About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Tuesday, September 27, 2011

WALIMU WAWILI WANUSURIKA KUUAWA KUTOKANA NA WIVU WA KIMAPENZI WILAYANI TUNDURU

Katibu wa Chama Cha Walimu (CWT)Mkoa wa Ruvuma Luya Ngonyani

Na, Augustino Chindiye Tunduru

WATU watano wanashikiriwa na jeshi la Polisi Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma kwa tuhuma za kufanya majaribio ya kutaka kuwaua Walimu wawili wa Shule ya Msingi Ruanda iliyopo katika Tarafa ya Nakapanya Wilayani humo.

Taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa Walimu walionusulika katika tukio hilo ni Mwl. Ezakieli Ngaleka na Mwl.Emmanuel Hyao wanaodaiwa kuwa na urafiki wa kimapenzi na mke wa mtu.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda  amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Ally Brashi (19) ambaye pamoja na mambo mengine amekiri kuhusika katika tukio hilo akidai kuwa alitekeleza tukio hilo kwa nia ya kutaka kumuua Mwl. Naleka akiwa anamtuhumu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Mkewe.

Wangine wanaoshikiriwa kutokana na tukio hilo ni pamoja na Mustafa Mariki (19), Mahamudu Juao (21), James Mathayo (20) na Hamisi Athuman (19)  wote wakiwa ni wakazi wa kijiji hicho.

Akizungumzia tukio hilo Kaimu afisa elimu wa shule za Msingi wa Wilaya ya Tunduru Mwl.Fravia Nchimbi alisema kuwa kufuatia tukio hilo idara yake imeamua kuwabadirishia vituo vya kazi ili kuwahakikishia usalama wa maisha yao.

Nae Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mwl. Rashid Mandoa alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alisema kuwa ofisi yake imewaagiza viongozi wa serikali ya kijiji hicho kufanya mazungumzo na  wananchi wao ili waachane na matukio ya aina hiyo.

Kuhusu nyumba iliyoteketea na moto huo alisema kuwa siyo mali ya Halmashauri hiyo bali ilikuwa ikimirikiwa na mkazi wa kijiji hicho  Fikirini Brashi ambaye alikuwa na mkataba wa kuwapangisha walimu hao na kwamba baada ya tukio hilo kamati ya shule na uongozi wa kijiji ndio utakaowajibika kumjengea nyumba nyingine.

Wakiongea kwa nyakati tofauti walimu hao walimshukuru mungu kwa kuwaokoa na tukio hilo pamoja na uongozi wa halmashauri hiyo ambao umekubali kuwagharamia kwa kuwanunulia vifaa na kuwafidia mali zilizo teketea katika tukio hilo zinazo kadiliwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni moja.

Mwisho


Sunday, September 25, 2011

SAKATA LA UMEYA SONGEA LAWAKUTANISHA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA RUVUMA NA WAZIRI DKT NCHIMBI

 Waziri wa Habari,Utamaduni na Michezo Dkt Emmanuel Nchimbi katikati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu sakata la kukimbia na sanduku la kura wakati wa uchaguzi wa umeya uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Saccos wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea,kushoto ni Charles Mhagama anayedaiwa kuwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea,kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Naftan Saiyoloi
 Waandishi wa habari wakiendelea kusikiliza hoja mbalimbali katika kikao cha waandishi wa habari na Waziri Dkt Nchimbi
 Waziri Dkt Nchimbi aliyekaa katikati akiwa kwenye picha ya pamoja na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Waliokaa kutoka kushoto Charles Mhagama(Anayedaiwa kuwa Mstahiki Meya),Waziri wa Habari,Utamaduni na Michezo Dkt Nchimbi,Endre w Kuchonjoma(Mwenyekiti wa Ruvuma Press Club),Waliosimama kutoka kulia Nathan Mtega(Katibu Msaidizi wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Ruvuma),Endrew Chatwanga(Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini),Gerson Msigwa(TBC),Emmanuel Msigwa(Channel Ten) Ngaiyona Nkondora(Star Tv na Redio Free) Juma Nyumayo(Uhuru Fm) Alpius Mchucha(HabariLeo)Stephano Mango(Dira ya Mtanzania) Amon Mtega(Mtanzania) Joseph Mwambije(Majira) Anuciata Ngatunga(Ps wa Dkt Nchimbi)Cresencia Kapinga(Majira) Meja Mgumba(Msaidizi wa Waziri) Joyce Joliga(Mwananchi) Naftan Saiyoloi(Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Na Mwandishi wetu
 WAZIRI wa Habari Utamaduni na Michezo Dkt Emmanuel Nchimbi amekutana na waandishi wa habari na kuzungumzia sakata la kudaiwa kukimbia na sanduku la kura kabla ya kudhibitiwa na Madiwani wa Chadema juzi katika uchaguzi wa nafasi wazi ya Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea

Akisoma tamko lake katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea alisema kuwa amesikitishwa na vyombo vya habari,magazeti ya Tanzania Daima,Majira na Mwananchi vilivyolipoti habari hiyo iliyojaa upotoshaji mkubwa

Dkt Nchimbi amevitaka vyombo hivyo kukanusha na kumuomba radhi katika matoleo yao ya Septemba 26 katika ukulasa wa mbele kwani vimemshushia hadhi yake katika jamii na kumjengea misingi ya ukosefu wa uaminifu

Alisema kuwa mnamo tarehe 23 Septemba 2011 magazeti ya Tanzania Daima,Mwananchi na Majira yaliripoti taarifa inayofanana kwamba Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo amekimbia na sanduku la kura kufuatia vurugu zilizotokea katika uchaguzi wa Meya wa Manispaa ya Songea

“Napenda kuutaarifu umma kwamba habari hizo siyo za kweli na ni uzushi mtupu,ukweli ni kwamba mimi katika kikao hicho sikukimbia na sanduku la kura wala hakuna diwani yeyote aliyetoka au kukimbia nje ya ukumbi na sanduku la kura kama ilivoripotiwa na magazeti hayo”alisema Dkt Nchimbi

