About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Wednesday, November 30, 2011

WENGI WATEKETEA KWA UGONJWA WA MALARIA WILAYANI NYASA MKOANI RUVUMA

   Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Daniel Malekela
Na Thomas Lipuka,Songea
UGONJWA wa malaria katika vijiji  kumi vya tarafa ya Ruhuhu wilayani Nyasa mkoani Ruvuma,unatishia ustawi wa jamii kutokana na wananchi wengi kuugua na kupoteza maisha kila mwaka.
Mganga mkuu wa hospitali ya Lituhi Dk.Martin Ndunguru amesema  katika kipindi cha mwaka 2009/2010  jumla ya watu 130 walikufa kati yao watoto 93 wenye umri chini ya miaka mitano na watu wazima 37.
Amevitaja vijiji ambavyo vinakabiliwa na ugonjwa wa malaria katika tarafa ya Ruhuhu kuwa ni Lituhi, Litumbakuhamba, Ngingama,Tumbi,Mbaha,Lundu,Hinga,Mkili,Ngumbo,Yola,Liwundi, Mbuli,Liweta na Njomole.
Kwa mujibu wa Dk.Ndunguru  vifo vingi vinavyotokana na ugonjwa wa malaria vinasababisha na wagonjwa kupungukia damu na kuchelewesha kupelekwa kwenye vituo vya tiba,umbali kutoka katika kijiji husika hadi kituo cha tiba.
Mganga mkuu huyo wa hospitali ya Lituhi alisema tarafa hiyo ina vituo vichache vya tiba ambapo zahanati zipo katika vijiji vya Litumbakuhamba,Ngingama,Ndumbi,Lundo,Mbuli na Mkili ambako kuna kituo cha afya.
Hata alisema vituo hivyo vya tiba vinakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni upungufu wa madawa,watalaamu wa afya,miundombinu hafifu,vifaa hasa vya maabara na kituo cha afya cha Mkili  kukosa  benki ya damu hali ambayo inaleta usumbufu kwa wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu.
Wakazi wa vijiji vya Ngingama na Litumbakuhamba ambao ni Helumina Chawala,Martina Haule,Sophia Kayombo na Kalistus Mapunda wamedai kuwa  malaria ni ugonjwa ambao unawatesa siku hadi siku  na kwamba upungufu wa dawa kwenye zahanati na bei kubwa ya dawa za malaria kwenye maduka yamadawa  ni kikwazo.
Mganga wa zahanati ya kijiji cha Ndumbi Yohana Kanyanja amekiri malaria ni tishio kwa wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa ambapo katika zahanati ya kijiji cha Ndumbi pekee kwa mwezi  hupokea zaidi ya wagonjwa  356 wengi wao wakiwa ni watoto chini ya miaka mitano.
Anabainisha kuwa katika kipindi cha mwaka 2009/2010 watoto chini ya umri wa miaka mitano wapatao 2460 waliugua malaria katika kijiji cha Ndumbi na watu wazima katika kipindi hicho walikuwa ni 1200.
Mganga wa kituo cha afya Mkili Thomas Magulilo anazitaja changamoto ambazo zinakikabili kituo hicho kuwa ni  kituo kukosa gari la wagonjwa, upungufu mkubwa wa watumishi ambapo kituo kina watumishi wane tu kati ya mahitaji ya watumishi 25 na kwamba kituo hakina vitendea kazi vya kutosha katika maabara.
“Kituo chetu hakina gari la wagonjwa ili kuwasafirisha wagonjwa wanaozidiwa  na kuwapeleka katika hospitali za Litembo,Liuli na Mbinga ambazo zipo zaidi ya kilometa 64 kutoka hapa,hivyo inawalazimu wananchi kuwabeba wagonjwa waliozidiwa kwenye machela au kwenye mtumbwi hali inayosababisha baadhi yao kufia njiani’’,alisema.
Hata hivyo amesema hatua mbalimbali kituo kinachukua ili kukabiliana na tatizo la ugonjwa wa malaria ikiwemo kutoa elimu ya kupambana na ugonjwa huo,kugawa vyandarua na kuwahamasisha wananchi kuua mazalia ya mbu  na kuhakikisha wagonjwa  wanamaliza dozi  ya malaria.
Andrew Niliwani ni mkazi wa kijiji cha Mkili anatoa ushuhuda kuwa kuna wagonjwa watatu wa malaria waliobebwa kwenye machela walifia njiani wakati wanapelekwa katika hospitali ya Litembo,wagonjwa hao walifia katika maeneo ya Ndandaghala,Nahande na Mbugu.
Mganga mkuu wa hopsitali ya Liuli Dk.Daniel Ndimbo anazitaja changamoto zinazoikabili hospitali hiyo kuwa ni upungufu wa mashine za kuchunguza damu ya malaria,upungufu wa vitanda 50 na upungufu mkubwa wa wauguzi.
 Mganga mkuu wa kituo cha afya Mbambabay Wenceslaus Socky  anaeleza kuwa dawa za malaria huwa hazifiki kwa wakati katika kituo hicho na kwamba hata kiwango kinachofika hakilingani na mahitaji ya maombi yao  hali inayosababisha upungufu wa dawa hizo kila mwezi
 Mganga mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk.Daniel Malecela amesema katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria mwaka 2010 jumla ya watoto 246,927 walio chini ya umri wa miaka mitano wamepewa bure vyandarua vyenye dawa.
Dk. Malekela alisema kuwa walifanya sensa ya kutambua idadi ya kaya zinazohitaji vyandarau ambapo jumla ya vyandarua 274,687 vimeshasambazwa katika vijiji na mitaa 539 ya mkoa wa Ruvuma
Licha ya kugawa vyandarua vyenye dawa mkoa wa Ruvuma umeviwekea  dawa vyandarua vipatavyo 254,400 vinavyotumika katika kaya bila jamii kuchangia gharama zozote.
"Tumeamua kufanya kampeni hii kwani katika tafiti ya kitaifa iliyofanywa mwaka 2007/2008 inaonyesha kuwa ni kaya nne tu kati ya 10 zinatumia chandarua kimoja chenye dawa hii inaonyesha kuwa kaya nyingi katika jamii yetu hazitumii vyandarua vyenye dawa na hivyo kuwa katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa malaria", alisema Dk. Malekela.
Aliendelea kusema kuwa takwimu za mkoa wa Ruvuma za mwaka 2008 zinaonyesha kuwa asilimia 55 ya wagonjwa wote waliopata huduma katika vituo vya kutolea huduma wenye umri chini ya miaka mitano waliugua ugonjwa wa malaria na vifo chini ya miaka mitano vilikuwa ni asilimia 56 ya vifo vyote vilivyotolewa taarifa.
Ugonjwa wa malaria unashika nafasi ya kwanza katika mkoa wa Ruvuma kwa kusababisha vifo  kwa kiwango cha asilimia 23.9. Takwimu za mwaka 2004  hadi 2008 zinaonyesha kuwa  asilimia 50.3 ya wagonjwa wote wa malaria walikuwa ni watoto chini ya umri wa miaka mitano na zaidi ya miaka mitano walikuwa ni asilimia 49.7.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ugonjwa wa malaria ndio unaoongoza kwa mahudhurio ya wagonjwa wanaofika kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya, na kwamba matukio takriban 12 milioni ya malaria hutolewa taarifa.
 Takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa watu kati ya 60,000 hadi 80,000 hupoteza maisha kila mwaka kwa ugonjwa  malaria ambapo asilimia 80 ya wanaofariki ni watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano na mama wajawazito.  Kwa wastani, malaria humuua mtu mmoja katika kila dakika tano.

 Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ugonjwa wa Malaria wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, unalenga kupunguza idadi ya wagonjwa na vifo kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2013.  Kwa maneno mengine, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ina lengo la kuwapunguza wagonjwa wa malaria hadi kufikia milioni 6 na idadi ya vifo hadi kufikia kati ya 30,000  hadi 40,000 kwa mwaka ifikapo
mwaka 2013.

Sunday, November 27, 2011

MAWAKALA WA KUSAMBAZA PEMBEJEO ZA KILIMO TUNDURU WAPATIKANA

                 Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Madaha
Na,Augustino Chindiye TunduruKAMATI inayosimamia ugawaji wa pembejeo za Ruzuku Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma imeteua Mawakala Sita watakao husika katika zoezi la usambazaji wa Mbolea na Mbegu za Mfumo wa Vocha zitakazo tumika katika msimu huu.

Sambamba na kamati hiyo kuwateua mawakala hao baada ya Kampuni zao kufikia viwango vilivyo ainishwa na Wizara husika Mawakala hao wametakiwa kuhakikisha kuwa wanatimiza maelekezo waliyopewa yakiwemo ya kuhakikisha kuwa wameleta Pembejeo hizo kabula ya Desemba 10 mwaka huu na kuanza kuzisambaza katika vijiji vyote vya Wilaya hiyo kabla mvua hazija aanza kunyesha vinginevyo nao watafutwa

Katika zoezi hilo pia kamati hiyo inayo ongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Juma Madaha pia imewafuta uwakala Mawakala 11 bada ya kampuni zao kushindwa kufikia viwango vilivyo bainishwa na Wizara ya Chakula,viwanda na biashara.

Akizungumzia taarifa hiyo Mwenyekiti wa kamti hiyo aliwataja Mawakala walioteuliwa kutoa huduma hiyo kuwa ni Zuberi Namahala, Crispin Mumba, Halima Luambano,Joseph Kalaliche,Augustino Lukosi na Alli Chimwala ambao pamoja na mambo mengine kamati hyo ilijiridhisha kuwa kampuni za wafanyabiashara hao zimekuwa zikifanya kazi hiyo muda wote ikiwa ni tofauti na Mawakala waliofutwa

Dc Madaha aliendelea kueleza kuwa wengi wa mawakala waliofutwa kwa sababu ya kukosa sifa baada ya kamati hiyo kubainika kuwa kampuni zao kutokuwa na ofisi wala maduka ya kutolea huduma hali iliyosababisha wafanyabiahsara hao kujitokeza wakati wa kutafuta Vocha tuna si kutoa huduma kwa wakaulima.

Katika taafa hiyo Dc Madaha aliwataja mawakala hao kuwa ni
Michael Mdete ambaye pamoja na kukosa Duka la kuuzia Pembejeo hizo lakini alikosa sifa kutokana na kuwa na kesi mahakamani baada ya kubainika kuchakachua kwa kugushi na kujipatia Vocha wakati akiwa hajatoa huduma husika kwa waklima.

Wengine ni Bernadetha Methodi Pili aliyekosa sifa za uwakala
kutokana na kuwa ni mke wa Afisa kilimo msaidizi wa Wilaya hiyo ambaye pia ndiyo mratibu mkuu wa huduma hiyo kwa Wakuliwa wa Wilaya hiyo, Craudio Kiwone anaye kabiliwa na tuhuma za kusambaza Mbengu za kienyeji kwa wakulima badala ya mbegu Bora katika msimu uliopita.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Mawakala wengine walifutwa ni Hadini
Ngunguni,Haridi Kalisinje,Yusuph Kapindo, Mjesye Mjesye,Mohamed
Limbe,Kiyonjo Hasan, Reheme Kalengo na Mchekenae ambao walikosa nafasi hiyo kutokana na kutokuwa na maduka ya kuuzia pembejeo hizo

Akizungumzia mahitaji ya Pembejeo kwa Wakulima wa Wilaya hiyo Afisa Kilimo na Mifugo wa Wilaya ya Tunduru Chiza Marando alisema kuwa jumla ya tani 12 elfu za Mbolea za kupandia na kukuzia pamoja na Tani 400  za Mbegu Bora za mpunga na mahindi ili kukidhi mahitajika kwa Wakulima wa Wilaya hiyo na kuzisambaza  kabla ya kipindi cha mvua

Mwisho

PIKIPIKI ZA MCHINA ZAENDELEA KUWAMALIZA WATANZANIA NA WENGINE KUACHWA WAKIWA WALEMAVU

Kamanda wa Polisi Mkoani Ruvuma Michael Kamuhanda Na,Augustino Chindiye Tunduru

MKAZI wa Mjini Tunduru Ramadhani Namadogo (31 ) amefariki dunia baadaya kupata ajali mbaya ya pikipiki aina ya SANLG  yenye namba za usajiri T310 BVM ambayo ilidaiwa kuwa ikiiendesha mwenyewe.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa katika tukio hilo pia ajali hiyo ilimjeruhi rafiki wa marehemu aliyefahamika kwa jina la Mussa Saanane(27) ambaye hivi sasa amelazwa katika Hospitali ya serikali ya Wilaya ya Tunduru kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Mashuhuda hao waliendelea kueleza kuwa ajali hiyo ilitokea katika mta wa Lambayi Mjini hapa wakati marehemu huyo akirejea nyumbani kwake akiwa anatokea katika maeneo ya Kadewelere ambako ilidaiwa kuwa yeye na majeruhi walienda kupata kinywaji ili kujiliwaza kutokana na ugumu wa maisha.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda
amedhibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa chanzo cha tukio hilo ni ulevi na kwamba uchunguzi wa Polisi umebaini kuwa Pikipiki hiyo aambayo ilikuwa ni mali ya Marehemu ilikuwa ikiendeshwa na Majeruhi ambaye kwa sasa yupo chini ya ulinzi wa Jeshi hilo.

Akiongea kwa shida majeruhi huyo ambaye amelezwa kitanda namba 12 katika Wodi ya Wanaume katika hospitali hiyo mbali nakukiri kuwa wakati ajali hiyo ikitokea walikuwa wamelewa alikanusha kuwa wakati ajali hiyo inatokea Pikipiki hiyo ilikuwa ikiendeshwa na marehemu pia alikiri kuwa yeye aliendesha pikipiki hiyo wakati yeye na marehemu
wakielekea Kadewele.

