About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Tuesday, July 26, 2011

Gari ya kubebea wagonjwa katika kituo cha afya cha Lituhi likiwa limeegeshwa katika kituo hicho baada ya kuharibika zaidi ya miezi ya miezi saba bila kufanyiwa matengenezo hali inayoendelea kuleta adha kubwa kwa wagonjwa na hasa akina mama wajawazito




WAJAWAZITO WALIA NA UMBALI MREFU KWENDA VITUO VYA AFYA
Na Stephano Mango,Songea
WANAWAKE wajawazito wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wanakabiliwa na umbali mrefu kutoka katika maeneo wanayoishi kwenda katika Vituo vya Afya Mbambabay,Liparamba na Lituhi kwa ajili ya kupata huduma za afya kabla na baada ya kujifungua

Uchunguzi uliofanya na gazeti hili kutoka katika vijiji vya
Chimate,Mtupale,Chinula,Ndengele na N’gombo umebaini kuwa akina mama wengi wajawazito wamekuwa wakikumbana na kero kubwa ya usafiri wa kutoka kwenye vijiji wanavyoishi hadi kwenye vituo vya afya kufuata huduma za kliniki ya mama na mtoto

Imebainika kuwa akina mama hao wajawazito wamekuwa wakichelewa kufika katika vituo vya afya na wakati mwingine kukosa kabisa huduma muhimu ya afya ya mama na mtoto kutokana na adha kubwa ya usafiri jambo linalopelekea kudhoofika kwa afya zao kabla na baada ya kujifungua

Baadhi ya wakina mama wajawazito kutoka katika Vijiji vya Mtupale,Mtipwili,Chiulu,Kwambe,Mbaha na Kingirikiti wakizungumza na gazeti hili walisema kuwa kutokana na umbali mrefu uliopo toka wanakoishi hadi kwenye vituo vya afya wamekuwa wakishindwa kuhudhulia kliniki kabla na baada ya kujifungua kwani wakina mama hao wamekuwa wakilazimika kujifungulia majumbani kwa sababu ya kukoasa nauli na wakati mwingine usafiri wa kuwafikisha katika vituo hivyo

Walisema kuwa hali hiyo licha ya kuwa ni hatari kwa afya zao lakini wamekuwa wakilazimika kufanya hivyo kutokana na mazingira magumu waliyonayo katika maeneo wanayoishi na kwamba Zahanati nyingi zilizopo kwenye maeneo jilani wanayoishi zimekuwa zikikosa dawa,wataalamu pamoja na vifaa tiba

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa Wilaya mpya ya Nyasa ina vituo vya Afya Vitatu ambavyo ni Lituhi kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga,Liparamba na Mbambabay pamoja na Hospitali Liuli ambayo inamilikiwa na kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma pamoja na Zahanati nyingi ambazo huduma yake ni duni

Imebainika kuwa wakina mama wajawazito kutoka kijiji cha Mango hadi kituo cha afya cha Mbambabay wamekuwa wakitembea kwa miguu umbali wa kilometa 43 na wakati mwingine wamekuwa wakitumia usafiri wa Yeboyebo(pikipiki) kwa nauli ya shilingi elfu 9,500 ambako kwa gari ni shilingi elfu 3000

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Chiwanda Oldo Mwisho aliliambia gazeti hili kuwa kufuatia adha wanazopata wakina mama wajawazito alisema kuwa sera ya afya ya Serikali imetamka wazi kuwa kila kata ni lazima kijengwe kituo cha afya ili kukabiliana na adha hizo na kila kijiji iwepo Zahanati

Mwisho alisema kuwa kutokana na hali wananchi wamekuwa wakihimizwa ujenzi wa vituo vya afya kwenye kata zao ambapo changamoto kubwa inayoikabili Serikali ni ubovu wa miundombinu, upungufu wa wataalamu wa afya,dawa na vifaa tiba

Akizungumza na gazeti hili Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi Kapteini John Komba alisema kuwa Wilaya ya Mbinga ina eneo kubwa la kiutawala hivyo ilikuwa imezidiwa uwezo wake wa kutoa huduma kwa jamii kwani ilikuwa ina hudumia wakazi wa majimbo mawili ya uchaguzi la Mbinga Magharibi na Mbinga Mashariki
Komba alisema kuwa Serikali kuu kwa kutambua ukubwa wa eneo hilo imeamua kuyagawa majimbo hayo katika Wilaya na kupata Wilaya ya Mbinga na Wilaya mpya ya Nyasa ambayo inaanza rasmi katika kipindi hiki cha bajeti ya mwaka wa 2011/2012 hivyo mara itakapoanza itapunguza adha hizo za wajawazito kwa kiasi kikubwa
MWISHO







Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Mbambabay kilichopo Wilayani Nyasa,Dkt Wenceraus Soky akimuonyesha Mwandishi wa Makala haya orodha ya dawa walizoletewa februari 26,2011 katika kituo chake na Bohari ya madawa nchini(MSD) ambapo madwa muhimu na vifaa tiba kwa ajili ya akinamama wajawazito vilikuwa ni vichache sana






LUGHA CHAFU,UKOSEFU WA DAWA NI TATIZO KWA WAJAWAZITO NYASA
Na Stephano Mango,Nyasa
SEKTA ya afya ni moja ya eneo nyeti katika maisha ya mwanadamu yoyote yule duniani lakini imekuwa ikilalamikiwa kwa kiasi kikubwa na wadau wa sekta hiyo kutokana na huduma mbovu na zenye kejeli kwa akina mama wajawazito

