About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Monday, November 21, 2011

UPIMAJI WA VIWANJA KWA KUTUMIA KAMPUNI KUNAKOMESHA MIGOGORO YA ARDHI NCHINI?

 Waandishi wa habari wakiwa kazini wakati Mwenyekiti wa Mtaa wa Mshangano Paulo Mangwe akitoa tamko la kutaka wapimiwe ardhi na Kampuni ya Ardhi Plan kwenye mkutano wa wananchi wa kata ya Mshangano
                                  Wananchi wakiwa kwenye mkutano huo

 Diwani wa Kata ya Mshangano Faustine Mhagama akizungumza kwenye mkutano huo
 Mkurugenzi Mtendaji wa Ardhi Plan Gombo Samandito akieleza namna kampuni yake itakavyopima viwanja Kata ya Mshangano kabla ya msimu wa mvua kuanza
 Mgeni Rasmi wa tatu toka kushoto ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati za Huduma za Uchumi na Jamii Genfrida Haule akizindua mradi wa upimaji viwanja 18000 kata ya Mshangano
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ardhi Plan akiwaonyesha wananchi ramani zilizopitishwa na Wiozara ya Ardhi ,Nyumba na Maendeleo na Makazi kwa ajili ya kupima viwanja kata ya Mshangano
Na Stephano Mango,Songea
ARDHI ni moja kati ya rasilimali yenye thamani kubwa endapo usimamizi wa matumizi yake utalenga kumuinua mwananchi kiuchumi,kijamii tofauti na ilivyo sasa kwenye maeneo mengi katika jamii kwani ardhi imekuwa chanzo kikubwa cha mapigano na migogoro
Maeneo mengi yamekuwa na migogoro ya ardhi kutokana na usimamizi mbovu wa matumizi ya ardhi usiozingatia sheria za nchi,tamaa za baadhi ya viongozi  na wakati mwingine dosari za uandaaji wa sera mbalimbali za nchi zisizozingatia uhalisia wa umiliki wa ardhi
Sera zote za maendeleo na mikakati mbalimbali ya maendeleo haiwezi kukamilika bila uwepo wa ardhi na rasilimali zake ikiwemo maji,misitu,madini,wanyamapoli,nishati na miundombinu mingine hivyo ni lazima kuwe na mipango mizuri ya matumizi ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuainisha ukubwa wa ardhi iliyopo,mtumiaji ni nani na inafaa kwa shughuli ipi ili kuepuka migogoro katika jamii
Ili kufanikisha hilo ni lazima kuwe na wataalamu wa mipango miji wenye kuzingatia maslahi ya umma badala ya maslahi binafsi,vifaa vya kisasa vya kupangia miji vizuri na kuondokana na ujenzi wa makazi holela yasiyozingatia ukuaji wa idadi ya watu
Akizungumzia hilo Mtaalamu wa mipango miji ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ardhi Plan Gombo Samandito alisema kuwa Halmashauri nyingi nchini hazijaona umuhimu wa kuajiri Wataalamu wa mipango miji kwasababu ambazo hazijawa wazi
Samandito alisema kuwa mara kadhaa utasikia Halmashauri na Manispaa  nyingi zimekuwa zikilalamika kukosa Walimu,Madaktari,Wauguzi na Wafanyakazi wengine lakini haijawahi kusikika Halmashauri hizo zikilalamika kukosa Wataalamu wa Mipango Miji
“Baadhi ya miji haina kabisa wataalamu wa mipango miji na hata pale wanapokuwepo hawatumiki ipasavyo hali inayosababisha wananchi kujenga makazi yao holela na kusababisha adha kubwa mijini kwa kushindwa kufikiwa na miundombinu muhimu kama vile maji,nishati ,miundombinu ya barabara na huduma zingine za dharura” alisema
Alieleza kuwa inapotokea wananchi wamejenga makazi yao holela na Serikali inamipango mingine ya maendeleo katika maeneo hayo yaliyojengwa ndipo inapoamriwa kubomolewa bila kulipa fidia na kuitwa wananchi kuwa ni wavamizi wa maeneo hayo na kusababisha malalamiko na migogoro baini ya Serikali na wananchi
Samandito alisema kuwa ni muda mrefu sasa Serikali imekuwa na utaratibu wa kutekeleza upangaji na upimaji wa miji kwa njia ya kutwaa maeneo kutoka kwa wamiliki wake wa kimila kwa kutumia sheria zilizopo ,kulipa fidia ya shilingi elfu 90 kwa hekta moja na kuamriwa kuhama eneo hilo na kupimwa kwa matumizi mengine itakavyokuwa imepangwa na mamlaka husika
Alieleza kuwa  utaratibu huu haujawahi kukamilika bila kuacha malalamiko kwa wananchi kwani mara nyingine fidia imekuwa ikichelewa kutolewa.kutokulipa kabisa na wakati mwingine kulipwa kidogo tofauti na uthamini wa eneo hilo na kuwaacha wananchi wakiwa maskini na wakimbizi kwenye ardhi yao