Akizungumzia tukio hilo Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Tunduru Dkt. George Chiwangu alisema kuwa kifo hicho kilisababiswa na kutokwa na damu nyingi zilizotokana na kitendo cha kupasuka kwa fuvu la kichwa.

Kuhusu hali ya majeruhi Saanane alisema kuwa hali yake inaendelea vizuri ingawa taarifa zinaonesha kuwa anahitaji kukaa chini ya uangalizi wa maafisa tabibu kwa muda mrefu ili kunusuru maisha yake kufutia majeraha mabaya aliyoyapata kichwani.

Msemaji wa familia hiyo Kaka wa Marehemu Seiph Namadogo alisema
kuwa kifo cha ndugu yake huyo ni cha kawaida na kwamba kinacho
wasikitisha wanafamilia wote ni kitendo cha marehemu kuuza nyumba na kununua piki piki hiyo ili aitumie kwa ajili ya kusanyia abiria akidai kuwa ingeweza kumsaidia kujikwamua kiuchumi kumbe alikuwa anakaribisha umauti wake.

Mwisho

Saturday, November 26, 2011

WANANCHI WA LITUHI WAANZISHA UMOJA WA KILIMO CHA UMWAGILIAJI

                                 Diwani wa Kata ya Lituhi Adam Mhaiki
Na Gideon Mwakanosya,Nyasa
WANANCHI wa kata ya Lituhi Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma wameanzisha umoja wa wakulima wa kilimo cha umwagiliaji ambacho kitaweza kuwakomboa katika kuondokana na njaa na tatizo la umaskini miongoni mwa jamii
Akizungumza na Mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/  jana Diwani wa Kata ya Lituhu Adam Mhaiki alisema kuwa hatua ya wananchi wa kata hiyo ya kuunda umoja huo imekuja baada ya kuona Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Chakula kuleta ushawishi mkubwa wa kuwa na mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika maeneo mbalimbali ya Vijiji vilivyo kandokando y a mto Ruhuhu kwa Wilaya ya Ludewa na Nyasa
Mhaiki alisema kuwa hatua za awali za upimaji wa maeneo ya kilimo cha umwagiliaji tayari zimekwisha fanyika ambapo ukubwa wa eneo hilo lililopimwa ni hekari 2800 na kwamba wakulima waliounda umoja huo ni wa Vijiji vya Mwela Mpya,Nkaya,Kihulu na lituhi
Alieleza kuwa mradi huo ukikamilika unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya mpunga,mahindi,vitunguu,nyanya na mbongambonga na kwamba kwa sasa jitihada zinafanywa kwa kushirikiana na Serikali ya Wilaya ya Mbinga na Wilaya ya Ludewa Mkoani Iringa ambako kuna wananchi wa kata ya Ngerenge kutafuta fedha ambazo zitaweza kusaidia kujenga miundombinu imara ya kilimo cha umwagiliaji katika maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kujenga daraja la kuunganisha wakulima wa wilaya ya Nyasa na Ludewa badala ya kutegemea kivuko kibovu kilichopo eneo la mto Ruhuhu ambacho kwa kipindi cha kiangazi huwa hakifanyi kazi kutokana na uhaba wa maji
Alieleza zaidi kuwa pia mradi huo ukikamilika utaweza kuinua hali za maisha za wananchi wa vijiji hivyo na taifa kwa ujumla kwa kupunguza umaskini wa kipato na njaa kwenye kaya nyingi katika maeneo hayo kwani kwa muda mrefu wananchi wa kata hizo wamekuwa wakitegemea kilimo cha mihogo na shughuli za uvuvi kwa kutumia vitendea kazi duni
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi Kapteni John Komba aliiomba Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Chakula kuhakikisha mradi huo mkubwa unakamilika mapema ili kuondoa kero kubwa ya wananchi wa maeneo hayo
Komba alisema wananchi wamehamasika kujiunga kwenye umoja wa wakulima ili waweze kupata nguvu ya pamoja ya mikopo na misaada kutoka kwenye mfuko wa jimbo ambao kazi yake kubwa ni kuwasaidia wananchi kwenye vikundi vya ujasiliamali ili waweze kupata ustawi katika maisha yao
Mwisho

RAIS KIKWETE ACHANGIA MILIONI 3 UJENZI WA HOSTELI YA WASICHANA WILAYANI NYASA

                             
                                                           Rais Jakaya Kikwete
                                                          RC Ruvuma Said Mwambungu
                                     DC Mbinga Kanali Edmund Mjengwa
             Mbunge Mbinga Magharibi Kapteni John Komba
Na Stephano Mango,Nyasa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete amechangia shilingi milioni tatu katika kusaidia ujenzi wa hosteli ya wasichana katika shule ya Sekondari ya Lituhu iliopo katika wilaya mpya ya Nyasa mkoani Ruvuma ili kukomesha utoro na mimba kwa wasichana wa shule hiyo
Akizungumza na Mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ Ofisini kwake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya kutwa ya Lituhi Benjamin Mwingira alisema kuwa wananchi wa kaya ya Lituhu wakiwemo wazazi wa watoto wanaosoma katika shule hiyo kwa pamoja wameridhia mpango wa ujenzi wa Hosteli ya wasichana ambayo itaweza kuwasaidia wanafunzi wa kike kuondokana na tatizo sugu la utoro na upatikanaji wa mimba
Mwingira alisema kuwa kwa sasa wananchi hao tayari wamefyatua na kuchoma tofari laki sita zitakzotumika kwenye ujenzi huo ambapo kazi iliyobaki ni kuanza kujenga Hosteli hiyo kwa kasi kubwa mara baada ya mvua kusimama kunyesha
Amewahimiza wazazi kuthamini michango iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu,Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Kanali Mstaafu Edmund Mjengwa na Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi Kapteni Mstaafu John Komba kwa kuhakikisha kuwa jingo hilo la Hosteli kwa wasichana linakamilika kwa wakati ili wanafunzi  wa kike 200 kati ya wanafunzi  403 wa shule hiyo waweze kulitumia
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi Kapteni Mstaafu John Komba alisema ametoa bati 50 na michango midogomidogo kwa ajili ya kuezekea hosteri hiyo na pia amewashukuru Rais Kikwete kwa kuwachangia shilingi milioni tatu,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu kwa kutoa mifuko 50 ya saruji na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga ametoa mifuko 10 ya saruji
Komba aliwaomba wananchi wa kata ya Lituhi na wananchi waliopo nje ya kata ya Lituhi wakiwemo waliowahi kusoma shule hiyo kuona umuhimu wa kuchangia ujenzi huo ambao unaboresha miondombinu ya shule hiyo na kupelekea utolewaji wa elimu bora
MWISHO

ASASI YA ROA YAFANIKIWA KUHUDUMIA WAGONJWA 489 SONGEA

                    Mwenyekiti wa ROA Methew Ngarimanayo
Na Stephano Mango,Songea

SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Ruvuma Orphans Association (ROA) katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu kwa kushirikiana na timu ya watoa huduma kwa wagonjwa majumbani limefanikiwa kuwatambua wagonjwa 516 kati ya hao wagonjwa 489 wamepatiwa huduma na wagonjwa 268 wanaendelea kupata huduma katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea na Halmashauri ya Wilaya ya Songea.

