About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Thursday, February 16, 2012

MWANASHERIA MBOGORO NA MTAZAMO MBADALA WA KAULI MBIU YA MIAKA 50 YA UHURU WA TANGANYIKA

 Mwanasheria Edson Mbogoro akifafanua jambo wakati wa mdahalo huo
 Mwanasheria Edson Mbogoro akiwa kwenye moja ya mikutano ya kuimarisha chama cha Chadema mjini Songea
Baadhi ya wananchi waliohudhulia mdahalo huo kwenye ukumbi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bombambili Jimbo Kuu la Songea hivi karibuni

Na Stephano Mango,Songea
SIAMINI kama kuna Mtanzania ambaye hajawahi kuisikia mahali popote kauli mbiu ya sherehe ya  miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika iliyokuwa inatangazwa kwa nguvu kubwa na Serikali ya kuwa Tumethubutu,tumeweza na tunazidi kusonga mbele.
Mwanasheria na Wakili wa Kujitegemea Edson Mbogoro ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) ameamua kutoa maoni yake juu ya kauli mbiu hiyo ili kuweza kuona kama inaakisi uhalisia wa mambo kwa kipindi hicho cha miaka 50 toka tupate uhuru.
Akizungumza hivi karibuni kwenye mdahalo wa kauli mbiu ya miaka 50 ya uhuru uliofanyika kwenye ukumbi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bombambili mjini hapa ,Mbogoro akiwasilisha mada kwenye mdahalo huo  alisema kuwa ukitafakari kwa umakini maneno yanayounda kauli mbiu ya miaka 50 ya uhuru na kuoanisha na uhalisia wa mambo toka tupate uhuru  utabaini kuwa kauli mbiu hiyo imetiwa chumvi.
“Maoni yangu sio msahafu yanaweza yakakosolewa au kupingwa kwa nguvu ya hoja kwani nayatoa kama mchokonozi kwa ajili ya kuibua mjadala wenye afya zaidi kwa ajili ya mustakabali wa nchi yetu”alisema Mbogoro.
Alisema kuwa uhuru katika ngazi ya mtu binafsi humaanisha uwezo wa kujiamulia mambo yako mwenyewe ambapo katika ngazi ya Taifa au Nchi humaanisha kujitawala,yaani kuondokana na hali ya kuwa chini ya himaya ya kigeni ambayo hushikilia na kuamua mustakabali wa kila jambo kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni nakadharika.
Uhuru humaanisha kujinasua toka kwenye minyororo ya kupuuzwa kifikra ambapo jamii huzaliwa upya na kujenga matumaini mapya ndio maana katika hotuba aliyoitoa siku ya uhuru hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliainisha maadui wakuu watatu ambao ni umaskini,ujinga na maradhi na kusema kuwa adui mkubwa kuliko wote ni umaskini.
Ninamnukuu Mwl Nyerere “…….Tukiweza kumshinda adui umaskini tutakuwa tumeweza kupata silaha itakayotuwezesha kuushinda ujinga na maradhi…namuomba kila raia wa Tanganyika aape kiapo cha kuwa adui wa umaskini, amshambulie adui huyo popote atakapoonekana”.
Mwalimu Nyerere alitutahadharisha kuwa katika kupigana vita dhidi ya maadui hao, hatuna wajomba wa kupigana badala yetu, kwamba tunaweza kupata misaada ya wafadhiri kutoka nje lakini jukumu la kujiletea maendeleo ni letu wenyewe kwanza.
Mbogoro alieleza kuwa Serikali ya uhuru ilijiwekea malengo hayo matatu, ni jambo la dhahiri kuwa tuliposherekea miaka 50 ya uhuru moja ya maswali ambayo tulipaswa kujiuliza ni kiasi gani tumeweza kuupiga vita umaskini .
Alisema kuwa wakati huo tatizo kubwa ni kwamba Mwalimu hakukabidhiwa na wakoloni nchi kama tunavyoiona leo bali alikabidhiwa makabila 120 yenye viongozi wa kimila yaani Machifu, utaifa haukuwepo ambapo kazi kubwa ni kuyaunganisha makabila hayo na kuwa taifa moja lenye umoja na mshikamano
Alifafanua kuwa Mwalimu Nyerere alifuta mfumo wa uchifu uliokuwepo akaunda Wizara ya sanaa ya taifa na vijana ili kumwezesha mtu mweusi kujitambua na kuthamini utu wake na utamaduni wake na kwa mvuto wa Mwalimu ulisaidia kuwaunganisha watanganyika ambapo mbio za mwenge zilihamasisha hisia za uzalendo na utaifa na lugha ya Kiswahili ilisaidia kuwaunganisha watanganyika.
Alieleza kuwa neno kuthubutu kwa mujibu wa kamusi ya standard Swahili/English iliyochapwa na chuo kikuu cha Oxford toleo la 1995, linamaana ya ujasiri wa kuamua na kutenda jambo gumu ambalo ni la hatari, ambalo mafanikio yake hayatabiri, kwa kukubali kupata uhuru, hakuna shaka kuwa tulithubutu kwa vile ulikuwa uamuzi mgumu unaotupelekea ambako hatuna uzoefu nako, kusikotabirika.
Alisema kuwa, mara baada ya kupata uhuru chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere Serikali iliweza kuwa na mipango mizuri na ambayo ilitekelezeka kama vile ujenzi wa viwanda vya kukoboa na kusindika mazao ya biashara kama vile, korosho, kahawa, kutengeneza nguo, viwanda vya kutengenezea zana za kilimo, viwanda vya kusindika chakula na vingine vingi.
Alieleza zaidi kuwa ujenzi wa mashirika imara ya uchukuzi na usafirishaji wa anga, nchi kavu na majini na mashirika ya ugavi na kwamba asilimia ya 90 ya watanzania walikuwa wanajua kusoma na kuandika na kwamba wakati Serikali ya awamu ya kwanza inaondoka madarakani ilikuwa imeshaweka msingi wa mapinduzi ya viwanda na teknologia ambapo kilichotakiwa ni marekebisho ya uendeshaji kwa ajili ya kuleta ufanisi zaidi.
Alisema kuwa wakati huo tulithubutu kuweka misingi mizuri ya maendeleo, swali la kujiuliza je tumeweza?, katika kujibu swali hilo viongozi wa Serikali wanatumia takwimu kuonyesha kiwango cha mafanikio kama vile idadi ya watu, upatikanaji wa maji,  afya,  miundombinu, vyuo vikuu, shule za msingi na sekondari toka wakati tunapata uhuru hadi sasa na vitu vingine.
Alisema kuwa kwa mtu wa kawaida ambaye anaheshi mu ukweli hawezi kujisifia hatua ya maendeleo tuliyoipiga kwani hailingani kabisa na umri wetu wa nusu karne kama Taifa, kwani tungeweza kufanya mara 50 zaidi ya hapa tulipo, hivyo hatujaweza bali tumeshindwa.
Alisema kuwa tunatakiwa kujilinganisha na nchi kama Malaysi, Indonesia, Singapore, Thailand, Veirtnam na nyingene ambazo tulipata nazo uhuru katika kipindi  kinachokaribiana zikiwa na hali duni kama tulivyokuwa nayo sisi wakati tunapata uhuru.
Alisema kuwa, mazuri yote ya awamu ya kwanza yameyeyushwa na awamu zilizofuata, kwani Mwalimu Nyerere aliacha viwanda 12 vya nguo vinavyofanya kazi lakini leo vimebaki vitatu ambavyo vinasuasua, aliacha mashirika ya umma 380 ambayo mengi yamebinafsishwa.
Alifafanua kuwa viwanda vya kuyeyusha chuma na kutengeneza vipuri na zana mbalimbali vya  Mang’ua na Kilimanjaro, Tanzania Scania Assembly Plan, Kibaha Mgololo kilichopo Mufindi, vimeuzwa kwa bei chee, tumerudi kwenye utegemezi hata kwenye kijiti cha kuchokonolea mabaki ya vyakula kwenye meno ni made in china.
Alieleza kuwa leo tunasubiri wafadhili hata kwa ajili ya kutujengea matundu ya vyoo vya watoto wetu mashuleni, ujinga umeongezeka kwa maana asilimia 90 ya watu wanaojua kusoma na kuandika alioiacha hayati Mwalimu Nyerere imepungua hadi kati ya asilimia 65 na 70.
Alieleza zaidi kuwa hatuna umeme wa uhakika baada ya miaka 50 ya kujitawala, ni asilimia 3 tu ya kilimo chetu ndio kinatumia trekta, asilimia 26 wanyama kazi na asilimia inayobaki bado ni jembe la mkono.
Alisema kuwa Tanzania ni nchi maskini ikiwa katikati ya utajiri kwa asilimia 18 ya maji baridi dunia yafaayo kwa kunywa na umwagiliaji yako Tanzania, nchi ya tatu barani Afrika  kwa uzalishaji  dhahabu nyingi baada ya Afrika Kusini na Ghana.
Alifafanua kuwa Tanzania ni nchi ya barani Afrika kwa kuwa na Ng’ombe wengi baada ya Ethiopia, pia inazalisha madini yenye thamani kubwa aina ya Tanzanite yanayopatikana Tanzania pekee lakini ni nchi inayoongoza kwa kupokea misaada mingi barani Afrika kuliko nchi yoyote ile
Alisema kuwa ni nchi ya tatu Duniani kwa kupokea misaada mingi baada ya Afghanistan na Iraq, misaada Tanzania imeongezeka toka dola za kimarekani 39.19 mwaka 1961 hadi dola za kimarekani bilioni 2.89 mwaka 2009 lakini misaada hiyo imekuwa kama ndoo ya maji inayovuja kwani imeshindwa kutukwamua.
Alisema ukosefu wa falsafa ya kuiongoza nchi kumepelekea utafunaji wa wazi wa rasilimali za taifa kwani ufisadi umetamalaki kwenye ofisi za umma,mikataba mibovu na kuwafanya wawekezaji kuja nchini kuchuma rasilimali zetu zote na kuwaacha watanzania wakiwa maskini.
“Uongozi wa umma umekuwa dili kwa baadhi ya watu kujineemesha mchana kweupe na kuwafanya watanzania wengi kubaki maskini na kusababisha maadui watatu waliotangazwa wakati tunapata uhuru, umaskini, ujinga na maradhi kushindwa kutokomezwa”alisema Mbogoro.
Alisema kuwa katika mazingira hayo hatuna sababu ya kusema kuwa tumeweza bali tumeshindwa bila kulekebisha matatizo ya msingi yanayotukabili kama Taifa kusonga mbele ni kujidanganya na kwamba kauli mbiu sahihi ya kuadhimisha miaka 50 ya uhuru ilipaswa kuwa Tumethubutu, Tumeshindwa, Tumekwama, Tunahitaji kujikwamua.
Alimalizia kwa kusema kuwa, nimejaribu kuonyesha tulikotoka na tulipo na si zaidi kuhusu tunakokwenda kwa sababu ni kiza kinene, hivyo kama taifa tunahitaji kujitazama upya kwenye kioo cha ukweli na tukubali vile kinavyotuonyesha kisha tujadiliane vya kutosha ili tujinasue na kusonga mbele.
Mwandishi wa Makala
Anapatikana 0715-335051
www.stephanomango.blogspot.com


