Sunday, April 21, 2013
KIBANDA AMPONZA WASSIRA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira
Na Josephat Isango,Dar
KAULI ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira kudai kuwa Idara ya Usalama wa Taifa haiwezi kumtesa Kibanda kwa kuwa hana umaarufu kisiasa nchini, imeibua mjadala mkali, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Juzi wakati akihitimisha hoja ya hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/ 2014, Wassira aliitetea Idara ya Usalama wa Taifa dhidi ya tuhuma zinazowahusu baadhi ya watendaji wake kuhusika katika matukio kadhaa ya utekeji na utesaji wa raia.
Wassira alisema haiwezekani kwa watumishi wa idara hiyo kujihusisha na matukio hayo na kueleza mafanikio mbalimbali ambayo imeliletea taifa.
Alihoji sababu za kulihusisha tukio la kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Absalom Kibanda na idara hiyo na kuhoji; ‘kwani yeye ni nani?’
Katika kuali hiyo ambayo imeibua mjadala, Wassira alisema haiwezekani idara hiyo ikahusika kwa kuwa Kibanda hana umaarufu katika siasa za Tanzania, na kwamba labda wangekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa angeelewa.
Kibanda alivamiwa akiingia nyumbani kwake Mbezi Juu jijini Dar es Salaam usiku wa Machi 6 mwaka huu na watu wasiojulikana, na kushambuliwa vibaya kwa kupigwa nondo kichwani, kutobolewa jicho la kushoto, kung’olewa ukucha, meno mawili na kukatwa kidole.
Kauli ya Wassira imepokelewa kwa mtazamo hasi na watu mbalimbali katika jamii, huku wengi wakisema kuwa hiyo ni ishara kwamba chombo hicho kinahusika na vitendo hivyo, lakini kwa kundi fulani la watu.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, mwanasheria maarufu nchini, Mabere Marando alisema mjadala huo unatokana na hoja aliyoanzisha yeye ya kuwataja watu wa Usalama wa Taifa kuwa wanahusishwa na utekaji na utesaji.
Marando ambaye pia ni ofisa wa zamani wa idara hiyo, alifafanua kuwa ni vema Wassira ashauri sera za Idara ya Usalama zifanyiwe mabadiliko, waache kulinda heshima ya chama badala yake walinde taifa.
“Kazi za usalama ni kugundua mapema na kutoa taarifa habari zinazohusu serikali kupinduliwa, kusaidia serikali katika ujasusi wa uchumi ili nchi iendelee na mwisho kabisa ni kushauri serikali kuhusu hali ya kisiasa nchini. Wala sio kupambana na wanasiasa au waandishi wa habari,” alisema.
Marando aliongeza kuwa Usalama wa Taifa sasa unafanya kazi za usalama wa raia ambazo ni za polisi kimsingi. Kwamba Usalama wa Taifa huwa hawakamati, lakini siku hizi wanakamata.
“Sasa kama hawa wakifanya hivi polisi watafanya kazi gani? Tunashindwa kutofautisha kazi za usalama wa taifa na usalama wa raia,” alisema.
Katibu wa TEF, Neville Meena alisema kuwa Wassira ni kielelezo cha ulevi wa madaraka. Anaona kuwa wanasiasa ndio watu zaidi kuliko wengine.
Alisema kwa kauli ile pengine ndiyo maana uchunguzi wa suala la Kibanda haufanyiki wala hakuna taarifa rasmi ya polisi iliyotolewa tangu atekwe na kuteswa.
“Tunafurahi kwa kuwa tumepata mawazo ya watawala na kauli ya Waziri huyu wa Nchi, Ofisi ya Rais pengine ndiyo msimamo wa serikali maana alisema bungeni.
“Huyu anatoka Ofisi ya Rais, tena anashughulikia mahusiano. Anapotoa kauli hii zikiwa zimefika siku 45 tangu Kibanda atekwe na kuteswa, mauaji au mateso kama hayo hayataisha katika nchi kwa kuwa sisi wengine sio watu kwa mujibu wa Wassira. Kauli hii ni mbaya na haina afya,” alisema Meena.
Mwandishi nguli wa habari nchini na mshauri wa masuala ya habari, Ndimara Tegambwage alisema; “Kwanza tunafurahi kwa kuwa Wassira amethibitisha kuwa wana usalama wanawaandama watu na mara zingine kuwadhuru viongozi wakubwa hasa wasiofuata au kukubaliana na sera zao.
“Pili, kwa mujibu wa Wassira kwa sasa Watanzania tunajua kuwa baya lolote likimpata Dk. Slaa au Mbowe litakuwa limetekelezwa na watu wa usalama.”
Ndimara aliongeza kuwa kwa kauli ya Wassira kusema kuwa Idara ya Usalama inashughulikia wanasiasa maarufu, ameivua nguo idara hiyo na wangetarajia idara hiyo imwajibishe kwa kutoa siri za Usalama wa Taifa.
“Linapokuja suala la haki za binadamu hakuna mdogo au mkubwa, hakuna rais au mama ntilie. Hakuna aliye mdogo asiyehusiana na mkubwa, ikifikia hatua ya dharau ya aina hii tunashindwa kumwelewa waziri huyu,” alisema.
Mkurugenzi wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotetea haki za binadamu, Onesmo Olengurumwa alisema Wassira amethibitisha kuwa kumbe Usalama wa Taifa kuna watu wanawateka na kuna wengine hawatekwi.
“Tunashukuru kwa kusema kuwa kuna kundi fulani linawindwa, ni dharau sana kwa kauli ile kwa kuwa Kibanda ni Mtanzania, awe na cheo asiwe na cheo, awe mwanasiasa au sio mwanasiasa serikali inapaswa kumlinda.
“Kauli ya Wassira inaleta matabaka, inaonesha wengine wana thamani zaidi, wengine hawana thamani,” aliema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana alizungumza kwa kifupi akisema; “hiyo kauli haikupimwa, sio kauli iliyotarajiwa kutoka kwa kiongozi wa CCM. Kweli hakutumia busara katika kutamka kauli hii tena bungeni.”