Uchunguzi uliofanywa na waandishi wa habari kwa ufadhiri wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP)hivi karibuni kwenye Zahanati na vituo vya afya vilivyopo mwambao mwa Ziwa Nyasa umebaini kuwa akina mama hao wamekuwa wakipewa lugha chafu na zilizojaa kejeli pindi wanapofika katika Zahanati na vituo vya afya kabla na baada ya kujifungua

Imebainika kuwa watumishi katika sekta ya afya katika kituo cha afya cha Mbambabay wamekuwa wakiwatolea lugha zilizokosa staha akina mama wajawazito kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuchelewa kufika kuanza kliniki na nyinginezo

Kutokana na hali hiyo imebainika kuwa akina mama wengi wajawazito wamekuwa wakishindwa kuendelea kuhudhulia kliniki kwa kuhofia lugha chafu zinazotolewa na wahudumu wa sekta ya afya na badala yake wamekuwa wakijifungua kwa wakunga wajadi

Wakizungumza kwa uchungu na hofu ya kukutwa na wahudumu wa afya katika kituo hicho baadhi ya akina mama wajawazito walisema kuwa wanapofika katika kituo cha afya wanakaa muda mrefu bila kusikilizwa na kupatiwa huduma ya afya

Annet Koleka mkazi wa Ndengere akizungumza na gazeti hili alisema kuwa licha ya kuwahi katika kituo cha afya kwa ajili ya kupatiwa matibabu wamekuwa wakikaa kati ya masaa manne hadi saba wakisubiri kupata huduma hiyo

Koleka alisema kuwa wahudumu wa afya katika kituo hicho wamekuwa wakiwadharau sana kwani muda mrefu wamekuwa wakipanga foleni kwa ajili ya kupata huduma na wakati mwingine wanaambiwa kuwa idadi yao inapaswa iongezeke ndipo waweze kutoa huduma kwa madai kuwa hawawezi kuwahudumia watu wachache jambo ambalo linawashangaza sana

Uchunguzi umebaini kuwa akina mama hao wamekuwa wakilipia huduma ya uzazi na mtoto bila mpangilio maalum wa bei kwani imekuwa ikipangwa kilanguzi na wahudumu wa afya na kwamba mara chache tena kwa kubahatisha wamekuwa wakipewa bure dawa za minyoo na wakati mwingine dawa za malaria

Alisema kuwa usafiri umekuwa ni wa tabu sana na kwamba wakati mwingine unapopatika kunakuwa siyo siku ya kliniki kwa wakazi wa eneo fulani na kuendelea kuwa na adha kubwa kwa akina mama hao kuwahi kliniki siku walizopangiwa

Imebainika kuwa kutoka na kero hizo akina mama hao wamekuwa wakilazimika kukodi pikipiki wakiwa wajawazito wawili wenye zamu moja ya kwenda kupima kliniki ili waweze kuhimili kuchangiana gharama za usafiri

Kutokana na adha mbalimbali wanazozipata akina mama hao wamesema kuwa ni vema wakaendelea kujifungulia kwa wakunga wajadi ili kuweza kukwepa kero hizo ingawa wanakili wazi kuwa kujifungulia kwa wakunga hao kunaweza kuhatarisha afya zao

Aidha uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini wazi kuwa wanaume wengi wilayani humo wamekuwa wakiwaacha wake zao ambao wajawazito wakitembea umbali mrefu kwenda kufuata huduma za afya pekee yao bila kuwasindikiza hali ambayo ina hatarisha afya ya mama mjamzito na mtoto aliyetumboni

Agnes Katuli mkazi wa Ngingama alisema kuwa katika kituo cha afya cha Lituhi wanakutana na changamoto ya kufuatana na wenza wao kwenda kliniki ili kupata elimu stahiki ya afya ya uzazi kwani wenza wao wamekuwa wakikaidi wito wa wahudumu wa afya wanapo takiwa kufika katika vituo vy afya

Imebainika kuwa wanaume wengi wa maeneo hayo wameshindwa kushirikiana na wenza wao ili kuhakikisha mama anakuwa na afya njema wakati wa ujauzito wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua ili kuweza kukomesha vifo vinavyotokana na uzazi

Wakizungumza na Gazeti hili katika Kituo cha Afya cha Lituhi akina mama wajawazito waliofika kituoni hapo kuhudhuria kliniki walisema kuwa wamekuwa wakitembea umbali mrefu pekee yao bila kuwa na wenza wao hadi kwenye kituo hicho cha afya

Veronika Rohomoja aliliambia gazeti hili kuwa amekuwa akitembea kwa miguu polini zaidi ya kilometa 5 kutoka katika kata ya Ngingama hadi kituoni hapo na kwamba anapokuwa amechoka hupumzika chini ya mti na kisha kuendelea na safari yake

“Hii ni mimba ya uzao wa tatu na inamiezi 8 nimekuwa nikija kituo cha afya pekee yangu ambapo mwenza wangu anakuwa kwenye shughuli za uzalishaji mali na kwamba tumezoea kutembea polini pekee yetu bila kuwa na msaada wa mtu yoyote na wakati mwingine tunakuwa akina mama wajawazito wawili kutoka kwenye eneo moja”alisema Rohomoja