Alisema kwenye maeneo mengine wamiliki wake wa kienyeji wamekuwa wakikata maeneo yao vipande vipande na kuviuza kwa haraka ili kuepuka fidia za Serikali,biashara hiyo ya vipande vidogovidogo maarufu kwa ishirini kwa ishirini
“Hali hiyo licha ya kusababisha migogoro ya ardhi baini ya familia lakini imekuwa chanzo cha makazi holela kutokana na kugawana viwanja kienyeji visivyopimwa na kuleta adha kubwa Serikalini”alisema Samandito
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Ardhi Plan Gombo Samandito alisema kuwa ili kuondokana na uvamizi,migogoro ya ardhi na makazi holela ni lazima Serikali ione umuhimu wa upimaji wa viwanja vya makazi,biashara kwa kutumia Kampuni binafsi kwa gharama za wananchi wenyewe kwani jambo hilo linawezekana
Samandito alisema kuwa kwa kutumia sheria ya mipango miji namba 8 ya mwaka 2007 ambayo katika kifungu cha 15(2) inamruhusu mmiliki wa ardhi kuandaa michoro ya mipango miji na kupima,ambapo mmiliki anaweza kuandaa mpango wake hata kama tayari kuna mpango mwingine umeshaandaliwa kabla ya kupitishwa na Halmashauri husika
Alisema kuwa sheria ya mipango miji kifungu cha 15(8) pia inamtaka mmiliki wa ardhi anayetaka kuandaa mpango kuandika barua kwa mamlaka husika(Halmashauri) kabla hajafanya shughuli hiyo na kwamba sheria hiyo inatoa fursa kubwa kwa mmiliki wa ardhi kutozuiwa kuandaa mpango katika eneo lake bali asaidiwe ambapo kifungu cha 15(9) ni wajibu wa Waziri wa Ardhi,Mkurugenzi wa mipango miji na vijiji na Katibu Tawala wa mkoa kumsaidia mmiliki wa ardhi kufanikisha mpango wake
Alisema kuwa sheria hiyo kifungu cha 35(1) inaeleza kuwa mamlaka husika au Mkurugenzi wa Halmashauri ndani ya siku 60 tokea kupokelewa kwa maombi ya kuombea kibali cha kutekeleza mpango au kubadilisha matumizi anatakiwa kutoa majibu ya kukubali au kukataa maombi hayo
Alieleza zaidi kuwa  kifungu cha 35(4) kinaeleza kuwa endapo mamlaka husika au Mkurugenzi wa Halmashauri ameshindwa kujibu barua ya maombi kwa muda ulioandikwa hapo juu kwenye kifungu kidogo cha 1,itachukuliwa kuwa maombi yaliyoombwa yamekubaliwa
Alisema kuwa kwa kutambua umuhimu wa mipango miji mizuri na uwepo wa sheria hiyo,Kampuni ya Ardhi Plan imeingia ubia na wananchi wa kata ya Mshangano Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma ya kuwapimia viwanja 18000 kwa kuanzia na mchoro namba 9 eneo la Beroya ambapo mradi huo ulizinduliwa Novemba 20 mwaka huu
Alifafanua kuwa mradi huo wa upimaji wa viwanja kwa kutumia Kampuni uliibuliwa na wananchi wenyewe baada ya kuona wanakaa na kuishi katika makazi holela yasiyopimwa kwa muda mrefu kwani miaka mingi wananchi wa kata hiyo wamekuwa wakipeleka maombi Halmashauri ya kuomba kupimiwa maeneo yao bila mafanikio kutokana na Halmashauri kukosa uwezo wa kifedha
“Mradi huo utawainua kiuchumi wananchi wa Kata ya Mshangano kwa sababu wataweza kukopaa kupitia makazi yao  na kwamba wataweza kuishi katika makazi bora yaliyopimwa na kufanya mji wa Mshangano kuwa wa kisasa zaidi kuliko maeneo mengine ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea”alisema Samandito
Alieleza kuwa mradi huo umezingatia upangaji wa miji wa kisasa na lazima utaenda sambamba na ulinganifu wa idadi ya watu katika kipindi cha miaka kuanzia 50 hadi 100 ijayo ili miundombinu na mahitaji mengine yawepo na yaweze kukidhi haja za wakati huo
Akielezea  Mradi huo Afisa Mtendaji wa Kata ya Mshangano Stan Kibiki alisema kuwa Mwaka 2010 kata yetu  ilibahatika kupata mradi wa upimaji viwanja wa Halmashauri lakini bahati mbaya fedha yenyewe ilikuwa kidogo kwani waliweza  kupima viwanja 347 katika mtaa wa Namanyigu eneo dogo mashambani hivyo tatizo la wananchi kuishi katika makazi holela lilibaki palepale
