About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Wednesday, April 11, 2012

WATANO WASHILIWA NA POLISI KWA KUKUTWA NA MBAO ZA POLINI KINYUME NA SHERIA

Na Stephano Mango, Songea
WATU watano wakiwemo askari watatu wa Idara ya Wanyama pori walioko kwenye Mbuga ya hifadhi ya Wanyama ya Taifa ya Serous Wilayani Namtumbo wanashikiliwa na Polisi Mkoani Ruvuma kwa tuhuma za kukutwa na mbao za mti pori 135 kinyume na sheria.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamhanda alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 5 asubuhi huko katika Kijiji cha Likuyu Sekamaganga kilichopo kwenye eneo la Mbuga ya hifadhi ya Wanyama ya Taifa ya Serous Wilayani Namtumbo.
Aliwataja askari wa Wanyama pori wanaoshikiliwa na Polisi kuwa ni Godian Mataba (30),Michael Mrutu (29) na Fabian Paul (34) ambao wote ni askari wa Idara ya Wanyama pori kwenye Mbuga hiyo ya Wanyama.
Amewataja wengine kuwa ni Sebastian Matembo (30) na Juma Iddi (35) maarufu kwa jina la Kilaza wote wakazi Kijiji cha Likuyu Sekamaganga   ambapo alieleza zaidi kuwa watuhumiwa hao wote walikamatwa wakiwa na mbao 135 ndani ya kambi ya hifadhi ya wanyamapori ya Mbuga ya Serous bila kuwa na kibali.
Alifafanua zaidi kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio Katibu wa Hifadhi ya Maliasili Abeid Nihuka akiwa na askari wa wanyama pori wa Mbuga ya Serous walifanya msako mkali wa kuwabaini watu wanaoharibu mazingira ya Mali asili kwenye hifadhi ya Mbuga hiyo.
 Alisema kuwa askari hao wa wanyama pori wakiwa kwenye doria walifanikiwa kuzikuta mbao 95 zikiwa zimehifadhiwa ndani ya Kambi na mbao 40 zilikutwa nje ya eneo la Kambi kwa watuhumiwa wawili ambao ni Matembo na Iddi Wakazi wa Kijiji hicho.
 Hata hivyo alieleza kuwa watuhumiwa wote watano wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kukutwa na mbao za miti pori kinyume na sheria na kwamba kwa hivi sasa Polisi inaendelea na Upelelezi zaidi na ukikamilika watafikishwa Mahakamani kujibu shtaka linalowakabili.
 MWISHO

Tuesday, April 10, 2012

ASHIKILIWA NA POLISI KWA KUKUTWA NA KETE 225 ZA MADWA YA KULEVYA

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamhanda
Na Gideon Mwakanosya, Songea
JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma limemtia mbaroni Hamza Mnadi (27) mkazi wa Mtaa wa Kalanje Wilaya ya Tunduru kwa tuhuma za kukutwa akiwa amehifadhi madawa ya kulevya aina ya Cocaine na Heroine  ambayo thamani yake bado haijafahamika
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamhanda alisema kuwa tukio hilo limetokea aprili 7 mwaka huu majira ya saa 11 jioni huko katika mtaa wa Kalanje mjini Tunduru
Alieleza kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio askari Polisi wakiwa doria walipewa taarifa toka kwa raia wema kuwa kuna mtu anafanya biashara ya madawa ya kulevya katika mtaa huo na kwamba tangu alipoanza biashara hiyo kumekuwa na watu wengi wamekuwa wakifika kwenye nyumba hiyo ya Mnadi kwa lengo la kununua madawa hayo
Alifafanua kuwa Askari hao baada ya kupata taarifa toka kwa raia wema walikwenda mpaka kwenye eneo la nyumba ya Mnadi ambako walifanikiwa kumkuta na baadae walipofanya upekuzi kwenye nyumba hiyo walimkuta akiwa na madawa ya kulevya ya Cocaine na Heroine yakiwa yamehifadhiwa kwenye paketi tisa
Alieleza zaidi kuwa madawa hayo ambayo yalikuwa yamehifadhiwa kwenye paketi 9 ambapo kila paketi kulikuwa kumehifadhiwa vipande 25 na kufanya jumla ya vipande 225 vya madawa hayo kwenye paketi zote 9 zilizokutwa ndani ya nyumba yake
Alisema kuwa kwa hivi sasa mtuhumiwa anashikiriwa na Polisi na upelelezi wa Polisi bado unaendelea na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabilI
MWISHO
MBARONI KWA KUKUTWA NA BUNDUKI NA RISASI KINYUME CHA SHERIA
Na Gideon Mwakanosya, Songea
JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma linamshikilia Lameck Ruben Halfan (38) mkazi wa eneo la Mtaa wa Aroma, Tabata Jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kukutwa akiwa na siraha aina ya Riffle na risasi zake mbili kinyume na sheria za nchi
Akizungumza na Kahama Fm jana Ofisi kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamhanda alisema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 9 mwaka huu majira ya saa 2 usiku huko katika kijiji cha Angalia kilichopo Wilaya ya Tunduru
Kamanda Kamhanda alisema kuwa siku hiyo ya tukio Askari waPolisi wakiwa kwenye doria ambao walikuwa wanashirikiana na Askari wa Wanyamapori wa Wilaya hiyo walimkamata Halfan akiwa na siraha yenye namba za usajiri 083972 ambayo ilikuwa na risasi mbili ambayo alikuwa ameifunga kwenye nguo zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye begi
Alifafanua zaidi kuwa mtuhumiwa huyo Halfan alikamatwa akiwa anatokea Kijiji cha Mwenge ambako inadaiwa kuwa anajishughulisha na shughuli za uwindaji haramu wa wanyamapori akielekea mjini Tunduru
Hata hivyo Polisi bado inaendelea kufanya upelelezi zaidi wa tukio hilo na kwamba utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma mashtaka yanayomkabili
MWISHO

Monday, April 9, 2012

MWANAFUNZI WA SEKONDARI YA MSAMALA AIBIWA MALI ZA THAMANI YA SHILINGI LAKI 9.5

NA AUGUSTINO CHINDIYE,SONGEA
WATU wasiojulikana wamevunja nyumba na kuiba mali mbalimbali zenye thamani ya Sh laki 9.5 kwenye nyumba inayomilikiwa na Dainess Mgumba (17) mkazi wa eneo la Mahenge B katika halmashauri ya manispaa ya Songea mkoani Ruvuma  .
Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma Michael Kamhanda alisema kuwa tukio hilo lilitokea aprili 3 mwaka huu majira ya saa 8 mchana huko katika eneo la Mahenge ambako Dainess ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha 3 katika shule ya sekondari ya kutwa ya Msamala aligundua kuvunjiwa nyumba yake na kuibiwa mali mbalimbali zilizokuwemo ndani .
Kamanda Kamhanda alizitaja mali zilizoibiwa kuwa ni keyboard ,DVD deck,Radio aina ya Aiwa,simu moja ya mkononi aina ya sumsung  na receiver aina ya media com vyote vikiwa na thamani ya Sh laki 9.5 na alidai kuwa watuhumiwa bado hawajakamatwa  na upelelezi wa tukio hilo unaendelea kufanywa ili kuwabaini wale wote waliohusika katika kutenda kosa hilo .
Alieleza zaidi kuwa kutokana na polisi kwa kushirikiana na sungusungu kuweka  ulinzi mkali nyakati za usiku kwa hivi sasa waharifu wamebadilisha mbinu za utendaji  wa makosa hivyo kwa sasa wamekuwa wakifanya uharifu huo nyakati za mchana ambapo alitoa mfano wa tukio hilo kuwa lilitokea wakati Dainess akiwa shuleni na aliporudi alikuta nyumba yake imevunjwa kufuli na alipoingia ndani alikuta mali zake zimeibiwa .
Alisema kuwa kwa hivi sasa polisi inaendelea kuwasaka waharifu wa tukio hilo lakini amewataka wananchi mkoani Ruvuma waone umuhimu wa kufanya dhana ya ulinzi jirani ambao utaweza kudhibiti kwa kiasi kikubwa hali hiyo ya uharifu unaofanywa na watu wanaodaiwa kuwa ni vibaka nyakati za machana .
Amewashauri viongozi wa serikari za mitaa  kwenye maeneo yao wawe na mikakati ya kuwa na dhana ya ulinzi jirani ambayo itaweza kuwakimbiza waharifu ambao walikuwa wamezoea kuiba nyakati za usiku na hivi sasa wameamua kuiba mchana baada ya kugundua kuwa zoezi la ulinzi shirikishi linalofanywa na polisi kwa kushirikiana na wananchi nyakati za usiku zimepamba moto mkoani Ruvuma.
MWISHO

