About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Wednesday, August 8, 2012

WAZEE WAITAKA SERIKALI KUTUMIA BUSARA MGOGORO NA MALAWI


Na Stephano Mango, Songea
WAZEE nchini wameitaka Serikali kutumia busara na hekima katika kutatua mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa ulioibuliwa kwa mara nyingine tena na viongozi wa nchi ya Malawi hivi karibuni na kusababisha hofu miongoni mwa jamii ya watanzania
Wito huo umetolewa jana na Katibu Mkuu wa mtandao wa Kinga Jamii Tanzania Iskaka Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa
Msigwa alisema kuwa mgogoro huo toka umeibuliwa na nchi ya Malawi na viongozi wetu kuendelea kutoa matamko makali kuhusu jambo hilo kumeendelea kuzua hofu miongoni mwa jamii ya wazee, wanawake na watoto
“ Penye hofu na wasiwasi, hapana amani wala usalama miongoni mwa jamii kutakapopelekea ukosefu wa maendeleo hivyo ni lazima serikali ikawa makini kwa kujiimarisha kijeshi mipakani licha ya kuitaka jambo hili kumalizwa kwa busara kwani adui anayetuchokoza ana malengo na ajenda zaidi ya Ziwa Nyasa kama tunavyodhani"alisema Msigwa
Alisema kuwa Serikali inawajibika kumaliza mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo ili nchi hizo ziendelee na mahusiano yaliyokuwepo toka awali badala ya kufikiria vita ambavyo vitaleta maafa makubwa kwa wazee, wanawake na watoto kwani jambo hilo halihitaji kupimana ubavu
Alieleza kuwa inawezekana kabisa mgogoro huo ukamalizika pasipo umwagaji wa damu au upotezaji wa maisha ya watu kwa vita badala yake watumie busara kwa kuangalia ramani zilizopo kwenye taarifa mbali mbali za miaka ya enzi za ukoloni hasa zilizoko kwenye maktaba wakati Tanzania inaitwa Tanganyika; na Malawi inaitwa Nyasaland ukweli kuhusu mipaka yetu utapatikana.
MWISHO

Tuesday, August 7, 2012

NGOMA ACHAGULIWA KUWA MAKAMU MWENYEKITI WA NAMTUMBO

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Namtumbo Titus Ngoma
Na Stephano Mango, Songea
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wamemchagua Titus Ngoma kwa kura 24 kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo atakayeongoza kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia agosti mwaka huu
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha  Baraza la Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Stivin Nana alisema kuwa Madiwani katika halmashauri hiyo wapo 24 na wote kwa ujumla wao wamemchagua Diwani wa Kata ya Kitanda kushika nafasi hiyo
Nana alisema kuwa sheria na kanuni za mabaraza ya Madiwani zinasema wazi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri akichaguliwa ataongoza kwa kipindi cha miaka mitano, lakini nafasi ya Umakamu Mwenyekiti na Kamati mbalimbali za Madiwani zinachaguliwa kila baada ya mwaka mmoja
Alisema kuwa awali nafasi hiyo ilikuwa inashikiliwa na Diwani wa Kata ya Hanga Kassim Ntala ambaye aliongoza nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja na kwamba awamu hii hakugombea tena nafasi hiyo
Alifafanua kuwa mchakato wa kumpata Ngoma ulianza ndani ya Chama cha Mapinduzi (Ccm) Wilaya ya Namtumbo na kupelekwa Ccm mkoa wa Ruvuma na kurudishwa kwenye Wilaya kwa ajiri ya uchaguzi wa kumpata mgombea mmoja kwani wagombea walikuwa watatu ambao ni Daniel Nyambo ambaye alipata kura 4, Gidion Mpilime alipata kura 6 na Titus Ngoma alipata kura 14 ndani ya chama na kwamba ndani ya Baraza la Madiwani alichaguliwa kwa kura 24
MWISHO