Hayo yamesemwa jana na Mwenyekiti wa Shirika hilo  Mathew Ngalimanayo wakati akizungumza na Mtandao huu wa www.stephanomango.blogspot.com  jana ofisini kwake mjini Songea.

Amefafanua zaidi kuwa Shirika hilo lisilo la Kiserikali la Roa lilianzishwa tangu Aprili mwaka 1999 na kusajiliwa rasmi Aprili 6 mwaka 2001 na kwamba lengo kubwa la kuanzishwa kwa Shirika hilo ni kushughulikia changamoto wanazokabiliana nazo watoto yatima na watoto waishio katika mazingira hatarishi.

Amebainisha zaidi kuwa Shirika hilo pia lilianzishwa kushughulikia changamoto ziletwazo na ugonjwa hatari wa Ukimwi katika jamii  kwa kushirikiana na Serikali,na wadau wengine wa Maendeleo.

Ameeleza zaidi kuwa shirika lake limetoa huduma kwa wgaonjwa wa muda mrefu majumbani katika Kata 15 zilizopo katika Manispaa ya Songea na Halmashauri ya Wilaya ya Songea na kwamba kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la The foundation for civil society la Jijini Dar es Saam limefanikiwa kuhamasisha mitaa na kata katika Manispaa ya Songea na Halmashauri ya Wilaya ya Songea kufungua na kuiendesha mifuko ya kusaidia watoto yatima na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Ngalimanayo amesema kuwa Shirika hilo lisilo la Kiserikali la Roa pia limefanikiwa kuwahudumia wagonjwa 489 kati ya wagonjwa 516 waliotambuliwa ambapo wagonjwa 29 wamepata nguvu na wanaendelea vizuri na shughuli zao za kila siku na wagonjwa 268 wanaendelea kuhudumiwa majumbani na pia Roa imefanikiwa kuwapatia huduma watoto yatima 234 walioko katika mfumo wa Elimu.

Amesema kuwa pia wamefanikiwa kuwakumbusha wananchi juu ya wajibu wao wa kimsingi wa ulinzi,matunzo na malezi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa kila mtaa kuwa na kamati ya kuratibu na kusimamia masuala ya watoto wanoishi katika mazingira hatarishi na kuanzisha mfuko maalumu wa kila mtaa wa kuhudumia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na watu wa makundi mbalimbali katika kata hizo wamehamasishwa juu ya masuala ya Vvu/ Ukimwi na kuendesha zoezi la upimaji Vvu/Ukimwi kwa hiyari.

Ametaja changamoto wanazokutana nazo kuwa ni ukosefu wa fedha za kutosha wa kuendeshea shughuli za shirika hilo kadiri ya malengo na mipango iliyopo,mwitiko hasi wa baadhi ya wananchi na watendaji wa Serikali kuhusu dhana ya mifuko ya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Ameitaja mipango ya shirika hilo ya baadaye kuwa ni kuendelea kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuanzisha mifuko ya jamii ya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi,kugharamia gharama za masomo kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapatia karo,sare za shule,vifaa vya darasani na gharama zingine zinazohusiana na masuala ya elimu na kujenga uelewa kwa jamii juu ya haki na wajibu wa watoto yatima na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

MWISHO


Friday, November 25, 2011

MCHINA ACHEZEA KIPIGO KUTOKA KWA MTANZANIA NA KUNYANG'ANYWA SIMU TATU ZENYE THAMANI YA LAKI SITA MBINGA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda
Na Gideon Mwakanosya,Songea

JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma linamsaka Dereva wa Kampuni ya Sinohydro inayotengeneza barabara kwa kiwango cha lami kutoka Songea kwenda Mbinga Said Ibrahim kwa tuhuma za kumnyang’anya Simu tatu za mkononi zenye thamani ya shilingi laki 6 na kumjeruhi kwa kumpiga na nondo kichwani Majianxin mwenye umri wa miaka (40) ambaye ni raia wa China mfanyakazi wa Kampuni hiyo ya ujenzi.

Kamanda wa Polisi wa Moka wa Ruvuma Michael Kamuhanda ameuambia mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ kuwa tukio lilitokea jana majira ya saa nane mchana kwenye eneo la Mkako Wilayani Mbinga.

Amesema kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio  Majianxin mwenye asili ya kichina akiwa kwenye shughuli zake za ujenzi wa barabara majira ya saa nane mchana alinyang’anywa simu tatu za mkononi na dereva wa Kampuni ya Sinohydro aliyejulikana kwa jina la Said Ibrahimu.

Amefafanua kuwa inadaiwa kabla ya Ibrahimu kumnyang’anya simu hizo alichukua nondo na kumpiga Majianxin na badae alikimbia na kutokomea kusikojulikana na kwasasa hivi Majianxin amepata majeraha makubwa kichwani na anaendelea kupata matibabu kwenye hospitali ya Wilaya Mbinga.

Ameeleza zaidi kuwa Majianxin alinyang’anywa simu tatu ambapo kati ya hizo mbili ni za aina ya Samsung na nyingine ni aina ya nokia zote zikiwa na thamani ya shilingi laki 6.

Hata hivyo Kamuhanda alisema kuwa kufuatia tukio hilo kutokea kwasasa hivi Jeshi la Polisi Mkoani humo linaendelea kumsaka mtuhumiwa ambaye anadaiwa kuwa ametorokea katika Mikoa ya Lindi na Mtwara.

MWISHO



MBARONI KWA TUHUMA ZA KUMUUA MTOTO KWA KUMPIGA NA MTI KICHWANI

Na Mwandishi Wetu,Songea

POLISI Mkoani Ruvuma imemtia mbaroni Joseph Ndunguru Mkazi wa Kijiji cha Mkumbi kilichopo Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma kwa tuhuma za kumuua mtoto mwenye umri wa miaka miwili na nusu kwa kumpiga na mti kichwani wakati anasindikizwa na mama yake kwenda chooni kujisaidia.

Akizungumza na mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com Jana ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amemtaja mtoto aliyeuwawa kuwa ni Agnes Ndimbo Mkazi wa Kijiji cha Mkumbi Wilayani Mbinga.

Amefafanua kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio novemba 22 mwaka huu majira ya saa moja usiku huko katika Kijiji cha Mkumbi Prisca Nditi (38) akiwa nyumbani kwake mtoto wake Agnes alimuomba amsindikize kwenda kujisaidia .

Amesema kuwa baada ya mtoto huyo kumuomba mama yake ampeleke chooni ndipo Prisca aliondoka na mwanaye wakaelekea nje ya nyumba kwenye eneo la choo ambapo wakati wanarudi mara tuu baada ya mtoto huyo kujisaidia inadaiwa kuwa Ndunguru alivizia na kumpiga mtoto na mti kichwani na kumsababishia kifo papo hapo.

