About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Thursday, June 16, 2011

TUWAJIBIKE KUZUIA UHARIBIFU WA MAZINGIRA NCHINI-MGOWOLE



TUWAJIBIKE KUZUIA UHARIBIFU WA MAZINGIRA NCHINI-MGOWOLE
 Na;Stephano Mango,Songea

NI wazi kuwa upatikanaji wa nishati ya umeme hapa nchini limekuwa ni tatizo sugu hali inayosababisha Watanzania wachache kutumia nishati hiyo na wengi kutumia mazao ya misitu kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku

Kwani kutokana na kukosa nishati ya umeme,wananchi wengi Mijini na Vijijini wanatumia nishati inayotokana na misitu kama vile kuni na mkaa kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwamo kupikia.

Matumizi ya mazao ya misitu yamesababisha kuwapo na uharibifu wa mazingira kutokana na wananchi wengi kukata miti ovyo bila kupanda mingine.

Akizungumza na gazeti hili Ofisini kwake hivi karibuni Afisa Misitu wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Robart Mgowole anasema kuwa mazingira ni jumla ya vitu vyote vinavyomzunguka mwanadamu vikiwamo mimea,maji,hewa, miundombinu, ardhi na vingine vingi. Kwa hiyo unapozunguzia mazingira unamgusa binadamu moja kwa moja.

Mgowole alisema kuwa  mazingira ni msingi wa maisha ya binadam na ukuaji wa uchumi wa nchi kwenye maeneo ya rasilimali kama vile misitu,uvuvi,kilimo,wanyamapori,makazi,maji na nishati

Alisema kuwa maisha ya binadamu na viumbe hai wengine hutegemea mazingira na uoto wa asili katika kujiletea maendeleo kwa kutambua hilo, uboreshaji wa mazingira ni jambo la lazima kwa kila mdau wa mazingira

Alieleza kuwa ukataji  wa miti, uchafuzi wa maji na matumizi mabaya ya ardhi ni miongoni mwa uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na binadamu katika maisha yake ya kila siku na hivyo huathiri pia viumbe hai na visivyo hai.


“Kutoweka kwa uoto wa asili kama vile miti,nyasi na hata viumbe vinavyoishi majini na ardhini,kutokea kwa ukame na milipuko ya magonjwa  mbalimbali kama vile kipindupindu na uti wa mgongo ni miongoni mwa matokeo ya uharibifu na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na binadamu katika shughuli zake.”alisema Mgowole


Alisema kuwa binadamu anapofyeka msitu ajue moja kwa moja kuwa anaharibu vyanzo mbalimbali vya maji na mvua hali ambayo itamfanya binadam mwingine asafiri  masafa marefu kutafuta maji ambapo zao tokeo ni kupata maumivu makali kutokana na umbali mrefu


Alieleza kuwa misitu ikifyekwa  na mahali pakaathirika kutakuwa na madhara makubwa katika eneo husika yakiwemo kukwama kwa shughuli za uzalishaji mali kama vile kilimo na ufugaji ambapo hapa nchi ndiyo uti wa mgongo wa Taifa letu kwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania hutegemea kilimo na ufugaji katika kuendeshea maisha yao .

Afisa huyo alisema uharibifu mwingine wa mazingira unatokana na kilimo cha kuhama hama,ujenzi wa viwanda,matumizi ovyo ya mitambo,utupaji wa taka ovyo na kufanya biashara ya mazao ya misitu bila kufuata sheria,kanuni na taratibu zilizopo.

Kutokana na hali hiyo inakadiriwa tangu kipindi cha mwaka juzi hapa nchini eneo la misitu linapungua kwa kasi ya hekta 91,000 kutokana na shughuli mbalimbali za binadamu sizizo zingatia utunzaji wa mazingira
 Alisema hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa katika uharibifu wa mazingira kwani athari za tabia ya nchi imedhihirika ndiyo maana Serikali inachukua hatua mbalimbali za kuhifadhi mazingira lakini bado wadau hawajapokea wito huo wa kuhifadhi mazingira kikamilifu.


Mgowole alisema kuwa moja ya hatua muhimu ambazo Serikali na wadau wa mazingira wanazichukua kupitia Wizara ya Nishati na madini ni uhamasishaji wa matumizi ya umeme nuru hasa kwa wananchi wa vijijini ambao hawajapata umeme wa gridi ya Taifa ambapo kinachoendelea hivi sasa kuhusiana na nishati hiyo ni ukuzaji na uendelezaji wa soko la umeme nuru katika maeneo mbalimbali kwa kuhamasisha wananchi.
  
