About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Friday, November 18, 2011

WALIMU WA SAYANSI NA LUGHA WILAYANI NAMTUMBO NI TATIZO SUGU


    Kaimu Afisa Elimu Wilaya ya Namtumbo Lidya Herbert
Na Stephano Mango, Namtumbo

HALMASHAURI ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma ambayo ina shule 30 za Sekondari zikiwemo Shule 24 za Serikali na Shule za Binafsi  6 inakabiliwa na tatizo kubwa la upungufu wa Walimu wa masomo ya Sayansi na Lugha na kusababisha Wanafunzi wa Shule hizo kushindwa kumudu masomo ipasavyo  wakiwa  kwenye Shule hizo.

Akizungumza na Mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com jana Ofisini kwake Kaimu Afisa Elimu wa Shule za Sekondari wa Wilaya ya Namtumbo Lydia Herbert alisema kuwa Halmashauri hiyo yenye jumla ya Wanafunzi wa Sekondari 7871 wakiwemo wavulana 4671 na wasichana 3193  ina uhaba mkubwa wa walimu wa Masomo ya Sayansi na Lugha.

Herbert alisema kuwa mpaka sasa Halmashauri hiyo ina walimu 208 wa Shule za Sekondari ambao hawawezi kukidhi haja ya wanafunzi waliopo kwenye Shule za Sekondari Wilayani humo na kwamba kutokana na hali hiyo kuna upungufu wa walimu 32 wa masomo ya sayansi na lugha.

Alieleza zaidi kuwa hali ya miundo mbinu katika shule za Sekondari zilizopo katika Wilaya hiyo ilikuwa inahitajika kuwa na vyumba vya madarasa 285 lakini vyumba vya madarasa vilivyopo kwasasa ni 164 na kufanya kuwepo tatizo kubwa la vyumba vya madarasa kwenye Shule hizo.

Alibainisha zaidi kuwa katika Shule hizo za Sekondari Wilayani humo zinahitajika maabara 115 lakini maabara zilizopo ni 3 tatu ambazo zipo katika Shule mbili za binafsi na Shule moja ya Serikali na walimu wa Shule hizo wanakabiliwa na tatizo kubwa la nyumba za kuishi ambapo nyumba za walimu zinazohitajika ni 384 na nyumba zilizopo ni 84 tu ,.

Alisema katika Shule hizo za Sekondari Wilayani humo kuna changamoto kubwa zinazojitokeza mara kwa mara ambaapo ni utoro wa wanafunzi wa kike na wakiume uliokithiri na mimba za utotoni ambapo wanafunzi 22 walibainika kuwa ni wajawazito katika kipindi cha January hadi October mwaka huu.

Ameitaja mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto hizo kuwa ni kuwaelimisha wananchi wa Wilaya ya Namtumbo juu ya umuhimu wa elimu kupitia mikutano ya ndani na ya hadhara ili waweze kuelewa kuwa wazazi wa wanafunzi hao wanapaswa kuchangia ujenzi wa madarasa,madawati na kujenga nyumba z akuishi walimu.

Mikakati mingine ni kuboresha miundo mbinu ya Shule za Sekondari Wilayani humo ili kuwa na Mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia kwa kujenga nyumba za walimu,vyumba vya madarasa pamoja na maabara kwa mwaka wa fedha 2011/2012.

Kaimu Afisa Elimu huyo Herbert ameiomba Serikali kupitia Wizara za Elimu Utamaduni na Ufundi na Wizara ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (TAMISEMI ) kuona umuhimu wa kuwaletea walimu wengi zaidi wa masomo ya sayansi ambao wataweza kuziba mapengo mengi ya walimu katika Shule za Sekondari Wilayani humo

Thursday, November 17, 2011

WANANCHI WATAADHARISHWA UZAGAAJI WA NOTI BANDIA MKOANI RUVUMA

Na Gideon Mwakanosya, Songea

JESHI la polisi Mkoani Ruvuma limewataadharisha wananchi wakiwemo wakulima na wafanyabiashara kuwa makini wanapofanya shughuli zao za kila siku hasa wanapouza mazao au wanaponunua bidhaa za biashara zao kwani katika Mkoa huo noti bandia za shilingi Elfu 5000 na shilingi Elfu 10,000 zimezagaa ambapo kufuatia hali hiyo Polisi imefanikiwa kuwanasa watu wawili wakiwa na noti bandia za shilingi alfu 10 kila mmoja zenye thamani ya shilingi laki 5.

Tahadhali hiyo imetolewa jana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda wakati alipokuwa akiongea na Waandishi wa habari ofisini kwake.

Kamuhanda amewataja wanoshikiliwa na polisi kuwa ni Joseph Kilagi ( 25) na Francis Nkunji (19) wote wakazi wa jijini Dar es salaam ambao walitiwa mbaroni tangu Novemba 13 mwaka huu majira ya saa mbili usiku kwenye kituo kikuu cha mabasi cha Mjini Songea wakiwa wanateremka kwenye basi wakitokea Dar es salaam.

Amesema kuwa askari ambao walikuwa doria kwenye eneo la Kituo cha mabasi waliwakamata watuhumiwa hao wakiwa na noti bandia 50 ambazo kila noti  moja ni shilingi elfu 10 zote zikiwa na thamani ya shilingi laki 5.

Amefafanua zaidi kuwa noti hizo bandia zilizokamatwa zina namba AC.0011601 kila moja na kwamba watuhumiwa walipohojiwa na askari hao waliokuwa doria walidai kuwa wametokea Dar es salaam na wamekuja Songea kufanya biashara ya kununua mahindi.

Kamanda Kamuhanda ameeleza kuwa kwasasa hivi polisi inaendelea kufanya upelelezi kuhusiana na tukio hilo na kwamba watuhumiwa hao watafikishwa Mahakami kujibu shtaka linalowakabili mara tu upelelezi utakapokamilika.

Amewataadhalisha wafanyabiashara wa Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma kuwa wanapofanyabiashara zao kuwa waangalifu pale wanapokutana na noti za shilingi Elfu 5000 na Elfu 10,000ambazo zinadaiwa ndiyo noti bandia zimezagaa kwenye magulio,minada na maeneo mengine ya biashara za jumla na rejareja na kwamba wananchi watakaowagundua watu wenye tabia mbaya ya kusambaza noti bandia watoe taarifa katika kituo chochote cha polisi kilicho karibu.