Uchunguzi huo umebaini kuwa wanaume wengi wamekosa elimu ya afya ya uzazi na mtoto na kwamba wamekuwa hawatambui kuwa wao ndio wadau muhimu katika kuhakikisha mama mjamzito anakuwa na afya njema muda wote wakati wa ujauzito,kujifungua na baada ya kujifungua

Akizungumza na gazeti hili Emilia Chawala (38) mkazi wa kijiji cha Mango ambaye anaujauzito wa miezi saba ikiwa ni mzao wake wa nne alisema kuwa wamekuwa wakikutana na changamoto ya dawa na vifaa tiba mara wanapofika katika zahanati na vituo vya afya

Chawala alisema wana kutana na changamoto ya vifaa hivyo ambavyo ni muhimu kwa ajili ya huduma ya kliniki hali ambayo inawalazimu kwenda kununua kwenye maduka ya dawa muhimu kwa bei kubwa

Akizungumza na gazeti hili Daktari Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Lituhi Dkt Martin Ndunguru alisema kuwa wanaume wamekuwa mara nyingi hawataki kuwasindikiza wenza wao kliniki ili waweze kujua matatizo wanayowakabili mama na mtoto kutoka na mazingira magumu ya maisha,mfumo dume na mila na tamaduni za eneo hilo

Ndunguru alisema kuwa licha ya wanaume kuwa na shughuli nyingi za kutafuta ridhiki,wamekuwa wakiendelea kuwaelimisha akina mama mbinu za kuwavuta wenza wao ili waje kupata elimu muhimu ya huduma ya afya ya uzazi na mtoto ili kuweza kunusuru vifo vitokanavyo na masuala ya uzazi

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Mbambabay Dkt Wenselausy Soky alisema kuwa kituo chake kinahudumia watu wengi kuliko uwezo wake hali inayopelekea wengine kukosa dawa muhimu kwa ajili ya maradhi yao

Dkt Soky alisema kuwa kituo hicho kinahudumia wagonjwa kutoka katika maeneo mengi na wale ambao wamepewa rufaa kutoka katika Zahanati 11 za Mwambao mwa ziwa Nyasa na kwamba wajawazito wamekuwa wakinunua dawa na vifaa tiba katika maduka ya dawa baridi na sio kuwa wahudumu wa afya ndio wamekuwa wakiwauzia akina mama hao kwa bei kubwa

Alisema kuwa wahudumu wa afya katika kituo hicho wanakutana na hangamoto nyingi kutoka kwa wagonjwa ikiwemo ya familia nyingi kuchelewa kutoa maamuzi ya kutafuta huduma kwenye kituo cha afya kutoka na uelewa mdogo wa kufahamu dalili za hatari kwa mama mjamzito

Alieleza kuwa akina mama hao mara wanapofika kuanza kliniki wamekuwa wakiambiwa waje na waume zao ili waweze kupata vipimo vya maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupatiwa elimu ya afya ya uzazi na mtoto hali inayosababisha kutokuelewana na kuhisi kuwa wametukanwa kwa sababu za tamaduni na mila zao

Alileza zaidi kuwa mara nyingi kituo chake kimekuwa kikikosa dawa muhimu na vifaa tiba kwa ajili ya dharura kwa mama mjamzito kwani huduma za msingi kama vile drip,dawa kwa ajili ya kukabiliana na uambukizi,kifafa cha mimba,kumsafisha mama ambaye mimba yake imetoka,kutoa dawa ya kuzuia damu kuendelea kutoka,kufanya vacuum imekuwa duni kutokana na ukosefu wa vifaa tiba na dawa muhimu kwa ajili ya huduma hizo

Mwandishi wa Makala haya
Anapatika kwa 0755-335051
Baruapepe;stephano12mango@yahoo.com
MWISHO

Thursday, July 21, 2011

Akina mama wajawazito wakiwa wanaendelea kusubiri huduma ya kliniki katika kituo cha afya cha Mbambabay ambapo wamekuwa wakitumia zaidi ya saa 7 kusubiri huduma za afya






UTASHI WA KISIASA UNAHITAJIKA KUBORESHA AFYA YA UZAZI  NYASA
Na Stephano Mango,Nyasa

SEKTA ya afya katika nchi yoyote duniani ina umuhimu mkubwa sana katika kuleta ustawi wa jamii na kwamba ili jamii iweze kujitegemea kielimu,kisiasa,kiuchumi ni lazima iwe na afya bora itakayowezesha nchi kupiga hatua kusudiwa

Kwa kutambua hilo hivi karibuni nilikuwa katika ziara kwenye wilaya mpya ya Nyasa Mkoani Ruvuma katika shughuli za kiuandishi kufuatilia hali ya huduma ya afya ya uzazi kwa wakazi wa wilaya hiyo iliyopo mwambao mwa Ziwa Nyasa

Nilibahatika kufika huko kwa ufadhiri wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)na kuweza kufanikiwa kutembelea kata sita za Lituhi,Mbaha,Kihagara,Mbambabay,Chiwanda na Kilosa katika wilaya hiyo

Katika shughuli zangu za uandishi nilibaini mambo kadhaa yanayowakumba akina mama wajawazito kabla na baada ya kujifungua wakati wa kwenda katika vituo vya afya na Zahanati kupata huduma ya afya ya uzazi na mtoto

Miongoni mwa mambo hayo ni umbali mrefu kutoka kwenye makazi hadi kufika katika vituo vya afya ili kuweza kupata huduma ya kliniki kwani akina mama wengi wajawazito wamekuwa wakitembea umbali mrefu pekee yao bila hata kusindikizwa na wenza wao

