About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Friday, September 30, 2011

HATMA YA KUFUKUZWA UWANACHAMA MADIWANI WATANO SONGEA MJINI MIKONONI MWA KAMATI YA SIASA YA HALMASHAURI KUU YA CCM MKOA WA RUVUMA

                       
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Songea Mjini Hemed Dizumba
                        
Katibu wa CCM wilaya ya Songea Alfonce Siwale
Na  Mwandishi Wetu,Songea
CHAMA cha  Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Songea mjini Mkoa wa  Ruvuma  kimetoa mapendekezo ya kuwafukuza uanachama wa chama hicho  madiwani  watano kwa madai ya kukiuka taratibu za chama hicho kwa kupiga kura za hapana kwa mgombea wa umeya Bw. Charles Mhagama anayedaiwa kupitishwa kwa kura za hapana 14 na za ndiyo 12.
Katika kikao cha kamati ya siasa kilichokaa hivi karibuni ambacho kolikuwa na ajenda tatu ikiwemo agenda ya kufungua mkutano,kupata taarifa ya kamati ya maadili ya Ccm Wilaya kuhusu uchaguzi wa Umeya uliofanyika Septemba 23 mwaka huu na kufunga mkutano ambapo Madiwani hao katika kikao cha kwanza cha maadili walitishia kurudisha kadi za chama hicho kutokana na kutoridhishwa na muenendo wa chama hicho unaotokana na kuvurugwa na kigogo mmoja wa ngazi ya Serikalini
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu sakata hilo jana ofisini kwake Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Alfonce Siwale alikiri kufanyika kwa vikao hivyo viwili cha maadili na kamati ya siasa na kudai kuwa madiwani wote wa chama hicho walihojiwa kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa Umeya
Siwale alisema kuwa baada ya kikao cha maadili kuwahoji madiwani wote ndipo kamati ya siasa ya halmashauri kuu ya wilaya ilipoketi na kujadili kwa kina kilichojili kutoka kwenye kamati ya maadili kuhusiana na uchaguzi huo

Katibu huyo alieleza kuwa kuna mambo mengi yamejadiliwa kwenye kikao hicho pamoja na mwenendo wa chama baada ya uchaguzi huo wa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea uliokitia doa chama cha Ccm na kumdharirisha Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Emmanuel Nchimbi
Alipotakiwa na waandishi wa habari kueleza kilichojadiliwa kwenye kikao hicho,Siwale alieleza  kuwa kanuni za chama hicho zinaeleza kuwa kinachojadiliwa na Kamati ya Siasa ya halmashauri kuu ya Wilaya kinakuwa siri kwani mambo yake mengi yanawasilishwa kwenye Kamati ya Siasa ya chama hicho mkoa ili kiweze kuyajadili na kuyatolea maamuzi hivyo wao ndio wanaweza kutoa taarifa sahihi kwa kile tulichowapelekea kutoka Wilayani
Alipoulizwa kuhusu habari zilizozagaa mitaani kuwa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Nchimbi ndiye aliyeshinikiza kurudishwa jina la Diwani wa kata ya Matogoro Charles Mhagama na Madiwani wawili wa Viti Maalum ,alikanusha kuwa sio kweli na kama mtu anaushahidi wa hilo basi ieleweke alifanya hivyo kwa ushawishi wa kawaida wa uchaguzi
Kwa upande wake wa Katibu wa Ccm Mkoa wa Ruvuma Emmanuel Mteming”ombe alipohojiwa na waandishi wa habari kuhusiana na sakata hilo alisema kuwa wamepokea mapendekezo kutoka Ccm Wilaya ya Songea Mjini  ya kuwafukuza madiwani watano wa chama hicho na Kamati ya Siasa ya Ccm Mkoa inaendelea na vikao vyake ili kuweza kufikia hitimisha la sakata hilo
Mteming”ombe alisema kuwa hali ya chama kwa sasa ni tete hivyo maamuzi mengi  yanayofikiwa katika vikao vya chama hicho vinapaswa kuzingatia matakwa ya wananchama wake ili kuweza kurudisha imani kwa wananchi ambao ndio wanaokiangalia chama hicho kwa ukaribu sana
Awali ilidaiwa kuwa madiwani saba wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea wanatarajiwa kunyang”anywa kadi na Chama hicho kutokana na kukisaliti chama hicho kwa kumpigia Diwani wa Kata ya Matogoro Charles Mhagama kura za hapana 12 na za ndio 14 katika uchaguzi wa septemba 23 mwaka 2011 na kuwataja madiwani hao kuwa na kata zao kwenye mabano  Christian Matembo ( SeedFarm),Faustine Mhagama(Mshangano)
Wengine ni Victor Ngongi(Ruvuma)Kurabest Mgwasa(Msamala)Gelard Ndimbo(Ruhuwiko)Wilon Kapinga (Ndilimalitembo)na Genfrida Haule diwani wa Viti Maalum wa Chama hicho
MWISHO

HAYA NDIYO MTANDAO HUU UMEWEZA KUKUSANYA SIKU YA UZINDUZI WA GARI YA DHAHABU ILIYOFANYIKA KWENYE VIWANJA VYA NSSF

 Mtendaji wa TCCIA mkoa wa Ruvuma Philemon Moyo akionyesha gari ya dhahabu iliyotolewa kwa wajasiriamali juzi kwa ushirikiano wa KOICA na TCCIA mkoa wa Ruvuma
 Wakorea wa Kujitolea wakiwa na nyuso za furaha wakati wa hafla ya uzinduzi wa gari ya dhahabu
 Wakorea wa Kujitolea wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa hafla ya uzinduzi wa gari ya dhahabu juzi
 Viongozi wa Korea,TCCIA na Kaimu Mkuuwa Mkoa wa Ruvuma Thomas Oley Sabaya wakizindua gari ya dhahabu kwa kupakia bidhaa za wajasiriamali katika gari hilo
 Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Thomas Oley Sabaya akimpa zawadi ya Mvinyo Meneja wa Programu ya Wakorea wa Kujitolea Hwang,Jin Yung(Jenne) kushoto ni Mwenyekiti wa TCCIA mkoa wa Ruvuma Mays Mkwembe
 Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Ruvuma Mays Mkwembe akizungumzia mfumo wa utafutaji wa Masoko na Uuzaji bidhaa kwa kutumia gari ya dhahabu
Meneja wa Programu ya Wakorea wa Kujitolea Hwang,Jin Yung akitoa hotuba wakati wa uzinduzi wa gari ya dhahabu
Mtaalamu wa Masoko wa Kujitolea Jaehong,Cho akitafsiri hotuba iliyotolewa na Meneja wa Programu ya Wakorea wa Kujitolea Hwang,Jin Yung wakati wa uzinduzi wa gari ya dhahabu