WASHIRIKI WA MAJADILIANO YA PAMOJA KUHUSU UTAFITI MDOGO WA VYOMBO VYA HABARI RUVUMA WAMALIZA WARSHA YA SIKU MBILI NA KUAZIMIA NJIA BORA YA KUKUSANYA NA KUSAMBAZA TAARIFA KWENYE VIKUNDI NA MITANDAO YA JAMII

 Washiriki wa warsha hiyo wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kumaliza mafunzo husika
 Washiriki wakiendelea na mijadala mbalimbali kwenye ukumbi wa warsha
 Bi Jenni akiwasirisha mada iliyojadiliwa kwenye kikundi chake wakati wa warsha
Washiriki wakisikiliza mada iliyokuwa inawasilishwa na Mwezeshaji kutoka TGNP Badi Darusi

TGNP NA DHANA YA UMUHIMU WA KUANZISHA VITUO VYA TAARIFA KWENYE VIKUNDI NA MITANDAO YA KIJAMII

VITUO VYA TAARIFA NA MAALIFA KATIKA JAMII
Na Stephano Mango,Songea
Ni sehemu maalumu ya kukutana kwa lengo la kujifunza na kuhabarishana masuala mbalimbali yanayohusu jamii zetu kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo
KWANINI VITUO HIVYO
-Kuleta chachu ya harakati za ukombozi wa mwanamke wa kimapinduzi katika jamii
-Kusaidia ujenzi wa nguvu za pamoja kwa kutumia kukusanya na kusambaza taarifa
-Kuendesha mijadala ya wazi na kuweka kumbukumbu kuhusu mijadala hiyo
-Kufanya uchambuzi na ufuatiliaji wa masuala au kero zinazoikabili jamii husika na kuchukua hatua za pamoja
LENGO KUU
-Kuwawezesha wanaharakati wa ukombozi wa mwanamke wa kimapinduzi,vikundi,mitandao ya jamii kufikia fursa za kupashana,kubadilishana maarifa na taarifa
-Kuongeza hamasa katika masuala yanayohusu haki za binadamu kwa mlengo wa ukombozi wa mwanamke wa kimapinduzi
MALENGO MAHSUSI YA VITUO
-Kuwa na eneo la vituo vya wanawake,vikundi na kuhamasishana ili kuchukua hatua za pamoja kuleta mabadiliko
-Kukita vuguvugu la ukombozi wa mwanamke wa kimapinduzi katika ngazi ya jamii kwa kuwawezesha wanawake na vikundi vya wanaharakati na mitandao kuweka kumbukumbu na kupashana habari
-Kuboresha na kuimarisha mahusiano na kupashana habari kati ya wanaharakati na vikundi ili kupunguza pengo kati ya wanaofaidi taarifa muhimu na wale ambao hawapati taarifa hizo kwa wakati muafaka

Tuesday, November 15, 2011

TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MPANGO KAZI WA ASASI YA RUVUMA ORPHANS ASSOCIATIONS(ROA)

RUVUMA ORPHANS ASSOCIATIONS
(ROA)

Sokoine Road
, Mfaranyaki ward. S.L.P. 1196, Songea
Simu: 0754-533 032, 0713-290 473



TAARIFA YA UTENDAJI KAZI
HALMASHAURI YA MANISPAA YA SONGEA

JULAI HADI SEPTEMBA, 2011


Imeandaliwa na;
Menejinemti ya ROA.                                               Oktoba, 2011





TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA TANZIA

Mtandao huu unaungana na familia ya Gerson Msigwa kwenye majonzi makubwa ya kuondokewa na ndugu yao mpendwa Pascalina Lukas Msigwa mwenye umri wa miezi 6 aliyefariki dunia jana mchana kwenye Hospital ya mkoa ya Songea na mazishi kufanyika leo kwenye makaburi ya Songambele,Bombambili,Bwana alitoa na bwana ametwaa jina lake lihimidiwe,Mungu mwenyezi aiweke roho ya marehemu na marehemu wengine wote mahali pema peponi Amina

 Ndugu wa familia ya Marehemu Pascalina Lukas Msigwa wakiwasha michumaa na kuiweka juu ya kabuli lake ikiwa ni ishara ya mwanga wa milele na upendo wao kwake baada ya mazishi yake yaliyofanyika leo mchana katika makaburi ya Songambele Bombambili mjini Songea na kuhudhuriwa na wananchi,viongozi wa vyama mbalimbali na Serikali,Waandishi wa Habari na wafanyabiashara mbalimbali mjini Songea na mkoa jilani wa Njombe
 Bibi wa Marehemu Pascalina Lukas Msigwa(Mama Lucy) akiweka ua kwenye kaburi la marehemu ikiwa ni ishara ya upendo

Msemaji wa familia ya Marehemu Pascalina Lukas Msigwa,Gorden Sanga(Sanga One) akiwashukuru ndugu,jamaa na marafiki waliojaribu kunusuru uhai wa marehemu na wale wote waliojitokeza kumsindikiza kwenye makazi ya milele ndugu yao mpendwa

WARSHA YA TGNP YAWAKUTANISHA WADAU MBALIMBALI WA HARAKATI ZA MWANAMKE WA KIMAPINDUZI

Naibu Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mariam Dizumba akiteta jambo na Mwenyekiti wa Kamati za Huduma ya Jamii na Uchumi wa Manispaa hiyo Genfrida Haule,akina Mama hao waligombea kwenye kinyanganyiro cha nafasi ya UMEYA wa Halmashauri hiyo na kufanikiwa kupita kwenye vikao mbalimbali kabla ya kuchujwa kwenye kikao cha mwisho

WASHIRIKI WAKIENDELEA KUPATA MAFUNZO MBALIMBALI KATIKA WARSHA MKOANI RUVUMA

MTANDAO WA JINSIA TANZANIA(TGNP) KATIKA UTAFITI MDOGO WA VYOMBO VYA HABARI MWAKA 2011 RUVUMA

 Waandishi wa Habari wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) Kanda za nyanda za juu Kusini Stephano Mango na Juma Nyumayo wakitambulishana Kiraghabishi kwenye warsha ya majadiliano ya pamoja kuhusu utafiti mdogo wa vyombo vya habari mwaka 2011 iliyofanyika kwenye ukumbi wa Saccos ya Walimu wa Songea Vijijini leo