AKUTWA AMEKUFA NA KUHISIWA KABLA AJAUAWA KUWA ALIBAKWA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamhanda
Na Gideon Mwakanosya, Songea
MWANAMKE mmoja aliyefahamika kwa jina la Mary Jonathan (23) Mkazi wa Mateka katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvvuma amekutwa akiwa amekufa kandokando ya mto Ruvuma na inasadikiwa kuwa kabla ya kuuwawa alikuwa amebakwa na watu kadhaa wasiofahamika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alisema kuwa tukio hilo lilitokea April 5 mwaka huu majira ya saa za asubuhi ambapo inadaiwa kuwa Mary alikutwa amekufa huku akiwa uchi wa mnyama pia alikutwa na jeraha upande wa kushoto wa kichwa chake.
Hata hivyo Kamanda Kamuhanda alisema kuwa Polisi inaendelea kufanya uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo ambalo bado linaonekana kuwa na utata kwani inadaiwa kuwa Mary aliondoka nyumbani kwa wazazi wake walioko eneo la Mateka kwenda Mahakama ya Mwanzo  ya Songea Mjini ambako alikuwa amekwenda kusikiliza kesi yake ya kutishiwa kuuwawa
Kwa mujibu wa baba yake mzazi wa Mary Sajent Jonathan wa Gereza la Mahabusu Songea ni kwamba Mary alitoka nyumbani April 4 mwaka huu majira ya saa za asubuhi na aliaga kuwa anaelekea Mahakamani kusikiliza kesi aliyokuwa amemfungulia mtu mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake anayedaiwa kuwa alimtishia kumuua kwa maneno.
Sajenti Jonathan alieleza zaidi kuwa mtoto wake tangu alipoondoka April 4 mwaka huu majira ya saa za asubuhi nyumbani kwake hakurudi hadi April 5 mwaka huu majira ya saa za asubuhi alipokutwa akiwa amekufa huku akiwa na jeraha moja upande wa kushoto wa kichwa chake.
“Ninawaambia ndugu zangu kuwa mtoto wangu Mary tangu alipoondoka juzi mpaka jana asubuhi ndiyo ameonekana akiwa ameuwawa na watu wasiofahamika na sasa hivi taarifa ya tukio hilo iko Polisi nafikiri ndiko taarifa kamili mnaweza mkazipata” alisema Sajenti Jonathan.
Alisema kuwa mwili wa marehemu hivi sasa umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Serikali ya Mkoa Songea na taratibu za mazishi zinatarajiwa kufanywa mara tu Polisi watakapomaliza uchunguzi wao.
 MWISHO

Wednesday, April 4, 2012

WAPAMBE WA CCM SONGEA WAMESABABISHA ANGUKO LA CHAMA KATIKA UCHAGUZI WA UDIWANI

Hamis Abdalah Ally akiwa kwenye moja ya mikutano ya kampeni za udiwani

NA STEPHANO MANGO, SONGEA

MAJIGAMBO na tambo za viongozi, wagombea na wapambe wa vyama vya siasa viwili vilivyoshiriki kwenye kampeni za kuwania kiti cha udiwani Kata ya Lizaboni Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma vimefikia tamati kwa wananchi kupiga kura kumchagua diwani waliokuwa wanamtaka

Vyama vilivyoshiriki kwenye mchakato wa kampeni vilikuwa ni viwili kwa maana ya Chama cha Mapinduzi (Ccm) mgombea wake alikuwa ni George Oddo Mbunda na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mgombea wake alikuwa ni Alanus Mwanja Mlongo


Wakati wa kampeni wananchi wa Kata ya Lizaboni walipata fursa ya kusikiliza sera za vyama hivyo ambapo wapigakura hao walihitimisha kwa kufanya uchaguzi wa kiongozi waliyemhitaji aprili mosi mwaka huu na kumfanya aliyekuwa mgombea wa Chadema  Alanus Mlongo kuibuka kidedea katika uchaguzi huo.


Uchaguzi huo mdogo umefanyika baada ya Kata hiyo kuwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo Ally Said Manya(CCM) pia alikuwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambaye alifariki dunia julai mwaka 2011.

Licha ya kampeni hizo kutawaliwa na vijembe, malumbano na kauli chafu kati ya vyama na wagombea, lakini wananchi wa Kata ya hiyo walizingatia sera zilizoonekana kuwa na tija kwao, ambazo pia zinatekelezeka na kumchagua kiongozi waliyekuwa wanamtaka kwa njia ya kumpigia kura.

Katika uchaguzi huo wapigakura waliopo kwenye orodha ya kudumu kwenye daftari la wapigakura walikuwa ni 7825 lakini waliopiga kura ni 3315 jambo ambalo limeonyesha wazi kuwa wakazi wengi wa Kata hiyo hawakuweza kujitokeza kupiga kura licha ya mgombea wa Chadema kupata kura 1712 wakati Mgombea wa Chama cha Mapinduzi katika Kata hiyo George Oddo Mbunda alipata kura 1579.

Nawapongeza wananchi wa kata ya Lizaboni waliotimiza wajibu wao wa kikatiba katika uchaguzi huo na kumpigia kura kiongozi ambaye alionekana kukidhi matakwa ya wananchi kutokana na sera alizokuwa anazinadi wakati wa kampeni.

Tume ya uchaguzi ilisimamia uchaguzi huu vizuri na hatua zote za uhesabuji wa kura zilikuwa za haki na utangazaji ndio maana zoezi zima lilimalizika kwa amani kwa wale wote ambao walikuwa wanasubiri matokeo kutokana na kura walizozipiga.

Matokea hayo ni salamu tosha kwa viongozi wa Ccm na wa Serikali kuhusu kupuuza haki na matakwa ya wananchi huku wakibeza kuwa kelele za mlango hazimsumbui mwenye nyumba, pamoja na kuwa vijana wengi wanaoshabikia upinzani hawana shahada za kupigia kura

Hayo ni matokeo ya mbinu dhaifu za kimkakati zilizokuwa zinafanywa na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea mjini chini ya uwenyekiti wa Hemed Dizumba za kuamua kufanya siasa za kihuni katika kampeni zilizopita na za uchaguzi huu mdogo wa udiwani

Kitendo chake cha kukataa baadhi ya maoni yaliyo wazi na yaliyojificha yaliyokuwa yanatolewa na wadau wa chama hicho katika kuhakikisha chama hicho kinaibuka ushindi katika Kata hiyo ndiko kulikosababisha Chama cha Chadema kiibuke na ushindi na kuongeza idadi yake ya madiwani na kufikia nane sasa kupitia chama hicho

Siasa za kihuni kwa sasa hazitakiwi zitumike katika chama kikongwe kama Ccm ambacho kimepoteza dira machoni na mioyoni mwa watanzania, hivyo kufanya kampeni dhaifu zilizogubikwa na kwaya, mashairi, ngonjera na lugha zilizokosa staha hakuwezi kukivusha chama hicho katika chaguzi zinazokuja

