About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Friday, November 4, 2011

WAZAZI WAUNGANA NA WATOTO WAO KUMKATAA KAIMU WA KAIMU WA MKUU WA SHULE

Naibu wa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Phillip Mulugo

Na Augustino Chindiye,Tunduru

WAZAZI wa Wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Sekondari ya Mataka Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma wameungana na Watoto wao kumkataa kaimu Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Steven Makina aliyeombewa kukaimu nafasi hiyo baada ya kuhamishwa aliyekuwa Mkuu wa Shule hiyo Mwl Johnes Liombo.

Hayo yalijitokeza katika kikao cha dharula kati ya walimu,wazazi na viongozi wa Wilaya hiyo kilichofanyika katika viwanja vya shule hiyo  ambapo pamoja na mambo mengine wazazi hao wamekitafsiri kitendo cha kuletwa kwa kaimu Mkuu wa shule hiyo kuwa kinatokana na rushwa.

Sambamba na tukio hilo pia Baraza la wazee wa Wilaya ya Tunduru nao wametoa tamko na kuunda tume itayo onana na uongozi wa Wilaya hiyo zikiwa ni juhudi za kumtaka Mwl. Johnes Liombo arudishwe Shuleni hapo vinginevyo wataiomba Wizara ya Elimu iifutwe Shule hiyo wakidai kuwa wamechoka kuburuzwa na watu wanaojiita wazawa.

Wakiongea kwa nyakati tofauti Ally Buji, Hasan Kindamba, Akimu Mbuula na Daria Rashidi mbali na kudai kuchoshwa na tabia za viongozi wa Wilaya hiyo kupeleka Makaimu wakuu wa Shule kwa muda mrefu walisema kuwa hawapo tayari kusikia lolote juu ya mabadiliko hayo isipokuwa wao wanamtaka Mwl. Liombo arudishwe shuleni hapo.

Nao Alli Mponda , Matumla Sekula na Fadhili Makanjila katika maelezo yao wakapigilia msumali wa moto kuwa mbali na watumishi wazawa wa Wilaya hiyo kuhubiri ukabila na kutamani nafasi zote zishikwe na kabila la Wayao wenzao lakini kitendo hicho kina lengo la kuididimiza wilaya yao na kuongeza kuwa kuhamishwa kwa Mwl. Liombo ambaye siyo mzawa wa Wilaya hiyo kunaonesha kuwepo kwa ukabila katika Wilaya yao na ama kuna kitu kilichojificha nyuma yake.

Aidha wazazi na walezi hao pia walikejeli kauli iliyotolewa na kaimu Mkurugenzi wa Halmashuri hiyo Mwl Rashidi Mandoa kuwa Shule hiyo inaye Mkuu wa Shule ambaye ni Mwl Hasan Mussa aliyepo masomoni wakidai kuwa mtindo wa kuwekeana nafasi kama wanavyofanya viongozi hao unatakiwa kufanywa katika mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na si kwa nafasi kama ilivyo hiyo Serikalini.

Walisema wameamua kuungana na madai ya watoto wao kutokana na kuamini kuwa Mwl. Liombo alikuwa muadilifu na alikuwa na uchungu wa kuiinua Shule hiyo kitaaluma na wakatahadharisha kuwa endapo uongozi wa Wilaya hiyo hautachukua hatua za haraka kumrejesha Mwalimu huyo kuna hatari ya kutokea kwa maafa makubwa katika shule hiyo.

Awali akisoma taarifa ya mahudhurio ya wanafunzi hao tangu mgomo huo uanze kaimu wa kaimu  mkuu wa Shule hiyo Mwl. Oden Masengo alidai kuwa tangu utokee mgomo huo mahudhurio ya wanafunzi wanaosoma katika Shule hiyo yamepungua na kufikia wanafunzi 170 tu kati ya wanafunzi 570 wanaosoma shuleni hapo hali inayotishia kushuka kwa taaluma kutokana na walimu kutoingia madarasani.

Akijibu malalamiko hayo kupitia maelezo yaliyosheheni data za kukidhiri kwa utoro na utovu wa nidhamu wa Wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo Afiasa elimu wa Shule za Sekondari ya Wilaya hiyo Mwl. Alli Mtamila aliahidi kuyawasilisha maono yao  kwa Mkurungezni Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi.

Mwisho.     

Thursday, November 3, 2011

KOICA KUISAIDIA WILAYA YA TUNDURU MKOANI RUVUMA WALIMU WA SAYANSI

                    Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Solomon Madaha
Na, Augustino Chndiye Tunduru

JUMUIYA ya watu wa Korea (KOICA) imeahidi kutoa msaada wenye jumla ya Walimu sita (6) ili wasaidie kufundisha Masomo ya sayansi katika Shule Tano kati ya Shule 20 za Sekondari zilizopo Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Jumuiya hiyo Hwng Jin Hee katika hafla fupi ya kukabidhi Mwalimu Mmoja kati ya walimu hao iliyofanyika katika ofisi za Afisa Elimu wa Shule za Sekondari wa Wilayani humo kwa maelekezo kuwa Mwalimu huyo  Lee Hyoo Kyung ataanza mara moja kufundisha katika Shule ya Tunduru Sekondari.

Jin Hee alisema kuwa KOICA imepokea kilio cha ukosefu wa walimu wa masomo ya Sayansi kwa vitendo ambapo kwa kuanzia wamemleta mwl. Hyoo Kyung na baada ya muda mfupi ujao watawaleta walimu wengine wanne ambao wamepangwa kufundisha katika shule za Sekondari Mataka, Masonya,FrenkWeston, Nandembo na Mbesa zilizopo wilayani humo.

Alisema nia ya nchi yake ni kusaidia Tanzani Walimu wengi zaidi wa Masomo ya Sayansi ambao wameonekana kuwa na upungufu mkubwa hapa nchini na kwamba hadi sasa KOREA imekwisha leta jumla ya Walimu 100 kupitia Shirika hilo na wanaendelea kutoa huduma hiyo katika maeneo mbalimbali ya Tanzani.
 
