Na Amon Mtega,Songea SOKO kuu la Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma lililoungua moto mwaka 2003 na kuteketeza kabisa fedha na mali za wafanyabiashara wa soko hilo na kisha kujengwa upya na Manispaa hiyo kwa fedha zilizotoka kwa wahisani na taasisi za mikopo na kisha kuendelea kutoa huduma hiyo lakini bado linakabiliwa na changamoto mbali mbali. Akitoa taarifa ya uendeshaji wa soko hilo mkuu wa Masoko ya Manispaa ya Songea Salum Homera kwa Mjumbe wa bodi ya mikopo ya Serikali za Mitaa George Mallima Lubeleje alisema kuwa baada ya soko hilo kujengwa upya likiwa na meza 308 na maduka 161 na kwamba linatoa huduma kwa wananchi wa ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma. Alisema kuwa pamoja na huduma hizo halmashauri hukusanya kiasi cha shilingi milioni 9.4 kwa mwezi ambazo hutumika kuisaidia halmashauri kugharamia shughuli mbambali za kiutawala na utoaji huduma kwa wananchi pia serikali kuu hukusanya kodi ya mapato kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo ambayo huisaidia serikali kutoa huduma boraa kwa wananchi. Aidha pamoja na mafanikio hayo Homera alisema kuwa zipo changamoto ambazo zinahitaji kutatuliwa ili kuboresha mapato zaidi ikiwemo mahitaji ya ukarabati ambayo ni makubwa kuliko kiasi kinacho kusanywa na soko hilo,baadhi ya wafanyabiashara kuendesha biashara zao nje ya soko na kulikosesha soko mapato na kuchelewa kusainiwa kwa sheria ndogo za halmashauri ambazo huwa zina mapendekezo ya maboresho ya viwango vya kodi na ushuru mbali mbali. Kwa upande wao wafanyabiashara na wananchi wanaolitumia soko hilo walisema kuwa soko hilo bado linahitaji ukarabati mkubwa ili liweze kuwa na hadhi ya Manispaa na hasa katika maduka ya kuuzia nyama ambako kunahitaji usafi wa hali ya juu tofauti na hali ilivyo sasa. Naye mjumbe wa bodi ya mikopo ya Serikali za Mitaa George Malima Lubeleje akizungumza baada ya kukagua soko hilo mbali na kupongeza matumizi ya fedha ya mkopo iliyotolewa na bodi hiyo kwa ajili ya ujenzi huo alisema kuwa halmashauri inapaswa kusimamia sheria ndogo ambazo zitasaidia kuongeza kipato na kuweza kumaliza kulipa deni la mkopo huo ili iweze kupewa mkopo mwingine. mwisho |
Wednesday, September 21, 2011
MJUMBE WA BODI YA MIKOPO WA SERIKALI ZA MITAA ATEMBELEA SOKO LA SONGEA NA KUJIONEA CHANGAMOTO ZAKE
MAJAMBAZI WAUA,WAJERUHI,KUPORA SHILINGI MILIONI MBILI NA KUTOKOMEA ZAO
Na Steven Augustino,Tunduru
WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamemuua kwa kumpiga mapanga mkulima wa kitongoji cha Mkangwala kilichopo katika kijiji cha Mbatamila Wilayani Tunduru aliyefahamika kwa jina la Bibie Mtenje (25) na kumjeruhi vibaya mume wake Kasim Shaibu (35).
Taarifa kutoka katika kijiji hicho zinaeleza kuwa baada ya watu hao kutekeleza uharamia huo walifanikiwa kupora fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni mbili pamoja na kuchoma moto nyumba ya jirani yake aliyetambulika kwa jina la Anafi Alifa aliyedaiwa kutoka na kupeleka taarifa kwa majirani wakati tukio hilo likiendelea.
Ndugu wa majeruhi Shaibu ,Bw.Sandali Shaibu na Kazembe Rajabu wanao muuguza majeruhi huyo aliyelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Tunduru akiwa hajitambui walisema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Septemba 21 mwaka huu.