Wednesday, February 15, 2012

KAPTENI KOMBA AMWAGA VIFAA VYA MICHEZO VYA SHILINGI MILIONI 3 MASHINDANO KOMBE LA MBUNGE

Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi Kapteni John Komba akimkabidhi Chogo Wachogo sare 3 za waamuzi wa Mashindano ya Kapteni Cup ambayo yanashirikisha timu 10 za Kata ya Lituhi

Kiongozi wa Timu ya Polisi Fc akikabidhiwa jezi kwa ajiri ya mashindano hayo

Kiongozi wa Timu ya Shujaa Fc akikabidhiwa jezi

                                     Kiongozi wa Timu ya Ngingama akikabidhiwa jezi

Viongozi wa Timu mbalimbali shiriki katika mashindano hayo wakikabidhiwa jezi za mashindano na Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi Kapteni John Komba


MVUA YA MAWE ILIYOAMBATANA NA UPEPO YAEZUA NYUMBA SONGEA


                         MKUU WA WILAYA YA SONGEA THOMAS OLEY SABAYA

Na Gideon Mwakanosya,Songea

NYUMBA  kumi na tatu zimeezuliwa kata ya Ruvuma  Manisipaa ya Songea kutokana na  mvua ya mawe iliyo ambatana na upepo ambayo  ilinyesha jana kuanzia majira ya saa tisa  mchana hadi saa kumi .

Uchunguzi uliofanywa na mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com katika kata za Mshangano ,Bombambili ,Mfaranyaki ,Lizaboni, Ruhuwiko ,Majengo ,Subira na Ruvuma  umebaini kuwa kata ya Ruvuma  mtaa wa mjumbe  Saidi Ndenyende  ndio ulioathirika sana na mvua hizo.

Hata hivyo mitaa yote ya katikati ya mji wa Songea  mvua hizo zimeangusha baadhi ya miti ya kivuli ,nguzo za umeme , nyaya za simu  na zile za kuingizia picha za runinga .

Akiongea kwa uchungu Laita Swedi  alisema  “Umekuja upepo mkali ulioambatana na mvua ya mawe nikasikia kishindo kwuuuuuapo ndipo niliona mbingu na bati likawa limeondolewa nyumbani mwangu na kuacha vyumba vitatu vikinyeshewa mvua “Alisisitiza Laita Swedi .

Naye Stella  Komba wa kata hiyohiyo ya Ruvuma ameleza kuwa  yeye alikuwa anatoka hospitali ambako alikuwa amempeleka mwanaye kwa matibabu lakini  alipoikaribia nyumba yake akakuta imeezuliwa na paa limetupwa mbali  na nyumba yake  hivyo  kuacha vyumba zaidi ya vinne kuwa wazi .

Mtandao huu ulilifanya juhudi ya kumtafuta Mwenyekiti wa mtaa Said Ndenyende  ili aweze kueleza iwapo amewatembelea  waathirika  wa mvua hizo lakini taarifa zilizo patikana nyumbani kwake alikuwa amekwenda  shambani kwake eneo la  Sanangula umbali wa kilometa 24 kutoka  katikati ya mji wa Songea  ,pia mtendaji wake hakupatikana ofisini kwake .

Mtaaramu mmoja ambaye hakutaka jina lake  litajwe alisema yeye ni fundi  wa ujenzi  kama angeweza  kufanya ukandarasi wa kutengeneza nyumba hizo kila nyumba angeitengeneza kwa shilingi  milioni mbili na kwamba  nyumba zote kumi na tatu zingegharimu shilingi milion ishirini na sita .