Sunday, August 5, 2012

NANI ANAMWAMINI WAZIRI MKUU AU RAIS

 
        Na Ansbert Ngurumo
KATIKA miaka saba aliyokaa madarakani, Rais Jakaya Kikwete anajivunia mambo kadhaa mbele ya Watanzania. Kwanza, “ameua” chama chake. Pili, amedhoofisha Bunge. Tatu, amethubutu kuiweka mahakama mfukoni mwa serikali. Nne, ameonyesha ubabe uliokithiri kwa “kuziba midomo” ya vyombo vya habari. Amebakiza nini?
Niliwahi kusema huko nyuma kwamba Watanzania walidanganywa na tabasamu la JK mwaka 2005. Wapo pia waliozuzuka kwa utanashati wake. Wengine walikumbwa na wimbi kali la mkakati wa wanamtandao. Wapo pia waliomshabikia kwa sababu ya ushawishi wa fedha.
Leo watu hawa wanasikitikia au wanafurahia uamuzi wao? Waliomwingiza JK madarakani CCM kikiwa imara; waliomkabidhi uenyekiti wa chama hicho kikitambia ushindi wa kishindo; leo wanajivuna kwa yaliyokipata CCM kwa miaka saba mfululizo?
Je, chini ya Kikwete, wana CCM wana jeuri tena ya kuzungumzia ushindi wa kishindo huko tuendako?
Wale waliomkabidhi serikali ikiwa na hazina imara; ambayo hata yeye alikiri hadharani kwamba ameachiwa mahali pazuri la kuanzia; leo wanapomsikia yeye na mawaziri wake wakilalama kwamba serikali haina pesa, wanamwelewa? Nani ametafuna hazina yetu?
Wanaokumbuka jeuri ya Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta; wakatafakari jinsi alivyoingia kwa mbwembwe na kuondoka kwa kishindo cha aibu iliyoasisiwa na watu wake wale wale waliomwingiza; wanapopima utendaji wa spika aliyepita na wa huyu aliyepo; wanajivuna kwamba Bunge linafanya kazi yake iliyokusudiwa?
Katika mazingira ambamo spika amejigeuza sehemu ya serikali; kwa jinsi anavyoitetea na kuilinda bungeni kuliko hata waziri mkuu; katika mazingira ambamo spika naye anashiriki katika vikao vya chama na serikali vya kunusuru chama au serikali katika masuala mazito, hata yenye kashfa; nani anakataa kwamba waliomwingiza na kumwondoa Sitta, na baadaye kumweka Anne Makinda walikuwa na malengo machafu?
Bahati nzuri, katika utendaji wa Makinda, Watanzania wameanza kuelewa maana ya hoja yetu ya siku nyingi, kwamba spika wa Bunge asitokane na chama cha siasa; au akitokana na chama, mara tu baada ya kushika wadhifa huo, ajivue uanachama, awe kiongozi huru.
Si hayo tu. Hata mfumo wetu wa mahakama umeingiliwa na serikali. Nimewahi kuhoji staili ya sasa ya jinsi serikali kutumia mahakama kuzima madai nyeti ya wafanyakazi wake. Ilianza kuzitumia kuzima madai ya wafanyakazi wa serikali. Juzi juzi ilizitumia tena kuzima madai ya madaktari. Sasa imezitumia kuzima madai ya walimu.
Mahakama haikutoa “haki” kwa watumishi hao; bali imewatisha kwa kuwalazimisha kuripoti sehemu zao za kazi. Serikali haikutimiza madai yao. Tatizo limebaki pale pale! Wao na wananchi wanaendelea kulalamika. Serikali ya namna hii itadumu?
Hata kama madaktari wote wanakuwa kazini; hata kama walimu wote wataingia madarasani; tuna uhakika gani na ubora wa huduma zinazotolewa? Tuna uhakika gani na umakini wao kazini?
Huu ni uthibitisho mwingine kwamba serikali ndiyo inayoua mifumo ya afya na elimu. Wakubwa hawajali kwa sababu wakiugua hawatibiwi katika hospitali zetu; na watoto wao hawasomei katika shule zetu.
Viongozi wasiojali wananchi kwa kiwango hiki, wanaweza kutushawishi kwamba wana uzalendo na nchi hii? Wanaweza kuaminika kwa kauli zozote wanazotoa?
Tabia hii ya serikali ya JK ndiyo imewafanya wananchi wakose imani na uongozi wake. Siku hizi serikali haiaminiki kwa Watanzania.
Kwa miaka saba aliyokaa madarakani, wananchi wameanza kuona mwisho wa utawala wa CCM. Haya ni maandalizi ya anguko la watawala, na mwanzo wa zama mpya chini ya utawala mpya, na mfumo mpya.
Na wana CCM ambao bado wana mishipa hai ya kisiasa, wanalitambua hili na wanatafuta jinsi ya kujinusuru, hata kama itabidi kukitosa chama chao cha sasa. Baadhi yao wamewahi kuniambia kwamba, kwa jinsi wanavyotazama mambo ndani ya CCM, Rais Kikwete amefika mwisho wa safari yake ndefu.
Amepata alichotafuta kwa muda mrefu. Ameridhika. Hajali kama serikali inadhoofika, na haiaminiki. Hajali kama chama chake kinakufa. Baadhi yao wanasema wameanza kutafuta mahali pa kuponea kisiasa, na kumwacha “afe na chama chake.”
Lakini, wapo pia wanaoamini kwamba JK hapendi kuangusha serikali wala kuua chama chake, bali analazimishwa na mambo mawili – uwezo wake mdogo kimenejimenti, na hitaji la wakati, baada ya miaka 50 na ushei ya utawala ule ule.
Hizi ni dalili za serikali inayoanguka. Tatizo ni kwamba inataka kuanguka na kila mtu, na kila kitu. Ndiyo maana haitaki kuona mahakama zikiwa huru; Bunge likifanya kazi yake kwa uhuru na uaminifu; na vyombo vya habari vikiwa huru.
Ni ajabu kwamba serikali, ambayo nayo inamiliki vyombo vya habari, yenye idara za habari kila wizara, yenye wataalamu kila eneo; badala ya kujibu hoja zinazoibuliwa na vyombo vya habari visivyo vya serikali, inakimbilia kuvifungia au kuvifuta. Woga!
Ni aibu kwamba serikali inayojitapa inazingatia utawala wa sheria, inashindwa kutumia mahakama kudai haki dhidi ya vyombo vya habari; au hata kuvipeleka mbele ya Baraza la Habari; badala yake inatumia mabavu ya sheria kandamizi kuvifungia na kuvifuta. Woga!
Inaweza kuvifungia sasa. Inaweza kupenyeza fikra chafu hata miongoni mwa wahariri wa vyombo hivi kuwagawa, ili wakose msimamo wa pamoja wanaponyanyaswa na serikali.
Lakini, ukweli ni kwamba vyombo hivi vinavyofutwa vina nguvu na ushawishi kwa umma, na vinaaminika kuliko serikali yenyewe, hata huko kifungoni vilikofungiwa.
Na bahati mbaya ni kwamba serikali haijui kuwa kadiri inavyojitahidi kuvifungia au kuvifuta, pole pole inaandaa mazingira ya kujifungia na kujifuta. Mara zote, mwisho wa serikali za kibabe ni mbaya.
Bahati mbaya zaidi, serikali inafungia vyombo vya habari, lakini haiwezi kufunga wala kufuta mawasiliano ya umma, hasa katika zama hizi zenye njia nyingi sana za kuwasiliana.
Na kadiri serikali inavyozidi kuwa katili, ndivyo umma unavyozidi kuamini kila kibaya kinachosemwa dhidi ya serikali yao.
Inaweza kukanusha tuhuma kupitia kwa waziri, waziri mkuu, au rais wa nchi. Lakini siku hizi nani anamwamini waziri mkuu au rais?