Saturday, April 20, 2013
VIBAKA WAUA ASKARI POLISI KAHAMA
Na Ali Lityawi, Kahama
ASKARI polisi wa kitengo cha usalama barabarani, wilayani Kahama, Salum Mtepa, ameuawa usiku wa kuamkia jana na watu wanaosadikiwa kuwa ni vibaka kutoka machimbo madogo ya dhahabu ya Nyangarata na Mwime, baada ya kumpiga na kitu kizito kifuani.
Tukio hilo lilitokea nyumbani kwake eneo la kata ya Majengo mjini Kahama usiku wa kuamkia jana baada ya watu hao wanaokadiriwa kuwa wanne kwenda nyumbani kwa askari huyo mwenye cheo cha Staff Sajenti na kuvunja kibanda cha biashara kwa lengo la kuiba ndipo askari huyo alipotoka nje kwenda kupambana nao.
Inadaiwa kuwa baada ya kutoka nje vibaka hao waliokuwa na pikipiki, watatu kati yao walikimbia akabaki mmoja aliyekuwa na kifaa ambacho hutumiwa na wachimbaji wa dhahabu katika machimbo madogo madogo kwa ajili ya kuvunjia miamba ya mawe ambacho hujulikana kwa jina la Moko.
Kwa mujibu wa taarifa ya mkuu wa polisi wilaya ya Kahama, George Simba, askari huyo alipigwa na kifaa hicho kifuani wakati akijaribu kupambana na kibaka huyo, hali iliyosababisha avuje damu nyingi ndani ya kifua na kusababisha kifo chake.
Simba alisema hali ya vibaka katika mji wa Kahama ni mbaya kwani wameongezeka kutokana na machimbo ya Nyangarata kujaa maji na Mwime kuisha uzalishaji wake, hali iliyofanya vijana wengi kutoka kwenye maeneo hayo kutokuwa na fedha.
Alisema hivi sasa wimbi la vibaka hao limekuwa tishio huku akiahidi kupambana nao pia kuwasaka kwa nguvu zote waliohusika na kifo cha askari huyo wa usalama barabarani, ingawa hadi jana hakuna mtu yeyote aliyekuwa amekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Friday, April 19, 2013
ZAO LA UFUTA KUBADILI MAISHA YA WAKULIMA MKOA WA PWANI
Miongoni mwa wakulima wa ZAO la ufuta waliopo mkoani Ruvuma wakiwa kwenye Picha ya Pamoja
Na Stephano Mango
UFUTA ni zao lisilotiliwa maanani na wakulima wengi nchini kwa miaka mingi pamoja na uwingi wa faida zake kwa binadamu, lakini kwa miaka ya hivi karibuni, takribani sehamu zote ambako hali ya hewa imekuwa rafiki wa kulistawisha zao hilo, wakulima wameligeukia na kuanza kulima kwa kasi.
Zao la ufuta linatabiriwa kuwa zao kuu mbadala la kibiashara mkoani Pwani kutokana na mahitaji ya soko kuwa makubwa kwa sasa likifuatiwa na Muhogo pamoja na Embe.
Wilaya ya Rufiji ni mojawapo ya wilaya ambazo zinastawisha zao la ufuta kwa siku nyingi na siku za hivi karibuni kasi ya uzalishaji imeongezeka kutokana na upatikanaji wa uhakika wa soko la ufuta.
Katika msimu wa mwaka 2010 mpaka 2011, kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya hiyo Nurdin Babu. zao la ufuta liliiingizia mapato halimashauri ya wilaya ya Rufiji kiasi cha shilingi milioni sitini (60,000,000/=), hivyo kuongoza katika kuiingizia halimashauri mapato kupitia vyanzo vyake vya mapato
Hata hivyo, Mkuu wa wilaya hiyo alisema kuwa ni lazima kujiwekea malengo ya kuzalisha walau kwa kuanzia tani elfu tano (5000) katika msimu ujao wa kilimo 2012/2013 kutoka tani za sasa 400 kwa mwaka na tani 280 mwaka 2005/06.
Utafiti uliofanywa na jarida la “MUVI – Nuru ya Mafanikio” umebaini kuwa tofauti na mazao mengine ya kibiashara yanayolimwa mkoa wa Pwani kama vile Embe, Nanasi na Muhogo ni kuwa zao la ufuta hususani wilayani Rufiji wanunuzi hununua likiwa bado shambani na kulipa pesa pale linapoanza kuvunwa na mteja ndiye anayepanga bei na sio mnunuzi.
Hali ya soko kwa zao la ufuta ni kuwa bei ya kilo moja ya ufuta imepanda toka Tshs500/= mwaka 2000 hadi Tshs 1500/= mwaka huu 2012 kwa kilo, na hivyo kuchochea uzalishaji wa zao la ufuta kwa wakulima, anaeleza mkufunzi wa mafunzo na Afisa Mazao wa Wilaya ya Rufiji Ndugu Bahinga.
Kwa mujibu wa tafiti iliyofanywa na Dkt.Elly Kafriti, kutoka katika kituo cha utafiti Naliendele mkoani Mtwara katika mazao ya mbegu za mafuta,zao la ufuta linaongoza kwa kulipatia taifa fedha nyingi za kigeni.Mwaka 2005 taifa lilipata zaidi ya shilingi bilioni 20 kutokana na mauzo ya tani 32,000 za ufuta nje ya nchi.
Nchini Tanzania zaidi ya asilimia 75% ya ufuta hulimwa katika mikoa ya kusini ya Mtwara, Lindi na Ruvuma na katika mikoa hiyo ufuta ni zao la Pili la biashara baada ya Korosho. Mikoa mingine ni Tanga,Pwani na Morogoro.
Katika wilaya ya Rufiji Ufuta hulimwa ukanda wa juu yaani tarafa za kibiti,Kikale,Mohoro na Ukanda wa tambalale tarafa za Mkongo na Ikwiriri.
Inafahamika wazi kuwa mradi wa MUVI ni wa miaka saba (7) uliibuliwa na Serikali kupitia wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko ambao unatekelezwa kwa mkopo wa Serikali toka Shirika la IFAD ambapo SIDO inatekeleza mradi huu kwa niaba ya Serikali ya Tanzania.
Madhumuni ya mradi ni kumwezesha mjasiriamali mdogo wa kijijini awe mkulima, mfanyabiashara, msindikaji vyakula n.k ili aweze kujiongezea kipato katika shughuli zake na kupunguza umasikini. Hivyo basi mradi wa MUVI unalenga kutoa ajira kwa vijana toka familia masikini vijijini.
