About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Saturday, December 3, 2011

KAPTENI KOMBA AMWAGA MISAADA YA AFYA JIMBO LA MBINGA MAGHARIBI

Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi Kapteni John Komba
Vitanda ambavyo amekabidhi kwenye Kituo cha Afya Mkili na Zahanati ya Mbuli vikiwa vinatengenezwa kwa fundi

Magodoro na Vitanda vikiwa kwenye uwanja wa Kituo cha afya Mkili wilayani Nyasa kabla havijakabidhiwa
Wananchi waliojitokeza wakati Mbunge Kapteni Komba alipokuwa anakabidhi msaada huo kwa ajili ya kuimalisha sekta ya afya
Na Stephano Mango,Songea
MBUNGE wa Jimbo la Mbinga Magharibi wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma Kapteni Mstaafu John Komba ametoa msaada wa vitanda,mito,shuka,chandarua na magodoro  wenye thamani ya shilingi 3 milioni kwenye kituo cha Afya Mkili na Zahanati ya Kijiji cha Mbuli ili kuondokana na tatizo la wagonjwa kulala chini kwa kutumia mikeka
Akitoa misaada hiyo kwenye viwanja vya Kituo cha Afya Mkili Komba alisema kuwa kwa muda mrefu nilikuwa nafahamu kero ya wananchi wa maeneo hayo kuwa ni afya,maji,barabara,elimu na mawasiliano lakini kwa miaka mitano iliyopita nilichagua kushughulikia suala la elimu ,mawasiliano na barabara ambapo kwa sasa nashughulikia afya na maji
“Natambua matatizo yaliyopo kwenye sekta ya afya katika Jimbo la Mbinga Maghalibi hivyo kwa kuanzia natoa msaada wa shuka 24,magodoro 14,vyandarua 14,mito 14,vitanda 14 kwa ajili ya kituo cha afya cha Mkili na pia Vitanda 6,shuka 12,magodoro 6,Vyandalua 6,mito 6,na mzani wa kupimia watoto na wajawazito 1 kwenye Zahanati ya Kijiji cha Mbuli”alisema Komba
 Komba alisema kuwa vituo vya afya na Zahanati karibu zote katika Wilaya hiyo hazina wataalamu,Vifaa Tiba na usafiri wa wagonjwa lakini tatizo hilo limeanza kushughulikiwa kwa kasi kubwa na nguvu zaidi kwa kuanzia kutoa vitu hivyo
Alisema kuwa natambua kuwa wananchi wamelalamikia kwa muda mrefu matatizo hayo hasa ya ukosefu wa vitanda na shuka kwani wanapotakiwa kulazwa hulazimika kutafuta mikeka na vitenge kwa ajili ya kujifunika wakati wa kulala huku wakipata mwanga wa vibatali kutokana na kukosa umeme
Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo Emmanuel Nchimbi akipokea msaada huo alisema kuwa kwa muda mrefu kituo hicho kilikuwa kinakabiliwa na matatizo hayo hivyo kwa msaada huo wananchi wanaopata huduma za matibabu watakuwa wameondokana na matatizo yaliyokuwa sugu katika kituo hicho
Naye Mganga wa Kituo hicho cha Afya Thomas Magulilo alieleza kuwa kituo chake cha afya kwa sasa kinakabiliwa na tatizo la watumishi wa kada ya afya,usafiri kwa wagonjwa na ukosefu wa maji kwani wagonjwa wamekuwa wakichota maji Ziwa nyasa na kuyatumia kwa kunywa,kuoga na shughuli zingine na kusababisha kuongezeka kwa magonjwa ya matumbo
Magulilo alisema kuwa kituo hicho kinahudumia wagonjwa kutoka Vijiji vya Yola,Luhundi,Ndonga na Mkili na wengine kutoka maeneo jilani hivyo kituo kimekuwa kikitoa huduma kwa wagonjwa wengi kuliko uwezo wake kwani vifaa tiba vipo vichache,wataalamu wa kada ya afya wapo wachache na kusababisha huduma inayotolewa kuwa duni
Alisema kuwa magonjwa sugu yanayosumbua wananchi wa maeneo hayo kuwa ni Malaria,upungufu wa damu,Minyoo,magonjwa yatokanayo na hali ya hewa,kuhala na kutapika pamoja na ugonjwa hatari wa ukimwi
Mwisho

Friday, December 2, 2011

WALIPAKODI WATAKIWA KULIPA KWA WAKATI ILI KUKUZA UCHUMI WA NCHI

 Meneja wa TRA mkoa wa Ruvuma Apili Mbaruku

 Meneja Msaidizi wa TRA mkoa wa Ruvuma Novatus Millinga
Afisa elimu huduma kwa Mlipakodi Mkoa wa Ruvuma Jackson Mseti

 Kaimu Mhasibu wa TRA mkoa wa Ruvuma Zahoro Said akiwa na Afisa Manunuzi wa TRA mkoa wa Ruvuma Kasindi Joel wakati wa mkutano wa waandishi wa habari mjini hapa


 Waandishi wa habari wakiendelea kunasa pointi toka kwa Meneja wa TRA mkoa wa Ruvuma Apili Mbaruku

 Mwandishi wa TBC Catherine Nyoni akinasa matukio mbalimbali kwenye mkutano wa waandishi wa habari mkoa wa Ruvuma na Viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) mkoa wa Ruvuma ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya mlipa kodi mwaka 2011
 Viongozi wa TRA mkoa wa Ruvuma wakitoa msaada kwa wanafunzi wenye ulemavu wa macho wanaosoma shule maalum ya Mshangano wakati wa wiki ya mlipakodi mwaka 2010
 Wanafunzi wenye ulemavu wa macho wakiwa kwenye picha ya pamoja