Friday, August 3, 2012

KIKWETE AMSAFISHA CHENGE, ASEMA HAKUNA RUSHWA KWENYE KASHFA YA RADA

 
                                    Rais Jakaya Kikwete
 Na Martin Malera

RAIS Jakaya Kikwete amevunja ukimya kwa kusema kwamba hakuna rushwa kwenye kashfa ya ununuzi wa rada kutoka nchini Uingereza.
Ingawa Rais Kikwete hakutaja jina, lakini kwa kauli hiyo ni dhahiri kwamba amemsafisha Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge (CCM), ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitajwa ndani na nje ya chama chake kuhusika na kashfa ya ununuzi wa rada kutoka Kampuni ya BAE- System.
Chenge, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, anatajwa kuhusika kutoa ushauri wa kisheria wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ushauri ambao unatajwa kuzingatiwa katika hatua za uamuzi.
Mwingine anayehusishwa na kashfa hiyo ni aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT) Dk. Idriss Rashid.
Pamoja na hao, wanatajwa wafanyabiashara wenye asili ya India, lakini ambao wanaishi/walipata kuishi Tanzania, Tanil Somaiya, ambaye alikuwa akimiliki kampuni ya uwakala wa simu ya Shivacom na Sailesh (Shailesh) Vithlani kuwa watu wa kati wa biashara hiyo.
Akijibu swali kutoka kwa mmoja wa wahariri aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa kwa waliohusika na ununuzi wa rada wakati chenji yake imesharejeshwa, Rais Kikwete alisema Serikali ya Uingereza iliyokuwa ikichunguza kashfa hiyo imebaini kuwa hakukuwa na rushwa katika ununuzi wa rushwa.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, uchunguzi wa Serikali ya Uingereza ulibaini kuwa kulikuwa na makosa ya uchapaji, lakini hakuna mtu aliyehusika kutoa wala kupokea rushwa.
“Kama Uingereza waliochunguza kashfa hiyo wamefika mahala wanasema kulikuwa na makosa ya uchapaji tu, mtu wenu mnamfikisha mahakamani kwa ushahidi upi?” alihoji Rais Kikwete.
Mchakato wa ununuzi wa rada, uliwahusisha watu wa madaraka na kada mbalimbali ambao ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair.
Blair anatajwa kuwa ndiye aliyemshawishi aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, Benjamin Mkapa, kununua rada hiyo kutoka Kampuni ya kutengeneza silaha ya Uingereza BAE-Systems. Wakati huo aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa, Clare Short, alikataa katakata Tanzania, moja kati ya nchi masikini kabisa duniani, kutumia sh bilioni 40 kununua rada katikati ya umasikini unaonuka.
Hata hivyo chenji hiyo ya rada, zaidi ya sh bilioni 75 zimerejeshwa nchini baada ya hati ya makubaliano baina ya pande zinazohusika kusainiwa.
Hati hiyo ilisainiwa kati ya Serikali ya Tanzania, Kampuni ya Uuzaji wa Silaha ya Uingereza (BAE - System), Ofisi ya Uingereza ya Kupambana na Ufisadi (SFO) na Idara ya Kimataifa ya Misaada ya Maendeleo (DFID).
Chenge mwenyewe huko nyuma alipata kuzungumzia suala hilo na hasa, kumiliki kwake kwa akaunti ya fedha nyingi nje ya nchi inayohusishwa na mlungula wa ununuzi wa rada.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Edward Hosea, alipata mara mbili kunukuliwa akisema Chenge hakuwa na kesi ya kujibu katika kashfa hiyo ya rada.
Kuhusu sakata la wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), iliyohusisha Kampuni ya Kagoda iliyochota sh bilioni 40, Rais Kikwete alisema suala haliko kwake bali mikononi mwa vyombo vya dola.
“Hili la Kagoda liko mikononi mwa vyombo vya dola, wanaendelee nalo,” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo Rais Kikwete alitamba kuwa serikali yake imejitahidi sana kupambana na rushwa kwa kuimarisha uwezo wa TAKUKURU.

Chanzo Tanzania Daima

Wednesday, August 1, 2012

CCM YAMSHUKIA TUNDU LISU

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, ya CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye

L Yadai orodha yake inalenga kupotosha tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge.
L Anataka kuwaokoa wa Chadema katika sakata hilo.
L Yasema tuhuma za rushwa kwa wabunge lisigeuzwe la kisiasa


NA MWANDISHI WETU
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimelaani juhudi zinazofanywa na baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kujaribu kupotosha na kuuficha ukweli juu ya tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge.

Akizungumza na waandishi a habari leo mjini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, ya CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alisema, zipo juhudi za baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kujaribu kulifanya suala la tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wabunge kuwa la kisiasa kwa malengo yao.

