About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Thursday, June 30, 2011

KILICAFE YATIMIZA MIAKA 10 YA UZALISHAJI WA KAHAWA SPESHELI
Na,Stephano Mango,Songea
KAHAWA ni moja ya mazao muhimu katika kuliingizia taifa pato la kigeni ambapo Tanzania ni moja ya nchi zinazozalisha zao hilo na jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanya ili kuboresha zao hilo muhimu kwa uchumi wa taifa letu

Ili kutimiza adhima hiyo Serikali mara nyingi imekuwa ikihamasisha wakulima kujiunga na kuanzisha vikundi au ushirika ili kuongeza uzalishaji na ufanisi zaidi katika kurahisisha wataalam wa kilimo kuwatembelea na kutoa elimu ya kilimo bora

Katika uzalishaji wa kahawa bora wakulima wa kahawa aina ya Spesheri waliamua kuanzisha umoja wao ambao unafahamika kwa jina la Association of Kilimanjaro Specialty Coffe Growers wenye makao makuu mjini Moshi mkoani Kilimanjaro

Umoja huo kwa jina la kibiashara na maarufu unaitwa Kilicafe ikiwa ni alama muhimu ya mlima Kilimanjaro ambao ni fahari ya Tanzania na Afrika kwa ujumla ambapo wakulima hao wa kahawa aina ya Spesheli wakiwa kwenye umoja wao wanatarajia  mwaka huu wa 2011 kutimiza miaka 10 ya uzalishaji wa kahawa hiyo katika kanda ya kanda ya Kaskazini,Mbeya na Mbinga na sherehe ya kutimiza miaka hiyo inatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi juni mwaka huu

Akizungumza kwenye mkutano wa mwaka wa wanachama wa umoja huo uliofanyika wilayani Mbinga na kuhudhuliwa na viongozi wa Serikali na taasisi mbalimbali mei 17 mwaka huu Mkurugenzi Mtendaji wa umoja huo wa Kilicafe Geoffrey Mwangulumbi alisema kuwa umoja huo ulisajiliwa mwaka 2001

Mwangulumbi alisema kuwa umoja huo ulianza katika mikoa ya Kilimanjaro,Arusha na Manyara kwa ushirikiano wa vikundi kutokana na ushauri wa Shirika la Marekani la TechnoServe ambako umoja huo ulikuwa na vikundi wanachama 10

Alisema kuwa Kilicafe haikukomea mikoa ya Kaskazini bali ilijitanua hadi katika mikoa ya Mbeya na Ruvuma mwaka 2002 ambapo katika kurahisisha utendaji kazi wa umoja huo ulibuni mfumo wa uongozi wa kikanda na kugawanyika katika kanda ya kaskazini yenye mikoa ya Manyara,Kilimanjaro na Arusha,kanda ya Mbinga na kanda yaa Mbeya

Alisema kuwa umoja huu katika kanda ya Mbinga una vikundi vya kibiashara vya wakulima 120 na upo katika tarafa za Mbuji,Mbinga mjini,Mpepo na Namswea kukiwa na jumla ya wakulima zaidi ya 7000

Alisema kuwa malengo makuu ya umoja huo ni kuzalisha kahawa aina ya Spesheri iliyo bora ambayo itapata soko la uhakika katika masoko ya kimataifa,kuboresha maisha ya mkulima kwa kuhamasisha wakulima wanachama kuzalisha kwa wingi na kuandaa kahawa inayokidhi viwango vya soko na kutoa uwiano mzuri kiuchumi

Malengo mengine ni kutafuta masoko mazuri na endelevu kwa ajili ya kahawa inayozalishwa na wanachama ,kutoa mafunzo ya kilimo hususan agronomia na uandaaji bora wa kahawa kwa wananchama na kuwaunganisha kwenye taasisi za fedha ili waweze kupata mikopo ya mitaji ya kununua mashine za kumenyea kahawa na wagavi wa pembejeo

Mkurugenzi huyo wa Kilicafe alisema kuwa umoja huo umepata mafanikio na changamoto kadhaa ambazo zinawakabili kutimiza malengo yao ya kujikomboa kiuchumi ambapo alitaja mafanikio waliyoyapata kuwa ni pamoja na Umoja huo katika kanda hii kudumu kwa miaka tisa sasa, tangu mwaka 2002 ambapo kulikuwa na vikundi 22 tu, sasa vipo vikundi 120 na vikundi 17 vipya vimeomba kujiunga mwaka huu

Alisema kuwa mafanikio mengine ni chama kudumu kwenye shirika la fair-trade ambapo hupata faida ya bei ya wastani wa juu kwa kuwekewa kima cha bei ambapo ikishuka zaidi ya hapo kama ni hasara watafidia ambapo pia kwa kilo ya kahawa inayouzwa hulazimika kimfumo kupata fedha za kuendeleza miradi ya chama na kwamba miradi iliyonufaika na mpango huo ni ujenzi wa ofisi za vikundi na jengo la ofisi ya kanda pamoja na ghala la kuhifadhia kahawa za chama.

