About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Saturday, November 5, 2011

MAWAKALA WA USAMBAZAJI PEMBEJEO WAONYWA RUVUMA

                  Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu
Na Mwandishi Wetu,Songea
SERIKALI  ya Mkoa wa Ruvuma imewaagiza Maafisa kilimo wa Wilaya zote Mkoani humo na Mawakala wa pembejeo kusimamia vizuri ugawaji wa vocha za pembejeo za Mkoa huo ambao umepewa mgao wa vocha  64,417.
Maagizo hayo yametolewa  jana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ,Said Mwambungu wakati akifunga kikao cha pembejeo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Songea Club kilichohudhuriwa na wadau zaidi ya 500.
Aliwataka mawakala wa kugawa pembejeo kutoongozwa na maslahi ya fedha bali wanapaswa kuifanya kazi hiyo kwa moyo wa kupenda na kuwajali wananchi jambo ambalo litaondoa malalamiko na kufanya falsafa ya kilimo kwanza  ifanikiwe.
Alisema kuwa katika msimu uliopita wa 2010/2011 Mkoa  huo ulifanikiwa kwa kiwango kikubwa katika kilimo cha mahindi na kuwapongeza wakulima kwa kuitikia falsafa ya kilimo kwanza.
‘Kwa kweli Mkoa wa Ruvuma umepiga hatua kubwa katika msimu huu na matokeo yake mnayaona ambapo tumekuwa na  mahindi mengi na hadi sasa tumetumia shilingi bilioni 7 kulipa madeni  na kununua mahindi na yaliyopo zinahitajika shilingi bilioni 8 kuyanunua’alisema.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa kila ambaye anaidai serikali baada ya kuuza mahindi yake atalipwa na hivyo hakuna  haja kwa mwananchi kuwa na wasiwasi wa kutolipwa pesa yake hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kupeleka mahindi yao kwenye hifadhi ya Taifa ya chakula.
Mwambungu alisema agenda yake kubwa  na kipaumbele chake ni maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma hususani katika suala la kilimo kwa kuwa Mkoa huo ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kulima zao la mahindi Nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Songea, Thomas Sabaya alisema mawakala wasumbufu katika zoezi la ugawaji wa vocha wataondolewa katika kazi hiyo na wale watakaohujumu zoezi hilo watachukuliwa hatua kisheria kama walivyochukuliwa maofisa wa Manispaa waliotuhumiwa na wizi wa vocha 459  katika msimu uliopita.
 MWISHO

VETA RUVUMA KUWAFUATA WAHITAJI MAFUNZO KWENYE MAENEO YAO

Mkurugenzi wa VETA kanda ya Kusini Monika Mbelle

Na Gideon Mwakanosya,Songea
MAMLAKA ya mafunzo ya ufundi stadi(VETA) Mkoani Ruvuma imeanza kutoa mafunzo ya ufundi wa aina mbalimbali na udereva maeneo ya vijijini kwa malengo ya kupunguza ajali na kuwafuata wahitaji huko waliko na kukuza uchumi wa wananchi wa vijijini kupitia ufundi.
 
Mku wa Chuo hicho Mkoani humo  Gideon Ole Lairumbe akizungumza na mtandao huu wa www.stephanomango.blogspot.com ofisini kwake jana amesema mafunzo hayo kwa kuanzia yamefanyika katika  kijiji cha Langiro Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma ambapo  wananchi 45 wamenufaika na mafunzo hayo ya wiki mbili huku wengine 56 wakijiandikisha kwa mafunzo mengine.
 
Alisema kuwa baada ya mafunzo hayo kwenye kijiji hicho mafunzo mengine yatafuata kwenye kijiji cha Luanda ,Liuli na Mbamba’bay katika Mji mdogo wa Mbamba bay Wilayani humo.

Lairumbe alisema mafunzo yaliyotolewa ni ya ufundi wa umeme jua ili waweze kunufaika  na nishati hiyo vijijini,ufundi wa kutengeneza pikipiki na udereva wa pikipiki na magari na kwamba kwa kuanzia wametoa mafunzo ya ufundi na udereva wa pikipiki kwa wiki mbili katika kijiji cha Langilo.
 