Viongozi wa TRA mkoa wa Ruvuma wakiwa kwenye picha ya pamoja na watoto waishio katika mazingira magumu waliopo kwenye kituo cha Kanisa la Matogoro mara baaya ya kupewa msaada wa Mchele,Sabuni,Chumvi,Mafuta ya kupaka na kupikia,miswaki na dawa ya meno wiki ya mlipakodi mwaka 2010
Na Stephano Mango,Songea
WALIPAKODI mkoani Ruvuma wametakiwa kuongeza juhudi ya kulipa kodi kwa wakati ili kuifanya Serikali iweze kujitegemea na kufanikisha kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini
Akizungumza na Waandishi wa habari jana Ofisini kwake kuhusu wiki ya mlipakodi mkoani Ruvuma Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA)Mkoani Ruvuma Apili Mbaruku alisema kuwa mamlaka ya mapato nchini inathamini na kumtambua mlipakodi kama mhimili wa kukua kwa uchumi kupitia mapato yatokanayo na kodi wanazolipa
Mbaruku alisema kuwa watanzania walio wengi wameendelea kutimiza wajibu wao na kusaidia kukuza uchumi wa taifa na ndio maana TRA kupitia mpango wake wa kimkakati (Corporate Plan)suala la kutoa huduma bora kwa walipakodi linaendelea kupewa kipaumbele
“Mtazamo wetu ni kujenga imani kwa jamii katika kusaidia wafanyabiashara kama wabia muhimu kwa kutoa huduma bora tukitumia mifumo ya kisasa yenye kukidhi matarajio ya wateja wetu ili hatimaye walipe kodi kwa ustawi wa taifa letu”alisema Mbaruku
Alieleza kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2010/2011 mkoa wa Ruvuma ulikusanya kodi kwa kiwango cha asilimia 97.27% kodi za ndani na 101.5% kwa kodi ya forodha ambapo kodi za ndani ilipangiwa 4.289.bil=/ na ilikusanya 4.173 bil./= wakati forodha ilipangiwa 4.289.bil/= ilikusanya 178.4m./= lengo halikufanikiwa kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na makusanyo halisi yalikuwa zaidi ya asilimia 22% ya makusanyo halisi ya mwaka 2009/2010
Alisema kuwa kuanzia disemba 1 hadi 6 ni wiki ya mlipakodi kwa mwaka wa 2011 ambapo kauli mbiu yake ni”Tulipe Kodi Tujitegemee” lengo lake ni kuifahamisha jamii umuhimu wa kulipa kodi ili taifa lijitegemee,kupata mrejesho kutoka kwa walipakodi na wateja wetu ili kuweza kujua huduma zinazotolewa na mamlaka zina ubora wa kiwango kilichojiwekea
Alifafanua kuwa lengo  ni kuwakumbusha walipakodi haki na wajibu wao katika ulipaji wa kodi,kuonyesha uwajibikaji kwa jamii na kwamba katika maadhimisho ya mwaka huu mamlaka inategemea kuendesha semina kwa wanafunzi shule za sekondari,kutoa misaada kwa wahitaji mbalimbali na kutoa vyeti kwa walipakodi bora walioteuliwa kwa vigezo mbalimbali vilivyowekwa kitaifa
MWISHO

DIWANI WA VITI MAALUMU CHADEMA ATOA MSAADA WA MADAWATI SONGEA

      Diwani wa Viti Maalum kupitia tiketi ya Chadema katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Rhoda Komba 
 Wanafunzi wa darasa la awali katika shule ya Msingi Zimanimoto iliyopo kwenye Kata ya Mfaranyaki Halmashauri ya Manispaa ya Songea wakiwa wamekalia madawati yaliyotolewa na Diwani wa Chadema Rhoda Komba



 Wazazi wa wanafunzi wa darasa la awali wakiwa kwenye viwanja vya shule ya msingi Zimanimoto kwa ajili ya kusherehekea mahafali ya watoto wao na kupokea msaada wa madawati kutoka kwa Diwani wa Chadema Rhoda Komba

Diwani Rhoda Komba akimtunuku cheti cha kuhitimu darasa la awali Juma Abasi
Na Stephano Mango,Songea
DIWANI wa Viti Maalum kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Rhoda Komba amekabidhi msaada wa madawati 10 yenye thamani ya TSh 450,000 kwa ajili ya darasa la awali katika Shule ya Msingi Zimanimoto
Komba akizungumza wakati wa hafla fupi ya mahafali ya awali katika viwanja vya shule hiyo jana alisema kuwa kuna siku alipita kandokando ya shule hiyo na kuwaona wanafunzi wa darasa la awali wakiwa wamerundikana kwenye darasa moja na kugombania madawati
“Hali ile ilinihudhunisha sana nikaamua kutafuta fedha kwa ajili ya kutengeneza madawati ili nije niwakabidhi kwa lengo la kupunguza idadi ya wanafunzi wanaokaa chini na kukuza malezi ya watoto hao kwa kuwapatia elimu bora”
Alisema kuwa elimu bora kwa mtoto ni nguzo muhimu sana kwa maendeleo ya taifa letu na endapo atalelewa vizuri katika darasa la awali atakuwa amejengeka vyema kitabia na kielimu na kumsababisha kuwa na uwezo anapoingia darasa la kwanza
Aidha Diwani huyo pia ameahidi kumsomesha mtoto aliyehitimu darasa la awali katika mahafari hayo Immakulata Gomela mwenye ulemavu wa ngozi kwa kumpatia sare za shule,madaftari,michango ya shule,viatu na huduma ya afya kuanzia darasa la kwanza hadi darasa la saba
Akizungumza kwenye hafla hiyo Mwalimu wa darasa la awali Joha Tambulu alisema kuwa darasa la awali lina wanafunzi 90 ambao wanakalia madawati tisa na kusababisha adha kubwa ya ufundishaji kwani dawati moja linapaswa likaliwe na wanafunzi watatu lakini wanakaa wanafunzi saba na wengine wanakalia matofali
Tambuli alisema kuwa kwa msaada huu wa madawati  10 kunafanya darasa la awali kuwa na madawati 19 ambayo kwa kiasi kikubwa kumepunguza mlundikana wa wanafunzi kwenye dawati moja na kufanya wanafunzi wengi kushindwa kuandika vizuri na kupelekea kuwa na mwandiko mbaya
MWISHO