Alisema kuwa wananchi  kwa kushirikiana na viongozi wao katika kutatua tatizo hili waliamua kutafuta njia mbadala ambayo kwa kutumia sheria namba 8 ya Mipango Miji ya 2007 walitafuta Kampuni ya Ardhi Plan ya Jijini Dar Es Salaam ili iweze kuwapimia viwanja katika maeneo yao
Alieleza kuwa baada ya kuipata Kampuni hiyo makubaliano yakawa malipo ni ardhi kwa ardhi yaani wanapima ardhi wanalipwa ardhi kwa asilimia za kwamba mwananchi anapata 60% ya ardhi iliyopimwa na Kampuni inapata 40% ya ardhi iliyopimwa
Alifafanua kuwa asilimia 40% inayotolewa kwa Kampuni inatumika katika kuandaa michoro ya ubunifu wa mipango Miji (10%),kupima viwanja (10%)kuchonga barabara (10%) na faida ya Kampuni (10%) na kwamba mradi huu hauhusishi malipo ya fidia yoyote hii ni kwa makubaliano ya wananchi wenyewe na itakuwa kwa kusogezana
Afisa huyo alisema kuwa maeneo ya umma kama vile soko,shule,zahanati ,makaburi,stendi,msikiti,kanisa na maeneo ya wazi(open space)  yatatolewa bure katika mradi huo na kufanywa kuwa mradi wa kwanza kuibuliwa na wananchi wenyewe kwa kuitumia Kampuni ya Ardhi Plan kupanga mji wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Alieleza kuwa gharama za mradi huo zinatolewa na wananchi wenyewe kwa kutoa ardhi badala ya kusubiri  Serikali mpaka ipate uwezo wa kifedha ambapo kwa wale wenye maeneo madogo yaani kiwanja kimoja mpaka viwili wanatozwa gharama ya fedha shilingi laki moja(100,000/=) kwa kiwanja kimoja na laki mbili(200,000) kwa viwanja viwili kama gharama za upimaji
Kibiki alisema kuwa mitaa ambayo  michoro yake imekamilika ni Mshangano,Namanyigu, na Mitendewawa yenye jumla ya viwanja elfu kumi na nane (18,000/=) ambapo mitaa mingine itafuata baadaye
Alieleza zaidi kuwa huduma za jamii kama maji ya bomba,umeme,barabara na miundombinu mingine itawafikia kama ambavyo wananchi wa kata ya Mshangano wanavyotegemea kupata mara baada ya mradi kukamilika
Kibiki alisema kuwa katika mradi huo wananchi watapata faida nyingi ikiwemo ya ajira kuanzia hatua ya kupima viwanja kwani mchoro mmoja umetoa ajira kwa watu 40 ambao wamekuwa wanalipwa  Tshs 4000/= kwa kutwa moja na kwamba kwa michoro 23 itatoa ajira kwa watu 920
Alifafanua kuwa kwenye uchongaji wa barabara mchoro mmoja umetoa ajira kwa watu 80 ambapo kila mmoja analipwa Tshs 5000/= kwa kutwa hivyo michoro 23 itatoa ajira kwa watu 1840 ambapo jumla ya michoro yote 23 wananchi watakao kuwa wamepata ajira kwenye upimaji na kuchonga barabara ni watu 2760 wanawake na wanaume
Alieleza jumla ya fedha watakayokuwa wanapata wananchi wa kata hiyo kwenye upimaji wa viwanja ni 920X4000=3680,000/= na kwenye uchongaji wa barabara 1840x5000=9,200,000/= na kufanya jumla ya fedha yote kuwa ni Tshs 12,880,000/= kwa siku
Alifafanua kuwa wafanyakazi hao watatoka ndani ya kata ya Mshangano ambapo mradi unatekelezwa kwani hiyo inaweza kuwasaidia sana wananchi kujikimu kimaisha na kumudu kununua pembejeo za kilimo katika msimu huu na hivyo kuzalisha mazao kwa wingi
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Ardhi Plan Gombo Samandito alimalizia kwa kusema kuwa wakati nchi yetu inapata uhuru ilikuwa na watu na watu milioni 9 lakini kwasasa inawatu milioni 40 na wanaishi kwenye maeneo yasiyopimwa
Alisema inakadiliwa kuwa ifikapo mwaka 2028 idadi ya watanzania itakuwa milioni 75 hii ni kwa kutumia ongezeko la asilimia 2.9 kwa mwaka ikilinganishwa na watu milioni 33.67 mwaka 2002 hali hiyo ni lazima Serikali ione umuhimu wa Kampuni binafsi kupima ardhi ili wananchi waweze kuishi kwenye makazi yaliyopimwa kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo
Alieleza kuwa jambo hilo linawezekana kwa makubaliano ya wananchi kulingana na maeneo wanayoishi kwa gharama zao ili kujenga mustakabali mzuri na usimamizi mzuri wa matumizi ya ardhi na Kampuni zitakazohitajika kupima ardhi hiyo na kuondoa migogoro mingi ya ardhi iliyopo kwenye maeneo yetu na kukomesha adha ya kuwepo kwa makazi holela kwani uwepo wa makazi holela ni kipimo cha umaskini
Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana 0755-335051

