Afisa Elimu wa Mkoa wa Ruvuma Paulina Mkonongo
Na Mwandishi Wetu,Songea
SERIKALI Mkoani Ruvuma imetangaza matokeo ya Mtihani wa kumaliza elimu ya Msingi mwaka 2011 ambapo wanafunzi 16,941 wamechaguliwa kuendelea na masomo kidato cha kwanza mwaka wa 2012 kati ya wanafunzi 36,718 waliofanya mtihani mwaka huu.
Aidha walimu wakuu wa shule za msingi 7 zilizopo katika Wilaya za Mbinga na Tunduru wamevuliwa madaraka na walimu waliosimamia mtihani ya kumaliza elimu ya msingi katika shule hizo 7 wameondolewa dhamana ya kusimamia sensa ya Taifa na mitihani baada ya baraza la mitihani la Taifa kubaini kuwa kulikuwa na udanganyifu wakati wa kufanya mtihani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake Kaimu katibu tawala wa Mkoa wa Ruvuma Dr. Anselem Talimo amesema kuwa mkoa huo ulikuwa na watahiniwa wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi waliofanya mtihani walikuwa 36,718 kati yao wavulana walikuwa 17,772 na wasichana walikuwa 18,946 hivyo watahiniwa waliofanya mtihani ni sawa 97.2% ya wanafunzi 37,778 walio sajiliwa kufanya mtihani mwaka huu.
Dr. Talimo ameeleza kuwa idadi ya watahiniwa ni sawa na 85.0% ya wanafunzi 43,149 walioandikishwa darasa la kwanza mwaka 2005 ambapo asilimia hiyo ya waliofanya mtihani inaonesha wazi kuwa baadhi ya wanafunzi walikuwa watoro, walio acha shule na ujauzito.
Dr. Talimo amewahimiza walimu wakuu wa shule za msingi Mkoani Ruvuma kusimamia maudhulio ya wanafunzi shuleni kila siku ili kuongeza asilimia za wanao hitimu elimu ya msingi kama yalivyo malengo ya milenia kwa wote.
Kaimu katibu tawala wa Mkoa Ruvuma Dr. Talimo akitangaza matokeo hayo amefafanua kuwa watahiniwa waliofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mkoani humo mwaka huu ni 16,941 kati yao wasichana ni 8606 wa wavulana 8335 sawa asilimia 46.1 ya watahiniwa 36,718 waliofanya mtihani mwaka huu Mkoani Ruvuma.
Ameeleza zaidi kuwa kwa ujumla ufaulu huo ni wa chini sana kwa kuwa haujafikia asilimia 50 pia ni pungufu kwa asilimia 1.78 ikilinganishwa na mwaka 2009 ambapo matokeo hayo ni ya wastani ni matokeo ya kiwilaya alihalisi inaonyesha kuwa Halmashauri za wilaya ya Mbinga, Namtumbo na Tunduru zimeshuka ufaulu ikilinganishwa na mwaka 2010.
Amebainisha zaidi kuwa Halimashauri ya wilaya ya Mbinga inaufaulu wa asilimia 40.2 ambayo ni chini kwa asilimia 0.82 ikilinganishwa na ufaulu wa asilimia 41.02 wa mwaka 2010, Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo inaufaulu wa asilimia 50 ikilinganishwa na asilimia 53.89 ya mwaka 2010 ambayo ni pungufu kwa 3.89 na Halmashauri ya wilaya ya Tunduru inaufaulu wa asilimia 41.2 ambayo ni upunguvufu wa asilimia 10.56 ikilinganishwa na asilimia 51.86 ya mwaka 2010.
Ameongeza kuwa Halmashauli ya wilaya ya Songea vijijini inaufaulu wa asilimia 47 ambayo ni nyongeza kwa asilimia 7.58 ikilinganishwa na asilimia 39.42 ya mwaka 2010 hivyo Halmashauli hiyo ufaulu umepanda kidogo kuliko ufaulu wa matokeo ya mwaka jana na kwamba bado ufaulu huo uko chini ya asilimia 50 na Halmashauli ya Manispaa Songea inaufaulu wa asilimia 67.2 ambayo ni nyongeza kwa asilimia 2.46 ikilinganishwa na ufaulu wa 64.54 ya mwaka jana hivyo amewapongeza walimu wa shule za msingi na Maafisa Elimu wa Manispaa hiyo kwa kuwa na ufaulu wa asilimia zaidi ya 50 na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi hata hivyo walimu pamoja na Maafisa Elimu wa Manispaa hivyo wanapaswa kujiwekea malengo zaidi na kusimamia malengo ikiwa pamoja na viongozi na waalimu wa shule za msingi mkoani humo kujipanga upya hali ya kushuka na kupanda matokeo ya mtihani ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara.
Aidha kaimu katibu tawala wa Mkoa wa Ruvuma Dr. Talimo ameeleza kuwa wanafunzi 163 wa shule za msingi 7 Mkoani Ruvuma wamefutiwa mtihani yao kufuatia kuwepo kwa udanganyifu ambao inadaiwa kuwa kati yao walikutwa na majibu ya mitihani wakiwa kwenye vyumba vya mithani na wengine walikuwa na mawasiliano na wasimamizi wa mithani hiyo.
Dr. Talimo ametaja shule ambazo walimu wakuu wameng’olewa madaraka kutokana na udanganyifu uliofanwywa na mtihani wa kumaliza elimu ya msingi katika wilaya ya Tunduru ni shule ya msingi Namapungwa ambako wanafunzi 59 wamefutiwa mtihani , shule ya msingi Mchekeni watahiniwa 23 kati ya 35 waliofanya mtihani wamefutiwa mtihani, shule ya msingi mchemba wanafunzi 2 wamefutiwa mtihani kati ya wanafunzi 30 waliofanya mtihani na katika wilaya ya mbinga kwenye shule ya msingi ya mnazi mmoja baraza la mtihani Tanzania limefuta matokeo ya watahiniwa 18 kati ya watahiniwa 46.
Dr. Talimo amezitaja shule zingine wameondolewa madaraka kuwa ni shule ya msingi Rulala watahiniwa 10 wamefutiwa mtihani kati ya wahitimu 18 na wanafunzi 43 waliofanya mtihani kati ya watahiniwa 63 wamefutiwa mtihani .
Mwisho