Hata hivyo amesema kuwa habari zaidi kutoka Kijijini Mkumbi zinaeleza kuwa Ndunguru maarufu kwa jina la Kapalanza kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa akili ambao unahofiwa kuwa ndio ulisababisha atende kosa hilo na Jeshi la Polisi linaendelea kufanya upelelezi wa kina juu ya tukio hilo na utakapokamilika mshtakiwa atafikishwa mahakamani kujibu shtaka linalomkabili.

MWISHO

Thursday, November 24, 2011

MADAKTARI WAISHAURI SERIKALI KUVICHUNGUNZA VYUO VISIVYOSAJILIWI ILI KUWEZA KUPUNGUZA MALALAMIKO YA UKOSEFU WA MAADILI YA UUGUZI

               Mganga Mkuu wa Mkoa Ruvuma Daniel Malekela
Na, Augustino Chindiye Tunduru

SERIKALI imeombwa kuvifuta vyuo ambavyo vimekuwa vikitoa elimu ya Uuguzi na Ukunga bila kuwa na usajili na kupelekea fani hiyo kuvamiwa na watu wasioiva kitaaluma ( Makanjanja) na kusababisha utoaji wa huduma kushuka.

Rai hiyo imetolewa na Wanachama wa Mkutano Mkuu wa 39 wa Chama cha Wauguzi na Wakunga (TANNA) wa Mkoa wa Ruvuma uliofanyika katika Ukumbi wa  Kanisa la Bibilia mjini hapa.

Akifafanua taarifa hiyo Mwenyekiti wa Chama hicho  Jordan Nchimbi alisema kuwa pamoja na vyuo hivyo kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza idadi ya watumishi wa kada hiyo, lakini pia kada hiyo imeonekana kutokuwa na maadili kutokana na kuvamiwa na kundi hilo ambalo uchunguzi unaonesha kutokuwa na maadili kutokana na kutosoma masomo yenye maelekezo ya kufuta mitaala wakati wa utumishi wao.

Sambamba na maombi hayo pia Wajumbe hao walibainisha baadhi ya vikwazo ambavyo vimekuwa vikiwakatisha tamaa wakati wa utendaji wao kuwa ni pamoja na ucheleweshaji wa upatikanaji wa haki zao kutoka hazina, makato ambayo hufanyika bila taarifa wala  kupata ridhaa yao na  kutokuwepo kwa usafiri kwa watumishi wa kada ya chini hasa wanaofanya kazi vijijini huku kukiwa na matishio ya kujeruhiwa na wanyama wakali.

Akiongea kwa niaba ya Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Dkt. Alex Kazula. Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya hiyo Dkt. Goerge Chiwango alitumia nafasi hiyo kuwaasa wanachama hao kutumia nafasi hiyo vizuri hasa wakati wa kujikumbusha Masomo mbalimbali pamoja na muda wa kubadilishana uzoefu kupitia mijadala.

Nao Muuguzi Mkuu wa Mkoa huo Nenedikter Ndumbaro, Katibu mwenezi wa TANNA Norbart Haule na Katibu wa Chama hicho Mkoa wa Ruvuma  Paul Mtimba pamoja na mambo mengine waliwahiza wauguzi wote wa mkoa huo kujiunga na chama hicho ili waweze kupaza sauti zao kwa pamoja,

Walisema Chama hicho chenye wanachama 662 lakini takwimu za wanachama hai zinaonesha kuwa ni 490 tu, hali inayotishia uwepo utengano miongoni mwao na wakatumia nafasi hiyo kukemea tabia za wauguzi kutumia lugha za matusi kwa wateja ili kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza.

Akijibu kero za Wauguzi hao wakati akifungua Mkutano huo Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini Alhaji Mtutura Abdalah Mtutura, pamoja na mambo mengine aliwataka wakuu wa idara na viongozi waliopewa mamlaka ya kusimamia utendaji wa Shughuli za Serikali kutekeleza wajibu wao kwa haki ili kuondoa manung`uniko ya watumishi waliopo chini yao .

Aidha Mtutura pia alikemea tabia za viongozi na wakuu wa idara kuchukua hatua za kuwahamisha watumishi waliopo chini yao bila malipo hali ambayo imekuwa ikilisanbabishia Taifa Kero kubwa ya kudaiwa huku hali ikionesha kuwa hamisho nyingi hufanyika kwa hira za viongozi hao kutaka waabudiwe.

Kuhusu kero ya Malalamiko ya wauguzi hao kutolipwa malipo yao mbalimbali Alhaji Mtutura aliahidi kulifikisha suala hilo kwa Waziri mwenye dhamamna ili kulitafutia ufumbuzi wa kudumu zikiwa ni juhudi za kuboresha utoaji wa huduma.
Mwisho 

KIKAO CHA BODI YA BARABARA MKOA WA RUVUMA CHENYE AGENDA 7 KIMEANZA ASUBUHI HII

                         Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabiti Mwambungu

 Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Madaha kulia akiteta jambo kwenye kikao hicho na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Savery Maketta


 Wanahabari wakiendelea kupata taarifa mbalimbali kwa ajili ya kuuhabarisha umma kuhusu yaliyojili kwenye kikao hicho
 Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Peramiho Vastus Mfikwa kushoto akifurahia jambo na Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Endrew Chatwanga
Wajumbe wa kikao hicho wakiendelea na majadiliano ya agenda zilizoainishwa kwenye kikao hicho

AGENDA ZA KIKAO HICHO

1,Kufungua kikao

2,Kusoma na kuthibitisha muhtasari wa kikao cha bodi ya barabara kilichofanyika tarehe 11 Mei 2011

3,Yatokanayo

4,Taarifa ya matengenezo ya barabara kuanzia Mei 2011 hadi Octoba 2011 toka Wakala wa Barabara

5,Taarifa ya matengenezo ya barabara kuanzia Mei 2011 hadi Octoba 2011 toka Halmashauri

6,Mengineyo

7,Kufunga Kikao

Wednesday, November 23, 2011

AJARI YAUA MMOJA NA KUJERUHI WATU KUMI KUTOKANA NA MWENDO MKALI

                   Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma michael Kamuhanda
Na Gideon Mwakanosya, Songea

MTU mmoja amefariki dunia na wengine kumi wamejeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka  Dar Pori kwenda Mbinga kuacha njia na kupinduka katika eneo la barabara ya Mpepo maarufu kwa jina la babu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amesema kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 9 alasiri kwenye eneo hilo ambako gari lenye namba za usajili T537AUQ Aina ya Toyota Landcruser ambayo ilikuwa ikiendeshwa na Prosper Ndunguru ikiwa imesheheni mizigo pamoja an abiria iliacha njia na kupinduka.

Kamuhanda amemtaja aliyekufa kuwa ni Nikodem Ndunguru (45) Mkazi wa Mbinga Mjini na amewataja waliojeruhiwa vibaya kuwa ni dereva wa gari hilo Prosper Ndunguru  Mkazi wa Mbinga, Immaculata Ndomba (19) Mkazi wa Songea Mjini na Lucy Martin Mkazi wa Furaha Store Mbinga ambao kwasasa wamelazwa katika hospitali ya Misheni ya Mbinga wakiendelea kupata matibabu.

