Hakimu mkazi Mfawidhi Mwandamizi Baptisti Mhelela amesema,washitakiwa  wote kwa pamoja walitenda  kosa hilo  kati ya oktoba 22 mwaka 2008 na desemba  5 mwaka 2010 .

Amesema,katika kosa la pili mshitakiwa namba moja Cosmas Haule (35) anashitakiwa peke yake kwa kujipatia mkopo wa fedha   shilingi milioni arobaini kwa udanganyifu  kati ya kipindi hicho hicho cha oktoba 22 mwaka 2008 na 5 desemba 2010 na aliposomewa kosa alikana.

Amesema,mshitakiwa Cosmas yupo nje kwa dhamana  na  ametoa hati ya nyumba na dhamana ya mali isiyo hamishika yenye thamani ya shilingi milioni kumi pamoja na dhamana ya milioni 15  kesi hiyo inatarajiwa kutajwa septemba 30 mwaka huu,upelelezi bado haujakamilika.

Katika kosa la tatu,Mshitakiwa namba tatu Asha Banda (35) anashitakiwa kwa kosa la kujifanya  mmiliki wa nyumba namba 22 kitalu L L Mateka B wakati ilikuwa siyo jambo la kweli na kubadili jina kuwa anaitwa Consolata Alphonce Soko .

Inadaiwa kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kati ya tarehe hizo hizo  oktoba 22 ,2008 na 5 desemba 2010 katika benki ya NMB tawi la Songea.

Mshitakiwa amekana shitaka na yupo nje kwa dhamana ya shilingi milioni tano ,na mshitakiwa namba 2 Onesmo Soko  naye yupo nje kwa dhamana  ya milioni tano.
Mwisho.

CHADEMA WAKATAA KUSIMAMISHA MGOMBEA UMEYA SONGEA





                                     Katibu wa Chadema Jimbo la Songea Masumbuko Paulo
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) wilaya ya Songea  kimemuandikia barua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuhusu dhamira ya chama hicho kutosimamisha mgombea wa nafasi wazi ya Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo kutokana na mizengwe na ghiliba zinazofanywa na Mkurugenzi huyo

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za Chama hicho zilizopo kata ya Mfaranyaki Katibu wa Chadema Jimbo la Songea Masumbuko Paulo alisema kuwa Chama chake kimeamua kutosimamisha mgombea wa kuziba nafasi hiyo kutokana na mizengwe mingi inayoendelea katika harakati za uchaguzi huo

Paulo alisema kuwa Viongozi wa Chadema wamekutana na kutoa msimamo wao kuhusu muenendo huo na kuamua kumjulisha Mkurugenzi wa Manispaa kuwa Chadema hakitasimamisha mgombea katika uchaguzi wa Septemba 23 mwaka huuu

Alisema kuwa Chadema kimemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kutopindisha kanuni na sheria kwa maslahi ya Chama Cha Mapinduzi alivyofanya katika uchaguzi uliopita wa kumpata Meya

“Chama kinakukumbusha kufuata kanuni ili kuondoa migongano isiyo ya lazima tena tunamtaadharisha kutoegemea kwa upande mmoja kama unavyofanya sasa”alisema Paulo

Mtandao huu umefanikiwa kuipata barua hiyo ya tarehe 21 Septemba 2011 iliyoenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea yenye kumbukumbu namba CH/SMJ/RV/18 yenye kichwa cha habari “Taarifa ya kutosimamisha mgombea wa nafasi wazi ya Mstahiki Meya Manispaa”

Sehemu ya barua hiyo inasomeka “….uchaguzi uliopita wa aina hii haukuwa huru na haki kwani mazingira ya kupiga kura hayakuwa ya siri wala hukuandaa eneo la siri la mtu kupiga kura badala yake ulifanya wajumbe wapiga kura wapige kura ya wajumbe iwe inaonekana kwa wazi tu”

Katika mkutano huo na waandishi Paulo alisema kuwa Chadema ina madiwani 7 ambapo Chama cha Mapinduzi (Ccm) ina madiwani 20 na wabunge wawili kwa maana ya mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Emmanuel Nchimbi,na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma Devota Likokola na kufanya kuwa Ccm iwe na Madiwani 22

Katika uchaguzi huo Ccm imemsimamisha Diwani wa Kata ya Matogoro Charles Mhagama kutokana na Chadema kutomsimamisha mgombea wa kuziba nafasi wazi ya Meya wa Manispaa kunamfanya Charles Mhagama kuwa mgombea pekee wa nafasi