Ili kufanikisha hilo Afrikan Image imepewa jukumu la kusimamia utoaji huduma ya mawasiliano ya kibiashara vijijini kwa wajasiriamali wadogowadogo katika mikoa sita na Pwani ikiwemo.
Njia mbalimbali zimekuwa zikitumika kama kutengeneza na kurusha vipindi mbalimbali vya radio, kutengeneza machapisho mbalimbali, mbao za matangazo vijijini, taarifa za bei za mazao kwa njia ya simu na mtandao wa MUVI kwa lugha ya Kiswahili ili kuwezesha mawasiliano ya kibiashara kufanikiwa vijijini.
Hadi robo ya pili ya mwaka wa tatu wa uhai wa mradi, jumla ya vikundi 90 vya wajasiriamali vimefikiwa, wanaume wakiwa 803 na wanawake 775, machapisho mbalimbali yanayofikia zaidi ya 50 elfu yakiwemo ya maembe, mananasi, jarida la muvi, kalenda, alizeti, muhogo na mwongozo wa namna ya kutumia ubao wa matangazo kwa wajasiriamali vijijini,
Kwa kipindi cha miaka miwili ya uhai wa mradi katika wilaya tatu za mkoa wa Pwani, Mkuranga, Bagamoyo na Rufiji yamesambazwa vijijini na kutoa mchango mkubwa katika kubadili mazoea ya wakulima na hivyo kuongeza tija katika kilimo.
Afrikan Image wanatarajia kuzindua huduma ya mawasiliano kwa njia ya ujumbe mfupi ili kupata taarifa za masoko kwa mazao mbalimbali pamoja na kuanza kurusha vipindi vya radio ifikapo katika ya mwezi machi mwaka huu.
Ili kuweza kuongeza chachu ya ustawishaji wa zao hilo Serikali kupitia wizara ya viwanda, biashara na masoko, chini ya mradi wa MUVI mkoa wa Pwani, hivi karibuni waliendesha mafunzo kwa maafisa ugani ishirini (20) kutoka Kata mbali mbali za Wilaya ya Rufiji ambapo wamepatiwa mafunzo maalum ya kilimo bora cha zao la ufuta.
Mafunzo kwa maafisa ugani wa Kata na Vijiji ni muhimu katika kuleta ufanisi katika utekelzaji wa shughuli za kitaaluma kwa walengwa. Mradi umebaini ya kwamba kutoa mafunzo ya namna hii kutasaidia kueneza taaaluma ya kilimo bora kwa wakulima wadogo wadogo kwa urahisi kwa sababu maafisa ugani wanaishi pamoja na walengwa kila siku.
Ni rahisi kufikisha ujumbe kuliko kungoja taarifa za taaluma kuletwa na maafisa mradi walioko mbali na wakulima hao. Kwa kuzingatia fursa iliyopo sasa ya zao hilo, Elimu waliyoipata wataipeleka moja kwa moja kwa walengwa, ambao ni wakulima wadogowadogo walioko kwenye kata na vijiji husika.
Mafunzo hayo yamelenga kumuwezesha mkulima kupata taaluma na uelewa mzuri zaidi katika kilimo cha zao hili tofauti na wanavvoelewa sasa ili kuboresha uzalishaji kwa lengo la kuongeza mazao yaliyo bora yatakayowezesha kupata bei nzuri kwenye soko.
Nurdini Babu ni mkuu wa wilaya ya Rufiji na hapa anasisitiza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika mji mdogo wa Ikwiriri wilayani Rufiji, “Hili ni zao lenye faida kubwa kama utekelezaji wa taaluma ya uzalishaji utafuatwa kwa makini, ambalo ndiyo lengo kuu la mafunzo haya”, anasisitiza Babu.
Katika ziara ya kutathmini shughuli za mradi iliyofanywa na wafadhili wa mradi,yaani IFAD, ilipendekezwa kwamba zao lenye mzunguko mfupi linaloweza kuleta mafanikio ya kuongeza kipato kwa mkulima liongezwe kwenye mchakato wa uendelezaji wa mnyororo wa thamani sambamba na mazao ya muhogo na matunda yaliyopo sasa.
Ufuta ulichaguliwa katika ushindani na mazao mengine kama, mahindi, mpunga na mtama mweupe. Mafunzo yanatolewa ili kilimo cha ufuta kianze mara moja katika msimu huu.
Zao la ufuta sio zao geni machoni mwa wakulima waliowengi mkoani Pwani, kwa vile uzalishaji wake hautakuwa mgumu hasa ikizingatiwa kwamba soko la kueleweka lipo na pia ni endelevu.
Pendekezo la kujumuisha zao hili pamoja na mazao ya muhogo na matunda unatokana na faida yake kuwa kubwa katika kuongeza kipato kwa mkulima kwa muda mfupi tofauti na mazao ya muhogo na matunda.
Mjadala mkali wa jinsi zao la ufuta linavyoweza kuendelezwa na kumkomboa mkulima sambamba na fursa za soko zinazolizunguka zao hilo ulitawala kwa muda wa siku tano za mafunzo maalumu kuhusu kilimo bora cha ufuta, uliowashirikisha maafisa ugani zaidi ya ishirini na wadau mbalimbali wa zao la ufuta wilayani Rufiji.
Katika mafunzo hayo ya maafisa ugani, wamejifunza kanuni za kilimo bora cha zao la ufuta, kuanzia uchaguzi wa mbegu bora, utayarishaji wa shamba, udhiti wa mgonjwa na wadudu, utunzaji wa shamba na uhifadhi wa mazao baada ya kuvuna pia na usafirishaji.
Nchini Tanzania zaidi ya asilimia 75% ya ufuta hulimwa katika mikoa ya kusini ya Mtwara, Lindi na Ruvuma na katika mikoa hiyo ufuta ni zao la Pili la biashara baada ya Korosho.
Mikoa mingine ni Tanga,Pwani na Morogoro. Katika wilaya ya Rufiji Ufuta hulimwa ukanda wa juu yaani tarafa za kibiti,Kikale,Mohoro na Ukanda wa tambalale tarafa za Mkongo na Ikwiriri.
