Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Charles Mhagama anayedaiwa kuchakachua matokeo na kuitwa Meya wa Mbunge
Mbunge wa Songea Mjini Dkt Emmanuel John Nchimbi
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu aliyesimama,kutoka kushoto Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Nachoa Zakaria,wa pili Charles Mhagama,wa pili kulia Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomasn Oley Sabaya
Na Stephano Mango,Songea
SAKATA la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kumkataa Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo limechukua sura mpya na kusababisha kikao cha kuzungumza na Mkuu wa Mkoa Mpya wa Ruvuma Said Mwambungu kuhahirishwa kutokana na idadi ndogo ya madiwani wanaodaiwa kuwa kwenye mgomo
Hali hiyo ilijitokeza jana katika kikao maalumu cha Mkuu wa Mkoa mpya wa Ruvuma na Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Akizungumza kwenye kikao hicho baada ya utambulisho Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu alisema kuwa leo nilipanga kuzungumza na Madiwani wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambapo nimejulishwa kuwa idadi yao ni 27 lakini mliofika ni 16 tu
Mwambungu alisema kuwa kutokana na jambo nyeti ninalotaka kuwaeleza ni vyema kikao hichi ambacho nimekiitisha kikahahirishwa hadi pale nitakapo panga tena ili Madiwani wengi mhudhurie katika kikao hicho kwani nimejulishwa Madiwani wengine wameenda kwenye ziara ya Kamati ya Siasa ya Wilaya ya kukagua miradi iliyotekelezwa na Halmashauri hiyo
"Naomba nitoe rai kwenye kuhusu kuhahirisha kikao hichi ili kifanyike siku nyingine ambayo Madiwani wengi watapatikana hivyo nawaombeni mnikubarie rai yangu kwa lengo jema"alisema Mwambungu
Jambo hilo liliungwa mkono na Madiwani wote ambapo Mkuu wa Mkoa aliwaruhusu Madiwani kutoa maoni yoyote ili kuweza kuiboresha siku hiyo itakayopangwa kwa ajiri ya kuzungumza naye
Ndipo aliposimama Diwani wa Kata ya Bombambili Kenny Mbangala na kueleza kuwa wakati meza kuu inajitambulisha nimemsikia Diwani wa Kata ya Matogoro anajitambulisha kama Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea wakati Baraza hili katika uchaguzi wake wa Septemba 23 mwaka huu hatukumchagua yeye na uchaguzi ukavurugika
"Sina hakika kama nimemsikia vibaya Mheshimiwa Mhagama wakati anajitambulisha kwani nimesikia akijitambulisha kuwa yeye ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea badala ya kujitambulisha kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii na Uchumi kwa kuwa tumeharifiwa kuwa Naibu Meya Mariam Dizumba anaumwa na amelazwa hivyo tumeshtushwa na utambulisho huo"alisema Mbangala
Akichangia hoja hiyo Diwani wa Kata ya Matarawe James Makene alisema kuwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kina Madiwani 7 ambapo Chama cha Mapinduzi(CCM) kina Madiwani 20 ambapo siku ya uchaguzi tulimchagua Charles Mhagama kuwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Ndipo aliposimama Diwani wa Kata ya Mjini Joseph Fuime na kusema kuwa siku ya uchaguzi Madiwani tulikuwepo tulikuwa 26 kwa ujumla wetu bila kuangalia itakadi ya Chama Madiwani 14 tulimkataa Charles Mhagama kuwa Mstahiki Meya ambapo Madiwani 12 walimpigia kura za ndiyo na kila mmoja anajua hilo
"Tumesikitishwa na kitendo cha kubadilisha matokeo siku hiyo ambapo uchaguzi ulivurugika baada ya Naibu Meya Mariam Dizumba kutangaza matokeo wakati Msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Mkurugenzi Nachoa Zakaria ambaye siku ya uchaguzi alikuwepo na kumuachia mpiga kura kama Madiwani wengine Meya atangaze matokeo hayo kinyume"alisema Fuime
Alifafanua kuwa huyo mtu aliyepo mbele yetu sisi tulimkataa ingawa alikuwa mgombea pekee yake hata Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Nachoa Zakaria anajua,yemwenye Charles anajua kuwa yeye sio Mstahiki Meya kwani hakuchaguria kila mtu anajua hilo iwe ni mfanyakazi wa Manispaa na umma wote kwa ujumla wao wanajua kuwa Charles Mhagama hakuchaguria kuwa Mstahiki Meya
Alieleza zaidi kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ipo katika wakati mgumu sana hivyo muda umefika sasa Charles Mhagama ajiudhuru nafasi hiyo aliyojipachika ili kuweza kupisha uchaguzi mwingine kwa maslahi ya wananchi wetu kwani hata yeye mwenyewe hanajua hilo na bila kufanya hivyo hakuna jambo ambalo litaendelea kutokana na sakata hili
Akizungumza baada ya sakata hilo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu alisema kuwa yote mliyosema Madiwani nimewasikia na yanazungumzika lakini mmeyasema mahali ambapo sio pake na kwamba kwa sababu mmenikubalia kuzungumza nanyi siku nyingine basi leo tuhahirishe hadi wakati ujao
MWISHO
Wednesday, October 12, 2011
Monday, October 10, 2011
MADIWANI WAMFYATUKIA DKT NCHIMBI SAKATA LA UMEYA SONGEA
Na Mwandishi Wetu,Songea
MADIWANI 14 wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma waliopiga kura za hapana dhidi ya 12 za ndiyo za kumkataa Charles Mhagama kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo wametoa tamko la kusisitiza kutomtambua Meya huyo na kueleza masikitiko makubwa ya hujuma iliyofanya katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni
Wakitoa tamko lao jana mbele ya waandishi wa habari kwenye Viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini hapa walisema kuwa wamesikitishwa sana na kulaani vikali hujuma iliyofanywa na Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Emmanuel Nchimbi kwenye uchaguzi huo ambao ulifanyika kwenye ukumbi wa Saccos ya Manispaa hiyo Septemba 23 mwaka huu
Katika tamko hilo lililosomwa kwa niaba ya Madiwani hao Diwani wa Kata ya Mjini Joseph Fuime lilisema kuwa miongoni mwa hujuma hizo ambazo alizifanya Dkt Nchimbi ni pamoja na kuchukua sanduku la kura ,kukimbia nalo kabla hajadhibitiwa na kumpa nafasi Naibu Meya wa Manispaa hiyo Mariam Dizumba kuziiba na kukimbia nazo nje ya ukumbi na kutokomea nazo kusikojulikana
Tamko hilo lilisema hujuma nyingine kuwa ni kumwamuru Naibu Meya ambaye si msimamizi wa uchaguzi amtangaze Charles Mhagama ambaye alipata kura za hapana 14 na za ndiyo 12,kumtumia msaidizi wake kuwatisha baadhi ya Madiwani na kutaka kuwatoa nje ya ukumbi huku akijua kuwa msaidizi huyo sio Askari wa Baraza la Madiwani na kutoa lugha ya ufedhuri kwa baadhi ya madiwani wa Manispaa hiyo
Katika tamko hilo pia lilieleza kuwa mnamo Septemba 25 mwaka huu Dkt Nchimbi alitoa taarifa ya uongo kwa vyombo vya habari na kudai aombwe radhi huku akijua anatumia madaraka yake vibaya kuvitisha vyombo vya habari abapo alivituhumu baadhi ya vyombo vya habari kuwa Septemba 23 mwaka huu vilitoa habari inayofanana wakati tarehe hiyo ilikuwa ni mkutano wa Baraza la Madiwani na hakuna chombo kilichoripoti habari hiyo