Thursday, December 1, 2011

KIJANA TAIFA LA KESHO NI FALSAFA ILIYOPOTOSHWA KWA MAKUSUDI

Vijana wa kundi la sanaa la Wazalendo wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kumaliza kikao chao cha maandalizi ya uzinduzi wa filamu ya The Challenge(Majaribu) inayotarajiwa kuzinduliwa Disemba 22 mwaka huu

Na Stephano Mango.Songea
 
TAIFA lolote Duniani haliwezi kukua na kuwa imara kiuchumi na kijamii bila makundi yote ya jamii kushirikishwa kikamilifu katika mapambano dhidi ya umasikini,maradhi na ujinga.

Ni wazi kuwa katika ulimwengu huu wa sasa,asilimia kubwa ni vijana ambao kimsingi ndio wanaopaswa kuwa viongozi wa leo na kesho na nguvu yao inahitajika sana katika jamii zetu kutokana na maarifa na mchango wao katika kusukuma gurudumu la maendeleo ulivyo mkubwa.

Hivyo basi, vijana ni kundi kubwa na rasilimali muhimu katika kuleta maendeleo ya taifa lolote lile duniani kutokana na nguvu na fikra za kimapinduzi walizo nazo.

Ukweli wa jambo hilo huwa ni rahisi kudhihirika waziwazi endapo vijana wataandaliwa vyema katika jamii zao kushiriki na kushirikishwa katika kubuni, kupanga na kutekeleza mikakati mbalimbali ya mandeleo.

Viongozi wengi wamekuwa wakisema mara kwa mara hasa wanapowapa nasaha utasikia wakisikika wakisema “Vijana ni Taifa la kesho fanyeni kazi kwa bidii na sio kuzurula ovyo, hampaswi kuishi lelemama na kuzubaa katika vijiwe huku mkipiga soga ambazo hazina umuhimu katika maisha yenu kwa kuwa kuwepo kwa vijiwe husababisha vishawishi vikubwa katika anasa na tamaa za kumiliki mali pasipo kufanya kazi.
 
Kitendo cha kuwafungua vijana masikio na kuyeyusha fikra mgando ambazo zinatawaliwa na uvivu,uchu wa mali na maisha ya anasa kilikuwa ni kizuri na chenye busara katika fikra yakinifu katika kukabiliana na changamoto zao

Ufanyaji wa shughuli za kimaendeleo ambazo zinaleta ukombozi katika jamii zetu ni jambo la kheri na huleta faraja katika maisha na mustakabali wa harakati za vijana wenyewe na jamii zao.
 
Nimekusudia kuandika makala haya kutokana na kushindwa kuivumilia falsafa inayotumika mara nyingi hasa na viongozi wengi ambao wanadhamana mbalimbali katika nchi hii,ujumbe unaotolewa huenda ulikuwa mzuri katika maisha ya vijana lakini kauli ya kusema vijana ni taifa la kesho ndiyo inayoleta ugomvi katika harakati za vijana na hapa ndio hoja yangu.

Ni dhahiri kuwa falsafa ya “vijana Taifa la kesho” imekuwa ikisemwa mara nyingi ambayo ni upotoshwaji mkubwa katika uhalisia wa mambo licha ya kuwa kauli yenyewe sio ngeni katika masikio ya jamii, kwani imekuwa ikijirudia mara kwa mara katika majukwaa mbalimbali.

 Kuna juhudi kadha wa kadha zimefanyika na wanaharakati mbalimbali wa masuala ya vijana katika kuipinga falsafa hiyo na kuonyesha falsafa mbadala katika kuweka mambo sawa na kupunguza malumbano yasiyo ya msingi

Ila kutokana na ugumu wa wanasiasa wengi kukubali mabadiliko chanya na yenye kueleweka katika maisha ya vijana kwa sababu zao binafsi ikiwemo hofu ya kizazi kipya kuchukua nafasi katika nyanja mbalimbali za uongozi,wanaendelea kuleta mikaganyiko katika jamii kwa faida zao za ulafi wa madaraka

Viongozi hao wamebaki kutoa mahubiri hasi ambayo hayana mantiki bali ni nguvu ya kuwavesha vijana kilemba cha ukoka na fikra mgando za kusubiri muda wa kuitumikia nchi yao kwa kutumia hoja hafifu ya kjana Taifa la kesho pasipo kesho kutimia

 Lugha wanayoitumia ni laghai na kimantiki neno kesho huwa halikamiliki katika mfululizo wa siku ingawa kimsingi kesho ni neno ambalo lina uhalisia wake kinadharia zaidi kuliko kivitendo.

 Jambo ambalo linathibitishwa na kamusi ya Kiswahili sanifu iliyotungwa na Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili chuo kikuu cha Dar-es-salaam ambapo inafafanua kuwa kesho ni “siku inayofuata baada ya leo, ni wakati ujao”.

Hiyo ina maana kuwa hakuna siku itimiayo katika mawazo ya kawaida ya binadamu iitwayo kesho kwa kuwa kesho huwa haifiki, ni siku ambayo inapaswa kusubiriwa tu kila kunapokucha.
 
Napata tabu sana katika kufikiri ili nielewe katika tafsiri ya kijana taifa la kesho,sielewi mwanzilishi wa falsafa hiyo alikuwa anamaanisha nini na kwa maslahi ya nani? Endapo yupo basi nahitaji mjadala naye ili kuweka sawa hoja husika

Wengi katika jamii waliisikia falsafa hii kwa mara ya kwanza katika utoto wao na hasa walipokuwa katika madarasa ya watoto kwenye shule za awali au za msingi.

