About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Saturday, October 26, 2013

DKT NCHIMBI APIGWA MAWE SONGEA NA MSAFARA WAKE


Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi Dkt Emmanuel Nchimbi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini

Na Stephano Mango,Songea

MSAFARA wa Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi Dkt Emmanuel Nchimbi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma wapigwa mawe na wananchi waliojitokeza kuzungumzia kero ya daraja la Matarawe ambalo linadaiwa kusababisha vifo vya watu zaidi ya watatu katika mwezi huu wa octoba mwaka huu

Wananchi hao wa kata ya Matarawe  Manispaa ya Songea,wakiwemo waendesha  Pikikipiki maarufu kwa jina la Yebo Yebo  walifunga barabara kwa  zaidi ya masaa mawili na kufanya fujo za kung’oa kingo za daraja  pamoja na kuweka  magogo na mawe  katikati ya daraja na kuchoma matairi moto  ili Mbunge huyo asipite mpaka atoe majibu ya kina kuhusu daraja

Hali hiyo ililazimisha Jeshi la polisi kuwatawanya  wananchi hao kwa kuwafyatulia mabomu ya machozi kwa lengo la kuzuia uharibifu zaidi na kuufanya msafara upite wakati ukirudi kutoka kwenye Mkutano wa hadhara wa Matarawe baada ya kuzuiriwa wakati wa kwenda na wakati wa kurudi ambapo hadi sasa watu nane wanashikiliwa na Jeshi hilo kutokana na vurugu hizo.

Tukio hilo limetokea jana kati ya saa kumi  hadi saa kumi na mbili jioni  ambapo wananchi hao wakiwa na hasira walifanya fujo hizo  wakiwa na lengo la kumshinikiza Mbunge wa Jimbo la Songea  mjini ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt.Emmanuel Nchimbi  awasaidie kupanua daraja  la mto Matarawe ambalo ni dogo kwani kwa  muda mrefu limekuwa likisababisha ajalli mara kwa mara katika eneo hilo kutokana na ufinyu wa daraja hilo.

Awali  Mbunge huyo akiwa katika ziara yake ya siku ya pili akitokea  mtaa wa Liumbu kata ya Mletele  kukagua shughuli mbali mbali za maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi akiwa anaelekea kata ya matarawe  kwenye mkutano wa hadhara ndipo alikutana na umati mkubwa wa wananchi wakiwemo  waendesha piki piki  walikuwa wamezuia njia na kusimama njiani ili asikilize kero zao kutokana na watu kufa mara kwa mara ambapo siku moja kabla ya mbunge huyo kufanya ziara kuna kijana aliyetambulika kwa jina la Mashaka Nuhu mkazi wa Matarawe akiwa anaendesha piki piki alitumbukia mtoni na kufariki dunia papo hapo.

Hata hivyo Dkt.Nchimbi alilazimika kusimama na kushuka kwenye gari yake  akiwa ameongozana na viongozi mbali mbali wa  chama na Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Songea Joseph Joseph Mkirikiti  ambapo Mbunge huyo aliwapa pole kwa ajali zinazotokea na kwa watu ambao wamepoteza ndugu zao alizungumza nao na kuwataka wawe na subira  wakati ombi lao linashugulikiwa, majibu ambayo wanachi hao hawakulizika nayo

“Natoa pole sana kwa msiba na ajali ambazo zimetokea nimewasikia, na ninaahidi  nitawajengea daraja  hili ,kama nimeweza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami bila maandamano wala kufungiwa barabara nitashindwa daraja? hivi ni vitu vinavyozungumzika  hili ni jambo dogo hivyo naomba  twende kwenye mkutano wa hadhara na tutaongea vizuri zaidi , kwani ni kweli daraja ni finyu na linahitaji kufanyiwa maboresho zaidi, ‘alisema Dkt. N chimbi.

Dkt.Nchimbi akiwahutubia Wananchi  kwenye mkutano wa hadhara  uliofanyika kwenye viwanja vya  Shule ya sekondari ya kutwa ya matarawe  amesema,amesikitishwa na tukio hilo kwani tabia hiyo haipendezi ,haikubaliki na haina maadili na aina
tija kama wangekuwa na busara wangefika kwenye mkutano na kutoa kero zao badala ya kufanya fujo ambapo ameliagiza jeshi  la polisi kuwasaka wahusika wa fujo hizo.

Amesema, ni kweli daraja hilo ni dogo ila siyo ustarabu kufunga barabara kwa masaa mawili kwani wamesababisha shughuli mbali mbali za maendeleo kusimama kutokana na barabara hiyo kufungwa  na kwamba tayari ameshamuagiza Mhandisi wa halmashauri ya Manispaa hiyo kufanya tathmini ili kujua gharama zinazohitajika ili liweze kupanuliwa.