Tamko hilo lilifafanua kuwa tarehe hiyo kulikuwa na kikao cha Baraza la Madiwani ambacho kilianza saa nne na nusu asubuhi kikiwa na ajenda nne za kufungua mkutano,Uchaguzi wa Mstahiki Meya,Taarifa ya kupitisha kwa mpango na michoro ya Kampuni ya Ardhi Plan kwa mitaa ya Mitendewawa,Namanyigu na Mshangano katika Kata ya Mshangano na ya mwisho ilikuwa ni kufunga mkutano
Lilieleza zaidi tamko hilo Sasa Mh.huyu anashangaza kwani tulipofika ajenda ya pili tu kabla haijaisha kwa msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Mkurugenzi kutangaza matokeo yeye aliingilia kati na kumuamuru Naibu Meya Mariam Dizumba atangaze matokeo na kwa kufanya hivyo vurugu kubwa ilitokea na kikao kusambaratika,sasa yeye anaudanganya umma kuwa kikao kilifungwa majira ya saa 6 mchana
“Sisi Madiwani hatuoni kuwa kuna sehemu huyu Mh.Nchimbi kaonewa,tunavipongeza vyombo vya habari vyote vilivyoripoti kuwa amekimbia na sanduku la kura kwani vilizingatia ukweli wa tukio hilo na tunaamini kuwa vilimtendea haki na kwamba hadi sasa hakuna Meya wa Manispaa ya Songea kwani hakuchaguliwa”lilisema tamko hilo
Akizungumza katika mkutano huo na waandishi wa habari Diwani wa Kata ya Bombambili Kenneth Mbangala alisema kuwa katika uchaguzi wa kumpata Meya taratibu zilivunjwa kwa makusudi ili kumpa nafasi Charles Mhagama kuwa Meya kwani msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Songea Mjini ni Mkurugenzi wa Manispaa Nachoa Zakaria ambaye siku alikuwepo na ndiye aliyepaswa kutangaza matokeo hayo kwani Naibu Meya alikuwa ni mpigakura kama walivyokuwa kuwa madiwani wengine hivyo hakupaswa kutangaza matokeo hayo
Mbangala alisema kuwa licha ya madiwani kumkataa Charles Mhagama ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Matogoro kwa kumpigia kura za hapana 14 na za ndiyo 12 tangazo hilo halikuwa sahihi kwani aliyetangaza ni mtu batili na kufanya uchaguzi huo kuvurugika
Kwa upande wake Mbunge wa Songea Mjini Dkt Emmanuel Nchimbi ambaye pia ni Waziri wa Habari,Utamaduni na Michezo alipoulizwa kwa njia ya simu yake ya kiganjani kuhusiana na madai ya kuhujumu uchaguzi huo alisema kuwa hahusiki na hujuma hizo ikiwemo ya kukimbia na sanduku la kura
Dkt Nchimbi alisema kuwa sio vyema kwa kiongozi kama yeye kumsingizia mambo kwani kunaweza kumsababisha kushuka kwa morali ya utendaji kazi wake katika utumishi wa umma na kuwataka madiwani hao kuwatumikia wananchi wao badala ya kuzungumzia sakata la uchaguzi wa Meya
MWISHO
Saturday, October 8, 2011
RAIS KIKWETE VURUGU ZA UMEYA SONGEA DKT NCHIMBI AMEKUZALILISHA
Rais Jakaya Mrisho Kikwete
DKT Emmanuel Nchimbi aliyeshika kipaza sauti
DKT Emmanuel Nchimbi aliyeshika kipaza sauti
Charles Mhagama Diwani wa Kata ya Matogoro ambaye anadaiwa kuwa Chaguo la Dkt Nchimbi katika nafasi ya UMEYA
Na Gideon Mwakanosya,Songea
SAKATA la uchaguzi wa Meya Mjini Songea Mkoani Ruvuma lililopelekea kupitishwa kwa Charles Mhagama kuwa Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa utata mkubwa limezidi kuchukua sura mpya ambapo baadhi ya madiwani wa CCM wameanza kususia vikao vinavyoitishwa na Chama chao wilayani humo.
Ikumbukwe hivi karibuni katika Manispaa hiyo kulifanyika uchaguzi wa Meya wa Manispaa hiyo ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Meya aliyefariki miezi michache iliyopita marehemu Ally Manya.
Lakini kabla sijachambua kwa ufupi na kuchambua jinsi mkutano huo ulivyokuwa nieleze jinsi mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM ulivyokuwa na jinsi ulivyotawaliwa na mizengwe ya kila namna.
Baada ya kutangazwa uchaguzi wa kura za maoni ndani ya CCM madiwani wanane na kada mmoja wa Chama hicho walichukua fomu za kuomba kuteuliwa na Chama hicho ili mmoja kati yao agombee nafasi hiyo akichuana na mgombea atakayechaguliwa na Chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA).
Licha ya Nchimbi kuhojiwa na Mwandishi wa makala hii kama alikuwa akimtaka Meya aliyepitishwa kwa kupindua matokeo Charles Mhagama lakini habari zilivuja baada ya habari kusambaa kuwa alisambaza meseji za simu zikitaka madiwani wapitishe Mhagama kuwa Meya wa Manispaa ya Songea.
Madiwani na makada wa Chama hicho walionya tabia ya Nchimbi kuwachagulia kiongozi anayemtaka yeye ili afuate matakwa yake lakini Nchimbi alikanusha uvumi wa habari hizo zilizoenea katika viunga vya Mji wa Songea na kuthibitisha kuwa zilikuwa na chembe ya ukweli fulani.
Kiongozi mmoja wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Songea ameuambia mtandao huu wa www.stephano mango.blogspot.com kuwa Nchimbi alibanwa kwenye kikao cha kamati ya siasa kilichofanyika Septemba 25 mwaka huu kuwa yeye ndiye aliyesababisha vurugu zilizotokea kwenye uchaguzi wa Meya uliofanyika kwenye Ukumbi wa SACCOS ya Manispaa 23 Septemba kwa kulazimisha mtu anayemtaka kuwa ndiye awe Meya.
Mmoja wa Madiwani machachari wa Chama hicho Manispaa ya Songea ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema madiwani walibanwa kwenye vikao vya Chama hicho ili wachague diwani huyo asiyekubalika kuwa ndiye agombee Umeya na vikao vya Chama hicho vikapendekeza jina lake na majina ya madiwani wawili wanawake na kuyakata majina ya madiwani wanaokubalika.
Majina yaliyopitishwa na vikao vya Chama hicho ili wakapigiwe kura na madiwani wa CCM ni Mariam Dizumba,Genifrida Haule na Charles Mhagama na katika uchaguzi wao wa CCM walibanwa ili wamchague Mhagama ili apeperushe bendera ya CCM’anasema diwani huyo’.Anasema kuwa Mariam Dizumba ambaye pia ni mke wa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Mjini Hemedi Dizumba hata kura yake mwenyewe alijinyima hivyo aliambulia sifuri.
Anasema kuwa kwa kumuonyeshea au kumkomoa Nchimbi wakaamua kumpigia kura diwani huyo ili wakamuumbue kwenye uchaguzi wa jumla ambao ungevipambanisha Chadema na CCM kwa kumpigia kura za hapana au maarufu kwa kura za maruhani.
Hata hivyo Katibu wa CCM Songea mjini Alphonce Siwale alipoulizwa kuhusiana na ushawishi wa Nchimbi wa kumtaka Mhagama awe Meya alisema kama alituma ujumbe wa simu wa kuwataka madiwani wa CCM kumchagua diwani huyo alisema alifanya hivyo kwa ushawishi wake binafsi.
Katika uchaguzi uliofanyika 23 Septemba mwaka huu Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) hakikusimamisha mgombea hivyo kukatokea majadiliano ni jinsi gani uchaguzi utakuwa huru na wa haki kwa kuwa Chadema hawakusimamisha mgombea.
Kutokana na hali hiyo ndipo Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Nachoa Zakaria ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo alisimama na kutoa ufafanuzi wa kanuni za uchaguzi wa nafasi hiyo na kusema wanatakiwa kupiga kura za ndiyo kama wanamtaka mgombea huyo na ikiwa hawamtaki basi wanatakiwa kupiga kura za hapana.