Thursday, September 29, 2011

WAJASIRIAMALI WATAKIWA KUTUMIA FURSA ZILIZOPO KUKUZA SHUGHULI ZAO

                    Na Stephano Mango,Songea
WAJASIRIAMALI wa mkoa wa Ruvuma wametakiwa kutumia rasilimali zilizopo mkoani humo katika shughuli zao ili ziweze kuwasaidia kuondokana na umasikini miongoni mwa jamii zinazowazunguka

Wito huo umetolewa jana kwenye viwanja vya NSSF na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Thomas Oley Sabaya wakati wa uzinduzi wa  mradi wa utafutaji wa masoko na uuzaji wa bidhaa kwa kutumia gari ya dhahabu iliyotolewa kwa wajasiriamali wa mkoa wa Ruvuma kwa ushirikiano wa Chemba ya Wafanyabiashara,Wenye Viwanda na Kilimo(TCCIA) na Wakorea chini ya mradi wa KOICA

Sabaya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Songea alisema kuwa Mkoa wa Ruvuma una hali ya hewa nzuri ambayo unaweza kuifanyia shughuli yoyote ile ya kijasiliamali hivyo wananchi wanapaswa waitumie fursa hiyo vizuri katika kukuza uchumi wao na wa jamii yote kiujumla

Alisema kuwa imebainika kuwa wajasiliamali ni muhimu sana katika kukuza uchumi endelevu wa nchi lakini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi ambazo tunapaswa kuziondoa ili waweze kuchangia kikamilifu uchumi wan chi yao

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Meneja wa Programu ya Wakorea wa Kujitolea Hwang,Jin Yun(Jenne) alisema kuwa mradi huo ni ushirikiano kati ya KOICA na TCCIA Ruvuma wenye dhumuni la kuimarisha mfumo wa utafutaji wa masoko na uuzaji bidhaa kwa kutumia gari katika mkoa wa Ruvuma

Jin Yung alisema kuwa KOICA kupitia Programu ya Korea ya marafiki wa kujitolea wa dunia ambao husambazwa sehemu mbalimbali husaidia kuijengea uwezo miradi midogo iliyopo kwenye taasisi wanazofanyia kazi

‘Katika mradi huu Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini kupitia Shirika la Kimataifa la maendeleo la Korea(KOICA) imetoa msaada wa dola za Kimarekani 29,550 ambapo TCCIA Mkoa wa Ruvuma imechangia dola za Kimarekani 650 katika kukamilisha mradi huu pia napenda kuushukuru uongozi wa TCCIA kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Jaehong Cho kwani bila yeye tusingeweza kufanikisha mradi huu”alisema Jin Yung

Awali Mwenyekiti wa TCCIA mkoa wa Ruvuma Mays Mkwembe akitoa utangulizi wa uzinduzi huo alisema kuwa kwa kushirikiana na KOICA tulifanikiwa kuibua mradi huu ambao unazinduriwa ukiwa na lengo la kuwasaidia wajasiliamali katika nyanza ya usafirishaji na uuzaji bidhaa mbalimbali ili ziwafikie wateja kwa urahisi na kwa muda muafaka

Mkwembe alisema kuwa mradi huu utasaidia kutatua changamoto zinazowakabili wajasiriamali kama vile tatizo la usafiri wa bidhaa kwa gharama kubwa pia bila kuwa na gari ya uhakika,tatizo la kutafuta masoko,kuvumisha na kutangaza bidhaa zao

Alifafanua kuwa kazi ya gari la dhahabu itakuwa ni usafirishaji wa bidhaa hadi kwenye soko ambapo muuzaji anahitaji,kuuza bidhaa mbalimbali katika gari,kutangaza na uvumishaji wa bidhaa mahali popote,maonyesho ya bidhaa kupitia gari,kutangaza shughuli mbalimbali za biashara,kukodisha gari kwa shuguli mbalimbali

 Mwenyekiti huyo alisema kuwa taasisi ya TCCIA ilianzishwa mwaka 1998 mkoani Ruvuma ambapo hadi sasa TCCIA iko katika mikoa yote 21 ya Tanzania Bara na kwamba ipo mbele katika kukuza na kuendeleza sekta binafsi katika mkoa wa Ruvuma

Mkwembe alisema kuwa kazi kubwa ya taasisi hiyo ni pamoja na utetezi na ushawishi katika kujenga mazingira vutivu ya kuendeleza sekta binafsi,kujenga mazingira ya mahusiano na majadiliano na Serikali katika kuendeleza dhana ya ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma

Alizitaja kazi nyingine kuwa ni utoaji wa taarifa za masoko na biashara mbalimbali kwa kupitia kituo cha taarifa,kutoa mafunzo mbalimbali ya kuendeleza biashara na ujasiriamali,utoaji wa hati ya uasili wa bidhaa
MWISHO