"Mfano mzuri wa juhudi hizi ni kitendo cha Tundu Lissu, ambaye ni mbunge wa Chadema na Mnadhimu Mkuu wa Kkambi ya upinzani Bungeni cha kutoa aliyoiita orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kufanya biashara na TANESCO na kwamba ndio watuhumiwa wa rushwa inayozungumziwa", Alisema Nape na kuongeza;

"Cha kushangaza orodha yake ilikuwa na wabunge wa CCM peke yake wakati wote tunajua kuwa yapo majina ya baadhi ya wabunge wa vyama vingine hasa Chadema, yanayotajwa katika orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa hii".

Nape alisema juhudi hizo za Lissu na wenzake zinalengo la kuuficha ukweli na kujaribu kuwalinda watuhumiwa wa uhalifu wanaotokana na Chadema.

"Tunamtaka Lissu na wengine wanaofanya juhudi hizo kuacha mara moja, na badala yake tuvipe nafasi vyombo vinavyohusika vichunguze na matokeo ya uchunguzi huo yatangazwe hadharani ili tuwajue wabunge waliotusaliti", alisena Nape.

Alisema CCM inalaani vitendo vya rushwa hasa vinapohusishwa na viongozi ambao wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa na kwamba rushwa ya namna hiyo inavuruga sana uchumi wa nchi, hivyo wanaohusika nayo haitoshi kuwaita wala rushwa tu bali ni zaidi ya wahujumu uchumi.

"Wakikithibitika ni muhimu hatua kali zichukuliwe kulikomesha kabisa hili na iwe fundisho kwa wengine", alisema Nape.

Nape alisema CCM inawapongeza watendaji wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini wakiongozwa na Waziri wao Prof. Sospeter Muhongo, Manaibu wake, Massele na Simbachawene na Katibu Mkuu, Maswi kwa uzalendo, ujasiri na umahiri wao mkubwa waliouonyesha kwa muda mfupi waliokaa kwenye wizara hiyo.

"Tunaamini uzalendo walioonyesha katika kusimamia wizara hii,utaigwa na watumishi wengine wa umma katika kuhakikisha matumizi mazuri ya rasilimali za nchi zinalindwa ili kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania yanatimia. Tunaunga mkono jitihada zao", alisema Nape.

Alisema, pia CCM inalipongeza bunge kwa kuendelea kusimamia serikali na rasilimali za nchi katika kuhakikisha nchi inapiga hatua kubwa ya maendeleo.

"Tunawaomba waheshimiwa wabunge wazidi kutanguliza masilahi ya taifa mbele na uzalendo mkubwa katika shughuli zao za kila siku", alimalizia.

mwisho

Monday, July 30, 2012

NAMI NILIVYOSHIRIKI MECHI YA YANGA NA AZAM

Mmiliki wa mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com , Stephano Mango akiwa kwenye uwanja wa Taifa kabla ya mechi kati ya Yanga na Azam
Mgombea Uwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma (FARU) Golden Sanga akiwa na Dickson kwenye uwanja wa Taifa wakishuhudia mechi kati ya Yanga na Azam
Mgombea Uwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma (FARU) Golden Sanga akiwa na Dickson kwenye uwanja wa Taifa kushuhudia mechi kati ya Yanga na Azam
Mgombea Uwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma (FARU) Golden Sanga akiwa na Dickson kwenye uwanja wa Taifa kushuhudia mechi kati ya Yanga na Azam
 Mgombea Uwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma (FARU) Golden Sanga akifurahia ushindi wa Yanga kutwaa kombe la Kagame nje ya uwanja wa Taifa

 
Wachezaji wa Yanga wakishangilia huku wakiwa na Kombe la Kagame, baada ya kutawazwa tena kuwa wafalme wa michuano ya soka ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kwa kuibwaga Azam FC mabao 2-0.
Kocha Mkuu wa Yanga, Tom akiungana na wachezaji kushangilia ubingwa huo

Mashabiki wakiungana na wachezaji wa Yanga kushangilia ubingwa huo
Mmiliki wa Blogu ya Michuzi, Muhidini Michuzi akiendelea kuchukua matukio
Ubao ulivyokuwa unaonekana baada fainali hiyo kumaliziki


Mshambuliaji wa yanga Said Bahanunzi akimtoka beki wa Azam FC Agrey Morris wakati wa mchezo wao wa Fainali ya Kagame Cup uliomalizika hivi punde kwenye uwanja wataifa jijini Dar es Salaam ambapo Yanga wameibuka na Ushindi wa mabao 2-0, huku Bahanuzi akipachika bao kwenye dakika za nyongeza za mwamuzi.
Mshambuliaji wa Yanga Hamis Kiiza Akimtoka Beki wa Azam Fc Jabir Azizi kabla ya kupachika bao la kwanza kwenye mchezo huo.
Mashabiki wa Yanga wakijimwayamwaya kwenye uwanja wa Taifa leo baada ya Said Bahanuzi kupachika bao la pili.
Wachezaji nao waliburudika kimtindo baada ya kupata ushindi.