Mtandao huu, bado unaendelea  na uchunguzi wa uharibifu uliofanywa na mvua hizo hasa upande wa mazao ,miti ya kupandwa na mifereji ya maji,Hata hivyo jitihada za kumpata mkuu wa wilaya  ya Songea  Thomas Ole  Sabaya ili aweze kutoa tathimini ya hasara iliyojitokeza  hakuweza kupatikana  kwa kuwa alikuwa kwenye shughuli maalumu za kikazi.

Mwisho.

Monday, February 13, 2012

WAANDISHI WA RUVUMA PRESS CLUB WAKUTANA KUJADILIANA MAREKEBISHO YA KATIBA YAO

Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Ruvuma Press Club Andrwe Kuchonjoma, Katibu wa Ruvuma Press Club (katikati) wakiendesha kikao cha mabadiliko ya katika katika ukumbi wa ushirika juzi
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Ruvuma Press Club wakijadiliana jambo, kutoka kulia ni Alpius Mchucha, wa pili Crecencia Kapinga, wa tatu Mpenda Mvula na wanne Julius Konala
Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Revocatus Kassimba akiwa na Mweka Hazina wa Ruvuma Press Club wakati wa kikao cha mabadiliko ya Katiba

Waandishi wa Habari wa Ruvuma Press Club wakiendelea kuchangia mabadiliko ya katiba yao

Kutoka kulia ni Christian Sikapundwa, Gideon Mwakanosya na Thomas Lipuka

Kutoka kushoto ni Judith Lugome, Adam Nindi, Gerson Msigwa, Mark Mapunda, Catherine Nyoni

MAKAMU WA RAIS DKT BILAL KUFANYA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU NNE MKOANI RUVUMA


MKUU WA MKOA WA RUVUMA SAID THABIT MWAMBUNGU
Na Stephano Mango,Songea
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, Mohamed Gharib Bilal anatarajia kufanya ziara ya  kikazi ya siku nne mkoani Ruvuma  kuanzia kesho  jumanne (leo) hadi  februari 17 mwaka huu siku ya ijumaa
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa Maliasili Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu alisema kuwa Makamu wa Rais Dkt Bilal atawasili uwanja wa ndege wa Songea majira ya saa tano asubuhi na kupokelewa na viongozi wa chama na Serikali mkoa wa Ruvuma ambapo ataveshwa skafu na kukagua vikundi vya ngoma uwanjani hapo
Mwambungu alisema kuwa akitoka uwanjani hapo, Dkt Bilal atapokea taarifa ya maendeleo ya Mkoa na taarifa ya Chama tawala mkoa katika ikulu ndogo mjini Songea ambapo pia siku hiyo atatembelea, kukagua na kupata taarifa ya kituo cha hifadhi ya chakula kisha kuweka jiwe la msingi ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Songea na kuwasalimu wananchi
Alisema siku ya jumatano Dkt Bilal ataelekea Wilaya ya Namtumbo ambako atapewa taarifa ya mradi wa Uranium wa Mkuju unaofanywa na Kampuni ya Mantra, atakagua eneo la mradi na kuzungumza na waananchi wa Likuyusekamaganga ambao wanazunguka eneo la mradi kisha kurudi mjini Songea kuzungumza na Halmashauri kuu ya Ccm Mkoa
Alieleza kuwa siku ya Alhamisi Makamu wa Rais Dkt Bilal ataelekea Wilaya ya Mbinga na kupokelewa na viongozi wa Wilaya Kitai Gerezani na kupewa taarifa ya maendeleo ya Wilaya na kukagua shamba la mbegu bora, kisha ataelekea kukagua na kupata taarifa ya mradi wa uchimbaji wa makaa ya mawe Ruanda na kuelekea Mbinga mjini kuzindua mashine za kuzalisha umeme
Alieleza zaidi kuwa siku ya ijumaa Makamu wa Rais Dkt Bilal atafanya majumuisho ya ziara yake Mkoa wa Ruvuma katika ukumbi wa Umati Wilayani Mbinga na kuondoka kuelekea uwanja wa ndege wa Songea ili kuagana na viongozi wa Chama na Serikali na kuondoka kuelekea Mkoa wa Rukwa kwa ajiri ya majukumu mengine
Aliwataka wakazi wa Mkoa wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi kumpokea mgeni huyo kama ilivyo tamaduni za mkoa huo wa kuwapokea wageni kwa amani, upendo na ukalimu
MWISHO

Sunday, February 12, 2012

WANANCHI WAVAMIA OFISI YA SERIKALI NA OFISI YA CHAMA KWA SABABU MGANGA WA JADI AMEKOSA KIBALI CHA KUSHUGHULIKA NA WACHAWI



                      

MKUU WA WILAYA YA MBINGA KANALI EDMUND MJENGWA

Na Stephano Mango, Songea

KUNDI la wananchi wenye hasira kali katika Mji mdogo wa Mbambabay  wilaya mpya  ya Nyasa Mkoani Ruvuma wamevamia baadhi ya ofisi za serikali na CCM pamoja na baadhi ya nyumba za makazi ya watu na kuharibu samani za ofisi  na za watu kisha kuchoma nyaraka za Serikali na CCM zilizokuwa zimeifadhiwa kwenye majengo hayo yaliyo kuwa yamevamiwa

Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo walieleza kuwa lilitokea baada ya uongozi wa Serikali  kata ya Mbambabay kukataa kutoa kibali cha kumruhusu Mganga wa Jadi aliyetoka Jijini Tanga kwa lengo la kufanya kazi ya kuwafichua  baadhi ya watu wanaojishughulisha  na imani za ushirikina  kwenye  mji mdogo wa Mbambabay .

Watu hao ambao hawakutaka majina yao  yatajwe gazetini walieleza kuwa  Mganga  huyo anaitwa  Fakii Yahaya  maarufu kwa jina la Jongo ambaye alikuwa amefika wilayani humo kuja kufanya kazi hiyo kwenye kijiji cha Ndengele ambako tayari alikuwa amesha fanya kazi ya kuwabaini  watu wanaofanya shughuli za ushirikina na  wananchi wa kijiji hiko walitangaza kuwakataa, hadharani wale wote waliobainika kuwa ni wachawi .

Walisema kuwa kufuatia hali hiyo baadhi ya wananchi wa mji mdogo wa Mbamba-bay walimwomba Mganga huyo ili aende akawasaidie kuwafichua  watu wanaojihusisha na mambo ya ushirikina katika mji huo,jambo ambalo lilipingwa na uongozi wa Serikali ya kata ambayo inadaiwa kuwa ilikataa kutoa kibali cha  kumhidhinisha Mganga huyo kufanya kazi  Mbamba bay  .

Walieleza kuwa  baada ya Serikali kutokubali kumruhusu Mganga huyo  kutofanya kazi ndipo wananchi wenye hasira kali walikusanyika na kuanza kuvamia baadhi ya majengo ya Serikali na ofisi ya CCM ya kata hiyo kisha waliaribu samani za ofisi na kuchoma moto nyaraka zote na baadaye walitawanyika.

Kwa upande wake  Mkuu wa wilaya ya Mbinga Kanali   Mstaafu Edmundi Mjengwa alipoulizwa na mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/  kwa njia ya simu kuhusiana na tukio hilo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwepo uharibifu wa mali lakini alikataa kuelezea zaidi kwa madai  alikuwa safarini vijijini  kwa shughuli za kikazi .