Katika wimbi kubwa la ufisadi, ukosefu wa ajira kwa vijana, migomo na maandamano ya makundi mbalimbali na kila aina ya uchafu ambao Serikali ya Ccm inatupiwa huwezi kumtegemea hata kwa akili ndogo kiasi gani Lukas Ngongi, Grayson, Juma Kangala na Hamis Abdalah Ally waweze kuleta ushindi kwa mgombea yoyote yule ndani ya chama hicho kinachojichimbia kaburi

Ni watu ambao hawawezi kujenga hoja zenye mantiki katika kuleta ushindi stahiki kwasababu popote wanaposimama hawawezi kuzungumza lugha zenye staha, kueleza mikakati ya ushindi, kujibu hoja kwa mpangilio na kueleza miradi ambayo inatekelezwa na Serikali ya mtaa na hata ya wilaya katika maeneo wanayoishi

Kutokana na tabia zao ambazo zimejaa utata watu wenye akili timamu,hawawezi kushawishika na maneno yaliyojaa dhihaka, matusi katika jukwaa la kampeni walilokuwa wanalitumia watu wa Ccm kumnadi mgombea wake George Oddo na badala yake watu walikuwa wanazibeza kampeni zao kwasababu zimejaa hadithi tupu

Badala ya kujikita kueleza utekelezaji wa miradi mbalimbali uliofanywa na aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo marehemu Said Ally Manya, wao wanahangaika kutoa ahadi au kumshambulia mtu ambaye hana uhusiano na ugumu wa kampeni waliokuwa wanaupata katika kampeni hizo

Kitendo cha uongozi wa Ccm kuwaweka watu hao waliojaa siasa za majitaka ambao walikataliwa kabla ya kuanza na baada ya kumaliza kampeni hizo ndiko kulikosababisha fedheha kubwa kwa wananchi kukataa kushabikia chama hicho wakati wa kampeni zake na mwisho kukataliwa katika uchaguzi huo na kuonyesha uhai mdogo siku za mbeleni na hasa katika uchaguzi mdogo wa Mletele

Hakuna sababu yoyote ya msingi utakayoambiwa na viongozi wa Ccm wilaya ya Songea mjini na wapambe wao kuhusu anguko kubwa tunalolishuhudia hivi sasa kwa wapinzani kuchukua kwa kasi ya ajabu uongozi kuanzia serikali za mitaa na sasa udiwani ambapo madiwani wa upinzania wanaingia kwa kasi kubwa

Washabiki wa chama cha Ccm kila siku wanaendelea kuamia upinzani huku waliobaki huko wakiwa wamekata tamaa kabisa na wengine wakiwasha endiketa ya kutaka kukimbilia chama hicho ambacho kimejaa majungu na siasa za kuviziana kila kukicha

Dizumba na viongozi wenzake wa Ccm wa wilaya na wapambe wao ndio wanaosababisha anguko la chama hicho katika Wilaya ya Songea mjini, hivyo kama kweli wanakitakia mema chama hicho wanapaswa kutambua kuwa utawala wa serikali inayofuata mfumo wa demokrasia, viongozi hawateuliwi bali huchaguliwa na hatma yao ipo mikononi mwa wananchi

Tambo na majigambo yao wanapokuwa kwenye kijiwe cha kisiwa ndui hazitakiacha chama hicho salama hata kidogo kwa sababu watu wengi wana malalamiko na majonzi kwa vitu vya ajabu wanavyovifanya ambavyo vitapelekea Ccm Songea mjini kionekana chama dhaifu cha upinzani kutokana na mwenendo huo

Wanapaswa kutambua kuwa uchaguzi maana yake ni utaratibu wa kuonesha utashi wa kile unachokitaka na usichokitaka, ni tendo la kuchagua kitu au mtu kwa sababu ya sifa nzuri. Ndiyo maana watu hupiga kura kuchagua wawakilishi wao kwenye vikundi mbalimbali vya kijamii,  Halmashauri,bungeni na maeneo mengine

Suala la wagombea kusimama ili wapigiwe kura kamwe haliwezi kuhusishwa na utashi wa kiongozi  kwani wanaohudhuria mikutano ya kampeni ndio wanaopima na kumchagua mtu anayefaa kuwawakilisha katika Halmashauri, bungeni na sehemu zingine kusudiwa

Kampeni ni wakati wa wagombea kunadi sera za vyama vyao kwa wananchi ili wajue ni kina nani, wa chama kipi wanaofaa kupewa ridhaa ya kuwawakilisha halmashauri,bungeni au kwingineko hivyo kuwatumia watu ambao toka wamezaliwa hawajawahi kuongoza hata kikundi cha watu kumi na wakati mwingine kutoa lugha za ovyo ni kutafuta anguko kubwa katika mizania ya siasa.

Chama cha Mapinduzi kinawasemaji wazuri wengi kuanzia ngazi ya shina hadi Wilaya pia kina madiwani, wabunge ambao wanafahamu kuzungumza na wapiga kura , hivyo kinapaswa kiwatumie watu hao kwani ni hazina kubwa, kwa sababu wao kuelezea mazuri ya chama na yale yaliyotekelezwa na Serikali ya chama wanauwezo mkubwa lakini kimewasahau au kuwadharau watu hao badala yake kinawaendekeza wahuni katika kuutafutia ushindi chama.

Wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 watu hao walitumika kukipigia kampeni chama na matokeo yake kata tano zilizopo mjini kabisa kuchukuliwa na Chama cha Chadema na katika uchaguzi huu mdogo uliofanyika hivi karibuni watu hao wametumika tena na kusababisha Kata hiyo ichukuliwe na upinzani.

Katika kampeni hizo zote zilifanywa kinyume cha makusudio yake kwa sababu badala ya wapiga debe kunadi sera za vyama vyao, walijikita zaidi kwenye maisha binafsi ya wagombea na familia zao wakiwachafua na kuwazushia mambo chungu nzima yasiyowahusu wapiga kura.

Waliokwenda shule wameshindwa kuonyesha tofauti na wasiokwenda shule ndio maana tumeona hata wapiga ramli wakiukwaa uongozi na kujidai kuwa uongozi wamepewa na Mungu.


Waimbaji wakichukua jukumu la kuishauri na kuidhibiti serikali. Na matokeo yake tunayaona. Tupo tulipo kwa sababu tumejiweka tulipo na kama hatua madhubuti hazitachukuliwa uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Mletele Manispaa ya Songea yatajitokeza kama yaliyotokea katika uchaguzi wa Lizaboni.


Kwa maneno mengine ninachokisema ni kwamba tunakwama kimaendeleo kwa sababu tunafanya siasa zisizo na akili. Ushahidi wa kauli yangu hii ni kampeni tulizoshuhudia hadi sasa. Tuhuma za kutekwa na kuteswa tumezisikia.tuhuma za rushwa na matusi tumezisikia


Siasa zinazolindwa kwa mtutu wa bunduki haziwezi kuwa siasa zitakazomkomboa mwananchi. Siasa zinazoangalia uwiano wa jinsia badala ya uchangamfu wa ubongo haziwezi kuja na suluhu ya matatizo yetu katika Wilaya ya Songea na mkoa kiujumla


Wakati wengi walioingia katika fani ya siasa wameamua kupumzisha akili zao, wananchi nao wameanza kuwashabikia wanasiasa mithili ya mashabiki wa soka ambao hushabikia timu fulani bila kuwa na sababu za msingi.


Ushabiki wa mpira huwa ni ushabiki kutoka moyoni tu, hakuna mtu anakaa na kufikiria kisha kuamua aipende timu ipi. Ndipo tulipofika na matokeo yake sasa tunayaona na tutaendelea kuyaona.


