Na, Stephano Mango,Pwani
MAAFISA Ugani nchini wametakiwa kukithamini na kukiendeleza kilimo
cha zao la Ufuta ili kiweze kubadilisha maisha ya watanzania kutokana na mahitaji ya
soko kuwa makubwa kwa sasa na kufanya zao hilo kwa baadhi ya maeneo kuwa zao
kubwa la kibiashara
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya
Rufiji Nurdin Babu kwenye ufunguzi wa mafunzo maalumu kuhusu kilimo bora cha
ufuta, uliowashirikisha maafisa ishirini na wadau mbalimbali wa zao la ufuta
wilayani Rufiji Mkoani Pwani yaliyofanyika Mji mdogo wa Ikwiriri Wilayani Rufiji
Babu alisema kuwa Ufuta ni zao lisilotiliwa
maanani na wakulima wengi nchini kwa miaka mingi pamoja na uwingi wa faida zake
kwa binadamu, lakini kwa miaka ya hivi karibuni, takribani sehamu zote ambako
hali ya hewa imekuwa rafiki wa kulistawisha zao hilo, wakulima wengi
wameligeukia na kuanza kulima kwa kasi.
Alisema kuwa Wilaya ya Rufiji ni
mojawapo ya wilaya ambazo zinastawisha zao la ufuta kwa siku nyingi na siku za
hivi karibuni kasi ya uzalishaji imeongezeka kutokana na upatikanaji wa uhakika
wa soko la ufuta.
“Hili ni zao lenye faida kubwa kama
utekelezaji wa taaluma ya uzalishaji utafuatwa kwa makini, ambalo ndiyo lengo
kuu la mafunzo haya na ni lazima walau
kwa kuanzia tani elfu tano (5000) katika msimu ujao wa kilimo 2012/2013 kutoka
tani za sasa 400 kwa mwaka na tani 280 mwaka 2005/06.”,
anasisitiza Babu.
Akizungumza kwenye Mafunzo hayo Afisa
Habari Mshauri Mkoa wa Pwani Silas Bwena alisema kuwa Serikari kupitia wizara ya
viwanda, biashara na masoko, chini ya mradi wa MUVI mkoa wa Pwani imetoa mafunzo
hayo kwa maafisa ugani ili waweze kuifikisha Elimu waliyoipata moja kwa moja kwa
walengwa, ambao ni wakulima wadogowadogo walioko kwenye kata na vijiji husika.
Bwena alisema kuwa Mafunzo hayo yamelenga kumuwezesha
mkulima kupata taaluma na uelewa mzuri zaidi katika kilimo cha zao hili tofauti
na wanavvoelewa sasa ili kuboresha uzalishaji kwa lengo la kuongeza mazao
yaliyo bora yatakayowezesha kupata bei nzuri kwenye soko
MWISHO