Naye Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda  amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo ambalo alidai limetokea February 9 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi huko Mbamba -bay  ambako kundi kubwa la watu wenye hasira kali lilivamia majengo mbalimbali  ya Serikali zikiwemo ofisi  ya Afisa  Mfawidhi  wa bandari  ya Mbambabay ambako waling’oa madirisha matatu ya jengo hilo ,ofisi ya Afisa tarafa ya Ruhekei ambako walibomoa mlango na kisha kuchoma  moto nyaraka zilizokuwa zimehifadhiwa ndani ya ofisi hiyo  na baadaye walikwenda ofisi ya CCM nako walivunja mlango na kuzichoma moto nyaraka zilizomo .

Alifafanua  kuwa baadhi ya samani zilizo haribiwa na kundi la wananchi wenye hasira kali ni pamoja na pikipiki aliyokuwa akiitumia Afisa Tarafa ,umemejua (sola) , Radio pamoja na mashine ya kupigia chapa  ambazo ni mali ya bandari na ofisi ya Tarafa .


Kamanda Kamuhanda alisema kuwa chanzo cha vurugu hizo ni baada ya Mganga wa Jadi Yahaya (Jongo) kunyimwa kibali cha kuwafichua na kuwatambua  watu wanaodaiwa kuwa ni wachawi kataka mji huo,hata hivyo mpaka sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiriwa kuhusiana na tukio hilo na polisi inaendelea kufanya upelelezi wa kina .
MWISHO             

Saturday, February 11, 2012

WAWILI WAUAWA KWA KUCHOMWA MOTO KWA KUDHANIWA MAJAMBAZI

WAWILI WAUAWA KWA KUCHOMWA MOTO KWA KUDHANIWA MAJAMBAZI
Na Gideon Mwakanosya, Songea
WATU  wawili kati ya wanne ambao majina yao haya kuweza kufahamika wameuawa kwakupigwa na kisha kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali katika eneo la Ruhuwiko Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.
Habari zilizopatikana jana mjini hapa ambazo zimethibitishwa na kamanda polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda tukio hilo limetokea February 8 Mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi eneo la Ruhuwiko nje kidogo ya mji wa Songea.
Kamanda Kamuhanda alisema kuwa siku hiyo ya tukio inadaiwa watu wanne wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki mbili tofauti walikwenda katika eneo la Ruhuwiko ambako walimkuta mwanamke mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa alikuwa anafunga mbuzi wake kwenye eneo la malisho ambaye walimsalimia na kumuuliza kama anamfahamu msichana mmoja aitwaye Neema.
Alisema kuwa mwanamke huyo badaye aliwajibu kuwa huyo Neema hamfahamu lakini baadaye aliwahoji awaeleze sababu wanayo mtafutia jambo ambalo lilipelekea kuwa na mashaka na watu hao ambao baadaye waliondoka na kuelekea mbele zaidi kwa lengo la kumuulizia msichana huyo ambako walikutana na watu wengine na waliwauliza kama wanamfahamu msichana Neema ambapo watu hao walianza kuwauliza mahali wanapo tokea.
 Alifafanua kuwa watu hao baada ya kuona kuwa majibu yao yana utata ghafla watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki walianza kukimbia na kutokomea kusiko julikana na  kuwaacha wenzao wawili jambo ambalo lililowafanya kuwa na mashaka na watu hao kisha walianza kuwapiga huku mmoja kati ya watuhumiwa hawa alifungwa kamba na baadaye waliwachoma moto.
Alieleza zaidi kuwa wakati wananchi hao wanaendelea kuwapiga watuhumiwa walikili kuwa ndio waliohusika katika matukio matatu ya mahuaji yaliyo tokea katika kipindi cha mwezi mmoja ambapo inadaiwa katika eneo la Ruhuwiko kumekuwa na wimbi la wasichana kuuawa na watu wasiofahamika.
Alibainisha zaidi kuwa katika kipindi cha mwezi mmoja wasichana watatu wameuwawa katika mazingira ya kutatanisha inadaiwa kuwa watu wanaofanya vitendo hivyo vya kinyama wanatoka nchi jirani ya msumbiji ambao licha ya kuwa uhakika wa jambo hilo bado haujafahamika na polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kufuatia kuwepo uvumi wa watuhumiwa hao ambao wamekuwa wakiwavamia wasichana na kuwauwa kisha wamekuwa wakiwakata baadhi ya sehemu za siri na kwenda nazo nchi jirani ya msumbiji ambako wamekuwa wakichimba madini.
Kamuhanda alieleza kuwa baada ya muda si mrefu polisi walipata taarifa ya tukio hilo na walikwenda eneo la tukio hilo ambako waliwakuta watuhumiwa hao wakiwa tayari wameuawa na wananchi wenye hasira kwa kuchomwa moto ambapo maiti hao walichukuliwa na jeshi hilo na kupelekwa kuhifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Serikali ya Mkoa Songea ambako mamia ya wakazi wa manispaa hiyo walifulika kwa ajiri ya kutambua maiti hizo na kuwafanya polisi waweke ulinzi mkali  katika milango ya kuingilia katika  hospitali hiyo ili kudhibiti usalama wa wagonjwa waliofika kutibiwa na waliolazwa katika hospitali hiyo .
Hata hivyo polisi inamshikilia mwanamke mmoja kwa mahojiano zaidi na kuwataka wananchi kujichukulia sheria mkononi na amedai kuwa polisi inaendelea kufanya uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo .
 Mwisho

WAWINDAJI HARAMU WAWILI WAKAMATWA KWENYE HIFADHI YA WANYAMA
Na  Mwandishi Wetu, Songea
WAWINDAJI haramu wawili wakazi wa Kijiji cha Muhuwezi Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na bunduki aina ya gobole kwenye mbuga ya hifadhi ya wanyama poli iliyopo kijijini Muhuwezi.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya 12: 30 jioni huko katika mbuga ya wanyama poli ya muhuwesi  eneo la kata ya kalulu wilayani humo.
 Kamuhanda aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Habedi Kahama (25) na Mohamed Mohamed (29) wote wakazi wa kijiji cha Shauritanga kilichopo wilayani Tunduru ambao inadaiwa siku hiyo ya tukio wakiwa katikati eneo la mbuga la wanyama ghafla walijikuta wako mikononi  mwa Askari wa kikosi cha kuzuia ujangili Kanda ya Kusini ambao walikuwa wakifanya doria kwenye eneo hilo.
Alfafanua kuwa watuhumiwa hao inadaiwa waliingia kwenye mbuga ya hifadhi ya wanyama bila ya kuwa na kibali na walikutwa wakiwa na silaha ambayo inahofiwa kuwa imekuwa ikitumika na watuhumiwa hao kuwinda wanyama bila ya kuwa na leseni.
 Alieleza zaidi kuwa askali wa kikosi cha kuzua ujangili waliwakamata watuhumiwa hao wakiwa na silaha aina ya gobole isiyo kuwa na namba wala kibali cha kumiliki silaha hiyo na kwamba watuhumiwa ni wahindaji haramu kwenye eneo la mbuga la wanyama la Muhuwesi.
Hata hivyo Kamanda Kamuhanda alisema kuwa kwa sasa hivi taratibu zinafanywa za kuwafikisha watuhumiwa hao Mahakamani mara tu upelelezi utakapo kamilika.
 Mwisho.