Sipendi nirudie yale yaliyoandikwa na wenzagu lakini napenda kujadili muktadha mzima uliozunguka tukio hilo na ni nani alisababisha kama vile Chemsha bongo ya yai na kifaranga cha kuku nini kilianza.
Katika uchaguzi huo ni wazi kabisa kanuni zilivunjwa baada ya kubainika kuwa Charles Mhagama alipigiwa kura za Hapana 14 na za ndiyo 12 na waswahili husema kwa nini tuandikie mate wakati wino upo?hivyo basi kama uchaguzi ule ulikuwa huru na wa haki na kanuni hazikuvunjwa basi kura zingehesabiwa tena kabla ya Naibu Meya kuiba kura na kuziweka kwenye kipima joto chake kidogo na kukificha sehemu zake za siri.
Baada ya kupigwa kura na kuhesabiwa hadharani Msimamizi wa uchaguzi Nachoa alimwonyesha matokea Dizumba ndipo alipotaka kusoma alionyesha mstuko mbele ya madiwani na kumuonyesha Nchimbi ambaye alimuamuru kuyasoma kwa kuyapindua na alipoyasoma madiwani wakataka kura zirudiwe kuhesabiwa kwa madai alichokitangaza hakikuwa na ukweli.
Hapo ndipo kulitokea vurumai kubwa na ndipo Naibu Meya huyo alipopigwa mtama na diwani wa Kata ya Mjini kupitia Chadema Joseph Fuime na kuanguka chini kisha kuinuka kukimbilia nje na kura alizokwapua na hapo ndipo diwani huyo alipomwendea Nchimbi na kumwambia ni aibu kwake kusimamia wizi wa kura.
‘Ni aibu kubwa kwa Waziri kama wewe kusimamia wizi wa kura na hapa huwezi kunifanya chochote kwa kuwa Uwaziri wako ni nje ya ukumbi huu na tukiwa ndani humu wewe ni diwani kama mimi na utambue kuwa Songea wamechoka na tabia yako ya kuwachagulia viongozi’alisema diwani huyo huku akiwa amemkodolea macho Nchimbi ambaye alikuwa akinon’gonezana jambo na diwani wa Matarawe James Makene.
Wakati akitoka nje ndipo alipopokewa na watu waliokuwa nje ya ukumbi huo ambao walikuwa wakimwimbia Nchimbi mwizi wetu na yeye alionekana akizungukazunguka akichezea simu asijue la kufanya hadi pale alipokuja dereva wake na gari na kumpakia na kisha kuondoka eneo hilo ambalo lilikuwa lina vurumai kubwa.
Baada ya Naibu Meya kutoka nje ya ukumbi alikimbilia kwenye gari moja na kuingia huku akifuatwa na madiwani wawili wa Chadema ambao walikuwa wakimzuia asikimbie na kura,katika sakata hilo Kada wa CCM Hamis Abdalah Ally alitaka kumgonga na gari diwani wa Mfaranyaki(CHADEMA) Salumu Mfamaji ambaye alikuwa mbele ya gari hiyo.Kada huyo wa CCM alifanikiwe kumkimbiza Naibu Meya huyo ili asiweze kupigwa.
Baada ya tukio hilo maneno yalizagaa mitaani kwamba Nchimbi ametishia kuwanyang’anya kadi madiwani saba wanaodaiwa kupiga kura za hapana dhidi ya mgombea pekee wa Chama chake,jambo ambalo lilijadiliwa na wachunguzi wa masuala ya siasa kwamba wanawezaje kuwanyang’anya kadi madiwani hao wakati kura ni siri ya mtu na wao wamewajuaje?.
Siku ya pili baada ya tukio hilo Nchimbi ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Songea Mjini na Waziri wa habari utamaduni na michezo alipigiwa simu na mwandishi wa habari wa Gazeti la Majira Joseph Mwambije ili kutaka kujua kama kweli aliwatisha madiwani hao kuwanya’nganya kadi alisema hawezi kufanya hivyo kwa kuwa kanuni na taratibu za Chama hicho anazijua.
Lakini pia alisema kuwa waandishi ni wajinga na wapumbavu kwa kuwa wameandika habari za uongo kuwa yeye amekimbia na sanduku la kura.
Septemba 25 mwaka huu aliitisha mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea na kutoa tamko la kukanusha kuwa yeye hakukimbia na sanduku la kura akiyatuhumu magazeti matatu ya kila siku kwa kumuandika habari za kumchafulia jina.
Ama kwa hakika Nchimbi amechanganyikiwa na tukio lile limemchanganya pengine na kupunguza kasi yake ya mbio za Urais wa mwaka 2015 kwani yeye katika tamko lake anayatuhumu magazeti yaliyoandika habari hiyo Septemba 23 lakini ukweli ni kwamba siku hiyo ndiyo kilifanyika kikao cha Baraza la madiwani na hakuna gazeti lililoandika habari hiyo siku hiyo bali magazeti yaliripoti habari za tukio hilo Septemba 24 mwaka huu.
Harakati za Waziri huyo kijana kukanusha tuhuma hizo zitaishia kumuumbua zaidi ikiwa picha za video zitaonyeshwa kwenye halaiki ya watu kwa kuwa yeye Nchimbi anasema hakuna diwani aliyetoka nje ya ukumbi huo na kura lakini kama hakuna diwani aliyetoka nje ya ukumbi na kura,Mariam Dizumba kwa nini alitoka ndani ya ukumbi akikimbia na kwanini alipigwa ngwala na kudondoka na kwa nini aliondoka wakati kikao hakijafungwa?
Pia katika tamko lake anasema Meya aliyechaguliwa alifunga mkutano lakini ukweli ni kwamba mkutano au kikao hicho hakikufungwa hivyo kiliparaganyika baada ya utaratibu mzima na kanuni za uchaguzi huo kuvurugwa kwa kuwa aliyetakiwa kutangaza matokeo hayo ni Mkurugenzi wa Manispaa na si Naibu Meya ambaye ni mpigakura kwenye uchaguzi huo na pia ana maslahi.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanahoji ni kwa nini CCM Songea Mjini imetoa mapendekezo ya kuwafukuza uanachama madiwani watano kati ya saba waliopiga kura za hapana dhidi ya Mhagama wakati mwaka 2007 hawakumchukulia hatua Mariam Dizumba ambaye alipiga kura ya hapana kwa Elizabeti Ngongi ambaye alishinda unaibu meya kwenye uchaguzi wa mwaka huo na akaenda mahakamani kuzuia uchaguzi huo.
Katika sakata la mwaka huo Manispaa hiyo ilikaa bila Naibu Meya kwa miezi mitano hadi pale nafasi hiyo alipopewa Mariam Dizumba ambaye alishindwa na ndipo akaamua kufuta kesi sasa madiwani hao watano na huyu aliyekishtaki Chama chake,Mkurugenzi na Elizabeti Ngongi yupi mwenye kosa kubwa?
Anaendelea kusema katika tamko lake’mkutano huu wa madiwani ulirekodiwa kwa picha za video,mikanda ya picha hizo ipo inaweza kupatikana kwa ushahidi’anasema.Lakini picha hizo za video zinaonyesha akizomewa kwa kuitwa mwizi wa kura na huku akielezwa kuwa ni aibu kwake kusimamia wizi wa kura na kama alionyeshwa picha hizo basi alionyeshwa sehemu tu ya picha za tukio.
Lakini ni katika mkutano huo ndipo alipobanwa na waandishi wa habari athibitishe ujinga na upumbavu wao na ikiwa atashindwa kufanya hivyo afute kauli yake na atoe ufafanuzi kuhusu madai yake kwamba habari hizo zimeandikwa na mtu mmoja na kwamba katika tukio hilo amemdhalilisha Rais kwa nini asijiuzulu kwa kumdhalilisha Rais aliyemteua?