Mapema Diwani wa kata ya Matarawe James Makene aliungana na kundi kubwa la wananchi hao na alimweleza Nchimbi kuwa  hiyo ni changamoto ambayo wakazi wa matarawe  wamekuwa wakilia kila mara hivyo wanahitaji msaada wa kupanua daraja hilo ambalo limeonekana kuwa ni kero ya muda mrefu.

Kwa upande wake kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Deusdedit Msimeki ameeleza kuwa kufatia vurugu hizo tayari watu nane wanashikiliwa na wanaendelea kuhojiwa zaidi ili kuwabaini vinara wengine wa fujo waliowashawishi wananchi kufanya fujo hizo .
MWISHO.

Thursday, October 3, 2013

MASHINE ZA TRA ZAZUA BALAA, WENGINE WASHUSHIANA MKON'GOTO



Na Kenneth Ngelesi

WAFANYABIASHARA mkoani Mbeya wamezua kizaazaa wakigoma kufungua maduka wakipinga agizo la Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) linalowataka kununua mashine za kielektroniki kwa ajili ya kukatia risiti za wateja pindi wanapowauzia bidhaa.

Katika sokomoko hilo lililotokea jana na kusababisha taharuki kwa muda kadhaa, wafanyabiashara hao wanadai kuwa gharama za mashine zitolewe na serikali.

Eneo la Soko la Sido ambalo lina wafanyabiashara wengi na tegemeo katika uchumi wa Jiji la Mbeya, walifunga biashara zao kwa muda usiojulikana.

Kadhia hiyo inakuja siku moja tangu Mkuu wa Mkoa huu, Abbas Kandoro, akutane na viongozi wa wafanyabiashara kutoka Soko la Sido na kuwataka viongozi kuwataarifu wenzao wasitishe mkutano ambao walitaka kuufanya jana katika uwanja wa Shule ya Msingi Ruanda Nzovwe.

Kandoro alifikia uamuzi wa kukutana na viongozi hao baada ya kupata taarifa kupitia gari la matangazo ambalo lilikuwa likipita na kuzunguka katikati ya jiji na kuwataka wafanyabiashara hao kufunga maduka na kufika mkutanoni ili kujadili suala zima la mashine hizo.

Taarifa zinadai kuwa baada ya Kandoro kusikia matanagzo hayo, aliliagiza Jeshi la Polisi kumkamata dereva wa gari hilo pamoja na Mwenyekiti wa Soko la Sido na kuwaweka rumande kwa muda usiojulikana.

Baada ya wawili hao kuwekwa ndani, lilitolewa agizo la kuzunguka tena mitaani kwa kutumia gari hilo ili kuwatangazia wafanyabiashara hao kuwa mkutano huo umesitishwa.

Uamuzi wa kusitisha mkutano huo ulipuuzwa na wafanyabiashara hao ambao jana waliendelea na maandilizi ikiwa ni kukodi gari jingine la matangazo kupita mitaani kuwahimiza wenzao kujitokeza kwa wingi. 

Hatua hiyo iliufanya uongozi wa mkoa kuwasambaza polisi mitaani kuzuia mkutano huo. Mabomu ya machozi na maji ya kuwasha vilitembezwa kwa wafanyabiashara hao ambao walikuwa wamekusanyika huku maduka yao yakiwa yamefungwa.

Mabomu hayo ya polisi yaliwaathiri wanafunzi wa Shule ya Msingi Kagera na kuwafanya wataharuki na kuanza kukimbia hovyo huku wengine wakizirai.

Kufuatia hali hiyo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ayoub Kiwanga, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ilomba, Erasto Mwakaponda na Diwani wa kata hiyo, Dickson Mwakilasa, walikubaliana kuwakabidhi wanafunzi hao kwa wazazi wao waliofika shuleni hapo kuwajulia hali baada ya kupokea taarifa za kupigwa mabomu.

Wakizungumza na Tanzania Daima, wafanyabiashara hao walisema kuwa wanashindwa kuelewa nguvu kubwa ambayo inatumiwa na polisi wakati hakuna vurugu zozote katika eneo hilo.

Alex Oswald, kwa niaba ya wenzake alisema kuwa wao waliamua kufunga maduka kwa hiari yao na kwamba lengo la mkutano lilikuwa kutoa msimamo wa kuiomba serikali itoe mashine hizo bure.

Naye Peter Tweve, alisema kuwa kimsingi wao hawajagoma kutumia mashine hizo bali wanataka wawekewe bure, kwani si kila mfanyabiashara anaweza kuinunua mashine hiyo ambayo kwa sasa inauzwa kwa sh 800,000.

