About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Saturday, July 6, 2013

AMINA CHIFUPA HUYU HAPA, AWASUMBUA VIJANA



             AMINA CHIFUPA AKIWA KATIKA POZI ENZI ZA UHAI WAKE

Na; Stephano Mango, Songea

JUNI 26 mwaka 2007 Tanzania hususani jamii ya vijana ilikumbwa na msiba mzito wa kuondokewa na Mwanaharakati wa Vijana,mpendwa wetu Amina Chifupa Mpakanjia.

Hadi anafariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi katika hospitari ya Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) ya Lugalo alikokuwa amelazwa akiugua homa kali na kisukali alikuwa ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia tiketi ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi(UV-CCM)

Amina Chifupa amefariki akiwa na umri wa miaka 26 ya kuzaliwa kwake, tarehe aliyofariki ni siku ya upingaji wa madawa ya kulevya Dunia ambayo yeye ndie alikuwa miongoni mwa Vijana ambao wanapinga matumizi ya madawa hayo

Kimsingi msiba ule ulikuwa ni pigo kubwa sana kwa wanajamii wote na hasa vijana tulio katika mapambano ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotukabili katika maisha yetu.

Mazishi ya mwanadada huyo chipukizi na jasiri katika kuwakomboa Vijana na makundi mengine yaliyopembezoni yalifanyika katika kijiji cha Lupembe,wilayani Njombe katika mkoa wa Iringa zamani.

Katika maombolezo ya Mbunge huyo ilithibitika pasipo na shaka hata chembe kwamba alikuwa anakubalika na watu wengi na ni mtu wa watu ,na kwa kweli ujasiri aliouonyesha katika kipindi kifupi alichofanya kazi akiwa Mbunge,kilithibitisha kuwa jamii ilimkubali.

Pamoja na umri wake mdogo (26) akiwa Mbunge wa Viti Maalum na aliyekaa Bungeni kwa kipindi cha miezi kumi na nane (18),habari za msiba wake na namna watu walivyouomboleza ni mambo yaliyoonyesha dhahiri njia bora inayowafaa wabunge na viongozi wetu kutimiza wajibu wao

Kujitokeza kwa watu wenye hadhi ya juu kabisa kitaifa na kimataifa katika mazishi yake na wingi wa wananchi wa kada mbalimbali nyumbani kwa baba yake Mikocheni na huko Njombe ambako yalifanyika mazishi yake, ni ushahidi unatuonesha kuwa dada huyu alikuwa mpiganaji wa kweli katika mambo mazito ambapo kifo chake kilipaswa kuguswa na wengi hususani vijana.

Ingawa imekuwa ni desturi kwetu kuwaenzi watu waliokufa hata wakati mwingine kwa wale ambao hawastahili sifa tunazowapa, lakini kwa Amina hali hiyo ni tofauti kabisa, kwani kila sifa ambayo amekuwa akipewa imekuwa ni sehemu ya mambo ya msingi aliyoyafanya na wananchi wakasikia au kushuhudia kwa macho yao

Hakika kifo cha Amina Chifupa kiliibua mambo mengi sana , wapo waliohusisha kifo chake na siasa kwa kuwa alitamani kuwa kiongozi wa juu katika umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UV-CCM).

Wapo waliofananisha kifo chake na cha Horace Kolimba ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa CCM ambapo aliwaambia wenzake waziwazi kuwa “CCM haina dira wala mwelekeo” lakini hawakumwelewa, na wakamwita Dodoma ajieleze kwenye kikao maalumu, alipowapatia maelezo, ghafla tukasikia Kolimba amefariki dunia.

Wengine walithubutu kukifananisha kifo cha Amina Chifupa na cha Ipyana Malecele ambaye alikuwa ni mtoto wa kiongozi na Mbunge mkongwe hapa nchini John Malecele.