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kutoka katika vijiji vya
Chimate,Mtupale,Chinula,Ndengele na N’gombo umebaini kuwa akina mama wengi wajawazito wamekuwa wakikumbana na kero kubwa ya usafiri wa kutoka kwenye vijiji wanavyoishi hadi kwenye vituo vya afya kufuata huduma za kliniki ya mama na mtoto

Imebainika kuwa akina mama hao wajawazito wamekuwa wakichelewa kufika katika vituo vya afya na wakati mwingine kukosa kabisa huduma muhimu ya afya ya mama na mtoto kutokana na adha kubwa ya usafiri jambo linalopelekea kudhoofika kwa afya zao kabla na baada ya kujifungua

Baadhi yao kutoka katika Vijiji vya Mtupale,Mtipwili,Chiulu,Kwambe,Mbaha na Kingirikiti wakizungumza na gazeti hili walisema kuwa kutokana na umbali mrefu uliopo toka wanakoishi hadi kwenye vituo vya afya wamekuwa wakishindwa kuhudhulia kliniki kabla na baada ya kujifungua kwani wakina mama hao wamekuwa wakilazimika kujifungulia majumbani kwa sababu ya kukosa nauli na wakati mwingine usafiri wa kuwafikisha katika vituo hivyo

Walisema kuwa hali hiyo licha ya kuwa ni hatari kwa afya zao lakini wamekuwa wakilazimika kufanya hivyo kutokana na mazingira magumu waliyonayo katika maeneo wanayoishi na kwamba Zahanati nyingi zilizopo kwenye maeneo jilani wanayoishi zimekuwa zikikosa dawa,wataalamu pamoja na vifaa tiba

Uchunguzi huo umebaini kuwa Wilaya mpya ya Nyasa ina vituo vya Afya Vitatu ambavyo ni Lituhi kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga,Liparamba na Mbambabay pamoja na Hospitali ya Liuli ambayo inamilikiwa na kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma pamoja na Zahanati nyingi ambazo huduma yake ni duni

Imebainika kuwa wakina mama wajawazito kutoka kijiji cha Mango hadi kituo cha afya cha Mbambabay wamekuwa wakitembea kwa miguu umbali wa kilometa 43 na wakati mwingine wamekuwa wakitumia usafiri wa Yeboyebo(pikipiki) kwa nauli ya shilingi elfu 9,500 ambako kwa gari ni shilingi elfu 3000

Aidha imebainika kuwa gharama za matibabu ni kikwazo kwa akinamama hao kwani wamekuwa wakichangia huduma za kliniki na matibabu kati ya shilingi 2000 na shilingi 6000 kila wanapohitaji kupata huduma kinyume na sera ya taifa ya matibabu bure kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili katika kata ya Lundo akina mama hao walisema kuwa Serikali imekuwa ikisema akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano wanatakiwa kupata huduma ya afya bila kuchangia malipo lakini wao wamekuwa wakichangia fedha nyingi

Kutokana na kuchangia gharama hizo ambazo kwao zimekuwa kero kubwa wamekuwa wakilazimika kwenda kliniki wanapokaribia kujifungua tu ili kuweza kukwepa gharama zinazotozwa mara wanapofika katika Zahanati na vituo hivyo kutokana na ugumu wa maisha

Walisema kuwa katika kata hiyo kuna Zahanati ya Lundo ambayo mara nyingi imekuwa ikikosa dawa muhimu za wajawazito na wahudumu wake wamekuwa na lugha chafu kwa wagonjwa hali inayopelekea akina mama wengi kutohudhulia Kliniki kwa kuhofiwa kutukanwa na kupoteza muda wa kufanya kazi zao za kujitafutia ridhiki

Mary Haule mkazi wa kata hiyo ambaye anaujauzito wa miezi saba alisema kuwa kutokana na hali hiyo amekuwa akienda kupata matibabu katika Kituo cha Afya cha Mbambabay kwa kuhofia usalama wake wakati wa kujifungua

Haule alisema kuwa wajawazito wengi wamekuwa wakinyanyaswa sana pindi wanapofika katika Zahanati kwa ajili ya kupata huduma za matibabu jambo ambalo linaonyesha uzalilishaji wa hali ya juu kwa wanawake

Uchunguzi uliofanya na Gazeti hili umebaini kuwa Zahanati nyingi za Mwambao mwa Ziwa Nyasa zimekuwa zikikosa dawa muhimu kwa ajili ya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kutokana na mgawanyo usio wa uwiano unaotolewa na Bohari ya Madawa Nchini(MSD)

Aidha kutokana na ukosefu huo wa dawa uchunguzi umebaini kuwa wahudumu wa Zahanati hizo wamekuwa wakiwauzia dawa na vifaa tiba wajawazito kwa bei kubwa hali inayopelekea unyanyasaji mkubwa kwa akina mama hao ambao wanatoka umbali mrefu kwa ajili ya kupata matibabu stahiki

Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya wajawazito 3 katika Kituo cha Afya cha Mbambabay wakitokea Kata ya Tumbi umbali wa kilometa 43 ambapo wamekuwa wakitembea kwa miguu na wakati mwingine kwa pikipiki kwa kutozwa nauli kubwa kwenda kuhudhulia Kliniki