 Ni wazi kuwa walimu walisikika mashuleni wakiitumia falsafa hii ili kutufanya tujifunze kwa maarifa na ujuzi na tuzoee kutenda mema na kujijengea sifa nzuri kwa ahadi kuwa sisi ni viongozi wa baadaye yaani tafsiri nzuri ni “Taifa la kesho”.
 
Je inawezekana kauli hiyo ilikuwa sahihi kipindi cha utoto wetu,sisi ambao kwa sasa ni vijana? naamini kila mmoja kwa kutumia vigezo vyake anaweza kujibu swali hilo hapo juu,

Katika mikataba na sheria mbalimbali za kimataifa zinafafanua kuwa binadamu mwenye umri kuanzia miaka 0-17 ni mtoto na haruhusiwi kufanya maamuzi yeyote mazito kuhusu maisha yake, ingawa kamusi tajwa hapo mwanzo inaleta utata katika vipande viwili vya umri hasa katika maana ya kijana,kamusi inasema kijana ni mwana mdogo,mtoto mwenye umri wa miaka 7 hadi12.

 Lakini katika mtazamo wa kawaida tunaamini kuwa kijana ni binadamu mwenye umri wa
kuanzia miaka 18-40 na wakati mwingine mpaka miaka 45.

 Ukirejea kamusi tajwa hapo juu tafsiri ya Taifa ni jamii ya watu wanaoishi katika Nchi moja na wanaounganika kutokana na matukio ya kihistoria,mfumo wa uchumi na utamaduni chini ya serikali moja.
  
Kauli ya kijana ni taifa la kesho kwa namna yoyote ile imepotoshwa kwa mujibu wa tafsiri ya kamusi kuhusu taifa.Nasema hivyo kwa sababu tunapozungumzia kesho kimantiki ni wakati ambao unasubiriwa,hata ukizungumza juu ya taifa huwezi kukwepa kutaja ardhi,mipaka,watu na serikali yao kama vielelezo vya taifa husika,sasa itakuwaje kijana ambaye yupo useme ni taifa la kesho,rejea tafsiri ya taifa na kesho

Tafsiri ya mtu kama kijenzi kimojawapo katika taifa haitugawi katika makundi ya umri wala kabila,awe mtoto,kijana,mzee,kilema ama vyovyote vile bado mtu atabaki kuwa ni sehemu ya Taifa tena la leo sio kesho

 Pasipo kujali dhana ya wakati uwe uliopita,uliopo au ujao bali kwa kuzingatia kipindi chote ambacho binadamu yupo hai.
  
Naamini huhitaji nguvu nyingi ili uweze kubaini upotoshwaji uliopo katika falsafa ya kijana ni taifa la kesho kwa kuwa inapoteza maana ya kijana na juhudi zake katika kufikiri,kubuni na kuthubutu kutenda.
  
Kimsingi falsafa hii ina walakini katika kuichanganua na kuelewa kusudio la mwanzilishi wa falsafa hii kwa kuwa watu wengi katika mtazamo wao mara wasikiopo neno kijana,humaanisha ni mtu mwenye umri wa miaka 18 hadi 40 sasa mtu huyo atakuwaje taifa la kesho wakati yupo leo

Binadamu siku zote tunapaswa kuwa makini katika fikra zetu na kauli tuzitoazo kwani uzoefu unaonyesha kuwa ndizo zinazozaa matendo yetu.

Lakini ni muhimu zaidi kusoma matendo yetu na kuyaelewa kwani matendo tuyatendayo ndiyo hasa tabia zetu.

Natambua pasipo shaka utofauti uliopo kutoka binadamu mmoja na mwingine katika jamii zetu,juu ya uwezo wa kufikiri na kuchambua mambo kutokana na sababu za kibailojia.
 
Hivyo naamini kuwa wapo watu wenye mtazamo wa kuwaona vijana ni taifa la kesho,binafsi naona mtazamo huo ni potofu,asiye amini kauli na mtazamo wangu basi mlango upo wazi hivyo karibu katika mjadala ili kuweka mambo sawa.

 Kwa kutumia akili ya kawaida haitamuwia vigumu binadamu yeyote yule kuona,kushawishika na kukubali mchango wa vijana katika maendeleo na ustawi wa jamii katika taifa lolote lile.

 Kwa kuwa vijana ndio wajenzi wazuri wa taifa hata hoja kulingana na mazingira stahiki,na wao ndio wanaopaswa kufanya shughuli zote za kimaendeleo ambapoa wazee wanapaswa kuwa washauri na kuwaachia vijana nafasi ili waweze kulitumikia taifa lao
  
Ni wazi kuwa endapo vijana wakipewa nafasi ya kushiriki katika kuunda taifa na kushughulikia mambo ya kimaendeleo kama vile ulinzi na usalama,biashara ndogo ndogo na kubwa,udaktari,ukulima,masuala ya michezo,sheria na mengineyo taifa litapiga hatua zaidi kimaendeleo.

 Kwa misingi hiyo,falsafa ya kumwona kijana ni taifa la kesho itanapaswa kufa iwe yenyewe au kwa kuiua kwani bila shaka falsafa hiyo inapaswa kuwa ni taifa la wakati wa sasa wafanyapo kazi za kujenga taifa lao (Taifa la leo),hivyo itakuwa ni vigumu kuwahadaa vijana kusubiri taifa la kesho wakati wao wanaishi leo

Falsafa ya vijana ni taifa la kesho ina ukakasi sana kwa sababu inawejengea vijana tabia ya kusubiri katika kuchukua hatua juu ya maisha yao.Hivyo inawapa na kuwajengea matumaini ya kuwa wajinga na wanyonge sambamba na kuhimizwa kuwa na subira kwa vitu visivyokuwepo.
 