Wakifafanua taarifa hiyo wanafamilia hao walidai kuwa fedha alizo porwa majeruhi na kusababisha kifo cha mkewe zilitokana na mauzo ya viroba 24 vya mpunga ambao walilima na kufanikiwa kuvuna msimu uliopita wakiwa na matumaini ya kujiletea maendeleo baada ya kuuza.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda mbali na kukiri kuwepo kwa tukio hilo alisema kuwa jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na kwamba endapo watabainika watu kuhusika na tukio hilo sheria itafuata mkondo wake.
Mganga wa hospitali ya Wilaya ya Tunduru Dkt. George Chiwangu ambaye alimpokea na kumshughulikia majeruhi Shaibu alisema kuwa, majeruhi huyo ameumizwa vibaya kichwani na sehemu za tumboni kutokana na kukatwa mara nyingi na mapanga.
Naye Mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Mtenje, Dkt.Titus Tumbu alisema kuwa kifo chake kimesababishwa na kutokwa na damu nyigi zilizosababishwa na majeraha ya kukatwa na mapanga sehemu za kichwani.
Mwisho
MANISPAA YA SONGEA WAFANIKIWA KUDHIBITI MIMBA KWA WANAFUNZI WA SHULE ZA MSINGI
Na Thomas Lipuka,Songea
IDARA ya Elimu na wadau wa Elimu katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma,wamefanikiwa kuondoa tatizo la mimba kwa wanafunzi wa Shule za Msingi kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi 2011 ambapo hakuna mwanafunzi aliyepata mimba katika Shule zote za Msingi katika Manispaa hiyo.
Taarifa ya hali ya Elimu ya mwaka 2010/2011 iliyosomwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Zakaria Nachoa kwa wadau wa Elimu katika Ukumbi wa Songea Club hivi karibuni imebaini kuwa hakuna mimba iliyoripotiwa kwa wanafunzi wa Shule kwa Kata zote 21 za Manispaa hiyo.
Nachoa alisema mbinu iliyotumika katika kuzuia suala la mimba ni pamoja na ushirikiano wa karibĂș baina ya wazazi,walimu,wadau wa Elimu na Viongozi wa Elimu ngazi zote za Manispaa na hatimaye kufikia kufuta kabisa tatizo la mimba katika Shule za Msingi zote za Manispaa ya Songea.
Taarifa ya mandeleo ya Elimu katika Manispaa hiyo imetaja pia mafanikio zaidi yaliyojitokeza katika sekta ya Elimu ni pamoja na ufaulu kwa Wanafunzi waliomaliza Elimu ya Msingi 2010 ambapo Manispaa hiyo imekuwa ya kwanza Kimkoa, na kuzipita Wilaya za Songea,Mbinga,Namtumbo na Tunduru.
Hata hivyo changamoto kadha zimejitokeza katika tathmini elimu Manispaa ya Songea ambapo kuna uhaba wa vitabu vya kiada,jambo ambalo linapelekea kitabu kimoja cha kiada kutumiwa na wanafunzi 11 ama zaidi.
Changamoto zingine zilizotajwa katika tathmini hiyo ni uhaba wa walimu darasani, hivi sasa kuna walimu 820 wakati mahitaji ni walimu 1259 hivyo Manispaa ya Songea kuwa na upungufu wa walimu 439 darasani ,jambo ambalo linahitaji msaada toka Serikali kuu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea amewaambia wadau wa Elimu kuwa kuna upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa,vyoo na nyumba za walimu,ameomba wadau wa Elimu kujipanga kwa hatua za awali za ujenzi wa maboma ili wanafunzi wote watakao faulu 2011 waweze kupata nafasi kidato cha kwanza.
Kuhusu changamoto ya upatikanaji wa madawati wadau wamesema ni vema kujipanga upya kwani suala la miti ya kutengenezea madawati lipo kwenye uwezo wao, isipokuwa Serikali iwezeshe Manispaa ya fedha kwa vifaa vya kiwandani ili kuondoa tatizo la madawati hatimaye wanafunzi wapate mazingira bora ya kujifunzia na kuleta usikivu,wanaposoma ili kuongeza ufaulu.