Amewataja majeruhi wengine ambao kwasasa wamepelekwa katika hospitali ya Misheni Peramiho Wilaya ya Songea kuwa ni Rukia Jofrey (47) Mkazi wa Jijini Dar es Salaam,Rukia Myovela (50) Mkazi wa Songea Mjini,Magreth Ndomba (27) Mkazi wa Mbinga mjini,Peter John (84) Mkazi wa Manispaa ya Morogoro,Sara Mkinga ambaye ni mfanyabiashara kati ya Mbinga na Dar Pori,Asha Katau (37) Mkazi wa Mfaranyaki Songea na Simon Komba Mkazi wa Tanki la Maji Mbinga Mjini.

Kamuhanda amefafanua kuwa Nikodem alifariki dunia baada ya ajali hiyo kutokea wakati alipokuwa akipelekwa kwenye Zahanati ya Mpepo na majeruhi wengine walikimbizwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mbinga na Hospitali ya Misheni Peramiho ambako bado wanaendelea kupata matibabu na hali zao bado ni mbaya .

Ameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kwamba gari ilikuwa kwenye mwendo kasi ambao ulimsababishia dereva kushindwa kuumudu usukani kisha gari ikaacha njia na kupinduka.

MWISHO

Tuesday, November 22, 2011

USHIRIKI WAKO KATIKA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA KANDA YA KUSINI NI NGUZO MUHIMU KUIMARISHA TANZANIA HURU

 Mmiliki wa mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com, Ndugu Stephano T.Mango anaungana na wanaharakati wengine nchini na nje ya nchi akiwemo Dada yangu Yasinta Ngonyani na Mzee Mbelle kwenye maandalizi ya kuadhimisha siku hizo 16 na kwa wale wote ambao kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao wameshindwa kushiriki siku hizo,Nawapa Pole na tuzidi kuombeana kwani naamini walipenda kushiriki lakini wasihofu naomba waniruhusu niwawakilishe

Mwanabloga Mwenzangu,Mwandishi Mwenzangu wa Habari,Mwalimu Mwenzangu,Mwaharakati Mwenzangu bila kusahau Baba yangu Juma Nyumayo akionyesha bango linaloonyesha ukatili wa kijinsia kwa waandishi wa habari
Na Stephano Mango,Songea
MKOA wa Ruvuma umepewa heshima ya kuadhimisha siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia Kanda ya Kusini inayojumuisha Mikoa ya Iringa,Mbeya,Ruvuma,Lindi na Mtwara kuanzia Tarehe 25/11/2011 hadi 10/12/2011
Katika siku hizo 16 za maadhimisho wadau wanategemea kufanya maandamano,kutoa elimu ya jinsia kwa makundi mbalimbali na kutoa msaada wa sheria katika kata nne zilizopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea chni ya kauli mbiu” Miaka 50 ya Uhuru pinga ukatili wa kijinsia kuimarisha Tanzania huru”
Vikundi mbalimbali vya sanaa vitatumbuiza vikiwa na ujumbe lengwa hivyo wadau wote wanatakiwa kuhudhuria kwani ushuhuda mbalimbali wa ukatili wa kijinsia utatolewa na wahusika waliofanyiwa vitendo hivyo

WAWILI WABAKWA KATIKA MATUKIO MAWILI TOFAUTI NA KUACHIWA MAUMIVU MAKALI SEHEMU ZAO ZA SIRI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda
Na Mwandishi Wetu, Songea
JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma linamshikilia Jaibu Alli ambaye umri wake haukuweza kufahamika mara moja kwa tuhuma za kumbaka msichana wa umri wa miaka kumi na sita ambaye jina lake limehifadhiwa anayesoma katika Shule ya Sekondari ya kutwa ya Kalembo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea na kumsababishia maumivu makali sehemu za siri.

Akizungumza na mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com  jana ofisini kwake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amesema kuwa tukio hilo limetokea juzi jioni majira saa kumi  jioni huko katika eneo la Matogoro Songea Mjini nyumbani kwa Wazazi wake.

Kamuhanda amefafanua kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio msichana huyo akiwa jirani na nyumbani kwake alikutana na Jaibu ambaye alikuwa ni Mwanafunzi mwenzake katika Shule ya Kalembo na amehitimu Elimu ya Sekondari mwezi mmoja uliopita na walisalimiana na baadaye mvulana huyo alianza kumwambia maneno ambayo msichana huyo hakukubaliana nayo .

Ameeleza zaidi kuwa baada ya Jaibu kuona kuwa msichana huyo hakubaliani na maelezo aliyoyatoa ya kumtaka afanye mapenzi naye ndipo inadaiwa kuwa aliamua kumbaka kwa kutumia nguvu na kumsabishia sehemu za siri kuharibika na baadaye alikimbizwa katika hospitali ya Serikali ya Mkoa kwa matibabu ambako amelazwa akiendelea kupata matibabu.

Amesema mara tu baada ya kutokea tukio hilo mzazi wa msichana alitoa taarifa katika kituo kikuu cha polisi cah Songea na askari walipokwenda kwenye eneo la tukio walifanya upelelezi wa awali kisha walifanikisha kumkamata Jaibu.

Hata hivyo Kamanda Kamuhanda amesema kuwa Polisi bado inaendelea kufanya upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hilo na kwamba ukikamilika mtuhumiwa atapelekwa mahakamani kujibu shtaka linalomkabili.

WAKATI HUOHUO Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma linamsaka mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Simon Mkazi wa Soko la wakulima Mbinga Mjini kwa tuhuma za kumbaka Mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Kiwanjani Mbinga Mjini ambaye jina lake limehifadhiwa.

Kamuhanda amesema tukio hilo lilitokea novemba 20 mwaka huu majira ya saa nane mchana huko katika eneo la mtaa wa soko la wakulima lililopo Mbinga Mjini ambako inadaiwa kuwa msichana wa umri wa miaka 12 akiwa nyumbani kwa wazazi wake alivamiwa na kubakwa na mtu mmoja ajulikanae kwa jina moja la Simon.

Amesema kuwa mtuhumiwa alitoroka mara tuu baada ya kumfanyia kitendo cha kinyama msichana huyo na kwamba kwasasa hivi Jeshi la polisi Mkoani Ruvuma  linamtafuta mtuhumiwa huyo ambaye anadaiwa kuwa amekimbia na kutokomea kusikojulikana.
MWISHO

Monday, November 21, 2011

UPIMAJI WA VIWANJA KWA KUTUMIA KAMPUNI KUNAKOMESHA MIGOGORO YA ARDHI NCHINI?