Uchunguzi uliofanywa na mtandao huu umebaini kuwa watu wengi hawajaridhiki na kitendo cha Ccm  kumpitisha Charles Mhagama kuwa mgombea Umeya kutokana na nafasi hiyo kuwa nyeti katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo
Imebainika kuwa baadhi ya madiwani wa Ccm wanamkakati kabambe wa kumpigia kura za hapana mgombea wao ili uchaguzi uhitishwe upya kutokana na Charles Mhagama kutokuwa na mahusiano mazuri na madiwani wezake na kuonekana sio chaguo stahiki

Akizungumza na mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Nachoa Zakaria alikiri kupokea barua ya Chadema na kueleza kuwa kanuni zinaruhusu kufanya uchaguzi ambapo kutakuwa na kura ya ndiyo au hapana

Zakaria alisema kuwa ikiwa wajumbe therusi mbili wakipiga kura za hapana uchaguzi huo utaitishwa upya kwa mujibu wa kanuzi za uchaguzi wa nafasi hiyo ya umeya na kuongeza kuwa uongozi anatoa Mungu na kwamba Halmashauri hiyo inahitaji apatikane Meya na ipo siku atapatikana

Alisema kuwa katika uchaguzi huo atasimamia kikamilifu kanuni na sheria za uchaguzi kwa maslahi ya Halmashauri na wananchi na kudai kuwa madai ya Chadema katika barua yao sio ya msingi kwa kuwa wanalalamikia kitu kilichopita badala ya kuzungumzia uchaguzi uliopo

Uchaguzi huo unafanyika kuziba pengo lililoachwa wazi na marehemu Ally Said Manya aliyefariki Julai 29 mwaka huu katika hospitari ya Misheni ya Peramiho baada ya kuugua muda mrefu maradhi ya moyo na kisukari

AWALI Chadema walimcharukia mgombea wa nafasi ya Umeya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kupitia Chama cha Mapinduzi(Ccm) Charles Mhagama kwa madai kuwa sio kiongozi makini na muadilifu anayeweza kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa maslahi ya wananchi

Akihutubia mamia ya wakazi wa Manispaa ya Songea  hivi karibuni katika viwanja vya soko la Manzese,kata ya Misufini Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Ruvuma Joseph Fuime alisema kuwa nafasi ya Umeya ni nafasi nyeti sana katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea hivyo ina hitaji mtu makini na muadilifu wa kuweza kushirikiana na wadau mbalimbali kuweza kulisukuma gurudumu la maendeleo

Fuime alisema kuwa kutokana na umuhimu huo mgombea aliyepitishwa na Chama cha Mapinduzi (Ccm)Charles Mhagama ili kuweza kuziba nafasi ya Umeya iliyoachwa wazi na Marehemu Ally Manya aliyefariki mwezi julai 29 mwaka huu,kuwa hana uwezo wa kushika nafasi hiyo kutokana na kujaa tamaa ya kujitajirisha kiharamu kupitia fedha za wananchi

Alieleza kuwa Mhagama ni kiongozi mbabe na mwenye kupenda rushwa hali inayodhorotesha maendeleo ya wananchi kwani alishawahi kufanya vitendo viovu ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa ushawishi wa rushwa katika ununuzi wa gari ya kuzima moto,uuzwaji wa Katapila la Halmashauri akiwa ni Diwani wa kata ya Matogoro na kiongozi wa Kamati mbalimbali za baraza la madiwani

“Mhagama hawezi kuwa kiongozi bora na atakayeweza kutupeleka kwenye ustawi stahiki wa maisha kwani vitendo vyake vingi ni viovu kwani kuna kipindi alikuwa na mahusiano na mwanafunzi mmoja miaka ya nyuma ambapo alikutwa naye kwenye nyumba ya wageni na wazazi wa mwanafunzi huyo na kupelekewa kupigwa viboko hadharani”alieleza Fuime

Alifafanua kuwa vitendo hivyo vinadhihirisha ni jinsi gain alivyokuwa mchafu na kiongozi mbovu asiyestahili kupewa majukumu makubwa ya Umeya hasa katika kipindi hiki kilichogubikwa na ufisadi,rushwa na urasimu mkubwa Serikalini