Nchimbi alishindwa kuyajibu maswali hayo na kupandwa na jazba na kutoa maelezo ambayo hayahusiani na maswali aliyoulizwa na kushusha heshima yake.
Wakati hali ikiwa hivyo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na maendeleo(CHADEMA)Mkoa wa Ruvuma Joseph Fuime anasema kuwa kwa tukio lile ingekuwa enzi ya Mwalimu Nyerere Nchimbi angejiuzulu.
Akihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Shule ya msingi mfaranyaki maarufu kama Soko la samaki Fuime alisema ni aibu kwa Manispaa ya Songea ambayo ni maskini kumchagua Meya aliyedai kuwa ni mwizi aliyehusika na uuzaji wa greda kwa shilingi milioni 18, na ununuzi wa gari bovu la Zimamoto kwa shilingi milioni 350 ambapo Mhagama alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo alisema greda liliuzwa kwa kufuata sheria zote na kuhusu gari bovu la Zimamoto halimuhusu kwani magari hayo yalinunuliwa saba Nchi nzima.
Alisema huo ni mpango wa wabunge kuwaweka watu wao kwenye nafasi za uongozi ili waibe fedha na kwamba walifanya makosa kumchagua Nchimbi na wangemchagua aliyekuwa mgombea wa Chadema Edson Mbogoro asingewaletea Meya mwizi.’Anamtaka Meya huyo ili ajinufaishe na mimi nasema Charles Mhagama atakuwa Meya wa Mbunge si wa madiwani na akipita mitaani mumzomee Meya huyo’alisema.
Alisema hiyo ni aibu kwa Rais aliyemteua na kwamba Chama Chake kimejipanga kuzunguka kata zote 21 kueleza ubaya wa Nchimbi na mwenendo mzima wa uchaguzi wa Meya na kueleza kuwa Manispaa hiyo haina Meya hivyo baada ya mikutano hiyo watafanya maandamano makubwa ya kupinga uchaguzi huo na kumpinga Meya huyo na kuvigeuza viwanja vya manipsaa hiyo kuwa Tahariri Squere ambavyo vilim’ngoa madarakani aliyekuwa Rais wa Misri Hosni Mubarak.
Hivyo basi ili kunusuru vurugu zitakazotokea kwenye maandamano yanayotarajiwa kufanyika ni wazi basi inatakiwa kurudia uchaguzi kwa kuwa uchaguzi uliofanyika ulikiuka utaratibu na CCM wana wasiwasi gani kurudia uchaguzi?Hapa ndipo Intelejensia ya Polisi inapaswa kufanya kazi kunusuru hali ya hewa ili yasije yakatokea mauaji kama yale yaliyotokea Arusha.
Mapendekezo ya CCM Wilaya ya Songea kufukuza madiwani waliopiga kura za hapana kwa mgombea wa Chama hicho yamepokelewa na Chama hicho Mkoa wa Ruvuma ili yaweze kutolewa maamuzi na Katibu wa Chama hicho Mkoa huo Emmanuel Mteming'ombe amesema Kamati ya maadili ya Chama hicho imewahoji madiwani hao ambao anasema kwenye Kamati ya siasa Wilaya hawakusikilizwa na kamati ya siasa Mkoa itatoa uamuzi wa kuwafukuza au kutowafukuza.
Hata hivyo wachunguzi wa mambo wa siasa wanasema madiwani hao hawatafukuzwa na kamati hiyo kwa kuwa ni kiongozi mmoja pekee na genge lake ndiye anayeshinikiza wafukuzwe na kwamba hawajafanya kosa linalofanya wafukuzwe na ikiwa watafukuzwa kwa upepo wa siasa Songea upande wa chama hicho si mzuri na kata hizo zinaweza kudondokea upinzani.
Hivi karibuni CCM Wilaya ya Songea mjini iliitisha kikao na madiwani wake kwa ajili ya kusafisha hali ya kisiasa ambayo imechafuka lakini hakikuweza kufanyika kutokana na madiwani kukisusia kwa kile kinachodaiwa kuwa ni mgomo wa kudumu kushinikiza kujiuzulu kwa Meya huyo anayedaiwa kupitishwa kwa mizengwe huku nguvu ya kigogo mmoja ikitajwa kuhusika.
Lakini pia katika kikao hicho madiwani waliopendekezwa kufukuzwa waliitwa na walifika wakiwa na kadi zao mfukoni tayari kwa kuzikabidhi ikiwa wataambiwa watoke kwenye Chama hicho.
Katibu wa CCM wa Wilaya ya Songea mijini Alphonce Siwale alipohojiwa kuhusu kuitishwa kwa kikao hicho alithibitisha kukiitisha na kusema kuwa kilishindikana kufanyika kutokana na mahudhurio hafifu ya madiwani ambao hawakufika hata nusu.
Alisema kuwa madiwani wengi walishindwa kuhudhuria kikao hicho kwa kuwa walikuwa safarini na kwamba kitafanyika tena kitakapopangwa na kilipaswa kusafisha hali ya hewa iliyochafuka kutokana na uchaguzi wa Meya.
Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa anapaswa kumuondoa Nchimbi kwenye nafasi ya Uwaziri wa habari,utamaduni na michezo kwani kwa tukio lile alimdhalilisha na aibu ile itamfuata Nchimbi kokote atakakokwenda iwe Dares salaam,Dodoma,Mbeya na Songea hivyo basi aibu ya Nchimbi ni aibu ya Kikwete aliyemteua.
MWISHO
Friday, October 7, 2011
NI NGUMU KUAMINI,LAKINI ASHIKILIWA NA POLISI KWA KUSABABISHA KIFO AKILAZIMISHA PENZI
Na Mwandishi Wetu, Songea
JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma limemtia mbaroni Elly Millinga (33) Mkazi wa Kijiji cha Matiri Wilayani Mbinga kwa tuhuma za kumchoma kisu sehemu za tumboni Mzazi mwenzake Florida Mhaiki (26) Mkazi wa mtaa wa Masumuni Mbinga mjini ambaye anadaiwa alikataa kufanya nae mapenzi
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Naftan Mantamba alisema kuwa tukio hilo lilitokea Octoba 7 mwaka huu majira ya saa 6.30 huko katika Mtaa wa Masumuni Mbinga mjini.
Mantamba alifafanua kuwa siku hiyo ya tukio Florida alichomwa kisu sehemu za tumboni na mzazi mwenzake Millinga ambaye alifika nyumbani kwa Florida majira ya saa za jioni ya Octoba 6 mwaka huu na kuanza kuongea nae kwa lengo la kumshawishi mzazi mwenzake waendelee kuishi kama mke na mume
Ameeleza zaidi kuwa Millinga pamoja na kutoa ushawishi huo Florida alikataa katakata na kudai kuwa watoto wawili aliozaa nae ameshindwa kuwahudumia hivyo hakuna sababu yeyote ya msingi ya kuridhia kurudiana na Millinga.
Amesema kuwa ilipofika majira ya saa 3 usiku ya Octoba 6 mwaka huu usiku Florida alimweleza mzazi mwenzake Millinga kuwa muda wa kwenda kulala umefika hivyo aliamua kumpatia nafasi ya kulala chumba ambacho kipo uani mwa nyumba kubwa na Millinga alienda kulala.
Amefafanua zaidi kuwa ilipofika saa 6 usiku Millinga aliamka na kwenda hadi kwenye chumba ambako Florida alikuwa amelala na kumtaka amfungulie mlango na baada ya kuingia aliendelea kumsihi Florida ili akubaliane na ombi alilomweleza hapo awali lakini ombi hilo halikuweza kukubalika ndipo Millinga alipoamua kuchukua kisu mfukoni na kumchoma sehemu za tumboni.