 Akizungumzia msaada huo  Afisa elimu Shule za Sekondari wa Wilaya ya Tunduru Alli Mtamila alisema kuwa msaada huo umefika kwa wakati na kwamba idara yake inaamini kuwa Walimu hao watawasaidia wanafunzi wa Shule hizo kuwainua kitaaluma.

Mwl. Mtamila aliendelea kueleza kuwa wakati hayo yakiendelea takwimu zinaonesha kuwa idara yake inakabiliwa na upungufu wa walimu 158 kati ya walimu 289 wanaohitajika kufundisha katika Shule hizo huku takwimu hizo zikionesha kuwa walimu waliopo ni 164 tu.

TANI 7000 ZA KOROSHO KUNUNULIWA MSIMU WA 2011/2012 WILAYANI TUNDURU

Na Augustino Chindiye ,Tunduru
JUMLA  ya Tani 7000 za Korosho kutoka kwa  Wakulima wa Wilayani Tunduru zimepangwa kununuliwa na Chama kikuu cha Ushirika cha wakulima wa Wilaya hiyo (TAMCU) katika msimu wa Mwaka 2011/2012.

Hayo yamesemwa na Meneja Mkuu wa chama hicho Imani Kalembo na kuongeza kuwa ununuzi huo utaanza kufanyika Novemba 10 mwaka huu baada ya kukamirika kwa taratibu za mkopo wa Shilingi Bilioni 5.986 kutoka Benki ya CRDB.

Kalembo aliendelea kufafanua kuwa katika msimu huu ambao chama hicho kinaendelea kununua kupitia mfumo wa Stakabadhi Gharani mkulima atalipawa mkononi Shilingi 850/= kwa kila kilo atakayoiuza na baada ya Korosho hizo kuuzwa na chama hicho mkulima atapatiwa fedha zake zilizo bakia ambazo ni  Tsh.350/= na kufanya jumla ya Tsh.1200/=  ambayo ndiyo bei ya soko kwa kila kilo moja ya zao hilo katika msimu huu.

Kalembo aliendelea kueleza kuwa kufuatia hali hiyo kwa kuanzia Chama hicho kimekwisha leta Shehena ya magunia 72,300 zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 300  zenye  uwezo wa kununulia wastani wa Tani 6000. 

Alisema katika kuhakikisha kuwa mpango huo unafanikiwa na kuhakikisha kuwa korosho zote zinauzwa ndani ya Wilaya hiyo na kuiwezesha halmashauri yao kukusanya Ushuru wake TAMCU imeandaa mitego na mikakati mbalimbali ya kuwanasa walanguzi ambao hununua Korosho hizo kwa kutumia vipimo visivyo kuwa halali maalufu kwa jina la Kangomba.

Meneja huyo alibainisha baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuunda vikosi kazi vinavyo shirikiana na viongozi na waandishi wa Vyama vya Msingi (AMCOs LTD) pamoja na kupeleka fedha na kuanza kununulia Korosho zilizopo katika vyama vya msingi vya Namitili na Mtetesi mpakani mwa Wilaya za Tunduru Mkoani Ruvuma na Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara zikiwa ni mbinu za kuwadhibiti walanguzi hao na kwamba atakaye kwepa katika maeneo hayo na kukamatwa wakati wa mauzo ya Korosho hizo atanyang`anywa korosho zote bila malipo.

Nae Mwenyekiti wa Chama hicho Wilaya ya Tunduru Mahamudu Katomondo akizungumzia ucheleweshwaji wa zoezi la kuanza kununua Korosho hizo kutoka kwa wakulima ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja toka Bodi ya Korosho Tanzania itangaze kufunguliwa kwa msimu kuanzia Oktoba 1 mwaka huu alisema kuwa hali hiyo ilitokana na kuchelewa kuiva kwa Korosho za wakulima wa Wilaya hiyo.
Mwisho

Wednesday, November 2, 2011

KIONGOZI WA CHAMA AKIFUATILIA HABARI MBALIMBALI KWENYE KIJIWE CHA KUUZIA MAGAZETI SONGEA

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea Mjini Alfonce Siwale akiperuzi magazeti mbalimbali hivi karibuni mjini hapa wakati huu muhimu wa kuvuana magamba ndani ya chama hicho

ABIRIA 19 WANUSURIKA KUFA BAADA YA GARI LAO KUACHA NJIA NA KUPINDUKA

Na Gideon Mwakanosya ,Songea.

WATU 19 wamenusurika kufa baada ya basi dogo maarufu kwa jina la daladala walilokuwa wamepanda kuacha njia na kupinduka katika mteremko uliopo katika barabara ya Bombambili katika Manispaa ya Songea na kusababisha watu watatu kati yao kujeruhiwa vibaya.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma  Naftan Mantamba alisema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa 11 jioni huko katika eneo la mteremko wa Bombambili .

Alisema kuwa gari hilo lenye namba za usajiri T301 AQD aina ya Nissan Haice ambayo ilikuwa inaendeshwa na Frenk Honde iliacha njia na kupinduka na baada ya tukio hilo dereva alikimbia.

Mantamba alisema kuwa baada ya gari hilo kupinduka abiria  19 wamejeruhiwa lakini kati yao abiria 3 wamejeruhiwa vibaya sana na hali zao ni mbaya kwa sasa wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa  kwa matibabu na wengine walitibiwa na kuruhusiwa kurudi majumbani mwao.

Amewataja majeruhi ambao hali zao ni mbaya kuwa ni Sakila Ramji(22) Abdul Mohamed (34) na Emma Komba(30) wote wakazi wa Songea mjini.

Chanzo cha ajari inadaiwa kuwa gari iliaribika likiwa kwenye mwendo mkali na kusababisha dereva kushindwa kumudu usukani kisha likaacha njia na kupinduka.

Kwa upoande wake Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Serikali ya Mkoa Songea Dkt. Benedkto Ngaiza amethibitisha kupokea majeruhi wa ajari hiyo ambapo alieleza kuwa walioletwa walikuwa 19 lakini ambao hali zao ni mbaya wapo watatu na wamelazwa kwenye wodi ya majeruhi.