WANAWAKE WATAKIWA KUACHA UWOGA WA KURIPOTI TAARIFA ZA UKATILI WA KIJINSIA
Na Stephano Mango,Songea
WANAWAKE nchini wametakiwa kuacha uwoga wa kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kwenye vyombo vya habari ili kuweza kujenga mazingira ya kukomesha ukatili mbalimbali wa kijinsia uliokithili miongoni mwa jamii za Kitanzania
Wito huo umetolewa jana na Naibu Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mariam Dizumba alipokuwa akichangia mada ya wadau muhimu wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) kwenye warsha ya majadiliano ya pamoja kuhusu utafiti mdogo wa vyombo vya habari iliyofanyika kwenye ukumbi wa Saccos ya Walimu wa Songea Vijijini
Dizumba alisema kuwa vyombo vya habari ni wadau muhimu sana katika harakati za ukombozi wa mwanamke wa kimapinduzi hasa wakati huu ambao taifa letu linaelekea kwenye miaka 50 ya uhuru ili kuweza kuzibaini changamoto mbalimbali za wanawake zilizokuwa zinawakabili wanawake miaka hiyo na sasa tuweke mikakati mingine ya kuzikabili changamoto za sasa
Akizungumza kwenye warsha hiyo ya siku mbili Mwanaharakati wa Mtandao wa Jinsia Nyanda za Juu Kusini Juma Nyumayo alisema kuwa vyombo vya habari nchini vimetoa mchango mkubwa sana katika harakati za kuleta usawa ,uwiano wa kijinsia na haki sawa za kijamii ili kuboresha ustawi wao
Nyumayo alisema kuwa kwa muda mrefu sasa vyombo hivyo vimeweza kusambaza taarifa za ujengaji wa vuguvugu la ukombozi wa wanawake wa kimapinduzi hasa wanaoishi pembezoni ili kukuza uwepo na upatikanaji wa habari na maarifa kuhusu harakati za ujenzi wa vuguvugu hilo na kusaidia kujenga mitandao na kuendeleza vuguvugu hilo
Kwa upande wake Mwezeshaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) Badi Darusi alisema kuwa lengo kuu la majadiliano hayo ya siku mbili ni kuelewa ni kwa kiasi gani vyombo vya habari vimeweza kuchangia katika kazi za Tgnp na kusambaza habari kupitia kampeni ya na harakati za ukombozi wa mwanamke wa Kimapinduzi mkoani Ruvuma
Darusi alisema kuwa washiriki watapata fursa ya kuwatambua wadau muhimu wa Tgnp katika ngazi za jamii,fursa na changamoto zao,kuainisha na kuchambua hatua zilizochukuliwa na katika harakati za Tgnp,kupima kiwango cha uelewa wa kuhusu Tgnp na Waandishi wa habari katika dhana ya majadiliano,dodoso,visa mkasa,maswali chokozi,kazi za vikundi na uchambuzi wa pamoja

 Mwezeshaji toka TGNP Badi Darusi akieleza maudhui ya warsha hiyo kwa washiriki
Washiriki wa warsha hiyo wakisikiliza mada mbalimbali zilizowasilishwa na Mwezeshaji Badi Darusi

Monday, November 14, 2011

NBC WATAMBA KUICHARAZA BAKORA CRDB KATIKA MECHI YA KIRAFIKI

             Nahodha wa Timu ya NBC Emmanuel Ntobi akizungumza na waandishi wa habari
Na Stephano Mango,Songea
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) tawi la Songea wametamba kuwanyeshea mvua ya magori watani wao wa jadi Benki CRDB katika mechi ya kirafiki inayotarajiwa kuchezwa Novemba 20 mwaka huu katika uwanja wa Majimaji
Akizungumza na Waandishi wa habari jana kwenye viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya Majiamaji Songea Nahodha wa timu ya NBC Songea  Emmanuel  Ntobi alisema maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika kwani wachezaji wote wana ari nzuri wanaendelea na mazoezi  kwa ajili ya mechi hiyo ya aina yake
Ntobi alisema kuwa lengo mechi hiyo ni kukuza urafiki,ujirani na undugu kati ya taasisi za kifedha na wateja wao kiujumla kwani muda mwingi wamekuwa wakikutana katika shuguli za kibenki tu na kufanya wateja wasifurahi  pamoja na wafanyakazi wa taasisi za kibenki
Alisema kuwa lengo jingine ni kujenga afya njema za wafanyakazi wa taasisi hizo za kifedha kwani michezo licha ya kuwaweka watu pamoja pia ni nguzo muhimu ya kujenga afya stahiki kwa binadamu yoyote
Alisema kuwa siku hiyo ni muhimu sana kwa kutengeneza na kudumisha mtandao baina ya wateja na maafisa wa taasisi hizo za benki na kwamba kutakuwa na burudani mbalimbali zitakazoporomoshwa na maafisa wa benki hizo muhimu kibiashara nchini
Alifafanua kuwa mechi hiyo ya kirafiki ni hatua muhimu ya kuendelea na mipango stahiki ya kuboresha shughuli za kibenki na wateja wa taasisi za kifedha ndani ya mkoa na nje ya mkoa ili waweze kufaidi huduma za taasisi hizo kikamilifu na kukuza mahusiano
Nahodha huyo Ntobi alisema kuwa baada ya mechi hiyo kukamilika kutakuwa na programu nyingine mbalimbali za ujrlani mwema ikiwa pamoja na midaharo kuhusu thamani ya shilingi ya Tanzania na kudorora kwa uchumi wake
Alieleza zaidi kuwa katika mechi hiyo ya aina yake mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Meneja wa Kampuni ya Tigo Mkoa wa Ruvuma  Wilfred Nestory na kwamba wateja wa taasisi za fedha na wapenzi wa soka wanapaswa kuhudhuria mechi hiyo muhimu
MWISHO

HAYA NDIYO YALIYOJIRI KATIKA UZINDUZI WA MRADI WA KISASA NA WA AINA YAKE WA UPIMAJI WA VIWANJA 18000 KATIKA KATA YA MSHANGANO