Ameeleza zaidi kuwa Florida baada ya kuchomwa kisu na mzazi mwenzake alipiga kelele kwa lengo la kupata msaada majirani walifika kwenye eneo la tukio na kumkuta Florida akiwa kwenye hali mbaya na kwenye chumba chake kulikuwa kumetapakaa damu.
Amesema kuwa majirani walimchukua Florida na kumkimbiza kwenye hospitali ya Serikali ya Mbinga kwa matibabu ambako alifari dunia wakati akiwa anaendelea kupata matibabu na polisi baada ya kupata taarifa ya tukio hilo walikwenda kwenye eneo la tukio na walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Millinga ambaye kwasasa anaendelea kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.
MWISHO
Thursday, October 6, 2011
AJINYONGA KWA KUMKATAA MKE MWENZA WILAYANI MBINGA
Na Gideon Mwakanosya, Songea
MWANAMKE mmoja Apolonjali Hyera (45) Mkazi wa Kitongoji cha Mapendano kilichopo katika Kijiji cha Mzuzu Wilayani Mbinga amekufa kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani baada ya mume wake kuoa mwanamke mwingine.
Habari zilizopatikana jana mjini hapa ambazo zimethibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Naftani Mantamba zimesema kuwa tukio hilo limetokea Octoba 5 mwaka huu majira ya saa 6 mchana huko katika Kitongoji cha Mapendano kilichopo katika Kijiji cha Mzuzu Wilayani Mbinga.
Mantamba amesema kuwa siku hiyo ya tukio inadaiwa Apolonjali alikutwa akiwa amejinyonga kwa kutumia kamba ya katani kwa kujining’iniza juu ya mti kwenye msitu mkubwa wa Kijiji hicho.
Ameeleza zaidi kuwa Apolonjali anadaiwa kuwa aliamua kujinyonga baada ya kumtuhumu mume wake kuamua kuoa mwanamke mwingine wakati yeye ametoka nyumbani kwa wazazi wao na yupo kwaajili yake hivyo alikuwa akijiuliza ni kwanini ameamua kuchukua uamuzi huo.
Amefafanua zaidi kuwa kutokana na kuwepo kwa mvutano huo kati yake na mume wake Kelvin Sesilisi (45) ndiyo aliamua kuchukua uamuzi wa kujiua na kuacha maagizo kuwa ameamua aondoke amuache mwanamke aliyempata
Mantamba amesema kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi ambao umemsababishia Apolonjali kufikia uamuzi wa kujiua kwa kujinyonga kwa kujining’iniza kwenye mti uliopo katikati ya msitu
ANYWA SUMU,AFARIKI BAADA YA KUONYWA KUACHA UASHERATI MBAMBABAY
Na Mwandishi Wetu,Songea
JANETH Mwanjali ni msichana mwenye umri wa miaka 15 mkazi wa mji mdogo wa Mbamba bay uliopo Wilayani Nyasa Mkoa wa Ruvuma amefariki dunia baada ya kunywa dawa ya kuulia panya iliyokuwa imehifadhiwa nyumbani kwa wazazi wake.
Akizungumza na mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Naftani Mantamba amesema kuwa tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 4 asubuhi nyumbani kwa wazazi wa Janeth.
Mantamba amesema kuwa siku hiyo kabla ya tukio kutokea inadaiwa kuwa Janeth aliitwa na mama yake mzazi Anna Kalima ambaye alikuwa akimuonya aache tabia ya kulala kwa wanaume na baadaye ulitokea ugomvi kati yake na mama yake ambaye alikuwa akimtuhumu kuwa anamuonea wivu kisha alikwenda ndani ya nyumba na kutafuta dawa ya kuulia panya ambayo aliinywa.
Amesema kuwa baada ya kuinywa dawa hiyo muda mfupi alianza kubadilika na hali yake ikawa mbaya hivyo mama yake mzazi aliamua kumchukua na kumpeleka hadi Kituo cha afya cha Mbamba bay ambako muda mfupi baadaye alifariki dunia akiendelea kupatiwa matibabu.
Mantamba amesema kuwa Chanzo cha tukio hilo ni kwamba Janeth alikuwa amegombana na mama yake mzazi aliyekuwa akimkanya kuwa aache tabia ya kulala nje kwa wanaume jambo ambalo lilimtia hasirá na kuchukua uamuzi wa kutafuta dawa ya kuulia panya na kunywa kwa lengo la kujiua.
Hata hivyo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Mantamba ameeleza kuwa kwasasa Polisi wanaendelea kufanya upelelezi wa kina kuhusiana na tukio hilo licha ya kuwa Upelelezi wa awali umebaini kuwa Janeth alipandwa na hasira wakati anaonywa na mama yake mzazi.
Wednesday, October 5, 2011
MADIWANI WA CCM SONGEA WASUSIA KIKAO CHA CHAMA CHAO NA WENGINE WAWATUPIA MADONGO VIONGOZI WAO
Na Mwandishi Wetu,Songea
MADIWANI wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Mjini wamesusia kikao kilichoitishwa na viongozi wa Chama hicho Wilaya kwa kile kilichodaiwa ni mgomo wa kudumu kushinikiza kujiuzuru kwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Charles Mhagama
Wakizungumza na waandishi wa habari jana kwa nyakati tofauti nje ya Ofisi ya Chama hicho ambapo kikao hicho kilipangwa kufanyika walisema kuwa wameshtushwa na taarifa ya kuitwa kwenye kikao hicho bila kuelezwa ajenda zake wala muda wa kukaa kikao hicho
Walisema kuwa wamefika kwenye kikao hicho wameshindwa kuwaona baadhi ya viongozi wa Chama hicho ambao ndio waliowaita kitendo ambacho kinaonyesha ni dharau dhidi ya madiwani
Baadhi ya Madiwani hao Christian Matembo wa Kata ya SeedFarm,Kurabest Mgwasa wa Kata ya Msamala na Faustine Mhagama wa Kata ya Mshangano walisema kuwa kiu kubwa ya Madiwani ni kutaka kuona Charles Mhagama ambaye anadaiwa kuwa ni Mstahiki Meya anajiuzuru ili uchaguzi mpya uitishwe kwani kura alizopata wakati wa uchaguzi hazikuwa halali
“Tumechoka kuogopana ndani ya chama kwa kuwaacha wachache wanawaburuze wengi kwa maslahi yaliyojificha kwani hatuwezi kuvumilia vitendo vya uvunjifu wa demokrasia vya kuwatisha madiwani waliotimiza haki yao ya kupiga kura za hapana kwenye uchaguzi wa umeya uliopita hivi karibuni kwa kuwaita ni wasaliti wa chama”alisema Matembo
Alisema kuwa Madiwani wengi wamempigia kura za hapana Charles Mhagama lakini tunashangaa kuona mtu huyo anatembelea gari ya Mstahiki Meya na kufanya kazi kama Meya wakati siku ya kupiga kura uchaguzi ulivurugika na kusababisha madiwani kushikana kutokana na kumkataa Mhagama
Diwani wa Kata ya Mshangano Faustine Mhagama ambaye pia ni Katibu wa Madiwani wote wa Ccm alisema kuwa kitendo cha Viongozi wa Ccm Wilaya cha kupendekeza Madiwani watano wa Chama hicho wavuliwe uanachama ni kuongeza mpasuko ndani ya chama kwani kura walizopiga zilikuwa za siri hivyo kuwahukumu hao ni kuwanyanyasa na kuwanyima haki zao za msingi
Mhagama alisema kuwa kanuni za kudumu za Halmashauri zina eleza kuwa jambo lolote litakalo fanyika kwenye kikao cha Baraza la Madiwani halipaswi kuhojiwa wala kujadiliwa na mamlaka nyingine hivyo Ccm Wilaya ya Songea Mjini kupitia Kamati ya Maadili na y a Siasa kuwahoji Madiwani kwa kile kilichotokea kwenye Baraza ni kukiuka kanuni na kusababisha utendaji wa kosa kwa makusudi na kuendekeza makundi bila sababu ya msingi