Ni wazi kuwa muda umefika wa kumwona kijana ni taifa la leo,sasa hii ndio inapaswa kuwa kauli au falsafa mbadala kuliko kuiendekeza falsafa ambayo haieleweki katika akili za watu

Katika karne hii ambapo maendeleo ya sayansi na teknolojia yamesambaa duniani kote vijana wanapaswa kushika madaraka mbalimbali katika taifa lao,ni jambo la aibu kumkuta mzee ambaye kimsingi anapaswa kuwa amestaafu bado yupo kazini,huu ni ubinafsi,uchoyo na ulafi.Inashangaza kuona wazee wakipunguza umri wa kuzaliwa na kuongeza umri wa kustaafu ili waendelee kung’ang’ania madaraka
  
Vijana tuamke tuseme ukweli dhidi ya wazee wetu,wang’atuke na watupishe ili nasi tutimize wajibu wetu,hakuna ulazima wowote wa wao kuendelea kuzeekea katika madaraka ili hali wana watoto ambao kimsingi wana elimu ,hali kufikiri,kubuni na kuumba vitu anuai,wazee pumzikeni kwani wajibu wenu tayari mmeutimiza ulio baki ni wetu vijana
  
     
        0755 33 50 51 au 0715 33 50 51 au 0784 33 50 51
 

KAPTENI LOWASSA UNAKUMBUKA SWALI LA KIJANA ARON SHERA

 
                                                        Edward Lowassa(Mb)
Na,Stephano Mango,songea
NIMEAMUA leo kuandika makala haya ili kuweka kumbukumbu sawa dhidi ya kauli tata zinazotolewa na Mbunge wa Monduli Kapteni Edward Lowassa mara kadhaa anapopata fursa ya kuzungumza jambo
 
Nimemsikia mara nyingi kiongozi huyu akitamka na kuwataadharisha viongozi wenzake hatari inayokaribia kutokea endapo vijana wataendelea kuachwa nguvu yao ikipotea bure bila kupewa ajila itakayoweza kuleta mabadiliko chanya kwa taifa letu
 
Hakuna ubishi kuwa taifa lolote duniani  haliweza kukua  na kuwa imara kiuchumi na kijamii bila makundi yote ya jamii kushirikishwa kikamilifu katika mapambano dhidi ya umasikini, ujinga na maradhi na hasa kundi kubwa la vijana.
   
Kwani katika ulimwengu huu wa sasa asilimia kubwa ni vijana, na ndio viongozi wa leo na kesho, na nguvu kazi yao inategemewa sana katika kuendeleza jamii zetu licha ya ukweli huo kufahamika, jambo hili linapuuzwa na kuwafanya vijana kukosa thamani kutokana na mambo  mengi yanayo wazunguka ambayo hupelekea kupoteza heshima, utu na nafasi yao katika jamii na Taifa kiujumla
 
Leo anapotokea kiongozi ambaye kimsindi ndio sehemu ya kuasisijambo hilo kwa vijana kupoteza heshima yao na kutoa kauli tata kuhusu ajira kwa vijana,natafakari kwa umakini ili kuweza kuona agenda iliyopo nyuma ya panzia na anayezungumzia hoja hiyo na kubaini usafi wake
 
Na kwasasa nimeamua kuanza na tendo  lililotokea mwishoni mwa mwezi septemba 2007 wakati aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Ngoyai Lowassa alipoenda mkoani Mwanza  kwa ziara ya kikazi
 
Ziara hiyo ilikuwa ni muendelezo wa kile kilicho tafsiriwa na watu wengi kuwa ni kwenda kuifafanua na kutangaza uzuri wa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2007 na 2008 kwa wananchi.
 
Katika ziara hiyo,Lowassa kamwe hatasahau alipo kumbwa na vituko ikiwemo kushuhudia  majibu ya uongo kutoka kwa aliyekuwa Waziri wa Miundo Mbinu Andrwe Chenge kuhusu kivuko kibovu kilichopo kisiwa cha Ukelewe.
 
Bila aibu wala uwoga Chenge alilazimika kuanzisha malumbano na wananchi waliokuwa wakipinga kauli yake mbele ya  Mbunge wa jimbo hilo wakati huo Getrude Mongela,huku Chenge akiendelea kutetea jibu lake la uongo kwa madai kuwa kivuko kina fanya kazi vizuri
 
Jambo ambalo dhahiri lilikuwa ni utovu wa nidhamu mbele ya Waziri Mkuu,ndipo mbunge wa jimbo husika Getrude Mongella alipo lazimika kuweka mambo sawa kwa kupinga kauli ya Chenge waziwazi na kuacha siasa za kulindana huku akiwaunga mkono wapiga kura wake kwa kusema ukweli.
Hali hiyo ilimfanya Kapteni Lowassa aende eneo husika akajionee hali halisi,akiwa kivukoni almanusula azame pale mashine(Ingine) ya kivuko ilipozima ghafla mbele yake ndipo alipo amuru kivuko hicho kifanyiwe matengenezo ya haraka.
 
Akiwa katika kisiwa hicho cha Ukelewe Kapteni Lowassa aliulizwa swali na kijana Aron Wambura Shera,mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Pius Msekwa ambapo kijana Aron alimuuliza Lowassa  akiwa Waziri Mkuu wakati huo,ninanukuu”Mheshimiwa Waziri Mkuu tumekuwa tukikusikia kupitia vyombo vya habari,wewe pamoja na wasaidizi wako mkituhimizi tusome kwa bidii na maarifa ili kusudi tuje kuwa viongozi wa taifa la kesho, lakini mbona hatuoni hayo katika matendo yenu?
 
Alihoji uhalali wa viongozi wengi kupewa nyadhifa zaidi ya moja wakati kuna wasomi wengi vijana ambao wangeweza kushika nyadhifa hizo huku vijana wengi wakiwa wameachwa wakizubaa mitaani.
 