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Chiwanda Oldo Mwisho aliliambia gazeti hili kuwa kufuatia adha wanazopata wakina mama wajawazito alisema kuwa Halmashauri yake inazitambua adha hizo na kwamba sera ya afya ya Serikali imetamka wazi kuwa kila kata ni lazima ijenge kituo cha afya ili kukabiliana na adha hizo na kila kijiji ijenge Zahanati

Mwisho alisema kuwa kutokana na hali wananchi wamekuwa wakihimizwa ujenzi wa vituo vya afya kwenye kata zao ambapo changamoto kubwa inayoikabili Serikali ni ubovu wa miundombinu, upungufu wa wataalamu wa afya,dawa na vifaa tiba

Akizungumza na gazeti hili Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi Kapteini John Komba alisema kuwa Wilaya ya Mbinga ina eneo kubwa la kiutawala hivyo ilikuwa imezidiwa uwezo wake wa kutoa huduma kwa jamii kwani ilikuwa ina hudumia wakazi wa majimbo mawili ya uchaguzi la Mbinga Magharibi na Mbinga Mashariki

Komba alisema kuwa Serikali kuu kwa kutambua ukubwa wa eneo hilo imeamua kuyagawa majimbo hayo katika Wilaya na kupata Wilaya ya Mbinga na Wilaya mpya ya Nyasa ambayo inaanza rasmi katika kipindi hiki cha bajeti ya mwaka wa 2011/2012 hivyo mara itakapoanza itapunguza adha hizo za wajawazito kwa kiasi kikubwa

Alisema kuwa mara nyingi amekuwa akipigania ustawi wa afya za akina mama wajawazito anapopata wasaa wa kuchangia bungeni akiwa mwanasiasa aliyepewa dhamana na wananchi katika kushirikiana nao kujiletea maendeleo kusudiwa katika jimbo hilo

Mwandishi wa makala
Anapatikana kwa 0755-335051
Barua pepe;stephano12mango@yahoo.com





Wednesday, July 6, 2011

Mkuu wa kituo cha michezo kanda ya kusini Vicent Mbaya akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya maafisa mipango miji,wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa michezo nchini Juliana Yassoda,wa pili ni Afisa elimu Taaluma mkoa wa Ruvuma Frezier Zombe,wa kwanza kulia ni Afisa Michezo mkoa wa Ruvuma Hassan Katuli,wa pili ni mkufunzi wa michezo nchini Mohamed Madenge

MAAFISA MIPANGO MIJI NI NGUZO MUHIMU KWA MAENDELEO YA MICHEZO
Na Stephano Mango,Songea
SUALA la michezo lina mchango mkubwa sana katika maendeleo ya nchini yoyote ile duniani lakini sote ni mashahidi kuwa michezo mingi inayoshirikisha watu wengi haichezwi kwa ufanisi kutokana na kutokuwepo maeneo ya kutosha kwa ajili ya michezo hiyo

Maeneo mengi ambayo yalikuwa yametengwa kwa ajili ya michezo na burudani yamevamia na kupewa matumizi tofauti mbali na yale yaliyokusudiwa na hivyo kuwanyima wananchi fursa ya kucheza michezo

Viwanja vingi vilivyopo nchini vimekosa matunzo kutoka kwa mamlaka husika na wadau wa michezo nchini kwani miundombinu yake imekuwa chakavu na kusababisha viwanja hivyo kushindwa kukidhi haja ya matumizi yake

Ili michezo iweze kuendelea inahitaji kuwepo kwa viwanja kwani sheria namba moja ya kila michezo ni viwanja na vifaa vya kuchezea michezo kwa kutambua hilo juni 20 hadi 24,2011 Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo kupitia Kituo cha Michezo Kanda ya Kusini

Kiliandaa mafunzo ya ushiriki wa Maafisa Mipango Miji katika maendeleo ya michezo nchini ambapo wadau kutoka katika Halmashauri za Miji,Manispaa na Majiji kutoka katika mikoa ya Shinyanga,Mbeya,Iringa,Mwanza,Ruvuma,Rukwa,Morogoro walihudhuria mafunzo hayo

Akizungumza kwenye mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT) tawi la Ruvuma Mkuu wa Kituo cha Michezo Kanda ya Kusini Vicent Mbaya alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea wa kuthubutu Maafisa Mipango Miji juu ya kutenga,kujenga na kutunza viwanja ambavyo vinatengwa kwa matumizi ya michezo

Mbaya alisema kuwa pia mafunzo hayo yalilenga kuwaunganisha pamoja wataalamu wa Mipango Miji na wa michezo ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo ya historia ya michezo Duniani na Tanzania,namna ya kutoa ushauri wakati wa ujenzi wa viwanja vya michezo kwa maafisa Mipango Miji ,ustawishaji wa viwanja vya michezo

Alisema kuwa mada zingine ni Tasnia ya michezo(Sports Industry)Sera ya maendeleo ya michezo na utawala bora,Uongozi na utawala katika michezo,Viwanja vya michezo katika michezo,Upimaji wa viwanja vya michezo na Tathimini na majadiliano mbalimbali

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Michezo Nchini Juliana Yassoda akitoa salamu zake kwenye mafunzo hayo alisema kuwa  Serikali ya awamu ya tatu na nne zimelipa msukumo mkubwa suala la miundombinu ya michezo ili watanzania waweze kupata fursa ya kucheza michezo