“Ili kulinda heshima ya Chama ni Vema Charles Mhagama aridhie kujiuzuru nafasi hiyo ili uchaguzi urudiwe upya badala ya kuwanyanyasa baadhi ya Madiwani wanaodaiwa kupiga kura za hapana na kupelekea Diwani huyo kupitishwa kwa kura za hapana 14 na za ndiyo 12”alisema Mhagama
Alisema kuwa Madiwani wataendelea kususia vikao vitakavyoitishwa na Chama na Halmashauri ya Manispaa ya Songea mpaka uitishwe uchaguzi mwingine ambapo Madiwani watamchagua kiongozi watakaomuona anafaa na sio kulazimishiwa kiongozi
Naye Diwani wa Kata ya Msamala Kurabest Mgwasa alisema kuwa Ccm Wilaya imependekeza Madiwani watano wavuliwe uanachama ambapo hatma yao ipo kwenye ngazi ya Chama hicho Mkoa lakini cha kushangaza Madiwani hao nao wameitwa kwenye kikao hicho jambo ambalo lingeweza kuleta vurugu kubwa
Kwa upande wa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Mjini Alfonce Siwale alikiri kuitisha kikao hicho ambacho kilipaswa kifanyike jana lakini kilishindikana kutokana na mahudhurio hafifu ya Madiwani ambao hawakufika hata nusu yao
Siwale alisema kuwa kikao hicho kilikuwa na agenda za kutaka kurudisha hali ya hewa sawa kutokana na vurugu za uchaguzi wa umeya uliofanyika Septemba 23 mwaka huu ambao haukumalizika
Alisema kuwa Madiwani wengi wameshindwa kuhudhuria kikao hicho kwa kuwa wapo safarini na hivyo kikao hicho kimepangwa kufanyika Octoba 11 katika ofisi za Chama hicho na kueleza kuwa Madiwani hao hawana mgomo wowote
Alieleza kuwa Chama hicho kina Madiwani 21 lakini waliofika kwenye kikao hicho walikuwa nane na kufanywa kikao hicho kutofanyika na kwamba kwenye kikao hicho Madiwani waliopendekezwa kufukuzwa na chama ndio waliojitokeza kwa wingi
MWISHO
Tuesday, October 4, 2011
TAKUKURU WAMNASA AFISA MTENDAJI WA KATA WA HALMASHAURI YA MANISPAA YA SONGEA KWA RUSHWA KIDUCHU
Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Shule ya Tanga Expedito Luambano(aliyesimama)
Na Mwandishi Wetu ,Songea
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoani Ruvuma inamshikilia Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Shule ya Tanga iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya shilingi 20,000 kutoka kwa mwananchi ambaye jina lake limehifadhiwa wa Kata hiyo ambaye alikwenda Ofisini kwake kuomba asaidiwe kulipwa deni toka kwa Mfanyabiashara mmoja ambaye naye jina lake limehifadhiwa.
Akizungumza na mtandao huu wa www.stephanomango.com Ofisini kwake Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoani Ruvuma Daudi Masiko amesema tukio hilo limetokea Octoba 2 mwaka huu majira ya saa za mchana huko kwenye eneo la nane nane Msamala Songea Mjini.
Masiko amemtaja anayeshikiliwa na Takukuru kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya shilingi elfu 20,000 Expedito Luambano (36) ambaye ni Kaimu Afisa Mtendaji wa Shule ya Tanga ambapo amebainisha zaidi kuwa siku chache zilizopita Luambano akiwa Ofisini kwake alifikiwa na mwananchi mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa ambaye alikuwa anataka asaidiwe na Ofisi hiyo ili Mfanyabiashara anayemdai aweze kumlipa deni ambalo ni la muda mrefu.
Amefafanua zaidi kuwa mwananchi huyo akiwa kwenye Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata hiyo alishawishiwa na Luambano kuwa atafute shilingi elfu 20,000 ili aweze kumsaidia kumsaka Mfanyabiashara huyo anayemdai aweze kulipwa deni .
Ameeleza kuwa mwananchi huyo alikubaliana na maelezo aliyopewa na Luambano kisha alitoka kwenye Ofisi hiyo kwa makubaliano kuwa wangekutana kwenye eneo la nane nane lililopo Msamala kwenye bar iliyopo kwenye eneo hilo.
Amesema kuwa mwananchi huyo baadae alishtuka na kupata wazo kwenda kwenye Ofisi za Takukuru ambako alitoa taarifa na kuwaeleza kwa kina juu ya maelezo aliyopewa na Afisa Mtendaji Luambano ambapo baadae Maafisa wa Takukuru waliweka mtego kisha walimtaka mwananchi huyo awasiliane na Afisa Mtendaji mahali watakapokutana kupeana fedha hizo.
Mkuu wa Takukuru Mkoani Ruvuma Masiko amesema kuwa baada ya mwananchi huyo kufanya mawasiliano na Afisa Mtendaji Luambano Takukuru ilimpatia fedha shilingi elfu 20,000 na kumtaka ande mahali walipokubaliana kupeana fedha hizo huku maafisa wa Takukuru wakiwa wanamfuatilia kwa karibu na walipofika kwenye eneo la tukio alimkuta Luambano akiwa anamsubiri kwenye bar ambako alimkabidhi fedha hiyo na baada ya muda mfupi maafisa wa Takukuru waliizingira bar hiyo na kumkuta Luambano akiwa na fedha shilingi elfu 20,000 aliyopewa na mwananchi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa.
Amefafanua zaidi kuwa Luambano ambaye pia ni Afisa Mtendaji wa Serikali wa Mtaa wa Tanga anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya shilingi elfu 20,000 ambayo ni kosa chini ya kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007
MWISHO
MAJAMBAZI WAPORA,WAJERUHI ABIRIA NA KUSABABISHA KIFO CHA MTOTO
Na Mwandishi Wetu,Songea.
JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma linawasaka majambazi wawili ambao walivamia gari lililokuwa limebeba abiria 14 kutoka Mbamba bay kwenda Mbinga na kufyatua risasi tano ambazo ziliwajeruhi watu wawili akiwemo mtoto wa umri wa mwaka mmoja na nusu ambaye alikuwa amepigwa risasi kwenye mguu wa kushoto akiwa amebebwa na mama yake mzazi kisha majambazi hao walifanikiwa kuwapora abiria fedha Shilingi 930,000 na baadaye walikimbia na kutokomea kusikojulikana.
Akizungumza na mtandao huu wa www.stephanomango.blogspot.com Ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amesema kuwa tukio hilo lilitokea Octoba 3 mwaka huu majira ya saa 1.30 asubuhi huko katika Kijiji cha Ng’ombo kilichopo katika Kata ya Kilosa Wilaya ya Nyasa .
Kamuhanda amesema kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio Dereva wa gari lenye namba za usajili T 554 ASE Toyota Hilux Joseph Hamza (35) akiwa anaendesha gari hilo lililokuwa na abiria 14 waliokuwa wanatoka Mbamba bay kuelekea Mbinga Mjini akiwa katikati ya daraja ghafla aliwaona watu wawili wakiwa wamefunga vitambaa usoni huku wakiwa na Bunduki mbili ambao walilivamia gari hilo kisha walianza kufyatua risasi hewani ambazo ziliwajeruhi abiria wawili .
Amefafanua kuwa watu hao wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi ambao walikuwa na siraha za SMG na SAR waliwapiga risasi Rehema Haule (11) ambaye alijeruhiwa vibaya kwenye mguu wa kushoto wakati akiwa amebebwa na mama yake mzazi na Castory Kinunda (31) Mkazi wa Mbamba bay alijeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi na majambazi hao kwenye mkono wa kushoto .