 Afisa Mtendaji wa kata ya Mshangano Stan Kibiki akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa upimaji wa viwanja 18000 wakati wa uzinduzi
 Diwani wa Kata ya Mshangano Faustine Mhagama akizungumza siku ya uzinduzi
 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ardhi Plan Gombo Samandito akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa mradi wa upimaji wa viwanja 18000 katika kata ya Mshangano
Sehemu ya mradi wa upimaji viwanja 18000 linavyoonekana katika eneo la Beroya kata ya Mshangano

MRADI WA UPIMAJI VIWANJA 18000 WAZINDURIWA KWA MBWEMBWE MBALIMBALI KATIKA ENEO LA BEROYA KATA YA MSHANGANO

 Mgeni Rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati za Huduza za Uchumi na Jamii katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Genfrida Haule wa tatu toka kushoto ambaye alimwakilisha Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Charles Mhagama akizindua mradi wa upimaji wa viwanja 18000 katika eneo la kata ya Mshangano kwa kutumia Kampuni ya Ardhi Plan huku akishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali
Mgeni rasmi Genfrida Haule akikagua barabara iliyochimbwa na wananchi wa Kta ya Mshangano ndani ya eneo la mradi wa upimaji wa viwanja huku akisindikizwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali katika Manispaa ya Songea
 Mgeni Rasmi Genfrida Haule akiwahutubia wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa mradi wa kisasa na wa aina yake wa upimaji wa viwanja 18000
 Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa mradi wa upimaji wa viwanja iliyokuwa ikitolewa na mgeni rasmi Genfrida Haule
Sehemu ya barabara iliyochongwa na wananchi kwa kupata ujira wa kulipwa Tshs 5000 kwa kila mmoja kwenye eneo la mradi