 Viongozi wa ngazi mbalimbali wa TCCIA Ruvuma wakifuatilia hotuba zilizokuwa zikitolewa kwenye uzinduzi huo
 Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Thomas Oley Sabaya akisikiliza hotuba iliyokuwa inatolewa na Meneja wa Programu ya Wakorea wa Kujitolea Hwang,Jin Yung(Jenne)katikati,wa kwanza kushoto ni Mtaalamu wa Masoko wa Kujitolea Jaehong Cho ambaye alikuwa mkalimani wa lugha ya Kikorea kwenda kiswahili
Afisa Biashara Mkoa wa Ruvuma Nehemia Jemes akipita mbele ya kikundi cha ngoma kilichotumbuiza wakati wa uzinduzi wa gari ya dhahabu

UZINDUZI WA MRADI WA UTAFUTAJI WA MASOKO NA UUZAJI BIDHAA NI MKOMBOZI WA WAJASILIAMALI

 Kikundi cha Mletere kikitumbuiza wageni na Wajasiriamali mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo ya uzinduzi wa gari ya dhahabu jana
 Wageni mbalimbali wakifuatilia kwa umakini hafla hiyo muhimu kwa wajasiliamali jana

Bidhaa ambazo zinazalishwa Tanzania na wajasiliamali wake zikiwa zimepangwa vizuri kwenye shelfu maalumu ili kuwawezesha washiriki kuangaria na kuzinunua ikiwa ni fahari kununua bidhaa zinazotengenezwa na wajasiliamali wa ndani

HALI TETE NDANI YA CCM,VIJANA WA CCM SONGEA WATISHIA KUKIMBILIA UPINZANI


                       Na Joseph Mwambije,Songea

VIJANA wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM) Mkoani  Ruvuma wamekitaka Chama hicho  kurejesha nguvu iliyokuwa nayo miaka ya 70 enzi ya Mwalimu Nyerere ya kuwachukulia hatua Viongozi wa Serikali wanaojihusisha na ufisadi vinginevyo watakihama na kwenda Upinzani.
 
Walitishia kukihama Chama hicho hivi karibuni kwenye Mkutano ulioitishwa kwa ajili ya kupata maoni yao ya namna ya kurejesha heshima yake na kujua  kwa nini Vijana wanakichukia Chama hicho kilichoshika dola.
 
Walitoa  kauli za kukitahadharisha Chama hicho mbele ya wajumbe wawili wa Baraza la vijana wa CCM  Taifa  ambao pia ni wajumbe wa kamati ya watu nane inayozunguka Nchi nzima kuchukua maoni ya vijana na kuyafanyia kazi kwa lengo la kurejesha heshima ya Chama hicho.
 
Mmoja wa Vijana hao ambaye anatoka kwenye kundi la vijana wasomi Razalo Komba alisema shida kubwa inayokipata Chama hicho inatokana namna ya watendaji wabovu wa Serikali ambao wanatumia vibaya madaraka yao ndani ya Serikali na kuwatendea vibaya wananchi.
 
Alisema kuwa wapinzani wameijengea chuki inayotokana na Viongozi wa juu wa Serikali kushindwa kutimiza wajibu wao na kufanya mambo kana kwamba hakuna utawala wa sheria hivyo wanajiona wao ni Miungu watu wanaoweza kufanya chochote bila kuguswa.
 
‘Kwa jinsi mambo yanavyokwenda inaonyesha dhahiri kwamba CCM haiwapendi wasomi na udhaifu huo wapinzani wameutumia na kuwateka wasomi na hivi sasa inaungwa mkono na wasomi wengi ambao wana uzalendo na Nchi yao ambao wanaona mambo yanakwenda ndivyo sivyo,kama mambo yatakwenda hivi yanavyokwenda hata mimi nitahamia  Upinzani’alisema.
 
Kijana mwingine  Amoni Mtega alisema Chama hicho kimepoteza mvuto mbele ya watu kwa kuwa kinashindwa kujibu hoja za Wapinzani hivyo akakitaka kujibu hoja hizo tena kwa wakati huku akisisitiza kwamba kwa kushindwa kuzijibu hoja hata kama ni za uongo wananchi wanayaaamini yanayosemwa.
 
Alisema kuwa vijana wamedharauliwa na kunyimwa fursa za maendeleo na ndio sababu wanakimbilia kwenye vyama vya upinzani ambavyo wanaviona kuwa mkombozi wao mpya badala ya Chama cha CCM.
 
Akizungumza mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo Joseph Mkilikiti  alisema maoni hayo watayafikisha kwenye Baraza kuu Taifa ambalo litapeleka kwenye uongozi wa juu wa Chama hicho ili yaweze  kufanyiwa kazi.

Mkutano huo ulitonosha vidonda vya makundi ya uchaguzi wa mwaka jana kati ya kambi za Oliver Mhaiki na ya Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Emanuel Nchimbi baada ya Vijana  wa kambi ya Nchimbi ambao walitokea upinzani kumsifia Mbunge huyo na kumponda Mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa CCM Songea Mjini Vikta Ngonyani ambaye hakuwa kambi ya Mbunge huyo kwamba hajasoma,hafanyi ziara kuwatembelea vijana na kwamba hawezi kukabiliana na siasa za sasa.
 
Akifunga mkutano huo huku akionekana kujibu hoja za vijana hao Mwenyekiti huyo wa vijana wa CCM Songea mjini alisema kuwa inashangazwa na maneno ya vijana hao kuwa bado hawajui taratibu za chama hicho kwani waliingia na kukuta ziara zimeshafanyika  hivyo amewataka watulie iliwajifunze na siku zijazo watapata uongozi ndani ya chama hicho.
 
Alisema vijana hao ndio waliosababishan CCM kupoteza Kata tano za Mjini kwa kuwa Mbunge alikuwa akiwatumia kufanya kampeni na badala ya kuomba kura wao walikuwa wakiwatukana wapiga kura hivyo wapiga kura waliwaadhibu kwa kuwachagua madiwani wa CHADEMA.
       MWISHO.  