Mkurugenzi wa Manispaa pia alitoa taarifa ya maendeleo ya Elimu ya watu wazima mbele ya Mwenyekiti wa kikao cha tathmini Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Sabaya kuwa Manispaa ya Songea ina watu 2883 ambao hawajui kusoma kuhesabu na kuandika sawa na asilimia 40% ya watu wazima wote wa Manispaa hiyo ambapo Mkuu huyo wa Wilaya akatia mkazo kwa Kata zote kuendeleza kwa kasi Elimu ya watu wazima ili kufuta kabisa asilimia ya wasiojua kusoma,kuandika na kuhesabu katika Manispaa ya Songea.
“Naagiza kisomo sasa kipambe moto kata zote waratibu Kata,walimu wakuu,watendaji ngazi zote wajibikeni ipasavyo” alisisitiza Bwana Sabay.
Mwenyekiti huyo wa Kikao hicho ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Sabaya amewaagiza viongozi wa Elimu Manispaa,Waratibu Kata,walimu na wadau wa Elimu kusimamia kikamilifu malengo ya kukuza taaluma katika Manispaa kwa kuhimiza mahudhurio ya wanafunzi,walimu kufundisha kikamilifu,wakaguzi kufuatilia ufundishaji na viongozi kutekeleza wajibu wao kwa kutoa stahiki zote za walimu ikiwemo malipo ya likizo,matibabu na posho zao za kujikimu.
MWISHO
Tuesday, September 20, 2011
HII, NIMIONGONI MWA SHUGHULI ZINAZOFANYWA NA TCCIA MKOA WA RUVUMA KATIKA KUTANGAZA BIIDHAA ZA WAJASILIAMALI WANAOLELEWA NA TAASISI HIYO MUHIMU KWA WAJASILIAMALI
Afisa Mtendaji wa TCCIA Mkoa wa Ruvuma Philemon Moyo akiangalia bidhaa aina ya mvinyo ikiwa katika aina mbalimbali zilizowekwa kwenye fremu maalum katika ofisi za TCCIA mkoa wa Ruvuma zilizopo kwenye jengo la NSSF mjini hapa
AJIKUTA MIKONONI MWA DOLA KWA KUSABABISHA KIFO CHA ADERINA KWA MADAI YA WIVU WA KIMAPENZI
Na Gideon Mwakanosya,Songea
JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma linamshikilia Mfanyabiashara mkazi wa wa Mbinga mjini Timotheo Komba (21) kwa tuhuma za kumuua muhudumu ya baa ya Mbuji iliyopo mjini humo ambaye awali alikuwa mpenzi wake
Akizungumza na Mwaandishi wa mtandao huu wa www.stephanomango.blogspot.com jana ofisini kwake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alimtaja mwanamke aliyeuawa kuwa ni Aderina Nchimbi(21) ambaye ni mkazi wa mtaa wa eneo la Shule ya Msingi Kiwanjani Mbinga Mjini
Kamuhanda alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 20 mwaka huu,majira ya saa moja asubuhi huko katika mtaa wa eneo la Shule ya Msingi Kiwanjani
Alisema kuwa inadaiwa siku ya tukio Afisa Upelelezi wa makosa ya jinai wa Wilaya ya Mbinga Mrakibu Msaidizi wa Polisi Edward Kavalambi akiwa na Askari wenzake wa kitengo cha Upelelezi ambao walikuwa doria waligundua kuuawa kwa Aderina ambaye alikutwa kando kando ya barabara jilani kabisa na nyumbani kwake
Alifafanua zaidi kuwa Maaskari kanzu hao baada ya kugundua tukio hilo la mauaji muda mfupi walifanikiwa kumkamata Komba ambaye anadaiwa kuwa katika kipindi cha nyuma alikuwa mpenzi wake tangu walipokuwa wakiishi katika Kijiji cha Mpepai