MRADI WA UPIMAJI VIWANJA 18000 SONGEA KUWAKOMBOA WANANCHI KIUCHUMI
Na Stephano Mango,Songea
IMEDHIHIRIKA kuwa tatizo la makazi holela ambalo limeshamiri nchini limetokana na kutokuwa makini katika mipango miji na ukosefu wa wataalamu wa mipango miji wenye ubunifu na kusababisha adha kubwa kwa wananchi kutokana na wananchi kuvamia maeneo mengi na kujenga holela
Na kusababisha maeneo hayo  mengi ya aina hiyo kukosa miundombinu ya maji safi na maji taka,barabara na nishati ya umeme na kufanya mikakati mbalimbali ya maendeleo  kutofikiwa kikamilifu,jambo ambalo linawezekana kuepukwa ikiwa kila mtu atatimiza wajibu wake kwa kukomesha ujenzi wa makazi holela
Novemba  19 mwaka 2011 nilibahatika kuhudhuria uzinduzi wa mradi wa kisasa  na wa aina yake ambao haujawahi kutokea tangu nchi ipate uhuru wake mwaka 1961 wa upimaji wa viwanja 18,000 katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Mradi huo umezinduriwa katika kata ya Mshangano yenye mitaa  mitano ya Namanyigu,Mitendewawa,Mhumbezi,Chandarua na Mshangano yenye jumla ya kaya 1508 zenye wakazi 7540 ikiwa wanaume 3196 na wanawake 4344
Ambapo wakazi wa kata hiyo kama walivyo wakazi wa kata zingine 20 zilizopo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Songea wanajishughulisha na kilimo,ufugaji,na biashara ndogondogo katika  kujitafutia kipato cha maisha yao,
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa upimaji wa viwanja hivyo alikuwa Mshahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Charles Mhagama ambaye aliwakilishwa na Mwenyekiti wa Kamati za Huduma za Uchumi na Jamii wa Manispaa hiyo Genfrida Haule
Akizindua mradi huo wa upimaji viwanja hivyo  Haule alisema kuwa  Suala la upimaji viwanja ni hatua kubwa ya maendeleo kwa kuwa baada ya upimaji miundombinu ya maji na umeme itakuja na wananchi wameongeza kipato kwa kuweza kukopa  na kuendesha miradi kupitia viwanja  na nyumba zao huku viwanja vikipandishwa thamani
“Mradi huo utawainua kiuchumi wananchi wa Kata ya Mshangano kwa sababu wataweza kukopaa kupitia makazi yao  na kwamba wataweza kuishi katika makazi bora yaliyopimwa na kufanya mji wa Mshangano kuwa wa kisasa zaidi kuliko maeneo mengine ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea”alisema Haule
Akielezea historia ya Mradi huo Afisa Mtendaji wa Kata ya Mshangano Stan Kibiki alisema kuwa mradi huo wa upimaji wa viwanja kwa kutumia Kampuni uliibuliwa na wananchi wenyewe baada ya kuona wanakaa na kuishi katika makazi holela yasiyopimwa kwa muda mrefu
Kibiki alisema kuwa kwa muda wa miaka mingi wananchi wa kata hii wamekuwa wakipeleka maombi Halmashauri ya kuomba kupimiwa maeneo yao bila mafanikio kutokana na Halmashauri kukosa uwezo wa kifedha
“Mwaka 2010 kata yetu ilibahatika kupata mradi wa upimaji wa viwanja ilibahatika kupata mradi wa upimaji viwanja wa Halmashauri lakini bahati mbaya fedha yenyewe ilikuwa kidogo kwani waliweza  kupima viwanja 347 katika mtaa wa Namanyigu eneo dogo mashambani hivyo tatizo la wananchi kuishi katika makazi holela lilibaki palepale”alisema Kibiki
Alisema kuwa wananchi  kwa kushirikiana na viongozi wao katika kutatua tatizo hili waliamua kutafuta njia mbadala ambayo kwa kutumia sheria namba 8 ya Mipango Miji ya 2007 walitafuta Kampuni ya Ardhi Plan ya Jijini Dar Es Salaam ili iweze kuwapimia viwanja katika maeneo yao
Alieleza kuwa baada ya kuipata Kampuni hiyo makubaliano yakawa malipo ni ardhi kwa ardhi yaani wanapima ardhi wanalipwa ardhi kwa asilimia za kwamba mwananchi anapata 60% ya ardhi iliyopimwa na Kampuni inapata 40% ya ardhi iliyopimwa
Alifafanua kuwa asilimia 40% inayotolewa kwa Kampuni inatumika katika kuandaa michoro ya ubunifu wa mipango Miji (10%),kupima viwanja (10%)kuchonga barabara (10%) na faida ya Kampuni (10%) na kwamba mradi huu hauhusishi malipo ya fidia yoyote hii ni kwa makubaliano ya wananchi wenyewe na itakuwa kwa kusogezana
Afisa huyo alisema kuwa maeneo ya umma kama vile soko,shule,zahanati ,makaburi,stendi,msikiti,kanisa na maeneo ya wazi(open space)  yatatolewa bure katika mradi huo na kufanywa kuwa mradi wa kwanza kuibuliwa na wananchi wenyewe kwa kuitumia Kampuni ya Ardhi Plan kupanga mji wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Alieleza kuwa gharama za mradi huo zinatolewa na wananchi wenyewe kwa kutoa ardhi badala ya kusubiri  Serikali mpaka ipate uwezo wa kifedha ambapo kwa wale wenye maeneo madogo yaani kiwanja kimoja mpaka viwili wanatozwa gharama ya fedha shilingi laki moja(100,000/=) kwa kiwanja kimoja na laki mbili(200,000) kwa viwanja viwili kama gharama za upimaji
Kibiki alisema kuwa mitaa ambayo  michoro yake imekamilika ni Mshangano,Namanyigu, na Mitendewawa yenye jumla ya viwanja elfu kumi na nane (18,000/=) ambapo mitaa mingine itafuata baadaye
“Mchoro ambao tayari mawe yameshapandwa ni mchoro namba 9 ujulikanao kama Beroya na sasa wananchi wanaendelea na uchongaji wa barabara mchoro ambao una jumla ya viwanja 800”alisema Kibiki
Alisema kuwa mradi huo umesifiwa na viongozi wengi na wanaharakati mbalimbali wa masuala ya ardhi na maendeleo ya wananchi wanyonge kwani wamefanikiwa kupata maeneo yaliyopimwa na kuthaminiwa kwa ajili ya makazi yao na kuondokana na makazi holela
“Tunaomba wananchi wa maeneo mengine wenye matatizo kama yetu watuunge mkono wafanye kama tulivyofanya sisi kwani watapata maisha bora kwani thamani ya ardhi yao itapanda na kuwa na thamani kubwa”alisema
Alieleza zaidi kuwa huduma za jamii kama maji ya bomba,umeme,barabara na miundombinu mingine itawafikia kama ambavyo wananchi wa kata ya Mshangano wanavyotegemea kupata mara baada ya mradi kukamilika
Kibiki alisema kuwa katika mradi huo wananchi watapata faida nyingi ikiwemo ya ajira kuanzia hatua ya kupima viwanja kwani mchoro mmoja umetoa ajira kwa watu 40 ambao wamekuwa wanalipwa  Tshs 4000/= kwa kutwa moja na kwamba kwa michoro 23 itatoa ajira kwa watu 920
Alifafanua kuwa kwenye uchongaji wa barabara mchoro mmoja umetoa ajira kwa watu 80 ambapo kila mmoja analipwa Tshs 5000/= kwa kutwa hivyo michoro 23 itatoa ajira kwa watu 1840 ambapo jumla ya michoro yote 23 wananchi watakao kuwa wamepata ajira kwenye upimaji na kuchonga barabara ni watu 2760 wanawake na wanaume
Alieleza jumla ya fedha watakayokuwa wanapata wananchi wa kata hiyo kwenye upimaji wa viwanja ni 920X4000=3680,000/= na kwenye uchongaji wa barabara 1840x5000=9,200,000/= na kufanya jumla ya fedha yote kuwa ni Tshs 12,880,000/= kwa siku
Alifafanua kuwa wafanyakazi hao watatoka ndani ya kata ya Mshangano ambapo mradi unatekelezwa kwani hiyo inaweza kuwasaidia sana wananchi kujikimu kimaisha na kumudu kununua pembejeo za kilimo katika msimu huu na hivyo kuzalisha mazao kwa wingi
Naye  Diwani wa Kata ya Mshangano Faustine Mhagama akizungumza kwenye uzinduzi huo alisema kuwa mti wenye matunda ndio unaopigwa mawe hivyo kwa kuwa mradi huo una manufaa kwa wananchi wake umekuwa ukipigwa sana mawe,lakini hata hivyo anasema atasimamaimara kupigania haki za wananchi wake.
Anasema kuwa  kwa mradi huo wananchi wamenufaika kwa kuweza  kuuza viwanja vyao kwa bei kubwa lakini pia Halmashauri imepunguziwa gharama  ya kulipa fidia ambayo mara nyingi imekuwa ikichelewa kulipa au kushindwa kulipa na kuzua malalamiko na migogoro kwa wananchi
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Ardhi Plan inayopima viwanja hivyo Gombo Samandito anasema kuwa Mradi huo ni wa  aina yake hapa Nchini na kwamba hakujawahi kuwa na mradi kama ule wa kupima viwanja 18,000 kwa muda mfupi tangu nchi ipate uhuru na kwamba dhamira yao ni kuona wananchi wakiishi katika makazi bora.
Samandito alisema kuwa mradi huo umeisaidia sana Serikali  kwani umeipunguza tatizo la kushindwa kupanga mji kutokana na ukosefu wa fedha za kugharamia mipango stahiki ya makazi bora kwani wananchi wa Mshangano wamethubutu kupanga mji kwa gharama zao jambo ambalo halijawahi kutokea kwa wananchi kupima viwanja vingi kiasi hicho kwa gharama zao
Mwandishi wa Makala
Anapatikana Simu 0755-335051/0715-335051/0784-335051/0778-335051
Barua pepe;stephano12mango@yahoo.com