Friday, July 27, 2012

SANGA ONE ALONGA KUHUSU KUGOMBEA NAFASI YA UWENYEKITI WA CCM WILAYA YA SONGEA

             Diwani Mstaafu wa Kata ya Bombambili Golden Sanga( Sanga One)

Na Stephano Mango, Songea
KADA wa Chama cha Mapinduzi(Ccm) Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Golden Sanga (Sanga One) ametangaza nia ya kugombea Uwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Songea katika uchaguzi ambao unatarajiwa kufanyika mapema mwezi Septemba mwaka huu
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea Golden Sanga alisema kuwa ameamua kugombea nafasi hiyo ili kuweza kurudisha heshima ya Chama cha Mapinduzi mjini hapa
Sanga alisema kuwa kila kukicha mvuto wa Ccm miongoni mwa jamii umekuwa ukipungua kutokana na matendo maovu yasiyokuwa ya kimaadili yanayofanywa na Viongozi wa chama hicho ambayo yamekuwa yakiwakatisha tamaa wananchi na wanachama wa chama hicho
Alieleza kuwa kutokana na hali hiyo kumesababisha kata 6 kati ya 21 kuchukuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Urais wa mwaka 2010
Alieleza zaidi kuwa amejipanga kikamilifu kwa kushirikiana na viongozi wenzake watakaochaguliwa kushika nafasi mbalimbali ndani ya chama katika uchaguzi unaoendelea kufanyika mwaka huu ili kuweza kukijenga chama na kuleta ushindi stahiki katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa 2015
Kwa mujibu wa taarifa ya Chama cha Mapinduzi Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuwa wagombea wana haki ya kutangaza nia za kugombea nafasi wanazozitaka ndani ya chama ambapo kwa nafasi ya uwenyekiti wa Wilaya fomu zinatolewa agosti 1 na kurudishwa ndani ya siku mbili ambapo uchaguzi unatarajiwa kufanyika mapema septemba
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa waliotangaza nia hadi sasa ni Gerald Mhenga ambaye ni Katibu wa mipango na uchumi wa Ccm Wilaya ya Songea na Golden Sanga ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho ikiwemo udiwani wa kata ya Bombambili katika halmashauri hiyo
MWISHO

Thursday, July 26, 2012

URAIS WAMTESA ZITTO KABWE

<>
<>
<>



<>
<>
<>
Asema ana uwezo,uadilifu kuwa Amiri Jeshi Mkuu
Na Edson Kamukara
HARAKATI za kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015 umeanza kuwatesa viongozi wa vyama vya siasa ambapo safari hii, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA (Bara), Zitto Kabwe, amesema kama akiandikiwa kuwa rais hakuna wa kumzuia.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alijitapa kuwa kama urais upo, utakuja tu, kwani ana uwezo, uadilifu na uzalendo wa kuwa Amiri Jeshi Mkuu.
Zitto ameibuka na kuzungumzia sakata la urais ikiwa ni siku moja tu imepita baada ya wabunge wenzake kulalamika na kukanusha taarifa za kumpigia debe kwa ajili ya urais mwaka 2015.
Wabunge hao, Halima Mdee (Kawe) na Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), waliandika barua za kulalamikia habari iliyochapishwa na gazeti moja la kila siku (si Tanzania Daima), wakidai liliwalisha maneno kuwa walimpigia debe Zitto wakiwa mkoani Kigoma kwamba anapaswa kuwa rais mwaka 2015.
Akichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Mawasilaino, Sayansi na Teknolojia jana mjini hapa, Zitto alitumia muda mfupi kufafanua sakata hilo lililozagaa kwenye vyombo kadhaa vya habari na kwenye mitandao ya kijamii.
“Tamasha letu la wasanii la Kigoma limeleta maneno maneno…lakini napenda kusema kuwa urais kama upo utakuja tu. Sina mashaka hata kidogo kwamba uwezo, uadilifu na uzalendo wa kuwa Amiri Jeshi Mkuu ninao,” alisema Zitto na kushangiliwa na wabunge wenzake.
Mjadala huo ulichukua sura mpya kwenye mitandao ya kijamii juzi ambapo baadhi ya watu walionekana kumlaumu Zitto, wakimhusisha na habari hiyo kuwa aliitengeneza mwenyewe kama sehemu ya kujiandalia mazingira hayo.
Zitto ambaye amekuwa akiandamwa mara kadhaa na wanasiasa ndani na nje ya chama chake, baadhi wakimtuhumu kuwa mamluki na wengine wakimwelezea kuwa ni mwanasiasa mwenye malengo makubwa hapo baadaye, alifafanua zaidi suala hilo kwenye taarifa yake kwa kusema:
“Katika gazeti la Mwananchi la tarehe 23 Julai 2012, kulikuwa na habari yenye kusomeka: ‘Wabunge wamsafishia Zitto njia ya urais 2015?. Habari hii imeleta mjadala mara baada ya kutoka na kusomwa. Mjadala umekuzwa zaidi baada ya wabunge, Halima Mdee na Joshua Nassari kukanusha maneno waliyonukuliwa kusema. Napenda kusema masuala yafuatayo:
“Moja, waheshimiwa wabunge Halima Mdee, Joshua Nassari, Kangi Lugola, Esther Bulaya, Deo Filikunjombe, Raya Ibrahim, Amina Mwidau na David Kafulila walihudhuria tamasha la vijana wa Kigoma All Stars kwa kualikwa na Mratibu wa kundi hilo, Mwasiti Almasi.
“Wabunge wengine walialikwa lakini hawakutokea wakiwamo Joseph Mbilinyi, David Silinde, Amos Makala, Vicky Kamata na Peter Serukamba. Wabunge hawa hawakualikwa na mimi na wala sikufanya mazungumzo nao yoyote ya awali au kuwaambia au kukubaliana nini cha kuzungumza au hapana. Tamasha lilikuwa la muziki na halikuhusika kabisa na siasa.
“Waheshimiwa wote walipewa nafasi ya kusalimia na wote walizungumza. Wabunge waliozungumza kwa muda mrefu kidogo ni ndugu Halima Mdee, Joshua Nassari, Deo Filikunjombe na Kangi Lugola.
“Hotuba za wabunge wote zilirekodiwa kwenye video neno kwa neno na video hizo zitawekwa wazi kwenye blogu yangu kama sehemu ya documentary ya tamasha lile la kihistoria.
“Pili, sikuhusika kwa namna yoyote ile na kuandikwa kwa habari hii iliyozusha mjadala. Wala sikujua kama habari hii ingeandikwa, maana katika ziara ile sikuita mwandishi hata mmoja, maana nilitaka liwe tukio la Kigoma tu.
“Kama mwandishi kaandika mambo ambayo wabunge hawa hawakuyasema basi itaonekana kwenye video hizo. Wabunge wenyewe wanajua kwenye nafsi zao nini walichosema Kigoma na kipi kiliwasukuma kusema waliyoyasema. Nisingependa kuhusishwa kwa njia yoyote ile na matamshi yao, habari iliyowanukuu na hata makanusho yao. Maana mwisho wa siku ukweli ndio utasimama.
“Suala la urais lisitupotezee muda kwani kuna mambo mengi sana ya kujadili kuhusu nchi yetu. Taharuki ambazo watu wanazipata masuala ya urais yanapotajwa zinashangaza sana.
“Chama changu bado hakijatangaza rasmi mchakato wa kupata mgombea urais. Hivi sasa chama hakina mgombea urais mpaka hapo mchakato utakapotangazwa, ambapo wanachama wataruhusiwa kuomba kupeperusha bendera ya chama. Mwanachama wa chama chetu atakaye kubalika na jamii na wajumbe wa mkutano wa uteuzi ndiye atakuwa mgombea wetu. Kwa sasa hayupo na hivyo tusipoteze muda kujadili jambo hili.
“Mzee Thabiti Kombo alituachia usia tunapokuwa tunazungumza. Alisema ‘weka akiba’ si akiba ya fedha, bali ya akiba ya maneno. Tuweke akiba ya maneno. Tusimalize yote.”
Hata hivyo akizungumza na gazeti hili mjini hapa jana mara baada ya Bunge kuahirishwa kwa ajili ya mapumziko ya mchana, Zitto alikanusha tuhuma hizo zinazomhusisha kuandaa habari hiyo akisema ni matusi kwa tasnia ya habari, hivyo kuvitaka vyombo vya habari kutowaendekeza wanasiasa wanaotukana waandishi na vyombo vyao.
“Ni upuuzi kudhani kwamba mimi naweza kuandaa habari kwenye gazeti hilo…nimeshangaa na wewe unaweza kuniuliza jambo hili…unaliamini?” alihoji Zitto.
Kuhusu habari hiyo inayolalamikiwa na wabunge wenzake kuwa ilipotoshwa, alisema kwamba haoni ubaya kwenye habari husika akidai hata hivyo mengi yaliachwa kuliko kuongezwa chumvi. “Hakuna aliyenukuliwa kwa ambalo hakusema. Tamasha zima limerekodiwa kwenye video”.
Kwa muda sasa kumekuwepo na mjadala juu za Zitto kuhusu kauli yake kwamba anautaka urais, jambo liliotafsiriwa kuwa ni mikakati ya kutaka kukivuruga chama chake kwa kikigawa kimakundi lakini Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, amekuwa akisema kila wakati kuwa ajenda yao kwa wakati huu si kujadili nani anafaa kugombea urais 2015 badala yake wanajikita kutatua kero za wananchi.