Alisema kuwa chanzo cha tukio hilo la mauaji kinasadikiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi ambapo inadaiwa kuwa marehemu Aderina kabla ya mauti hayajamkuta alikuwa akilazimishwa kufanya mapenzi na Mfanyabiashara huyo Komba ambaye alikuwa akijitahidi kumshawishi warudiane tena na mahusiano yao kama awali lakini mwanamke huyo alikuwa anakataa
Kamuhanda alisema kuwa mara upelelezi utakapokamilika mtuhumiwa Komba anatarajiwa kufikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma zinazomkabili,
MWENDESHA PIKIPIKI ASABABISHA KIFO CHA MTEMBEA KWA MIGUU
Na Gideon Mwakanosya,Songea
POLISI wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma wanamshikilia Mwendesha Pikipiki Felix Ndimbo (18) mkazi wa Kijiji cha Langilo kwa tuhuma za kumgonga mtembea kwa miguu Joseph Ndimbo (76) mkazi wa Kijiji cha Mkoha wilayani humo na kumsababishia kifo papo hapo
Habari zilizopatikana jana mjini hapa ambazo zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma zimeeleza kuwa lilitokea juzi majira ya 1:30 usiku kwenye barabara inayotoka Mbinga kwenda kijiji cha Langilo
Kamuhanda alibainisha zaidi kuwa siku hiyo ya tukio kwenye barabara hiyo Felix akiwa anaendesha Pikipiki ambayo haina namba za usajili aina ya SanLg ilimgonga mtembea kwa miguu mzee Joseph Ndimbo ambaye alikuwa anatoka Kijiji cha Langilo kwenda katika Kijiji cha Mkoha na kumsababishia kifo papo hapo
Alieleza zaidi kuwa chanzo cha tukio hilo mwendesha Pikipiki Felix akiwa anatokea Kijiji cha Mkoha kuelekea Kijiji cha Langilo akiwa kwenye mwendo mkali alimgonga mtembea kwa miguu Joseph ambaye alikuwa anatembea kandokando ya barabara upande wa kulia
Kamuhanda alisema kuwa mtuhumiwa Felix amekamatwa na anaendelea kuhojiwa na Polisi ambapo upelelezi wa tukio hilo ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili
MWISHO
Monday, September 19, 2011
WANANCHI KILIMANJARO WAPINGA SERIKALI KUWANYAN'GANYA ARDHI YAO NA KUMPATIA MWEKEZAJI
Na Efracia Massawe
WANAKIJIJI wanaoishi katika Msitu wa Westi Kilimanjaro eneo la Ngaranairobi Kata ya Nduma, wamesema kitendo cha serikali kubinafsisha eneo lao na kuwapatia wawekezaji kimewasababishia kutokuwa na makazi ya kuishi.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es salaam na wakilishi wa wanakijiji hao, Emmiliana Kimaro, wakati alipokuwa akiwasilisha mada katika Tamasha la Mtandao wa Jinsia lililofanyika makao makuu TGNP kuanzia septemba 13-16 mwaka huu.
Kimaro alisema kitendo kilichofanywa na serikali kuchukua eneo la msitu huo wakati ndani yake kulikuwa na wakazi wa kudumu bila kuwatafutia njia mbadala ya kuwahamishia wanakijiji hao, wamekifananisha na ukatili.
“Serikali ilitangaza kuwa wanakijiji wa Ngaranairoi tumepatiwa ardhi ni uongo, ila waliomilikishwa ardhi na serikali ni wanakijiji wa Ngurushani, na wengi wao ni wazee hata hivyo ardhi waliyokabidhiwa ni vipande vya roborobo” alisema Kimaro.
“Naongea kwa masikitiko pia naomba mtandao huu unilinde kwani kufichua siri iliyofichwa na serikali kwa muda lolote linaweza kutokea ila ukweli utabaki pale pale lazima kilio chetu jamii ikifahamu” alisisistiza Kimaro.