Matokeo ya ushabiki bila fikra, tumejikuta tuna wanasiasa uchwara wengi na bahati mbaya sana katika fikra zao hizo zilizoshindwa kupevuka wanaendelea kuwa viongozi wetu na wanaoamua mustakabali wa maisha yetu na kesho ya taifa letu.


Siasa za leo kwanza zinaanzia maslahi binafsi, halafu maslahi ya chama na labda ndio yanafuata maslahi ya taifa. Na ushahidi wa hili ni tatizo la rushwa katika chaguzi zetu. Mtu mzima anakubali kumpigia huyu au yule kura kwa sababu yeye amepewa chochote bila kujali ukubwa au thamani ya alichopewa

Nachelea kutoa hitimisho kwamba inabidi tufike mahali tuweke mikakati ya kuwapima uelewa wale wanaotaka nafasi za uongozi katika ngazi zote. Lakini mchawi wa yote ni vyama vya siasa. Vyama hivi vina nafasi nzuri sana ya kuchuja wanaofaa na wasiofaa.

Kutokana na muktadha huo, anguko la Ccm katika uchaguzi wa udiwani wa Lizaboni nililitegemea na kama watashindwa kujirekebisha kutokana na hulka zao basi natarajia anguko kubwa zaidi katika uchaguzi mdogo kata ya Mletele na chaguzi zingine

Mwandishi wa Makala
Anapatikana 0715-335051

Monday, April 2, 2012

CHADEMA YASHINDA UDIWANI MANISPAA YA SONGEA

DIWANI MPYA WA KATA YA LIZABONI (CHADEMA) ALANUS MLONGO

Na Stephano Mango,Songea.

MGOMBEA Udiwani kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Kata ya Lizaboni iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma kwenye Uchaguzi mdogo ameshinda kwa kupata kura 1712 wakati Mgombea wa Chama cha Mapinduzi katika Kata hiyo George Oddo Mbunda alipata kura 1579.

Akitangaza matokeo hayo mara tuu baada ya kumaliza zoezi la uchaguzi lililoanza majira ya saa 1 asubuhi hadi saa 10 jioni Msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa Kata ya Lizaboni Mussa Chiwango alimtangaza Alanus Mlongo wa Chadema kuwa ndiye aliyeshinda katika Uchaguzi huo.

Chiwango ambaye pia ni Afisa Mtendaji wa Kata hiyo alisema kuwa kwenye orodha ya daftari ya kupigia kura inaonyesha kuwa Wananchi waliojiandikisha ni 7825 lakini waliopiga kura ni 3315 jambo ambalo limeonyesha wazi kuwa wakazi wengi wa Kata hiyo hawakuweza kujitokeza kupiga kura.

Kwa upande wake Diwani Mteule wa Kata ya Lizaboni Mlongo mara tuu baada ya kutangazwa kuwa ni mshindi alieleza kuwa nafasi hiyo amepewa na Mwenyezi Mungu hivyo anawajibu mkubwa wa kuangalia changamoto zilizopo kwenye Kata hiyo ambazo zinahitajika zifanyiwe kazi haraka iwezekanavyo.

Alieleza zaidi kuwa mara tuu baada ya kuapishwa kazi yake ya kwanza itakuwa ni kuhakikisha kuwa ana ubana uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ili kumaliza tatizo kubwa lililopo la Miundo mbinu ya barabara,maji na Ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye Shule za Sekondari za Londoni na Mjimwema.

Naye Katibu wa Jimbo la Songea la Chama hicho Masumbuko Paul Masumbuko aliiambia
www.stephanomango.blogspot.com kuwa ushindi walioupata kwenye uchaguzi mdogo kwenye Kata ya Lizaboni ni endiketa kwa Ccm kwamba kila Uchaguzi utakapofanyika kuanzia sasa Chadema lazima washinde kwani mpaka sasa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ina Kata 21 ambapo kati ya hizo Kata sita zina ongozwa na Madiwani wa Chadema.

Alibainisha zaidi kuwa mbinu zilizotumika ambazo zimefanikisha ushindi kwenye Kata ya Lizaboni ndizo mbinu zinazotarajia kufanyika kwenye Kata nyingine ya Mletele ambayo iko wazi tangu Diwani wa Kata hiyo alipofariki dunia miezi 2 iliyopita.
Aidha Masumbuko alisikitishwa na kitendo cha baadhi ya wafuasi wa Ccm ambao walikwenda kwenye maeneo ya kupigia kura huku wakiwa na vitisho lakini kwa vile wafuasi wa Chadema nao walijipanga walifanikisha kukamata gari la kigogo mmoja wa Ccm likiwa limesheheni fimbo ambazo zinahofiwa kuwa zilikuwa zinatakiwa kutumika kwaajili ya kuwapigia wafuasi wa Chadema jambo ambalo liliufanya uongozi wa Chama cha Chadema kumtafuta mmiliki wa hilo gari ambaye hakutaka kutaja jina ili aweze kueleza ni kwanini aliamua kuchukua fimbo kwenye gari lake na kupeleka kwenye eneo la kupigia kura.

Alisema kuwa licha ya mmiliki wa gari hilo kutoa sababu ambazo ni dhaifu kuwa alikuwa amemtuma dereva wake kwenda kijijini kutafuta fito ambazo zingemsaidia kujengea zizi la mbuzi askari Polisi waliokuwakwenye doria waliikamata gari hiyo na kuiondoa kwenye eneo hilo na kufanikisha mpaka uchaguzi unakwisha usalama kwa wapiga kura unakuwepo jambo ambalo amelieleza kuwa jeshi hilo la Polisi linastahili pongezi tofauti na walivyokusudia.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alipoulizwa
www.stephanomango.blogspot.com kuwa katika zoezi zima la uchaguzi mdogo wa Kata ya Lizaboni kama kulikuwepo na tofauti yeyote alisema kuwa Jeshi lake lilijipanga katika maeneo yote ya Kata hiyo kwa kuhakikisha kuwa Vituo vyote vya kupigia kura vinalindwa bila kuwepo vurugu ya aina yeyote na aliongeza kuwa suala la gari kukamatwa likiwa limebeba fimbo Ofisini kwake lilikuwa bado halijamfikia na alidai kuwa inawezekana lilimalizwa na askari wake wa chini ambao waliona hakuna sababu ya msingi ya kuendelea kulishikilia gari.

Mgombea wa Udiwani wa Chama cha Mapinduzi Mbunda alipoulizwa na
www.stephanomango.blogspot.com kuhusiana na zoezi zima la uchaguzi alisema kuwa kubwa zaidi anawashukuru Wakazi wa Lizaboni ambao walionyesha nia ya kutaka awe Diwani wao lakini kwa bahati mbaya kura hazikutosha hivyo amewaomba wawe na subira hadi hapo mambo ya uchaguzi yatakapojitokeza tena.

Mweneykiti wa Umoja wa Vijana wa Ccm (UVCCM) wa Wilaya ya Songea Mjini Victor Ngonyani amesema kuwa kuvunjika koleo sio mwisho wa uhunzi hivyo kushindwa kwa Ccm kwenye uchaguzi mdogo huo wa Udiwani ni changamoto kubwa ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi na Chama cha Mapinduzi ili changamoto kama hizo zisijirudie tena na kwa kuto kuoneana haya kwa Wanachama ambao wanaonekana kuwa ndiyo waliosababisha Ccm kupigwa na Chadema.
MWISHO.