Alieleza kuwa ukisoma upotoshwaji huu katika magazeti yaliyoandika habari hizo utagundua kwamba habari hizo zimeandikwa na mtu mmoja na kuwagawia waandishi wenzake wa magazeti mengine bila kuthibitisha wakazipeleka kwenye magazeti yao

“Taarifa hizo zilizopotoshwa kwa makusudi zimenidhalilisha,kunichafulia jina langu na kunifanya kuwa mtu nisiyeaminika kitaifa na kimataifa”alisema Dkt Nchimbi

Alieleza zaidi kuwa tabia iliyoanza kuzoeleka hivi sasa ya mwandishi mmoja kuandika kisha kuwasambazia wenzake unawazalilisha waandishi wenyewe na vyombo wanavyoviandikia

Alisema kuwa kwa taarifa hii nayataka magazeti ya Tanzania Daima,Mwananchi na Majira kukanusha na kusahihisha taarifa hizo kwenye magazeti yao ya kesho tarehe 26 September 2011
 Kwenye ukurasa wa mbele na kuniomba radhi
MWISHO

KUNDI LA TEMBO LASABABISHA MAUAJI YA BINADAMU TUNDURU

Na Augustino Chindiye ,Tunduru

MKAZI wa kitongoji cha Ndola kilichopo katika kijiji cha marumba Wilayani Tunduru Daud Rashid (50) amefariki dunia baada ya kuvamiwa na kushambuliwa na kundi la tembo.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa tukio hilo lilitokea wakati marehemu akiende shambani ambako inadaiwa kuwa alikuwa akienda kufanya maandalizi ya shamba la kulima msimu ujao.

Akizungumzia tukio hilo Kaimu Afisa Wanyama pori wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma  Abdalah Mbanganike mbali na kukiri kuwepo kwa tukio hilo alisema kuwa marehemu alifariki dunia kutokana na kuchomwa na meno ya Tembo hao.

Alisema kufuatia hali hiyo idara yake imetoa askari watatu waliongozwa na Ally Salumu kwa ajili ya kuwasaka tembo hao na wameruhusiwa ku ua ili wasilete madhara mengine.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma  Michael kamuhanda katika maelezo yake alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi kujenga tabia ya kutembea katika makundi ili waweze kusaidiana.

Mganga aliye ufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Rashid Dkt. Moses Mwahasunga amesema kuwa kifo chake kimesababishwa na kutokwa na damu nyingi pamoja na kutobolewa tumbo na kuhalibu mfumo wa utendaji kazi wa viungo vilivyopo ndani ya mwili wa binadamu

Mwisho



CCM TUNDURU PECHEPECHE KWA UDHAIFU WA VIONGOZI WAKE WA WILAYA

Na Augustino Chindiye ,Tunduru

VIONGOZI,Wanachama na Wakereketwa wa Chama Cha Mapinduzi CCM Tarafa ya Nakapanya wametoa siku tatu kwa viongozi wa Chama hicho ngazi ya Wilaya kwenda kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua zikiwemo za kufukuzwa kwa kupigiwa kura za kuto kuwa na imani nao.

Tamko hilo limetolewa na wanachama hao katika kikao kilicho wahusisha viongozi wa Chama na jumuiya zake kilicho fanyika katika ukumbi wa ofisi ya Serikali ya Kata ya Namiungo kikiwa na nia ya kujadili mikakati ya kukinusuru chama hicho ili kisifanye vibaya katika chaguzi zijazo.
Sambamba na tamko hilo pia wanachama hao wametishia kutopiga kura katika uchaguzi ujao ama ikiwezekana watamuomba Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete awaruhusu wajiunge na kupiga kura katika Jimbo la Nanyumbu lililopo Mkoani Mtwara.

Wakiongea kwa jaziba wana CCM hao kutoka katika Kata za Nakapanya ambao waliongozwa na Mjumbe wa Mkutano wa  Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Tunduru  Likambale Omari, Shaib Akijo kutoka Kata ya Mindu, Yasini Kaweje kutoka Kata ya Ngapa na Mjumbe wa halmashuri Kuu ya CCM Wilaya Maimuna Bora kutoka Kata ya Muhuwesi walisema wameamua kuchukua maamuzi hayo baada ya kubaini kuwepo kwa ubabaishaji uliokithiri ndani ya Chama hicho huku kukiwa na taarifa za kubebana na kuwachagulia wananchi viongozi wanaotoa fedha kwao.

Aidha wanachama hao wakatolea mfano ubabaishaji wa taarifa za kuteuliwa kwa Diwani wa Viti Maalumu Wanawake wa Tarafa hiyo Salima Limbalambala ambaye mbali na kushiriki katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo  Faridu Khamisi baadae zilitolewa taarifa zenye utata za kutenguliwa kwa wadhifa huo na kuiweka Tarafa yao katika mkanganyiko ambao hadi leo Uongozi wa Chama hicho ngazi ya Wilaya haujatolea kauli yoyote ikiwa ni tofauti na walivyofanya baada ya kutenguliwa kwa udiwani wa Selemani Chisopa aliyetuhumiwa kufanyia kampeni vyama vya upinzani katika uchaguzi mdogo wa Kuziba nafasi ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Tunduru Marehemu Juma Akukweti.

Nao Diwani mstaafu  Hasan Futali, Dastan Amlima na Husen Ndayani ambao pamoja na mambo mengine walihoji vigezo na sababu za uhalali wa kutenguliwa kwa udiwani wa Salima Limbalambala ambaye jina lake lipo katika barua zilizo andikwa na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Taifa Rajab Kiravu na badala yake viongozi wa CCM Wilaya wakapendekeza na kumchagua Diwani wa Viti Maalumu wanaweke kutoka Tarafa ya Mjini Siwema Kalipungu ambaye hakupiga kura za Kumchagua mwenyekiti wa halmashuri huyo huku matokeo ya kuchaguliwa kwake yakiendelea kuheshimiwa.