Alisema kuwa siku zote Chama cha Mapinduzi kimekuwa kikiwaacha viongozi wazuri na kuwateua viongozi wabovu ili waweze kukinufaisha chama kwa maslahi yao binafsi hivyo hatuwezi kuongozwa na kiongozi wa aina hiyo na ndio maana tunapaza sauti ili umma ujue na kuwaambia Madiwani wao waliowachagua kutokumpigia kura mgombea huyo wa Ccm kwenye uchaguzi wa Serikali unaotegemewa kufanyika Septemba 23 mwaka huu na kuongeza pia Halmashauri ya Manispaa ya Songea ni mali ya wananchi wote na sio mali ya kikundi cha watu wachache wenye malengo yao binafsi
MWISHO

Wednesday, September 21, 2011

MJUMBE WA BODI YA MIKOPO WA SERIKALI ZA MITAA ATEMBELEA SOKO LA SONGEA NA KUJIONEA CHANGAMOTO ZAKE

    Na Amon Mtega,Songea
 
SOKO kuu la Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma lililoungua moto mwaka 2003 na kuteketeza kabisa fedha na mali za wafanyabiashara wa soko hilo na kisha kujengwa upya na Manispaa  hiyo kwa fedha zilizotoka kwa wahisani na taasisi za mikopo na kisha kuendelea kutoa huduma hiyo lakini bado linakabiliwa na changamoto mbali mbali.
 
Akitoa taarifa ya uendeshaji wa soko hilo mkuu wa Masoko ya Manispaa ya Songea Salum Homera kwa Mjumbe wa bodi ya mikopo ya Serikali za Mitaa George Mallima Lubeleje alisema kuwa baada ya soko hilo kujengwa upya likiwa na meza 308 na maduka 161 na kwamba linatoa huduma kwa wananchi wa ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma.
 
 Alisema kuwa pamoja na huduma hizo halmashauri hukusanya kiasi cha shilingi milioni 9.4 kwa mwezi ambazo hutumika kuisaidia halmashauri kugharamia shughuli mbambali za kiutawala na utoaji huduma kwa wananchi pia serikali kuu hukusanya kodi ya mapato kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo ambayo huisaidia serikali kutoa huduma boraa kwa wananchi.
 
 Aidha pamoja na mafanikio hayo Homera alisema kuwa zipo changamoto ambazo zinahitaji kutatuliwa ili kuboresha mapato zaidi ikiwemo mahitaji ya ukarabati ambayo ni makubwa kuliko kiasi kinacho kusanywa na soko hilo,baadhi ya wafanyabiashara kuendesha biashara zao nje ya soko na kulikosesha soko mapato na kuchelewa kusainiwa kwa sheria ndogo za halmashauri ambazo huwa zina mapendekezo ya maboresho ya viwango vya kodi na ushuru mbali mbali.
 
 Kwa upande wao wafanyabiashara na wananchi wanaolitumia soko hilo walisema kuwa soko hilo bado linahitaji ukarabati mkubwa ili liweze kuwa na hadhi ya Manispaa na hasa katika maduka ya kuuzia nyama ambako kunahitaji usafi wa hali ya juu tofauti na hali ilivyo sasa.
 
Naye mjumbe wa bodi ya mikopo ya Serikali za Mitaa  George Malima Lubeleje akizungumza baada ya kukagua soko hilo mbali na kupongeza matumizi ya fedha ya mkopo iliyotolewa na bodi hiyo kwa ajili ya ujenzi huo alisema kuwa halmashauri inapaswa kusimamia sheria ndogo ambazo zitasaidia kuongeza kipato na kuweza kumaliza kulipa deni la mkopo huo ili iweze kupewa mkopo mwingine.
 mwisho





MAJAMBAZI WAUA,WAJERUHI,KUPORA SHILINGI MILIONI MBILI NA KUTOKOMEA ZAO

               Na Steven  Augustino,Tunduru

WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamemuua kwa kumpiga mapanga mkulima wa kitongoji cha Mkangwala kilichopo katika kijiji cha Mbatamila Wilayani Tunduru aliyefahamika kwa jina la Bibie Mtenje (25) na kumjeruhi vibaya mume wake Kasim Shaibu (35).