“Hivi sasa wananchi wengi hasa katika maeneo ya vijijini hawana huduma ya umeme kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo hali ya kijiografia ya vijiji vingi kutofikika kwa urahisi hali inayosababisha Wizara kushindwa kufikisha huduma ya nishati ya umeme ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya  wananchi “ anasema.
  
Alisema kuwa kutokana na miundombinu hafifu katika vijiji hivyo Wizara ya Nishati na madini kwa kushirikiana na shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA) wameanzisha mpango wa kuhamasisha matumizi ya umeme nuru ambao utasaidia wananchi katika matumizi mbalimbali.
  
Ameyataja matumizi hayo kuwa ni pamoja na ya nyumbani, shuleni, katika vituo vya kutolea huduma za afya ,kwenye taasisi mbalimbali pamoja na matumizi mengine ambapo hadi sasa mradi wa umeme jua umeanza kutekelezwa katika mikoa ya Tanga,Mbeya,Iringa Mtwara, Rukwa, Dodoma,Pwani na Morogoro na kwamba mradi huo wa umeme nuru katika Mkoa wa Ruvuma uliingia Desemba mwaka juzi
  
Alieleza zaidi kuwa takwimu za Kitaifa zinaonyesha kuwa ni asilimia mbili tu ya watu kati ya asilimia 89 ya Watanzania wanaoishi vijijini ndio wanaotumia nishati ya umeme na  asilimia 87 wanaendelea kutumia nishati inayotokana na misitu hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira kila mwaka.
  
Jambo la msingi hivi sasa ni kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira pamoja na matumizi ya umeme nuru pamoja na gharama nafuu za vifaa vya nishati hiyo ili kuwawezesha wananchi wengi kupata huduma hiyo ili hatimaye wananchi wajikomboe kutokana na matumizi makubwa ya nishati inayotokana na mazao ya misitu.
  
Ni wazi kuwa makamu wa Rais Dk.Mohamed Ghalib Bilal mara kwa mara amekuwa akisisitiza wakulima wa tumbaku,chai na watumiaji wengine wakubwa wa miti,kuni na makaa ya mawe waanzishe mashamba  yao ya miti na ameagiza kila Kijiji kiwe na shamba au mashamba mahsusi ya miti kwa matumizi ya nishati ya kuni,mkaa na biashara ya mbao.
  
Mgowole alisema pia inashauriwa kila kijiji kiandae vitalu vya miche ya miti ifaayo na kupanda miti kila ifikapo Januari mosi na April ya kila mwaka na kuendelea kuitunza ambapo kila mji utenge maeneo ya mashamba ya miti kwa ajili ya nishati, biashara na kuendeleza mandhari ya Mji husika.
  
“Kutokana na madhara yanayoendelea kutokea ya mabadiliko ya tabia ya nchi sisi kama Taifa hatuna budi sasa kuyalinda na kuyahifadhi mazingira yetu kwa nguvu zetu zote ikiwa ni pamoja  na kuacha kabisa tabia sugu ya uchomaji moto na ufyekaji wa misitu ambao huchangia uharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira”alisema Mgowole.
  
Anasisitiza kuwa matukio ya uchomaji moto wa misitu na nyika ni marufuku,wahalifu wachukuliwe hatua kali za kisheria na uongozi wa eneo husika uwajibike kikamilifu katika kusimamia hilo na wananchi wahamasishwe kushiriki katika kampeni ya kudumu ya kupanda na kuitunza miti wanayoipanda kila mwaka na kwamba Manispaa ya Songea imetekeleza agizo la Serikali la kupanda miti milioni  1.5 kila mwaka.

Alisema kuwa Halmasshauri ya Manispaa ya Songea imevuka lengo hilo na kufanikiwa kupanda miti milioni 1.7 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mazingira na kwamba kuna maeneo ambayo yanapandwa miti na wadau mbalimbali wakati wa mvua na kwamba kuna vikundi vya utunzaji wa mazingira navyo vina maeneo yao wanayopanda miti na kuitunza

Alieleza zaidi kuwa Halmashauri hiyo imekuwa ikizalisha miche ya miti kwenye vitalu vya watu binafsi na kuwagawia wananchi kwa bei nafuu kwenda kuipanda na wakati mwingine hupewa bure kwa ajili ya kuipanda kwenye maeneo yao
  
Alisema kuwa ni vema kampeni ya mazingira ya umma ianzishwe kwa vitendo kwa kushirikisha Serikali za Mitaa na taasisi mbalimbali na kwamba ifanyike jitihada za kudhibiti uvunaji holela wa mazao ya misitu katika maeneo yote nchini,mazao hayo ya misitu ni pamoja na magogo,nguzo,mbao,kuni na mkaa.
  
