About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Tuesday, October 25, 2011

UCHAKACHUAJI WA MAPATO YATOKANAYO NA MAZAO YA MISITU MBINGA WASABABISHA HASARA

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Shaib Mnunduma
Na Gideon Mwakanosya,Mbinga
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imepata hasara ya shilingi milioni 18 kupitia idara yake ya maliasili na mazingira kutokana na uzembe uliofanywa na watumishi wachache wa idara hiyo, waliopewa dhamana ya ukusanyaji wa ushuru wa mazao ya misitu.
Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika kutoka katika halmashauri hiyo ambavyo vilizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti kwa sharti la kutotaja majina yao, vilisema kuwa hasara hiyo imetokea kufuatia vitabu vyenye risiti ambavyo hutumika kukusanyia ushuru huo vimepotea katika mazingira ya kutatanisha.
Habari zinaeleza kuwa jitihada za kutafuta vitabu hivyo vilivyopotea mpaka sasa zimegonga mwamba jambo ambalo uongozi wa wilaya ya Mbinga, ulilazimika kuchukua hatua za kuripoti kituo kikuu cha polisi kwa msaada zaidi ambapo baadhi ya watumishi wa idara ya maliasili na mazingira wilayani humo waliwekwa mahabusu kwa siku kadhaa.
Aidha pamoja na watumishi hao kuwekwa mahabusu hivi sasa wameachiliwa huru na hakuna hatua zingine walizochukuliwa huku wakiendelea na kazi zao kama kawaida kitendo ambacho kimekuwa kikisababisha kuzua maswali mengi kutoka kwa watumishi wengine wa halmashauri hiyo.
Utaratibu wa halmashauri ya wilaya hiyo katika utoaji wa vitabu hivyo unaeleza kuwa alikabidhiwa mkuu wa kitengo cha kukusanya ushuru wa mazao ya misitu Nambole   Nanyanje ambaye huwagawia watumishi wenzake wanaohusika na suala la kukusanya ushuru huo.
Mwandishi wa habari hizi alipomuuliza kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Bernard Semwaiko juu ya tuhuma hizo alikiri kuwepo kwa upotevu wa fedha na vitabu hivyo huku akisema halmashauri yake imekwisha kamilisha utatuzi wa jambo hilo.
“Ni kweli kiasi hiki cha fedha kilipotea kutokana na upotevu wa vitabu vilivyokuwa vikitumika kukusanyia ushuru wa mazao ya misitu, najua umewahi kusikia kuna baadhi ya watumishi tuliwaweka mahabusu”, alisema Semwaiko.
 Kadhalika Mwandishi alipotaka kujua undani wa tatizo hilo Semwaiko alifafanua kuwa lilibainika kufuatia wakaguzi waliokuwa wakifanya kazi ya kukagua mahesabu ya halmashauri hiyo, ndipo wakaguzi hao waligundua kuna upotevu wa fedha hizo na vitabu, yenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 18 kutoka idara ya maliasili na mazingira wilayani humo ambavyo vilitumika kukusanyia ushuru wa mazao ya misitu.

AJALI YAUA MMOJA NA KUJERUHI WATU SITA BAADA YA GARI KUACHA NJIA NA KUPINDUKA

Na, Gideon Mwakanosya SongeaMTU mmoja mkazi wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma amekufa papohapo na wengine sita wamejeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Songea mjini kwenda Namtumbo kuacha njia na kupinduka.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Naftari Mantamba amesema kuwa tukio hilo limetokea oktoba 24 mwaka huu majira ya saa 8.00 mchana katika eneo la Mletele Songea mjini.
Mantamba amemtaja aliyefariki dunia kuwa ni Sabina Similia(80) mkazi wa eneo la Faraha Store Mbinga mjini na kwamba waliojeruhiwa amewataja kuwa ni Failuna Komba(70) na Hassan Ally(40) wote wakazi wa kijiji cha Mgombasi kilichopo katika wilaya ya Namtumbo.
Amewataja majeruhi wengine kuwa ni Flora Mamzi(39) mkazi wa mtaa wa Furaha Store Mbinga mjini,Amina Komba(63) mkazi wa kata ya Lizabon Songea mjini,Mohammed Hassan(50) mkazi wa mtaa wa Ruhila Songea mjini na Omary Mtumbuka(42) mkazi wa kijiji cha Litola kilichopo wilayani Namtumbo.
Kaimu Kamanda Mantamba amefafanua kuwa basi hilo lenye namba za usajili T761 ATN aina ya Isuzu Forward ambalo lilikuwa limebeba abiria kutoka Songea mjini kuelekea Namtumbo na kwamba lilikuwa likiendeshwa na Hamis Chidumule(35) mkazi wa kata ya Ruvuma Songea mjini likiwa kwenye mwendo mkali liliacha njia na kupinduka.
Amesema kuwa majeruhiwa mpaka wamelazwa katikahospitali ya mkoa kwenye wodi za majeruhi ambapo hali zao zinaendelea vizuri  na kwamba chanzo cha ajali hiyo gari hiyo ilikuwa kwenye mwendo mkali hali iliyosababisha dereva ashindwe kumudu ukukani na hivyo kuacha njia na kupinduka.
Hata hivyo polisi mkoani hapa imefanikiwa kumkamata dereva wa gari hilo na kwamba kwa sasa uchunguzi unaendelea kufanyika ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