Alitaja mafanikio mengine ni makusanyo ya kahawa kuongezeka kutoka tani 420 msimu 2002/03 hadi tani 2,460 kwa msimu uliopita ingawa mwaka uliopita makusanyo yalishuka sana kutokana na hali mbaya ya hewa, ugonjwa wa vidung’ata na ushindani kuwa mkubwa ingawa hatimaye wastani wa mapato ya mkulima wetu ni ya juu kuliko wakulima walio wengi kwani tulikusanya tani 1700 na malipo ni wastani wa Sh 3975 kwa kilo ya kahawa ambapo jumla ya fedha Bilion 6.8 zimeingia wilaya ya Mbinga kwa wakulima wanachama wa Kilicafe

Pia alisema mafanikio mengine kusimika mitambo ya kukobolea kahawa 77 yenye ukubwa kuanzia nusu tani (0.5), tani moja na nusu (1.5) hadi tani mbili na nusu (2.5) kwa saa ambapo mitambo hiyo ya kumenyea kahawa ni za teknolojia ya hali ya juu ukiwa ni uwekezaji vijijini kwa wakulima wenyewe na kwamba mitambo hiyo inanunuliwa na wakulima wenyewe kwa mkopo ambapo umoja unakatwa fedha zake baada ya mauzo ya kahawa.

Alisema kuwa umoja unajivunia mafanikio ya kupata masoko mazuri ya kahawa ambayo hutuwezesha kupata bei nzuri kwa wastani kwani kwa kawaida ni sera ya Kilicafe kurejea nyuma kusawazisha malipo ya awali hii maana yake ni kwamba iwapo bei imeanza kwa TSh 2,000 kwa kilo na kisha kupanda hadi TSh 2,500. Soko huria hawarejei nyuma kuwalipa wakulima waliouza kahawa kwa bei ya TSh 2000 kwa kilo, jambo ambalo ni kinyume na sera yetu ya umoja wa kibiashara ambao hutoa malipo ya awali (bei ya ushindani).

“Sisi ama tunarejea nyuma na kufidia wote ili wawe na malipo sawa ya awali au malipo ya mwisho baada ya kuuza kahawa, hesabu za uwazi huwekwa mezani na kutoa gharama kisha kiasi chote kinachobakia huenda kwa mkulima hivyo, bei ya mwisho hupatikana baada ya mauzo ndipo tunaweza kutofautiana kutegemea ubora wa kahawa na soko ilikouzwa”alisema Mwangulumbi

Alisema kuwa kanda ya Mbinga imejenga ofisi yake hivyo imeondokana na gharama za kupanga kwani ukumbi wa ofisi hutoa huduma kwa wadau wengine kufanyia vikao vyao bila bughudha ni moja ya mafanikio ya miaka 10 ya Kilicafe

Alieleza zaidi mafanikio mengine ni vikundi vingi vya wanachama vimeweza kujenga ofisi zao, kununua mitambo, kujenga visima vya kuoshea kahawa, kujenga meza za kuanikia kahawa, kujenga maghala madogo ya kuhifadhia kahawa ambapo chama kimefanikiwa kujenga ghala la kuhifadhia kahawa katika mji wa Makambako na kupunguza gharama ya uhifadhi wa kahawa kwenye maghala mengine ambapo kwa mujibu wa taratibu za bodi ya kahawa ya Mbinga huuzwa kutokea Makambako.


“Kanda ya Mbinga imeendeleza mfuko wa Pembejeo wa kanda ambao pamoja na mfuko wa akiba wa chama, tumeweza kuwakopesha wakulima mbolea na madawa kila mwaka kiasi cha mifuko ya mbolea zaidi ya 6,000 mbalimbali na kulipa kodi na michango ya wilaya kwani imeweza kulipa kodi ya wilaya zaidi ya milioni 182 na mchango wa vidung’ata sh 19 milioni kama ilivyoamriwa na wilaya ili kupambana na janga la ugonjwa wa vidung’ata unaoteketeza kahawa”alisema Mwangulumbi

Alisema kuwa chama kiliasisi mpango wa umeme jua ili kuwanufaisha wakulima wa vijijini kupata nishati hivyo tumeweza kusimika paneli za umemejua 21 na paneli 103 zitasimikwa Juni 2011 ambapo paneli hizi ni za bei nafuu na kwa mkopo kwa wakulima kwa muda wa miaka mitatu.