Taarifa kutoka katika kijiji hicho zinaeleza kuwa baada ya watu hao kutekeleza uharamia huo walifanikiwa kupora fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni mbili pamoja na kuchoma moto nyumba ya jirani yake aliyetambulika kwa jina la Anafi Alifa aliyedaiwa kutoka na kupeleka taarifa kwa majirani wakati tukio hilo likiendelea.

Ndugu wa majeruhi Shaibu ,Bw.Sandali Shaibu na Kazembe Rajabu wanao muuguza majeruhi huyo aliyelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Tunduru akiwa hajitambui walisema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Septemba 21 mwaka huu.

Wakifafanua taarifa hiyo wanafamilia hao walidai kuwa fedha alizo porwa majeruhi na kusababisha kifo cha mkewe zilitokana na mauzo ya viroba 24 vya mpunga ambao walilima na kufanikiwa kuvuna msimu uliopita wakiwa na matumaini ya kujiletea maendeleo baada ya kuuza.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma  Michael Kamuhanda mbali na kukiri kuwepo kwa tukio hilo alisema kuwa jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na kwamba endapo watabainika watu kuhusika na tukio hilo sheria itafuata mkondo wake.

 Mganga wa hospitali ya Wilaya ya Tunduru Dkt. George Chiwangu ambaye alimpokea na kumshughulikia majeruhi Shaibu alisema kuwa, majeruhi huyo ameumizwa vibaya kichwani na sehemu za tumboni kutokana na kukatwa mara nyingi na mapanga.

Naye Mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Mtenje, Dkt.Titus Tumbu alisema kuwa kifo chake kimesababishwa na kutokwa na damu nyigi zilizosababishwa na majeraha ya kukatwa na mapanga sehemu za kichwani.

Mwisho   

MANISPAA YA SONGEA WAFANIKIWA KUDHIBITI MIMBA KWA WANAFUNZI WA SHULE ZA MSINGI

               Na Thomas Lipuka,Songea

IDARA ya Elimu  na wadau wa Elimu katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma,wamefanikiwa kuondoa tatizo la mimba kwa wanafunzi wa Shule za Msingi kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi 2011 ambapo hakuna mwanafunzi aliyepata mimba katika Shule zote za Msingi katika Manispaa hiyo.
Taarifa ya hali ya Elimu ya mwaka 2010/2011 iliyosomwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Zakaria Nachoa kwa wadau wa Elimu katika Ukumbi wa Songea Club hivi karibuni imebaini kuwa hakuna mimba iliyoripotiwa kwa wanafunzi wa Shule kwa Kata zote 21 za Manispaa hiyo.
Nachoa alisema mbinu iliyotumika katika kuzuia suala la mimba ni pamoja na ushirikiano wa karibú baina ya wazazi,walimu,wadau wa Elimu na Viongozi wa Elimu ngazi zote za Manispaa na hatimaye kufikia kufuta kabisa tatizo la mimba katika Shule za Msingi zote za Manispaa ya Songea.
Taarifa ya mandeleo ya Elimu katika Manispaa hiyo imetaja pia mafanikio zaidi yaliyojitokeza katika sekta ya Elimu ni pamoja na ufaulu kwa Wanafunzi waliomaliza Elimu ya Msingi 2010 ambapo Manispaa hiyo imekuwa ya kwanza Kimkoa, na kuzipita Wilaya za Songea,Mbinga,Namtumbo na Tunduru.
Hata hivyo changamoto kadha zimejitokeza katika tathmini elimu Manispaa ya Songea ambapo kuna uhaba wa vitabu vya kiada,jambo ambalo linapelekea kitabu kimoja cha kiada kutumiwa na wanafunzi 11 ama zaidi.
Changamoto zingine zilizotajwa katika tathmini hiyo ni uhaba wa walimu darasani, hivi sasa kuna walimu 820 wakati mahitaji ni walimu 1259 hivyo Manispaa ya Songea kuwa na upungufu wa walimu 439 darasani ,jambo ambalo linahitaji msaada toka Serikali kuu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea amewaambia wadau wa Elimu kuwa kuna upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa,vyoo na nyumba za walimu,ameomba wadau wa Elimu kujipanga kwa hatua za awali za ujenzi wa maboma ili wanafunzi wote watakao faulu 2011 waweze kupata nafasi kidato cha kwanza.
Kuhusu changamoto ya upatikanaji wa madawati wadau wamesema ni vema kujipanga upya kwani suala la miti ya kutengenezea madawati lipo kwenye uwezo wao, isipokuwa Serikali iwezeshe Manispaa ya fedha kwa vifaa vya kiwandani ili kuondoa tatizo la madawati hatimaye wanafunzi wapate mazingira bora ya kujifunzia na kuleta usikivu,wanaposoma ili kuongeza ufaulu.
Mkurugenzi wa Manispaa pia alitoa taarifa ya maendeleo ya Elimu ya watu wazima mbele ya Mwenyekiti wa kikao cha tathmini Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Sabaya kuwa Manispaa ya Songea ina watu 2883 ambao hawajui kusoma kuhesabu na kuandika sawa na asilimia 40% ya watu wazima wote wa Manispaa hiyo ambapo Mkuu huyo wa Wilaya akatia mkazo kwa Kata zote kuendeleza kwa kasi Elimu ya watu wazima ili kufuta kabisa asilimia ya wasiojua kusoma,kuandika na kuhesabu katika Manispaa ya Songea.
“Naagiza kisomo sasa kipambe moto kata zote waratibu Kata,walimu wakuu,watendaji ngazi zote wajibikeni ipasavyo” alisisitiza Bwana Sabay.
Mwenyekiti huyo wa Kikao hicho ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Sabaya amewaagiza viongozi wa Elimu Manispaa,Waratibu Kata,walimu na wadau wa Elimu kusimamia kikamilifu malengo ya kukuza taaluma katika Manispaa kwa kuhimiza mahudhurio ya wanafunzi,walimu kufundisha kikamilifu,wakaguzi kufuatilia ufundishaji na viongozi kutekeleza wajibu wao kwa kutoa stahiki zote za walimu ikiwemo malipo ya likizo,matibabu na posho zao za kujikimu.