Alipotafutwa Kandoro kuelezea tukio hilo, aligoma akisema kuwa yupo katika kikao, pia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, simu yake iliita bila kupokewa.

Wiki moja iliyopita, Mkurugenzi wa Elimu ya Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alitoa taarifa kuwa wafanyabiashara wenye mapato ya zaidi ya sh 45,000 kwa siku wanapewa hadi Oktoba 14, mwaka huu wawe wamenunua mashine hizo.

Friday, September 20, 2013

WAZIRI AMTISHA JK

Na, Betty Kangonga

WAZIRI wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe amemtisha Rais Jakaya Kikwete akisema kuwa endapo hatasaini muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013, atakuwa ameingia kwenye mgogoro na Bunge.

Muswada huo uliopitishwa hivi karibuni na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Augustine Mrema wa TLP (Vunjo), unapingwa vikali na vyama vya upinzani pamoja na makundi mbalimbali ambayo sasa yanamshinikiza rais asiusaini kuwa sheria.

Makundi hayo ambayo yamepata msukumo wa vyama vitatu vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi ambavyo wabunge wake walikataa kuujadili muswada huo wakipinga uchakachuaji uliofanyika wa kuongeza vifungu na kutoishirikisha Zanzibar, tayari yametishia kwenda kortini ikiwa watapuuzwa.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Chikawe alisema kuwa ni vyema makundi mbalimbali yakaacha kumlaghai Rais Kikwete ili asiusaini muswada huo.

Kwa mujibu wa Chikawe, iwapo Rais Kikwete ataliafiki suala hilo la wapinzani na makundi mengine, na kuacha kutia saini muswada huo, atakuwa ametengeneza mgogoro na mhimili wa Bunge kutokana na chombo hicho kukamilisha kazi yake.

Alisema kuwa taratibu zote zilifuatwa kuhusiana na kupitishwa kwa muswada huo, na kudai kushangazwa na baadhi ya makundi yanayopiga kelele.

“Hao wanaolalamikia juu ya jambo hilo hawatendi haki kwani sheria zote zilifuatwa na hayo mapendekezo wanayotoa ya kutaka Rais Kikwete asitie saini sio sahihi hata kidogo, huko ni kutaka ‘kumblack mail’ na kumsababishia mgogoro na Bunge,” alisema.

Waziri Chikawe alisema kuwa ameshangazwa na baadhi ya matamshi yanayotolewa juu ya kuwepo kwa fujo au kumwagika damu na kusema jambo hilo haliwezi kufanikiwa kama halijapangwa.

“Fujo zinapangwa, hivyo wale wanaotaka kumwaga damu ni vyema wakajitaja na kusema kuwa ‘sisi tutamwaga damu’ kwa kuwa naamini damu haiwezi kumwagika yenyewe,” alisema.

Waziri huyo alisema kuwa ni vyema wale wanaotaka kuzunguka kwa wananchi na kufanya udanganyifu juu ya suala hilo, wangekubali kuwasilisha hoja hizo ndani ya Bunge na si mahali kwingine.
Kuhusu Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kutopeleka muswada huo kwa wananchi wa Zanzibar, 

Chikawe alisema kuwa utaratibu uliotumika ni hisani tu, kwani hakuna sheria inayotaka muswada wa aina yoyote kupelekwa kwa Watanzania.

“Utaratibu wa kupitisha muswada huo sio huo tu, bali zipo njia nyingi ambapo anaweza kuandika anayohitaji na kuwasilisha kwa kamati ya Bunge na wapo waliofanya hivyo,” alisema.
Chikawe aliongeza kuwa inawezekana Kamati ya Katiba na Sheria ikawa na  sababu za kushindwa kuwafikia wananchi wote, lakini kwa upande wao walipokea maoni ya Serikali ya Zanzibar yaliyotolewa Mei 27, mwaka huu.

Alisema kuwa moja ya pendekezo lililotolewa na Serikali ya Zanzibar ni juu ya kuongezwa kwa siku 20 kati ya 70 zinazotakiwa kutumiwa na Bunge Maalumu la Katiba.
Chikawe alisema kuwa ni vyema yale yanayoenda kutolewa kwenye mkutano wa wapinzani kesho katika viwanja vya Jangwani, yangepelekwa bungeni kwa kuwa hata wakitoa katika viwanja hivyo haitasaidia.


ju





Thursday, September 19, 2013

WAANDISHI WAKWIDWA , WANYANYASWA NA KUPOKEA KIPIGO




Na Dixon Busagaga, Moshi

WAKATI watuhumiwa wanne zaidi wakiongezwa katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini ya tanzanite mkoani Arusha, Erasto Msuya, waandishi wanaoiripoti jana walionja joto ya jiwe kwa kukwidwa na kutaka kunyang’anywa vitendea kazi vyao.