MWISHO

WATU 26 WAMENUSURIKA KUFA BAADA YA GARI YAO KUGONGA LORI BOVU

Na Gideon Mwakanosya,Songea
WATU 26 wamenusurika kufa baada ya basi dogo waliokuwa wakisafilia kutoka Songea Mjini kwenda Chipole kuligonga loli lililokuwa limeegeshwa kandokando ya barabara kwenye kona karibu na Daraja la mto Mlale ambalo lilikuwa bovu linasubiri kutengenezwa.
Kaimu kamanda Polisi Mkoa wa Ruvuma Naftari Mantamba amesema kuwa tukio hilo limetokea oktoba 31 mwaka huu majira ya saa 10:45 jioni huko kwenye eneo la daraja mto mlale uliopo katika kijiji cha Msanga Wilaya ya Songea vijijini
Mantamba amefafanua zaidi kuwa basi hilo dogo linalofahamika kwa jina la Tumaini ambalo linamilikiwa na kanisa Katoliki Jimbo kuu la Songea , Parokia ya Chipole lilikuwa linatoka Songea Mjini kwenda Chipole huku likiwa limebeba abilia 26 akiwemo Dereva wa gari hilo pamoja na tingo wake.
Ameeleza kuwa basi hilo dogo ambalo lilikuwa linaendeshwa na Christofa Mapunda (42), iliigonga lori lenye namba za usajili T 770 AYL aina ya skania ambalo lilikuwa limeegeshwa kandokando ya barabara bila kuweka alama ya aina yeyote ya kuashilia kuwa mbele kuna gari bovu.
Amebainisha zaidi kuwa basi hilo dogo lenye namba za usajili T 182 ANV aina ya Isuzu baada ya kuligonga loli imesababisha watu wa 5 wakiwemo dereva na tingo wake kujeruhiwa vibaya na kwamba kwasasa majeruhi wamekimbizwa katika hospitali ya Peramiho kwa matibabu zaidi na abilia wengine wamepata majeraha madogo madogo na kwamba wamepata huduma ya kwanza katika zahanati ya Misheni katoliki parokia Chipole na kuruhusiwa kurudi majumbani kwao.
Amewataja majeruhi walio pelekwa Peramiho ambao hali za mbaya kuwa ni dereva wa gali hilo Christofa mapunda (42) mkazi wa Songea Mjini, utingo wa basi hilo Englibeti Mbepera (26) mkazi wa Mbinga Mjini Sista Hapiñes Kihwili na Sista Leliana Muhanje miaka (25) wote wanatoka Shirika la chipole pamoja na mwalimu Velinaundi Kawonga (48) wa Shule ya Msingi chipole
Amesema kuwa gali hilo ambalo lilikuwa na abilia 26 ambapo kati yao walio jeruhiwa vibaya ni wale waliokuwa wamekaa kwenye viti vya mbele na chanzo cha ajali hiyo ni kuwa lori likuwa limegeshwa kandokando ya  barabara karibu na daraja bila kuweka alama ya aina yeyote ambayo ingemwonyesha dereva wa basi dogo kuwa mbele kuna gari bovu limeengeshwa kandokando ya babara na kusababisha kuligonga.

Tuesday, November 1, 2011

AUAWA KWA MTWANGIO WA NAFAKA AKICHEZA MUZIKI UKUMBINI

                    Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda
Na Gideon Mwakanosya,Songea
MKAZI mmoja wa Kijiji cha Ruanda kilichopo katika Wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma Afred Milinga (27) amekufa papo hapo baada ya kupigwa kichwani na mchi wa kutwangia nafaka na Festo Mahundi (21) wakati wakiwa kwenye ukumbi wa starehe wakicheza disko.

Akizungumza na Mwandishi wa habari wa mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ Gideon Mwakanosya jana ofisini kwake Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma  Naftan Mantamba alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi usiku majira ya saa 2.30 huko kwenye ukumbi wa starehe kijijini hapo.

Alisema kuwa inadaiwa kuwa kabla ya tukio hilo Milinga aliondoka nyumbani kwake na alielekea kwenye kilabu cha pombe za kienyeji ambako baadae alikwenda kwenye ukumbi wa starehe na alifanikiwa kuingia ukumbini humo ambamo alimkuta Mahundi.

Alieleza zaidi kuwa wakiwa kwenye ukumbi huo walianza kuzozana kati ya milinga na Mahundi ambako Mahundi baadae alitoka nje ya ukumbi huo hadi kwenye nyumba ya jirani ambako alichukuwa mchi wa kutwangia nafaka kisha aliingia nao ukumbini na kumpiganao kichwani Milinga na kumsababishia kifo papo hapo.

Mantamba alisema kuwa baada ya kutokea kwa tukio hilo Mahundi alikimbia na kutokomea kusikojulikana lakini baada ya muda Polisi walipopata taarifa ya tukio hilo walifanikiwa kumkamata Mahundi akijiandaa kutaka kukimbia kuelekea kijiji cha Lituhi.

Hata hivyo Mantamba alieleza kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliotokea kati ya Milinga na Mahundi uliotokea kwenye ukumbi wa starehe ambako kulikuwa na disko na kwamba mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani mara tu upelelezi utakapo kamilika.

WANAFUNZI SEKONDARI WAANDAMA KUSHINIKIZA KUREJESHWA KWA MKUU WAO WA SHULE

                      Afisa Elimu Mkoa wa Ruvuma Paulina Mkonongo

Na Steven Chindiye,Tunduru
ZAIDI ya Wanafunzi 500 wa Shule ya Sekondari ya Kutwa Mataka wametishia kutoingia madarasani hadi uongozi wa Halmasahuri ya Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma watakapofanya mabadiliko ya kumrejesha Shuleni hapo aliyekuwa Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Johnes Liombo.