WANANCHI SONGEA KUPIMIWA VIWANJA 18,000 KUONDOKANA NA MAKAZI HOLELA

 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ardhi Plan Gombo Samandito akiwaonyeshwa wananchi RAMANI zilizopitishwa na Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya upimaji wa viwanja kata ya Mshangano
Na Joseph Mwambije,Songea
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma imezindua mradi wa upimaji viwanja zaidi ya 18,000 unaofanywa na Kampuni binafsi ya Ardhi Plan Limited  kwenye Kata ya Mshangano baada ya kuibuliwa na wananchi wenyewe baada ya kuona  wanaishi katika makazi holela kwa muda mrefu.
Mradi huo umezinduliwa juzi na Meya wa Manispaa ya Songea Charles Mhagama aliyewakilishwa na Mwenyekiti wa huduma za jamii na elimu wa Manispaa hiyo  Genifrida Haule aliyekata utepe kuzindua mradi huo.
Akizungumza baada ya kuzindua mradi huo Haule alisema Mradi huo utawainua kiuchumi wananchi wa Kata ya Mshangano kwa sababu wataweza kukopaa kupitia makazi yao  na kwamba wataweza kuishi katika makazi bora,
‘Suala la upimaji viwanja ni hatua kubwa ya maendeleo kwa kuwa baada ya upimaji miundombinu ya maji na umeme itakuja na wananchi wameongeza kipato kwa kuweza kukopa  na kuendesha miradi kupitia viwanja vyao na nyumba zao huku viwanja vikipandishwa thamani’alisema.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa  Mradi huo Afisa Mtendaji wa Kata ya Mshangano Stan Kibiki alisema Kata hiyo ina Kaya 1508 zenye wakazi 7540  na mitaa mitano ya Mshangano,Namanyigu,Chandarua,Mitendewawa na  Muhumbezi.
Alisema kuwa wananchi baada ya kuona kwa muda mrefu wanakaa na kuishi katika makazi holela yasiyopimwa wakaamua kuibua Mradi wa upimaji viwanja hasa baada ya kupeleka maombi ya kupimiwa viwanja   Halmashauri lakini ilishindwa kuwapimia  kwa kile ilichodai kuwa haina fedha.
“Mwaka 2010 Kata yetu ilipata bahati ya kupata mradi wa upimaji viwanja  ulioendeshwa na Manispaa ya Songea lakini fedha ilikuwa kidogo na hivyo waliweza kupima viwanja 347 tu katika Mtaa mmoja wa Namanyigu katika eneo dogo na hivyo tatizo la wananchi kuishi katika makazi holela likabaki palepale’alisema katika taarifa hiyo.
Alisema kuwa wananchi katika kutatua tatizo hilo kwa kushirikiana na viongozi wao waliamua kutafuta njia mbadala kwa kutumia sheria namba 8 ya  ya mipango miji ya mwaka 2007 walitafuta Kampuni ya Ardhi Plan Limitedya Dares-salaam ili iweze kuwapimia viwanja katika maeneo yao.
Alisema Mitaa ambayo michoro yake imekamlika ni  Mshangano,Namanyigu, na Mitendewawa  yenye jumla ya viwanja 18,000 na mitaa mingine itafuata baadaye na kufafanua kuwa mchoro namba 9 wa Beroya wenye viwanja 800 umekamilika na kazi ya kuchonga barabara inaendelea.
Afisa Mtendaji huyo alisema  mradi huo umesaidia kutoa ajira kwa wananchi kwa kuwa mchoro mmoja umetoa ajira kwa wananchi 40 ambao walikuwa wanalipwa sh. 4000 kwa kutwa na kwamba michoro23 ya mradi huo itatoa ajira 920.
Alisema katika uchongajio barabara mchoro mmoja unatoa ajira kwa watu 80 ambapo kila mmoja analipwea sh. 5000 na kwamba wananchi 2760 wanawake na wanaume watakuwa wamepata ajira katika zoezi la uchongaji wa barabara.
Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Kampuni hiyo inayopima viwanja hivyo Gombo Samandito anasema kuwa Mradi huo ni wa  aina yake hapa Nchini na kwamba hakujawahi kuwa na mradi kama ule wa kupima viwanja 18,000 kwa muda mfupi tangu nchi ipate uhuru na kwamba dhamira yao ni kuona wananchi wakiishi katika makazi bora.
Naye Diwani wa Kata hiyo  Faustin Mhagama anasema  mti wenye matunda ndio unaopigwa mawe hivyo kwa kuwa mradi huo una manufaa kwa wananchi wake umekuwa ukipigwa sana mawe,lakini hata hivyo anasema atasimamaimara kupigania haki za wananchi wake.
Anasema kuwa  kwa mradi huo wananchi wamenufaika kwa kuweza  kuuza viwanja vyao kwa bei kubwa lakini pia Halmashauri imepunguziwa gharama  ya kulipa fidia ambayo mara nyingi imekuwa ikichelewa kulipa au kushindwa kulipa na kuzua malalamiko na migogoro kwa wananchi.
MWISHO

Saturday, November 12, 2011

MAGARI YA ABIRIA YAKWAMA KITUO CHA MABASI KUTOKANA NA MVUA

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Nachoa Zakaria
Na Mwandishi Wetu, Songea
WAKAZI  wa Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wakiwemo wamiliki wa mabasi yanayo safirisha abiria wameulalamikia uongozi wa Halmashauri ya Manspaa hiyo kutokana  na kushindwa kuzifanyia ukarabati barabara pamoja na kituo kikuu cha mabasi ambacho kimekithili kuwa na ubovu ambao umesababisha kuwepo na mashimo mengi katikati ya kituo hicho na kupelekea magari kukwama wakati mvua zinaendelea kunyesha

Mtandao huu wa stephanomango.blogspot.com ulitembelea kituo hicho cha mabasi kwa lengo la kujionea hali halisi ya ubovu wa miundo mbinu kwenye eneo hilo ambalo lilikuwa limejaa tope wakati mvua zinaendelea kunyesha huku mabasi yaliyosheheni abiria yakiwa yametitia kwenye tope hilo.

Uharibifu huo ambao umechangia kwa kiasi kikubwa kujaa kwa tope  na kusababisha wananchi na magari kupita kwa tabu na mengine kukwama kabisa kutokana na utelezi uliotokana na uongozi wa  Halmashauri hiyo kuridhia  kumwaga kifusi cha udongo wa mfinyaji katikati ya kituo hicho kwa madai kuwa wanafukia mashimo yaliyokithili kwenye  eneo hilo jambo ambalo limeonekana kuwa ni kero kubwa kwa wakazi wa Songea wakiwemo abiria na wamiliki wa mabasi .  