Thursday, April 18, 2013
DC TUNDURU AMWAGIZA MKURUGENZI KUWACHUKULIA HATUA WATUMISHI WAZEMBE
Na Steven Augustino, Tunduru
MKUU wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Chande Nalicho amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halamashauri ya Wilaya hiyo kuwachukulia hatua ikibidi hata kuwafukuza kazi Watumishi wasio wajibika zikiwa ni juhudi za Serikali kuinua taaluma Wilayani humo.
Nalicho alisema hayo wakati akifungua Mkutano wa kutathmini matokeo kidato cha pili,Nne na Sita uliofanyika katika ukumbi wa klasta Mjini hapa na kuongeza kuwa hali hiyo imetokana na Serikali kubaini kuwa watumishi wa kada zote Wilayani humo hawako tayari kufanya kazi kwa kujituma hali iliyopelekea Wilaya hiyo kuwa nyuma kielimu.
“Viongozi ndio wasiopenda kufanya kazi, wamebakia kulalamikia mishahara tu na ndiyo maana katika Wilaya hiyo imeendelea kuwa nyuma kielimu” alisema Nalicho na kumtaka Mkurugenzi awachukulie hatua za kinidhamu.
Alisema inashangaza kuona kuwa Wilaya ikiwa imekithiri kwa utoro wa wanafunzi lakini inapotokea ofisi yake inahitaji taarifa za matukio hayo hata Maafisa tarafa ,watendaji wa kata na viongozi wa vijiji wengi wanapoulizwa juu ya idadi ya wanafunzi waliofauru na kucahaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari wanadai kutokuwa na takwimu zake.
Nalicho aliendelea kubainisha viashiria vingine vya viongozi hao kutowajibika kuwa ni pamoja na kuwepo kwa takwimu kubwa za utoro uliokithiri ambazo hazifanyiwi kazi ambapo alitolea mfano Shule ya msingi Njenga ambayo takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2010 ilifaulisha wanafunzi 41 waliokwenda shule walikuwa 3, mwaka 2011 waliofauru 46 walioendelea na masomo 7 na mwaka 2012 walifaulu 17 waliokwenda shule hadi sasa 1.
Nae Mwenyekiti wa Huduma za jamii na uchumi Diwani Athumani Nkinde pamoja na kukiri kuwa zipo Shule za Sekondari ambazo zilijengwa kisiasa na kutolea mfano shule za Sekondari Nampungu ambayo inaonesha kutelekezwa na wananchi kwa kutopeleka wanafunzi
Nkinde alipigilia msumali wa moto kwa kuzitaka mamlaka kuchukua hatua za kisheria kwa wanafunzi na wazazi wao kwavile kusoma ni lazima
Akizungumzia mikakati ya kuinua taaluma na kuiondoa idara yake katika kashfa ya kupeleka Sekondari wanafunzi wasiojua kuandika kusoma na kuhesabu Kaimu afisa elimu wa Shule za Msingi Mwl. Fraviani Nchimbi alisema kuwa Wilaya inaendelea kujidhatiti kwa kutumia mitihani ya majaribio katika kata pamoja na kuendesha mafunzo ya mada ngumu kwa walimu zikiwa ni juhudi za kuinua taaluma kwa wanafunzi.
Awali akisoma taarifa ya matokeo ya ufaulu wa wanafunzi katika kipindi cha mwaka 2011 na 2012 Afisa elimu Sekondari Mwl. Ally Mtamila alisema kuwa mbali na Wilaya hiyo kufanya vibaya lakini idadi ya walimu imeongezeka kutoka walimu 213 mwaka 2011 na kufikia 282 mwaka huu ongezeko ambalo pia limeongeza idadi ya walimu na kufikia wastani wa zaidi ya walimu 10 kwa kila shule ya sekondari Wilayani hapa.
Mwisho
Wednesday, April 17, 2013
MADIWANI WA CCM WAHOJIWA KWA KOSA LA KUSHIRIKI KUTAKA KUMNG'OA MEYA SONGEA
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Charles Mhagama
Charles Mhagama ambaye ni Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea akiwa na Diwani wa Kata ya Matarawe James Makene ambaye ndiye MHASISI wa kumtuhumu Meya
Na Stephano Mango, Songea
MADIWANI Sita wa Chama Cha Mapinduzi wakiwemo Madiwani wawili ambao waliungana na Madiwani nane wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo( Chadema) kuandika barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ya kumuomba kuitisha mkutano maalumu wa Madiwani wenye madhumuni ya kujadili hoja za kutokuwa na imani na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Charles Mhagama ambaye anadaiwa kutumia nafasi yake vibaya wamehojiwa kwa nyakati tofauti na Kamati ya Siasa Ccm ya Wilaya ya Songea Mjini ikiwataka kujua muanganiko wao na Chadema katika sakata la kutokuwa na imani na Meya wao.