Msimamo huo umetolewa na wanafunzi hao wakati wakiongea na uongozi wa Halmashauri hiyo baada ya uongozi huo  kupokea maandamano ya  amani yaliyofanywa na wanafunzi hao kwa nia ya kupinga uhamisho wa mwalimu huyo.

Sambamba na msimamo huo wanafunzi hao, wakiwemo wanafunzi  wa kidato cha Pili wanaotarajia kufanya Mtihani wa Taifa hivi karibuni walidai kuwa endapo mgogoro huo hautapatiwa ufumbuzi mapema nao hawataingia katika chumba cha mtihani huo.

Akisoma taaria ya wanafunzi hao kaka Mkuu wa shule hiyo Rajab Said alisema kuwa wanafunzi hao wamechukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa uhamisho wa Mwalimu Liombo ambaye amekaa miezi mitatu katika Shule yao ni wa uonevu na kwamba kitendo hicho hakiitakii mema Shule yao.

Alisema mwl. Liombo  ni mwalimu wa msaada kutokana na tabia yake ya kujituma katika ufundishaji na kwamba wanafunzi  wote wanaamini kuwa endapo angeendelea kubakia katika shule hiyo wanafunzi wote wangepiga hatua kitaaluma.

Akijibu kero hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mwl. Rashid Mandoa ambaye alikuwa akisaidiwa na baadhi ya wakuu wa Idara mbalimbali na kuwaomba wanafunzi hao warudi shuleni kwa ajili ya kuendelea na masomo na kuwataka waliwataka wanafunzi hao kutokubali kutumiwa ama kufanya maandamano kwa maslahi ya watu.
“kweli nimeamini kuwa wanafunzi wa Mataka Sekondari hawana nidhamu” alisema Mwl. Mandoa na kuongeza  kuwa endapo wanafunzi hao wangekuwa na nidhamu walipaswa kufuata taratibu za kuonana na uongozi kwa kufuata taratibu zinazotakiwa na sio kufanya maandamano kama walivyo fanya.

Aidha Mwl.Mandoa aliwahakikishia wanafunzi hao kuwa uhamisho wa mwalimu Liyombo ni wa kawaida kama wanavyohamishwa watumishi wengine wa Halmashauri hiyo

Nae Afisa Elimu wa Shule za Sekondari wa Wilaya hiyo Mwl. Alli Mtamila katika maelezo yake pamoja na mambo mengine aliwataka wanafunzi hao kurejea Shuleni kwa madai kuwa idara yake inafuatilia tatizo hilo na kulitafutia ufumbuzi ombi ambalo lilikataliwa na wanafunzi hao na kuwafanya watawanyike kurejea majumbani mwao.  

Akiongea kwa niaba ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo Fadhili Makanjila alisema kuwa kitendo cha uhamisho huo kimewakatisha tamaa wazazi na wanafunzi kwa katika kipindi cha Mwalimu Liombo kulikuwa na mikakati mizuli ya kuiinua kitaaluma shule hiyo.

 Makanjila aliitaja miongoni mwa mikakati hiyo kuwa ni pamoja na Mkuu huyo kuwa na mipango shirikishi tofauti na walimu wengine na akatolea mfano mpango wa kuwaweka wanafunzi wa kidato cha pili katika KAMBI ambalo wanafunzi hao walikuwa wakipatiwa masomo ya ziada nyakati za usiku ikiwa ni mikakati ya kuwa andaa  na  mithani ijayo

WANACHAMA 130 WA NEW MUUNGANO SACCOS WAPATIWA ELIMU YA UJASILIAMALI NA USHIRIKA

Na Gideon Mwakanosya,Songea
CHAMA cha akiba na Mikopo cha New  Muungano SACCOS kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kimetoa mafunzo kwa wanachama wake 130 ya elimu ya ujasiliamali na elimu ya ushirika ili kuwasaidia wajasiliamali hao kufanya kazi kwa umahili zaidi.
Akifungua mafunzo hayo ya siku mbili Katibu wa New Muungano SACCOS  Biatha Komba kwenye ukumbi wa shule ya msingi Mfaranyaki alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwasaidia wanachama wake kujua elimu ya ushirika na ujasiliamali ili wanapokopa mikopo yao waitumie kwa matumizi sahihi kama walivyoomba.

Komba alisema kuwa pia wananchama wake ni lazima wajue sheria ,kanuni na misingi ya ushirika ili wanapofanya kazi zao za kila siku wasipatwe na usumbufu wa aina yeyote katika mitaji,na masoko kwa biashara wanazofanya.

Aliainisha changamoto ambazo zinaikabili chama hicho kuwa ni pamoja na mfumuko mkubwa wa taasisi zisizo rasmi za kifedha ambazo zimekuwa zikifanya kazi ya kukopesha wafanyabiashara na wafanyakazi wakiwemo walimu fedha, vitendea kazi vya kisasa kama kompyuta,fotokopi mashine pamoja na usafiri kwaajiri ya kuwafuata wanachama na kupeleka fedha benki.

Kwa upande wake Afisa Tawala wa Tarafa ya Songea Magharibi Blanka Luambano ambaye ndio alikuwa mgeni rasmi aliupongeza mradi wa SELF  kwa kuifadhiri SACCOS hiyo ambayo imeonekana kuwa ni msaada mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Songea.

Alisema kuwa New Muungano SACCOS ni miongoni mwa taasisi chache za fedha ambazo zimejikita zaidi katika kusaidia kuondoa umasikini kwa wafanyabiashara wadogo na kwamba kwa muda wote imekuwa ikiwahimiza wanachama wake kukopa fedha kwaajiri ya kukuza biashara zao wanazozifanya kila siku.

