Gideon Mwakanosya ,Songea
WAHAMIAJI haramu 68 kati ya 82 Raia wa Somalia waliokamatwa katika kijiji cha Lihuli wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wamehukumiwa kwenda kutumikia kifungo cha miazi sita jela kila mmoja baada ya kukiri kosa la kuingia nchini kinyume na sheria za nchi.
Akizungumza na Waandishi wa habari jana ofisini kwake Afisa uhamiaji wa mkoa wa Ruvuma Koku Rwebandiza amesema kuwa wahamiaji haramu hao walikamatwa oktoba 8 mwaka huu majira ya saa moja jioni kwenye msitu wa miti uliopo katika kijiji hicho wakiwa safarini kuelekea Afika kusini kupitia Malawi.
Amesema,wahamiaji 14 kati ya hao 82 waliokamatwa ambao umri wao ni kati ya miaka 13-17 mahakama imeamuru Idara ya uhamiaji kufanya utaratibu wa kuhakikisha kuwa wanarudishwa Somaria kwa kupitia ubalozi wa nchi yao.
Amesema kuwa,ofisi yake ilipata taarifa toka kwa raia wema kuwa kuna kundi la watu wasihofahamika wanahofiwa kuwa ni wahamiaji haramu wako kwenye msitu na baada ya kupata taarifa hizo kikosi maalum cha maafisa wa uhamiaji walienda katika msitu huo na kufanikiwa kukamata kundi kubwa la wahamiaji haramu .
Ameeleza zaidi kuwa,wahamiaji haramu hao baada ya kuhojiwa walisema kuwa wametoka Somalia kupitia bahari ya hindi kwa njia ya maboti hadi tanga na baadaye walipata usafiri wa gari aina ya roli ambayo iliwafikisha njombe na baada ya hapo walipata usafiri mwingine hadi Ludewa ambapo walifanikiwa kupata boti hadi Lihuli ambapo ziwa lilichafuka kutokana na mawimbi kuwa makubwa hivyo walilazimika kupumzika hadi ziwa litakapo kaa sawa ili waendelee na safari hadi walipokamatwa na maafisa uhamiaji.
Aidha,ameongeza kuwa Idara ya uhamiaji kwa kushirikiana na Jeshi la polisi Mkoa wanaendelea kulisaka boti liliowasafirisha wahamiaji haramu hao kwani mara baada ya kukamatwa wahamiaji hao nahodha wa boti hiyo alikimbia pamoja na boti yake.
MWISHO