Kwa ujumla maelezo ya viongozi hao Kero kubwa inayotembea vichwani na katika midomo yao ni Usimamizi mbovu wa Viongozi wa Chama hicho ngazi ya Wilaya ambao wamedai kuwa umeshindwa kusimamia haki kwa wanachama wake, hawafanyi mikutano ya uhamasishaji na wanasema uongozi huo kuwa umepoteza Dira na wakaendelea kutahadharisha  kwamba endapo CCM Taifa itawaachilia waendelee kuiongoza Wilaya hiyo kuna hatari ya chama hicho kufanya vibaya zaidi katika chaguzi zijao ukiwewmo uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.

Hata hivyo baada ya kutoa dukuduku zao hizo zenye maneno makali kwa uongozi wao ukafuata wasaa wa kutoa tamko la kuita kikao cha dhalula kilicho pangwa kufanyika Septembar 28 mwaka huu na kwamba watakao tolewa kafala katika kikaango hicho ni  uongozi wa CCM Wilaya unao ongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya  Mustafa Bora, Katibu wa CCM Wilaya Ramadhan Amer. Katibu Mwenezi CCM Wilaya Hasan Kindamba.

Wakizungumzia mgogoro huo baadhi ya madadisi wa masuala ya siasa walisema kuwa kupotea kwa mwelekeo na utashi wa viongozi wa chama Tawala CCM kunatokana na mfumo mbovu wa ufuatiliaji na upembuzi wa viongozi wanao takiwa kuwekwa madarakani tofauti na mfumo wa wasisi wa taifa hili Baba wa taifa hayati Mwl. Julius Nyerere  ambao wakati wao walikuwa makini nia viongozi wao na walikuwa wakihakikisha kuwa kiongozi anayefaa ni yule aliyepikwa na kuifa kisiasa.

Saturday, September 24, 2011

VIONGOZI WA CHADEMA KUUNGURUMA VIWANJA VYA SOKO LA SAMAKI KUPINGA UCHAKACHUAJI WA UMEYA SONGEA

Joyce Joliga,Songea

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kesho kinatarajia kufanya mkutano mkubwa wa hadhara ili kuwajulisha wananchi vurugu zilizotokea jana wakati wa uchaguzi wa Meya wa manispaa ya Songea na kusababisha uchaguzi kuvurugika kutokana na madai ya kuwepo kwa wizi wa kura.

Akizungumza na mwandishi wa mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ na Mwenyekiti wa chama hicho mkoa Joseph Fuime amesema, mkutano huo unatarajiwa kufanyika kesho majira ya saa 9 alasili hadi saa 12:00 katika  uwanja wa soko la Samaki lililopo karibu na shule ya Msingi Mfaranyaki .

Amesema,tayari kila kitu kimeshakamilika na wamepata vibali vya kufanya mkutano huo ambapo viongozi mbali mbali watahudhuria  akiwemo Mbunge wa jimbo la Mbozi Magharibi Silinde pamoja na wakili wa kujitegemea Edson Mbogoro.

Aidha,Fuime ametoa wito kwa wananchi wa Manispaa ya Songea kujitokeza kwa wingi kuhudhuria mkutano huo na tayari mambo yote yamekwenda vizuri na wanatarajia kuwa wananchi watafahamu kila kitu kilichojitokeza kutokana na vurugu hizo.

Kwa Upande wake Katibu wa Chadema Jimbo la Songea Paul Masumbuko amesema,chama kimesikitishwa na vitendo vya vurugu vilivyofanywa wakati wa uchaguzi huo na kueleza kuwa wanaungana mkono na Madiwani wao kutomtambua Mgombea wa umeya ikiwa ni pamoja na kutojishugulisha na shuguli zozote hadi uchaguzi utakaporudiwa.

"Kwanza kwa niaba ya chama  tunapenda kuwapongeza Madiwani wa CCM kwa kuungana na wenzao wa  Chadema ambao wapo  7 katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea wakati madiwani wa Ccm wapo 20 ambapo kwenye uchaguzi wa leo walikuwepo 19"lakini kwa kuonyesha kuwa hawamkubali mgombea wao wamempigia kura za hapana hiyo ndiyo demokrasia ya kweli ", alisema Masumbuko

 Amesema, kitendo kilichofanywa na Madiwani wa CCM kuungana na wenzao wa Chadema kimeonyesha ukomavu mkubwa wa demokrasia na kinapaswa kupongezwa kwa nguvu zote kwani upinzani si kupingana kwa kila kitu bali inapotokea maslahi ya wananchi ni vema waungane na kuonyesha uzalendo mkubwa kwa nchi na wananchi waliowachagua.

Katika tamko lililosomwa  jana na Madiwani wa Chadema  kwa niaba ya madiwani wenzake wa Chadema kwenye ukumbi wa Saccos ya halmashauri hiyo Diwani wa kata ya Bombamabili Kenny Mpangara alisema kuwa mazingira yote ya zoezi la uchaguzi yameonekana na utata kwa maslahi binafsi na kudai kuwa Madiwani wa Chadema watasusia vikao vyote vya halmashauri mpaka Meya mpya atakapopatikana .

Kwa upande wao Madiwani wa Chama cha Mapinduzi wakitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari na kusomwa na Diwani wa kata ya Lilambo Yobo Mapunda lilisema kitendo walichofanya Madiwani wa Chadema cha kufanya fujo na kutaka kuwapiga wengine ni kitendo kibaya sana katika kukuza demokrasia na kwamba CCm inamtambua Mstahiki Meya kuwa ni Charles Mhagama
MWISHO.