Aron akijithibitishia kauli yake alitoa mfano wa aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza Alex Mselekela ambaye pia ni mbunge wa Tabora kaskazini na kuhoji mtu huyo anawezaje kufanya kazi zote mbili kikamilifu?
 
Kapteni Lowassa  hakujibu swali hilo bila sababu za msingi ila alisema atarudi kujibu swali hilo siku nyingine bila kuitaja  siku husika ambapo staili aliyoitumia Kapteni Lowassa kukwepa swali lenye mantiki liliwashangaza wanafunzi wengi waliokuwepo katika eneo hilo,
 
Toka siku hiyo vijana walikatishwa tamaa na Kapteni Lowassa kwa kuwa walitegemea watapewa majibu mazuri,hii ni kutokana na uwezo wa Kapteni Lowassa kujibu maswali kwa umahiri mkubwa wakati huo akiwa Waziri Mkuu
 
Hadi leo tumetimiza miaka minne Kapteni Lowassa ameshindwa kujibu swali la kijana Aron ambalo liliulizwa kwa niaba ya vijana wa Tanzania kwani swali hilo linaeleza hisia halisi za vijana wa Tanzania na uwepo wa mashaka yao lukuki dhidi ya watawala wao
 
Swali lilikuwa wazi kabisa, kwanza linatoa ujumbe kwa watawala wetu kuwa hawatendi sawa na wanachokisema ni uthibitisho kuwa watawala wanaamini wasichokijua na kudharau wanachokijua .
 
Pili inaonyesha kuwa viongozi hawafanani na kile wanachodai kuwa wanatutumikia ingawa ukweli utabaki palepale kuwa viongozi wengi hutumikia matumbo yao huku wakitulaghai kwa maneno ya kinafiki kama vile uchumi unapaa huku umasikini ukionekana dhahiri kukithiri kwa watanzania wengi.
 
Tatu huo ni uthibitisho wa kukua  kwa kasi kwa fikra za kimapinduzi miongoni mwa vijana ambao Lowassa aliwakatisha tama toka mwaka 2007 ambapo leo tunashangaa anawazungumzia hadharani bila kukumbuka swali aliloulizwa na kijana Aron
 
Ni wazi sasa vijana wanathubutu kuhoji,kueleza mawazo yao na kuwabana viongozi kuhusu matendo yao machafu wayafanyayo wakiwa madarakani,ambayo kimsingi yana haribu mustakabali wa kizazi kilichopo na kijacho.
 
Vijana wamechoshwa na mtazamo wa kuwaona wao kuwa ni viongozi wa taifa la kesho huku leo wakikosa malezi stahiki na maandalizi mazuri katika kuchukua majukumu yao leo na hiyo kesho.
 
Kutokana na viongozi wengi kuwa na  fikra za ulafi wa mali za umma huku watanzania wengi wakiteseka na kushuhudiwa na vijana ambao ndio kundi muhimu na ni nguvu kazi ya taifa lolote lile duniani vijana wameamua kuchukua hatua wao wenyewe
 
Vijana wameamua kupaza sauti zao hasa pale nafasi inapojitokeza kwani wamekandamizwa kwa muda mrefu ambapo kumewafanya waweza kuthubutu  kutoa maoni yao waziwazi bila hofu kutokana na uhalisia na ugumu wa maisha wanaouona kwa wazazi wao na hivyo kujiandaa katika kuonyesha njia stahiki itakayo wasaidia kupata maisha yenye neema huko mbele
 
 Hivyo wanajua fika kuwa hali ngumu ya maisha inasababishwa na viongozi walafi ambao wanakula bila kunawa kwa kuingia mikataba mibovu ,kufanya ufisadi na ubadhilifu wa mali za umma bila huruma na kutuacha tukiwa masikini huku  wakifirisi nchi na kwenda kuwekeza nje ya nchi sambamba na kujirundikia vyeo lukuki ili kulinda maslahi yao
 
Vijana wakiwa katika fikra za mapambazuko na kutafuta mwanga stahiki katika maisha yao wanathubutu kuhoji uhalali wa viongozi kujirundikia vyeo kwa mara moja na wanapiga hatua kwa kutaka mafisadi na wabadhilifu wachukuliwe hatua na sio kuchukua nafasi ya kuwatetea
 
Hebu rejea maandamano ya wanafunzi yaliofanyika Agosti mosi mwaka 2007 yenye lengo la kupinga ongezeko jipya la nauli ya sh 50  na kuwa sh 100  kwa usafiri wa mabasi maarufu kama daladala kwa wanafunzi jijini Dar Es Salaam
 
Katika hali ya kimapinduzi na ukakamavu vijana walithubutu kubeba mabango yenye ujumbe mbalimbali wenye maana pana sana,bango moja lilisomeka “Mh JK utawala umekushinda?tulipe sh 100 kwa kipi mlichoboresha? Kiama chenu 2010, bango hilo halikuishia hapo liliendelea kusomeka”wafilisiwe chege ,lowaza , mkaapa kalamaagi na yona”na tuletewe  mabasi ya shule.
 
Kauli ya vijana ni ishara ya uwepo wa kiu kali miongoni mwa vijana wenyewe dhidi ya kusambaratisha mtandao wa viongozi mafisadi nchini ambao kimsingi ndio chanzo ulafi wa madaraka na kurundikiana vyeo ili kulindana katika maslahi ya kifisadi, ambapo watu wengi huishi katika maisha magumu na yanayozidi kuwavujisha jasho watanzania wengi.
  
Ni wazi kuwa hiki ni kizazi ambacho kimeanza kutambua wajibu wake kwa jamii,ni kizazi kinachoandaliwa katika mazingira ya hasira dhidi ya serikali hii kutokana na kudharauliwa pale wanapodai haki zao.
 