MWISHO

Tuesday, September 20, 2011

HII, NIMIONGONI MWA SHUGHULI ZINAZOFANYWA NA TCCIA MKOA WA RUVUMA KATIKA KUTANGAZA BIIDHAA ZA WAJASILIAMALI WANAOLELEWA NA TAASISI HIYO MUHIMU KWA WAJASILIAMALI

 Afisa Mtendaji wa TCCIA Mkoa wa Ruvuma Philemon Moyo akiangalia bidhaa aina ya mvinyo ikiwa katika aina mbalimbali zilizowekwa kwenye fremu maalum katika ofisi za TCCIA mkoa wa Ruvuma zilizopo kwenye jengo la NSSF mjini hapa

AJIKUTA MIKONONI MWA DOLA KWA KUSABABISHA KIFO CHA ADERINA KWA MADAI YA WIVU WA KIMAPENZI


                             Na Gideon Mwakanosya,Songea
JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma linamshikilia Mfanyabiashara mkazi wa  wa Mbinga mjini Timotheo Komba (21) kwa tuhuma za kumuua muhudumu ya baa ya Mbuji iliyopo mjini humo ambaye awali alikuwa mpenzi wake

Akizungumza na Mwaandishi wa mtandao huu wa www.stephanomango.blogspot.com  jana ofisini kwake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alimtaja mwanamke aliyeuawa kuwa ni Aderina Nchimbi(21) ambaye ni mkazi wa mtaa wa eneo la Shule ya Msingi Kiwanjani Mbinga Mjini

Kamuhanda alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 20 mwaka huu,majira ya saa moja asubuhi huko katika mtaa wa eneo la Shule ya Msingi Kiwanjani
Alisema kuwa inadaiwa siku ya tukio Afisa Upelelezi wa makosa ya jinai wa Wilaya ya Mbinga Mrakibu Msaidizi wa Polisi Edward Kavalambi akiwa na Askari wenzake wa kitengo cha Upelelezi ambao walikuwa doria waligundua kuuawa kwa Aderina ambaye alikutwa kando kando ya barabara jilani kabisa na nyumbani kwake

Alifafanua zaidi kuwa Maaskari kanzu hao baada ya kugundua tukio hilo la mauaji muda mfupi walifanikiwa kumkamata Komba ambaye anadaiwa kuwa katika kipindi cha nyuma alikuwa mpenzi wake tangu walipokuwa wakiishi katika Kijiji cha Mpepai

Alisema kuwa chanzo cha tukio hilo la mauaji kinasadikiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi ambapo inadaiwa kuwa marehemu Aderina kabla ya mauti hayajamkuta alikuwa akilazimishwa kufanya mapenzi na Mfanyabiashara huyo Komba ambaye alikuwa akijitahidi kumshawishi warudiane tena na mahusiano yao kama awali lakini mwanamke huyo alikuwa anakataa