 Hali hiyo ndiyo iliyopelekea watumiaji wa kituo hicho kutoa malalamiko yao kwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea wakidai kilio chao cha kutengenezewa stendi hiyo kimekuwa ni cha muda mrefu na kitu cha kushangaza hakuna hatua zozote zinazo chukuliwa kwa ajiri  ya kukinusuru kituo hicho ambacho kipo katikati ya Manispaa hiyo

Mmoja  wa wakazi wa Manispaa ya Songea Lucas Haule alisema  inashangaza kuona kituo hicho ambacho kimekuwa kikilalamikiwa kwa muda mrefu kutokana na miundo mbinu yake kuwa mibovu huku Halmashauri ikitoza ushuru  mkubwa kwa magari yanayo ingia kwenye kituo hicho yakiwemo mabasi ya kusafirishia abiria .

Nae mmoja wa watumiaji wa kituo hicho cha mabasi Paulo Ndunguru  alisema kuwa  anashangazwa kuona kituo hicho kilicho kithiri mashimo kinatengenezwa kiholela bila kufuata utaalamu  na kudai kwamba endapo kama ungetumika utaalamu yakinifu tatizo hilo la kukwama kwa magari katikati ya kituo lisingeweza kujitokeza .

Hata hivyo jitihada zilizofanywa  na mtandao huu za kumpata mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Nachoa Zakaria ziligonga mwamba baada ya kutopatikana ofsini kwake ambapo Katibu muhutasi wake alieleza kuwa Mkurugenzi alikuwa kwenye vikao vya maandalizi ya mapokezi ya mwenge na maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru na kwamba simu yake ya kiganjani alipopigiwa mara tatu iliita bila kupokelewa.
MWISHO

WANANCHI WATWANGANA KUGOMBEA ARDHI WILAYANI TUNDURU

                             Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Madaha

Na Augustino Chindiye,Tunduru    

MAPIGANO makali ya kugombea Ardhi ya kulima  yamezuka kati ya wakazi wa vijiji vya  Semeni Chikomo Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma na kumjeruhi kwa kukata kata kwa Mapanga mtu mmoja aliyefahamika kwa jina  la Mohamed Abdalah.

Kufuatia tukio hilo majeruhi huyo amelazwa katika Hospitali ya Missioni ya Mbesa baaya ya kujeruhi vibaya sehemu mbali mbali za mwili wake hali iliyo pelekea zaidi ya watu 50 wakazi wa kijiji cha Chikomo Wilayani humo wanatafutwa na Polisi ili waweze kujibu tuhuma hizo zilizotokaka na wananchi wa vijiji hivyo kuanzisha mapigano hayo.

Wakizungumzia tukio hilo kwa nyakati tofauti mbali na kukiri kutokea kwa ugomvi huo madiwani wa Kata za Mtina Mahamudu Katomondo na Kata ya Mbesa , Mohamedi Mtiko kila mmoja wao alitoa lawama kuwa wananchi wa kijiji jirani ndio chanzo cha mgogoro huo.

Upande wa Diwani wa kata ya mtina Katomondo yeye alidai kuwa wananchi wa kijiji cha Chikomo ndio waliofanya makosa ya kuvamia mipaka ya kijiji chake akidai kuwa mpaka unaotenganisha kijiji cha Semeni na Chikomo iliwekwa eneo la ng’ambo ya Mto Lukumbule.

Wakati diwani huyo akitoa madai hayo Diwani wa Kata ya Mbesa Mtiko yeye alidai kuwa na watu watatu waliohusika wakati wa upimaji wa mipaka hiyo mwaka 1978 na wanayo ramani hiyo inayo onesha mipaka ya vijiji hivyo  na kwamba ugomvi uliopo kati ya vijiji hivyo umetokana na wananchi wa kijiji cha Semeni kukaidi kulipa ushuru unaotakiwa kutozwa pindi wakulima wanapovuka mipaka na kwenda kulima kijiji jirani.

Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo,Katibu tawala wa Wilaya ya Tunduru  Martini Mulwafu mbali na kukiri kuwepo kwa mgogoro huo alisema kuwa ofisi yake imepanga kufanya mazungumzo kati ya viongozi kutoka katika Tarafa, kata na vijiji vinavyohusika na mgogoro huo ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu.

ASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA ZA KUMUUA BABA YAKE WILAYANI TUNDURU

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda

Na Augustino Chindiye ,Tunduru

KIJANA wa miaka 21 aliyetambulika kwa jina la Hasan Adam Chimsala anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kumuua Baba yake mzazi Mwalimu mstaafu Mwl. Adamu Isaa Chimsala (60).

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya familia hiyo pamoja na kijana huyo kudaiwa kushindikana kutokana na tabia yake ya unywaji wa pombe na uvutaji bangi wa kupindukiwa  inadaiwa kijana huyo alichukua uamuzi huo kwa kumtuhumu baba yake huyo kuwa amekuwa hampatii matunzo kwa muda mrefu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael kamuhanda alisema kuwa tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Chemchem Wilayani Tunduru.

Kamanda Kamuhanda aliendelea kufafanua kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Novemba 11 mwaka huu wakati mzee huyo akiwa amejipumzisha kwa ajili ya kusubiri chakula cha jioni.

Alisema wakati marehemu akiwa katika maandalizi hayo ghafla kijana kuyo alimvamia na kuanza kumshambulia kwa kumtoboa na kitu chenye ncha kali kichwani na sehemu mbali mbali za mwili wake.

Taarifa zilizotolewa na Mganga aliyeufanyia mwili wa marehemu Chimsala uchunguzi Dkt.Jeshi Daraja zinasema kuwa kifo hicho kilisababishwa na kutokwa na damu nyingi zilizosababishwa na majeraha hayo.

Alisema marehemu Chimsala alijeruhiwa vibaya kichwani ambako alipasuka fuvu la kichwa chake na kusababisha damu kutoka kwa wingi kupitia masikioni,puani na mdomoni.