Tafrani hiyo ilitokea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi saa 5:30 wakati kesi hiyo inayowakabili washtakiwa saba wanaodaiwa kushiriki kupanga na kutekeleza mauaji ya Msuya ilipofikishwa mbele ya mahakama kwa ajili ya kutajwa.

Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa waandishi hao, Fadhili Athuman alisema kuwa walipata wakati mgumu walipojaribu kuchukua picha za ndugu wa Msuya.

Athuman alisema kuwa baada ya kupiga picha kadhaa, alikwidwa na wanafamilia hao, wakitaka kumpora kamera huku mwandishi mwenzake akishikwa na kupigwa kibao.

“Baada ya kesi kuahirishwa iliibuka tafrani, walitaka kuninyang’anya kamera ili wafute picha nilizokuwa nimepiga. Mwenzangu yeye alikamatwa na kupigwa vibao kabla askari wa kikosi cha FFU kumuokoa,” alisema.

Kwa mujibu wa mmoja wa watu wa karibu na familia ya Msuya ambaye aliomba kuhifadhiwa jina, wamechukizwa na hatua ya baadhi ya waandishi kutochapisha picha za watuhumiwa, na badala yake zinatolewa za wanafamilia hiyo.

Hali ya taharuki ilianza mapema baada ya chumba kilichozoeleka kuendeshea kesi hiyo kubadilishwa kwenda kwenye chemba kutokana umati wa watu uliohudhuria kuwa mkubwa.

Wakati huo huo, vilio viliendelea kutawala mahakamani hapo baada ya kesi hiyo kuahirishwa. Mama mzazi wa Msuya, Marry Msuya alipoteza fahamu na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Awali mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Ruthi Mkisi, mawakili wa serikali, Stella Majaliwa akisaidiwa na Janeth Sipule waliieleza mahakama kuwa washitakiwa wanne wameunganishwa katika kesi hiyo na kufikia saba.

Majaliwa aliwataja waliounganishwa kuwa ni mshitakiwa wa nne hadi saba ambao ni Jalila Zuberi, Karimu Kihundrwa, Sadiki Jabiri (Chusa) na Joseph Mwakipasile ambao wote walifika mahakamani hapo.

Hakimu Mkisi alisema kesi hiyo imeahirishwa kutokana na upelelezi kutokamilika na hivyo kutaka washitakiwa hao kurudi rumande hadi Oktoba 2, mwaka huu.

Agosti 21, mwaka huu, washitakiwa watatu; Sharifu Mohammed, mkazi wa Kimandolu Arusha, Shaibu Mpungi, mkazi wa Kijiji cha Songambele wilayani Mererani na Musa Mangu mkazi wa Shangarai kwa Mrefu Arusha, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza.

Washitakiwa wote saba waliondolewa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa askari wenye silaha za moto wakiwa ndani ya gari lenye namba za usajili T 743 ADC lenye vioo vyeusi.

Msuya aliuawa Agosti 7 mwaka huu saa 6:30 mchana kwa kupigwa risasi 13 kifuani, kando ya barabara kuu ya Arusha – Moshi katika eneo la Mjohoroni wilayani Hai.

Friday, September 13, 2013





 Mkurugenzi  Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania ( TGNP) U ssu Mallya

Na,Alpius Mchucha—Namtumbo

BAADHI ya wanawake wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,wamesema wangetamani  siku moja kuona katika katiba ijayo kunakuwa na kipengele maalum cha kuwabana wanaume wanaowakashifu wanawake kwa kutaja sehemu za siri za wanawake hao kwani tabia hiyo imekuwa ikiwadhalilisha sana kwa jamii na kuwavunjia heshima na utu wao.

Wakizungumza katika mdahalo wa siku moja jana uliowakutanisha wanawake zaidi ya 50 kutoka katika vijiji mbalimbali  vya wilaya hiyo wanawake hao walisema,wameshachoshwa na matusi yanayotolewa na wanaume ambayo yanataja sehemu za mwili wa mwamke hivyo ni lazima  kutafuta njia ya kukomesha kwakuwa matusi hayo yamewafanya kuonekana kama siyo watu wanaotoa mchango kwa jamii na  nchi.

Mdahalo huo wenye lengo la kujadili,kubadilishana uzoefu, kujifunza masuala ya  kijinsia na elimu ya uraia uliandaliwa kwa pamoja na shirika lisilokuwa la kiserikali la Oxfam na mradi wa kuwawezesha vijana wa Restless Devolopment ulifanyika katika ukumbi wa Parokia mjini Namtumbo.

