About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Friday, May 24, 2013

ASKOFU MTEGA ASANTE NA KWAHERI JIMBO KUU LA SONGEA




Mhashamu Askufu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea Dkt Norbert Wendelin Mtega akizungumza na Wanahabari mara baada ya KUJIUDHURU


Na, Stephano Mango, Songea

JUMATANO Mei 15, mwaka 2013 ni siku ya historia kubwa na  ilioyo dhahiri kwa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Songea na kwa Waamini wote wa Yesu Kristo na wote wenye mapenzi mema



Ni siku pekee ambayo haikutarajiwa na Wateule, Watakatifu na Wanakanisa pale Mhashamu Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea Dkt Norbert Wendelin Mtega alipoamua kuwatangazia Taifa la Mungu kustaafu ( Kujiudhuru) nafasi yake hiyo



Aliamua kuwatangazia uamuzi wake huo Viongozi mbalimbali wa Kanisa Majira ya saa saba Mchana Hanga Monasteri iliyopo Wilaya ya Namtumbo Mkoa wa Ruvuma nje kidogo ya Wilaya ya Songea, siku ya Jumatano Mei 15, 2013



“…kwa kuzingatia hali yangu ya afya , kwa kuzingatia jinsi nilivyoonja utendaji wangu unavyoonyesha dalili za kuchoka na  pengine kuzorota nikiwa katika mwaka wangu wa 28 wa Uaskofu kwa hiari yangu kabisa niliamua kumuandikia barua Baba Mtakatifu ili aniruhusu kustaafu kabla ya kufikia umri wa sheria na kanuni za kustaafu rasmi” alisema Mtega



Alisema kuwa nafurahi kwa kuwa Baba Mtakatifu leo amenijibu na kunikubalia ombi langu na dakika hii mbele yenu natua jukumu lote la Uongozi juu ya Jimbo Kuu la Songea



Kwa hiari yangu na kwa kuashiriwa na hali ya afya yangu na jinsi kazi inavyonielemea kupita uwezo wangu wa awali, nafanya hivyo kwa ajili ya ustawi wa Taifa la Mungu, na hasa Kanisa lililoko Songea kwa hiyo mimi staki niwe kikwazo na hoja ya Jimbo kuzorota katika siku za mbele



Alisema kuwa kuanzia sasa Msimamizi wa kitume wa Jimbo kuu la Songea katika kipindi ambacho ambaye ameteuliwa na Baba Mtakatifu ni Mhashamu Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa



Ni msimamizi kwa kuwa ataliongoza Jimbo kuu la Songea katika kipindi ambacho Baba Mtakatifu anapitia mchakato wake wa kumteua na kumtuma rasmi Askofu Mkuu mwingine wa Songea



Hakuna shaka kuwa yeye ni msimamizi kwa kuwa yeye anaendelea kuwa Askofu halali kabisa na mwenye mamlaka kamili bado juu ya Jimbo la Iringa, hivyo yeye ni wa kitume kwa sababu ameteuliwa na Baba Mtakatifu.



“Kwa hiyo tangu sasa mamlaka yote ya Uongozi wa , Usimamizi na maamuzi ninajivua kikamilifu kabisa naye Askofu Taricisius Ngalalekumtwa na achukue sasa nafasi yake kikamilifu kabisa” Alisema Dkt Mtega



Alisema kuwa kuanzia sasa saa saba mchana ya mei 15, mwaka 2013 nikiwa mbele yenu kwa moyo wa dhati kabisa na kwa upendo mkubwa kuwashukuru ninyi nyote wakiwemo Mapadre na Watawa na kwa kupitia kwenu nawaaga wale wote mnaowaongoza, waamini na wafadhiri na marafiki wote wa Jimbo kuu la Songea



Mhashamu Askofu Mkuu Dkt Norbert Wendel Mtega ni Askofu wa pili wa Jimbo Kuu la Songea ambaye alishika nafasi hiyo baada ya Askofu Mkuu Hayati Yakob Yafunani Komba



Dkt Mtega kiasili alizaliwa tarehe 17 Agosti 1945 katika Kijiji cha Kinyika, Parokia ya Lupanga , Wilaya ya Ludewa, Jimbo la Njombe, ambapo Jina la Baba yake ni Wendelin Mbwatilo Paulo Mtega



Jina la Mama yake ni Martha Msafiri Petro Mtweve na katika familia yao walizaliwa watoto kumi wakiwemo wavulana sita na wasichana wanne ambapo wavulana wawili walikufa, mmoja ni kaka yake na mmoja ni mdogo wake.



Askofu Mtega aliwapa jina moja Marehemu hao ambalo lilifahamika kwa Boniventura sababu ambazo yeye alizipenda, Yeye alikuwa ni mtoto wa nne katika familia yake hiyo yenye watoto kumi waliozaliwa pamoja naye, na yeye ni wanne katika nane walio hai.



Alibatizwa tarehe 9 Septemba 1945 na Padre Leonhard Wuesst OSB Mmisionari Mbenedikitine Mswisi, ambapo Septemba 10, mwaka 1955 akiwa darasa la Tatu, aliungama kwa mara ya kwanza na kupokea Komunyio ya Kwanza katika Kigango cha Lupanga akiwa na umri wa miaka kumi.



Tarehe 2 Octoba 1956 akiwa darasa la nne alipata Sakramenti ya Kipaimara ( LC 3034) Parokiani Madunda kwa Askofu Eberhard Spiess OSB.