Thursday, February 9, 2012

TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA

Diwani wa Kata ya Mletele, Halmashauri ya Manispaa ya Songea Fravian Tamaambele Legele (Mzee Panya) enzi za uhai wake

Taarifa za kifo cha Mzee Panya zilianza kusambaa majira ya asubuhi leo, baada ya mtandao huu kuwasiliana na ndugu na jamaa wa Marehemu Mzee huyo, walithibitisha kutokea kwa msiba huo

Marehemu Mzee Panya kama alivyokuwa anapenda kujiita mwenyewe, alianza kuugua ghafla mwishoni mwa mwezi wa kwanza akiwa njiani anatoka Wilayani Tunduru ambako alikuwa anafanya shughuli ya kutekeleza mradi wa ujenzi

Ikumbukwe kuwa Mzee Panya licha ya kuwa Diwani mwenye hekima na busara alikuwa ana kampuni yake ya ukandarasi ambayo ilikuwa inatekeleza miradi mbalimbali katika Halmashauri za Mkoa wa Ruvuma

Mzee Panya alikimbizwa Hospital ya Mkoa wa Songea kwa ajili ya matibabu ambako alilazwa hadi mauti yana mkuta hii leo majira ya asubuhi

Toka uchaguzi mkuu wa Wabunge, Madiwani na Rais ufanyike Octoba 30 mwaka 2010, Mzee Panya ni Diwani wa pili kufariki ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea, kwani wa kwanza alikuwa ni Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ally Said Manya ambaye alifariki mwaka jana 2011 katika Hospitali ya Misheni ya Peramiho

Mtandao huu, utaendelea kuwaletea habari zitakazokuwa zinajiri kwenye eneo la mazishi huko nyumbani kwake Mletele

Bwana alitoa, bwana ametwa jina lake lihimidiwe,
Sote tu wasafiri yeye ametangulia nasi tunamfuata
Roho yake na Roho za marehemu wengine wastarehe kwa amani
                ############# AMINA ##############

Wednesday, February 8, 2012

UCHAKAVU WA MIUNDOMBINU NA UHABA WA WATUMISHI WA MAHAKAMA NI KIKWAZO CHA UPATIKANAJI HAKI

Na Augustino Chindiye Tunduru

IMEELEZWA kuwa Uchakavu wa Miundombinu ya Majengo ya Mahakama za Mwanzo Wilayani Tunduru Moani Ruvuma na kutokuwepo kwa Watumishi wa Kutosha katika Idara hiyo ni kikwazo kikubwa cha upatikanaji wa haki kwa wakati.

Hayo yalisemwa na Hakimu Mkazo mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya hiyo Geofrey Muhiuni wakati akiongea na wadau wa Sheria katika maadhimisho ya siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama ya Wilaya hiyo.

Akifafanua taarifa hiyo Muhini alisema kuwa Wilaya hiyo inayotambulika kuwa na Mahakama 9 na Mahakama 3 tu ndizo zenye majengo yenye sifa za kufanyiwa hazi na mahakama 6 zilizobakia majengo yake
yapo hoi bini taabani.

Katika Taarifa hiyo Bw. Muhini alibainisha kuwa uchakavu huo mkubwa wa majengo hayo ya kutolea haki unazukabiri Mahakama za mwanzo Nakapanya,Lukumbule,Mtina, Namasakata Matemanga na Nalsi.
Alisema kufutia hali hiyo Wananchi wengi wamekuwa wakitembea umbali mrefu ili kufuata huduma hiyo ambayo imekuwa ikipatikana katika Mahakama ya Mwanzo Mlingoti iliyopo Mjini Tunduru hali ambayo
imesababisha kuwepo kwa mlundikano wa kesi.

Akizungumzia upungufu wa ikama ya watumishi katika idara hiyo alisema kuwa kati ya Mahakama hizo Tisa zinazotakiwa kutoa huduma hiyo mbali na uchakavu wa majengo yake idara hiyo inao Mahakimu Watatu tu (3)hali amyo imekuwaa ikiwawia vigumu kutembelea katika mahakama zote ndani katika kipindi cha wiki.

Alisema pamoja na idara hiyo kukabiliwa na upungufu huo mkubwa wa mahakimu pia ina upungufu mkubwa wa watumishi katika ngazi za Ukarani,Walinzi na wahuduma hali mbayo huwafanya mahakimu hao kufanya
pia baadhi ya kazi zilizotakiwa kufanywa na watumishi wa idara hizo.


Awali akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Madaha, Afisa tarafa wa Tarafa ya Mlingoti  Manufredi Hyera aliwataka wadau hao kutoa elimu kwa watu wanao waznguka ili watambue umuhimu wa kutii sheria na kwamba kutoifahamu Sheria siyo kisingizio cha kufanya makosa.
Upande wa ujumbe uliotolewa kupitia Wimbo wa Kwaya kutoka katika kikundi cha Uwanja wa Ndege Mjini hapa uliwasomba mahakimu kuangalia uwezekano wa kutoa adhabu Mbadala wakati wanapotekeleza wajibu wao badala ya kila mtuhumiwa kuhukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo Gerezani zikiwa ni juhudi za kupunguza mirundikano katika Magereza yote Nchini.
Mwisho

Tuesday, February 7, 2012

WAKAMATWA KWA KUKUTWA NA MISOKOTO 19 YA BANGI NA WAKIVUTA BANGI NA

                KAMANDA WA POLISI MKOA WA RUVUMA MICHAEL KAMUHANDA

Na Gideon  Mwakanosya, Songea

POLISI  mkoani  Ruvuma imewatia mbaroni wakazi kumi na tatu wa Songea mjini kwa tuhuma za kukutwa wakivuta  bangi na pia wakiwa na misokoto kumi na tisa na glamu 250 ya bangi  ndani ya uwanja wa  michezo wa majimaji wakati wa mashindano ya mpira wa miguu ligi ya daraja la kwanza ngazi ya taifa kati ya timu ya Majimaji na JKT Mlale.

Habari zilizopatikana jana mjini hapa ambazo zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda zimesema kuwa tukio hilo lilitokea  February 4 mwaka huu majira saa kumi na moja na nusu jioni ndani ya uwanja wa Majimaji ambapo watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na kiongozi wao Ally Hassani (20) mkazi wa majengo Songea.

Kamhanda alisema kuwa wakati timu za Majimaji na JKT Mlale zikiendelea kucheza kwenye mpambano wa ligi ngazi ya kwanza ya Taifa watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa waliendelea kuvuta bangi na Ally Hassani  ndiye anadaiwa kuwa alikuwa akipita kuiuza.

Alifafanua kuwa watuhumiwa wote kumi na tatu ambao wengine hakuwataja majina, watafikishwa Mahakamani mara tu upelelezi wa tukio hilo utakapo kamilika na kwamba kwa hivi sasa polisi inaendelea kuwasaka wengine ambao wanadaiwa kuwa walikimbia pindi walipoona wenzao wanakamatwa na polisi.

Katika pambano hilo ambalo lilihudhuliwa na wapenzi wa Club za majimaji  na JKT Mlale  katika pambano hilo pamoja na kuwepo purukushani zilizo sababishwa na watuhumiwa hao mpira uliendea kuchezwa hadi dakika ya mwisho ambapo majimaji na JKT Mlale zilitoka bila bila.

Mwisho.

Monday, February 6, 2012

WATOTO YATIMA WANAOSOMA SEKONDARI TUNDURU WAKOSA CHAKULA


                            MKUU WA WILAYA YA TUNDURU JUMA MADAHA

Na,Augustino Chindiye Tunduru
ZAIDI ya Watoto yatima 3000 wanaosoma katika Shule za Sekondari na Msingi Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma wamelalamika kukosa huduma ya chakula ambacho hutolewa katika shule hizo kutokana na wao kutochangia fedha za kuchangia ili kuwawezesha kupata huduma hiyo.