 Waandishi wa habari wakiwa kazini wakati Mwenyekiti wa Mtaa wa Mshangano Paulo Mangwe akitoa tamko la kutaka wapimiwe ardhi na Kampuni ya Ardhi Plan kwenye mkutano wa wananchi wa kata ya Mshangano
                                  Wananchi wakiwa kwenye mkutano huo

 Diwani wa Kata ya Mshangano Faustine Mhagama akizungumza kwenye mkutano huo
 Mkurugenzi Mtendaji wa Ardhi Plan Gombo Samandito akieleza namna kampuni yake itakavyopima viwanja Kata ya Mshangano kabla ya msimu wa mvua kuanza
 Mgeni Rasmi wa tatu toka kushoto ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati za Huduma za Uchumi na Jamii Genfrida Haule akizindua mradi wa upimaji viwanja 18000 kata ya Mshangano
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ardhi Plan akiwaonyesha wananchi ramani zilizopitishwa na Wiozara ya Ardhi ,Nyumba na Maendeleo na Makazi kwa ajili ya kupima viwanja kata ya Mshangano
Na Stephano Mango,Songea
ARDHI ni moja kati ya rasilimali yenye thamani kubwa endapo usimamizi wa matumizi yake utalenga kumuinua mwananchi kiuchumi,kijamii tofauti na ilivyo sasa kwenye maeneo mengi katika jamii kwani ardhi imekuwa chanzo kikubwa cha mapigano na migogoro
Maeneo mengi yamekuwa na migogoro ya ardhi kutokana na usimamizi mbovu wa matumizi ya ardhi usiozingatia sheria za nchi,tamaa za baadhi ya viongozi  na wakati mwingine dosari za uandaaji wa sera mbalimbali za nchi zisizozingatia uhalisia wa umiliki wa ardhi
Sera zote za maendeleo na mikakati mbalimbali ya maendeleo haiwezi kukamilika bila uwepo wa ardhi na rasilimali zake ikiwemo maji,misitu,madini,wanyamapoli,nishati na miundombinu mingine hivyo ni lazima kuwe na mipango mizuri ya matumizi ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuainisha ukubwa wa ardhi iliyopo,mtumiaji ni nani na inafaa kwa shughuli ipi ili kuepuka migogoro katika jamii
Ili kufanikisha hilo ni lazima kuwe na wataalamu wa mipango miji wenye kuzingatia maslahi ya umma badala ya maslahi binafsi,vifaa vya kisasa vya kupangia miji vizuri na kuondokana na ujenzi wa makazi holela yasiyozingatia ukuaji wa idadi ya watu
Akizungumzia hilo Mtaalamu wa mipango miji ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ardhi Plan Gombo Samandito alisema kuwa Halmashauri nyingi nchini hazijaona umuhimu wa kuajiri Wataalamu wa mipango miji kwasababu ambazo hazijawa wazi
Samandito alisema kuwa mara kadhaa utasikia Halmashauri na Manispaa  nyingi zimekuwa zikilalamika kukosa Walimu,Madaktari,Wauguzi na Wafanyakazi wengine lakini haijawahi kusikika Halmashauri hizo zikilalamika kukosa Wataalamu wa Mipango Miji
“Baadhi ya miji haina kabisa wataalamu wa mipango miji na hata pale wanapokuwepo hawatumiki ipasavyo hali inayosababisha wananchi kujenga makazi yao holela na kusababisha adha kubwa mijini kwa kushindwa kufikiwa na miundombinu muhimu kama vile maji,nishati ,miundombinu ya barabara na huduma zingine za dharura” alisema
Alieleza kuwa inapotokea wananchi wamejenga makazi yao holela na Serikali inamipango mingine ya maendeleo katika maeneo hayo yaliyojengwa ndipo inapoamriwa kubomolewa bila kulipa fidia na kuitwa wananchi kuwa ni wavamizi wa maeneo hayo na kusababisha malalamiko na migogoro baini ya Serikali na wananchi
Samandito alisema kuwa ni muda mrefu sasa Serikali imekuwa na utaratibu wa kutekeleza upangaji na upimaji wa miji kwa njia ya kutwaa maeneo kutoka kwa wamiliki wake wa kimila kwa kutumia sheria zilizopo ,kulipa fidia ya shilingi elfu 90 kwa hekta moja na kuamriwa kuhama eneo hilo na kupimwa kwa matumizi mengine itakavyokuwa imepangwa na mamlaka husika
Alieleza kuwa  utaratibu huu haujawahi kukamilika bila kuacha malalamiko kwa wananchi kwani mara nyingine fidia imekuwa ikichelewa kutolewa.kutokulipa kabisa na wakati mwingine kulipwa kidogo tofauti na uthamini wa eneo hilo na kuwaacha wananchi wakiwa maskini na wakimbizi kwenye ardhi yao
Alisema kwenye maeneo mengine wamiliki wake wa kienyeji wamekuwa wakikata maeneo yao vipande vipande na kuviuza kwa haraka ili kuepuka fidia za Serikali,biashara hiyo ya vipande vidogovidogo maarufu kwa ishirini kwa ishirini
“Hali hiyo licha ya kusababisha migogoro ya ardhi baini ya familia lakini imekuwa chanzo cha makazi holela kutokana na kugawana viwanja kienyeji visivyopimwa na kuleta adha kubwa Serikalini”alisema Samandito
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Ardhi Plan Gombo Samandito alisema kuwa ili kuondokana na uvamizi,migogoro ya ardhi na makazi holela ni lazima Serikali ione umuhimu wa upimaji wa viwanja vya makazi,biashara kwa kutumia Kampuni binafsi kwa gharama za wananchi wenyewe kwani jambo hilo linawezekana
Samandito alisema kuwa kwa kutumia sheria ya mipango miji namba 8 ya mwaka 2007 ambayo katika kifungu cha 15(2) inamruhusu mmiliki wa ardhi kuandaa michoro ya mipango miji na kupima,ambapo mmiliki anaweza kuandaa mpango wake hata kama tayari kuna mpango mwingine umeshaandaliwa kabla ya kupitishwa na Halmashauri husika
Alisema kuwa sheria ya mipango miji kifungu cha 15(8) pia inamtaka mmiliki wa ardhi anayetaka kuandaa mpango kuandika barua kwa mamlaka husika(Halmashauri) kabla hajafanya shughuli hiyo na kwamba sheria hiyo inatoa fursa kubwa kwa mmiliki wa ardhi kutozuiwa kuandaa mpango katika eneo lake bali asaidiwe ambapo kifungu cha 15(9) ni wajibu wa Waziri wa Ardhi,Mkurugenzi wa mipango miji na vijiji na Katibu Tawala wa mkoa kumsaidia mmiliki wa ardhi kufanikisha mpango wake
Alisema kuwa sheria hiyo kifungu cha 35(1) inaeleza kuwa mamlaka husika au Mkurugenzi wa Halmashauri ndani ya siku 60 tokea kupokelewa kwa maombi ya kuombea kibali cha kutekeleza mpango au kubadilisha matumizi anatakiwa kutoa majibu ya kukubali au kukataa maombi hayo