Uchunguzi uliofanywa na mtandao kwa zaidi ya wiki mbili sasa umebaini kuwa lengo kubwa la kamati hiyo ya siasa ni kutaka kufunika hoja ya msingi ya Madiwani kumi wa Halmashauri hiyo ya kutaka kuitisha mkutano ambao una lengo la kuelezea tuhuma zinazomkabili Charles Mhagama ambaye ni Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo bila kujali itikadi zao za kisiasa kwa masloahi ya wakazi wa Manispaa ya Songea
Imebainika kuwa Kamati hiyo ya Siasa iliyokutana tarehe 11/4/2012 iliwahoji, kuwatisha na kuwaonya Madiwani hao kuacha kuungana na Chadema kumtisha tisha Meya wao kwani kufanya hivyo kunaendelea kuwapa umaarufu Chadema ambao hawakitakii mema Chama cha Mapinduzi na badala yake kujikita kulinda heshima ya Ccm
Taarifa za ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa ndani ya kikao hicho kuliibuka malumbano makali yenye kupinga wazo la Chama kumbeba Meya ambaye anaonekana waziwazi kuwa hakubaliki ndani ya Baraza la Madiwani na nje ya baraza la hilo kutokana na mwenendo wake mbovu licha ya uchaguzi wake kutokuchaguliwa na Madiwani hao kwani alipigiwa kura 12 za ndiyo na kura 14 za hapana
Mtandao umebahatika kuiona barua ya Madiwani kumi wa Halmashauri hiyo yenye kumbukumbu namba MD/SO/013 ya Tarehe 15/3/2013 yenye hoja mbili ambazo zina vipengele vitano vinavyosisitiza kumuomba Mkurugenzi kuitisha mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa hiyo ,
Imebaini kuwa barua hiyo ndiyo ambayo imeichanganya kamati hiyo ya Siasa na kuamua kuitisha kikao cha dharula cha kuwatisha Madiwani hao kuacha mara moja mkakati huo na Chadema kwa maslahi ya Ccm kwani kufanya hivyo ni kukiaibisha chama na kukidhorotesha mbele ya umma
Madiwani hao ambao wamehojiwa na Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Mjini ni James Makene Diwani wa Kata ya Matarawe, Victa Ngongi Diwani wa Kata ya Ruvuma, Faustini Mhagama Diwani wa Kata ya Mshangano, Kulabest Mgwasa Diwani wa Kata ya Msamala, Wilon Kapinga Diwani wa Kata ya Ndilimalitembo na Genfrida Haule Diwani wa Viti Maalum
Imebainika kuwa Madiwani wawili wa Chama cha Mapinduzi (Ccm)walioungana na Madiwani nane wa Chadema kuandika barua hiyo ni Diwani wa Kata ya Matarawe James Makene na Victa Ngongi ambaye ni Diwani wa Kata ya Ruvuma
Taarifa zilizoufikia mtandao huu zimesema kuwa Kanuni za Kudumu za Halmashauri hiyo za mwaka 2003 ibara namba 4 na ibara namba 80 zinaeleza ili kuitisha mkutano maalum wa baraza la Madiwani kujadili hoja mbalimbali za kutokuwa na imani na Meya kujiorodhesha na kufikia idani ya theluthi moja ya Madiwani na kueleza malengo ya mkutano huo
Katika Halmashauri hiyo kuna jumla ya Madiwani 28 ambao theluthi yao ni Madiwani 9 ambapo madiwani 10 ndio waliojiorodhesha na kuweka saini zao za kusudio hilo ambalo linaonekana kuwa ni mwiba mkali kwa Ccm
Mmoja wa Madiwani wa Ccm ambao wamehojiwa na Viongozi wa Chama hicho ambaye hakutaka jina lake litajwe ameuambia mtandandau huu kuwa toka awali Charles Mhagama hakuchaguliwa na Madiwani wa Halmashauri hiyo ndio kiini cha kuwepo kwa makundi mawili ambayo moja linamuunga mkono na na kundi jingine ambalo halikubaliani na kundi linguine licha ya utendaji kudaiwa kuwa ni mbovu
Diwani huyo alilesema kuwa Chama hakina uwezo wa kuwachagulia Madiwani Meya Mbovu na kuendelea kuweka mazingira ya kumlinda licha ya kuwa tuhuma zake kuwa wazi na kuwatesa wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Alifafanua kuwa jukumu la kumchagua Meya ni la Madiwani bila kujali itikadi ya chama chochote kwani Meya huyo ni kiongozi wa Madiwani kwa maslahi ya wakazi wa Manispaa ya Songea ambao ndio waliowachagua madiwani wawawakil;ishe kwenye malengo ambayo yana maslahi kwa jamii
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ccm Wilaya ya Songea Mjini Gerod Mhenga alipohojiwa kwa njia ya simu jana alithibitisha kuwepo kwa kikao hicho cha Kamati ya Siasa ya Wilaya yenye lengo la kubaini tatizo lililopo kati ya Madiwani na Meya wao hadi kufikia hatua ya kuungana na Madiwani wa Chadema ya kumtaka Mkurugenzi kuitisha mkutano maalum wa kujadili mwenendo wa Meya
Akizungumza na mtandao huu Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo Charles Mhagama alikanusha baadhi ya tuhuma wanazo mtuhumu na kusema kuwa kama Madiwani wana jambo lao basi wanatakiwa kufuata kanuni ili ziwaruhusu kulisema jambo lao
Hata hivyo Mkurugenzi wa Manispaaa hiyo Nachoa Zakaria alipohojiwa jana ofisini kwake alisema kuwa Halmashauri inaweza kumuondoa madarakani Meya ni lazima kuwe na theluthi mbili ya madiwani wanaotaka kumuondoa na sio theluthi moja kama walivyoomba Madiwani hao kumi hivyo hawezi kuitisha kikao hicho bila kukidhi matakwa ya kanuni.
MWISHO
Thursday, April 4, 2013
KANISA LAFUNGUKA VURUGU ZINAZOENDELEA NCHINI
Na
Steven Augustino, Tunduru
KANISA
limesema kuwa kama Serikali itaendelea kushindwa kuchukua hatua za kuwalinda
wananchi wake na kuwatendea kwa usawa bila ya ubaguzi kwa mujibu wa ibara ya 12
na 13 ya Katiba ya jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kanisa litachukua hatua kwa kuwaaeleza waumini
wake kwa uwazi kuwa Serikali iliyopo madarakani inaibeba Dini moja
Hayo
yalisemwa na Katibu wa umoja wa Makanisa Kikrsto Wilaya ya Tunduru Padre
Dominiki Mkapa wakati akiwasomea waumini wake Waraka wa Tamko lililotolewa hivi
karibuni na Jukwa la Wakristo Tanzania (TCF) na kusambazwa katika Makanisa yote
nchini na kuongeza kuwa baada ya kufikia maamuzi hayo pia Kanisa litatafakari
upya juu ya mahusiano kati yake na Serikali.
Waraka
huo uliotisa saini na Mwenyekiti wa Umoja huo (CCT) Askofu Peter Kitula Machi
19 mwaka huu ambao mtandao huu umefanikiwa kuuona na kuipata
nakala yake unafafanua kuwa hatua hiyo imetokana na Serikali kutochukua hatua
madhubuti kwa watu wanaobainika wazi wazi kutumia mwamvuli wa Dini kufanya
vitendo vibaya yakiwemo mauaji na vitisho kwa viongozi wa Dini nyingine na
kuivuluga amani na utulivu wa taifa letu.
Aidha
waraka huo uliendelea kueleza kuwa kutokana na udhaifu huo wa Serikali
kuendelea kufumbia macho vitendo hivyo kikundi hicho kimekuwa kikiendeleza
utekelezaji wa matukio hayo hali inayolishawishi Kanisa kufikilia vinginevyo
likiwemo wazo la kutamani kuutangazia kuwa hivi sasa Tanzania ni nchi
inayovunja haki za Binadamu kwa ubaguzi wa dini na kulitesa Kanisa kimfumo.