Friday, March 30, 2012

CCM SONGEA YAISHIKA PABAYA CHADEMA KAMPENI ZA UDIWANI MANISPAA YA SONGEA

Hamis Abdala Ally ambaye ni mmoja wa timu mahiri ya kampeni ya Chama cha Mapinduzi Manispaa ya Songea akizungumza kwenye mkutano huo wa kampeni wa kumnadi George Oddo kuwa diwani katika kata ya Lizaboni

Ibrahimu Ngaponda akiwahutubia wananchi wa Madizini kata ya Lizaboni kwa lengo la kuwahamamisha wananchi hao kumchagua George Oddo ili awe Diwani wa Kata ya Lizaboni

Add caption

Mgombea udiwani kupitia Ccm Kata ya Lizaboni George Oddo akiomba kura kwenye moja ya mikutano ya kampeni za udiwani

Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi Manispaa ya Songea Zuberi Mtelela akiwahutubia wananchi wakati wa mkutano wa kampeni za kumnadi George Oddo jana

Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Diwani wa Vitimaalumu Manispaa ya Songea Genfrida Haule akiwaomba wananchi wamchague George Oddo kuwa diwani wa Kata ya Lizaboni



Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Matogoro Charles Mhagama akiwahutubia wananchi wa kata ya Lizaboni kwenye mkutano wa kampeni za Ccm

Meneja Kampeni wa Kata ya Lizaboni Kwinyelesa kulia akimnadi George Oddo kuwa diwani wa Kata hiyo ili aweze kushirikiana na wananchi wa kata hiyo kusukuma mbele gurudumu la maendeleo mbele
Na Stephano Mango, Songea
WANANCHI wa Kata ya Lizaboni Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wametakiwa kuwa makini katika kufanya maamuzi sahihi ya kumchagua Diwani wa Kata hiyo katika uchaguzi unatarajiwa kufanyika aprili mosi mwaka huu kwa kumchagua mgombea wa Chama cha Mapinduzi ili aweze kushirikiana na wananchi katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo
Wito huo umetolewa jana na Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Diwani wa Vitimaalum Manispaa ya Songea Genfrida Haule kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za udiwani kata ya Lizaboni uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Madizini
Haule alisema kuwa Chama cha Mapinduzi kina hazina kubwa ya makada ambao wanaweza kuipeperusha bendera ya chama katika uchaguzi huu wa udiwani lakini kutokana na busara za viongozi wa Ccm na matakwa ya wananchi tumemteua George Oddo aweze kuwatumikia wananchi wa kata hii
Alisema kuwa awali Kata hiyo ilikuwa ina matatizo mengi sana katika sekta ya Afya, elimu, barabara, maji na masoko lakini kutokana na sera nzuri za Ccm kwa kupitia aliyekuwa Diwani wa Kata hii marehemu Said Ali Manya Serikali ya inayoongozwa na Ccm ilikuwa sikivu na ndio maana mnaona maendeleo makubwa katika Kata ya Lizaboni
Alieleza zaidi kuwa kuna baadhi ya kero bado zipo kwenye kata hii hivyo ni vema mkamchagua diwani kupitia tiketi ya Ccm ili aweze kumalizia ahadi na kero ambazo marehemu ally Said Manya aliziorodhesha kwa kuweka mikakati ya utekelezaji ili kuleta mabadiliko zaidi ya kimaendeleo
Naye Hamis Abdala Ally ambaye ni mmoja wa timu mahiri ya kampeni ya Chama cha Mapinduzi alisema kuwa wananchi wanapaswa wazipuuze kelele za wapinzani ambao kwao kuona damu inamwagika katika Kata ya Lizaboni kwao ni ushindi
Ally alisema kuwa Chadema wamekosa sera na umakini katika kampeni zao kwa kushindwa kueleza mambo ambayo yataweza kuwasaidia wananchi badala yao wanaendekeza fujo na matusi huku wakishabikia kwa nguvu ukubwa uvunjifu wa amani katika kata hiyo
“ Nimesikitika sana kuona viongozi wa Chadema wanafurahia kuona kuna kijana amepigwa panga na kujeruhiwa vibaya na ajali ya kugongwa kwa mtoto juzi na kudai kuwa kwa kuwa damu imemwagika sasa ndio dalili ya ushindi kwao jambo ambalo linatia shaka wananchi na kudhani kuwa wao ndio waliopanga uvujaji damu huo” alisema Ally
Alieleza zaidi kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi imefanya mambo mengi toka upatikana uhuru wan chi hii kwa kuwawezesha wananchi kupata barabara safi, maji safi na salama, elimu, afya, masoko, na uwezeshaji wa mitaji ya kiuchumi kwa kuzungumza na taasisi za fedha kupunguza masharti katika mikopo yao kwa wananchi
Alifafanua kuwa kupatikana kwa vitu hivyo ndiko kunakosababisha wananchi wapate ustawi wao na kuchangia kuleta maendeleo kusudiwa kwani watakuwa wamekombolewa kwa kiasi kikubwa sana na kwamba mapungufu mengine yanafanyiwa kazi kwani yanafahamika waziwazi
Alisema kuwa kwa kuwa Serikali iliyopo madarakani ni ya Ccm na iliwekwa na wananchi hivyo kuwasikiliza Chadema kuwa wataleta maendeleo ni uongo mkubwa na kitendo cha kuwapigia kura aprili mosi mwaka huu ni kutupa kura zenu na mtasimamisha maendeleo kwa kipindi kirefu
Alifafanua kuwa nyinyi wenyewe wananchi ni mashahidi hakuna mwaka ambao wananchi wamelima mahindi mengi kama mwaka jana lakini Serikali imeyanunua yote na mengine yanaendelea kupelekwa kwenye hifadhi ya chakula sasa hao wanaosema mbolea imechakachuliwa na kusema Serikali imeshindwa kununua mahindi wanapata wapi ujasiri kama sio kuwadanganya wananchi?
“ Eti Zitto Kabwe anafika nyumbani kwa watu badala ya kuuliza wenyeji, yeye anakurupuka na kusema hapa kuna matatizo ya wizi wa mbolea, mafuta ya jenereta za umeme hivyo ichagueni Chadema ili idhibiti hilo, sasa kama wao wanafahamu kuna wizi kwanini wasiiambie Polisi ili mwizi akamatwe badala yake wanataka udiwani kwani Diwani ni Polisi? Watadhibiti kwa njia gani? Kama sio wao ndio wanaofanya mchezo huo mchafu?”
Alisema kuwa hali ya umeme ni ya uhakika kwasababu kulikuwa na tatizo la kiufundi lakini tayari Shirika la Tanesco limeshafanya kazi yake na umeme unapatikana ambapo wananchi wanaendelea na shughuli zao za kujiingizia kipato ili kuyafikia malengo ya maendeleo
Akizungumza kwenye mkutano huo Katibu wa Siasa na Uenezi wa Ccm Wilaya ya Songea Mjini Zuberi Mtelela alisema kuwa wananchi mpigieni kura Oddo George ili aweze akaungane na madiwani wenzake ili aweze kutimiza ahadi ambazo tuliziahidi wakati wa uchaguzi  mkuu wa mwaka 2010
Mtelela alisema kuwa mkiichagua Chadema licha ya kuwa mtakuwa mmepoteza kura zenu na kusimamisha maendeleo kwa miaka mitatu bali mtakuwa mmeongeza kikundi cha watu wenye fujo kinachoshabikia mambo mabaya kwa jamii ya Manispaa ya Songea
Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya Vijana Mkoa wa Ruvuma Mwajuma Rashid alisema kuwa Chadema wamejipanga kuleta vurugu siku ya uchaguzi na tayari wameanza kuwapiga na kuwatishia viongozi wa Ccm hivyo wananchi mkiwapa kura watu hao mtakuwa mnajenga kizazi cha vurugu na kukwamisha maendeleo yaliyopangwa katika kata ya Lizaboni
Rashid alisema kuwa sisi tumetulia lakini uvumilivu una mwisho wake na endapo mamlaka zinazo husika hazitadhibiti mwenendo huo ambao unahatarisha amani katika uchaguzi huo nasi tunaweza tukatumia nguvu zetu ili wapiga kura na wanachama wa Ccm wawe salama
Naye Mwenyekiti wa Ccm Manispaa ya Songea Hemed Dizumba alisema kuwa kazi kubwa inafanywa na wananchi wa Lizaboni ndio maana Chadema wana haha kwani tayari wenyewe wanajua kuwa ushindi kwao haupo
Dizumba alisema kuwa ushahidi upo wazi kutokana na maneno wanayowasema wenyewe kwasababu hizo mbwembwe walizonazo wameshagundua kuwa zinaletwa na washabiki wao kutoka Bombambili, Majengo, Mjini, Mfaranyaki, Misufini na Ruvuma lakini sisi tunazungumza na watu wa Lizaboni ambao ndio wapiga kura
Kwa upande wake mgombea udiwani kupitia Chama hicho Oddo George alisema kuwa uzuri wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi wananchi mmeuona hivyo hakuna sababu ya kuichagua Chadema katika uchaguzi huo
George alisema kuwa mipango ipo wazi kinachotakiwa ni wananchi kukubari april mosi mwaka huu kuwa inapaswa kuitekelezwa na Chama cha Mapinduzi kupitia Diwani wake ambaye ni mimi hivyo wananchi naomba kura zenu zote ili niweze kuibeba mikoba aliyoiacha marehemu Ally Said Manya mabaye alikuwa Diwani wa kata hii kupitia Ccm
Alisema kuwa kama kweli wananchi wa Kata ya Lizaboni mnaheshimu maendeleo mliosaidiana kuyaleta Kata ya Lizaboni na Marehemu Manya basi msipoteze kura zenu kwa kumchagua mgombea wa Chadema ambaye ameshaonyesha kuwa hana dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo watanzania
MWISHO

