About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Saturday, April 20, 2013

VIBAKA WAUA ASKARI POLISI KAHAMA



Na Ali Lityawi, Kahama

ASKARI polisi wa kitengo cha usalama barabarani, wilayani Kahama, Salum Mtepa, ameuawa usiku wa kuamkia jana na watu wanaosadikiwa kuwa ni vibaka kutoka machimbo madogo ya dhahabu ya Nyangarata na Mwime, baada ya kumpiga na kitu kizito kifuani.

Tukio hilo lilitokea nyumbani kwake eneo la kata ya Majengo mjini Kahama usiku wa kuamkia jana baada ya watu hao wanaokadiriwa kuwa wanne kwenda nyumbani kwa askari huyo mwenye cheo cha Staff Sajenti na kuvunja kibanda cha biashara kwa lengo la kuiba ndipo askari huyo alipotoka nje kwenda kupambana nao.

Inadaiwa kuwa baada ya kutoka nje vibaka hao waliokuwa na pikipiki, watatu kati yao walikimbia akabaki mmoja aliyekuwa na kifaa ambacho hutumiwa na wachimbaji wa dhahabu katika machimbo madogo madogo kwa ajili ya kuvunjia miamba ya mawe ambacho hujulikana kwa jina la Moko.

Kwa mujibu wa taarifa ya mkuu wa polisi wilaya ya Kahama, George Simba, askari huyo alipigwa na kifaa hicho kifuani wakati akijaribu kupambana na kibaka huyo, hali iliyosababisha avuje damu nyingi ndani ya kifua na kusababisha kifo chake.

Simba alisema hali ya vibaka katika mji wa Kahama ni mbaya kwani wameongezeka kutokana na machimbo ya Nyangarata kujaa maji na Mwime kuisha uzalishaji wake, hali iliyofanya vijana wengi kutoka kwenye maeneo hayo kutokuwa na fedha.

Alisema hivi sasa wimbi la vibaka hao limekuwa tishio huku akiahidi kupambana nao pia kuwasaka kwa nguvu zote waliohusika na kifo cha askari huyo wa usalama barabarani, ingawa hadi jana hakuna mtu yeyote aliyekuwa amekamatwa kuhusiana na tukio hilo.