Wakiongea kwa nyakati tofauti wanafunzi hao wamesema kuwa toka shule zifunguliwe mwanzoni mwa mwaka huu ambapo wanafunzi hao wamekuwa hawaruhusiwi kunywa uji wala chakula cha mchana kama ambavyo wanafunzi wenzao hupewa huduma hiyo.

Katika taarifa hiyo wanafunzi hao walisema kuwa hali hiyo mbali na kuonekana kuwa wanabaguliwa lakini kitendo hicho kimekuwa
kikiwakatisha tamaa ya kuendelea na masomo katika shule zao.

Aidha wanafunzi hao walidai kuwa kitendo hicho cha viongozi wa Shule kuwabagua kupata huduma hiyo pia kimewasababisha kuonekana kwa tabaka la Watoto hao wasio na Wazazi na walezi kunyanyaswa na wanafunzi wenzao hali inayotishia kulididimiza kundi hilo kitaaluma.

Alipotakiwa kuzungumzia hali hiyo Afisa Elimu Shule za Sekondari
Wilayani humo Ally Mtamila mbali na kukiri kuwepo kwa changa moto hiyo alisema kuwa ipo haja ya kuboreshwa kwa taarifa za Watoto hao hasa kwa wasio kuwa na Walezi wa kuwahudumia ili wanapo pangiwa Shule vigezo vyao viwawezeshe kupangwa katika Shule za Bweni ambazo chakula chao hutolewa na Serikali.

Upande wa afisa maendeleo ya jamii wa Wilaya hiyo Mary Ding`ohi alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo mbali na kukiri kuwepo kwa kero hiyo alisema kuwa tatizo hilo limetokana na kuchelewa kwa fedha za kuwaghalamia wanafunzi hao.

Alisema hata hivyo tayari idara yake imekwisha pokea kiasi cha Shiligi Milioni 35.763 ambazo kati yake Tsh. 15,976,000 zimepangwa kughalamia malipo ya Ada, kununua sare za Shule na Michango hiyo ya Chakula kwa Watoto 3215 wanaosoma katika Shule hizo.

Ding`ohi aliendelea kufafanua kuwa Fedha hizo ambazo kila
mwanafunzi yatima amepangiwa kulipiwa Tsh. 70,000 kwa mgawanyo wa Tsh.20,000 za Ada na Tsh.50,000 kama mchango wa chakula kwa mwaka mzima fedha hizo zimepangwa kulipwa kuanzia Wiki ijayo.