Semina hiyo ya siku mbili ambayo washiriki wake ni kutoka kata 13 zilizopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambayo imefadhiriwa mradi wa kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo (SELF) ambao uko chini ya Wizara ya fedha inatarajiwa kuwa na mada za uongozi wa utawala bora,ujasiliamali, sheria na kanuni za vyama vya ushirika

DC MJENGWA ACHARUKA UCHOMAJI MOTO OVYO WILAYANI MBINGA

                     Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Kanali Edmund Mjengwa
Na Cresencia Kapinga,Mbinga
SERIKALI wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma imeagiza kuwachukulia hatua kali za kisheria viongozi wa kijiji na kata wakiwamo Madiwani pamoja na makatibu tarafa ,ambao maeneo yao yatakumbwa na uchomwaji moto bila wahusika kuchukuliwa hatua yoyote.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Kanali Mstaafu Edmund Mjengwa kwenye kikao cha baraza la Madiwani  kilichofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa  jumba la maendeleo uliopo wilayani humo.

Kanali Mjengwa alisema kuwa ipo tabia ya viongozi kama vile Watendaji wa Vijiji na kata pamoja na Madiwani wao ambao wamekuwa wakiona matukio ya uchomaji moto kwenye maeneo yao lakini hakuna hatua wanazozichukuwa.

"Naagiza ya kwamba kuanzia sasa tukio la moto likitokea kijijini kwako na zisipochukuliwa hatua za kuuzima,viongozi wa eneo husika watakuwa wa kwanza kuchukuliwa hatua za kisheria vinginevyo muhusika afikishwe katika vyombo vya sheria ili sheria ichukuwe mkondo wake" alisema Kanali Mjengwa.

Aidha amewaagiza Madiwani wa Wilaya hiyo kuwaelimisha Wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwani imeonekana wananchi wengi hawajui umuhimu wake hivyo kufanya vitendo vya ukataji wa miti na uchomaji moto kuwa ni vya kawaida na ni sehemu ya maisha yao ya kila siku pasipo kujua athari zake.

Pia amewaagiza makatibu tarafa wote wa wilaya hiyo kuwachukulia hatua watu wote ambao wamejenga kwenye vyanzo vya maji ili kuvinusuru vyanzo hivyo kukauka na kusababisha wananchi waingie kwenye janga la ukosefu wa maji kutokana na watu kufanya makazi kwenye vyanzo hivyo.

 Alisema kiutaalamu maeneo ya vyanzo vya maji hayapaswi kuwekwa makazi ya watu kwani yanaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo magonjwa ya mlipuko na kukauka kwa vyanzo hivyo kutokana na baadhi ya watu wengine kulima kwenye vyanzo hivyo bila kujari hathari ambayo inaweza kutokea hapo baadae.

Friday, October 28, 2011

MHANDISI STELLA MANYANYA AKAMILISHA ZIARA WILAYA YA TUNDURU NA SONGEA VIJIJINI KWA CHEREKOCHEREKO

 Mhandisi Stella Manyanya(Mb) na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akisaini kitabu cha wageni cha chama na Serikali Wilayani Tunduru alipowasili Wilayani humo kwa ziara ya siku moja



 Mhandisi Stella Manyanya(Mb) na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akisaini kitabu cha wageni cha Chama cha CCM  Wilaya ya Songea Vijijini alipotembelea ofisi ya chama hicho kabla ya kuanza ziara ya siku moja wilayani humo
 Viongozi wa CCM Wilaya ya Songea Vijijini wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mhandisi Stella Manyanya(Mb) na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa

 Wananchi wa kata ya Mtyangimbole ndivyo walivyokuwa wanampokea Mhandisi Stella Manyanya(Mb) na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alipofanya ziara leo Songea Vijijini




Viongozi wa CCM Wilaya ya Songea Vijijini wakiagana na Mhandisi Stella Manyanya(Mb) na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa katika ofisi za BetterLife Tanzania tawi la Ruvuma

SHAMLA SHAMLA YA MAPOKEZI YA WILAYA YA NAMTUMBO ILIVYOKUWA KUWA WAKATI WA ZIARA YA MBUNGE MHANDISI STELLA MANYANYA NA MKUU WA MKOA WA RUKWA

 Mhandisi Stella Manyanya(Mb) Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akicheza ngoma baada ya kupokelewa Kata ya Kitanda Wilayani Namtumbo
 Uwt Wilaya ya Namtumbo wakitoa Zawadi kwa Mgeni rasmi Mhandisi Stella Manyanya(Mb)Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alipomaliza kuhutubia wananchi wa kata ya Kitanda
 Mhandisi Stella Manyanya (Mb) Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akitoa msaada wa shilingi laki mbili na themaanini kwa vikundi vya ujasiliamali kata ya Kitanda
Diwani wa Kata ya Kitanda Vitus Ngoma akipokea jezi kwa ajili ya timu ya Kata kutoka kwa Mhandisi Stella Manyanya(Mb) Mkuu wa Mkoa wa Rukwa

AUAWA BAADA YA KUVAMIWA NA WATU WANAOHISIWA KUWA NI MAJAMBAZI LUPAPILA

Na Gideon Mwakanosya, Songea
NESTORY  Ndomba (20) Mkazi wa Mtaa wa Lupapila katika Manispaa ya Halmashauri ya Songea Mkoa wa Ruvuma amevamiwa na kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi na kumsababishia kifo papo hapo baada ya kumpiga na kitu kizito kichwani wakati akiwa anaendesha pikipiki akitokea Lizaboni kwenda Lupapila.
Akizungumza na mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com jana ofisini kwake Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Naftari Mantamba amesema kuwa tukio hilo limetokea octoba 27 mwa huu majira ya saa 2.30 usiku huko katika eneo la Mtaa wa Londoni uliopo jirani na Lizaboni.
Mantamba amebainisha zaidi kuwa Ndomba anadaiwa kuwa aliuwawa na kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi ambao wote walijifunga vitambaa vyeusi usoni huku wakiwa wameshika nondo mikononi.
Amesema kuwa majambazi hao baada ya kumkamata walianza kumpiga na kitu kizito kichwani huku wengine wakiendelea kumpekua mifukoni na baadaye walimfunga mikono yote miwili kwa nyuma kiunoni kwa kutumia kamba ya katani ndipo walipomlaza chini na kumnyang’anya pikipiki aina ya sunlug ambayo alikuwa akiiendesha akitokea Lizaboni kwenda Lupapila.
Ameeleza zaidi kuwa Ndomba baada ya kufungwa kamba hiyo majambazi hao walitokomea kusikojulikana na pikipiki hiyo yenye namba za usajili T 846 AYS ambayo thamani yake ni shilingi milioni 1.8 .
Hata hivyo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Mantamba amesema kuwa mpaka sasa majambazi hayo hayajakamatwa na jeshi la Polisi Mkoani humo linaendelea kuyasaka ili yafikishwe mikononi mwa vyombo vya dola.
Wakati huo huo mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Thadei Luambano (45) Mkazi wa Mtaa wa Madizini Kata ya Lizaboni katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea amefariki dunia baada ya kukosa hewa wakati akichimba kisima cha maji huko katika eneo la Jeshi Kambi ya Chabruma mjini Songea.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Naftari Mantamba amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo amedai kuwa lilitokea octoba 27 mwaka huu majira ya saa 10 jioni huko katika kambi ya JWTZ Chabruma ambako Afisa mteule namba 1 wa jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) Augustino Rashid ndiye aliyetoa taarifa ya tukio hilo katika kituo kikuu cha Polisi cha Songea na Polisi bado inaendelea na uchunguzi juu ya  tukio hilo