CHADEMA KUMPINGA MEYA ANAYEDAIWA KUCHAKACHUA MATOKEO YA KITI HICHO TUKUFU

Na  Joseph Mwambije,Songea
CHAMA cha demokrasia na maendeleo(CHADEMA)Mkoani Ruvuma kimepanga kufanya maandamano makubwa ya kupinga uchaguzi wa Meya wa Manispaa ya Songea ulio mwezesha Charles Mhagama kuwa Mstahiki Meya anayedaiwa kuchaguliwa kwa kura za ndiyo 12 na za hapana 14 na kuweka kambi kwenye viwanja vya Manispaa.
 
Hayo yamebainishwa juzi na Mwenyekiti wa Chama hicho wa Mkoa wa Ruvuma Bw. Joseph Fuime wakati akiwahutubia maelfu ya wananchi wa Songea kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya msingi mfaranyaki.
 
Alisema kuwa sababu kubwa ya kufanya maandamano hayo ni kupinga uchaguzi huo uliofanyika bila kufuata taratibu na kwamba licha ya kuwa Halmashauri ya Manispaa Songea kuwa maskini lakini wamemchagua Meya aliyedai kuwa ni mwizi.
 
‘Wamemchagulia Meya aliyehusika na uuzaji wa greda kwa shilingi milioni18,ununuzi wa gari  bovu la Zimamoto kwa shilingi milioni 350 ambalo halifanyi kazi na huu ni mpango wa Wabunge kuweka watu wao ili waibe fedha’alisema na kuongeza
 
‘Mlifanya makosa makubwa kumchagua Nchimbi(Emanuel Nchimbi) na mngemchagua Mbogoro(Edson Mbogoro) kuwa  Mbunge wenu  tusingepata Meya mwizi na kama ingekuwa enzi ya Nyerere Nchimbi angejiuzulu anamtka Meya huyo ili amtumie kujinufaisha na tunatamka kuwa huyo si Meya wa wananchi ni Meya wa Mbunge na atapopita mitaani mumzomee’alisema.
 
Alimshambulia Mbunge wa jimbo la Songea Mjini  Emmanuel Nchimbi kuwa hana nia njema na wananchi wake na kwamba watakuwa tayari kutoa ushahidi kuwa kura ziliibwa na hivyo watapambana kwa kutumia  akili na busara na watashinda.
 
Alisema kuwa kabla ya kufanya maandamano hayo watazunguka kata 21 za Manispa ya Songea kufanya mikutano ya kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwenye  maandamano na kuanda vyakula na taa na kisha kuvigeuza viwanja vya Manispaa kuwa Viwanja vilivyomng’oa  madarakani aliyekuwa Rais wa Misri.
 
Hata hivyo  Bw. Mhagama alipoulizwa kuhusu tuhuma za kuhusika na ununuzi wa gari bovu la Zimamoto,uuzaji wa greda alisema yeye hausiki na tuhuma hizo kwa kuwa magari hayo yalinunuliwa saba Nchi nzima na kwamba greda liliuzwa kwa kufuata sheria zote.
 
Naye  katibu wa Jimbo la Songea Mjini Bw. Masumbuko Paul alisema kuwa Wabunge wa Mkoa wa Ruvuma wamekuwa mzigo kwa wananchi wao kwa kushindwa kuwatatulia matatizo yao kama tatizo kubwa la umeme na ajira kwa wananchi,alisema kuwa siku za CCM kukaa madarakani zinahesabika.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Songea Mjini Idd Abdalah alilaani kukihusisha CHADEMA na udini,ukabila  na urangi na kuwataka Waislamu kuondoa dhana hiyo na kuungana kuiondoa CCM madarakani huku akiwapongeza madiwani wa CCM waliopiga kura za hapana kwa Mhagama.
Mwisho
 




MGODI WA MAKAA YA MAWE WA NGAKA KUZALISHA UMEME MEGAWATTS 120

Na Joseph Mwambije,Songea
 
MGODI wa Makaa ya mawe wa Ngaka uliopo katika kijiji cha Ruanda , wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma utaanza kuzalisha Umeme kiasi cha megawatts 120 katika kipindi cha miaka miwili kuanzia sasa baada ya Kampuni ya TANCOAL Energy inayomiliki Mgodi huo kupata leseni ya biashara hiyo.
 
Shughuli za uchimbaji wa Makaa ya Mawe zilizozinduliwa rasmi hivi karibuni  na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Cyril Chami aliyeambatana na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo la Taifa NDC Dkt.Chrisant  Mzindakaya.
 
Mgodi huo wa Makaa ya mawe wa Ngaka, unamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania yenye asilimia 30, na kampuni ya Intra Energy ya Australia yenye hisa asilimia 70.
 
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri huyo wa Viwanda na Biashara  alisema mradi huo utaleta ukombozi mkubwa kwa Tanzania ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya kukosekana kwa nishati ya umeme wa kutosha.
 
“Ukikosa umeme maana yake viwanda haviwezi kufanya kazi, ajira zinapungua, wafanyabiashara wanaathirika na shughuli zingine za uzalishaji mali zinakwama” Alisema Dkt Chami.
 
Aidha Waziri huyo aliongeza kuwa Wizara yake itaunga mkono juhudi za kufanikisha mradi huo kwa kuwa inaamini utakua mkombozi wa Taifa katika kipindi kifupi kijacho.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TANCOAL Energy Bw. Graeme Robertson alisema kwa sasa mradi huo unazalisha tani 30,000 za makaa ya mawe kwa mwezi sawa na tani 360,000 kwa mwaka ambazo huzisambaza katika viwanda vya hapa nchini ikiwemo viwanda vya saruji vya Mbeya na Tanga.
 
