About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Wednesday, February 22, 2012

SONGEA YAGEUKA UWANJA WA MAPAMBANO KATI YA POLISI NA WANANCHI


MADEREVA PIKIPIKI WAKIWA WAMEFUNGA BARABARA YA SONGEA KWEWNDA TUNDURU KARIBU NA MLANGO WA KUINGILIA OFISI YA MKUU WA MKOA WA RUVUMA

Polisi wakiwatawanya na kuwakamata baadhi ya waandamanaji hao katika manispaa ya Songea baada ya wakazi wa manispaa hiyo wengi wao wakiwa madereva wa pikipiki kuandamana hadi ofisi ya kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma kupinga mauaji ya watu yanayoendelea kwa kasi mjini humo ambao hadi sasa jeshi la polisi halijafanikiwa kuwakamata wauaji.
 Polisi wakiwa katika mishemishe za kutuliza fujo na kujeruhi raia


Mama ambaye hakufahamika jina lake mara moja akiwa anaokotaa vipande vya taa ya gari yake baada ya kujeruhiwa katika vurugu hizo

Na Stephano Mango,Songea.

WATU watatu wamefariki dunia na idadi kubwa ya watu wanadaiwa kujeruhiwa kutokana na hali tete iliyozuka katika mji wa Songea mkoani Ruvuma, baada ya mamia ya wananchi na madereva wa pikipiki maarufu kwa jina la yeboyebo, kuandamana kuelekea kituo kikuu cha polisi na ofisi ya mkuu wa mkoa huo, wakipinga mauaji ya raia ambayo yameshamiri katika mji huo.
Kufuatia maandamano hayo kushika kasi katika mji huo, jeshi la polisi lililazimika kuingilia kati kwa kuanza kupiga mabomu ya machozi na risasi za moto hewani ikiwa ni lengo la kuwatawanya raia hao wasiendelee kuleta vurugu.  
Wakati mabomu na risasi hizo zikipigwa, ghasia za hapa na pale zilianza kujitokeza baadhi ya wananchi wakirusha mawe kuelekea kituo kikuu cha polisi na wengine wakipaza sauti wakielekeza lawama kwa jeshi hilo kwamba limeshindwa kudhibiti mauaji hayo.
Vurugu hizo zimesababisha ofisi za serikali na taasisi binafsi mkoani Ruvuma kufungwa kwa muda yakiwemo maduka na huduma za kifedha katika mabenki zimesimama kwa muda.
Huduma za usafiri katika stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani nazo zimesimama huku madereva wa mabasi na abiria wakikimbia kujificha kwa lengo la kuepukana na mabomu ya machozi na risasi za moto zilizokuwa zikipigwa hewani.
Pia huduma za matibabu katika hospitali ya mkoa huo nazo zimesimama kwa muda baada ya walinzi wa hospitali hiyo kufunga lango kuu kutokana na raia wengi walikuwa wakikimbilia huko wakiepukana na mabomu yaliyokuwa yakipigwa hewani.
Matukio ya mauaji katika mji wa songea yalianza kujitokeza mapema mwezi Novemba mwaka jana yakiendelea hadi sasa, ambapo kila baada ya siku kadhaa watu walikuwa wanauawa katika mazingira ya kutatanisha huku miili ya marehemu ikikutwa imejeruhiwa vibaya.
Watu tisa wameuawa katika mji huo tokea matukio ya mauaji yaanze kujitokeza katika mji wa Songea huku miili mingine ikiokotwa bila kuwa na sehemu za siri na kwamba watuhumiwa wanne wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo wanashikiliwa na polisi.
Watuhumiwa wanaoshikiliwa na jeshi la polisi ni Johari Kassim (16), Onesmo Hinju (14), Samason Haule (22) na Mussa Fuala (20) wote wakazi wa mtaa wa Lizaboni mjini Songea.
Pamoja na mambo mengine mpaka habari hizi zinaingia mitamboni Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma hawakuweza kupatikana kuzungumzia sakata hilo huku simu zake zikiwa zimefungwa na askari polisi mjini hapa wakiendelea kupiga mabomu ya machozi, kwa lengo la kutawanya watu.
Uchunguzi uliofanywa na mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com umebaini kuwa vurugu hizo zimetokana na  wananchi hao kutokuwa na imani kwa Jeshi hilo kwa madai kwamba  halifanyi kazi yake ipasavyo katika kusaka majambazi na watu wengine wanaojihusisha na vitendo hivyo viovu badala yake nguvu kubwa wanaitumia katika kusaka na kukamata pikipiki zinazodaiwa kuwa na makosa
Vurugu hizo zilitokea jana baada ya wananchi hao wenye hasira kali kuona mauaji hayo yakizidi kuendelea siku hadi siku jambo ambalo liliwafanya waanze kufanya maandamano yenye lengo la kuilalamikia serikali kutokana na siku hiyo ya tukio kuokota mwili wa mtu mmoja ambaye anadaiwa kuwa ni muendesha pikipiki akiwa ameuwawa na watu wasiofahamika hali iliyowafanya wananchi hao walifuatilie gari la Polisi ambalo lilifika kuchukua mwili wa marehemu huyo ambaye jina lake halikuweza kufahamika wakati wakiiupeleka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mkoa Songea ambako vurugu hizo zilianzia
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com  baadhi ya wananchi Mkoani humo wamedai kwamba tangu matukio haya yaanze kutokea Jeshi hilo halijachukua hatua ya kupita kila kata  kwa lengo la kutoa Elimu kwa wananchi hususani kwenye maeneo ambayo yamekumbwa na mkasa huo na kuongea na wananchi wake.
Akizungumza kwa njia ya simu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu alisema kuwa kitendo cha wananchi kuleta vurugu sio cha kushabikia hivyo aliwataka wananchi  kutoa ushirikiano kwa Jeshi hilo katika kuwafichua watu wanaojihusisha na vitendo hivyo viovu kwa kuwa watu hao wanaishi katika jamii na kudai kwamba Jeshi peke yake bila ya kupata ushirikiano toka kwa raia wema haliwezi kufanya kazi yake ipasavyo.