Yassoda alisema pia waweze kuibua vipaji katika michezo ili kujenga afya zao,kupambana na umasikini,kuchelewesha uzee,kuongeza umri wa kuishi na hivyo kufanikisha dhana ya maisha bora kwa kila mtanzania kwani ushahidi katika hilo ni uamuzi wa Serikali kujenga uwanja wa kisasa mpya uliopo Dar es Salaam
                                                                                                                                                                                                              
Alisema kuwa katika kuleta maendeleo ya michezo nchini,Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 ibara ya 201 kipengele cha michezo,kipengele kidogo cha (g),(i) na(1)vinatutaka kuimarisha,kulinda na kutenga maeneo ya wazi kwa ajili ya maendeleo ya michezo

Alieleza kuwa washiriki wa mafunzo wanatakiwa kuisoma vizuri ilani hiyo,kuitafakari na kuifanyia utekelezaji ili michezo iweze kuendelea kwani sote tunajua ya kuwa michezo bila viwanja haiwezi kuchezeka kwa kuwa sheria namba moja ya kila michezo ni viwanja na vifaa vya kuchezea michezo

Akifungua mafunzo hayo Afisa Elimu Taaluma mkoa wa Ruvuma Frezier Zombe alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha washiriki ambao ni Maafisa mipango miji,Mameneja wa viwanja,Wizara ya Habari,Utamaduni na Michezo na Kituo cha Michezo Kanda ya Kusini kutambua changamoto mbalimbali katika kutenga,kujenga na kutunza viwanja vya michezo

Zombe aliwaasa washiriki kutambua wajibu wao katika kusimamia maendeleo ya michezo kulingana na utekelezaji wake na kazi za kila siku ndani ya mamlaka husika ikiwa ni pamoja na kutambua na kutafakari manufaa ya michezo katika nyanza mbalimbali kama vile kiuchumi,kijamii na kiafya

Alisema kuwa washiriki wanapaswa kutumia vema muda huo wa mafunzo kutambua mahitaji halisi ya ukubwa wa viwanja,eneo linalostahili kujengwa kiwanja na uelekeo wa uwanja

Akizitaja changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa mafunzo Afisa Michezo wa Mkoa wa Ruvuma Hassan Katuli alisema kuwa licha ya washiriki kujadili mada mbalimbali zilizopangwa zimejitokeza changamoto kadhaa

Katuli alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kutokuwepo kwa mawasiliano kati ya Wizara Mama ya Michezo na Halmashauri,kubadilika kwa matumizi kwa viwanja vya michezo kuwa matumizi mengine bila kufuata taratibu husika

Alisema kuwa halmashauri kuwa na uhaba wa fedha za kulipia fidia hususani viwanja vya michezo na maeneo ya wazi,mwamko finyu wa halmashauri pamoja na jamii juu ya umuhimu wa michezo katika kujenga na kukua kijamii

Alieleza kuwa changamoto nyingine ni uhaba wa wataalamu wa kusimamia michezo(maafisa michezo)kuanzia ngazi ya kata na halmashauri,jamii kuwa na mwamko mdogo juu ya tasnia ya michezo kutoka ngazi ya familia hadi Taifa

Alisema pia kukosekana kwa warsha mbalimbali za kujadili michezo katika ngazi mbalimbali za Serikali,idadi ndogo ya washiriki hasa (Maafisa mipango Miji) kutokana na waandaaji kushindwa kugharamia malazi,chakula na nauli kwa washiriki

Akitoa mapendekezo kwa Serikali kutokana na changamoto hizo kwa niaba ya washiriki wote wa mafunzo hayo Afisa Mipango Miji Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Wickriph Benda alisema kuwa wanasiasa waheshimu maoni na maamuzi ya wataalamu yanapotolewa kwa lengo la kukuza michezo nchini

Benda alisema kuwa kuwepo na mijadala,warsha mbalimbali kuanzia ngazi ya mtaa hadi Taifa juu ya umuhimu wa michezo,Serikali iajiri Maafisa michezo kuanzia ngazi ya kata,kuwepo kwa ushirikiano kati ya Wizara mama ya michezo,Tamisemi,Halmashauri na wadau mbalimbali wa michezo

Wizara mama ya michezo na halmashauri zitenge fedha kwa ajili ya kulipa fidia ya kutwaa ardhi ambayo itatumika kwa ajili ya viwanja,utaratibu wa kubadilisha matumizi ya ardhi ufuatwe kwa kufuata ushauri wa Maafisa mipango miji

Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana kwa 0755-335051
Baruapepe;stephano12mango@yahoo.com

Monday, July 4, 2011

UWAJIBIKAJI WA HALMASHAURI NI NGUZO MUHIMU KWA MAENDELEO NCHINI
Na Stephano Mango,Songea
HALMASHAURI ya Wilaya ya Songea ni moja kati ya Halmashauri tano za mkoa wa Ruvuma ambayo ilianzishwa julai 1,mwaka 2002 chini ya sheria namba 7 ya Serikali za mitaa ya mwaka 1982

Eneo la mamlaka ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea ni kilometa za mraba 16,727.143 ambapo inakadiliwa kuwa na jumla ya watu 188,368 ikiwa wanaume 96,465 na wanawake 91,903 ambao wanaishi katika Vijiji 63 vyenye kufanya kata 17 na Tarafa 3

Halmashauri hiyo ina Madiwani 23 kati ya hao 17 ni wa kuchaguliwa, 5 wawakilishi Viti Maalum na 1 kwa nafasi yake Mbunge na kwamba Halmashauri ina maeneo matatu ya mamalaka ambayo ni Serikali za Vijiji,Kamati ya Maendeleo ya Kata(WDC)  na Baraza la Madiwani ambalo ndilo mamlaka ya juu kabisa katika Halmashauri hiyo