Mwisho.
WANAHARAKATI WAITAKA SERIKALI KUREKEBISHA SERA NA SHERIA KANDAMIZI
Na Stephano Mango
WANAHARAKATI wameshauri sera na sheria mbalimbali zilizotungwa na zitakazotungwa kwa ajili ya kukuza uchumi ili kuleta maisha bora endelevu kwa wananchi nchini zifanyiwe ufatiliaji ili kuhakisha zinawanufaisha watoto na wasichana wanaofanya ajira za ndani .
Wakichangia mada katika warsha ya Mapambano ya wanaharakati kwa wanawake katika njia za kujiajiri,kupata ajira na kujiletea maisha endelevu katika Tamasha la 10 la wiki ya Jinsia lililo malizika juzi jijini Dar es salaam wanaharakati hao walisema sheria nyingi zimetungwa na zimelenga kuleta maisha bora kwa watanzania wakiwemo wanawake lakini hakuna ufatiliaji unaofanyika kuhakikisha zinatekelezwa ili kuwanufaisha katika masuala ya kupata ajira.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Jinsia Tanzania,Mary Rusimbi alisema ili kuondokana na matatizo ya ajira kwa wanawake ni vizuri sera za kitaifa za kuondokana na umaskini zikiwemo sera ya ajira zitekelewe.
“Sera hizi inabidi zifanyiwe ufatiliaji ili kutambua kasi ya utekelezaji katika kuleta maisha bora na endelevu kwa wananchi,elimu katika masuala ya ajira inabidi itolewe ili mfanyakazi akiwemo wa nyumbani aweze kujua haki na wajibu wake katika kazi hizo”alisema Rusimbi.
Na kufafanua kuwa elimu hiyo itampa mwongozo kutambua kazi za nyumbani anazopaswa kufanya na sizopaswa kufanya.
Alieleza kuwa haki mojawapo ambayo mfanyakazi wa ndani anapaswa kuidai ni kutambulika katika chama cha wafanyakazi nchini.
Wanaharakati hao walieleza kuwa wasichana wanaofanya kazi za ndani wanaishi katika mazingira magumu na hii ni kutokana na kunyimwa fursa za kushiriki katika mijadala,kupata elimu na kufanya maamuzi.
Naye Ruth meena akizungumza katika warsha alisema kuwa ili kuondoa tatizo hilo basi sera za elimu ziboreshwea ili kuwawezesha wafanyakazi wa ndani kufahamu haki zao za ajira na kujipatia maisha endelevu.
Lakini pia alitoa wito kama mtoto wa kike amefeli mtihani wa shule ya msingi si vizuri akiozeshwa au kulazimishwa kufanya kazi za ndani badala yake apelekwe shule za ufundi stadi ili baadae aweze kujikomboa kiuchumi.
Andrew Njau kutoka Kilimanjaro, wilaya ya Hai alisema elimu endelevu kwa vijana ni suluhisho pekee la kupambana na tatizo la ajira na umaskini nchini hivyo basi serikali inatakiwa kuwajibika kuanzia ngazi za chini kuhakikisha utekeleaji wa sera hizo unatiliwa mkazo.
Kwa upande wake Veronica Ngweya ,kutoka Msumbiji alisema ili kutatua tatizo la ajira kwa wasichana wa ndani serikali yao imeanzisha kampeni maalum ya kuwafikia na kukusanya maoni ili kutambua matatizo wanayaokumbana nayo na kisha kuwapatia elimu.