Kamwe vijana wasipuuzwe kupewa haki zao, hakika sio busara kuomba haki,hivyo haki inapaswa kudaiwa waziwazi na yoyote anayefinyanga haki za watu ni adui mkubwa,ni wazi kuwa maneno yaliyo andikwa kwenye mabango yaliyobebwa  na wanafunzi hao yasipuuzwe kwani ujumbe wao umefika ingawa leo vijana tunamshangaa Kapteni Lowassa baada ya kuachia ngazi ya Uwaziri Mkuu anajitokeza kuwatetea vijana
 
Vijana wanajifunza kufikiri kisayansi na kujenga hoja zenye mantiki na zenye ushawishi mkubwa kwa jamii,hivyo majibu sahihi yanahitajika katika kukidhi hamu na matakwa yao kwa manufaa ya nchi yetu.
 
Wanapothubutu kuwahoji watawala wana haki ya kupewa majibu yenye mantiki kwa wakati husika kwani kutokutoa majibu stahiki ni kujiaibisha mbele ya macho ya jamii na kutengeneza mshangao hasa wakati huu ambapo utetezi wa vijana unapotolewa na mtu aliyeshindwa kuandaa mfumo mzuri wa maisha ya vijana nchini alipokuwa kwenye madaraka makubwa kama ya Uwaziri Mkuu
  
 Hivyo Kapteni Lowassa hakuwa na sababu ya kukwepa swali aliloulizwa na kijana Aron Shera kwani swali hilo ni la msingi sana kwa mustakabali wa maisha ya vijana ambao leo kwa unafiki mkubwa anajidai kuwatetea katika suala la ajira
 
Lowassa wakati huo alipaswa kutoa majibu ya kina bila kumung’unya maneno kwani swali hilo halikuhitaji takwimu wala utafiti katika kujibu,sasa ilikuwaje Kapteni Lowassa ashindwe kuwa na jibu hadi aseme angerudi kujibu swali hilo kwa wakati mwingine.
 
Vijana hatutaki kuzubaishwa kwa majibu yenye utata kwa kuwa Kapteni Lowassa alishindwa kutupa jibu hadi alipojiudhuru ambapo bila kificho alijifedhehesha mwenyewe mbele ya vijana kwa kutotimiza wajibu na ahadi yake.
 
Akiwa madarakani Kapteni Lowassa alikumbushwa kulijibu swali la kijana Aron na wanaharakati mbalimbali wa masuala ya vijana nikiwemo mimi lakini aliupuuza ushauri wetu na kutuona tuliokuwa tunamkumbusha tumepungukiwa akili
 
Leo bila kificho tunamtaka ajibu swali aliloulizwa,baada ya hapo atuambie kwanini alishindwa kuweka mikakati stahiki na inayotekelezeka ya kutoa ajira kwa vijana wengi katika sekta binafsi na za umma alipokuwa Waziri kwa mara ya kwanza hadi pale alipokuwa Waziri Mkuu
 
Kwanini leo anajitokeza hadharani kuzungumzia suala la ajira kwa vijana akiwa kwenye madaraka ya Ubunge na katika hali ya uchafu anaodaiwa kuwa nao baada ya kubainishwa kashfa kadhaa ambazo anahusika nazo
 
Vijana tunajitambua kamwe hatuko tayari kuwa muhuri wa watenda dhambi kwani tulipothubutu kueleza mawazo yetu tulipuuzwa na kuendelea kushushwa heshima katika jamii na viongozi wetu leo tunapata tabuu kweli kuamini kuwa wanachokisema ndicho wanachomaanisha ikiwezekana watupishe nasi tushike hatamu katika kuwavusha miaka mingine hamsini baada ya uhuru
 
Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana simu 0755-335051
 
 