Chanzo Tanzania Daima

Tuesday, July 24, 2012

MWANAFUNZI AFA MAJI KATIKA LAMBO LA KUNYWESHEA NG’OMBE

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsimeki
Na Steven Augustino, Tunduru
MWANAFUNZI wa Darasa la nne katika Shule ya Msingi Majimaji Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma aliyefahamika kwa jina la Rehema Salum (12) amefariki dunia baada ya kutumbukia katika lambo la kunyweshea ng’ombe.

Mashuhuda wa tukio hilo wamedai kuwa marehemu alikubwa na mkasa huo wakati akijaribu kuogelea katika lambo hilo lililochimbwa na Idara ya magereza kwa ajili ya kunywesha Ng,ombe wa Gereza la Mifungo la Kilimo la Majimaji lililopo kijijini hapo.

Wakifafanua taarifa hiyo mashuhuda hao walidai kuwa katika tukio hilo marehemu alikuwa ameongozana na kundi la watoto wenzake kwa nia ya kwenda kuoga katika lambo hilo kama ambavyo hufanya siku zote na kwamba kilichotokea ni bahati mbaya iliyotokana na yeye kuogelea eneo
lenye kina kirefu.

Mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Rehema, Dkt. Mosses Mwahasunga alidai kuwa chanzo cha kifo hicho ni kukosa hewa kulikosababishwa na kunywa maji mengi.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsimeki mbali na kukiri kuwepo kwake alidai kuwa polisi wanaendelea na uchuinguzi tukio hilo.
Mwisho

Monday, July 23, 2012

MAVETERANI WA SIMBA WACHAPWA BAO MOJA NA MAVETERANI WA YANGA

 Maveterani wa Yanga wakiwa katika uwanja wa mazoezi ili kuweza kujiweka sawa katika mechi na Maveterani wa Simba

Mechi ambayo ilimalizika kwa kuichapa Simba bao 1 katika dakika ya 13 ya kipindi cha pili na mchezaji Kelvin Haule



 Wachezaji wa Maveterani wa SIMBA wakifanya mazoezi ili kuweza kuleta upinzani wa dhati katika mechi yake na YANGA




