Na Stephano Mango, Songea
WANAWAKE nchini wametakiwa kuzisikiliza sera za Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema na kujiunga na chama hicho chenye malengo ya kuleta ukombozi kutoka mikononi mwa Chama cha Mapinduzi ambacho kimewanyonya watanzania kwa muda mrefu na kuwafanya maskini
Wito huo umetolewa jana na Katibu wa wanawake wa Chadema Jimbo la Songea Asia Ngonyani akiwahutubia mamia ya wananchi baada ya kufungua Tawi la Chadema na Ofisi ya Chama hicho mtaa wa Kuchile kata ya Seedfarm Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwenye ziara yenye lengo la kuimarisha chama katika kata za pembezoni mwa mji
Ngonyani alisema kuwa Chama cha Mapinduzi kimekuwa kikiwatumia wanawake kwenye chaguzi mbalimbali na kuwavesha vilemba na vitenge ambavyo hata ukivaa vinaangaza na baada ya kumaliza uchaguzi na kuunda Serikali ambayo imekuwa ikikosa mipango na vipaumbele vya kuwakomboa wanawake kiuchumi na kijamii
Alieleza kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekuwa ikiwanyanyasa na kuwadhalilisha sana wanawake wanapokuwa kwenye biashara zao ndogondogo kwa kuwakamata na kuwanyang’anya vitu vyao kwa kutumia mgambo wa mji hali ambayo inaendelea kuwaondolea utu katika jamii
Alisema kuwa kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikiwadanganya wakina mama kuwa huduma za kujifungua ni bure na matibabu ya mtoto wa chini ya miaka mitano ni bure wakati wakina mama wanalipia huduma hizo kwa fedha nyingi
Alifafanua kuwa licha ya wakina mama kulala wanne wanne kwenye kitanda kimoja na wengine kulala chini , basi ukitaka kufa au kupoteza mtoto katika vituo vya afya au Hospital za Serikali usiwe na fedha au umwambie muuguzi kuwa natakiwa kupata huduma za matibabu bure
Naye Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Ruvuma na Diwani wa Kata ya Mjini Joseph Fuime akiwahutubia wananchi hao alisema kuwa Serikali imeshindwa kuwaheshimu watanzania kutokana na matendo yao katili dhidi ya wananchi kutokana na kuwapandishia gharama za maisha kila kukicha,kushindwa kutekeleza ahadi ya maisha bora kwa kila mtanzania,kuwatoza kodi nyingi huku wakishindwa kutoa huduma stahiki kulingana na kodi zinazotozwa kwa wananchi
“Ili kufanya mabadiliko katika nchi hii ni lazima wananchi waamue kuchukua hatua za kuzisikiliza sera za Chadema na kujiunga nacho ili kuweza kuleta ukombozi stahiki mara uchaguzi wa Serikali za Vijiji,Mitaa na katika uchaguzi mkuu wa Madiwani,Wabunge na Urais”alisema Fuime
Alisema kuwa leo tumefungua Ofisi ambayo imegharamiwa na baadhi ya wanachama wa Chadema katika kata yenu hivyo tumewaletea chama chenye uhai na matumaini kwa watanzania na ambacho kina dhamira ya kweli ya kuwakomboa watanzania
Alieleza kuwa hakuna anayelazimishwa kukipokea na kujiunga nacho hivyo kama mnataka kuendelea kukandamizwa na Serikali ya Ccm miaka 50 ijayo ya uhuru,mnahiyali ya kukipokea au kukikataa kwa faida yenu na vizazi vijavyo
MWISHO