Bw. Robertson alisema kwa kuanzia TANCOAL Energy itazalisha megawatts 120 za umeme katika kipindi cha miaka miwili kuanzia sasa, lakini uzalishaji huo utakua ukiongezeka hadi kufikia megawatts 2,000 kwa kuwa eneo hilo la Ngaka lina hifadhi kubwa ya makaa ya mawe inayozidi tani milioni 250 na kwamba utafiti unaoendelea unaonesha eneo hilo linaweza kuwa na hifadhi kubwa zaidi.
 
Aliongeza kuwa katika utekelezaji wa Mradi huo kampuni hiyo licha ya kuinufaisha Tanzania kwa nishati ya kutosha ya umeme, pia itahakikisha inaisaidia jamii kwa kutoa ajira na kununua bidhaa za kilimo zinazozalishwa na wananchi
 
Naye Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la Maendeleo la Taifa NDC Dkt.  Mzindakaya aliwaondoa shaka watanzania, akisema mradi huo una manufaa makubwa zaidi kwa Tanzania kuliko kwa mwekezaji.
 
Alisema kuwa Tanzania pamoja na kunufaika na umiliki wa kampuni ya TANCOAL Energy kwa asilimia 30 pia itanufaika na matokeo ya kuwepo kwa umeme wa kutosha ambao utaihakikishia ustawi wa viwanda, biashara na kilimo.
 
Mzindakaya pia alisema haina sababu kwa Taifa kulaumiana kwa kuchelewa kuitumia rasilimali hiyo na badala yake viongozi wachukue hatua ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
 
Mbunge huyo Mstaafu aliongeza kuwa wapo baadhi ya wanasiasa ambao wamekua wakinung’unika na kulaumu wakati wao wenyewe hawachukui hatua zozote za kuwasaidia wananchi.
 
“Hata huu mradi sio watu wote watauunga mkono, wapo watakaoupinga lakini sisi NDC tutasonga mbele” Alitamba Dkt Mzindakaya na kuongeza kuwa NDC na bodi yake hawawezi kuingia mkataba wa kijinga.
 
Katika hatua nyingine Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt Chami amekanusha vikali uvumi ulioenezwa kuwa Mradi wa Makaa ya mawe wa Ngaka unapanga kujenga mitambo ya kuzalisha umeme katika wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya badala ya Mbinga Mkoani Ruvuma.
 
Chami alisema uvumi huo hauna ukweli wowote na kwamba, mitambo hiyo itajengwa katika makutano ya Mto Ruhuhu na Mto Ngaka yaliyopo jirani na yanapochimbwa makaa hayo wilayani Mbinga.
 
Pamoja na kuzindua uchimbaji wa makaa hayo ya mawe alisema pia alikabidhi vyeti kwa wanafunzi wa shule ya msingi Mtunduwalo ambao wamefuzu majaribio ya kujifunza kazi za makaa ya mawe na pia amezindua madarasa matatu ya shule hiyo ya msingi ambayo yamejengwa kwa ufadhili wa kampuni ya TANCOAL Energy.
 
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la  Mbinga mashariki Bw. Gaudence Kayombo ambaye amekua chimbuko la Mradi huo alielezea furaha yake ya kuanzishwa kwa mradi huo na kutoa wito kwa wananchi wake kujipanga kuuza bidhaa za kilimo kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo pamoja na kuchangamkia fursa ya ajira
Mwisho

Tuesday, September 27, 2011

SAKATA LA UMEYA SONGEA; KAMATI YA SIASA YA CHAMA CHA MAPINDUZI WILAYA YA SONGEA YADHAMIRIA KUWATIMUA MADIWANI WATANO

Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Songea Alfonce Siwale

MJI WA SONGEA UMEKUMBWA NA UHABA MKUBWA WA NISHATI YA MAFUTA YA DIZEL NA PETROL NA KUSABABISHA ADHA KUBWA KWA WATUMIAJI WA NISHATI HIYO

 Watumiaji wa nishati ya Mafuta wakiwa wamefanikiwa kupata mafuta kiduchu kwenye vidumu ili waweze kuendeshea shughuli zao zinazotegemea nishati hiyo
 Foleni ya kuhitaji nishati ya mafuta katika kituo cha mafuta cha Kisumapai

AFARIKI KWA KUTUMBUKIA KWENYE MFEREJI WA MAJI,MWINGINE ALAZWA KWA KUGONGWA NA TREKTA

   Na Augustino Chindiye,Tunduru

MKAZI wa kitongoji cha Ndondwa katika kijiji cha Ujamaa Lelolelo aliyefahamika kwa jina la Ashimu Likungwa (35) amefariki dunia baada ya kutumbukia katika mfereji wa banio la kumwagilia mashamba ya wakazi wa kijiji hicho.

Taarifa za tukio hilo ambazo zimedhibitisha ma Mtendaji wa kijiji cha Leloleo Reheme Mangochi zinasema kuwa marehemu Likungwa amefariki dunia kutokana na kupatwa na ugonjwa wa kifafa wakati akitaka kuoga katika mfereji huo na kwamba ugonjwa huo umekuwa ukimsumbua siku nyingi.

Mangochi aliendelea kufafanua kuwa mwili wa marehemu Likungwa uliokotwa na Watoto ambao alienda nao kuoga katika maeneo hayo na kwamba kabla ya kupatwa na mauti hayo marehemu alifanikiwa kuvua nguo zote kwa nia ya kuoga akiwa peke yake hali ambayo ilimfanya ashindwe kujiokoa baada ya kupatwa na ugonjwa huo.

Wakati huo huo mtoto wa Miaka 13 aliyefahamika kwa jina la Arifa Saidi amelazwa katika hospitali ya serikali ya Wilaya ya Tunduru baada ya kugongwa na Trekta dogo aina ya Power tilla na kuvunjika mguu wake wa kulia.

Akiongea kwa tabu mtoto huyo alisema kuwa mkasa huo ulimkuta wakati akijaribu kudandia baada ya kukamirisha zoezi la kupakia matofari ambayo walikuwa wakipakia kwa nia ya kujipatia chochote ili waweze kuendesha maisha yao ya kila siku.