Mwisho

Sunday, February 5, 2012

TAIFA LIMEKWAMA KIUCHUMI LINAHITAJI UFUFUO NA UJENZI MPYA WA VIWANDA

                                                     RAIS JAKAYA KIKWETE
Na Stephano Mango,Songea
MSINGI wa uchumi wa nchi kwa sasa ni lazima utazamwe katika kuanzisha na kufufua viwanda kwa ajiri ya maendeleo ya kiuchumi ili wananchi na taifa liweze kusonga mbele kwani kwa dalili zilizopo tutaendelea kulalamika na hatimaye kushindwa kujitegemea kabisa.
Ni wazi kuwa sehemu kubwa ya matatizo ya uchumi yanayoikabili serikali ya Rais Jakaya Kikwete, yana mizizi katika utendaji kazi wa awamu mbili zilizomtangulia kwani udhaifu ulijidhihirisha katika kupanga uchumi kwa maendeleo ya nchi
Kuna sura tatu za kuzingatia katika uchumi wa Tanzania na ule wan chi zote za Dunia ya tatu,kwanza ni dhaifu kiuchumi,pili kwa sehemu kubwa ni tegemezi kwa fedha kutoka nje,tatu,kadri utegemezi kiuchumi unavyoendelea ndivyo uhai wa kisiasa na kiuchumi utakavyoendelea kuwa tegemezi
Ufufuaji wa viwanda vilivyokufa na ujenzi wa viwanda vipya nchini uwe msingi mkubwa wa kuiondoa nchi hapa ilipo na kulijenga Taifa na watu wake wawe  wenye uchumi imara ambao utasababisha kuwe na maendeleo ya vitu
Katika Dunia hii ambayo nchi zinazoendelea zinashindana  kwa ujenzi wa viwanda,nasi hatuwezi kujiondoa kwenye sekta hiyo kama kweli tunataka kujikwamua kiuchumi ,kitendo cha kupuuza hoja hiyo ni kukimbilia kwenye uibuaji wa mipango mahututi ya kuokoa uchumi wa nchi na ile ya kuwajaza wananchi mabilioni ya Jk ambayo ni mipango mfu
Rasilimali tulizo jaliwa kuwa nazo hapa nchini hazitakuwa na maana kubwa kama zitashindwa kutumika katika kutokomeza umaskini wa watanzania kutokana na ukosefu wa ajira ambazo wangezipata kwa kuajiriwa kwenye viwanda ambavyo vingekuwa vinatumia rasilimali tulizonazo
Uwepo wa viwanda ni msingi mkubwa wa maendeleo katika nchi yeyote dunia licha ya kupunguza umaskini kutokana na watu wake kuajiriwa,pia husababisha wananchi kupenda bidhaa za kwao na kwamba fedha zinazotumika kununua  bidhaa nje ya nchi kama vile viatu,kanga,vitenge,majembe,pini,sindano na bidhaa zingine ambazo zinaweza kutengenezwa hapa
 Zingeweza kuchangia kasi ya mzunguko wa fedha ambapo matokeo yake yangeleta ustawi kwa wananchi na taifa kiujumla kwani pengo la wenye nacho na wasio nacho lingepungua sana na hata kupanda kwa gharama za maisha kungepungua
Ili kuweza kuleta hali chanya katika kuondokana na umaskini wa watanzania na uchumi goigoi,msingi wa kwanza ni kuasisi kwa makusudi uhusiano kati ya sekta mbili kuu za uzalishaji ambazo ni viwanda na kilimo ambapo sekta hizi zinaweza kuendelea kwa uhakika kama shughuli zake zitashabihiana na kutegemeana
Msingi wa pili ni kuweka uwiano wa ndani kwa hizi sekta mbili kwasababu ndani ya sekta ya kilimo kunapaswa kuwe na uwiano kati ya uzalishaji wa chakula na uzalishaji wa (mazao) malighafi za viwandani
Kati ya uzalishaji mkubwa na uzalishaji mdogo,kati ya mfumo wa sasa wa uzalishaji na ule wa kale,na kati ya uzalishaji binafsi na uzalishaji wa umma ambapo jambo muhimu hapa ni kuwa na kiunganishi kikuu katika kusukuma mbele maendeleo ya vingine
Hapa kiunganishi kikuu ni uzalishaji wa chakula kwasababu watu ambao ndio rasilimali muhimu na nguvu ya msingi kwa maendeleo hivyo lazima wale chakula bora kabla ya kupata nguvu ya kufanya mambo mengine
Msingi wa tatu ni kuwa na uwiano ndani ya viwanda ambapo idara muhimu katika sekta hii ni viwanda vikuu na viwanda vyepesi au vya kati,ikiwa jukumu la viwanda vikubwa ni kuvipatia viwanda vya kati mashine za uzalishaji mali
Kazi ya viwanda vikubwa ni kuzalisha mashine za kuzalisha mashine ambazo vinatumika kwenye viwanda vidogo kwa maana ya vipuri na kuondoa tatizo la kutegemea vipuri kutoka nje
Viwanda vya kati ni sekta inayozalisha bidhaa za walaji kama vile nguo,viatu,pamba(nyuzi),bia,zana za kilimo,vifaa vya kupasua mbao,mitambo ya maji na vingine vya aina hiyo ambapo pia viwanda vya kati ni sekta inayovigharamia viwanda vikuu kwa maana ya kuwa kule ambako inapata mashine na inatoa bidhaa za mlaji kwa watumishi wa sekta zote mbili
Siyo tu kwamba ujenzi wa viwanda vikubwa nchini ni muhimu katika kujenga msingi wa mapinduzi ya kiteknologia na uvumbuzi,bali pia unasaidia kuimarisha uwezo wa nchi katika kudhibiti vizuri mazingira
Katika mchakato wa maendeleo viwanda vikubwa vinajenga mabwawa ili kudhibiti mafuriko na kuhifadhi maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji,pia vinarahisisha kupeleka umeme vijijini,hatua ambayo ni muhimu na ya awali katika uwiano bora wa maendeleo ya viwanda,na upunguzaji tofauti ya maisha kati ya vijijini na mijini
Viwanda vikubwa ni muhimu pia katika kuendeleza mfumo imara wa uchukuzi na mawasiliano na kwa sababu ya umuhimu wake katika uchumi hakuna nchi iliyowahi kuendelea bila kuwa na viwanda vikubwa
Ni kutokana na nguvu ya eneo hili nchi zenye viwanda zimeweza kuzitawala na kuzidhibiti nchi maskini ikiwemo Tanzania ndio maana kutokana na maono stahiki ya kujenga Taifa linalopaswa kujitegeme,Serikali ya awamu ya kwanza ilijenga viwanda vingi vya kati ili kuondoa utegemezi kwa mataifa ya nje
Ilijenga viwanda vya nguo,mbolea,zana za kilimo na vya bidhaa karibu zote za mlaji,awamu hiyo ilifanikiwa kujenga viwanda vya kutengeneza mashine(Moshi Mashine Tools) viwanda vya kutengeneza magari(Nyumbu) kiasi cha kukaribia kujitosheleza kwa mahitaji ya ndani
Leo,viwanda hivyo havipo tena,vilitelekezwa,vikauzwa katika mkumbo wa ubinafsishaji,vikauawa na mabepari wa kimataifa ili kujenga na kuendeleza utegemezi wa Tanzania kwa bidhaa kutoka nje
Sababu nyingine ni ulimbukeni wa walioko madarakani na ushabiki unaoenezwa nao kwa bidhaa kutoka nje,jambo ambalo linaonyesha kujikana na kudharau chako na kuhangaika na bidhaa ambazo hawajashirikishwa
Kama nchi ingekuwa na watawala wabunifu wa maendeleo ya kweli,majengo ya minara pacha ya benki kuu yangejenga viwanda vingi ambavyo vingewezesha kuinua uchumi wa watanzania na nchi kiujumla lakini badala yake nchi imejiingiza kwenye ujenzi wa maghorofa yaendayo mawinguni na majumba ya anasa yasiyozalisha utajiri
Matumizi haya mabaya ya rasilimali yanafanya nchi kama Tanzania ziyapigie magoti mataifa makubwa kuomba mikopo zaidi,na wakati huo huo uchumi hauzalishi vya kutosha kuwezesha ulipaji madeni na riba ya mikopo hiyo
Misaada ya mabilioni tunatomwagiwa na nchi za China,Japan,Marekani na Uingereza na kufanya watawala kurukaruka kwa furaha kama ndama,ingekuwa ya manufaa zaidi kama ingetolewa kwa mfano wa viwanda ili kuliwezesha Taifa  kujitegemea na kujiendeleza
Ilivyo sasa,ni misaada inayoongeza na kuimarisha utamaduni wa utegemezi kwani wanaotoa mikopo na misaada hawataki  Tanzania iwe na ndoana wala ijue jinsi ya kuvua samaki kwasababu wanataka kila siku Tanzania na nchi za Dunia ya tatu zipige magoti langoni mwa tajiri na kuomba samaki
Ni wazi huu ni utumwa,je Mustapha Mkulo Waziri wa fedha na uchumi na wenzake Serikalini wanakubali kumeza dawa chungu ya kuponya ugonjwa unaolisumbua Taifa maskini lenye rasilimali zote muhimu zinazosababisha mchakato wa maendeleo kukamilika
Serikali inapaswa kuelewa kwamba bila ya kuweka mikakati bora,kasi ya ukuaji viwanda nchini itaendelea kuwa ndogo kama ilivyo sasa,hivyo inatakiwa kuona Serikali inaanzisha mpango wa kuendeleza viwanda na hatimaye kukuza na kuondoa umaskini
Mpango huo wa kuendeleza viwanda ni lazima uwe na sera na mikakati madhubuti ili ufanikiwe ambapo mbinu mbalimbali zina hitajika na mambo makuu mengine katika utekelezaji wenye ufanisi wa kuanzisha mchakato wa ufufuo na ujenzi wa viwanda kwa ukombozi wa Taifa letu
Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana 0715-335051
www.stephanomango.blogspot.com


Friday, February 3, 2012

JOHN KASEMBO AWALETEA WATANZANIA KITABU CHA MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA BARA: TULIKOTOKA, TULIPO NA TUNAKOKWENDA

                                                KIPO MITAANI SASA
                        JOHN MTWALE KASEMBO

JINA LA KITABU: MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA BARA: TULIKOTOKA, TULIPO NA TUNAKOKWENDA

MWANDISHI: JOHN MTWALE KASEMBO
Ni mzaliwa wa Mkoa wa Mwanza. Alisoma shule ya msingi Shamaliwa. Na baadaye masomo ya Sekondari kwenye Seminari za Nyegezi - Mwanza na Maua - Moshi. 

Ni mwezeshaji na mtoa mada wa mambo ya uongozi, dini, vijana, falsafa, ujasiriamali na amali za maisha. Ni mhitimu wa masomo ya falsafa na dini katika Chuo cha Mtakatifu Augustino Peramiho ambacho ni Chuo Kishiriki cha Chuo Kikuu cha Urbaniana, Roma.

Tena yeye ni mtafiti wa maendeleo ya Tanzania. Sasa anaendelea na masomo ya Shahada ya Kwanza ya Teolojia katika Chuo hicho hicho.

Kitabu hiki kimechapishwa na kampuni ya Kolbe printing press, Nairobi nchini Kenya.