MADIWANI WATISHIA KUJIUDHURU NYADHIFA ZAO MCHAKATO WA UMEYA SONGEA

Na Mwandishi Wetu,Songea
HALI ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea mjini mkoani Ruvuma ni tete kutokana na madiwani wake saba kutishia kurudisha kadi za chama hicho na kujiuzulu nafasi zao zote ndani ya chama ikiwemo na udiwani kwa kile kilichodaiwa kumpigia kura za hapana mgombea wa unafasi wazi ya umeya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Wakizungumza na waandishi wa habari jana kwa nyakati tofauti madiwani hao walisema kuwa wao kwa pamoja wameitwa kwenye kamati ya maadili ya chama hicho ili waweze kuhojiwa kwanini waliamua kukisaliti chama na kuungana na madiwani saba wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) na kumpigia kura za hapana mgombea wa nafasi ya umeya aliyepitishwa na Ccm Charles Mhagama katika uchaguzi uliofanyika jana na kuishia na vurugu kubwa kwa kurushiana makonde na matusi ya mwilini
Walisema kuwa ni kweli  walimpigia kura za hapana ili uchaguzi uitishwe upya kwa sababu mgombea wa chama chao hatoshi kushika wadhifa huo kwani kuna mambo mengi ambayo ameshindwa kuonyesha uongozi wenye umahili na kwamba Chadema wenye madiwani saba hawakusimamisha mgombea
“Ndani ya chama viongozi walilazimisha na akafanikiwa kupenya kwenye mchakato wa ndani nasi tukasema wamezoea kutuburuza kwa kutulazimisha kupitisha viongozi wanao taka wao kwa maslahi ya wachache sasa awamu hii tunawaonyesha nguvu zetu kwa kumpigia kura za hapana ili wahaibike vizuri mbele za watu wengi”walisema madiwani hao ambao hawakutaka majina yao yatajwe
Walisema kuwa kumpigia kura za hapana diwani mwenzangu wa Ccm kwenye uchaguzi wowote ule sio dhambi ila kumpigia kura za ndiyo diwani wa Chadema ndio ingekuwa dhambi kwa mujibu wa demokrasia mfu zilizopo ndani ya Ccm sasa tunashangaa kuitwa kwenye kikao cha maadili leo
“Tupo tayari kwa lolote ili wananchi wapime ubabe uliopo ndani ya Ccm kwani wao ndio waliotuchagua hivyo tunapaswa kushirikiana nao katika kulisukuma gurudumu la maendeleo na sio kuwadhurumu rasilimali zao na kuwasababishia ufukara mkubwa miongoni mwao
Juzi ulifanyika uchaguzi wa nafasi wazi ya Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambapo Chadema hawakusimamisha mgombea kwa madai kuwa mchakato mzima wa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki na kwamba Ccm walimsimamisha Diwani wa kata ya Matogoro Charles Mhagama
Katika uchaguzi huo uliotawala na vulugu za kila aina wajumbe waliopiga kura walikuwa 26 hivyo  kwa mujibu wa mtangaza matokeo Naibu Meya Mariam Dizumba kuwa Mhagama alipigiwa kura za ndiyo 14 na hapana 12 ndipo madiwani walipoanza kutaka uhesabuji ufanyike upya kwa uwazi kwa maana wanamashaka makubwa na utangazaji wa matokeo ambapo uchaguzi huo haukumalizika

Akizungumza na mtandao huu Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Alfonce Siwale alikiri kuwaita madiwani wote kwenye kikao cha maadili ili waweze kuhojiwa kuhusiana na zoezi zima la uchaguzi wa kuziba nafasi wazi ya umeya na kuongeza kuwa kama madiwani wanataka kujiudhuru nafasi zao itakuwa ni busara kwani mtu mzima alazimishwi jambo
MWISHO



NI AIBU NA FEDHEHA VULUGU ZA UCHAGUZI WA UMEYA SONGEA ! JE NANI WA KULAUMIWA?


 Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Emmanuel Nchimbi
 Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Songea Mjini Nachoa Zakaria
 Naibu Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mariam Dizumba