Kamuhanda alisema kuwa mara upelelezi utakapokamilika mtuhumiwa Komba anatarajiwa kufikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma zinazomkabili,

MWENDESHA PIKIPIKI ASABABISHA KIFO CHA MTEMBEA KWA MIGUU

 
                    Na Gideon Mwakanosya,Songea
POLISI wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma wanamshikilia Mwendesha Pikipiki Felix Ndimbo (18) mkazi wa Kijiji cha Langilo kwa tuhuma za kumgonga mtembea kwa miguu Joseph Ndimbo (76) mkazi wa Kijiji cha Mkoha wilayani humo na kumsababishia kifo papo hapo

Habari zilizopatikana jana mjini hapa ambazo zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma zimeeleza kuwa lilitokea juzi majira ya 1:30 usiku kwenye barabara inayotoka Mbinga kwenda kijiji cha Langilo

Kamuhanda alibainisha zaidi kuwa siku hiyo ya tukio kwenye barabara hiyo Felix akiwa anaendesha Pikipiki ambayo haina namba za usajili aina ya SanLg ilimgonga mtembea kwa miguu mzee Joseph Ndimbo ambaye alikuwa anatoka Kijiji cha Langilo kwenda katika Kijiji cha Mkoha na kumsababishia kifo papo hapo

Alieleza zaidi kuwa chanzo cha tukio hilo mwendesha Pikipiki Felix akiwa anatokea Kijiji cha Mkoha kuelekea Kijiji cha Langilo akiwa kwenye mwendo mkali alimgonga mtembea kwa miguu Joseph ambaye alikuwa anatembea kandokando ya barabara upande wa kulia

Kamuhanda alisema kuwa mtuhumiwa Felix amekamatwa na anaendelea kuhojiwa na Polisi ambapo upelelezi wa tukio hilo ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili
MWISHO

Monday, September 19, 2011

WANANCHI KILIMANJARO WAPINGA SERIKALI KUWANYAN'GANYA ARDHI YAO NA KUMPATIA MWEKEZAJI

                 Na Efracia Massawe
WANAKIJIJI wanaoishi katika Msitu wa Westi Kilimanjaro  eneo la  Ngaranairobi Kata ya Nduma, wamesema kitendo cha serikali kubinafsisha eneo lao na kuwapatia wawekezaji kimewasababishia kutokuwa na makazi ya kuishi.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es salaam na wakilishi wa wanakijiji hao, Emmiliana  Kimaro, wakati alipokuwa akiwasilisha mada katika Tamasha la Mtandao wa Jinsia lililofanyika makao makuu TGNP kuanzia septemba 13-16 mwaka huu.
Kimaro alisema kitendo kilichofanywa na serikali kuchukua eneo la msitu huo wakati ndani yake kulikuwa na wakazi wa kudumu bila kuwatafutia njia mbadala ya kuwahamishia wanakijiji hao, wamekifananisha na ukatili.
“Serikali ilitangaza kuwa wanakijiji wa Ngaranairoi tumepatiwa ardhi ni uongo,  ila waliomilikishwa ardhi na serikali ni wanakijiji wa Ngurushani, na wengi wao ni wazee hata hivyo ardhi waliyokabidhiwa ni vipande vya roborobo” alisema Kimaro.
“Naongea kwa masikitiko pia naomba mtandao huu unilinde kwani kufichua siri iliyofichwa na serikali kwa muda lolote linaweza kutokea ila ukweli utabaki pale pale lazima kilio chetu jamii ikifahamu” alisisistiza Kimaro.
Mwisho.