“Tunawafundisha sera zitakazowajengea uwezo wa kujitambua na kuzipigania hali zao pale wanapoona zimekiukwa”alisema Ngwenya.
mwisho
Saturday, September 17, 2011
WADAU MBALIMBALI NCHINI WAENDELEA KUTUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA FAMILIA YA MAREHEMU MOHAMED MNYACHI ALIYEKUWA MWENYEKITI WA CHAMA CHA TANZANIA LABOUR PARTY(TLP) WILAYANI TUNDURU
Marehemu Mohamed Mnyachi enzi za uhai wake(Picha kwa hisani ya Familia yake)
Na Agustino Chindiye,Tunduru
Mtandao huu unatoa pole kwa Familia ya Marehemu Mnyachi na inaungana na watanzania wote katika majonzi hayo;Tunaamini kuwa Marehemu Mnyachi ameacha pengo kubwa ambalo halitazibika lakini mchango wake umeonekana dhahili katika kuchangia harakati za ukombozi wa Taifa hili kutoka nikononi mwa Mafisadi na wabadhilifu nchini
Marehemu Mnyachi ametangulia mbele za haki nasi tunamfuata lakini aliweza kutimiza wajibu wake kikamilifu enzi za uhai wake,uliobaki ni wetu,wakati tunaendelea kumkumbuka tutafakari kwa umakini fikra zake ili ziweze kutusaidia katika ujenzi wa pamoja wa taifa tunalolihitaji
Bwana alitoa na Bwana ametwaa,Jina lake lihimidiwe
Na Agustino Chindiye,Tunduru
Mtandao huu unatoa pole kwa Familia ya Marehemu Mnyachi na inaungana na watanzania wote katika majonzi hayo;Tunaamini kuwa Marehemu Mnyachi ameacha pengo kubwa ambalo halitazibika lakini mchango wake umeonekana dhahili katika kuchangia harakati za ukombozi wa Taifa hili kutoka nikononi mwa Mafisadi na wabadhilifu nchini
Marehemu Mnyachi ametangulia mbele za haki nasi tunamfuata lakini aliweza kutimiza wajibu wake kikamilifu enzi za uhai wake,uliobaki ni wetu,wakati tunaendelea kumkumbuka tutafakari kwa umakini fikra zake ili ziweze kutusaidia katika ujenzi wa pamoja wa taifa tunalolihitaji
Bwana alitoa na Bwana ametwaa,Jina lake lihimidiwe
MAHAFARI YA KIDATO CHA NNE SHULE ZA WILAYANI TUNDURU YATUMIKA KUKUSANYA FEDHA YA KUBORESHA MIUNDOMBINU KATIKA SHULE ZILIZOPO MJINI HUMO
Na Steven Augustino,Tunduru
MAHAFARI ya kuwaaga wanafunzi wanaomaliza kidato cha Nne katika Shule za Sekondari za Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma yametumika kufanya harambee za kuchangisha fedha kutoka kwa wazazi na walezi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hizo ili ziweze kusaidia utengenezaji wa miundombinu mbalimbali .
Hali hiyo imetokana na Shule nyingi za Sekondari katika Wilaya hiyo kukabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa mbalimbali pamoja na kutokuwepo kwa miundombinu ya maji, uchakavu wa vyumba vya madarasa pamoja na upungufu wa thamani yakiwemo madawati, meza na viti vya kukalia wanafunzi.
Akizungumzia hali hiyo katika mahafari yaliyofanyika katika Shule za Sekondari za Masonya na Mataka afisa elimu wa Shule za Sekondari wa Wilaya ya Tunduru Mwl. Ally Mtamila alisema kuwa mpango huo umebuniwa kufuatia tabia za ukaidi na ugumu wa kuchangia maendeleo kupitia michango ambayo imekuwa ikiombwa na Shule kutoka kwa wazazi na walezi hao.
Alisema baada ya kupatikana kwa fedha hizo zitasaidia kuanzia kutatua matatizo yanayozikabiri yakiwemo ya kujenga, kufanya ukarabati au kufanya malipo ya kuanzia kutengenezea vitanda kwa shule za Hostel au kununulia mbao ambazo zitatumika kutengenezea meza na madawati zikiwa ni juhudi za kupunguza adha mbali mbali zinazo ikabili idara hiyo wakati huohuo pia idara hiyo ikijitahidi kuomba uwezeshwaji kutoka halmashauri ya Wilaya hiyo.