Akizungumza na gazeti hili Ofisini kwake hivi karibuni  Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Anna Mbogo alisema kuwa Halmashauri ina jumla ya watumishi 1,673 kati ya watumishi 1,932 wanaotakiwa kuwepo kwani kwa sasa inaupungufu wa watumishi 257 wa fani mbalimbali

Mbogo alisema kuwa upungufu mkubwa upo katika sekta ya elimu ambayo inaupungufu wa wa Walimu 142 ikifuatiwa na sekta ya afya watumishi 61,utawala 28,maji 9,kilimo 8,ujenzi 6 na mifugo 5

Alisema kuwa katika suala la uchumi Halmashauri hiyo inategemea zaidi kilimo kwani wakazi wengi wa Halmashauri hiyo wanapata riziki zao kutokana na shughuli za kilimo na kwamba mapato ya Halmashauri kwa asilimia 90% hutoka kwenye sekta hiyo

Alifafanua kuwa Halmashauri imekuwa ikitekeleza shughuli zake kwa kuzingatia maelekezo na ahadi zilizomo katika Ilani ya uchaguzi ya chama tawala ambapo imegusa mambo mengi muhimu

Alisema kuwa pia wamekuwa wakitekeleza malengo ya Mpango wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini(MKUKUTA) ambayo ni Kukuza Uchumi,Kuimarisha huduma za Jamii,Uwajibikaji na Utawala bora,Kushirikisha jamii katika hatua zote za kuboresha hali zao za maisha kwa kuinua mapato yao,ya Halmashauri na Taifa kiujumla

Alieleza kuwa asilimia 90% ya ardhi katika Halmashauri hiyo inafaa kwa kilimo ambapo mazao ya chakula yamekuwa yakistawi vizuri kama vile mahindi,maharage,mpunga,viazi vitamu na mihogo na kwa mazao ya biashara yanayolimwa na kustawi vizuri ni kama vile tumbaku,korosho,kahawa,karanga,ufuta na nazi

Alisema kuwa kilimo cha umwagiliaji kwa zao la mpunga kinaendelea kupewa kipaumbele hasa baada ya zao la tumbaku kuwa na utata katika soko ambapo upanuzi,uboreshaji na uendelezaji wa shughuli za kilimo ndio njia inayoweza kukuza uchumi na kuondoa umasikini katika Halmashauri yetu

Alikiielezea sekta ya mifugo alisema kuwa Halmashauri ina jumla ya ng’ombe 33,123,mbuzi 57,089,nguruwe 27,159,sungura 496,bata 8,618,mbwa 5918,paka 294,punda 326 na kuku 225,908 kati ya hao kuku wa kienyeji ni 217,609 na wakisasa ni 8,299 ambapo jitihada zinaendelea kuongeza mifugo na mazao yake

‘Tuna majosho 18,yanayofanya kazi ni 6,yasiyofanya kazi ni 12,pia kuna josho la kupuliza 1(Spray race) ambalo linafanya kazi na majosho 6 yanajengwa sasa na kwamba tuna machinjio ya kati(Min Abattoiirs) katika mji mdogo wa Madaba ambayo inafanya kazi”alisema Mbogo

Alisema kuwa katika sekta ya Maliasili Halmashauri ina misitu ya hifadhi 9 ambapo misitu 6 ni ya Serikali kuu ambayo ni Wino,Msitu wa nishati Songea,Chabruma,Machinjioni,Igawisenga na East-West Matogoro na misitu ya hifadhi inayomilikiwa na Halmashauri ni mitatu nayo ni Maposeni,Gumbiro na Lihanje

Alifafanua kuwa shughuli za uwindaji zitaendelea kupewa kipaumbele kwa kuanzisha vitalu zaidi na kwamba lengo la upandaji wa miti katika mwaka 2010/2011 ilikuwa ni kupanda miti1,500,000 ambapo hadi kufikia mei 2011 jumla ya miti 750,00 imeoteshwa na upandaji wa miti hiyo unaendelea ili kufikia lengo kusudiwa

Mbogo alieleza kuwa katika mpango wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini Halmashauri imekuwa ikiziangalia kwa umakini vyama vya ushirika vya mazao 8,chama kikuu cha ushirika 1,vyama vya akiba na mikopo vya kata 12 ambapo Saccos hizo zinajumla ya wanachama 11,795,hisa zao ni Shs. 167,918,850,akiba na amana jumla ya Shs.997,860,024 na kwamba Saccos hizo zimeweza kutoa mikopo yenye jumla ya Shs.2,262,831,160

Alifafanua kuwa pamoja na Saccos 12 za kata pia wafanyakazi wa Halmashauri wana Saccos 2 na makundi maalumu(wanawake) 1 ambazo zinajumla ya wanachama 2,597,hisa za Shs 70,204,490,akiba na amana ya Shs 773,808,775 ambapo mikopo iliyotolewa kwa mwaka 2010/2011 ni jumla ya Shs 1,806,100,366

Alisema kuwa kwa upande wa sekta ya ardhi Halmashauri inaendelea kupunguza kero za migogoro ya ardhi kwa kuelimisha wananchi sheria ya ardhi namba 5 ya vijiji ya mwaka 1999 ,pia inaendelea kuandaa matumizi bora ya ardhi katika vijiji