Ingawa mzee Malecele na mwenzake Hamis Chifupa walikana waziwazi kuwatuhumu Binadamu wenzetu kwamba ndio waliofanya vitendo vya kigaidi na kijasusi na kusababisha vifo kwa vijana hao

Ni katika mazingira tofauti walitoa kauli zao na kuwaasa watanzania waamini kuwa vifo hivyo vilitokana na mipango ya Mungu na kuwaomba watanzania wasihusishe vifo vya watoto wao na harakati za kisiasa.

Hata hivyo wapo waliohusisha kifo hicho na harakati zake za kupinga na kutaka kuwataja hadharani wauzaji na vigogo wa madawa ya kulevya hapa nchini, ndiyo maana wakasema kwa kuwa alihaidi kuwataja vigogo hao siku ya kupiga vita dawa za kulevya Duniani ambapo kimsingi inaadhimishwa Duniani kote Juni 26 ndiyo maana wakawahi kumwondoa mapema kabla hajasema kitu siku husika.

Lakini kuna baadhi ya watu wamefananisha kifo chake na cha Princess Diana wa Uingereza. Kwa sababu Diana alikufa katika umri mdogo wa miaka 36 na alipendwa na watu wengi na wenye nyadhifa mbalimbali

Diana na Amina maisha yao yalikatishwa ghafla na kuwaacha watu wakiwahitaji katika kuchangia maendeleo katika jamii zao na kutufanya tudondoshe machozi katika kuwaomboleza.

Hata hivyo watanzania wasingeweza kufanya makosa pale wanafananisha kifo cha Amina na cha Ipyana, kijana mdogo ambaye kama alivyokuwa Amina alikuwa ameanza harakati za kuwania uongozi wa juu ndani ya UVCCM, wote wawili walikutwa na janga na baadaye walipotea katika mazingira yenye utata na kigugumizi wakiwa wanahitajika katika harakati husika.

Lakini kimsingi katika kumkumbuka Amina chifupa tunapaswa kutambua kuwa kila nafsi katika ulimwengu huu itaonja mauti, ingawa kila mja kabla hajaumbwa, mwenyezi mungu alimjua na kumtaka atimize wajibu wake kama kiumbe hai.
Natambua na kuamini kila mtu ana sababu zake za kuumbwa na kuwekwa katika ulimwengu na ana wajibu stahiki ambao amelazimika kuja kuutimiza hapa Duniani.

Hii haimaanishi kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake kikamilifu, ingawa wajibu huo tumepewa na muumba wetu kuja kuutimiza kwa kutumia utashi wetu ulio kamilifu.

Kwa muda mfupi alioishi Amina Chifupa alipokuwa Bungeni amedhihirisha jinsi alivyotimiza wajibu wake, ameweza kuwa chachu kwa kuibua mambo mazito ambayo yalitoa cheche kali na kuzua mijadala mikali ndani na nje ya Bunge la tisa.

Akiwa kijana mtanzania na kwa kuzingatia majukumu yake aliweza kutimiza wajibu wake ipasavyo kama Mbunge na Mwakilishi wa Vijana, ni ukweli uliowazi kuwa tunapaswa kuziendeleza juhudi alizoziacha .

Naamini alipokuwa Bungeni hoja alizoibua na jinsi zilivyokuwa na hamasa na kuweza kufufua matumaini ya wengi na kukuza hadhi ya vijana wenye nia ya dhati katika kupigania nchi yao , ndiyo kilichonifanya niendelee kumkumbuka na kumuenzi daima leo akiwa ametimiza miaka 6 toka atutoke

Hicho ndicho haswa kilichofanya kifo chake kumshtua kila mtu bila kujali rika awe aliyekuwa anamfahamu vizuri marehemu aula. Kwa sababu ni miongoni mwa waheshimiwa waliokuwa na nia thabiti ya kurejesha hadhi ya Bunge na kufanya litimize wajibu wake.