Yaliyomo
Kutabaruku................................................................................................. 7
Salamu za Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ...................... 9
Shukrani..................................................................................................... 11
Dibaji.......................................................................................................... 15
Utangulizi................................................................................................... 17
Vifupisho................................................................................................... 23
Sehemu ya Kwanza
TANZANIA TULIKOTOKA
1. UKOLONI TANZANIA BARA........................................................... 27
2. HARAKATI ZA UKOMBOZI............................................................. 39
3. UHURU................................................................................................ 47
4. MAISHA BAADA YA UHURU......................................................... 57
Sehemu ya Pili
TANZANIA TULIPO
5. JUBILEI YA MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA BARA....... 69
6. JUBILEI NI KUANGALIA TUNU ZETU KAMA WATANZANIA. 78
7. JUBILEI NA CHANGAMOTO ZETU................................................ 86
Sehemu ya Tatu
TANZANIA TUNAKOKWENDA
8. JUBILEI NI KUANZA UPYA............................................................. 107
9. KANUNI YA TIBA MCHEPUO KWA MAENDELEO
YA TAIFA LETU..................................................................................... 133
TATHMINI NA MOTISHA..................................................................... 145
HITIMISHO.............................................................................................. 159
REJEA....................................................................................................... 169
PICHA YA JALADA LA KITABU NIMEIAMBATANISHA KAMA ATTACHMENT. UNAWEZA KUIDOWNLOAD NA KUIWEKA PIA.
MUHTASARI:
Ndugu Watanzania wenzangu, nimendika kitabu hiki kwa malengo matatu. Kwanza kitabu hiki kinalenga kupanua mawazo na mtazamo wetu Watanzania kuhusu dhana ya Jubilei ambayo sisi tunafanya kumbukumbu ya miaka 50 ya uhuru wetu yaani kujua kuwa nini tunatakiwa tufanye. Uelewa huu utakuwa wa msingi kwa kizazi kitakachofanya Jubilei ya miaka 75 au miaka 100 ijayo ya taifa letu. Tena, lengo la pili la kuandika kitabu hiki ni kutoa uelewa ambao utakuwa ni chagizo la mabadiliko, ukombozi na maendeleo kwa watu tulioamua kutafakari na kutenda kadiri ya ukweli kwa manufaa ya taifa letu katika kizazi hiki na kijacho wakati huu tunapofanya Jubilei ya miaka 50 ya uhuru wetu. Na zaidi, lengo langu la mwisho la kuandika kitabu hiki ni kuchukua wajibu kama Mtanzania wa kushirikisha mawazo yangu kwa  Watanzania wenzangu ili kuyatafuta maendeleo ya kweli ya taifa letu na zaidi sana ni kutoa mchango wangu katika sherehe hizi za taifa letu. Sikupenda sherehe kubwa kama hii ipite kama meli isiyoacha nyayo baharini.

Kitabu hiki kimegawanyika katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ni Tanzania - tulikotoka ambayo inaongelea masuala ya ukoloni, harakati za ukombozi, uhuru na maisha baada ya uhuru. Sehemu ya pili inaongelea Tanzania – tulipo inayozungumzia hali yetu leo kiuchumi, kisiasa na kijamii nikijadili changamoto zetu kama taifa na tunu zetu tulizonazo tangu uhuru mpaka sasa kama Watanzania na maana na umuhimu wa sherehe zetu za Jubilei ya miaka 50. Hatimaye, sehemu ya tatu, inazungumzia Tanzania – tunakokwenda (mwanzo mpya) ikijadili wapi tunakokwenda kama taifa yaani kuwa na mwanzo mpya na kuingalia kanuni ya tiba mchepuo kama nyenzo ya kutufikisha huko.  Kama yule mshairi na mtunzi wa vitabu wa Uingereza Robert Louis Stevenson alivyopata kusema kwamba, “Usipime siku yako kwa yale uliyovuna bali pima kwa yale uliyopanda.” Malengo hayo ndiyo yamenifanya nipande mbegu ya kitabu hiki kwa kuitakia mema nchi yangu kwa miaka 50 mingine.

Mwisho natabaruku kitabu hiki ni kwa heshima ya taifa langu Tanzania linalofanya Jubilei ya miaka 50 ya uhuru wake na kwa namna ya pekee Mama yangu mpendwa Christina Shija, baba yangu mpendwa marehemu Gabriel Kasembo, marehemu babu yangu Chifu Yohana Kilangabhana Kasembo, marehemu bibi yangu Agatha Mija Michael, Hayati Askofu Mkuu Anthony Mayala, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Watanzania wote ninaochangia nao utaifa na nia njema ya kuitakia mema nchi yetu na zaidi wenye moyo wa dhati wa kujenga taifa la Tanzania lenye heshima, upendo, amani na maendeleo ya kweli na ya uhakika kwa kizazi hiki na kijacho! Nakutakieni usomaji mwema na mafanikio tele katika maadhimisho ya jubilei ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania huku tu tukifakari  uwepo, maisha na mustakabali wa taifa letu !

KWA KUAGIZA NAKALA YA KITABU HIKI ADIMU NA ADHIMU KWA TAIFA LETU, WASILIANA NA:

JOHN MTWALE KASEMBO
P.O BOX 22, PERAMIHO.
SIMU: 0755 417 074 / 0712 120 775

WANNE WAFA KATIKA MATUKIO MANNE TOFAUTI MKOANI RUVUMA

KAMANDA WA POLISI MKOA WA RUVUMA MICHAEL KAMUHANDA

Na Gideon Mwakanosya, Songea
WATU wanne wa Vijiji vya Litolongi na Minango  vilivyopo Kata ya Kigonsera Wilayani Mbinga na Mkaya kilichopo Kata ya Lituhi Wilayani Nyasa Mkoa wa Ruvuma  wamekufa katika Matukio matatu tofauti yakiwemo ya kupigwa na radi wakati mvua zikiwa zinaendelea kunyesha.
Wametajwa waliokufa kwa kupigwa na radi kuwa ni Manfred Komba (18) na Pascar Ndomba (33) wote wakazi wa Kijiji cha Minango Kata ya Kigonsera na mwingine ni Maria Kinunda (18) Mkazi wa Kijiji cha Litolongi Kata ya Kigonsera Wilayani humo na Martias Charle (52) Mkazi wa Kijiji cha Mkaya Kilichopo Kata ya Lituhi Wilaya mpya ya Nyasa ambaye alikutwa Porini akiwa amekufa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alisema kuwa tukio la kwanza lilitokea January 27 Mwaka huu majira ya Saa 11 Jioni huko katika Kijiji cha Minango kilichopo Kata ya Kigonsera ambako Komba na Ndomba kabla ya kukutwa na mauti walikuwa shambani wakilima.
Alieleza zaidi kuwa wakiwa wanaendelea kulima Majira ya Saa 11 Jioni ghafla manyunyu ya mvua yalianza na baadaye Mvua kubwa iliongezeka huku ikiwa imeambatana na radi ndipo walipoamua kuacha kuendelea kulima kasha wakaanza kukimbilia kwenye kibanda kwa ajili ya kujificha mvua lakini kabla hawajafika kwenye kibanda hicho walipigwa na radi na kufa papohapo.
Kamuhanda alisema kuwa tukio jingine lilitokea January 27 mwaka huu Majira ya saa 12 Jioni huko katika Kijiji cha Litolongo Kata ya Kigonsera wilayani humo Maria alipigwa na radi na kufa papohapo wakati akikimbilia ndani ya Nyumba yake kujificha Mvua.
Alifafanua kuwa Maria mapema inadaiwa kuwa alikuwa akifanya shughuli zake nje ya nyumba yake na baadaye Mvua zilipoanza kunyesha ambazo ziliambatana na radi ndizo zilizosababisha kukatisha Maisha yake kwa kupigwa na radi na kufariki papo hapo.
Wakati huo huo  Matias Charle (52) Mkazi wa Kijiji cha Mkaya kilichopo Kata ya Lituhi Wilayani Nyasa ambaye anadaiwa kuwa alikuwa mgonjwa wa akili na ni mlemavu wa mikono na miguu alikutwa porini akiwa amekufa.
Alieleza zaidi kuwa Charle anadaiwa kuwa wakati wa uhai wake Oktoba mwaka jana alitoweka nyumbani kwake na kutokomea kusikojulikana na jitihada za kumtafuta zilifanywa bila kuwepo mafanikio na Juzi majira ya saa 9 alasiri alikutwa porini akiwa amekufa.
Mwisho.