Mmoja wa wanawake hao Christina Kuhimini alisema, sasa wameshachoshwa na  udhalilishaji dhidi yao  hivyo kuiomba serikali kutokuwa na huruma na watu hao  wasiokuwa na hata  chembe ya aibu ambao kila kukicha wanatafuta maneno mapya ya  kuwakashifu wanawake licha ya kutambua kuwa bila ya  mwanamke  basi hata wanaume hao wasingeweza kutokea hapa Duniani kwa kile alichoeleza kuwa hakuna binadamu anayeweza kuzaliwa na mwaume bila ya kuwa na mwanamke.

“bahati mbaya sana muda wa kutoa maoni kwa ajili ya katiba mpya umekwisha,lakini kupitia vyombo vya habari vilivyopo hapa leo naomba  sana watufikishie ujumbe wetu sisi wanawake wa Namtumbo tumechoshwa sana na matusi yanayotolewa na wanaume kila siku,tena ni mibaba mizima nayo utoa lugha za kuwakashifu wanawake ambao hawana hatia yeyote,ili siyo jambo jema hata kidogo ni baya linalowadhalilisha wanawake”alisema.

Aliongeza kuwa,  tabia hiyo  ya matusi licha ya kutaja maumbile ya ndani ya mwanamke lakini kwa bahati mbaya sana imekuwa ikiwarithisha watoto wadogo wanaohitajki kusikia au kufundishwa matendo  mazuri kutoka kwa watu wazima,lakini cha kushangaza hakuna hatua inayochukuliwa hivyo kuendelea kuota mizizi na kuonekana kama jambo la kawaida.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtandao wa polisi wanawake  na mratibu wa dawati la jinsia mkoani hapa Mrakibu wa jeshi la  polisi Anna Tembo alisema tatizo kubwa lililopo ni  wazazi kushindwa kuwafundisha maadili mema watoto wao tangu wakiwa wadogo hivyo kujikuta wakiiga tabia mbaya za mitaani ambazo hazina misingi bora kwao.

Pia amewataka wanawake kubadilika na kuanza kujitambua kwa kutojihusisha katika matukio yanayowafedhehesha ambayo yanawafanya kuonekana vituko kwa jamii ya kistaarabu na ambayo kwa kiasi Fulani yanawapa kiburi wanaume kufanya watakalo kwa wanawake.

Tembo alieleza kuwa,wanawake wengi wanafanya matukio   ambayo ndiyo yanayowapa hamasa wanaume kufikiria kuwa mwanamke ni chombo cha kutumika vibaya badala ya pambo ndani ya nyumba na kuendelea kuwafanyia unyama wa kila aina akina mama.

Alitaja uvaaji wa nguo fupi,  zinazobana na zinazoonesha maumbile yao,kucheza shoo nyakati za usiku katika sehemu za starehe,kujiuza, na hata ukatili kwa watoto navyo ni sababu kubwa ya kudhalilika kwao.
                 MWISHO

Wednesday, September 11, 2013

WANAJESHI WAJERUHI RAIA, KAMANDA AKANUSHA




Na Julieth Mkireri, Kisarawe

MKAZI wa Tondoroni, Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani, Omary Mohamed (47), amejeruhiwa kwa kupigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa ni wanajeshi katika mapishano yanayodaiwa kuhusiana na kugombea mpaka.

Tukio hilo lilitokea juzi, majira ya saa 3 asubuhi baada ya wanajeshi hao kutembelea katika eneo lao na kukuta familia moja ikiwa imejenga nyumba katika eneo ambalo linadaiwa kuwa ni mali ya jeshi.

Inaelezwa wanajeshi hao walijaribu kuzungumza na familia hiyo kwa kuwasihi kuondoka, lakini hali hiyo iliibua mzozo mkali kutokana na wanafamilia kukaidi amri hiyo.

Hata hivyo, baada ya kuona hakuna maelewano, ghafla Mohamed alipigwa risasi moja na watu hao wanaodaiwa kuwa wanajeshi.

Baada ya tukio la kupigwa risasi kwa mwananchi huyo, wanajeshi hao walitokomea kusikojulikana na ndipo wananchi waliamua kufunga barabara hadi polisi walipofika na kwenda kutuliza ghasia.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei, amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema majeruhi huyo amepigwa na kitu chenye ncha kali na kuwa bado haijajulikana kama waliomjeruhi ni askari ama la na kama amepigwa na risasi.

Alisema kuwa kwa sasa anafanya mawasiliano na kiongozi wa jeshi ili kubaini ukweli kama ni askari wa jeshi na wametumwa kwenda kwa wananchi hao au walikwenda wenyewe.