                     Mdhamini wa Mechi hiyo Golden Sanga (Sanga Transport) ambaye ni VETERANI WA YANGA
 Mdhamini wa Mechi hiyo Paskary Msigwa (Top One Inn) ambaye ni VETERANI WA SIMBA
 Mohamend Mchele (kushoto) akiwa na watazamaji wengine katika mechi hiyo
 wa kwanza toka kushoto ni Godfey Mvula, Peter Mhina na Amasha wakiwa na watazamaji wengine
 Washabiki wa Simba wakionyesha manjonjo yao katika uwanja wa Sokoine ambao mechi hiyo ilikuwa inachezwa jana
 Wachezaji wa Yanga Gerson Msigwa na Kabisama wakishusha pumzi wakati wa mapumziko
Methew Msigwa akiwa na wachezaji wenzake wakitafakari namna ya kuwafunga wapinzani wao wakati wa mapumziko ya kipindi cha kwanza

MKUTANO WA CCM MJINI KIGOMA

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI,) Aggrey Mwanri akihutubia, kwenye mkutano wa CCM uliofanyika, jana , Julai 22, 2012, kwenye Uwanja wa Community Centre, Mwanga mjini Kigoma.

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye akihutubia, kwenye mkutano wa CCM uliofanyika, jana , Julai 22, 2012, kwenye Uwanja wa Community Centre, Mwanga mjini Kigoma.

Waziri wa Nchi Ofsi ya Rais, Mahusiano, Steven Wasira akihutubia kwenye mkutano wa CCM uliofanyika, jana , Julai 22, 2012, kwenye Uwanja wa Community Centre, Mwanga mjini Kigoma.
Mamia ya wananchi waliofurika kwenye mkutano wa CCM katika Uwanja wa Community Centre, Mwanga mkoani Kigoma

Wazee kwenye mkutano wa CCM, Uwanjwa wa Community Cetre Mwanga Kigoma

Viongozi mbalimbali wa CCM waliohudhuria katika mkutano huo

AUAWA KWA TUHUMA ZA KUIBA KANISANI


Na Augustino Chindiye, Tunduru

WANANCHI wenye hasira wamempiga na kumuua kazi wa mtaa wa Kadewele mjini Tunduru mkoani Ruvuma aliyefahamika kwa jina la Nasoro Hashim (18) baada ya kutuhumiwa kuingia na kuiba katika nyumba ya Paroko wa Kanisa kuu lililopo katika Jimbo la Tunduru/ Masasi.

Mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa katika mkasa huo marehemu Hashim alikutwa na kidhibiti cha simu tatu za mkononi mali za viongozi wa Kanisa hilo.

Walisema katika tukio hilo marehemu alishtukiwa baada ya kuonekana wakati akitoka katika nyumba hiyo na Sista mmoja ambaye hawakutaja jina lake ambapo baada ya kugundua hali hiyo alipiga kelele za kuomba msaada na kulifanya kundi hilo kujitokeza.

Walisema baada ya kipigo hicho marehemu alikimbizwa katika hospitali ya serikali ya Wilaya kwa matibabu ambapo alifariki baada ya muda mfupi.

Mganga aliye ufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Hashim Dkt. Jeshi Daraja alisema kuwa chanzo cha kifo hicho ni kutokwa na damu nyingi kuliko sababishwa na kupasuka kwa fuvu la kichwa kulikotokana na kupigwa na kitu kizito.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsimeki, mbali na kukiri kuwepo kwa tukio hilo alisema kuwa Polisi wanaendelea na uchunguzi ili sheria iweze kufuata mkondo wake kwa waliohusika na tukio hilko.

Aidha kamanda Nsimeki alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi wa Mkoa huo kuachana na tabia za kuchukua sheria mikononi.
Mwisho

Sunday, July 22, 2012

WANANCHI WAPATA MASHAKA NA MKANDARASI WA UJENZI WA LAMI NAMTUMBO HADI TUNDURU

Na Steven Augustino, Tunduru SERIKALI imeombwa kuichukulia hatua kampuni ya progressive Constraction  iliyopewa kazi ya kujenga kwa kiwango cha Lami Barabara ya Tunduru hadi Namtumbo Mkoani Ruvuma zikiwa ni juhudi za Serikali kuiunganisha mikoa ya Kusini kwenye mtandao wa barabara za kiwango cha Lami.

Hayo yamesemwa na baadhi ya wananchi waliotakiwa kutoa maoni yao juu ya maendeleo ya Ujenzi wa Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 180 wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni. 180.66 ambazo ilipewa kampuni hiyo kwa makubaliano ya kuikamirisha katika kipindi cha miezi 27 inayoishia mwezi july 2013.

Wakifafanua maelezo yao walidai kuwa Mradi huo ambao hadi sasa umetimiza miezi 16 iliyopita kampuni hiyo bado haijakamirisha hata ujenzi wa kambi zao hali inayo onesha wazi kutokuwepo kwa matumaini ya mradi huo kukamirisha ujenzi wake hata ikipewa miaka 10 zaidi wakiwa na maana kuwa kampuni hiyo haina uwezo kwani hata vyombo haina.

Goerge Mrope, Fatu Alli, Mohamed Said na Adam Mkwanda ni miongoni mwa wananchi waliotoa maoni hayo na kudai kuwa endapo serikali haitachukua hatua za kuuokoa mradi huo na kuufanya ukamilike kwa wakati kuna hatari ya Chama tawala CCM kufanya vibaya katika matokeo ya uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 ambapo wapigakura hawatakuwa tayari kusikiliza la mtu na badala yake itakuwa ni kukisulubu tu.