Awali
Askofu wa Jimbo kuu la TUNDURU/Masasi Mhashamu Castory Msemwa aliwahimiza
wazazi na walezi kuwasaidia wachungaji katika malezi ya Watoto wao zikiwa ni
juhudi za kuwalea katika maadili mema na kuongeza kuwa vitendo vya uvunjifu wa
amani vinavyotekelezwa sasa vinatokana na kuporomoka kwa maadili.
Askofu Msemwa ambaye alikuwa akiongea na
waumini wake katika kanisa Katoliki kupitia mahubiri aliyo yatoa wakati wa
ibada ya maadhimisho ya sikukuu ya Pasaka taliyofanyika katika kanisa la
Mtakatiofu mathias Mulumba Kalemba mjini Tunduru Mkoani Ruvuma na kuongeza kuwa
Watoto wasipo lelewa na kupewa elimu ya kutosho katika maadili na misingi mikuu
ya imani ya Dini husika ipo hatari kwa watoto hao kuingia katika mikumbo mibaya
hali itakayo wasukuma kutotenda mema katika jamii.
Pamoja
kutolea mifano ya matukio yanayotishia kuvunjika kwa amani na utulivu wa taifa
la Tanzania yaliyoibika hivi karibuni, Askofu Msemwa aliwataka waumini wake
kusimamia imani yao kikamilifu na kuto waogopa wauaji hao wanaotishia imani za
wengine kwa madai kuwa wanacho weza kukitoa uhai ni mwili tu lakini Roho
itabaki hai.
Mwisho
Thursday, March 28, 2013
ZITTO: CHADEMA SI PANGO LA WAUAJI, ASEMA HAAMINI KAMA DK.SLAA ANAWEZA KUMUUA
| ||
|
Thursday, March 7, 2013
LA KIBANDA NALO LINAKUMBUSHA HAYA
Watanzania wenzangu,
Tumeshashughudia utekwaji wa watu kadhaa mara kwa mara. Tumeshashuhudia matukio mbalimbali ya ajabu, ambayo hata hivyo yalifanywa kwa namna ya kuwasingizia majambazi.
Leo, tunamwona tena Mwanahabari mahiri, Absalom Kibanda, akipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu, si ya ugonjwa, bali ya kipigo kutoka kwa watu wasiofahamika, watu waitwao majambazi.
Hili linatokea muda wa miezi takribani minne baada ya Mnaku Mbani, Mhariri wa gazeti la Business Times kupigwa risasi mdomoni na kupoteza meno matatu.
Hili linakuja baada ya Mwandishi mwingine wa Tanzania Daima, Shaaban Mtutu kupigwa risasi na Polisi eti akidhaniwa ni jambazi. Huyu alipigwa risasi akiwa nyumbani kwake mnamo tarehe 4 Disemba, 2012, eti polisi walimdhania ni jambazi, AKIWA NYUMBANI KWAKE.
Tukio la Kibanda, linatokea ikiwa ni miezi michache tangu Mwangosi Daudi, mwandishi wa Channel Ten kuuawa na jeshi la polisi tarehe 2 Septemba 2012.
Hili linakuja miaka michache baada ya mapema mwaka 2008 Saed Kubenea, Mkurugenzi wa kampuni ichapayo gazeti la Mwanahalisi (ambalo nalo limefungiwa), kumwagiwa tindikali machoni pamoja na Mhariri Mshauri wa gazeti hilo Ndimara Tegambwage kucharangwa kwa mapanga.
Linatokea miezi michache baada ya Dk. Ulimboka kutekwa na kupigwa nusu kifo, na kutupiwa msitu wa Mabwepande. Haya yote yanatokea Tanzania, na asilimia kubwa ya haya yote yamehusishwa na ujambazi.
Huwa najiuliza, ujambazi ni nini? Kwa nini hao majambazi hawaibi chochote zaidi ya kuwajeruhi na kunuia kuwaua hawa makamanda? Kwa nini wawavamie tu watu wenye kuikosoa serikali?
Hao majambazi kwa nini hawapatikani? Ikiwa juzi tu ameuawa kwa risasi Padre kule Zanzibar, na serikali imewaleta FBI kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hilo, kwa nini serikali isione haja ya kuwatumia FBI na taasisi nyingine za ukachero kutoka mataifa yaliyoendelea ili tuwapate hawa wahalifu wawavamiao wanahabari na wanaharakati wetu? Watanzania, tutanyamaza hadi lini ikiwa sauti zetu zinanyamazishwa?
Bwana Kibanda, hadi sasa, ana kesi mahakamani. Kesi ya uchochezi baada ya gazeti la Tanzania Daima (Wakati Kibanda akiwa Mhariri) kuchapa makala iliyoandikwa na Mwandishi na Mwanaharakati Samson Mwigamba. Kesi hii ingali ikisikilizwa, leo tunasikia kuwa amevamiwa na majambazi! Kweli? Latuingia akilini kweli? Latushawishi hili kweli?
Tanzania, serikali imetengeneza mtandao wa Kimafia (kama alivyoeleza Mh. Joseph Mbilinyi Bungeni Mwaka jana). Kumekuwa na mtandao wa kimafia unaowawinda makamanda, wanaharakati.
Habari/tetesi zilishawekwa wazi kuwa kuna kundi la watu limeundwa, linalojishughulisha na utekaji, utesaji, na uuaji wa watu wenye ushawishi katika jamii, wanaoikosoa serikali kwa uwazi. Yamkini kundi hili ndilo lililoripotiwa kuwafuatilia Mh. John Myinka, Mh. Godbless Lema, na Mh. Dk. Wilbroad Slaa.
Yamkini hilo ndilo kundi lililomwekea sumu Mwanaharakati mwingine Dk. Harryson Mwakyembe. Hili ndilo kundi lililoripotiwa kufuatilia maisha ya Mh. Samwel Sitta. Hili ndilo kundi, ndilo hasa!
Kundi hili la kimafia limeamua kuwanyamazisha Watanzania, na kuiacha serikali iendelee kutuibia, kutunyonya na kutufanya mafukara.
Kundi hili limenuia kuifanya serikali iendelee kutawala na kujinawirisha. Vigogo wa serikali na watoto wao waendelee kufurahia nchi, kwa kodi zetu wananchi.