Kamanda Matei alisistiza kuwa si rahisi kumtambua askari kwa kuwa tu amevalia sare za polisi lakini pia ni lazima namba za wahusika zijulikane, kambi gani na uthibitisho kutoka kwa kiongozi wa jeshi kwani baadhi ya watu huvalia mavazi hayo kwa manufaa binafsi.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Peter Datani, amekiri kumpokea majeruhi huyo akiwa na jeraha kwenye mguu wake wa kulia, na hali yake inaendelea vizuri.

Saturday, August 3, 2013

ENG, STELLA MANYANYA AMETHIBITISHA UONGOZI WAKE RUKWA

Na, Stephano Mango, Songea

SIKU za hivi karibuni  nimebahatika kufuatilia mambo mawili huko Mkoani Rukwa ambayo leo nakusudia kuwajuza wasomaji wa andiko la Ukanda wa Uranium popote pale mlipo kwani naamini bila kueleza nitakuwa sijawatendekea haki wasomaji na wapenzi wa Viongozi ambao wanafanya vyema kwenye Serikali hii ya awamu ya nne

Mambo hayo ni uandikaji wa kitabu cha Sumbawanga Ng’ara na uanzishaji wa Makumbusho ya Mkoa wa Rukwa iliyopo ndani ya jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambaye kwa sasa ni Mhandisi Stella Martin Manyanya(MB)

Nimebahatika kutembelea Mkoa huo na kuona Makumbusho hayo pamoja na kukisoma kitabu hicho  kizuri cha Sumbawanga Ng’ara ambacho kimeandikwa na Mkuu wa Mkoa huo

Licha ya mambo mazuri mengi ambayo yanapaswa kuelezwa kwa wananchi ili waweze kubadili mwenendo wao katika uendeshaji wa jamii zinazotuzunguka , leo mie nakusudia kueleza haya mawili ya kuhifadhi mazingira na kumbukumbu za maeneo yetu

Viongozi wengi nchini wanapenda kufanya vitu vya muda mfupi ambavyo vina maslahi kwao na havionekani kwenye  jamii pana wala havishikiki na kusababisha kutokikidhi dhana ya Uongozi kwa maslahi ya Umma

Naamini kuwa sifa za kiongozi bora ni miongoni na kuwa kiongozi wa vitendo na sio madaraka, kuwa na uwezo wa kushawishi watu ili kufanikisha jambo bora kwa manufaa ya watu na kuleta matokeo yanayotarajiwa

Uongozi ni mchakato wa kujua njia, kuonyesha njia, kutembea katika njia hiyo ili kufikia lengo kusudiwa mahali na wakati husika, uongozi ni kipaji na taaluma, ingawa wahenga wanasema kuwa “Kiongozi mzuri ni yule asiyependa kuwa kiongozi , lakini kutokana na uzembe wa viongozi waliopo, anashawishika  na kuamua kuwa kiongozi” 

Licha ya kuwa uongozi ni utumishi lakini sio ubwana na pia uongozi ni vitendo na sio madaraka, hivyo uongozi unahitaji nia thabiti na moyo wa kujitolea kwa kutumia taaluma na kipaji ulichonacho

Na katika maisha ya binadamu miongoni mwa mambo muhimu ni utamaduni na mazingira ambayo yanamzunguka katika kuimarisha uhai wake, na ndio maana mie leo nakusudia kuzungumzia kitabu cha Sumbawanga Ng’ara na uanzishaji wa Makumbusho katika Mkoa wa Rukwa

Leo nakusudia kumpa ushindi wa kiuongozi Mhandisi Stella Martin Manyanya kuwa ni kiongozi ambaye ameweza kukidhi malengo ya yeye kuwa Mkuu wa Mkoa wa kwanza Mwanamke Mkoani Rukwa na hasa kwa mambo ambaye ameyafanya katika mkoa huo katika Nyanja zote

Ni mengi mno aliyoyafanya lakini kama nilivyosema kuwa kwa leo nayazungumzia hayo mawili na nikipata muda mwingine nitayazungumzia mengine ambayo nayo yanafaida kwa wananchi na mustakabali wan chi yetu

Mhandisi Manyanya amethubutu kuwa ni Mkuu wa Mkoa wa kwanza kuandika kitabu cha mazingira katika eneo lake na pia amekuwa wa kwanza kuanzisha Makumbusho katika Mkoa wake tangu wakuu wa mikoa wapya katika awamu zote mbili za Uongozi wa Rais Jakaya Kikwete walipoteuliwa

Katika hali ya kumpongeza Mkuu huyo Manyanya mzaliwa wa Mkoa wa Ruvuma, Wilaya mpya ya Nyasa katika Kata ya Kihagara nayazungumzia mambo hayo  mawili aliyoyaasisi katika Mkoa wa Rukwa toka alipoteuliwa mwaka 2011 ambayo matokeo yake tumeyaona