Thursday, October 27, 2011

WANANCHI WAENDELEA KUMPOKEA KWA SHANGWE MBUNGE STELLA MANYANYA NA MKUU WA MKOA WA RUKWA KATIKA ZIARA YAKE YA KIKAZI MKOANI RUVUMA

Mbunge Mhandisi Sella Manyanya wa kwanza kulia akipiga ngoma ya Beta baada ya kufurahia mapokezi mazuri katika ziara yake,wa kwanza kushoto ni Katibu wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Frank Maten akishuhudia mapokezi hayo

Mhandisi Stella Manyanya ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Ruvuma akimpatia Katibu wa UWT Wilaya ya Songea Mjini shillingi laki mbili kwa ajili ya mahitaji madogo madogo ya ofisi ya UWT Wilaya ya Songea Mjini,baada ya kupokea ripoti ya utekelezaji kwa kipindi cha mwaka 2011, katikati ni Katibu wa UWT Mkoa wa Ruvuma Mariam Yusuph

Viongozi wa Chama na Serikali wakifanya maombi kwenye kabuli la Nduna Songea Mbano

Mjukuu wa Nduna Songea Mbano,Aidan Mbano akizungumza na Wazee Mashujaa 66 waliozikwa kwenye kabuli la pamoja ikiwa ni dua maalum kwa Mbunge na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea Mhandisi Stella Manyanya alipotembelea Makumbusho hayo ili kupata baraka za Wazee hao ikiwa ni desturi yake kabla ya kuanza ziara zake mkoani Ruvuma

Viongozi mbalimbali wa chama na Serikali wakimkaribisha Mbunge na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya kwenye viwanja vya mkutano vya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea

Mama wa Kimasai akimpatia zawadi za kabila hilo Mbunge Mhandisi
Stella Manyanya baada ya kuwahutubia wananchi wa Songea Mjini katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji
Viongozi wa chama wa Wilaya ya Namtumbo wakimpokea Mbunge Mhandisi Stella Manyanya

MAKANISA NDUGU KUFANYA TAMASHA LA UIMBAJI MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA


                    Mhashamu Askofu Mkuu Norbert Mtega
Na Gideon Mwakanosya,Songea
WAUMINI wa Makanisa ndugu katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani  Ruvuma wanatarajia kufanya tamasha kubwa la uimbaji  la Jubilei  ya miaka 50 ya uhuru wa Taifa la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Oktoba 29 Mwaka huu ambapo mgeni rasmi kwenye tamasha hilo ni Waziri wa Habari utamaduni na michezo Dr. Emmanuel  Nchimbi.
Akizungumza na mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com  jana ofisini kwake Katibu wa umoja wa Makanisa ndugu katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mackie Mguhi amesema kuwa tamasha hilo ambalo linatarajiwa kuhuzuliwa na mamia ya waumini wa Makanisa ndugu wakiwemo Askofu Mkuu wa Kanisa katoliki jimbo kuu la Songea Norbert Mtega, Askofu wa dayosisi wa Ruvuma kanisa la Angelikana  Dr. Martenius Kapinga, Mkuu wa kanisa la kiinjili la kiliteli Tanzania (KKKT) Mchungaji Nashoni kikalawa Pamoja na mkuu wa mkoa wa Ruvuma Saidi Mwambungu 
Mguhi ameyataja Makanisa yanayeunda umoja huo ambao umeandaa tamasha kubwa ni kanisa katoliki Parokia za Songea,Mjimwema na Bombambili kanisa la kinjili la kiluteli Tanzania (KKKT) Usharika na Songea mjini na Msamala kanisa la Anglikana Songea Mjini pamoja na kanisa la Moraviani Tanzania ushirika wa Songea.
Ameeleza zaidi kuwa Tamasha hilo litafanyika siku ya jumamosi oktoba 29 mwaka huu katika uwanja wa michezo wa mpira wa miguu wa Majimaji ambalo litatanguliwa na maandamano makubwa  ya waumini wa Makanisa ndugu yatakayoanzia katika kanisa la Luthelani Songea Mjini hadi uwanja wa Majimaji.
Amesema kuwa lengo la tamasha hilo ni kuonyesha furaha kubwa kwa waumini wa Makanisa ndugu katika manispaa ya Songea kwa jubilee ya nchi ya Tanzania Kwa vitendo pili kuendelea kumshukuru mungu na kumuomba kwa upendo ,Amani na uvumilivu aliyo ijalia nchi ya Tanzania pamoja na viongozi  na wananchi kwa ujumla .
Amebainisha zaidi kuwa  katika tamasha hilo pia litaudhuliwa na wanafunzi wa chuo cha elimu ya Taifa Songea , Shule ya wasichana na Wavulana Songea na kwaya zaidi ya ishirini zimesibitisha kushiriki kwenye tamasha hili na viongozi wa makanisa hayo wanatarajiwa kuongoza ibada ya maalumu ya kuiombea amani kwa mwenyezi mungu kwani  Tanzania toka ipate uhuru hawajawai kupata misuko suko ya aina yoyote tofauti  na nchi zingine zikiwemo baadhi ya nchi zilizo pakana na Tanzania ambazo wananchi wake wakipata shida kutokana na vita.