Kundi hili limenuia kuhakikisha viongozi waovu na wabadhirifu wa mali za umma wanaendelea kututawala kwa mabavu, kwa matisho na kwa dhuluma.
Kwa mtindo huu, lazima tuhoji waziwazi kuwa kwa nini watu hawa hawakamatwi na kutiwa nguvuni, iwapo kweli serikali haina uhusiano nao?
Si ndio hawa wafanyao kazi kama Ramadhani Ighondu? Hapa tusidanganyane, serikali inawafahamu watu wote wa kundi hili... Serikali inafahamu A hadi Z ya kundi hili, na yamkini serikali ndiyo iliyowapa kazi hii maalum.
Kufunika kombe ili mwanaharamu apite, tunaiona serikali ikienda kuwajulia hali wahanga wa uonevu huu. Serikali inamtuma Makamu wa Rais kwenda kumtazama Kibanda hospitalini, Rais Kikwete pia alikwenda kumjulia hali Saed Kubenea... Yote haya ni kujaribu kutudanganya (elude) kuwa hawajui kiendeleacho..
Serikali inafahamu kundi lake hili la kimafia. Kundi la uovu, inalifahamu vyema..
Sasa, kwa nini serikali ifanye hivi? Kwa nini wanaharakati wateswe, wakamatwe, wauawe? Ukweli wenyewe ndio huu:
Lengo kuu la serikali, ni kunyamazisha sauti zote zinazoikosoa bila kujali sauti hizo zinatokea wapi. Serikali inahitaji kunyamazisha sauti za watu binafsi, inahitaji kunyamazisha sauti za vikundi, vyama au jumuiya zinazoikosoa.
Sasa kwa sababu tasnia ya habari huwafikia wengi, na kwa sababu watu wengi huamini habari za vyombo vya habari, serikali imenuia kuinyamazisha kabisa tasnia ya habari kwa kushughulika na wakosoaji wakubwa katika vyombo vya habari.
Ndio maana hata waandishi wa makala kama hizi wanatafutiwa visa hata vya kufungwa gerezani. Mfano mzuri wa hili ni kesi ambayo inaendelea mahakamani dhidi ya Kibanda mwenyewe, na Samson Mwigamba, eti kwa sababu ya makala iliyochapwa kwenye gazeti la Tanzania Daima.
Pengine wengi wetu mnamkumbuka Sam Shollei. Huyu alikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, kabla ya Tido Mhando wa sasa.
Huyu si Mtanzania bali ni Mkenya. Shollei aliibadilisha taswira ya gaeti la Mwananchi na kulifikisha katika taswira lililokuwa nayo sasa.
Alifanya kazi kubwa sana. Lakini, mwisho wake alinyimwa kibali cha kuendelea kufanya kazi nchini Tanzania baada ya kibali chake cha awali kwisha muda.
Serikali, kupitia uhamiaji, ilimnyima Shollei kibali bila kuweka bayana sababu za kufanya hivyo. Zitto Kabwe alipiga kelele kidogo kuikosoa serikali kwa swala hilo lakini kelele zake hazikufua dafu.
Shollei, aliyelipa gazeti la Mwananchi umaarufu mkubwa na maendeleo makubwa akalazimika kuacha kazi.
Baada ya Shollei kulazimika kuondoka Tanzania, nafasi yake ikachukuliwa na Tido Mhando. Hapa tukumbuke kuwa, Tido Mhando alifuatwa na Rais Kikwete London mwaka 2007, akiwa Mkurugenzi wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, na Kikwete akamwomba aje aiongoze TBC.
Hata hivyo naye alipoiongoza TBC na kuwa chombo cha uwazi na ukweli, na pale aliporuhusu kuonyeshwa kwa mikutano ya kampezi ya vyama vyote vya siasa katika uchaguzi Mkuu wa 2010, bila upendeleo, Tido alinyimwa mkataba mpya mwaka 2011.
Tido, akiwa amebadilisha taswira ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), akanyimwa mkataba wa kuendelea kuiongoza. Sasa ni nani asiyejua kuwa TBC imeshapoteza ule umahiri wake ambao Tido aliisaidia kuwa nao? TBC sasa imerejea ilipotoka, imeanza kulichungulia kaburi tena...
Baada ya Tido kunyimwa mkataba na serikali, licha ya kwamba watu wengi walilaumu sana, Tido akachukuliwa na Mwananchi, kuziba nafasi ya Shollei.
Sasa, pengine kwa weledi wa Absalom Kibanda, kwa kazi ambayo ameifanya tangu akiwa Mhariri Mtendaji wa Tanzania Daima, naye ameanza kutafutwa roho yake na hao wanaoitwa "majambazi". Majambazi wasioiba chochote, majambazi watafutao roho za wanahabari mahiri na wanaharakati.
Nirudie tena, lengo la serikali ni kuifunga mdomo tasnia ya habari Tanzania. Lengo lake ni kuwa na vyombo vya habari kama Radio Uhuru na Gazeti la Mzalendo ambayo kazi yao ni kuitukuza serikali ya CCM hata pale pasipostahili.
Lengo la serikali, ni kuwanyamazisha makamanda wote waonekanao kuikosoa serikali kwa uwazi. Na hili linaonekana kufanikiwa kwa kiasi fulani.. Kwani gazeti la Mwanahalisi liko wapi leo? Mwangosi yuko wapi? Kubenea anasikika tena? Je ulimboka mmemsikia tena? Wote hawa wameshanyamazishwa kwa kiasi fualani, sauti zao zimefifia.
Watanzania wenzangu, Tanzania ya sasa si mahala salama kwa Wanahabari makini, na wanaharakati. Nawaomba na kuwasihi tuwe macho na tuamke tuungane na wenzetu hawa waliojitoa mhanga.
Tusimameni imara kuitetea nchi yetu, haijalishi watuue sote. Kwa hakika, tusiposimama imara, nchi hii tutaitumbukiza korongoni.
Tupazeni sauti zetu pale tuwapo na nafasi. Kwa wale tusioweza kuchapa makala kwenye magazeti mbalimbali, mitandao ya kijamii ndio silaha yetu iliyosalia.
Tusiandike jumbe za mapenzi kwenye kuta zetu za Facebook, Tiwitter, blogu zetu. Tuandikeni jumbe za kutafuta haki na usawa nchini.