Mgombea wa nafasi ya Umeya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Charles Mhagama
Na Mwandishi Wetu
MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamerushiana makonde baada ya Naibu Meya wa Halmashauri hiyo Mariam Dizumba kudaiwa kuiba kura zilizopigwa na madiwani hao ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi ya Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo aliofariki dunia miezi michache iliyopita
Katika uchaguzi huo ulioanza kwa marumbano makubwa yaliyodumu kwa zaidi ya dakika 20 kati ya madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) na Madiwani wa Chama cha Mapinduzi ambao walikuwa wanajadili namna uchaguzi huo utakavyokuwa  huru na haki kutokana na Chadema kutosimamisha mgombea na Ccm kusimamisha mgombea
Kutokana na hali hiyo Msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Nachoa Zakaria alitoa ufafanuzi wa kanuni za uchaguzi wa nafasi hiyo ambapo aliwataka madiwani kupiga kura za ndio au hapana na kwamba wapigakura halali waliojiorodhesha walikuwa ni Madiwani 26 akiwemo na Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Emmanuel Nchimbi
Baada ya hali hiyo kutulia Msimamizi wa uchaguzi Zakaria aliita orodha ya wajumbe na kuwataka wachukue karatasi za kupigia kula ambapo madiwani wote walipiga kura na kuitwa wahesabu kura waweze kuzihesabu kura hizo
Zoezi la kuhesabu kura lilipomalizika Naibu Meya wa Halmashauri hiyo Mariam Dizumba alilisimama na kuanza kutangaza matokeo kwa kudai kuwa Mgombea Umeya wa Halmashauri hiyo Charles Mhagama amepigiwa kura za ndio 14 na kura za hapana 12
Dizumba alisema kuwa kutokana na matokeo hayo namtangaza Diwani wa kata ya Matogoro Charles Mhagama kuwa ndiye Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuanzia sasa
“Naomba Msimamizi wa uchaguzi umuite Diwani Mhagama aweze kuvaa joho la Umeya na kukalia kiti chake”alisema Dizumba
Baada ya Msimamizi wa uchaguzi  Zakaria kumuita Diwani Mhagama na kumtaka avue joho la Udiwani na kuvaa joho la Umeya ndipo baadhi ya madiwani walipomtaka Msimamizi wa uchaguzi azihesabu upya kura hizo ili madiwani wote wazione
“Naomba msimamizi usitishe zoezi la kumtaka Diwani Mhagama akalie kiti cha Umeya kwa sababu kuna mashaka makubwa na zoezi la utangazaji wa matokeo yake hivyo zihesabiwe kura upya na madiwani wote wazione”alisema Diwani wa kata ya Mfaranyaki Seneta Yatembo
Jambo ambalo Msimamizi wa uchaguzi alionekana kupata kigugumizi nalo na kumsababisha Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Nchimbi kuingilia mgogoro huo na kupelekea kuharibu hali ya hewa na kuanza kurushiana lugha za matusi miongoni mwa madiwani
Wakati mgogoro huo ukiendelea Diwani wa Viti Maalum Chadema Rhoda Komba akaanza kuwaita madiwani wenzake  ili waweze kumuona Naibu Meya Mariam Dizumba alivyokuwa anaiba kura zilizopigwa za hapana kutoka kwenye sanduku la kura na kuchukua kura za ndiyo kutoka kwenye mkoba wake na kuziweka ndani ya sanduku la kura
Hali hiyo ilisababisha vurugu kubwa na kumfanya Mbunge Dkt Nchimbi akimbie na sanduku la kura kuelekea nje ya ukumbi kabla ya kunyanganywa na kutakiwa kurirudisha ndani na Madiwani wakiongozwa na Madiwani wa Chadema
Wakati Madiwani wanamnyang’anya sanduku la kura Dkt Nchimbi ndipo Naibu Meya Mariam Dizumba alipata mpenyo wa kukimbia na kufanikiwa kuingia ndani ya gari na kutokomea kusikojulikana na kufanya madiwani kuvua majoho na kuondoka zao huku wakimzomea Dkt Nchimbi na kurusha maneno ya matusi
Baada ya tafrani hiyo Madiwani wa Chadema waliitisha kikao na waandishi wa habari na kutoa tamko la kutomtambua Charles Mhagama kuwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo na kwamba wameiomba tume ya uchaguzi ione umuhimu wa kuitisha uchaguzi mwingine
“Akisoma tamko hilo kwa niaba ya madiwani wenzake kwenye ukumbi wa Saccos ya halmashauri hiyo Diwani wa kata ya Bombamabili Kenny Mpangara alisema kuwa mazingira yote ya zoezi la uchaguzi yameonekana na utata kwa maslahi binafsi na kudai kuwa Madiwani wa Chadema watasusia vikao vyote vya halmashauri mpaka Meya mpya atakapopatikana
"Madiwani wa Chadema wapo 7 katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea wakati madiwani wa Ccm wapo 20 ambapo kwenye uchaguzi wa leo walikuwepo 19"alisema Mpangara
Kwa upande wao Madiwani wa Chama cha Mapinduzi wakitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari na kusomwa na Diwani wa kata ya Lilambo Yobo Mapunda lilisema kitendo walichofanya Madiwani wa Chadema cha kufanya fujo na kutaka kuwapiga wengine ni kitendo kibaya sana katika kukuza demokrasia na kwamba Ccm inamtambua Mstahiki Meya Charles Mhagama
Akizungumza na waandishi wa habari Msimamizi wa uchaguzi Nachoa Zakaria kuhusiana na kitendo cha Naibu Meya Mariam Dizumba kutangaza matokeo badala ya Msimamizi wa uchaguzi alisema kuwa kwenye vikao vya baraza la madiwani Mkurugenzi ni katibu wa vikao na kwamba Naibu Meya ndiye alikuwa sahihi kutangaza matokeo hayo
MWISHO

Friday, September 23, 2011

BAADA YA UBAKAJI WA DEMOKRASIA YA UCHAGUZI WA UMEYA MAPAMBANO YANAENDELEA MIONGONI MWA MADIWANI

 Joseph Fuime ambaye ni Diwani wa Kata ya Mjini akiongoza mapambano ya kurudisha demokrasia mikononi mwa wapiga kura
 Sanduku la kura lalejeshwa meza kuu baada ya kurejeshwa toka mikononi mwa watu wasiopenda demokrasia
 Madiwani waendelea kutaharuki tukio la kihistoria la uchaguzi wa kuziba nafasi iliyoachwa wazi na marehemu Ally Said Manya

Wananchi wakiwatathimini kwa umakini mkubwa wawakilishi wao walipokuwa wanachapana makonde katika ukumbi wa Saccos wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea

VULUGU,TIMBWILI LAANZA BAADA YA NAIBU MSTAHIKI MEYA MARIAM DIZUMBA KUTANGAZA MATOKEO YA UCHAGUZI WA UMEYA

 Naibu Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mariam Dizumba akitangaza matokeo ya uchaguzi huo
 Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt John Nchimbi akiwatuliza Madiwani ambao walikuwa wakimzomea Mstahiki Meya aliyevaa Joho nyekundu Charles Mhagama na kuambiwa kuwa amechakachua matokeo na hivyo hawamtambui
 Viongozi hao wakiteta jambo baada ya kunusa harufu ya kushtukiwa mchezo wao walioufanya
 Madiwani wakianza kurushiana maneno yaliyokosa staha na kupelekea vurugu kuanza ndani ya kikao cha baraza la Madiwani
Hapa sasa ni ubabe wa kuzuia sanduku la kura lisitolewe ndani ya ukumbi wa uchaguzi ili zihesabiwe tena na madiwani waweze kujiridhisha kuhusu matokeo ya kura walizozipiga

KURA ZAENDELEA KUHESABIWA NA WASIMAMIZI WASAIDIZI WA UCHAGUZI

 Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi Jimbo la Songea Mjini wakiendelea kuhesabu kura zitakazo mkubali au kumkataa mgombea Umeya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Charles Mhagama
Wa kwanza kutoka kushoto ni Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Manispaa ya Songea Naftan Saiyoloi akiwa na Mweka hazina wa Halmashauri hiyo Kessy Mpakata