Wednesday, October 26, 2011

MHANDISI MANYANYA AANZA ZIARA KWA KUPOKELEWA NA DUA MBALIMBALI KUTOKA KWA WASAIDIZI WA CHIFU WA KINGONI

Wasaidizi wa Chifu wa Kabila la Kingoni (Mjukuu wa Nduna Songea Mbano na Gama) wakitoa dua zao kwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Ruvuma na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji alipotembelea Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea kabla ya kuanza ziara yake ya siku tano mkoani Ruvuma

Wazee wa Ngoma ya Beta wakimpa Nasaha mbalimbali  Mhandisi Manyanya kwa heshima na Mila za Desturi za Kingoni walipomtembelea Ofisini kwake kabla ya kuanza ziara yake

Ndivyo mapokezi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Manyanya alipopokelewa na wakina mama wa BetterLife Tanzania mara alipowasili mjini Songea kabla ya kuanza ziara yake ya siku tano mkoani Ruvuma

MBUNGE STELLA MANYANYA AFANYA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU TANO MKOANI RUVUMA

                                                     Mhandisi Stella Manyanya
Na Mwandishi Wetu,Songea
MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Stella Martin Manyanya ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa anatarajia kuanza ziara ya siku tano mkoani Ruvuma kuwashukuru wapiga kura wanawake na wananchi kwa ujumla wao  kwa kukipa ridhaa chama cha Mapinduzi (CCM)kushika dola
Katika ziara hiyo Octoba 26 Mhandisi Manyanya atafanya mkutano wa hadhara Songea Mjini na Kijiji cha Kitanda Wilayani Namtumbo ambapo atafungua vikundi vya ujasiliamali na kuwahutubia wananchi wa eneo hilo
Octoba 27 atawasili Wilayani Tunduru na kufanya mkutano wa hadhara ambapo Octoba 28 atafanya mkutano Songea Vijijini,Octoba 29 atasalimia Halmashauri kuu ya chama cha Mapinduzi pia atafanya mkutano wa hadhara  kata ya Burma Wilayani Mbinga
Ziara hiyo itakamilika Octoba 30 kwa kufanya mkutano wa hadhara Wilayani Nyasa katika Kata ya Ngumbo na kisha kurejea Mkoani Rukwa kwa shughuli zingine za kiserikali

Tuesday, October 25, 2011

UCHAKACHUAJI WA MAPATO YATOKANAYO NA MAZAO YA MISITU MBINGA WASABABISHA HASARA

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Shaib Mnunduma
Na Gideon Mwakanosya,Mbinga
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imepata hasara ya shilingi milioni 18 kupitia idara yake ya maliasili na mazingira kutokana na uzembe uliofanywa na watumishi wachache wa idara hiyo, waliopewa dhamana ya ukusanyaji wa ushuru wa mazao ya misitu.
Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika kutoka katika halmashauri hiyo ambavyo vilizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti kwa sharti la kutotaja majina yao, vilisema kuwa hasara hiyo imetokea kufuatia vitabu vyenye risiti ambavyo hutumika kukusanyia ushuru huo vimepotea katika mazingira ya kutatanisha.
Habari zinaeleza kuwa jitihada za kutafuta vitabu hivyo vilivyopotea mpaka sasa zimegonga mwamba jambo ambalo uongozi wa wilaya ya Mbinga, ulilazimika kuchukua hatua za kuripoti kituo kikuu cha polisi kwa msaada zaidi ambapo baadhi ya watumishi wa idara ya maliasili na mazingira wilayani humo waliwekwa mahabusu kwa siku kadhaa.
Aidha pamoja na watumishi hao kuwekwa mahabusu hivi sasa wameachiliwa huru na hakuna hatua zingine walizochukuliwa huku wakiendelea na kazi zao kama kawaida kitendo ambacho kimekuwa kikisababisha kuzua maswali mengi kutoka kwa watumishi wengine wa halmashauri hiyo.
Utaratibu wa halmashauri ya wilaya hiyo katika utoaji wa vitabu hivyo unaeleza kuwa alikabidhiwa mkuu wa kitengo cha kukusanya ushuru wa mazao ya misitu Nambole   Nanyanje ambaye huwagawia watumishi wenzake wanaohusika na suala la kukusanya ushuru huo.
Mwandishi wa habari hizi alipomuuliza kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Bernard Semwaiko juu ya tuhuma hizo alikiri kuwepo kwa upotevu wa fedha na vitabu hivyo huku akisema halmashauri yake imekwisha kamilisha utatuzi wa jambo hilo.
“Ni kweli kiasi hiki cha fedha kilipotea kutokana na upotevu wa vitabu vilivyokuwa vikitumika kukusanyia ushuru wa mazao ya misitu, najua umewahi kusikia kuna baadhi ya watumishi tuliwaweka mahabusu”, alisema Semwaiko.
 Kadhalika Mwandishi alipotaka kujua undani wa tatizo hilo Semwaiko alifafanua kuwa lilibainika kufuatia wakaguzi waliokuwa wakifanya kazi ya kukagua mahesabu ya halmashauri hiyo, ndipo wakaguzi hao waligundua kuna upotevu wa fedha hizo na vitabu, yenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 18 kutoka idara ya maliasili na mazingira wilayani humo ambavyo vilitumika kukusanyia ushuru wa mazao ya misitu.