Mwisho

Thursday, November 10, 2011

RC MWAMBUNGU AWAPIGA MKWALA WALANGUZI WA SARUJI RUVUMA

                                         MKUU WA MKOA WA RUVUMA SAID MWAMBUNGU
Na Gideon Mwakanosya, Songea
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amewaonya wafanyabiashara wanaouza saruji Mkoani humo kuacha mara moja tabia ya kuuza  bidhaa hiyo kwa ulanguzi ambapo Wakazi wa maeneo mbalimbali wamekuwa wakilalamikia bidhaa hiyo kuuzwa kati ya shilingi 25,000 na 28,000 kwa mfuko wa saruji wenye ujazo wa kilo 50 badala ya shilingi 15,000 bei ambayo ni elekezi toka kwa Kiwanda cha saruji Mbeya na amewapa siku tatu walanguzi wa bidhaa hiyo kuacha mara moja.
Akizungumza na mwandishi wa mtandao huu wa www.stephanomango.blogspot.com ofisini kwake  hivi karibuni Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa Serikali haitakubalia kamwe kuona baadhi ya Wafanyabiashara wakiwa wanauza saruji kwa bei kubwa ambayo Mwananchi wa kipato cha chini hawezi kuimudu.
Alisema kuwa kutokana na kuwepo malalamiko mengi toka kwa Wananchi kuwa bei ya Saruji imekuwa ni kubwa alilazimika yeye mwenyewe kufanya ziara ya ghafla kwenye baadhi ya maduka yanayouza Saruji na kukuta bidhaa hiyo ikiwa imewekwa lebo ya bei ya shilingi 28,000 kwa mfuko mmoja wenye ujazo wa kilo 50.
Alieleza zaidi kuwa baada ya kubaini kuwepo kwa tatizo hilo amewaagiza wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha kuwa Mawakala wa Saruji Mkoani humo kuhakikisha kuwa wanauza mfuko mmoja wa Saruji wenye ujazo wa kilo 50 kati ya shilingi 15,000 hadi 17,000 badala ya bei waliyokuwa wakiendelea kuwalangua wananchi.
“Ndugu Mwandishi nimefanya mawasiliano ya moja kwa moja kwenye Kiwanda cha Saruji Mbeya ambako nimewauliza ni kwanini bei ya Saruji imepanda ghafla,wamenijibu kwamba wao hawajapandisha bei na uzalishaji wa bidhaa hiyo haujashuka na wala gharama za uzalishaji hazijapanda” Alisema Rc Mwambungu.
Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na mtandao huu kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa umebaini kuwa bei ya Saruji imepanda tangu Agosti mwaka huu ambapo imekuwa ikiuzwa kati ya shilingi 25,000 hadi 28,000 kwa mfuko wa kilo 50.
Uchunguzi huo pia umebaini kuwa bidhaa hiyo imekuwa ikisafirishwa kutoka Mbeya hadi Makambako ambako baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wakiinunua kisha kuileta Ruvuma kuiuza kwa bei ya ulanguzi ambayo tayari imekuwa ikilalamikiwa na Wakazi wakiwemo Wakandarasi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya Wananchi waliiomba Serikali ione umuhimu wa kuchukua hatua za haraka za kuudhibiti mfumuko wa bei ya saruji Mkoani Ruvuma ambao umesababisha watu wengi waliokuwa wakiendelea na shughuli za ujenzi kusitisha kutokana na bidhaa hiyo kuuzwa kwa bei kubwa.
Kwa upande wake Mkuu wa ghala la kuhifadhia Saruji ya Kiwanda cha Saruji Mbeya tawi la Songea aliyejitambulisha kwa jina moja la Kagambi alipoulizwa na mtandao huu juu ya tatizo la uhaba wa bidhaa hiyo alisema kuwa ni zaidi ya miezi miwili hajapokea Saruji toka Mbeya na ghala lake lipo tupu na alikataa kuendelea kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa yeye si msemaji labda kuwasiliana na Meneja mauzo wa Kanda ndiye anayeweza kujua ni kwanini Saruji imeadimika.
Mtandao huu ulifanya jitihada ya kumtafuta Meneja mauzo wa Saruji Kanda ya Iringa kwa njia ya simu ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Maguu, alisema kuwa zaidi ya miezi miwili Saruji imeadimika lakini hawezi kusema lolote kwa madai kuwa yeye siyo msemaji wa Kiwanda.
Hata hivyo mtandao huu ulifanikiwa kuwasiliana kwa njia ya simu na Meneja mauzo wa Kiwanda hicho cha Saruji kilichopo Halmashauri ya Jiji la Mbeya aliyejitambulisha kwa jina la Mwakasege na kumtaka atoe ufafanuzi ni kwanini kuna tatizo la uhaba wa bidhaa inayozalishwa na Kiwanda chake ambapo alisema kuwa Kiwanda cha Saruji bado kina bidhaa hiyo nyingi lakini tatizo kubwa linalowakabili ni magari makubwa ya kusafirishia Saruji kwenda kwenye maghala ya mawakala.
Mwakasege alisema kuwa kwa Mkoa wa Ruvuma tangu octoba 6 mwaka huu Kiwanda kimeshindwa kupeleka saruji kutokana na ukosefu wa magari kusafirisha Saruji kwenda Songea lakini kuna mpango ambao umebuniwa na kiwanda ambao utaweza kupunguza tatizo hilo lililojitokeza.
Aliubainisha mpango huo waliobuni kuwa ni kwa vile Mkoa wa Ruvuma una machimbo ya makaa ya mawe katika Kijiji cha Mngaka kilichopo kata ya  Ruanda Wilaya ya Mbinga  ambayo yanahitajika sana kwenye kiwanda cha Saruji Mbeya hivyo magari yatakayokuwa yakienda kubeba makaa ya mawe yatakuwa yakibeba Saruji toka Kiwandani na kuipeleka Songea ambako kuna ghala kubwa la kuhifadhia Saruji hiyo ya kiwanda kisha wafanyabiashara watakuwa wakiinunua bidhaa hiyo kwenye depot ya Songea.
Alifafanua kuwa Malori hayo makubwa yatakuwa yakitoka Mbeya yakiwa yamesheheni saruji na wakati wa kurudi yatakuwa yakisheheni makaa ya mawe toka Mngaka Ruanda Mbinga hivyo hakutakuwa na shida tena ya uhaba wa Saruji endapo mpango huo utaenda kama ulivyopangwa
MWISHO