MADIWANI WAENDELEA KUPIGA KURA HUKU UTULIVU UKIWA WA KUTOSHA AMBAKO HAKI NA WAJIBU WA MPIGAJI KURA UKIENDELEA

 Mgombea Umeya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambaye ni Diwani wa Kata ya Matogoro akitoka kupiga kura katika uchaguzi huo
 Diwani wa Kata ya Mateka Maricelino Mapunda akitumia vyema haki yake ya kumchagua Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea

 Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Emmanuel John Nchimbi ambaye pia ni Waziri wa Habari,Utamaduni na Michezo akipiga kura wakati wa zoezi hilo la upigaji kura
Madiwani wakitafakari wakati wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huo wakihesabu kura

UCHAGUZI WA UMEYA MANISPAA YA SONGEA NI VITUKO VILIVYOSHEHENI AIBU MBELE YA MBUNGE DKT NCHIMBI

 Diwani wa Kata ya Matogoro Charles Mhagama ambaye ni mgombea Umeya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea akifuatilia kwa umakini mkubwa kanuni za uchaguzi wa nafasi hiyo kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi huo
 Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Emmanuel Nchimbi akiwasalimia madiwani kwenye mkutano huo wa uchaguzi wa nafasi wazi ya Umeya
 Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Songea Mjini Nachoa Zakaria ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea akionyesha wajumbe sanduku la kupigia kura katika uchaguzi huo uliofanyika leo
                                    
 Kutoka kulia ni Msimamizi wa uchaguzi Nachoa Zakaria akihakikisha majina ya wajumbe watakaopiga kura,kushoto ni Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mariam Dizumba
 Hapa ni dua kwanza,ndivyo alivyoanza Diwani wa Kata ya Misufini Salum Mfamaji,akiwa diwani wa kwanza kupiga kura katika uchaguzi huo

MADIWANI WAVUTANA ZAIDI YA DAKIKA 10 UCHAGUZI WA UMEYA MANISPAA YA SONGEA

 Kutoka kushoto ni Diwani wa Viti Maalum(CCM) Rehema Millinga,Rhoda Komba (CHADEMA)Christian Matembo wa kata ya Seedfarm
 Kutoka kushoto ni Madiwani wa CCM,Willon Kapinga kata ya NdilimaLitembo,James Makene kata ya Matarawe,Gerald Ndimbo kata ya Ruhuwiko

 Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Dkt Emmanuel Nchimbi ambaye pia ni Mbunge wa Songea Mjini
Mkurugenzi wa Halmashauri Manispaa ya Songea Zakalia Nachoa

Thursday, September 22, 2011

AZALIWA AKIWA NA UVIMBE KICHWANI NA KUPELEKWA KATIKA HOSPITAL YA MKOA WA SONGEA KWA AJILI YA MATIBABU ZAIDI

 Asante Umbulu mwenye umri wa miezi 3 akiwa amelazwa katika Hospital ya Mkoa ya Songea kwa ajili ya kupata matibabu ya uvimbe wa kichwa,mtoto huyo anatakiwa kupelekwa katika Hospital ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu kwani katika Hospital ya Mkoa ya Songea haiwezi kumfanyia Operesheni kutokana na kukosekana kwa vifaa na wataalamu wenye vigezo stahiki

Mtoto huyo anahitaji msaada wa kufika Jijini Dar es Salaam na kupatiwa matibabu,yeyote anayetaka kumsaidia mtoto huyo aende katika Hospital ya Mkoa wa Songea na aonane na DKT NGAIZA kwa maelezo zaidi au piga simu 0755-33 50 51utaunganishwa na Dkt Ngaiza


Waandishi wa habari wakizungumza na mama wa mtoto Asante Umbulu katika Hospital ya mkoa wa Songea,Martina Nombo,kutoka kushoto ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi,Joyce Joliga,katika ni Cresencia Kapinga mwandishi wa gazeti la Majira

Mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ unatoa pole kwa familia ya Martina Nombo kwa kumuuguza mwanao Asante Umbulu

Maskini mtoto IVVO PONERA anavyoteseka baada ya kuungua moto shambani baada ya kibanda alimukuwepo kuungua moto


 
 Mtoto IVVO PONERA mwenye umri wa mwaka mmoja akiwa amelazwa katika Hospital ya mkoa wa Songea baada ya kufikishwa Hospital hapo akitokea kijijini kwao Mchomolo Wilayani Namtumbo,

Mama wa mtoto huyo Paulina Lwambo akizungumza na mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ katika hospital hiyo alisema kuwa IVVO alikuwa analelewa kwenye kibanda shambani na kaka yake aitwaye Jackson Ponera wakati yeye anaendelea na shughuli za kuvuna mahindi

Alisema kuwa katika kibanda hicho alikuwa amepika chakula ili waweze kujipatia mlo baada ya kumaliza kuvuna,ghafla akasikia mwanaye Jackson anamwita huku akisema kibanda kinaungua moto

"Niliacha kuvuna na kukimbilia kwenye kibanda na kukuta kibanda kinaungua na mtoto IVVO yupo ndani,nilichanganyikiwa lakini nilifanikiwa kumuokoa akiwa ameharibika mwili wake kwa kuungua"alisema Lwambo

Alieleza zaidi kuwa nilimchukua kwa umakini mkubwa na kumleta hapa Hospital kwa ajili ya matibabu na anaendelea vizuri na matibabu

MTOTO AZALIWA NA UVIMBE KICHWANI,WENGI WANASEMA HUENDA ANA VICHWA VIWILI

Na Stephano Mango ,Songea

Martina Nombo (27) mkazi wa kijiji cha Lulambo Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma amejifungua Mtoto wa kike ambaye anadaiwa kuwa na vichwa viwili ameomba msaada kwa watu wenye uwezo wamsaidie wakiwemo wataalam wa upasuaji wa Kichwa wamsaidie kuhokoa maisha ya Mwanaye.