WANANCHI WA MPAKANI MWA MSUMBIJI NA TANZANIA WATAKA BARABARA KWA KIWANGO CHA LAMI

 Meneja wa Tanroads Mkoa wa Ruvuma Abraham Kissimbo akitoa maelekezo ya ujenzi wa daraja la Mkenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu hayupo pichani alipotembelea mpaka wa Msumbiji na Tanzania
 Daraja la Mkenda linalounganisha nchi ya Msumbiji na Tanzania
 Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu akiwa na Viongozi mbalimbali wakipita juu ya daraja la Mkenda wakielekea nchi jilani ya Msumbiji
 Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu akipata maelekezo ya ujenzi wa daraja linalounganisha nchi ya Msumbiji na Tanzania lililojengwa kivukoni Mkenda kutoka kwa Meneja wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Abraham Kissimbo
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu (katikati) akipokea maelezo ya jengo lililojengwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) kutoka kwa Meneja wa TRA mkoa wa Ruvuma Apily Mbaruku kushoto na Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Oley Sabaya kulia
Na Stephano Mango,Songea
WANANCHI wa kitongoji cha Mkenda kilichopo katika kijiji cha Nakawale kata ya Mhukuru wilaya ya Songea vijijini mkoani Ruvuma wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Miundombinu kuona umuhimu wa kuwakumbuka kwa kuwajengea barabara kwa kiwango cha lami ili waweze kusafirisha bidhaa zao yakiwemo mazao ya kilimo kiurahisi.
Ombi hilo wamelitoa jana kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu wakati alipofanya ziara ya kutembelea kitongoji hicho kilichopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ambako Serikali imefanikiwa kujenga daraja la kudumu ambalo linaunganisha na nchi hiyo jirani katika mto Ruvuma.
Mmoja wa wakazi wa kitongoji hicho Ramadhani Hussein alisema kuwa kitendo cha Serikali cha kujenga daraja la Mkenda kwenye mto Ruvuma kumepelekea kuwepo kwa maendeleo makubwa kwa wananchi wa eneo hilo kutokana na biashara zinazofanyika kati yao na wananchi wa nchi jirani ya Msumbiji.
Hussein alisema kutokana na hali hiyo ni vyema Serikali ikafikiria kujenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Songea mjini hadi Mkenda yenye urefu wa kilometa  124   hali itakayokuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa tarafa ya Mhukuru ambayo ipo mpakani.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha FRELIMO kijiji cha Congress nchini Msumbiji John Bosko ambaye alihudhuria mkutano huo wa hadhara alimwomba Mkuu wa mkoa wa Ruvuma kufanya mawasiliano na Serikali ya Msumbiji ili kuhakikisha kuwa barabara ya kutoka Songea hadi Mkenda inajengwa haraka na kwamba barabara kutoka Mkenda hadi Maputo inajengwa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Kwa upande wake Meneja wa wakala wa barabara mkoa wa Ruvuma(TANROADS) Mhandisi Abraham Kissimbo alisema kuwa Serikali imedhamira kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kwamba mpaka sasa tayari michoro imekamilika na kinachosubiriwa ni utekelezaji.
Naye Mkuu wa mkoa wa Ruvuma aliwaeleza wananchi hao kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kufanyia matengenezo barabara zote zikiwemo za mipakani ili zipitike kiurahisi na kwamba aliwahimiza wananchi kujikita kwenye kilimo ili barabara hizo zitakapokamilika waweze kusafirisha mazao yao pamoja na bidhaa zingine.
Aidha Mwambungu aliwataka wakazi wa kitongoji hicho kujitokeza kwa wingi kuchangia nguvu zao kwenye ujenzi wa kituo cha polisi hasa ikizingatiwa kitongoji hicho cha Mkenda kipo mpakani mwa nchi ambapo kwa siku za usoni unatarajia kuwa mji mdogo hali itakayopelekea pia kuwepo na vitendo vya uharifu na kwamba alichangia shilingi milioni moja kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.