Akizungumzia michango ya Shilingi 456,440 iliyopatikana kupitia harambe hiyo iliyofanyika katika Shule za Sekondari zilizopo mjini Tunduru ambazo ni Frenkweston, Mataka na Masonya wakati wa mahafari hayo, Mtamila alisema kuwa huo ni mwanzo mzuri na kwamba endapo utamaduni huo utaendelezwa kuna uwezekano wa Wilaya hiyo kupiga hatua kubwa za kimaendeleo katika nyanja hiyo ya elemu.
Aidha Mwl. Mtamila aliendelea kueleza kuwa idara yake yenye shule 19 inakabiriwa na upungufu wa walimu 130 kati ya mahitaji ya walimu 289 wengi wao wakiwa ni walimu wa masomo ya Sayansi hali inayotishia wanafunzi hao kufanya vibaya katika mitihani ya masomo hayo ambapo jumla ya wanafunzi 1200 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya sekondari mwaka huu.
Akiongea kwa nyakati tofauti wakati wa kufunga mahafari hayo pamoja na mambo mengine Mwl. Ally Mtamila aliwakumbusha wazazi na walezi wa wanafunzi waliomaliza darasa la saba kufanya maandalizi ili watoto wote watakao chaguliwa wajiunge kwa wakati na kuanza masomo ya sekondari.
Kuhusu wahitimu wa kidato cha Nne Mtamila aliwataka kufanya maandalizi mazuri ili waweze kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya taifa ili waweze kuendelea na masoma ya juu na kwamba wasikubali kudanganyika na maisha ya uraiani ambayo mwisho wake unaweza kufupisha maisha yao.
Awali wakisoma risala katika shule hizo kwa niaba ya wanafunzi wanaoagwa,Omari Jeuri wa Masonya Sekondari na Ayubu Adhuman wa Mataka sekondari walisema kuwa kukosekana kwa huduma ya maji katika shule zao kunatishia kulipuka kwa homa za matumbo ukiwemo ugunjwa wa kipindupindu.
Wakizungumzia madhara ya ukosefu wa Miundombinu ukosefu wa Walimu wa masomo ya sayansi, meza na viti vinavyo zikabili shule zao wakuu wa shule za Masonya Mwl. Mohamedi Ngaunje na Mkuu wa Shule ya sekondari ya Mataka Mwl. Johnes Liombo walidai kuwa endapo matatizo hayo yataachiliwa yaendelee kuna hatari ya idadi kubwa ya wanafunzi kuendelea kufanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya taifa na kuiweka Wilaya yao katika alama mbaya kila mwaka.
Mwisho.
MSAMA PROMOTIONS KUGAWA MAMILIONI KWA WALEMAVU NCHINI
NA MWANDISHI WETU
MKURUGENZI wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama amesema kuwa baada ya kupata mafanikio kwenye Tamasha la Pasaka,anatarajia kutoa baiskeli 50 za walemavu zenye thamani ya Sh. milioni 30.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Msama alisema kuwa fedha hizo alizoamua kuzielekeza kwa walemavu, zimetokana na mauzo mazuri ya DVD na VCD za tamasha la Pasaka lililofanyika mwaka huu, ambalo pia lilihudhuriwa na rais Jakaya Kikwete.
Alisema kuwa ameamua kufanya hivyo kutokana na kuguswa na matatizo ya watanzania wenzake hasa walemavu ambao wamekuwa wakitaabika kutafuta ridhiki, kutokana na kushindwa kutembea.
“Nimeona kuna haja ya kuwajali walemavu,nilichoamua ni kuwa ni vema hiki kidogo nilichokipata nimeona ni vema kama nitagawana nao,”alisema Msama.
Alisema kuwa tayari ameshaanza kazi ya kununua baiskeli hizo, ambazo zitakuwa ni za kisasa.
Baiskeli hizo atazigawa kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara,Songea na Tabora, ambapo Tabora na Songea kila mkoa mmoja utapata baiskeli 10 huku Lindi na Mtwara kila mmoja utapata baiskeli 15.