Alifafanua kuwa mafanikio mengine ni viongozi na wakulima wa vikundi vichache wamepewa mafunzo ya matumizi ya kompyuta ambazo zinatumika kutunza kumbukumbu za mkulima na kutoa stakabadhi hapo hapo kwa kila mkulima atakayeuza kahawa kwenye vikundi hivyo ambapo vikundi hivyo ni vya Mahenge, Ilela na Kihuka ambazo zitaunganishwa na mtandao wa Mkurugenzi Mtendaji wa chama.

Alisema kuwa ushirikiano kwa wakulima ni kitu muhimu sana hivyo wakulima wa kanda ya Mbinga wameanza kujenga urafiki na wakulima wa ushirika wa wakulima wa kahawa Mzuzu nchini Malawi ambao waliitembelea kanda kubadilishana ujuzi na uzoefu katika kahawa ili kumkomboa mkulima pia kitendo cha Serikali kutambua Kilicafe kuwa ni umoja wa wakulima wenye malengo thabiti ya kuimarisha ushirika kwa uwazi na ukweli ni mafanikio mengine

Mwangulumbi akizungumzia changamoto zinazoukabili umoja huo alisema kuwa ni pamoja na  uwezeshaji katika uwekezaji wa wakulima wadogo kwani ununuzi na usimikaji wa mitambo ni wa gharama kubwa ambapo hali hiyo imefanya vikundi kadhaa kushindwa kununua mitambo haraka kwani mahitaji ya mitambo ni makubwa na yanaongezeka kila mwaka ambapo tulianza na mitambo 4 mpaka msimu huu tuna mitambo 77 hivyo vikundi vipya  43 bado havina mitambo ya kisasa kwani hutumia mitambo midogo ya zamani hata vikundi vyenye mitambo,ujenzi wa miundombinu kama maji, matenki na meza za kuanikia kahawa hutugharimu sana na kwamba ombi letu kwa Serikali vikundi vikiomba visikilizwe na kusaidiwa maombi yao yakiwasilisha kwenye mfuko wa DADPS.

Alisema pia changamoto nyingine ni kuwa ushuru wa Halmashauri licha ya kuwa ni wajibu wetu kuchangia maendeleo lakini wakulima wanaomba angalau kiasi kipunguzwe kiwe asilimia 3 ya bei ya kuuza kahawa na kwamba Serikali iliamua kuwasaidia wakulima kwa kutoa ruzuku kwenye pembejeo bado wakulima wa kahawa hawajanufaika na pembejeo hizo, hivyo tunaomba sera ya pembejeo irekebishwe ili zao la kahawa ambalo ni kinywaji kizuri kwa biashara na chakula lipate kuimarika zaidi.

Baadhi ya wakulima wa zao hilo ambao ni wanachama wa Kilicafe wakizungumza kwenye mkutano huo waliipongeza Serikali ya wilaya ya Mbinga kwa kuamua kusikiliza kilio cha wakulima wa zao hilo kwa kuamua kutoa sehemu ya ushuru wa kahawa kwa ajili ya kununulia miche ya kahawa ambayo mkulima wa zao hilo wilayani humo amekuwa akipewa bure

Menas Msuha mkulima wa kijiji cha Marindindo alisema kuwa kutokana na serikali kutoa miche ya kahawa bure kumemfanya aweze kuzalisha kahawa kwa wingi na kwamba kwa sasa ameshachimba mashimo mengi akisubiri kupanda kahawa nyingine

Naye Edwin Mpolola mkulima wa zao hilo katika kijiji cha Ngima alieleza kuwa Kilicafe imeweza kumsaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha yake pamoja na familia kwani hivi karibuni imeweza kumpatia umeme wa jua(Solar Power)ambao umeweza kumsaidi kupunguza gharama za kununua mafuta ya taa ambayo kwa sasa hivi lita moja imekuwa ikiuzwa kwa bei kubwa wilayani Mbinga na kwamba anaweza akapata taarifa mbalimbali kupitia luninga ambayo amefunga nyumbani kwake tofauti na kipindi cha nyuma

Mwandishi wa makala
Anapatikana kwa 0755335051
Baruapepe;stephano12mango@yahoo.com




SERIKALI YATAKIWA KUSHIRIKIANA NA ASASI ZA KIRAIA NCHINI