Akizungumzia matukio hayo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael kamuhanda alisema kuwa Polisi wanaendelea na uchunguzi wa matukio hayo.
 MWISHO

WALIMU WAWILI WANUSURIKA KUUAWA KUTOKANA NA WIVU WA KIMAPENZI WILAYANI TUNDURU

Katibu wa Chama Cha Walimu (CWT)Mkoa wa Ruvuma Luya Ngonyani

Na, Augustino Chindiye Tunduru

WATU watano wanashikiriwa na jeshi la Polisi Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma kwa tuhuma za kufanya majaribio ya kutaka kuwaua Walimu wawili wa Shule ya Msingi Ruanda iliyopo katika Tarafa ya Nakapanya Wilayani humo.

Taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa Walimu walionusulika katika tukio hilo ni Mwl. Ezakieli Ngaleka na Mwl.Emmanuel Hyao wanaodaiwa kuwa na urafiki wa kimapenzi na mke wa mtu.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda  amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Ally Brashi (19) ambaye pamoja na mambo mengine amekiri kuhusika katika tukio hilo akidai kuwa alitekeleza tukio hilo kwa nia ya kutaka kumuua Mwl. Naleka akiwa anamtuhumu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Mkewe.

Wangine wanaoshikiriwa kutokana na tukio hilo ni pamoja na Mustafa Mariki (19), Mahamudu Juao (21), James Mathayo (20) na Hamisi Athuman (19)  wote wakiwa ni wakazi wa kijiji hicho.

Akizungumzia tukio hilo Kaimu afisa elimu wa shule za Msingi wa Wilaya ya Tunduru Mwl.Fravia Nchimbi alisema kuwa kufuatia tukio hilo idara yake imeamua kuwabadirishia vituo vya kazi ili kuwahakikishia usalama wa maisha yao.

Nae Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mwl. Rashid Mandoa alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alisema kuwa ofisi yake imewaagiza viongozi wa serikali ya kijiji hicho kufanya mazungumzo na  wananchi wao ili waachane na matukio ya aina hiyo.

Kuhusu nyumba iliyoteketea na moto huo alisema kuwa siyo mali ya Halmashauri hiyo bali ilikuwa ikimirikiwa na mkazi wa kijiji hicho  Fikirini Brashi ambaye alikuwa na mkataba wa kuwapangisha walimu hao na kwamba baada ya tukio hilo kamati ya shule na uongozi wa kijiji ndio utakaowajibika kumjengea nyumba nyingine.

Wakiongea kwa nyakati tofauti walimu hao walimshukuru mungu kwa kuwaokoa na tukio hilo pamoja na uongozi wa halmashauri hiyo ambao umekubali kuwagharamia kwa kuwanunulia vifaa na kuwafidia mali zilizo teketea katika tukio hilo zinazo kadiliwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni moja.

Mwisho


Sunday, September 25, 2011

SAKATA LA UMEYA SONGEA LAWAKUTANISHA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA RUVUMA NA WAZIRI DKT NCHIMBI

 Waziri wa Habari,Utamaduni na Michezo Dkt Emmanuel Nchimbi katikati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu sakata la kukimbia na sanduku la kura wakati wa uchaguzi wa umeya uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Saccos wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea,kushoto ni Charles Mhagama anayedaiwa kuwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea,kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Naftan Saiyoloi
 Waandishi wa habari wakiendelea kusikiliza hoja mbalimbali katika kikao cha waandishi wa habari na Waziri Dkt Nchimbi
 Waziri Dkt Nchimbi aliyekaa katikati akiwa kwenye picha ya pamoja na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Waliokaa kutoka kushoto Charles Mhagama(Anayedaiwa kuwa Mstahiki Meya),Waziri wa Habari,Utamaduni na Michezo Dkt Nchimbi,Endre w Kuchonjoma(Mwenyekiti wa Ruvuma Press Club),Waliosimama kutoka kulia Nathan Mtega(Katibu Msaidizi wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Ruvuma),Endrew Chatwanga(Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini),Gerson Msigwa(TBC),Emmanuel Msigwa(Channel Ten) Ngaiyona Nkondora(Star Tv na Redio Free) Juma Nyumayo(Uhuru Fm) Alpius Mchucha(HabariLeo)Stephano Mango(Dira ya Mtanzania) Amon Mtega(Mtanzania) Joseph Mwambije(Majira) Anuciata Ngatunga(Ps wa Dkt Nchimbi)Cresencia Kapinga(Majira) Meja Mgumba(Msaidizi wa Waziri) Joyce Joliga(Mwananchi) Naftan Saiyoloi(Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Na Mwandishi wetu
 WAZIRI wa Habari Utamaduni na Michezo Dkt Emmanuel Nchimbi amekutana na waandishi wa habari na kuzungumzia sakata la kudaiwa kukimbia na sanduku la kura kabla ya kudhibitiwa na Madiwani wa Chadema juzi katika uchaguzi wa nafasi wazi ya Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea

Akisoma tamko lake katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea alisema kuwa amesikitishwa na vyombo vya habari,magazeti ya Tanzania Daima,Majira na Mwananchi vilivyolipoti habari hiyo iliyojaa upotoshaji mkubwa

Dkt Nchimbi amevitaka vyombo hivyo kukanusha na kumuomba radhi katika matoleo yao ya Septemba 26 katika ukulasa wa mbele kwani vimemshushia hadhi yake katika jamii na kumjengea misingi ya ukosefu wa uaminifu

Alisema kuwa mnamo tarehe 23 Septemba 2011 magazeti ya Tanzania Daima,Mwananchi na Majira yaliripoti taarifa inayofanana kwamba Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo amekimbia na sanduku la kura kufuatia vurugu zilizotokea katika uchaguzi wa Meya wa Manispaa ya Songea