Kwa upande mwingine aliongeza kuwa utaratibu huo utaendelea kila mwaka, kwani anaamini wapo watanzania wenye matatizo ambayo yanahitaji kusaidiwa na anaona kwa upande wake analojukumu la kuwasaidia.
Mwisho..
DIWANI WA CHADEMA AWARUSHIA KOMBORA NZITO WABUNGE WA MKOA WA RUVUMA
Na Gideon Mwakanosya,Songea CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) Mkoani Ruvuma kimewashushia shutuma nzito Wabunge wa Majimbo mbalimbali Mkoani Ruvuma,pamoja na wa Viti Maalumu kuwa wamekuwa ni mzigo kwa wananchi waliowachagua kwani wamekuwa wakishindwa kuwakilisha matatizo yaliyoko katika majimbo yao kikamilifu. Akiwahutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara kwenye Kata mpya ya Mjimwema kwenye kiwanja cha eneo la Shule ya Msingi Samora Mwenyekiti wa chama hicho Mkoani Ruvuma Joseph Fuime alisema kuwa wabunge wa Mkoani wa Ruvuma wanapokwenda kuhudhuria vikao vya bunge wanashindwa kabisa kuwakilisha matatizo yaliyoko kwenye Manispaa ya Songea ambayo kwa muda mrefu kwa nyakati za usiku kunakuwa ni giza totoro lakini Mbunge wa Jimbo hilo amekaa kimya. Fuime ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa CCM katika Manispaa ya Songea ameeleza kuwa wabunge wa majimbo yaliyoko Mkoani Ruvuma inaonyesha wazi kuwa wanapokwenda kwenye vikao vya bunge wanakimbilia posho na sio kwenda kama wawakilishi bungeni kama wanavyofanya wabunge wengine toka majimbo ya Mikoa mbalimbali. “Wananchi niwaambieni Songea kumekuwa na matatizo mengi yakiwemo ya vocha za pembejeo zilizo chakachuliwa na wakubwa pamoja na tatizo Kubwa la kutopatikana umeme kwa muda mrefu katika mji wa Songea lakini tangu kikao cha bajeti ya bunge kilivyoanza mpaka kimeisha Mbunge wa jimbo hilo Dkt Emmanuel Nchimbi amekaa kimya kwa kisingizio cha kudai yeye ni Waziri” alisema Fuime. Vilevile amewataadharisha Watanzania wakiwemo wananchi wa Moka wa Ruvuma kuwaogopa viongozi wachache wa Serikali ya Ccm ambao wamekuwa ni mafisadi wakubwa na wamegeuza Watanzania kuwa ni sehemu la shamba la bibi ambalo halina mwenyewe. Amesema kuwa viongozi hao wamekuwa wakiuchezea uchumi wa nchi bila uoga na hakuna hatua zinazochukuliwa juu yao zaidi kumekuwepo na danganya toto kwa watanzania kuwa Serikali ya Ccm imeamua kupambana na mafisadi wakati mafisadi wenyewe wanaendelea kucheza kwenye shamba la bibi bila uoga. Kwa upande wake Katibu wa Chadema jimbo la Songea Masumbuko Paulo ameeleza kuwa kwa kitendo alichokifanya Mbunge wa Jimbo la Mbinga Kapteni John Komba cha kuamua kumsaidia Mbunge wa Songea Mjini Dkt Nchimbi kumfikishia bungeni tatizo Kubwa la miundo mbinu mibovu katika Kituo kikuu cha mabasi Songea,kinastahili pongezi kwani hali halisi ya miundo mbinu ya Kituo hicho cha Mabasi ni mbaya lakini mwakilishi wa wakazi wa Songea mjini bungeni kwa kipindi chote cha bunge la bajeti alishindwa kabisa kuliweka wazi ili Serikali ijue ni namna gani kusaidia ukarabati kwenye Kituo hicho. MWISHO |
Subscribe to:
Posts (Atom)