Kwani alitambua kuwa cheo ni dhamana na kwamba uheshimiwa aliopewa ulikuwa unamaanisha utumishi kwa wananchi na kuzingatia kundi alilopaswa kulitumikia kikamilifu ambalo ndilo lililompa dhamana (Vijana).

Kwa nguvu zake zote aliamua kutoa mchango wake ili kuwezesha vita dhidi ya madawa ya kulevya ishinde, kwa kuwa madawa ya kulevya yanaangamiza vijana wengi wa nchi hii ambao yeye alikuwa na wajibu wa moja kwa moja wa kuwatetea.

Sina hakika kama kuna mtanzania mwenye akili timamu anaweza kubisha kwamba Amina Chifupa alikuwa nuru ya matumaini kwa vijana na harakati zetu za kujiletea maendeleo.

Ni ukweli kuwa Taifa lolote Duniani haliwezi kuwa imara kiuchumi ,kisiasa, kiutamaduni na kijamii katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi bila kundi kubwa la vijana kulitengenezea mazingara ya kujikomboa.

Katika ulimwengu asilimia kubwa ni vijana na ndio viongozi wa leo na kesho na nguvu yao inategemewa sana katika jamii zetu.

Ndio maana mwanaharakati wa Vijana marehemu Amina Chifupa alijikita zaidi katika kutukomboa katika changamoto mbalimbali zinazotukabili ili atuoneshe njia stahiki na katika ustawi imara.

Hakuna ubishi kuwa Vijana ndio tumaini pekee la Taifa letu, kwaniTaifa lisilokuwa na vijana wazalendo na walio tayari kutetea taifa lao kwa gharama yoyote. basi nashawishika kuamini taifa hilo limepoteza mwelekeo (dira) na lipo hatarini.

Katika harakati za kuwakomboa Vijana na kupinga maovu naamini Amina Chifupa amekufa kifo cha kishujaa na ametutangulia mbele ya haki baada ya kutimiza baadhi ya wajibu wake
Mashujaa wapo wengi ambao wameshafariki ila kimsingi kila shujaa ameondoka akiwa na sifa zilizomfanya atambulike na aheshimike katika jamii iliyokuwa inamzunguka.

Mara nyingi shujaa hufikia hatua hiyo kutokana na ujasiri wake, uwezo wa kufikiri, kubuni,busara na pengine kujitoa kafara katika kuokoa watu wengine ambao kimsingi wamepotea

Ushujaa haupatikani kirahisi, mara nyingi mtu ambaye anaveshwa cheo cha ushujaa ni lazima akumbwe na vizingiti vingi (Maadui)ili afikie lengo husika la ukombozi na zawadi

Mwanaharakati Amina Chifupa alipata mapito magumu sana kimaisha katika safari yake hapa duniani na uwanaharakati wake kiujumla..Ingawa kifo chake kimeacha gumzo kubwa katika fikra za vijana.

Mwanaharakati huyu alikuwa tayari kufa akiongozwa na nanga ya kijasiri ya kusema ukweli na uwekaji wa mambo mengi bayana kwa kuipenda nchi yake na hasa jamii ya Vijana kwa kuyavalia njuga mambo mazito ambayo kimsingi yanaharibu maisha ya vijana.

Alitumia muda mfupi ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuonyesha uwezo na ujasiri mkubwa, kuwa Vijana wa leo wakipewa majukumu mazito wanaweza kufanya vizuri na wanastahili kupata dhamana hiyo.

Ni dhahiri kuwa Amina ni shujaa kwa kuwa kifo chake ni kielelezo kwa Vijana kuwa wakati wote tupo tayari kufa kwa ajili ya kutetea nchi yetu na kupambana na ufisadi ambao unalenga kuipeleka nchi mahali pabaya na kuharibu malengo ya vijana na Taifa kiujumla

Ni wazi kuwa katika harakati za Amina Chifupa za kusema na kudhamiria kufichua maovu alikuwa akizungukwa na maadui wa ndani na nje na pengine wengi ni wale wa nchi za nje ambao nia yao kuitumia nchi hii kama dampo la kuzalisha vijana matahira kutokana na Dawa za kulevya.