“Napenda kuutaarifu umma kwamba habari hizo siyo za kweli na ni uzushi mtupu,ukweli ni kwamba mimi katika kikao hicho sikukimbia na sanduku la kura wala hakuna diwani yeyote aliyetoka au kukimbia nje ya ukumbi na sanduku la kura kama ilivoripotiwa na magazeti hayo”alisema Dkt Nchimbi

Alieleza kuwa ukisoma upotoshwaji huu katika magazeti yaliyoandika habari hizo utagundua kwamba habari hizo zimeandikwa na mtu mmoja na kuwagawia waandishi wenzake wa magazeti mengine bila kuthibitisha wakazipeleka kwenye magazeti yao

“Taarifa hizo zilizopotoshwa kwa makusudi zimenidhalilisha,kunichafulia jina langu na kunifanya kuwa mtu nisiyeaminika kitaifa na kimataifa”alisema Dkt Nchimbi

Alieleza zaidi kuwa tabia iliyoanza kuzoeleka hivi sasa ya mwandishi mmoja kuandika kisha kuwasambazia wenzake unawazalilisha waandishi wenyewe na vyombo wanavyoviandikia

Alisema kuwa kwa taarifa hii nayataka magazeti ya Tanzania Daima,Mwananchi na Majira kukanusha na kusahihisha taarifa hizo kwenye magazeti yao ya kesho tarehe 26 September 2011
 Kwenye ukurasa wa mbele na kuniomba radhi
MWISHO

KUNDI LA TEMBO LASABABISHA MAUAJI YA BINADAMU TUNDURU

Na Augustino Chindiye ,Tunduru

MKAZI wa kitongoji cha Ndola kilichopo katika kijiji cha marumba Wilayani Tunduru Daud Rashid (50) amefariki dunia baada ya kuvamiwa na kushambuliwa na kundi la tembo.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa tukio hilo lilitokea wakati marehemu akiende shambani ambako inadaiwa kuwa alikuwa akienda kufanya maandalizi ya shamba la kulima msimu ujao.

Akizungumzia tukio hilo Kaimu Afisa Wanyama pori wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma  Abdalah Mbanganike mbali na kukiri kuwepo kwa tukio hilo alisema kuwa marehemu alifariki dunia kutokana na kuchomwa na meno ya Tembo hao.

Alisema kufuatia hali hiyo idara yake imetoa askari watatu waliongozwa na Ally Salumu kwa ajili ya kuwasaka tembo hao na wameruhusiwa ku ua ili wasilete madhara mengine.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma  Michael kamuhanda katika maelezo yake alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi kujenga tabia ya kutembea katika makundi ili waweze kusaidiana.

Mganga aliye ufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Rashid Dkt. Moses Mwahasunga amesema kuwa kifo chake kimesababishwa na kutokwa na damu nyingi pamoja na kutobolewa tumbo na kuhalibu mfumo wa utendaji kazi wa viungo vilivyopo ndani ya mwili wa binadamu

Mwisho



CCM TUNDURU PECHEPECHE KWA UDHAIFU WA VIONGOZI WAKE WA WILAYA

Na Augustino Chindiye ,Tunduru

VIONGOZI,Wanachama na Wakereketwa wa Chama Cha Mapinduzi CCM Tarafa ya Nakapanya wametoa siku tatu kwa viongozi wa Chama hicho ngazi ya Wilaya kwenda kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua zikiwemo za kufukuzwa kwa kupigiwa kura za kuto kuwa na imani nao.

Tamko hilo limetolewa na wanachama hao katika kikao kilicho wahusisha viongozi wa Chama na jumuiya zake kilicho fanyika katika ukumbi wa ofisi ya Serikali ya Kata ya Namiungo kikiwa na nia ya kujadili mikakati ya kukinusuru chama hicho ili kisifanye vibaya katika chaguzi zijazo.
Sambamba na tamko hilo pia wanachama hao wametishia kutopiga kura katika uchaguzi ujao ama ikiwezekana watamuomba Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete awaruhusu wajiunge na kupiga kura katika Jimbo la Nanyumbu lililopo Mkoani Mtwara.

Wakiongea kwa jaziba wana CCM hao kutoka katika Kata za Nakapanya ambao waliongozwa na Mjumbe wa Mkutano wa  Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Tunduru  Likambale Omari, Shaib Akijo kutoka Kata ya Mindu, Yasini Kaweje kutoka Kata ya Ngapa na Mjumbe wa halmashuri Kuu ya CCM Wilaya Maimuna Bora kutoka Kata ya Muhuwesi walisema wameamua kuchukua maamuzi hayo baada ya kubaini kuwepo kwa ubabaishaji uliokithiri ndani ya Chama hicho huku kukiwa na taarifa za kubebana na kuwachagulia wananchi viongozi wanaotoa fedha kwao.

Aidha wanachama hao wakatolea mfano ubabaishaji wa taarifa za kuteuliwa kwa Diwani wa Viti Maalumu Wanawake wa Tarafa hiyo Salima Limbalambala ambaye mbali na kushiriki katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo  Faridu Khamisi baadae zilitolewa taarifa zenye utata za kutenguliwa kwa wadhifa huo na kuiweka Tarafa yao katika mkanganyiko ambao hadi leo Uongozi wa Chama hicho ngazi ya Wilaya haujatolea kauli yoyote ikiwa ni tofauti na walivyofanya baada ya kutenguliwa kwa udiwani wa Selemani Chisopa aliyetuhumiwa kufanyia kampeni vyama vya upinzani katika uchaguzi mdogo wa Kuziba nafasi ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Tunduru Marehemu Juma Akukweti.

Nao Diwani mstaafu  Hasan Futali, Dastan Amlima na Husen Ndayani ambao pamoja na mambo mengine walihoji vigezo na sababu za uhalali wa kutenguliwa kwa udiwani wa Salima Limbalambala ambaye jina lake lipo katika barua zilizo andikwa na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Taifa Rajab Kiravu na badala yake viongozi wa CCM Wilaya wakapendekeza na kumchagua Diwani wa Viti Maalumu wanaweke kutoka Tarafa ya Mjini Siwema Kalipungu ambaye hakupiga kura za Kumchagua mwenyekiti wa halmashuri huyo huku matokeo ya kuchaguliwa kwake yakiendelea kuheshimiwa.