DEREVA AFA PAPO HAPO BAADA YA GARI LAKE KUACHA NJIA NA KUPINDUKA

  Kamanda wa Polisi Mkoani Ruvuma Michael Kamuhanda
 
Na Gideon Mwakanosya, Songea
 
Mtu mmoja amekufa papo hapo na kujeruhiwa watu sita huko katika Kijiji cha Mlilayoyo Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Njombe kwenda Hanga kuacha njia na kupinduka.
 
Akizungumza na mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/   jana ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amesema kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 11.45 jioni kwenye barabara ya Mlilayoyo kuelekea Hanga na amemtaja aliyekufa papo hapo baada ya gari hilo kuacha njia na kupinduka Leonala Msemwa (60) Mkazi wa Kijiji cha Hurika kilichopo Wilayani Njombe Mkoa wa Iringa.
 
Kamuhanda amewataja waliojeruhiwa vibaya kuwa ni Kristofa Salingwa (30),Roida Salingwa (37),Luciana Salingwa ( 25 ) na Nelson Mligo (1) wote wakazi wa Kijiji cha Itulika Wilayani Njombe Mkoa wa Iringa wengine waliojeruhiwa ni Prisca Salingwa ( 28) Mkazi wa Kijiji cha Mtwango kilichopo Wilayani Njombe Mkoa wa Ruvuma na dereva wa gari hilo Steven Ngonyani (28) Mkazi wa Mfaranyaki Manispaa ya Songea.
 
Amefafanua zaidi kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio huko kwenye barabara ya Mlilayoyo kwenda Hanga Wilayani Namtumbo gari lenye namba za usajili T 360 AJF TOYOTA MARK II, rangi nyeupe ambayo ilikuwa ikiendeshwa na Steven Ngonyani ikitokea Njombe kwenda Hanga iliacha njia na kupinduka kisha ilisababisha kifo cha Leonala Msemwa na majeruhi sita.
 
Amebainisha zaidi kuwa majeruhi wawili dereva wa gari hilo Steven Ngonyani na Kristofa Salingwa kwasasa wamelazwa katika hospitali ya Serikali ya Mkoa Songea wakiwa wanaendelea kupata matibabu na majeruhi wengine wanne wametibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani kwao na hali zao zinaendelea vizuri.
 
Kamanda Kamuhanda ameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kwamba dereva wa gari hilo alikuwa kwenye mwendo kasi ambao ulimsababishia ashindwe kuumudu usukani kisha gari hilo liliacha njia na kupinduka.
 
MWISHO