Kitendo chake cha kuandika kitabu cha Sumbawanga Ng’ara kimefufua na kuanzisha moyo mpya wa uhifadhi mazingira kwa wadau mbalimba , pamoja na kupendesha mji kwani ukienda katika mitaa ya Sumbawanga usiku imekuwa kama mchana. Hii ni kutokana na ushirikishwajiu wa wadau mbalimbali katika uhifadhi wa mazingira kama vile Vodacom, Tigo, na wengine

Katika mambo yalioredheshwa kwenye cha Sumbawanga Ngara kwani uchafuzi uliopo unaoendana na kusambaa kwa taka ngumu umeleta athari kubwa kwa viumbe hai ikiwemo binadamu, wanyama wanyonyeshao na wasionyonyesha, wadudu ambao wengine ni muhimu katika maendeleo chanya ya ardhi,

Kuongezeka kwa mmomonyoko wa ardhi unaosababisha vina vya maji kupungua katika maziwa kama Rukwa na Tanganyika na kukauka kwa baadhi ya mito , Utiririshaji wa maji taka yenye viashiria vya sumu au sumu kamili vinavyotokana na mabaki ya bidhaa za viwandani zimekuwa na athari kwa viumbe hai waishio nchi kavu na majini na kusababisha kupungua kwa wanyama na baadhi ya aina za samaki,  na wengine kubadilisha hata ladha yao ya asili.

Kwa ujumla wake uharibifu huo umechangia kwa kiwango kikubwa mabadiliko ya tabia nchi hususan, hali ya hewa katika baadhi ya maeneo, na hivyo  kubadili uzuri wa asili na kupoteza baadhi ya vivutio.

Mfano ni kuhama kwa wanyama na ndege katika maeneo yao ya asili, kukauka kwa maporomoko ya maji na kadhalika.Uharibifu unaoendana na taka umesababisha miji  ya maeneo ya Mkoa huo kuwa michafu na isiyovutia, milipuko ya magonjwa kama kuhara na kipindupindu, magonjwa ya ngozi kama upele, kudumaa kwaafya, kimsingi watu kuwa na afya hafifu na vifo. Matumizi ya dawa yamekuwa ya kiongezeka, gharama kubwa kwa ajili ya kutoa huduma za afya, kushuka kwa kipato kutokana na kupoteza nguvu kazi, au kuwa na nguvu kazi hafifu na kwa ujumla wake kuongezeka kwa umaskini uliokithiri hasa katika miji

Kitabu hicho ambacho kimezinduliwa na Waziri Mkuu  Mizengo Peter Pinda (Mb kinatoa mwongozo wa kufanikisha Mpango wa Sumbawanga Ng’ara kwa faida ya watanzania wote nchini

Ni muhimu kukisoma na kukielewa kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijacho kwani malengo yake ni kuona kuwa jamii ina ishi katika mazingira safi na salama , kwani hakuna maisha katika mazingira machafu na yenye viashiria vya hatari katika pumzi ya binadamu, leo ukifika Rukwa unakutana na mabadiliko mengi katika uhifadhi wa mazingira

Jambo jingine ambalo nimekusudia kulisema leo ni juhudi za Manyanya kuanzisha makumbusho katika Mkoa wa Rukwa Kwani Makumbusho ni sehemu ambayo watu wanaweza kujifunza namna ya uhifadhi bora wa mazingira kwa kuangalia watu wa kale walivyoweza kunufaika na mazingira yaliyowazunguka na mali asili zilizokuwepo kwa kupata dawa za miti shamba,chakula na vitoweo

Kupitia Makumbusho wananchi wanaweza kujifunza wajibu wao kwa nchi yao na jamii nzima inayowazunguka kwa kuangalia Mashujaa wa kale waliojitoa kwa moyo kupigana kwa ajili ya uhuru wa nchi,ulinzi na usalama wa mali zao