Alieleza zaidi kuwa Halmashauri ina jumla ya barabara zenye urefu wa kilometa 531 ambazo ni za changarawe na udongo ambapo kwa msimu wa 2010/2011 barabara nyingi ziliharibika na mvua lakini zimetengenezwa kwa kushirikiana na wananchi na sasa zinapitika vizuri

Kwa upande wa sekta ya elimu,Mbogo alisema kuwa Halmashauri inajumla ya walimu 771 wanaofundisha wanafunzi 43,642(msingi 37,161,na awali 6,481) ambapo shule za msingi zipo 94,pia kuna upungufu wa walimu 200 kwa kigezo cha uwiano wa Mwalimu 1 wanafunzi 45 pia kuna vyumba vya madarasa 709 kati ya mahitaji ya vyumba 982 ambapo nyumba za walimu zipo 360 kati ya nyumba 969 zinazohitajika na kwamba mikakati mbalimbali inaendelea kufanywa kutatua tatizo hilo

Akielezea elimu ya Sekondari alisema kuwa kuna jumla ya shule 26 kati ya hizo sekondari 23 za Serikali,3 zinamilikiwa na madhehebu ya dini na watu binafsi nako pia kuna changamoto mbalimbali ambazo zinaendelea kuwekewa mikakati ya kuboresha zaidi
Akizungumzia sekta ya afya alisema kuwa Wilaya ina Hospital 1 inayomilikiwa na Misheni,vituo vya afya vya Serikali 2 ambavyo ni Muhukuru na Madaba,Zahanati 36 kati ya hizo 13 zinamilikiwa na Misheni na 23 zinamilikiwa na Halmashauri

Alifafanua zaidi kuwa vituo hivyo vinatoa huduma kimgawanyo wa uwiano wa kitanda kwa wagonjwa 1:591,uwiano wa kituo cha afya kwa idadi ya watu 1:50,236,uwiano wa Zahanati kwa idadi ya watu1:5,494 pamoja na unafuu wa upatikanaji wa huduma za afya bado kuna changamoto nyingi katika magonjwa ya malaria,kuharisha,kifua kikuu,HIV/UKIMWI

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema kwa upande wa sekta ya maji wananchi 114,500 sawa na asilimia 60% ya wakazi wote wa Halmashauri ya Songea wanapata maji safi ambapo mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano wa wananchi,Serikali kuu, Halmashauri na wahisani na kwamba juhudi za kusambaza maji kwa wakazi waliobaki zinaendelea

Alisema kuwa katika mpango wa maendeleo ya vijana kuna jumla ya vikundi 100 vimepata mafunzo ya ujasiliamali yatakayo wawezesha kujiajiri katika sekta binafsi,vikundi 6 zimepata mkopo wa Shs.23,089,750 na mtandao wa vijana wenye lengo la kujenga umoja kati yao,elimu ya Ukimwi,madawa ya kulevya na kupambana na umasikini umesajiliwa

Alisema kuwa kwa upande wa utawala bora vikao vyote vya kisheria katika ngazi zote vimekuwa vikifanyika,uwazi na uwajibikaji katika mapokezi ya fedha na matumizi yake limefanyika kwani wananchi wamekuwa wakishirikishwa kwa ukaribu sana

Alifafanua kuwa mapato ya Halmashauri hutokana na ruzuku ya Serikali kuu na vyanzo vyake vya ndani ambavyo ni ushuru wa mazao,masoko,magulio na mapato mengine ambapo kwa mwaka 2010/2011 Halmashauri ilikasimia kukusanya Shs 10,145,866,000 kutokana na fidia ya vyanzo vya mapato,ruzuku ya mishahara na ruzuku ya matumizi ya kawaida

“Hadi mei 31,2011 Halmashauri ilikuwa imekusanya Shs 7,776,727,211.84 sawa na asilimia 76.65% ya mapato yote na ili kuongeza mapato zaidi kwa mwaka wa 2011/2012 Halmashauri imejipanga kutekeleza mikakati mingi”alisema Mbongo

Alisema kuwa miongoni mwa mikakati hiyo ni kupitia upya mikataba ya mawakala kwa kuwawekea malengo ya ukusanyaji ushuru na kuboresha mfumo wa kuwasimamia mawakala hao,kutungwa kwa sheria ndogo katika kila chanzo,timu ya mapato  kuwajibika kuratibu shughuli zote,mfumo wa motisha kwa wakusanyaji mapato wazuri utadumishwa ili kuleta ushindani na mikakati mingine mingi

Alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2010/2011 Halmashauri iliomba kuidhinishiwa kutumia Tshs 4,684,201,400 ambapo hadi mei 31 zilipokelewa Shs 3,347,542,178.30 ikiwa ni sawa na asilimia 71.5% ya fedha iliyokusudiwa na kwamba katika kipindi hicho Halmashauri ilitumia Shs 2,336,884,172.83 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo sawa na asilimia 49.9%

Ni wazi kuwa endapo Halmashauri nchini zikiwajibika kikamilifu katika kusimamia miradi ya maendeleo wananchi watakuwa na imani na serikali yao na malalamiko yatapungua kwa kiasi kikubwa na kufanya amani tuliyonayo iendelee kustawi

Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana kwa 0755-335051
Baruapepe;stephano12mango@yahoo.com


Mratibu wa Kampeni ya Ushindi ni Lazima Martha Lunyerere akipita mbele ya watazamaji katika uwanja wa majimaji wakati timu zikichezwa