TIMU YA MLALE JKT YAMWAGIWA VIFAA VYA MICHEZO

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu
Na Augustino Chindiye, Songea

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu ametoa vifaa vya Michezo kwa timu ya JKT MLALE ambayo ndio timu pekee ya Mkoa huo iliyotinga katika hatua ya Tisa Bora ya Ligi ya Taifa daraja la kwanza.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni Mipira 16, na viatu jozi 25 vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 2.5, zikiwa ni juhudi za serikali ya Mkoa huo kukamirisha maandalizi ya timu hiyo itakayowakilisha Mkoa wa Ruvuma katika Ligi hiyo inayo tarajia kutimua vumbi mwishoni mwa mwezi huu.

Akiongea katika makabidhiano ya msaada huo Mkuu wa mkoa Mwambungu pamoja na mambo mengine ali toa wito kwa wananchi wa Mkoa huo kuunganisha nguvu zao na kuiunga mkono timu yao.

Alisema baada ya timu ya Majimaji kufanya vibaya katika ligi hiyo hivi sasa mkoa wake umeelekeza nguvu katika timu hiyo wakiwa na matumaini kuwa timu hiyo ita watoa kwa kuujengea heshima mkoa Mkoa wa Ruvuma

Nao viongozi wa timu ya JKT Mlale na Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoani hapa (FARU) Joseph Mapunda na mwakilishi wa Kikosi cha Mlale Isack Kusimbwa pamoja na neno la shukiurani kwa msaada huo walimuahidi Mkuu wa Mkoa kuwa watahakikisha timu hiyo inatinga ligi kuu.

Walisema msaada huo umefika wakati muafaka na wakaahidi kufikisha vifaa hivyo kwa walengwa pamoja na salamu zake kwa wachezaji wote na wakatumia nafasi hiyo kumkaribisha kiongozi huyo kushiriki katika michezo hiyo ili aweze kujionea kazi ya vijana wake.
Mwisho

Thursday, March 29, 2012

WAKULIMA WA KOROSHO TUNDURU BADO HAWAJALIPWA MADAI YAO LICHA YA SERIKALI KUTOA AGIZO

       Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Madaha
Na Augustino Chindiye, Tunduru

WAKATI kukiwa na maelekezo kutoka Serikani kuwa mabenki yatoe fedha zitakazotumika kuwalipa malipo ya pili, pamoja na kulipia korosho ilizo kopwa kutoka kwa wakulima wa zao hilo wakulima wa wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma malipo hayo bado hayajaanza  kutolewa.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Chama kikuu cha Ushirika wa wakulima wilayani Tunduru (TAMCU) Imani Kalembo alipotakiwa kuzungumzia utekelezaji wa agizo hilo kutoka serikalini.

Akifafanuaa taarifa hiyo Bw. Kalembo alisema kuwa malipo hayo yameendelea kukwama kutokana na majibu ya viongozi wa Benki ya NMB tawi la Tunduru waliodai kuwa bado hawajapokea maelekezo kutoka makao yao makuu juu ya kuanza kutoa fedha hizo zitakazotumika wakati wa malipo hayo.

Katika taarifa hiyo Kalembo alisema kuwa jumla ya tani 4800 zimekwama katika maghala na kusababisha malipo kwa wakulima wa Korosho wilayani humo kushindwa kutolewa ni sehemu ya tani 7000 zilizozalishwa Msimu wa mwaka 2011/2012.

Alisema katika msimu huu Wilaya hiyo ilibahatika kuuza katika mnada mmoja tu kati ya minada 9. ambapo iliuza tani kama 1100 na kwamba hayo ilitokana na wanunuzi wakubwa kukataa kununua korosho hizo kwa bei ya shilingi 1480 kwa kilo moja  waliyoitaka wakulima hao wakiwa wanashinikiza wanunue kwa chini ya shilingi 1400.

Kufuatia hali hiyo baadhi ya vyama vya msingi vya ushirika vya wakulima wa wilaya hiyo vimepata changamoto ya baadhi ya wakulima wake kuondoa korosho maghalani na kuanza kuuza korosho zao kwa walanguzi ambao hutumia kipimo halamu kiitwacho KANGOMBA yaani bakuli linalobeba kilo 2 linanunuliwa kwa shilingi 600.

Akizungumzia hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Madaha pamoja na kuipongeza serikali kwa kutoa tamko hilo alisema kuwa ofisi ya kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa huo zikiwa ni juhudi zaa kuhakikisha kuwa malipo hayo yatolewe kwa haraka.
Mwisho

MKURUGENZI WA WILAYA YA NAMTUMBO MKOANI RUVUMA ATISHIWA KUUAWA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda
Na Stephano Mango, Songea
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linawasaka watu wasiofahamika wanaodaiwa kumtishia kumuua Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Mussa Zungiza(56) ambaye inadaiwa kuwa alitumiwa ujumbe wa maandishi kwenye simu yake ya mkononi akitishiwa kuuawa  .
Akizungumza na www.stephanomango.blogspot.com  jana mchana ofisini kwake Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Michael Kamhanda alisema kuwa tukio hilo lilitokea machi 25 mwaka huu majira ya saa za mchana huko katika wilaya ya Namtumbo .
Kamanda Kamhanda alieleza zaidi kuwa inadaiwa mnamo siku tofauti za mwezi machi mwaka huu huko katika wilaya ya Namtumbo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri  ya wilaya hiyo Zungiza alipokea ujumbe wa maandishi kupitia kwenye simu yake ya mkononi akitishiwa kuuawa. 
Alibainisha zaidi kuwa kwenye simu hiyo ya mkononi ujumbe huo ulitoka  katika namba  mbalimbali za simu,ambapo ujumbe wa kwanza ulitumwa machi 14 mwaka huu  majira ya saa 1:46 asubuhi na ujumbe wa pili ulitumwa  mach 14 mwaka huu majira ya saa 4:08 usiku .
Alieleza zaidi kuwa ujumbe huo ulieleza kuwa siku yoyote Zungiza atauawa kwa njia ya aina yoyote na kutoeleza chanzo au sababu ya kutaka kumuuwa ,jambo ambalo lilimpa hofu kubwa juu ya maisha yake .
Kamanda Kamhanda alisema kuwa Mkurugenzi Mtendaji huyo Zungiza  baada ya kupokea ujumbe huo kupitia kwenye simu yake ya mkononi  hatua ya kwanza alichukua ya kuwasiliana na kamati ya ulinzi ya wilaya hiyo na kisha alitoa taarifa juu ya ujumbe huo aliotumiwa wa vitisho katika kituo cha polisi cha wilaya ya Namtumbo ambako lilifunguliwa jalada la uchunguzi .
Hata hivyo kamanda Kamhanda alisema kuwa jeshi la polisi mkoani Ruvuma  linaendelea na upelelezi zaidi wa kina kuhusiana na tukio hilo ili kuwabaini watu waliohusika kumwandikia ujumbe kupitia simu yake ya mkononi ambao ulimtishia kumuuwa Zungiza.
 MWISHO