Akizungumza na mtandao huu wa www.stephanomango.blogspot.com  katika wodi namba tano  ambapo amelazwa na Mwanaye huyo hospitali ya Mkoa wa Ruvuma jana mara baada ya  kupata rufaa kutoka hospitali ya  Mbuyula iliyopo Wilaya ya Mbinga

 Mama wa Mtoto huyo amesema, alijifungua salama  kwa njia ya kawaida mapema  9 juni mwaka huu katika hospitali ya Mbuyula ambapo mara baada ya kukabidhiwa mwanaye na wauguzi aligundua kuwepo kwa tatizo hilo na aliwaarifu nao walimweleza kuwa aendelee kuwa na subira.

Amesema, tangu alipojifungua katika hospitali ya Mbuyula kichwa cha mtoto waki kilizidi kukua na kutengeneza kitu kama uvimbe ambapo mtoto  aliendelea kutibiwa hospitalini hapo hadi madaktari walipompatia rufaa ya kumwamishia  katika hospitali ya mkoa jana  kwa ajili ya matibabu zaidi.

Kwa upande Daktari Bingwa wa upasuaji wa hospitali hiyo Hassan Lumbe amesema, picha ya  X-ray imeonyesha kuwa ndani ya kichwa kuna shimo ambalo linasababisha ubongo utoke na kuingia kwenye  uvimbe ,pia mifupa ya kichwa aijajiunga vizuri.

Amesema,upasuaji wa mtoto huyo katika hospitali hiyo hauwezi kufanyika  kutokana na kutokuwa na vifaa  na utaalamu walionao hawakidhi viwango vya kutoa tiba kwa mtoto huyo hivyo wanamrufaa kwenda muhimbili .

Amesema,kesi kama hizo ni chache kuripotiwa katika Hospital hiyo na kwamba wao walimpokea  baada ya kupewa rufaa toka katika hospitali aliyozaliwa ya  Mbinga  nao wanatarajia kumpatia rufaa kwenda hospitali ya taifa ya  Mhubili kwani wamefanya vipimo na vimeonyesha kuwa opelesheni hiyo haiwezi kufanywa hapo na wanachofanya ni kuandaa rufaa pamoja na fedha kidogo ya kumsaidia kumsafirisha Mama huyo na Mwanaye.

Mwisho.



WATATU WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUITAPELI BENKI YA NMB

Na Gideon Mwakanosya, Songea
WATU watatu wamefikishwa Mahakamani  kwa kosa la kula njama na kutenda kosa la jinai  la kufanya udanganyifu  na kujipatia mkopo wa fedha toka  katika Benki ya NMB tawi la Songea Mkoani Ruvuma .

Wakisomewa shitaka hilo jana na  Hakimu mkazi Mfawidhi Mwandamizi Baptisti Mhelela amesema,washitakiwa  wote kwa pamoja walitenda  kosa hilo  kati ya oktoba 22 mwaka 2008 na desemba  5 mwaka 2010 .

Amesema,katika kosa la pili mshitakiwa namba moja Cosmas Haule (35) anashitakiwa peke yake kwa kujipatia mkopo wa fedha   shilingi milioni arobaini kwa udanganyifu  kati ya kipindi hicho hicho cha oktoba 22 mwaka 2008 na 5 desemba 2010 na aliposomewa kosa alikana.

Amesema,mshitakiwa Cosmas yupo nje kwa dhamana  na  ametoa hati ya nyumba na dhamana ya mali isiyo hamishika yenye thamani ya shilingi milioni kumi pamoja na dhamana ya milioni 15  kesi hiyo inatarajiwa kutajwa septemba 30 mwaka huu,upelelezi bado haujakamilika.

Katika kosa la tatu,Mshitakiwa namba tatu Asha Banda (35) anashitakiwa kwa kosa la kujifanya  mmiliki wa nyumba namba 22 kitalu L L Mateka B wakati ilikuwa siyo jambo la kweli na kubadili jina kuwa anaitwa Consolata Alphonce Soko .

Inadaiwa kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kati ya tarehe hizo hizo  oktoba 22 ,2008 na 5 desemba 2010 katika benki ya NMB tawi la Songea.

Mshitakiwa amekana shitaka na yupo nje kwa dhamana ya shilingi milioni tano ,na mshitakiwa namba 2 Onesmo Soko  naye yupo nje kwa dhamana  ya milioni tano.
Mwisho.

CHADEMA WAKATAA KUSIMAMISHA MGOMBEA UMEYA SONGEA





                                     Katibu wa Chadema Jimbo la Songea Masumbuko Paulo
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) wilaya ya Songea  kimemuandikia barua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuhusu dhamira ya chama hicho kutosimamisha mgombea wa nafasi wazi ya Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo kutokana na mizengwe na ghiliba zinazofanywa na Mkurugenzi huyo

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za Chama hicho zilizopo kata ya Mfaranyaki Katibu wa Chadema Jimbo la Songea Masumbuko Paulo alisema kuwa Chama chake kimeamua kutosimamisha mgombea wa kuziba nafasi hiyo kutokana na mizengwe mingi inayoendelea katika harakati za uchaguzi huo

Paulo alisema kuwa Viongozi wa Chadema wamekutana na kutoa msimamo wao kuhusu muenendo huo na kuamua kumjulisha Mkurugenzi wa Manispaa kuwa Chadema hakitasimamisha mgombea katika uchaguzi wa Septemba 23 mwaka huuu

Alisema kuwa Chadema kimemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kutopindisha kanuni na sheria kwa maslahi ya Chama Cha Mapinduzi alivyofanya katika uchaguzi uliopita wa kumpata Meya

“Chama kinakukumbusha kufuata kanuni ili kuondoa migongano isiyo ya lazima tena tunamtaadharisha kutoegemea kwa upande mmoja kama unavyofanya sasa”alisema Paulo

Mtandao huu umefanikiwa kuipata barua hiyo ya tarehe 21 Septemba 2011 iliyoenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea yenye kumbukumbu namba CH/SMJ/RV/18 yenye kichwa cha habari “Taarifa ya kutosimamisha mgombea wa nafasi wazi ya Mstahiki Meya Manispaa”