Uwepo wa Makumbusho ni jambo la kujivunia kwani yanaweza kutumika kujenga amani katika jamii ya watu wanaoishi kama ndugu na marafiki kwa kuangalia maisha ya watu wa kale walivyoishi kwa kushirikiana katika mambo yaliyokuwa yanawahusu wao na jamaa zao
Pia ni sehemu ambayo huwakutanisha watu wa mataifa mbalimbali wanaokuja kuzitembelea na kujifunza historia na tamaduni zetu hivyo kuifanya dunia kuwa mahali padogo kwani vitu wanavyojifunza hupelekwa nchi za mbali na kujulikana kwa watu wa mataifa mbalimbali
Nakufanya kuwa kiungo cha mabadiliko na maendeleo ya Taifa kwani kupitia Makumbusho watu wanaweza kujifunza umuhimu wa mabadiliko na umuhimu wa kila mmoja kujiletea maendeleo kwa kuangalia namna mwanadamu alivyopitia hatua mbalimbali za mabadiliko mpaka kufikia hatua tuliyopo hivi sasa
Kukuza amani na kuchangia kwa ufanisi zaidi katika kujenga amani Dunia,  Makumbusho yanaweza kuandaa midahalo, kuonesha filamu, jitihada za utafiti, matembezi, mikutano ya amani na maonyesho ya utalii
Ni sehemu ambayo huvuta watalii,hukuza sayansi,hushangaza/kustaajabisha,kuelimisha,kuburudisha na hutia chachu ya uwajibikaji kwani ndani yake yana kumbukumbu zilizohifadhiwa hivyo makumbusho ni historia inayoishi
Uwepo wa Makumbusho ni wasaa wa kutafakari sisi wenyewe maisha yetu hivyo tunapaswa kuweka juhudi za kutunza makumbusho zilizopo na zinazoendelewa kujengwa
Suala la kutunza Makumbusho ni tete kulibinafsisha kwani linabeba utamaduni na utambulisho wa Taifa au jamii husika, hivyo zinawezwa kutunzwa na mtu binafsi kwa maendeleo yake, taasisi au Taifa lakini kuwepo kwenye taasisi ya umma ni kufanya uhai uendelee kuwepo
Mchango wa Tanzania kwenye tamaduni za nchi za Ulaya ni mdogo mno na hajulikani vyema, japo tumeshuhudia watu wa mataifa mbalimbali wamekuja kujifunza tamaduni, ingawa kila siku tunaendelea kutothamini utamaduni wetu kwa kuendelea kuiga tamaduni za nje bila sababu za msingi
Utamaduni wa jamii za Watanzania unastahili kukuzwa,kutangazwa na kusimamia ili nasi tuweze kuchangia utamaduni wetu kwenye mataifa mengine na ustaarabu wa ulimwengu, hivyo utambulisho binafsi na wa pamoja, kati ya kumbukumbu na historia
Makumbusho ni benki ya kumbukumbu licha ya kuwa ni sehemu ya kuelimishana na kuburudisha, pia makumbusho ni kumbukumbu ya fikra, kazi,maisha,mtazamo wa matukio ya watu mbalimbali, Viongozi na wananchi wengi leo, kuna kila kila sababu ya wananchi  kutembelea na kuikuza Makumbusho yao kwa maslahi ya vijazi vilivyopo na vijavyo
Leo wakazi wengi wa Rukwa wanatembelea Makumbusho hayo kwa kasi kwani yamekuwa ya kwanza kuanzishwa katika mkoa huo licha ya kuwa ni Makumbusho ya kipekee katika mikoa yote nchini
Nimalizie makala yangu kwa kusema tunawajibika kuwaiga na kuwaenzi viongozi wenye nia ya dhati ya kusukuma guruduma la maisha ya jamii mbele, wakiwa hai au wakitangulia mbele ya mwenyezi Mungu
Mtazamo wangu na wako ndio unaotengeneza uhai wa Makumbusho na mazingira ya taifa letu, hivyo tuamue kuwa chombo cha mabadiliko kwa kuwaelimisha na kuwahamasisha umuhimu wa utamaduni, mazingira na makumbusho kwani utambulisho una uwezo mkubwa wa kuakisi maendeleo kusudiwa
Kama Mhandisi Stella Manyanya alivyomnukuu Mwandishi wa Marekani Hellen Keller alisema kwamba, “Peke yetu tunafanya machache, pamoja tunafanya mengi.” Tukijitoa sote kufanya kazi kwa bidii, ufahamu na maarifa hata yale yanayoonekana hayawezekani yatawezekana na hata yale yanayoonekana  magumu yatakuwa mepesi
Maandishi haya yatuongezee nguvu ya kuanza safari yetu ya kuhakikisha  kuwa  Sumbawanga ina Ng’ara na Halmashauri nyingine za Rukwa zifuate na maeneo mengine nchini nayo yanapaswa kuiga kwa nguvu kubwa
Hakika siwezi kukuzuia kusoma  maandishi yenye  tija kwako, kwa maana ya kuwa siwezi kuzuia sikio lako kusikia lakini naweza kuzuia mdomo wako usiseme,  nami kwa uhakika naweza kuzuia mkono wangu usiandike zaidi lakini siwezi kukuzuia wewe kusoma  uthubutu wa kiuongozi wa Mhandisi Manyanya kwani ameonyesha njia na wengine wanapaswa kujipanga na kuonyesha uongozi tarajiwa kwa faida ya wananchi wanaowaongoza na Taifa kiujumla, na hakika uongozi hauna  jinsi
Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana, 0715-335051
Barua pepe;stephano12mango@yahoo.com
www.stephanomango.blogspot.com