Amebainisha zaidi kuwa majambazi hao baada ya kufyatua risasi hewani walianza kuwapekua abiria mmoja hadi mwingine ambapo baadae walifanikiwa kuwapora abiria hao shilingi 930,000 na baada ya kuwanyang’anya fedha hizo walikimbia na kutokomea porini .
Alieleza zaidi kuwa majeruhi Rehema baada ya kupigwa risasi kwenye mguu wa kushoto alikimbizwa katika Hospitali ya Misheni ya Liuli ambako alifariki dunia muda mfupi wakati akiendelea kupata matibabu na majeruhi Kinunda kwasasa hivi amelazwa katika hospitali ya Serikali ya Mbinga akiendelea kupata matibabu na hali yake bado ni mbaya.
Kamanda Kamuhanda amesema kuwa Polisi baada ya kupata taarifa ya tukio hilo walienda kwenye eneo la tukio na kuwakuta baadhi ya abiria ambao walielezea tukio hilo lilivyotokea na kwamba upelelezi wa awali umefanyika ambao umebaini kuwa majambazi hao wametokea Kyela Mkoani Mbeya kwa kupitia Ziwa Nyasa.
MWISHO
VIONGOZI WA DINI WAOMBWA KUWANUSURU WANAFUNZI WA MTONYA NA MAPEPO
Na Augustino Chindiye,Tunduru
SHULE ya Msingi Mtonya Wilayani Tunduru imefungwa kwa muda usiojulikana ili kuwapisha Wazee wa mila,Mapadre na Mashehe ili wawasaidie kuomba na kuyaondoa Mapepo ambayo yamekuwa yakisababisha Wanafunzi wanaosoma katika Shule hiyo kupatwa na homa ya kuchanganyikiwa na kuanguka wakati wa masomo.
Amri ya kufungwa kwa Shule hiyo imetolewa na Afisa elimu wa Shule za Msingi Mwl. Rashid Mandoa baada ya juhudi za maafisa tabibu kutoka katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru kushindwa kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.
Mwl. Mandoa aliendelea kufafanua kuwa tatizo la kuanguka na kupoteza fahamu kwa wanafunzi hao limekuwa likiongezeka siku hadi siku ambapo awali idadi ya watoto waliokuwa wakianguka walikuwa ni kati na watoto mmoja na watano lakini hivi sasa tatizo hilo limefikia zaidi ya watoto hamsini kwa siku.
Alisema kufuatia hali hiyo wazazi wa watoto wanaosoma katika shule hiyo walikuwa wakilazimika kufuatana na watoto wao na kupiga kambi pembezoni mwa shule wakiwa na lengo la kuwasaida watoto watakao kumbwa na homa hiyo.
Alisema ingawa Serikali haiamini mambo ya ushirikina lakini idara yake imechukua maamuzi hayo baada ya kubaini kuongezeka kwa matukio hayo na kwamba endepo tatizo hilo litaachiliwa liendelee kuna
hatari ya kushusha kwa taaluma za wanafunzi kutakakosababishwa na kushuka kwa ari ya wanafunzi kutopenda masomo.
Mwisho.
BUNGE LATAKIWA KUHAKIKISHA SUALA LA PENSHENI KWA WAZEE LINAINGIZWA KWENYE BAJETI YA TAIFA
Mzee huyu ni miongoni mwa watu wanaotakiwa kupewa matibabu bure na pensheni nchini ili aweze kujikimu na maisha yake
Na Augusino Chindiye, Tunduru
BUNGE la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania limeahidi kusimamia na kuhakikisha kuwa mpango wa kuanza kuwalipa pensheni wazee hapa nchini unaingizwa katika Bajeti ya Bunge lijalo na kuanza kulipwa mapema 2012.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Madaha akiwa ananukuu Hotuba iliyokuwa imeandaliwa na Mwenyekiti wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Jenista Mhagama ambaye alitakiwa kuwa mgeni Rasmi katika maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani iliyofanyika katika viwanja vya Baraza la Iddi Mjini Tunduru.
Akifafanua taarifa hiyo Dc,Madaha alisema kuwa Mhagama kwa kushirikiana na Wabunge wenzake wakiwemo wabunge kutoka Mkoa wa Ruvuma ameahidi kutoa msukumo mkubwa na kuhakikisha kuwa mswada wa kuanza kuwalipa Pensheni unatungiwa sheria mapema iwezekanavyo ili wazee wa Tanzania waanze kunufaika na mafao hayo.
Hotuba hiyo iliendelea kueleza kuwa wakati Wabunge hao wakishughulikia tatizo hilo tayari Serikali imeanza kuweka msukumo wa kuendelea kuwahudumia Wazee kote nchini waanze kupata huduma za Matibabu bure kupitia mkakati wa kuwaagiza Waganga wakuu wa Hospitali zote nchini kutenga vyumba maalumu vya kutolea huduma hiyo kwa wazee zikiwa ni juhudi za kuwaondolea kero na foleni.
Alisema Sambamba na kuwepo kwa zoezi hilo pia Hotuba hiyo ilieleza kuwa tayari Serikali pia kupitia Wakuu wa Wilaya kote nchini wamewaagiza watenzaji wa Vijiji kutekeleza agizo la kuwaandikia Wazee barua zitakazo wafanya watambuliwe na kuanza kupatiwa huduma za matibabu bure kuanzia ngazi za Zahanati,Vituo vya afya na Hospitali.
Awali akisoma Risala ya Wazee katika madhimisho hayo Katibu wa Chama cha Wazee wa Wilaya ya Tunduru (HAWATU) Jafari Msonjele alisema kuwa pamoja na kundi hilo kukabiliwa na changamoto nyingi za kimaisha Wazee wengi kote nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kulea kundi kubwa la Watoto yatima ambao wengi wao wameachwa na ndugu,jamaa na Watoto wao waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.
Wazee hao pia katika taarifa yao wakagusia changamoto kubwa ya kitaifa inayo wakabiri wazee wenzao wastaafu ambao wamekuwa wakiyumbishwa kwa muda mrefu kulipwa pensheni zao na mashirika ya PPF,PSPF, na LPF na wakatumia nafasi hiyo kuyaomba mashirika hayo kuridhia maombi ya wanachama wake ya kuanza kuwalipa wanachama wake malipo ya mwezi mmoja, Mitatu na Sita bila kupitisha muda wake pamoja na kuangalia uwezekano wa kama kuna nyongeza basi iongezwe kwa wanachama wote ili kuwapunguzia makali ya maisha.
Nae Mwenyekiti wa Chama hicho Said Kabora akitoa neno la shukurani wakati wa kufunga maadhimisho hayo pamoja na kulipongeza Bunge kwa kauli hiyo alisema kuwa Wazee bado wanayo imani na serikali yao na wana amini kuwa macho hayo yaliyo ahidiwa kwa vipofu na chombo kinacho wawakilisha katika utoaji wa maamuzi yatatekelezeka na kuwafanya wazee kote nchini kufurahia matunda ya nchi yao.