Wednesday, November 30, 2011

WENGI WATEKETEA KWA UGONJWA WA MALARIA WILAYANI NYASA MKOANI RUVUMA

   Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Daniel Malekela
Na Thomas Lipuka,Songea
UGONJWA wa malaria katika vijiji  kumi vya tarafa ya Ruhuhu wilayani Nyasa mkoani Ruvuma,unatishia ustawi wa jamii kutokana na wananchi wengi kuugua na kupoteza maisha kila mwaka.
Mganga mkuu wa hospitali ya Lituhi Dk.Martin Ndunguru amesema  katika kipindi cha mwaka 2009/2010  jumla ya watu 130 walikufa kati yao watoto 93 wenye umri chini ya miaka mitano na watu wazima 37.
Amevitaja vijiji ambavyo vinakabiliwa na ugonjwa wa malaria katika tarafa ya Ruhuhu kuwa ni Lituhi, Litumbakuhamba, Ngingama,Tumbi,Mbaha,Lundu,Hinga,Mkili,Ngumbo,Yola,Liwundi, Mbuli,Liweta na Njomole.
Kwa mujibu wa Dk.Ndunguru  vifo vingi vinavyotokana na ugonjwa wa malaria vinasababisha na wagonjwa kupungukia damu na kuchelewesha kupelekwa kwenye vituo vya tiba,umbali kutoka katika kijiji husika hadi kituo cha tiba.
Mganga mkuu huyo wa hospitali ya Lituhi alisema tarafa hiyo ina vituo vichache vya tiba ambapo zahanati zipo katika vijiji vya Litumbakuhamba,Ngingama,Ndumbi,Lundo,Mbuli na Mkili ambako kuna kituo cha afya.
Hata alisema vituo hivyo vya tiba vinakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni upungufu wa madawa,watalaamu wa afya,miundombinu hafifu,vifaa hasa vya maabara na kituo cha afya cha Mkili  kukosa  benki ya damu hali ambayo inaleta usumbufu kwa wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu.
Wakazi wa vijiji vya Ngingama na Litumbakuhamba ambao ni Helumina Chawala,Martina Haule,Sophia Kayombo na Kalistus Mapunda wamedai kuwa  malaria ni ugonjwa ambao unawatesa siku hadi siku  na kwamba upungufu wa dawa kwenye zahanati na bei kubwa ya dawa za malaria kwenye maduka yamadawa  ni kikwazo.
Mganga wa zahanati ya kijiji cha Ndumbi Yohana Kanyanja amekiri malaria ni tishio kwa wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa ambapo katika zahanati ya kijiji cha Ndumbi pekee kwa mwezi  hupokea zaidi ya wagonjwa  356 wengi wao wakiwa ni watoto chini ya miaka mitano.
Anabainisha kuwa katika kipindi cha mwaka 2009/2010 watoto chini ya umri wa miaka mitano wapatao 2460 waliugua malaria katika kijiji cha Ndumbi na watu wazima katika kipindi hicho walikuwa ni 1200.
Mganga wa kituo cha afya Mkili Thomas Magulilo anazitaja changamoto ambazo zinakikabili kituo hicho kuwa ni  kituo kukosa gari la wagonjwa, upungufu mkubwa wa watumishi ambapo kituo kina watumishi wane tu kati ya mahitaji ya watumishi 25 na kwamba kituo hakina vitendea kazi vya kutosha katika maabara.
“Kituo chetu hakina gari la wagonjwa ili kuwasafirisha wagonjwa wanaozidiwa  na kuwapeleka katika hospitali za Litembo,Liuli na Mbinga ambazo zipo zaidi ya kilometa 64 kutoka hapa,hivyo inawalazimu wananchi kuwabeba wagonjwa waliozidiwa kwenye machela au kwenye mtumbwi hali inayosababisha baadhi yao kufia njiani’’,alisema.
Hata hivyo amesema hatua mbalimbali kituo kinachukua ili kukabiliana na tatizo la ugonjwa wa malaria ikiwemo kutoa elimu ya kupambana na ugonjwa huo,kugawa vyandarua na kuwahamasisha wananchi kuua mazalia ya mbu  na kuhakikisha wagonjwa  wanamaliza dozi  ya malaria.
Andrew Niliwani ni mkazi wa kijiji cha Mkili anatoa ushuhuda kuwa kuna wagonjwa watatu wa malaria waliobebwa kwenye machela walifia njiani wakati wanapelekwa katika hospitali ya Litembo,wagonjwa hao walifia katika maeneo ya Ndandaghala,Nahande na Mbugu.
Mganga mkuu wa hopsitali ya Liuli Dk.Daniel Ndimbo anazitaja changamoto zinazoikabili hospitali hiyo kuwa ni upungufu wa mashine za kuchunguza damu ya malaria,upungufu wa vitanda 50 na upungufu mkubwa wa wauguzi.
 Mganga mkuu wa kituo cha afya Mbambabay Wenceslaus Socky  anaeleza kuwa dawa za malaria huwa hazifiki kwa wakati katika kituo hicho na kwamba hata kiwango kinachofika hakilingani na mahitaji ya maombi yao  hali inayosababisha upungufu wa dawa hizo kila mwezi
 Mganga mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk.Daniel Malecela amesema katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria mwaka 2010 jumla ya watoto 246,927 walio chini ya umri wa miaka mitano wamepewa bure vyandarua vyenye dawa.
Dk. Malekela alisema kuwa walifanya sensa ya kutambua idadi ya kaya zinazohitaji vyandarau ambapo jumla ya vyandarua 274,687 vimeshasambazwa katika vijiji na mitaa 539 ya mkoa wa Ruvuma
Licha ya kugawa vyandarua vyenye dawa mkoa wa Ruvuma umeviwekea  dawa vyandarua vipatavyo 254,400 vinavyotumika katika kaya bila jamii kuchangia gharama zozote.
"Tumeamua kufanya kampeni hii kwani katika tafiti ya kitaifa iliyofanywa mwaka 2007/2008 inaonyesha kuwa ni kaya nne tu kati ya 10 zinatumia chandarua kimoja chenye dawa hii inaonyesha kuwa kaya nyingi katika jamii yetu hazitumii vyandarua vyenye dawa na hivyo kuwa katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa malaria", alisema Dk. Malekela.
Aliendelea kusema kuwa takwimu za mkoa wa Ruvuma za mwaka 2008 zinaonyesha kuwa asilimia 55 ya wagonjwa wote waliopata huduma katika vituo vya kutolea huduma wenye umri chini ya miaka mitano waliugua ugonjwa wa malaria na vifo chini ya miaka mitano vilikuwa ni asilimia 56 ya vifo vyote vilivyotolewa taarifa.
Ugonjwa wa malaria unashika nafasi ya kwanza katika mkoa wa Ruvuma kwa kusababisha vifo  kwa kiwango cha asilimia 23.9. Takwimu za mwaka 2004  hadi 2008 zinaonyesha kuwa  asilimia 50.3 ya wagonjwa wote wa malaria walikuwa ni watoto chini ya umri wa miaka mitano na zaidi ya miaka mitano walikuwa ni asilimia 49.7.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ugonjwa wa malaria ndio unaoongoza kwa mahudhurio ya wagonjwa wanaofika kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya, na kwamba matukio takriban 12 milioni ya malaria hutolewa taarifa.
 Takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa watu kati ya 60,000 hadi 80,000 hupoteza maisha kila mwaka kwa ugonjwa  malaria ambapo asilimia 80 ya wanaofariki ni watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano na mama wajawazito.  Kwa wastani, malaria humuua mtu mmoja katika kila dakika tano.

 Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ugonjwa wa Malaria wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, unalenga kupunguza idadi ya wagonjwa na vifo kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2013.  Kwa maneno mengine, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ina lengo la kuwapunguza wagonjwa wa malaria hadi kufikia milioni 6 na idadi ya vifo hadi kufikia kati ya 30,000  hadi 40,000 kwa mwaka ifikapo
mwaka 2013.