AKAMATWA NA POLISI BAADA YA KUMZIKA MWANAE KICHANGA MAMA AKIWA HAI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda

NA GIDEON MWAKANOSYA ,SONGEA
JESHI la polisi mkoani Ruvuma limemtia mbaroni Anna Mhenga (25) mkazi wa Bombambili katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kumtupa mtoto wake mwenye umri wa siku moja  kwenye eneo la msitu wa milima ya Chandamali ambako alichimba shimo na kumfukia .
Habari zilizopatikana jana mjini Songea ambazo zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Michael Kamhanda zilisema kuwa tukio hilo lilitokea machi 24 mwaka huu majira ya saa za mchana huko katika eneo la msitu wa Chandamali uliopo katika Manispaa ya Songea.
Kamanda Kamhanda alisema inadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio Anna alijifungua mtoto wa jinsia ya kike kisha aliondoka eneo la nyumbani kwake na alielekea kwenye eneo la msitu mkubwa wa miti wa Chandamali ambako aliamua kuchimba shimo na kukifukia kichanga alichotoka kujifungua .
Alifafanua kuwa inadaiwa kuwa Anna alijifungua mtoto huyo akiwa na ujauzito wa miezi 7 kisha alifikia uamuzi wa kumtupa mtoto wake kwa kumfukia  jambo ambalo liliwafanya majirani wamshitukie ambapo mmoja kati yao ambaye ndiye raia mwema alitoa taarifa katika kituo kikuu cha Polisi cha Songea.
Alieleza zaidi kuwa Polisi baada ya kupata taarifa ya tukio hilo walifanikiwa kumkamata Anna ambapo katika mahojiano ya awali mtuhumiwa alikataa kuhusika na tukio hilo na baada ya upelelezi zaidi wa Polisi alikiri kuwa ni kweli alikuwa na ujauzito .
Alifafanua zaidi kuwa machi 26 mwaka huu majira ya saa za asubuhi  mtuhumiwa Anna alipelekwa kwenye Hospitali ya Serikali ya mkoa Songea kupimwa ambako ilibainika kuwa mazingira yote yalionyesha kuwa mtuhumiwa alitokakujifungua .
Alieleza zaidi kuwa Polisi baadaye waliendelea kumhoji na alikubali kuwa ni kweli alijifungua mtoto wa jinsia ya kike ambaye alidai kuwa amemzika kwenye msitu mkubwa wa miti uliopo eneo la Chandamali .
Kamanda Kamhanda alibainisha zaidi kuwa inadaiwa mtuhumiwa baadaye aliwapeleka askari Polisi kwenye msitu wa Chandamali ambako aliwaonyesha mahali alipomfukia mtoto huyo ambapo walichukua jukumu la kufukua eneo hilo na kukuta maiti ya kichanga ikiwa ndani ya shimo.
Alisema kuwa maiti ya kichanga huyo baadaye ilichukuliwa na kupelekwa kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo katika hospitali ya Serikali ya mkoa Songea na Polisi bado inaendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo .
MWISHO

Wednesday, March 28, 2012

DKT EMMANUEL NCHIMBI MBUNGE WA SONGEA MJINI NA WAZIRI WA HABARI UTAMADUNI NA MICHEZO ATINGA KAMPENI ZA UDIWANI KATA YA LIZABONI MANISPAA YA SONGEA

 Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Dkt Emmanuel Nchimbi akimnadi mgombea wa Udiwani wa Kata ya Lizaboni, Manispaa ya Songea kupitia CCM  George Oddo aliyesimama kushoto kwenye mkutano uliofanyika kwenye ofisi za CCM kata ya Lizaboni jana
 Mamia ya wananchi wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Dkt Emmanuel Nchimbi akimnadi mgombea wa Udiwani wa Kata ya Lizaboni, Manispaa ya Songea kupitia CCM  George Oddo kwenye mkutano uliofanyika kwenye ofisi za CCM kata ya Lizaboni jana
Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Dkt Emmanuel Nchimbi akimnadi mgombea wa Udiwani wa Kata ya Lizaboni, Manispaa ya Songea kupitia CCM  George Oddo kwenye mkutano uliofanyika kwenye ofisi za CCM kata ya Lizaboni jana

Monday, March 26, 2012

KONGANO BUNIFU ZINA MCHANGO KATIKA KUKUZA UCHUMI WA NCHI


 Aliyekuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa mafunzo ya Wawezeshaji Kongano Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya( MB) akimkabidhi Cheti cha kuhitimu mafunzo hayo mmiliki wa mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com ,Stephano Mango,wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume Sayansi na Teknolojia Dkt Dugushilu Mafunda. wa kwanza kutoka kulia ni Wawezeshaji wa mafunzo hayo Dkt Flower Msuya na Mhandisi Peter Chisano