Alisoma Darasa la kwanza hadi la nne katika Shule ya Msingi ya Lupanga Wilayani Ludewa tangu Mwaka 1953 hadi 1957 na kwa kuwa Shule haikuwa mbali sana na nyumbani kwake, alikuwa ni mwanafunzi wa kutwa.



Jumamosi na Jumapili alikuwa anashinda nyumbani na kuchunga mbuzi na ng’ombe za Baba yake , kazi ambayo alikuwa anaipenda sana, hata hivyo mwaka 1956 alishinda mtihani wake wa darasa la nne ingawa alilalia darasa hilo.



Elimu ya Sekondari alisoma katika Seminari ya Kigonsera na baadaye Seminari ya Likonde mwaka 1962 , ambapo alimaliza kidato cha nne Novemba, mwaka 1964 na kuchaguliwa kwenda kidato cha tano Sekondari ya Serikali ya Tosamaganga Mkoani Iringa na kumaliza kidato cha sita mwaka 1967.



Mwishoni mwa mwaka 1967 alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa katika Kambi la Kitai Wilayani Mbinga na baadae Kambi ya Mafinga na kupata namba ya kijeshi A0468 ambapo alifuzu mafunzo na kutunukiwa cheti kinachotambulika kwa Best Trainee katika Kombania yake D.



Julai 1968 alijiunga na Seminari Kuu ya Peramiho kwa ajili ya Mafunzo ya  Falsafa kwa miaka miwili ambapo alimaliza Novemba mwaka 1969 na Januari 1970 hadi Novemba 1973 aliendelea na masomo ya Teolojia hapo Seminari Kuu ya Peramiho



Alijipatia Stahashahada ( Diploma) ya Teolojia kutoka Chuo Kikuu cha Makerere- Uganda na mara baada ya kutoka huko alipata madaraja mbalimbali katika Kanisa kama vile kuwa Mkleri mwaka 1970 katika Parokia ya Madunda , ambapo mwaka aliingizwa katika huduma ya Ungojezi Mlango na Uzinguaji na baadaye Ushemasi mdogo



Mwaka 1973 alipewa Daraja la Ushemasi Seminari ya Peramiho na Novemba 1973 alipewa Daraja Takatifu la Upadre Parokiani Lupanga ambapo madaraja yote mawili alipewa na aliyekuwa Askofu wa Jimbo la Njombe Raymond Mwanyika



Novemba 1973 alitolea misa Takatifu ya kwanza katika Parokia ya Lupanga, na kwamba kazi yake ya Uchungaji mara baada ya Upadrisho wake alitumwa Uaskofuni Njombe kuwa Mkurugenzi wa Caritas, Mkurugenzi wa Miito, Mwalimu wa Dini katika shule ya Sekondari ya Njombe, Mlezi wa YCS Jimbo na Paroko Msaidizi wa Pili wa Njombe



Septemba 1976 alijiunga na Chuo cha Kipapa Jijini Roma (Pontificia Universita Urbaniana), Septemba 9 mwaka huo alianza kozi ya lugha ya Kiitaliano ambapo Octoba 10, 1976 masomo ya Chuo Kikuu yalianza nay eye alichukua masomo ya Falsafa



Mwaka 1978 alijipatia Shahada ya kwanza nay a pili ya masomo ya Falsafa na kupewa Magna Cum na Januari 1981 alihitimu Shahada ya Tatu na kupewa Summa Cum Laude, baada ya kurejea Tanzania alifundisha Seminari Kuu ya Peramiho akifundisha masomo ya Falsafa , Historian a Kilatini



Novemba 28, 1985 aliteuliwa kuwa Askofu wa Tatu Jimbo la Iringa na kupewa daraja hilo la Uaskofu Januari 6, 1986 mjini Roma na Baba Mtakatifu John Paulo II, ambapo Julai 6, 1992 aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea kuchukua nafasi ya Hayati Askofu Mkuu Yakobo Yafunani Komba



Tarehe 20 Septemba 1992 alisimikwa kuwa Askofu Mkuu wa Pili wa Jimbo Kuu la Songea ambapo 2013 anatimiza miaka 27 ya Uaskofu na miaka 21 ya Uaskofu Mkuu na 40 ya Upadre na 68 ya umri



Mei 19, 2013 amewaaga rasmi Waamini katika Kanisa Kuu la Kiaskofu Songea na kuongoza misa maalumu akiwa Askofu Mkuu Mstaafu na kuwataka waumini wamuombee kwani Mei 31, 2013 anaenda nje ya nchi kwa matibabu



“ Mwenyezi Mungu awabariki sana, na awaneemeshe, Niombeeni kama vile nami nitakavyokuwa nawaombeeni, Amina” Alimalizia kwa kusema Askofu Mtega



Ni dhahiri kuwa Mhashamu Askofu Mtega amejiudhuru nafasi yake hiyo kubwa ndani ya kanisa na kusababisha sintofahamu miongoni mwa Taifa la Mungu, kila mmoja katika fikra zake anawaza kilichosababisha ang’atuke



Safari yake ya kiuchungaji ni ndefu inatupasa tuielewe na kuitathimini kwa dhati ili tuweze kuliimarisha Taifa la Mungu kwani sote tu mashahidi wa safari yake hiyo kwa ubora na udhaifu wake katika misingi ya Imani, Upendo, Amani na Mshikamano miongoni mwa jamii ya Kanisa, yatosha kusema Askofu Mtega asante na kwaheri Jimbo kuu la Songea

MWISHO

                         Mwandishi wa Makala

                         Anapatikana 0715-335051

                          www.stephanomango.blogspot.com