Na Stephano Mango, Songea
VIONGOZI wa dini na Wanakwaya nchini wametakiwa kumwomba Mungu kwa njia ya nyimbo na sala ili aweze kuwajalia viongozi wa Serikali nguvu za kumkataa shetani na mambo yake yote na awape busara na hekima katika kuliongoza Taifa kwa maendeleo ya wananchi
Wito huo umetolewa jana na Mhashamu Askofu Mkuu wa Jimbo la Songea Dkt Norbert Mtega wakati akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Cargo Stars Dionis Malinzi kwenye harambee ya uzinduzi wa Kanda ya Shetani Ameshindwa iliyoimbwa na kwaya ya Mt.Paulo Mtume Parokia ya Songea Mjini
Mtega alisema kuwa imeanza kujengeka tabia miongoni mwa viongozi wa Serikali kutoa maneno ambayo yanasababisha kuwepo kwa migawanyiko ya kiutendaji na kifikra miongoni mwa jamii kuhusu umoja na muungano wetu kama taifa
Alisema kuwa anapotokea mtu na kusema kuwa tusiliombee taifa, tusiimbe wimbo wa taifa au Tanzania igawanyike ni ishara ya nguvu za shetani kwasababu kazi yake kubwa ni kutia chuki miongoni mwa binadamu ili wachukiane na watengane na kuharibu tunu ya umoja wetu
Alifafanua kuwa umoja na muungano wetu kama taifa ni ishara ya maendeleo kwani kitendo cha kukaribisha migawanyiko husababisha amani kutoweka miongoni mwa jamii na ndio maana leo taifa linaanza kunuka damu kutokana na vitendo vya kikatili na mauaji yanayoendelea kutokea katika jamii zetu
“ Taifa limekumbwa na mambo ya kishetani sana kwani vitendo vya watu kuvamiwa, kutekwa, kuteswa, kujeruhiwa, kuuawa vinashamiri kwa kasi kubwa kutokana na wananchi kukosa imani na vyombo vya dola, jambo ambalo linaendelea kuathiri jamii zetu” alisema Mtega
Alisema Shetani akishindwa viongozi wetu watakuwa wakweli katika kuliongoza taifa na hapo ndipo amani, haki, uhuru wa kweli utapatikana na usawa wa binadamu na maendeleo yatasonga mbele
Kwa upande wake mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Cargo Stars Dionis Malinzi akitoa salamu zake kwenye harambee hiyo alisema kuwa kwaya zote zinapaswa kutunga nyimbo nzuri za kumtukuza mungu na kumkataa shetani ili upatikane wokovu wa kweli
Malinzi alisema kuwa kanda inayozinduliwa katika harambee hii inaitwa Shetani Ameshindwa ni njia nzuri ya kuimarika katika utume na imani za jamii ya watanzania
Kwa upande wake Mwenyeketi wa Kamati ya uzinduzi wa kanda hiyo Jumanne Nyingo alisema kuwa michango iliyopatikana ambayo imeletwa na mgeni rasmi kutoka kwake binafsi, kwa marafiki zake na michango iliyopatikana kutokana na ushawishi wake itasaidia mambo mengi sana katika kwaya hiyo kwa kununua vifaa mbalimbali
Nyingo alisema kuwa Mgeni rasmi Dionis Malinzi alitoa mchango wa shilingi milioni 16, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma alitoa shilingi laki tatu, ahadi milioni 1.6 na michango mingine ambapo jumla yake ni shilingi milioni 18.7 kwa ajiri ya kwaya, pia mgeni rasmi alitoa shilingi milioni 30 kwa ajiri ya Kanisa katoliki la Songea mjini
MWISHO