Sehemu ya barua hiyo inasomeka “….uchaguzi uliopita wa aina hii haukuwa huru na haki kwani mazingira ya kupiga kura hayakuwa ya siri wala hukuandaa eneo la siri la mtu kupiga kura badala yake ulifanya wajumbe wapiga kura wapige kura ya wajumbe iwe inaonekana kwa wazi tu”

Katika mkutano huo na waandishi Paulo alisema kuwa Chadema ina madiwani 7 ambapo Chama cha Mapinduzi (Ccm) ina madiwani 20 na wabunge wawili kwa maana ya mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Emmanuel Nchimbi,na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma Devota Likokola na kufanya kuwa Ccm iwe na Madiwani 22

Katika uchaguzi huo Ccm imemsimamisha Diwani wa Kata ya Matogoro Charles Mhagama kutokana na Chadema kutomsimamisha mgombea wa kuziba nafasi wazi ya Meya wa Manispaa kunamfanya Charles Mhagama kuwa mgombea pekee wa nafasi

Uchunguzi uliofanywa na mtandao huu umebaini kuwa watu wengi hawajaridhiki na kitendo cha Ccm  kumpitisha Charles Mhagama kuwa mgombea Umeya kutokana na nafasi hiyo kuwa nyeti katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo
Imebainika kuwa baadhi ya madiwani wa Ccm wanamkakati kabambe wa kumpigia kura za hapana mgombea wao ili uchaguzi uhitishwe upya kutokana na Charles Mhagama kutokuwa na mahusiano mazuri na madiwani wezake na kuonekana sio chaguo stahiki

Akizungumza na mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Nachoa Zakaria alikiri kupokea barua ya Chadema na kueleza kuwa kanuni zinaruhusu kufanya uchaguzi ambapo kutakuwa na kura ya ndiyo au hapana

Zakaria alisema kuwa ikiwa wajumbe therusi mbili wakipiga kura za hapana uchaguzi huo utaitishwa upya kwa mujibu wa kanuzi za uchaguzi wa nafasi hiyo ya umeya na kuongeza kuwa uongozi anatoa Mungu na kwamba Halmashauri hiyo inahitaji apatikane Meya na ipo siku atapatikana

Alisema kuwa katika uchaguzi huo atasimamia kikamilifu kanuni na sheria za uchaguzi kwa maslahi ya Halmashauri na wananchi na kudai kuwa madai ya Chadema katika barua yao sio ya msingi kwa kuwa wanalalamikia kitu kilichopita badala ya kuzungumzia uchaguzi uliopo

Uchaguzi huo unafanyika kuziba pengo lililoachwa wazi na marehemu Ally Said Manya aliyefariki Julai 29 mwaka huu katika hospitari ya Misheni ya Peramiho baada ya kuugua muda mrefu maradhi ya moyo na kisukari

AWALI Chadema walimcharukia mgombea wa nafasi ya Umeya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kupitia Chama cha Mapinduzi(Ccm) Charles Mhagama kwa madai kuwa sio kiongozi makini na muadilifu anayeweza kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa maslahi ya wananchi

Akihutubia mamia ya wakazi wa Manispaa ya Songea  hivi karibuni katika viwanja vya soko la Manzese,kata ya Misufini Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Ruvuma Joseph Fuime alisema kuwa nafasi ya Umeya ni nafasi nyeti sana katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea hivyo ina hitaji mtu makini na muadilifu wa kuweza kushirikiana na wadau mbalimbali kuweza kulisukuma gurudumu la maendeleo

Fuime alisema kuwa kutokana na umuhimu huo mgombea aliyepitishwa na Chama cha Mapinduzi (Ccm)Charles Mhagama ili kuweza kuziba nafasi ya Umeya iliyoachwa wazi na Marehemu Ally Manya aliyefariki mwezi julai 29 mwaka huu,kuwa hana uwezo wa kushika nafasi hiyo kutokana na kujaa tamaa ya kujitajirisha kiharamu kupitia fedha za wananchi

Alieleza kuwa Mhagama ni kiongozi mbabe na mwenye kupenda rushwa hali inayodhorotesha maendeleo ya wananchi kwani alishawahi kufanya vitendo viovu ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa ushawishi wa rushwa katika ununuzi wa gari ya kuzima moto,uuzwaji wa Katapila la Halmashauri akiwa ni Diwani wa kata ya Matogoro na kiongozi wa Kamati mbalimbali za baraza la madiwani

“Mhagama hawezi kuwa kiongozi bora na atakayeweza kutupeleka kwenye ustawi stahiki wa maisha kwani vitendo vyake vingi ni viovu kwani kuna kipindi alikuwa na mahusiano na mwanafunzi mmoja miaka ya nyuma ambapo alikutwa naye kwenye nyumba ya wageni na wazazi wa mwanafunzi huyo na kupelekewa kupigwa viboko hadharani”alieleza Fuime

Alifafanua kuwa vitendo hivyo vinadhihirisha ni jinsi gain alivyokuwa mchafu na kiongozi mbovu asiyestahili kupewa majukumu makubwa ya Umeya hasa katika kipindi hiki kilichogubikwa na ufisadi,rushwa na urasimu mkubwa Serikalini

Alisema kuwa siku zote Chama cha Mapinduzi kimekuwa kikiwaacha viongozi wazuri na kuwateua viongozi wabovu ili waweze kukinufaisha chama kwa maslahi yao binafsi hivyo hatuwezi kuongozwa na kiongozi wa aina hiyo na ndio maana tunapaza sauti ili umma ujue na kuwaambia Madiwani wao waliowachagua kutokumpigia kura mgombea huyo wa Ccm kwenye uchaguzi wa Serikali unaotegemewa kufanyika Septemba 23 mwaka huu na kuongeza pia Halmashauri ya Manispaa ya Songea ni mali ya wananchi wote na sio mali ya kikundi cha watu wachache wenye malengo yao binafsi
MWISHO