‘Tumejipanga kutoa mafunzo haya kwa lengo la kuwanufaisha wananchi hivyo natoa wito kwa WanaRuvuma  kuunda vikundi na kuomba mafunzo ili tuwaletee mafunzo hukohuko vijijini’alisema Mkuu huyo wa Chuo cha Veta Ruvuma .
 
Alisema kuwa mafunzo ya udereva wa magari na pikipiki yanatimiza maagizo ya Serikali ya kuwa na madereva wenye sifa wanaofuata sheria za barabarani hivyo kuamua kubadili leseni za madereva wote na kuzifanya ziwe za kisasa zaidi.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Nyanda za juu kusini inayojumisha Mkoa ya Mbeya,Iringa na Ruvuma , Monica Mbelle alsema kuwa baada ya Serikali kuruhusu pikipiki kutumika kama chombo cha kubebea abiria jamii imeshuhudia  ongezeko kubwa la ajali za barabarani.
 
Alisema kuwa  Wilaya ya Mbinga ina pikipiki nyingi kuliko Wilaya nyingine Mkoani Ruvuma na kwamba wenye pikipiki hizo wako mjini na vijini na kwa sababu hiyo anasema VETA ikaamua kuwafuata wahitaji wa mafunzo ya udereva huko waliko ili waweze kupata mafunzo hayo huku wakiendelea na   shughuli nyingine.
 
Akifunga mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya  Mbinga Kanali Mstaafu  Edmund Mjengwa aliwataka wahitimu wa mafunzo hayo kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kupunguza wimbi la ajali.
 
‘Mtambue kwamba ujuzi mlioupata hautakuwa na maana kama hamtautumia kwa manufaa yenu na kwa jamii inayowazunguka na katika hili mwendesha pikipiki asipoendesha kwa kufuata shera za usalama barabarani atapoteza maisha yake na ya abiria wake na  hii itakuwa haina maana kwa mafunzo haya’alisema.
 
Aliwataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kwamba wasipozingatia sheria za usalama barabarani na kusababisha ajali watachukuliwa hatua kali za kisheria.
MWISHO

UHABA WA SARUJI RUVUMA KUTOKUKAMILISHA MIRADI YA UJENZI

                           Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu
 Na Mwandishi Wetu,Songea
IMEBAINIKA kupanda kwa bei ya saruji Mkoani Ruvuma kutoka kati ya sh. 15000 na sh. 18,0000 na kufikia sh. 20000 hadi 25,000 kwa mfuko mmoja wa kilo 50 kumetokana na saruji hiyo inayozalishwa Mkoani Mbeya kuuzwa nje ya ya nchi na nyingine chache kuuzwa kwenye Makampuni makubwa yanayotengeneza barabara Mkoani Ruvuma,
 
Uchunguzi uliofanywa na www.stephanomango.blogspot.com  kwa kuzungumza na Mawakala wa kuuza saruji umebaini kuwa saruji hiyo nyingi imekuwa ikiishia nje ya nchi hasa Malawi na hivyo Mkoa wa Ruvuma hupata mgao mdogo unaoishia kwenye makampuni makubwa ya kutengeneza barabara.
 
Gazeti hili lililotembelea kwenye maduka ya kuuza saruji lilishuhudia kuadimika kwa bidhaa hiyo na kubaki maduka matatu pekee yakiuza kwa bei ya juu huku baadhi ya mawakala wakidai wanaiuza bidhaa hiyo kwa bei ya juu kwa kuwa wanainunulia kwenye soko la Makambako na si Mbeya ambako inatengenezwa.
 
Mmoja wa Wafanyabiashara ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alisema wamekuwa wakisafirisha saruji toka Makambako kwa bei ya sh. 2000 kwa mfuko,bei inayodaiwa kuwa ni kubwa sana na kwamba kama ingesafirishwa na kampuni ingesafirishwa kwa bei ya chini hivyo saruji ingeuzwa kwa bei ya awali. 
 