Nao Madiwani Athuman Nkinde, Msenga Said na Mchungaji Wiliam Mazuguni katika maoni yao walionesha mashaka ya kuanguka kwa chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi huo kutatokana na wananchi wengi kuwa na uelewa hasa wakati huu ambao vyama vya siasa vya Chadema na CUF vinaendelea kujijenga na kuanza kuimung`unyua na kuwateka wanachi wa mikoa ya kusini ambako kumekuwa ni ngome kubwa ya CCM toka nchi hii ipate Uhuru.

Walisema ili kuokoa hali hiyo hatua madhubuti zinatakiwa kuchukuliwa na kufanyika kwa kazi ya ziada kwa dalili za kushindikana kukamilika kwa barabara hiyo katika kipindi kilicho pangwa zinaonekana kugonga ukuta kutokana na kampuni hiyo kuonekana kuifanya kazi hiyo kwa mwendo wa Kinyonga huku ikiwa imebakia miezi 11 ya kuikabidhi huku wakibainisha kuwa chanzo cha kuichelewa kukamirika kwa mradi huo ni uchakachuaji uliofanywa viongozi wa Wizara ya Ujenzi kutokana na kutoa kazi zote kwa mkandarasi mmoja badala ya kila kipande kupewa kampuni tofauti.

Kwa mujibu wa maelekezo ya Mikataba ya Barabara hiyo ilyogawanywa katika vipande vitatu, kipande cha Tunduru Matemanga Kilometa 58.70 Shilingi Bilioni. 63.41 kilipangwa kukabidhiwa mwezi July 2013, Matemanga Kilimasera kilometa 68.20 chenye thamani ya Shilingi Bilioni. 64.02 kilipanwa kukabidhiwa mwezi Mei 2013 na Kilimasera Namtumbo Kilometa 60.70 Chenye thamani ya Shilingi Bilioni.53.23 kilipangwa kukamilika mwezi march 2013.

Wakizungumzia hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Bakari Nalicho na Meneja wa wakala wa Barabara TANROADs Mkoa wa Ruvuma Eng. Abraham Kisimbo waliungana na wananchi hao kwa madai ya kutoridhishwa wala kufurahishwa na maendeleo ya Mradi huo na kuongeza kuwa serikali inajitahidi kwa kutumia nguvu zao zote kubanana na kusukumana kukabiri vitendo vya Mkandarasi wa kampuni hiyo na kuhakikisha kuwa barabara hiyo inajengwa.

Aidha Mwambungu aliwapongeza wakandarasi wanaojenga Bara bara za Songea/ Namtumbo kilometa 67.00 utakao ghalimu Shilingi Bilioni.62.88 na Peramiho/Mbinga kilometa 78.00 wenye thamani ya shilingi Bilioni.79.81 kuwa inaendelea vizuri na akaongeza kwa kuonesha mashaka ya mdororo wa ujenzi wa Barabara ya Tunduru/ Namtumbo kuwa huenda mradi huo ukapitwa na miradi mipya ya Barabara za Tunduru Mtambaswala Kilometa 202.5, Shilingi Bilioni.240.858 na Mbinga /Mbambabey kilometa 66.00 utakao ghalimu shilingi Bilioni.2.90.

Wakati hayo yakiendelea taarifa zilizovuja kutoka kwa wakaguzi wa Barabara hiyo waliotembelea Wilayani Tunduru July 12 mwaka huu zinadai kuwa kampuni hiyo hadi sasa imefanya kazi kwa asilimia 1 tu toka ikabidhiwe kazi hizo katika kipindi hicho cha miezi 16 iliyopita

MWISHO

Friday, July 20, 2012

MAVETERANI WA SIMBA NA YANGA SONGEA DIMBANI JULAI 22

Mdhamini  mkuu wa mechi ya Simba na Yanga Gorden Sanga (Sanga One) akizungumza na waandishi wa habari

Na Stephano Mango, Songea
MAVETERANI wa Simba na Yanga wa Kata ya Bombambili Halmashauri ya Manispaa ya Songea wameanza mazoezi kwa ajiri ya mechi ya kirafiki ambayo wanatarajia kucheza Julai 22 mwaka huu yenye lengo la kuboresha mahusiano ya kijadi
Akizungumza na waandishi wa habari jana Mdhamini mkuu wa mechi hiyo Gorden Sanga (Sanga One) alisema kuwa mavetani wamekuwa wakikutana vijiweni na kufanya ushabiki wa timu hizo ambazo zina mashabiki wengi bila nao kushiriki kucheza katika maeneo yao
Sanga alisema kuwa tayari wachezaji wa timu zote mbili wamesha sajiriwa kutoka katika pande zote za Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa ajiri ya mechi hiyo yenye ushindani mkubwa na majigambo ya pande zote mbili
Alisema kuwa kamati ya maandalizi imejipanga kikamilifu kwa mechi hiyo ambapo zawadi za mfungaji bora, mchezaji bora na kipa bora zimeandaliwa na zitatolewa siku hiyo kwa lengo la kuthamini mechi hiyo na kanuni bora za michezo
Alieleza kuwa siku ya mechi ulinzi utakuwa wakutosha ili kuweza kudhibiti vitendo vya fujo na uhalifu wowote ule ambao unaweza kutokea kutokana na Maveterani hao kutambiana sana kutokana na hamu ya mechi hiyo itakayofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Sokoine mjini hapa
Alifafanua kuwa mechi hiyo inadhaminiwa na wapenzi wa michezo mjini Songea ambao ni Sanga One Transport, Top One Inn Hotel na Redio Jogoo na kwamba amewataka washabiki wa michezo kujitokeza kwa wingi katika mechi, pia amewaasa wachezaji kucheza kwa amani na upendo mkubwa na mashabiki kushangilia bila kuleta vurugu kwani michezo ni amani
MWISHO