Mwisho
Sunday, October 2, 2011
UCHAGUZI WA UDIWANI KATA YA MATIMIRA CCM WAIBUKA KIDEDEA
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Peramiho Anna Mbogo
Na Mwandishi Wetu,Songea
Na Mwandishi Wetu,Songea
Mtandao huu wa www.stephanomango.blogspot.com umefanikiwa kupata matokeo ya uchaguzi wa Udiwani Kata ya Matimila Wilaya ya Songea Vijijini ambapo Chama cha Mapinduzi(CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)walisimamisha wagombea
Matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Octoba 2 mwaka huu 2011 ambayo yamethibitishwa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Peramiho ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Songea Vijijini Anna Mbogo ni kuwa mgombea wa nafasi hiyo kutoka CHADEMA ,Eleuterius Kasmir Pili amepata kura 923 na mgombea wa CCM ,Menas Cosmas Komba amepata kura 1386
Kwa matokeo hayo,mtandao huu unaungana na wananchi wote wapenda maendeleo kumpongeza mshindi aliyeibuka kidedea katika uchaguzi huo,pia unatoa pole kwa wale wote waliojeruhiwa kwa namna moja au nyingine katika harakati za uchaguzi huo
Mungu awabariki na kuwapa nguvu wale walioumia kutokana na vurugu zilizojitokeza wakati wa kampeni na wakati wa kusubiri majibu
Mtandao huu una laani vikali nguvu za ziada zilizokuwa zinatumika na vyama vyote viwili ambavyo vilisimamisha wagombea katika uchaguzi huo ulioacha majeruhi zaidi ya 12na kusababisha haki za binadamu kuvurugika na kuchafua demokrasia stahiki
Tunaendelea kuwasiliana na Waandishi wengine waliopo kwenye uchaguzi wa udiwani na ubunge huko Igunga ili tuweze kuwajuza habari za matokeo ya uchaguzi katika maeneo hayo
MWISHO
KAMATI YA MAADILI YA CCM MKOA WA RUVUMA YAWAHOJI MADIWANI WATANO KUHUSU SAKATA LA UMEYA
Na, Mwandishi Wetu,Songea
KAMATI ya Maadili ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma imewahoji Madiwani watano wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambao walituhumiwa na Chama hicho Wilaya ya Songea mjini kuwa wamekisaliti chama kwa kumpigia kura za hapana mgombea Umeya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Kamati hiyo iliyokuwa na wajumbe Corneus Msuya ambaye ni Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Ruvuma,Emmanuel Mteming'ombe ambaye ni Katibu wa CCM mkoa wa Ruvuma,Henriet Ndimbo ambaye ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa chama hicho mkoa, na Mama Litunu iliwahoji Madiwani hao ili kujiridhisha na tuhumu walizotuhumiwa nazo na CCM Wilaya ya Songea Mjini
Madiwani ambao wamehojiwa ni Christian Matembo(SeedFarm) Victor Ngongi(Ruvuma)Kurabest Mgwasa(Msamala) Faustine Mhagama(Mshangano) na Genfrida Haule diwani wa Viti Maalum wa chama hicho
Kwa mujibu wa Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma Emmanuel Mteming'ombe akizungumza na mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ alisema kuwa kikao hicho cha Maadili kilikuwa kinawapa fursa ya kujitete madiwani walihotuhumiwa
Mteming'ombe alieleza kuwa kimewahoji madiwani hao na chama kimetafakari tuhuma zao na majibu ambayo wamejitetea,baada ya hapo kitatoa onyo kwa madiwani wote akiwemo na Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Emmanuel Nchimbi kutokana na utomvu wa nidhamu aliouonyesha katika uchaguzi huo wa Umeya wa Songea mjini
Mtandao huu utaendelea kuwajuza wasomaji wake kila kitu kitakachojili bila kumuonea mtu,kumuogopa kwa wadhifa wake ili kuwawezesha wadau wa mtandao huu kujiridhisha na kutafakari viongozi wao waliopewa dhamana na wananchi walivyokuwa na tabia ya uroho wa madaraka kwa faida yao binafsi huku wakiwaacha wananchi wakiwa maskini wa kutupwa
KAMATI ya Maadili ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma imewahoji Madiwani watano wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambao walituhumiwa na Chama hicho Wilaya ya Songea mjini kuwa wamekisaliti chama kwa kumpigia kura za hapana mgombea Umeya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Kamati hiyo iliyokuwa na wajumbe Corneus Msuya ambaye ni Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Ruvuma,Emmanuel Mteming'ombe ambaye ni Katibu wa CCM mkoa wa Ruvuma,Henriet Ndimbo ambaye ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa chama hicho mkoa, na Mama Litunu iliwahoji Madiwani hao ili kujiridhisha na tuhumu walizotuhumiwa nazo na CCM Wilaya ya Songea Mjini
Madiwani ambao wamehojiwa ni Christian Matembo(SeedFarm) Victor Ngongi(Ruvuma)Kurabest Mgwasa(Msamala) Faustine Mhagama(Mshangano) na Genfrida Haule diwani wa Viti Maalum wa chama hicho
Kwa mujibu wa Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma Emmanuel Mteming'ombe akizungumza na mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ alisema kuwa kikao hicho cha Maadili kilikuwa kinawapa fursa ya kujitete madiwani walihotuhumiwa
Mteming'ombe alieleza kuwa kimewahoji madiwani hao na chama kimetafakari tuhuma zao na majibu ambayo wamejitetea,baada ya hapo kitatoa onyo kwa madiwani wote akiwemo na Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Emmanuel Nchimbi kutokana na utomvu wa nidhamu aliouonyesha katika uchaguzi huo wa Umeya wa Songea mjini
Mtandao huu utaendelea kuwajuza wasomaji wake kila kitu kitakachojili bila kumuonea mtu,kumuogopa kwa wadhifa wake ili kuwawezesha wadau wa mtandao huu kujiridhisha na kutafakari viongozi wao waliopewa dhamana na wananchi walivyokuwa na tabia ya uroho wa madaraka kwa faida yao binafsi huku wakiwaacha wananchi wakiwa maskini wa kutupwa
Saturday, October 1, 2011
MADIWANI WA CCM WAITWA KWENYE KAMATI YA MAADILI YA CHAMA HICHO MKOA WA RUVUMA KUHOJIWA SAKATA LA UMEYA WA MANISPAA YA SONGEA
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Corneus Msuya
Katibu wa Ccm Mkoa wa Ruvuma Emmanuel Mteming'ombe
Na Mwandishi Wetu,Songea
MADIWANI wote wa Chama cha Mapinduzi Halmashauri ya Manispaa ya Songea wameitwa kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya Chama hicho Mkoa wa Ruvuma kuhusiana na sakata la uchaguzi wa umeya uliofanyika septemba 23 mwaka huu
Awali Kamati ya siasa ya Halmashauri kuu ya chama hicho wilaya ya Songea Mjini ilipendekeza madiwani watano wa Chma hicho wafukuzwe uwanachama kwa madai kuwa wamekidhalilisha chama katika uchaguzi huo kwa kumpigia mgombea wa nafasi ya Umeya Charles Mhagama kura za ndiyo 14 za hapana n kura 12
Baada ya chama hicho kupendekeza hivyo, kamati ya Siasa ya CCM mkoa wa Ruvuma ilikutana katika kikao chake cha ghafla na kujadili mapendekezo hayo ili kupata muafaka stahiki
Leo chama hicho kimewaita Madiwani wake wote na kuwahoji katika kikao cha maadili,mengi yatakayojili mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ utaendelea kukujuza
Katibu wa Ccm Mkoa wa Ruvuma Emmanuel Mteming'ombe
Na Mwandishi Wetu,Songea
MADIWANI wote wa Chama cha Mapinduzi Halmashauri ya Manispaa ya Songea wameitwa kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya Chama hicho Mkoa wa Ruvuma kuhusiana na sakata la uchaguzi wa umeya uliofanyika septemba 23 mwaka huu
Awali Kamati ya siasa ya Halmashauri kuu ya chama hicho wilaya ya Songea Mjini ilipendekeza madiwani watano wa Chma hicho wafukuzwe uwanachama kwa madai kuwa wamekidhalilisha chama katika uchaguzi huo kwa kumpigia mgombea wa nafasi ya Umeya Charles Mhagama kura za ndiyo 14 za hapana n kura 12
Baada ya chama hicho kupendekeza hivyo, kamati ya Siasa ya CCM mkoa wa Ruvuma ilikutana katika kikao chake cha ghafla na kujadili mapendekezo hayo ili kupata muafaka stahiki
Leo chama hicho kimewaita Madiwani wake wote na kuwahoji katika kikao cha maadili,mengi yatakayojili mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ utaendelea kukujuza
Subscribe to:
Comments (Atom)