Kwa ujumla maelezo ya viongozi hao Kero kubwa inayotembea vichwani na katika midomo yao ni Usimamizi mbovu wa Viongozi wa Chama hicho ngazi ya Wilaya ambao wamedai kuwa umeshindwa kusimamia haki kwa wanachama wake, hawafanyi mikutano ya uhamasishaji na wanasema uongozi huo kuwa umepoteza Dira na wakaendelea kutahadharisha  kwamba endapo CCM Taifa itawaachilia waendelee kuiongoza Wilaya hiyo kuna hatari ya chama hicho kufanya vibaya zaidi katika chaguzi zijao ukiwewmo uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.

Hata hivyo baada ya kutoa dukuduku zao hizo zenye maneno makali kwa uongozi wao ukafuata wasaa wa kutoa tamko la kuita kikao cha dhalula kilicho pangwa kufanyika Septembar 28 mwaka huu na kwamba watakao tolewa kafala katika kikaango hicho ni  uongozi wa CCM Wilaya unao ongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya  Mustafa Bora, Katibu wa CCM Wilaya Ramadhan Amer. Katibu Mwenezi CCM Wilaya Hasan Kindamba.

Wakizungumzia mgogoro huo baadhi ya madadisi wa masuala ya siasa walisema kuwa kupotea kwa mwelekeo na utashi wa viongozi wa chama Tawala CCM kunatokana na mfumo mbovu wa ufuatiliaji na upembuzi wa viongozi wanao takiwa kuwekwa madarakani tofauti na mfumo wa wasisi wa taifa hili Baba wa taifa hayati Mwl. Julius Nyerere  ambao wakati wao walikuwa makini nia viongozi wao na walikuwa wakihakikisha kuwa kiongozi anayefaa ni yule aliyepikwa na kuifa kisiasa.

Saturday, September 24, 2011

VIONGOZI WA CHADEMA KUUNGURUMA VIWANJA VYA SOKO LA SAMAKI KUPINGA UCHAKACHUAJI WA UMEYA SONGEA

Joyce Joliga,Songea

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kesho kinatarajia kufanya mkutano mkubwa wa hadhara ili kuwajulisha wananchi vurugu zilizotokea jana wakati wa uchaguzi wa Meya wa manispaa ya Songea na kusababisha uchaguzi kuvurugika kutokana na madai ya kuwepo kwa wizi wa kura.

Akizungumza na mwandishi wa mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ na Mwenyekiti wa chama hicho mkoa Joseph Fuime amesema, mkutano huo unatarajiwa kufanyika kesho majira ya saa 9 alasili hadi saa 12:00 katika  uwanja wa soko la Samaki lililopo karibu na shule ya Msingi Mfaranyaki .

Amesema,tayari kila kitu kimeshakamilika na wamepata vibali vya kufanya mkutano huo ambapo viongozi mbali mbali watahudhuria  akiwemo Mbunge wa jimbo la Mbozi Magharibi Silinde pamoja na wakili wa kujitegemea Edson Mbogoro.

Aidha,Fuime ametoa wito kwa wananchi wa Manispaa ya Songea kujitokeza kwa wingi kuhudhuria mkutano huo na tayari mambo yote yamekwenda vizuri na wanatarajia kuwa wananchi watafahamu kila kitu kilichojitokeza kutokana na vurugu hizo.

Kwa Upande wake Katibu wa Chadema Jimbo la Songea Paul Masumbuko amesema,chama kimesikitishwa na vitendo vya vurugu vilivyofanywa wakati wa uchaguzi huo na kueleza kuwa wanaungana mkono na Madiwani wao kutomtambua Mgombea wa umeya ikiwa ni pamoja na kutojishugulisha na shuguli zozote hadi uchaguzi utakaporudiwa.

"Kwanza kwa niaba ya chama  tunapenda kuwapongeza Madiwani wa CCM kwa kuungana na wenzao wa  Chadema ambao wapo  7 katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea wakati madiwani wa Ccm wapo 20 ambapo kwenye uchaguzi wa leo walikuwepo 19"lakini kwa kuonyesha kuwa hawamkubali mgombea wao wamempigia kura za hapana hiyo ndiyo demokrasia ya kweli ", alisema Masumbuko

 Amesema, kitendo kilichofanywa na Madiwani wa CCM kuungana na wenzao wa Chadema kimeonyesha ukomavu mkubwa wa demokrasia na kinapaswa kupongezwa kwa nguvu zote kwani upinzani si kupingana kwa kila kitu bali inapotokea maslahi ya wananchi ni vema waungane na kuonyesha uzalendo mkubwa kwa nchi na wananchi waliowachagua.

Katika tamko lililosomwa  jana na Madiwani wa Chadema  kwa niaba ya madiwani wenzake wa Chadema kwenye ukumbi wa Saccos ya halmashauri hiyo Diwani wa kata ya Bombamabili Kenny Mpangara alisema kuwa mazingira yote ya zoezi la uchaguzi yameonekana na utata kwa maslahi binafsi na kudai kuwa Madiwani wa Chadema watasusia vikao vyote vya halmashauri mpaka Meya mpya atakapopatikana .

Kwa upande wao Madiwani wa Chama cha Mapinduzi wakitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari na kusomwa na Diwani wa kata ya Lilambo Yobo Mapunda lilisema kitendo walichofanya Madiwani wa Chadema cha kufanya fujo na kutaka kuwapiga wengine ni kitendo kibaya sana katika kukuza demokrasia na kwamba CCm inamtambua Mstahiki Meya kuwa ni Charles Mhagama
MWISHO.