AJALI YAUA MMOJA NA KUJERUHI WATU SITA BAADA YA GARI KUACHA NJIA NA KUPINDUKA

Na, Gideon Mwakanosya SongeaMTU mmoja mkazi wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma amekufa papohapo na wengine sita wamejeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Songea mjini kwenda Namtumbo kuacha njia na kupinduka.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Naftari Mantamba amesema kuwa tukio hilo limetokea oktoba 24 mwaka huu majira ya saa 8.00 mchana katika eneo la Mletele Songea mjini.
Mantamba amemtaja aliyefariki dunia kuwa ni Sabina Similia(80) mkazi wa eneo la Faraha Store Mbinga mjini na kwamba waliojeruhiwa amewataja kuwa ni Failuna Komba(70) na Hassan Ally(40) wote wakazi wa kijiji cha Mgombasi kilichopo katika wilaya ya Namtumbo.
Amewataja majeruhi wengine kuwa ni Flora Mamzi(39) mkazi wa mtaa wa Furaha Store Mbinga mjini,Amina Komba(63) mkazi wa kata ya Lizabon Songea mjini,Mohammed Hassan(50) mkazi wa mtaa wa Ruhila Songea mjini na Omary Mtumbuka(42) mkazi wa kijiji cha Litola kilichopo wilayani Namtumbo.
Kaimu Kamanda Mantamba amefafanua kuwa basi hilo lenye namba za usajili T761 ATN aina ya Isuzu Forward ambalo lilikuwa limebeba abiria kutoka Songea mjini kuelekea Namtumbo na kwamba lilikuwa likiendeshwa na Hamis Chidumule(35) mkazi wa kata ya Ruvuma Songea mjini likiwa kwenye mwendo mkali liliacha njia na kupinduka.
Amesema kuwa majeruhiwa mpaka wamelazwa katikahospitali ya mkoa kwenye wodi za majeruhi ambapo hali zao zinaendelea vizuri  na kwamba chanzo cha ajali hiyo gari hiyo ilikuwa kwenye mwendo mkali hali iliyosababisha dereva ashindwe kumudu ukukani na hivyo kuacha njia na kupinduka.
Hata hivyo polisi mkoani hapa imefanikiwa kumkamata dereva wa gari hilo na kwamba kwa sasa uchunguzi unaendelea kufanyika ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

WANANCHI WA MPAKANI MWA MSUMBIJI NA TANZANIA WATAKA BARABARA KWA KIWANGO CHA LAMI

 Meneja wa Tanroads Mkoa wa Ruvuma Abraham Kissimbo akitoa maelekezo ya ujenzi wa daraja la Mkenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu hayupo pichani alipotembelea mpaka wa Msumbiji na Tanzania
 Daraja la Mkenda linalounganisha nchi ya Msumbiji na Tanzania
 Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu akiwa na Viongozi mbalimbali wakipita juu ya daraja la Mkenda wakielekea nchi jilani ya Msumbiji
 Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu akipata maelekezo ya ujenzi wa daraja linalounganisha nchi ya Msumbiji na Tanzania lililojengwa kivukoni Mkenda kutoka kwa Meneja wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Abraham Kissimbo
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu (katikati) akipokea maelezo ya jengo lililojengwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) kutoka kwa Meneja wa TRA mkoa wa Ruvuma Apily Mbaruku kushoto na Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Oley Sabaya kulia
Na Stephano Mango,Songea
WANANCHI wa kitongoji cha Mkenda kilichopo katika kijiji cha Nakawale kata ya Mhukuru wilaya ya Songea vijijini mkoani Ruvuma wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Miundombinu kuona umuhimu wa kuwakumbuka kwa kuwajengea barabara kwa kiwango cha lami ili waweze kusafirisha bidhaa zao yakiwemo mazao ya kilimo kiurahisi.
Ombi hilo wamelitoa jana kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu wakati alipofanya ziara ya kutembelea kitongoji hicho kilichopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ambako Serikali imefanikiwa kujenga daraja la kudumu ambalo linaunganisha na nchi hiyo jirani katika mto Ruvuma.
Mmoja wa wakazi wa kitongoji hicho Ramadhani Hussein alisema kuwa kitendo cha Serikali cha kujenga daraja la Mkenda kwenye mto Ruvuma kumepelekea kuwepo kwa maendeleo makubwa kwa wananchi wa eneo hilo kutokana na biashara zinazofanyika kati yao na wananchi wa nchi jirani ya Msumbiji.
Hussein alisema kutokana na hali hiyo ni vyema Serikali ikafikiria kujenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Songea mjini hadi Mkenda yenye urefu wa kilometa  124   hali itakayokuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa tarafa ya Mhukuru ambayo ipo mpakani.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha FRELIMO kijiji cha Congress nchini Msumbiji John Bosko ambaye alihudhuria mkutano huo wa hadhara alimwomba Mkuu wa mkoa wa Ruvuma kufanya mawasiliano na Serikali ya Msumbiji ili kuhakikisha kuwa barabara ya kutoka Songea hadi Mkenda inajengwa haraka na kwamba barabara kutoka Mkenda hadi Maputo inajengwa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Kwa upande wake Meneja wa wakala wa barabara mkoa wa Ruvuma(TANROADS) Mhandisi Abraham Kissimbo alisema kuwa Serikali imedhamira kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kwamba mpaka sasa tayari michoro imekamilika na kinachosubiriwa ni utekelezaji.
Naye Mkuu wa mkoa wa Ruvuma aliwaeleza wananchi hao kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kufanyia matengenezo barabara zote zikiwemo za mipakani ili zipitike kiurahisi na kwamba aliwahimiza wananchi kujikita kwenye kilimo ili barabara hizo zitakapokamilika waweze kusafirisha mazao yao pamoja na bidhaa zingine.
Aidha Mwambungu aliwataka wakazi wa kitongoji hicho kujitokeza kwa wingi kuchangia nguvu zao kwenye ujenzi wa kituo cha polisi hasa ikizingatiwa kitongoji hicho cha Mkenda kipo mpakani mwa nchi ambapo kwa siku za usoni unatarajia kuwa mji mdogo hali itakayopelekea pia kuwepo na vitendo vya uharifu na kwamba alichangia shilingi milioni moja kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.