Alieleza zaidi kuwa  kifungu cha 35(4) kinaeleza kuwa endapo mamlaka husika au Mkurugenzi wa Halmashauri ameshindwa kujibu barua ya maombi kwa muda ulioandikwa hapo juu kwenye kifungu kidogo cha 1,itachukuliwa kuwa maombi yaliyoombwa yamekubaliwa
Alisema kuwa kwa kutambua umuhimu wa mipango miji mizuri na uwepo wa sheria hiyo,Kampuni ya Ardhi Plan imeingia ubia na wananchi wa kata ya Mshangano Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma ya kuwapimia viwanja 18000 kwa kuanzia na mchoro namba 9 eneo la Beroya ambapo mradi huo ulizinduliwa Novemba 20 mwaka huu
Alifafanua kuwa mradi huo wa upimaji wa viwanja kwa kutumia Kampuni uliibuliwa na wananchi wenyewe baada ya kuona wanakaa na kuishi katika makazi holela yasiyopimwa kwa muda mrefu kwani miaka mingi wananchi wa kata hiyo wamekuwa wakipeleka maombi Halmashauri ya kuomba kupimiwa maeneo yao bila mafanikio kutokana na Halmashauri kukosa uwezo wa kifedha
“Mradi huo utawainua kiuchumi wananchi wa Kata ya Mshangano kwa sababu wataweza kukopaa kupitia makazi yao  na kwamba wataweza kuishi katika makazi bora yaliyopimwa na kufanya mji wa Mshangano kuwa wa kisasa zaidi kuliko maeneo mengine ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea”alisema Samandito
Alieleza kuwa mradi huo umezingatia upangaji wa miji wa kisasa na lazima utaenda sambamba na ulinganifu wa idadi ya watu katika kipindi cha miaka kuanzia 50 hadi 100 ijayo ili miundombinu na mahitaji mengine yawepo na yaweze kukidhi haja za wakati huo
Akielezea  Mradi huo Afisa Mtendaji wa Kata ya Mshangano Stan Kibiki alisema kuwa Mwaka 2010 kata yetu  ilibahatika kupata mradi wa upimaji viwanja wa Halmashauri lakini bahati mbaya fedha yenyewe ilikuwa kidogo kwani waliweza  kupima viwanja 347 katika mtaa wa Namanyigu eneo dogo mashambani hivyo tatizo la wananchi kuishi katika makazi holela lilibaki palepale
Alisema kuwa wananchi  kwa kushirikiana na viongozi wao katika kutatua tatizo hili waliamua kutafuta njia mbadala ambayo kwa kutumia sheria namba 8 ya Mipango Miji ya 2007 walitafuta Kampuni ya Ardhi Plan ya Jijini Dar Es Salaam ili iweze kuwapimia viwanja katika maeneo yao
Alieleza kuwa baada ya kuipata Kampuni hiyo makubaliano yakawa malipo ni ardhi kwa ardhi yaani wanapima ardhi wanalipwa ardhi kwa asilimia za kwamba mwananchi anapata 60% ya ardhi iliyopimwa na Kampuni inapata 40% ya ardhi iliyopimwa
Alifafanua kuwa asilimia 40% inayotolewa kwa Kampuni inatumika katika kuandaa michoro ya ubunifu wa mipango Miji (10%),kupima viwanja (10%)kuchonga barabara (10%) na faida ya Kampuni (10%) na kwamba mradi huu hauhusishi malipo ya fidia yoyote hii ni kwa makubaliano ya wananchi wenyewe na itakuwa kwa kusogezana
Afisa huyo alisema kuwa maeneo ya umma kama vile soko,shule,zahanati ,makaburi,stendi,msikiti,kanisa na maeneo ya wazi(open space)  yatatolewa bure katika mradi huo na kufanywa kuwa mradi wa kwanza kuibuliwa na wananchi wenyewe kwa kuitumia Kampuni ya Ardhi Plan kupanga mji wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Alieleza kuwa gharama za mradi huo zinatolewa na wananchi wenyewe kwa kutoa ardhi badala ya kusubiri  Serikali mpaka ipate uwezo wa kifedha ambapo kwa wale wenye maeneo madogo yaani kiwanja kimoja mpaka viwili wanatozwa gharama ya fedha shilingi laki moja(100,000/=) kwa kiwanja kimoja na laki mbili(200,000) kwa viwanja viwili kama gharama za upimaji
Kibiki alisema kuwa mitaa ambayo  michoro yake imekamilika ni Mshangano,Namanyigu, na Mitendewawa yenye jumla ya viwanja elfu kumi na nane (18,000/=) ambapo mitaa mingine itafuata baadaye
Alieleza zaidi kuwa huduma za jamii kama maji ya bomba,umeme,barabara na miundombinu mingine itawafikia kama ambavyo wananchi wa kata ya Mshangano wanavyotegemea kupata mara baada ya mradi kukamilika
Kibiki alisema kuwa katika mradi huo wananchi watapata faida nyingi ikiwemo ya ajira kuanzia hatua ya kupima viwanja kwani mchoro mmoja umetoa ajira kwa watu 40 ambao wamekuwa wanalipwa  Tshs 4000/= kwa kutwa moja na kwamba kwa michoro 23 itatoa ajira kwa watu 920
Alifafanua kuwa kwenye uchongaji wa barabara mchoro mmoja umetoa ajira kwa watu 80 ambapo kila mmoja analipwa Tshs 5000/= kwa kutwa hivyo michoro 23 itatoa ajira kwa watu 1840 ambapo jumla ya michoro yote 23 wananchi watakao kuwa wamepata ajira kwenye upimaji na kuchonga barabara ni watu 2760 wanawake na wanaume
Alieleza jumla ya fedha watakayokuwa wanapata wananchi wa kata hiyo kwenye upimaji wa viwanja ni 920X4000=3680,000/= na kwenye uchongaji wa barabara 1840x5000=9,200,000/= na kufanya jumla ya fedha yote kuwa ni Tshs 12,880,000/= kwa siku
Alifafanua kuwa wafanyakazi hao watatoka ndani ya kata ya Mshangano ambapo mradi unatekelezwa kwani hiyo inaweza kuwasaidia sana wananchi kujikimu kimaisha na kumudu kununua pembejeo za kilimo katika msimu huu na hivyo kuzalisha mazao kwa wingi
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Ardhi Plan Gombo Samandito alimalizia kwa kusema kuwa wakati nchi yetu inapata uhuru ilikuwa na watu na watu milioni 9 lakini kwasasa inawatu milioni 40 na wanaishi kwenye maeneo yasiyopimwa
Alisema inakadiliwa kuwa ifikapo mwaka 2028 idadi ya watanzania itakuwa milioni 75 hii ni kwa kutumia ongezeko la asilimia 2.9 kwa mwaka ikilinganishwa na watu milioni 33.67 mwaka 2002 hali hiyo ni lazima Serikali ione umuhimu wa Kampuni binafsi kupima ardhi ili wananchi waweze kuishi kwenye makazi yaliyopimwa kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo
Alieleza kuwa jambo hilo linawezekana kwa makubaliano ya wananchi kulingana na maeneo wanayoishi kwa gharama zao ili kujenga mustakabali mzuri na usimamizi mzuri wa matumizi ya ardhi na Kampuni zitakazohitajika kupima ardhi hiyo na kuondoa migogoro mingi ya ardhi iliyopo kwenye maeneo yetu na kukomesha adha ya kuwepo kwa makazi holela kwani uwepo wa makazi holela ni kipimo cha umaskini
Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana 0755-335051