Kupanda kwa bei ya mfuko wa Saruji kumewapa wakati mgumu wakandarasi  mkoani Ruvuma  katika  kutekeleza miradi ya ujenzi inayofanywa na baadhi yao na kuhofia miradi hiyo kutotekelezeka kwa wakati kama mikataba yao inavyo wataka .
 
Wakiongea na mtandao huu wa www.stephanomango.blogspot.com
  kwa nyakati tofauti wakandarasi hao walisema kuwa miradi mingi ambayo inajengwa hivi sasa haitamalizika kwa wakati kutokana na mfumuko wa bei ya vifaa vya ujenzi ikiwamo saruji kuwa kubwa na kuwafanya kushindwa kumudu gharama za ununuzi wa vifaa hivyo .
 
Mmoja wa wakandarasi hao Victor Ngongi alisema kuwa bei walizo andikia pindi wanaomba miradi hiyo zimekuwa tofauti na ilivyo sasa ambapo awali mfuko mmoja wa saruji uliunzwa kwa bei ya shilingi 15,000 hadi 18,000 jambo ambalo kwa sasa mfuko mmoja unauzwa kwa bei ya shilingi 20,000 hadi 25,000.
 
Ngongi alisema kufuatia hali hiyo baadhi ya  wakandarasi hao wameonyesha nia ya kuiandikia Serikali barua ya kusimamisha kuendelea na shughuli ya miradi ya ujenzi huo kwa lengo la kuepusha gharama zisizo kuwa za lazima kulingana na mikataba  waliyokubaliana ikiwemo kukabidhi kazi kwa wakati.
 
Hata hivyo baadhi ya wakazi wanaoishi mkoani humo walipohojiwa walisema kuwa suala hilo la mfumuko wa bei ya vifaa vya ujenzi  Serikali isipochukua hatua za haraka katika kudhibiti mfumuko huo  kunaweza kuahatarisha  majengo mengi kujengwa chini ya kiwango jambo ambalo ni hasara kwa serikali.
 
Naye wakala wa uuzaji wa saruji kupitia kampuni ya Mohamed Enterprises  Mkoani Ruvuma   Sadick Yusuph [Mpemba] alisema kuwa kuadimika kwa saruji hiyo kunatokana na saruji nyingi kuuzwa nje ya nchi na  asilimia kubwa ya mgao  huchukuliwa na makapuni makubwa ambayo yanajishughulisha na ujenzi wa barabara jambo  linalofanya asilimia inayobaki kuwa ndogo na kushindwa kutosheleza mahitaji.

Makampuni makubwa yanayojenga barabara Mkoani Ruvuma ni Sinno Hydro inayotengeneza barabara ya kutoka Peramiho hadi Mbinga,Sogea Sotom inayotengeneza barabara ya Songea hadi Namtumbo na Progresive inayotengeneza barabara ya Namtumbo hadi Tunduru ambazo zote zinatengenezwa kwa kiwango cha lami.

Aidha Sadick alisema kuwa njia pekee ya   kukabiliana na changamoto hiyo katika kufanikisha kupungua kwa bei  ni vyema viwanda vinavyotengeneza bidhaa hiyo vikaongeza uzalishaji zaidi kwa lengo la kutosheleza mahitaji ya wananchi .
 
Kwa upande wake Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Dr. Anselm Tarimo amewaagiza wafanya biashara wa saruji Mkoani humo kuangalia uwezekano wakupunguza bei ya bidhaa hiyo ambayo imepanda ghafla na kuwaumiza wananchi.
 
Alisema kupanda huko kwa saruji kunatokana na mgomo baridi kunatokana na mgomo baridi wa Wasafirishaji wanaosafirisha saruji kutoka Mbeya kuleta Songea wakati ambao wanaitoa Makambako wakati ambako ilitakiwa kusafirishwa na kampuni ya Tembo sementi ya Mbeya na kwamba  Makambako kuna saruji ya kutosha.
 
Alisema mfumo wa usafirishaji ndio unaoyumbisha bei hivyo Mkoa unajipanga kukutana na wasafirishaji na kuzungumza nao ili kuweza kutatua tatizo hilo ambalo linakwamisha miradi ya ujenzi ya maendeleo. 
 MWISHO.