About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Tuesday, September 11, 2012

VIONGOZI WA RUVUMA PRESS CLUB WAJIFICHA MAFICHONI KUTOKANA NA MAANDAMANO


KATIBU WA CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA RUVUMA( RUVUMA PRESS CLUB) AMBAYE PIA NA KATIBU WA MBUNGE WA JIMBO LA SONGEA MJINI DKT EMMANUEL NCHIMBI) ANDREW CHATWANGA

Na Stephano Mango, Songea

MGOGORO mkubwa umeibika kwa waandishi wa habari mkoani Ruvuma baada ya Viongozi wa chama cha waandishi wa habari mkoani humo kutoitisha maandamano na kuingia mafichoni kwa muda ili kuepusha kufanyika maandamano ya kuunga mkono maombolezo ya kifo cha mwandishi wa habari na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Iringa Daud Mwangosi aliyefariki kwa kupigwa na mlipuko uliosababishwa na polisi katika kijiji cha Nyololo mkoani Iringa.

Mgogoro huo umewagawa waandishi wa habari na kuwafanya baadhi ya waandishi kutishia kujitoa nafasi zao za uongozi na uanachama katika umoja huo kwa sababu ya kutokuwa na imani na viongozi wao ambao wanaonekana kufanya kazi kutokana na maslahi ya kisiasa.

Waandishi wa habari mkoani Ruvuma walianza kwa kushangazwa na hatua ya viongozi wa ngazi ya juu ya chama hicho kutowajulisha muda na njia zitakazotumika kwa maandamano hayo hadi pale kwa njia ya simu na baadhi ya waandishi wa habari ambao walishapanga waandamane saa 10. Jioni baada ya kujihakikishia kuwa viongozi wao wamewatosa na hawana ajenda muhimu ya kupinga maandamano hayo kwa hula.

Awali baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari ambao ni wanachama wa chama cha waandishi wa habari mkoani humo (RPC) walijikusanya pamoja na kufuatilia matangazo ya vyombo mbali mbali vya habari yaliyokuwa yakiendelea huku wakiangalia baadhi ya picha zilizopigwa wakati na baada ya kifo cha mwandishi huyo wa habari ambaye alipatwa na mauti wakati akiwa kazini na walipanga wandamane saa 10 jioni muda ambao ndio Marehemu Mwangosi aliuawa kinyama kupigwa na bomu na Polisi.

Katibu Msaidizi wa Chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Ruvuma , Julius Konala, alionyesha ushirikiano mkubwa kwa wanachama ambao muda wote walikuwa wanadai ratiba na hatua iliyofikiwa na viongozi wa chama hicho kwaajili ya maandamano na kuwajulisha kuwa viongozi wake hawajulikani waliko na wanapinga kufanyika kwa mnaandamano hayo.

“Jamani mimi mtanionea tuu, Mwenyekiti na katibu wamesema kuwa UTPC imeyasimamisha maandamano yetu bila kutaja sababu,” alisema Konala ambaye alichukua hatua ya kuwasiliana na viongozi wa Polisi mkoani hapa waliotaka kujua ni njia zipi zitakazotumika katika maandamano hayo ili walete askari wa kuyalinda maandamano hayo ya amani.

Tukio hilo limewakasirisha sana viongozi wa Chama hicho na kulazimika kuitisha mkutano wa dharura kwa baadhi ya wanachama wengi wao wakiwa ni mamluki na kusababisha viongozi hao kuomba radhi kwamba wamekosa mawasiliano nao na baadhi ya wanachama wametishia kujiuzulu akiwemo Katibu msaidizi Julius Konala kwa madai kwamba chama hicho kimeingiliwa na mikono ya wanasiasa.

“Naona mbele yangu kuna wingu kubwa na zito ambalo mwisho wake siujui, nafikiria kujiuzulu uongozi na kujitoa katika chama, “ alisema Konala.

Baadhi ya wadau wa habari mkoani humo wameonesha kushangazwa na ukimya wa wanahabari wa mkoa huo licha ya wanahabari wote nchini wakionekana kwenye runinga wakiandamana kupinga ukatili huo uliofanywa dhidi ya Mwandishi wa habari akiwa kazini.

Hata hivyo Mkurugenzi wa muungano wa Vyama vya waandishi wa habari nchini UTPC Abubakar Karsan akiongea na Tanzania Daima kwa njia ya Simu amekanusha vikali kuzuia maandamano bali wao waliyabariki na ndio maana walijumuika na waandishi wengine nchini na kutoa matamko mbalimbali katika viwanja vya Jangwani Jijini Dar es Salaam na kwamba wao walitoa maelekezo kwa Ruvuma Press Club kuungana na Press Club zingine nchi kufanikisha maandamano ya amani ambayo yameitishwa kiuhalali.
Mwisho