Maadui hao nia yao ni kuhakikisha kizazi chote cha Vijana kama Amina Chifupa kinaathirika na dawa za kulevya ili nchi hii iweze kutawaliwa kirahisi baada ya kuziharibu bongo zote za Vijana makini na wasomi ambao wanashawishika kutumia dawa za kulevya.

Jambo muhimu kwa sasa ni wajibu wa kuiga na kuendeleza mapambano dhidi ya dhuruma na masuala yote aliyopigania Mwanasiasa huyu, viongozi wetu wanao wajibu wa kutumia fikra za Amina kwa kuwa bado zinaishi kusahihisha makosa wanayofanya ambayo wamekuwa wakiambiwa mara kadhaa na makundi mbalimbali ya jamii lakini kwa makusudi wanayapuuza.

Uwakilishi wa Amina Chifupa haukuishia kuchangia mijadala Bungeni tu, bali tulimsikia na kumwona akifanya shughuli nyingine mbalimbali za kijamii,kwani aliwatembelea vijana na watoto wenye matatizo mbalimbali na kuwafariji na kuwapa misaada mbalimbali

Hivyo Vijana ndio tunatakiwa kuwa mstari wa mbele kwa kumuenzi Amina Chifupa na kuhakikisha kuwa Nchi hii haiendi mrama, ni vyema tukadhihirisha kumuenzi Amina Chifupa kwa vitendo vyetu, kwa kuwa tumeachiwa changamoto nyingi tunapaswa kuzitatua na kuweka mambo sawa katika harakati zetu za kujikomboa

Pamoja na kumkumbuka Amina ni vyema Vijana na wanajamii tukajiuliza tumejifunza nini kutoka kwake? Nani mtetezi wa Vijana aliyebaki Bungeni? Ni Zitto Kabwe, Dk Emmanuel Nchimbi , Deo Filikunjombe, Livingston Lusinde, Joshua Nassari, John Mnyika, Ester Bulaya au Waziri Mwenye dhamana ya Vijana?

Ni kweli kuwa Amina Chifupa hatunae tena katika ulimwengu huu, amefariki dunia, amelala na hatutamwona tena katika maisha haya ,lakini kauli na fikra zake zipo na zitaishi milele na itakuwa pumzi katika kizazi hiki na kijacho.

Amina tunakukumbuka na kukuenzi kwa yale yote uliyotuachia na tutashirikiana vyema na Mzee Hamis Chifupa kutoa mchango wetu katika taasisi yako ya Amina Chifupa Foundation ambayo ipo chini ya Mkurungezi Mzee Hamis Chifupa na ni jambo jema kuwa taasisi yako tayari imesajiriwa na Serikali na enaendelea kutimiza wajibu wake wa kusajiriwa

Kama mwenyezi mungu alivyotoa ndivyo alivyotwaa, Vijana sote tulikupenda na tutaendeleza juhudi zako ulizoziacha , sisi kama waja hatuna budi kumshukuru kwa kila jambo Mwenyezi mungu atupe faraja na busara katika kukabiliana na changamoto zinazotukabili watanzania wote.

Mheshimiwa Amina Chifupa uiombee nchi yako ili mafisadi wasiendele kuwaua kila kukicha eti kwa sababu za harakati ambazo wewe uliziasisi na watanzania wengine wasio na hatia ambao wanakosa Raslimali stahiki kwa sababu mafisadi wamezimaliza maliasili hizo kwa kuibia. Tunatambua kuwa wewe mbele sisi nyuma. Mungu Baba aipumzishe Roho yako katika mahali pa faraja na amani , Ameni.

Mwandishi wa Makala hii

Anapatikana kwenye, www.stephanomango.blogspot.com

Simu namba,0755 -0715 -0784 ,33 50 51