Mgeni rasmi aliyefunga mafunzo hayo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya (MB) akiwa kwenye picha ya pamoja naViongozi wa Tume ya Sayansi na Teknologia na washiriki wa mafunzo ya Wawezeshaji Kongano Tanzania yaliyofanyika Ukumbi wa The Beach Comber Hotel kuanzia Februari 27 hadi machi 1, 2012
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
HAKUNA ubishi kuwa umaskini nchini Tanzania umebaki kuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya nchini yetu ingawa pia Tanzania ina matajiri wakubwa wachache na maskini wengi.
Kwa mtazamo wangu mtu maskini ni yule asiye na uchaguzi kwenye chakula, hawezi kuyakataa magonjwa wala ujinga katika maisha yake kwani kwake kila kitu ni kigumu na amekuwa sugu katika hali hiyo
Umaskini nchini umeota mizizi wanaishi kwa kipato duni sana kwani wengi wanaishi chini ya dola moja ya marekani kwa siku, umaskini upo mijini na vijijini watu wanatia huruma ukiwaona kutokana na ugumu wa maisha kutokana na sababu mbalimbali
Ikiwemo ya viongozi wetu wengi wanashindwa  kutambua na kuifungua mifumo ya kiuchumi, kisiasa na hata kijamii ili kuwawezesha wananchi kwa wingi wao ili wawe washiriki na wadau muhimu katika kumiliki uchumi wao
Watanzania wengi kushindwa kuwa na maamuzi juu ya mustakabali wa Taifa lao leo na kesho kunaendelea  kuwafanya wageni kutumia vibaya rasilimali tulizojaliwa kuwa nazo
Ni wazi kuwa watanzania tuna rasilimali za kutosha ambazo zinaweza kutukwamua kwenye tope zito la umaskini lakini hatujaweza kuzitumia vizuri na mbaya zaidi tumewaachia wageni ndio wamiliki na kuzitumia kwa ujeuri rasilimali zetu kwa muavuli wa uwekezaji
Hali hiyo inatufanya tuendelee kuwa maskini wa kutupwa na kujenga utamaduni mpya wa utegemezi kwa mataifa ambayo tumewaachia wachume mali zetu na kukimbizia huko kwao
Taifa letu, leo limekuwa na watu tegemezi kuanzia ngazi ya mtu binafsi, kaya, jamii, na hata Taifa, swali la kujiuliza sasa ni je tu wategemezi kwa kiasi gani na je, miaka 50 ijayo tunataka tuwe na Taifa la aina gani?
Utegemezi sio jambo zuri kwani unapunguza uhuru wetu, unatukosesha thamani, tunakosa sauti ya kimaamuzi na unatufanya tuwe wadogo mbele ya wahisani au wafadhiri tunaowategemea
Katika makala haya, nakusudia kujadili jambo chanya la kongano bunifu kama ishara ya kufanya mageuzi ya kiuchumi na kuondoa dhana ya utegemezi kama Taifa na jamii kiujumla kwani katika nchi nyingine jambo hili limesaidia kuinua na kuimarisha uchumi wao
Kongano bunifu zipo nyingi nchini ambazo ili ziweze kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika ngazi ya kijamii hadi kitaifa zinahitaji kuunganika ili ziwe na nguvu ya pamoja katika soko la bidhaa kwa kushirikiana na  sekta binafsi, serikali na wanataaluma katika kongano mahsusi kwenye maeneo mbali mbali hapa nchini kwetu.
Katika nchi nyingi ushirikiano huu umekuwa kichocheo kikubwa cha  ubunifu  ambao husaidia katika kutoa bidhaa zenye viwango na sifa zinazoweza kuhimili ushindani ndani na nje ya nchi kwa malengo kusudiwa
Kongano bunifu zina uwezo mkubwa wa kupunguza umaskini na kutoa nafasi nyingi za kazi kwa jamii pia vilevile Kongano hizi huleta mahusiano ya karibu sana kati ya wanachama wa kongano na wadau wengine wa maendeleo kama vile  wanataaluma, sekta binafsi na serikali.
Wengi wanaweza kushangaa neno kongano bunifu kwani inawezekana halijazoeleka masikioni mwa watu wengi, ili niweze kuwatendea haki wasomaji na wananchi nieleze kidogo maana ya neno hilo
Kongano bunifu ni muunganiko wa shughuli za aina moja za wajasiliamali wenye malengo sawa na wanaofanya kazi katika eneo/ wilaya, mkoa na Taifa moja katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika shughuli yao
Mfano ni wachongaji vinyago, wahunzi, wakulima wa uyoga, mwani, alizeti, mahindi, maharage, ufuta mpunga, wavuvi, wafugaji kuku, watengenezaji batiki, wasindikaji wa mazao, wafugaji wa wanyama mbalimbali, wavuvi na vikundi vya wajasiliamali kama hao
Wajasiliamali wanaojishughulisha na ufugaji wa kuku katika wilaya nzima wanaweza wakatengeneza jukwaa lao(kongano bunifu) litakalokuwa linajadili namna bora ya kuimarisha ufugaji wa kuku ,soko, mitaji, changamoto nyingine zinazowakabili katika kufikia hali stahiki, hiyo ndiyo maana ya kongano bunifu
Kwa kutambua umuhimu wa kongano bunifu katika kuleta uchumi imara wa jamii na Taifa, kuanzia februari 27 hadi machi 1, mwaka huu wa 2012 Tume ya Sayansi na Teknolojia nchini iliweza kutoa mafunzo kwa wawezeshaji kongano katika ukumbi wa The beach Comber, jijini Dar es Salaam
Washiriki wa mafunzo hayo walitoka Tanzania bara na Visiwani ambapo jumla ya washiriki 46 kutoka kwenye kongano 26 nchini walifanikiwa kupata mafunzo hayo muhimu yenye lengo la kukuza kukuza uwezo wao katika kuhamasisha na kuanzisha ushirikiano kati ya sekta binafsi, serikali na wanataaluma katika kongano mahsusi kwenye maeneo mbali mbali hapa nchini kwetu.
Ili washiriki waweze kupata ujuzi wa kuweza kuimarisha kongano ambazo ziko katika mazingira wanakofanyia kazi ili kukuza mkakati wa kuongeza Ubunifu na Ushindani wa  sekta binafsi kupitia kongano bunifu kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini
Wawezeshaji wa mafunzo hayo walikuwa watanzania ambao ndio wamekuwa wawezeshaji katika nchi za Nigeria, Msumbiji, Ghana, Senegal, Tanzania na Kenya ambao ni Dkt Flower Msuya, Sostenes Sambua na Peter Chisano
Washiriki wa mafunzo hayo waliweza kutoa elimu stahiki ya kuimarisha kongano bunifu katika katika maeneo ambayo washiriki wanatoka ili ziweze kuwa na nguvu moja katika kufanya wazalishaji watengeneze bidhaa bora zenye kukidhi ushindani katika masoko ya ndani na nje.
Kutokana na hilo na kila mmoja akatimiza wajibu wake tuna kila sababu ya kuongoza bara zima la Afrika katika kuonyesha umuhimu wa Kongano bunifu jinsi zilivyoweza kusaidia katika kuongeza pato la taifa, ajira na maendeleo ya jamii , uchumi, ubunifu na Ushindani wa Taifa katika masoko ya nje
Ni vema sasa nchi ikaanza kuendeleza dhana ya kongano bunifu kama njia ya kufikia maendeleo ya kiuchumi nchini kwa kushirikisha wajasiliamali kutumia vema fursa zilizopo za maliasili zetu ili ziwe nguzo kubwa katika kufikia lengo stahiki
Kuanza upya kimtazamo ni fursa ya kubadilika na kuchukua mambo mazuri mapya ambayo kutoka kwa wengine au pale yanapopatikana hata ndani yetu kutasababisha kutuondoa kwenye utegemezi wa kiuchumi na kuondokana na umasikini uliokithili nchini
Kesho ya Tanzania hatuwezi kuongelea bila leo na kila tunachopanda leo ndicho tunachovuna kesho, hivyo msingi wa leo tuliujenga jana uwe mbovu au mzuri pia kwa sababu leo ipo kwa sababu ya kesho ipo na jana ilikuwepo basi leo tunapaswa kubadilika ili tuijenge vyema kesho yenye neema
Leo tukianza upya basi kesho tutazaliwa upya na tukizaliwa upya ndipo hapo tunapopaswa kuwa , hivyo kujifunza na kuanza upya ni ujasiri na ni njia ya kuleta mabadiliko katika dunia ya leo bila kujali gharama za kufanya hivyo
Tuanze upya kwa kuwa wajasiriamali mahiri chini ya kongano bunifu kwani ujasiriamali ni ile hali, uwezo na mkakati au mchakato wa kubuni, kuanzisha, kuendesha na kumudu shughuli halali ya maendeleo ya kiuchumi
Tunahitaji ujasiliamali wa kujiamini, kuthubutu, kubuni na kuendeleza zao tokeo la ubunifu huo kwa kuleta faida chanya katika maisha yake, jamii na Taifa kiujumla kwani ujasiliamali ni nguzo muhimu kwa uchumi wa kisasa wa karne ya 21
Dhana ya ujasiliamali inatimia endapo hali ya kugundua au kubuni biashara mpya au kuiendeleza ile ya zamani kwa ajili ya kuwekeza na kutoa huduma stahiki kwa jamii pana, hivyo tuamue sasa kuwa katika hali hiyo katika jukwaa la dunia ili kuzifaidi fursa za uchumi za ndani na nje ya nchi
Uchumi wa dunia umebadilika, uchumi wa soko katika utandawazi ndio unashikilia mfumo wa kiuchumi wa dunia ili kuharakisha maendeleo kwa kutoa ajira mbadala kwa kujiajili, kujitegemea na kujenga uwezo wa kujiamini katika maisha na biashara kubwa dhana ya ujasiliamali chini ya kongano bunifu inahitajika
Wahenga walisema huwezi kuzuia sikio lako kusikia lakini unaweza kuzuia mdomo wako usiseme, nami kwa hakika nasema nauzuia mkono wangu usiandike zaidi lakini siwezi kukuzuia msomaji kuendelea kusoma
Mwandishi wa Makala
Anapatikana 0715-335051
www.stephanomango.blogspot.com