Alifafanua kuwa mahitaji ya mazao hayo ni makubwa na uvunaji wa mazao hayo nao ni mkubwa. kutokana na hali hiyo ndio maana Wizara ya Maliasili na utalii imependekeza katika kuboresha usimamizi wa uvunaji wa mazao ya misitu.
  
Ambapo katika utaratibu huo mpya kwa mujibu wa Wizara ya maliasili na Utalii aina za miti zipatazo 24 hazitaruhusiwa kuvunwa ikiwamo miti ya matunda kama vile mibuni,mizambarau na mingineyo ambapo maofisa wa misitu katika kila Wilaya wanatakiwa wawe makini katika kuhakikisha utaratibu huu wa kuvunwa misitu unafuatwa.
  
Wasafirishaji wa mazao ya misitu nao wanatakiwa kuhakikisha wanafuata taratibu zilizowekwa na Wizara ya Maliasili na Utalii zikiwamo za hati za usajili wabiashara ya mazao ya misitu, kibali cha usafirishaji, leseni ya biashara na hati za malipo ya mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) ili Taifa liwe na uhakika wa upatikanaji wa mapato wa mazao ya misitu.
  
Katika utaratibu huo wa usimamizi wa uvunaji wa mazao ya misitu kila Wilaya inahusika zaidi na vibali vya kuvuna ambavyo vinatolewa na kamati maalumu ya Wilaya ya usimamizi wa uvunaji wa misitu ambayo inaongozwa na mkuu wa Wilaya husika na kwamba katika vijiji ambako mazao ya misitu yatavunwa vinahusika na udhibiti wa uvunaji na ofisa misitu wa Wilaya husika anatoa leseni baada ya kibali cha kamati.
  
“Kila Wilaya hapa Nchini kulingana na utaratibu huo mpya inatakiwa itenge maeneo ya misitu ya kutengenezea mkaa na kila mwaka na wananchi wayatambue maeneo hayo na shughuli za uchomaji mkaa zisifanywe katika maeneo tofauti na hayo yaliotengwa na kutangazwa na vijiji husika.”alisema Mgowole
  
Alisema kuwa katika utaratibu huo wa usimamizi wa mazao ya misitu kila atakayechoma mkaa anapaswa kuwa na leseni maalumu ya kuchoma mkaa itakayotolewa na Ofisa misitu kwa niaba ya Wizara na kwamba leseni hiyo itatumika katika eneo lililoruhusiwa kwa shughuli hizo.
  
“Watengenezaji hao wa mkaa wataonyeshwa katika kijiji eneo la wazi lenye ukubwa mara mbili ya eneo walilopatiwa kuvuna na kutengeneza mkaa na watatakiwa kupanda miti na kuitunza katika eneo hilo wakati wa msimu wa mvua utakaofuatia na kwamba maeneo hayo yatabakia kuwa mali ya Kijiji chini ya usimamizi wa serikali ya kijiji.’alisema Mgowole
  
Alisema ukataji miti katika misitu ya hifadhi kwa ajili ya kutengenezea mkaa umepigwa marufuku  kwa kuwa miti inayohifadhiwa kisheria hairuhusiwi kutengenezea mkaa na kwamba miti hiyo ni pamoja na msandali,mpingo,mvule, mninga, mpodo, mkora, mkora, muhuhu,mfimbo, mkangazi, mwangati, msekeseke na pangapanga na miti yote ya matunda ya porini ikiwamo mikwaju, mmitonga, mikusu, mitalali, mizambarau, mibula., mingwera, mipingipingi na mifuno.
  
Jamii itambue kuwa Tanzania ina eneo la misitu lipatalo hekta milioni 33.3 za misitu   ambayo inapaswa kulindwa na kutunzwa kwa ajili ya ustawi wa Taifa.
   
  Mwandishi anapatika kwa
  Simu 0755-335051 au 0715 335051
  Barua pepe;stephano12mango@yahoo.com