Tuandikeni jumbe za kuikosoa serikali na kuilalamikia kila uchwao uchao. Tusiishie hapo; tuwaamsheni Watanzia wenzetu; tuwaamsheni waliolala... Tuwaelezeni kumepambazuka.... Tusipofanya hivyo, tutakapoacha kazi hii mikononi mwa wenzetu wachache, kwa hakika tutashiriki kiliangamiza taifa letu. Mwisho tutalia na kusaga meno.
WANAKONGANO WATAKIWA KUJITUMA KATIKA UZALISHAJI WA UYOGA
Na,Mwandishi Wetu , Songea
WANAKONGANO wa Uyoga Songea wametakiwa kujishughulisha kwa
kasi na kujituma katika kilimo cha uyoga ili kuweza kuongeza uzalishaji wa zao
hilo ili walaji waupate kwa wingi kwa mahitaji mbalimbali katika Jamii
Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti kwenye
ukumbi wa Saccos ya Walimu Songea Mjini wakati akiwahutubia Wanakongano na
wageni waalikwa kwenye hafla fupi ya kuikabidhi hundi ya shilingi milioni nane
Kongano la Uyoga Songea
Mkirikiti alisema kuwa Kongano la Uyoga Songea linapaswa kuwa chachu ya kujiimarisha katika
uzalishaji wa zao la Uyoga kwa lengo la
kuongeza lishe na kipato miongoni mwa Jamii kama vile malengo yake ya
kuanzishwa yanavyosema
Alisema kuwa hadi sasa Kongano hili limethubutu kufanya
jambo la kimaendeleo ambalo leo limetukutanisha
katika ukumbi huu likiwa na malengo ya kuiwezesha jamii kupata lishe bora na
kipato miongoni mwao
Awali akizungumza na Wanakongano hao Mratibu wa Kongano
Nchini kutoka Tume ya Sayansi na Teknologia Omary Bakari alisema kuwa (Songea Mushroom
Cluster ) Kongano la Uyoga Songea limeonyesha mfano wa kuigwa kwani mara baada
ya kupata mafunzo ya uwezeshaji waliweka mpango kazi ambao leo umezaa matunda
stahiki
Bakari alisema kuwa mpango huo umeletewa fedha ya shilingi
milioni nane kutoka Tume ya Sayansi na Tecknologia ili uweze kutekelezwa na
kufikia mafanikio yaliyokusudiwa kadri ya shughuli zilizopangwa kwenye mpango
kazi
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Katibu Mtendaji wa
Kongano la Uyoga Songea Stephano Mango alisema kuwa haikuwa gazi rahisi
kutengeneza mpango huo wa kuiwezesha Kongano ili liweze kusonga mbele
Alisema kuwa mpango huo utaiwezesha Kongano kuimarika na
kuongeza uzalishaji wa uyoga kwa sababu fedha iliyofika itasaidia kutatua
vikwazo ambavyo vinaisumbua Kongano vikiwemo vya uharibifu wa Vimeng’enya,
wadudu waharibifu,zana duni za kilimo na kuhifadhia uyoga, elimu duni ya kumbukumbu
Mango alisema kuwa mpango huo ni wa miezi 18 na kwamba
umegawanyika katika vipengele vitatu vya uhamasishaji ,muda mfupi na muda mrefu ili
malengo yatimie
MWISHO
Wednesday, March 6, 2013
MAAFISA UGANI WAPATIWA MAFUNZO YA ZAO LA UFUTA
Na, Stephano Mango,Pwani
MAAFISA Ugani nchini wametakiwa kukithamini na kukiendeleza kilimo
cha zao la Ufuta ili kiweze kubadilisha maisha ya watanzania kutokana na mahitaji ya
soko kuwa makubwa kwa sasa na kufanya zao hilo kwa baadhi ya maeneo kuwa zao
kubwa la kibiashara
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya
Rufiji Nurdin Babu kwenye ufunguzi wa mafunzo maalumu kuhusu kilimo bora cha
ufuta, uliowashirikisha maafisa ishirini na wadau mbalimbali wa zao la ufuta
wilayani Rufiji Mkoani Pwani yaliyofanyika Mji mdogo wa Ikwiriri Wilayani Rufiji
Babu alisema kuwa Ufuta ni zao lisilotiliwa
maanani na wakulima wengi nchini kwa miaka mingi pamoja na uwingi wa faida zake
kwa binadamu, lakini kwa miaka ya hivi karibuni, takribani sehamu zote ambako
hali ya hewa imekuwa rafiki wa kulistawisha zao hilo, wakulima wengi
wameligeukia na kuanza kulima kwa kasi.
Alisema kuwa Wilaya ya Rufiji ni
mojawapo ya wilaya ambazo zinastawisha zao la ufuta kwa siku nyingi na siku za
hivi karibuni kasi ya uzalishaji imeongezeka kutokana na upatikanaji wa uhakika
wa soko la ufuta.
“Hili ni zao lenye faida kubwa kama
utekelezaji wa taaluma ya uzalishaji utafuatwa kwa makini, ambalo ndiyo lengo
kuu la mafunzo haya na ni lazima walau
kwa kuanzia tani elfu tano (5000) katika msimu ujao wa kilimo 2012/2013 kutoka
tani za sasa 400 kwa mwaka na tani 280 mwaka 2005/06.”,
anasisitiza Babu.
Akizungumza kwenye Mafunzo hayo Afisa
Habari Mshauri Mkoa wa Pwani Silas Bwena alisema kuwa Serikari kupitia wizara ya
viwanda, biashara na masoko, chini ya mradi wa MUVI mkoa wa Pwani imetoa mafunzo
hayo kwa maafisa ugani ili waweze kuifikisha Elimu waliyoipata moja kwa moja kwa
walengwa, ambao ni wakulima wadogowadogo walioko kwenye kata na vijiji husika.
Bwena alisema kuwa Mafunzo hayo yamelenga kumuwezesha
mkulima kupata taaluma na uelewa mzuri zaidi katika kilimo cha zao hili tofauti
na wanavvoelewa sasa ili kuboresha uzalishaji kwa lengo la kuongeza mazao
yaliyo bora yatakayowezesha kupata bei nzuri kwenye soko
MWISHO
Subscribe to:
Posts (Atom)