WANAHARAKATI WAITAKA SERIKALI KUREKEBISHA SERA NA SHERIA KANDAMIZI

                                                        Na Stephano Mango
WANAHARAKATI wameshauri sera  na sheria  mbalimbali zilizotungwa na zitakazotungwa  kwa ajili ya kukuza uchumi ili kuleta maisha bora endelevu kwa  wananchi nchini  zifanyiwe ufatiliaji ili kuhakisha zinawanufaisha watoto na wasichana wanaofanya ajira  za ndani .
Wakichangia mada katika warsha ya Mapambano ya wanaharakati kwa wanawake katika njia za kujiajiri,kupata ajira na kujiletea maisha endelevu katika Tamasha la 10 la wiki ya Jinsia lililo malizika juzi jijini Dar es salaam wanaharakati hao  walisema sheria nyingi zimetungwa na zimelenga  kuleta maisha bora kwa watanzania wakiwemo wanawake  lakini hakuna  ufatiliaji unaofanyika kuhakikisha zinatekelezwa ili kuwanufaisha  katika masuala ya kupata ajira.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Jinsia Tanzania,Mary Rusimbi alisema ili kuondokana na matatizo ya ajira kwa wanawake ni vizuri  sera za kitaifa za kuondokana na umaskini zikiwemo sera ya ajira zitekelewe.
“Sera hizi inabidi zifanyiwe ufatiliaji ili kutambua kasi ya utekelezaji katika kuleta maisha bora na endelevu kwa wananchi,elimu katika masuala ya ajira inabidi itolewe ili mfanyakazi  akiwemo wa nyumbani  aweze kujua haki na wajibu wake katika kazi hizo”alisema Rusimbi.
Na kufafanua kuwa  elimu hiyo itampa mwongozo kutambua kazi za nyumbani anazopaswa kufanya na sizopaswa kufanya.
Alieleza kuwa haki mojawapo ambayo mfanyakazi wa ndani anapaswa kuidai ni kutambulika katika chama cha wafanyakazi nchini.
Wanaharakati hao walieleza kuwa wasichana wanaofanya kazi za ndani wanaishi katika mazingira magumu na hii ni kutokana na kunyimwa fursa za kushiriki katika mijadala,kupata elimu na kufanya maamuzi.
Naye Ruth meena akizungumza katika warsha alisema kuwa ili kuondoa tatizo hilo basi sera za elimu ziboreshwea ili kuwawezesha wafanyakazi wa ndani kufahamu haki zao za ajira na kujipatia maisha endelevu.
Lakini pia alitoa wito kama mtoto wa kike amefeli mtihani wa shule ya msingi si vizuri akiozeshwa au kulazimishwa kufanya kazi za ndani  badala yake apelekwe shule za ufundi stadi ili baadae aweze kujikomboa kiuchumi.
Andrew Njau kutoka Kilimanjaro, wilaya ya Hai alisema elimu endelevu kwa vijana ni suluhisho pekee la kupambana na tatizo la ajira na umaskini nchini hivyo basi  serikali inatakiwa kuwajibika kuanzia ngazi za chini kuhakikisha utekeleaji wa sera hizo unatiliwa mkazo.
Kwa upande wake Veronica Ngweya ,kutoka Msumbiji alisema ili kutatua tatizo la ajira kwa wasichana wa ndani serikali  yao imeanzisha kampeni maalum ya kuwafikia na kukusanya maoni ili kutambua matatizo wanayaokumbana nayo na kisha kuwapatia elimu.
“Tunawafundisha sera zitakazowajengea uwezo wa kujitambua na kuzipigania hali zao pale wanapoona zimekiukwa”alisema Ngwenya.
mwisho

Saturday, September 17, 2011

WADAU MBALIMBALI NCHINI WAENDELEA KUTUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA FAMILIA YA MAREHEMU MOHAMED MNYACHI ALIYEKUWA MWENYEKITI WA CHAMA CHA TANZANIA LABOUR PARTY(TLP) WILAYANI TUNDURU

Marehemu Mohamed Mnyachi enzi za uhai wake(Picha kwa hisani ya Familia yake)

Na Agustino Chindiye,Tunduru

Mtandao huu unatoa pole kwa Familia ya Marehemu Mnyachi na inaungana na watanzania wote katika majonzi hayo;Tunaamini kuwa Marehemu Mnyachi ameacha pengo kubwa ambalo halitazibika lakini mchango wake umeonekana dhahili katika kuchangia harakati za ukombozi wa Taifa hili kutoka nikononi mwa Mafisadi na wabadhilifu nchini

Marehemu Mnyachi ametangulia mbele za haki nasi tunamfuata lakini aliweza kutimiza wajibu wake kikamilifu enzi za uhai wake,uliobaki ni wetu,wakati tunaendelea kumkumbuka tutafakari kwa umakini fikra zake ili ziweze kutusaidia katika ujenzi wa pamoja wa taifa tunalolihitaji
         Bwana alitoa na Bwana ametwaa,Jina lake lihimidiwe