DKT Emmanuel Nchimbi aliyeshika kipaza sauti
Charles Mhagama Diwani wa Kata ya Matogoro ambaye anadaiwa kuwa Chaguo la Dkt Nchimbi katika nafasi ya UMEYA
Na Gideon Mwakanosya,Songea
SAKATA la uchaguzi wa Meya Mjini Songea Mkoani Ruvuma lililopelekea kupitishwa kwa Charles Mhagama kuwa Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa utata mkubwa limezidi kuchukua sura mpya ambapo baadhi ya madiwani wa CCM wameanza kususia vikao vinavyoitishwa na Chama chao wilayani humo.
Ikumbukwe hivi karibuni katika Manispaa hiyo kulifanyika uchaguzi wa Meya wa Manispaa hiyo ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Meya aliyefariki miezi michache iliyopita marehemu Ally Manya.
Lakini kabla sijachambua kwa ufupi na kuchambua jinsi mkutano huo ulivyokuwa nieleze jinsi mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM ulivyokuwa na jinsi ulivyotawaliwa na mizengwe ya kila namna.
Baada ya kutangazwa uchaguzi wa kura za maoni ndani ya CCM madiwani wanane na kada mmoja wa Chama hicho walichukua fomu za kuomba kuteuliwa na Chama hicho ili mmoja kati yao agombee nafasi hiyo akichuana na mgombea atakayechaguliwa na Chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA).
Licha ya Nchimbi kuhojiwa na Mwandishi wa makala hii kama alikuwa akimtaka Meya aliyepitishwa kwa kupindua matokeo Charles Mhagama lakini habari zilivuja baada ya habari kusambaa kuwa alisambaza meseji za simu zikitaka madiwani wapitishe Mhagama kuwa Meya wa Manispaa ya Songea.
Madiwani na makada wa Chama hicho walionya tabia ya Nchimbi kuwachagulia kiongozi anayemtaka yeye ili afuate matakwa yake lakini Nchimbi alikanusha uvumi wa habari hizo zilizoenea katika viunga vya Mji wa Songea na kuthibitisha kuwa zilikuwa na chembe ya ukweli fulani.
Kiongozi mmoja wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Songea ameuambia mtandao huu wa www.stephano mango.blogspot.com kuwa Nchimbi alibanwa kwenye kikao cha kamati ya siasa kilichofanyika Septemba 25 mwaka huu kuwa yeye ndiye aliyesababisha vurugu zilizotokea kwenye uchaguzi wa Meya uliofanyika kwenye Ukumbi wa SACCOS ya Manispaa 23 Septemba kwa kulazimisha mtu anayemtaka kuwa ndiye awe Meya.
Mmoja wa Madiwani machachari wa Chama hicho Manispaa ya Songea ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema madiwani walibanwa kwenye vikao vya Chama hicho ili wachague diwani huyo asiyekubalika kuwa ndiye agombee Umeya na vikao vya Chama hicho vikapendekeza jina lake na majina ya madiwani wawili wanawake na kuyakata majina ya madiwani wanaokubalika.
Majina yaliyopitishwa na vikao vya Chama hicho ili wakapigiwe kura na madiwani wa CCM ni Mariam Dizumba,Genifrida Haule na Charles Mhagama na katika uchaguzi wao wa CCM walibanwa ili wamchague Mhagama ili apeperushe bendera ya CCM’anasema diwani huyo’.Anasema kuwa Mariam Dizumba ambaye pia ni mke wa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Mjini Hemedi Dizumba hata kura yake mwenyewe alijinyima hivyo aliambulia sifuri.
Anasema kuwa kwa kumuonyeshea au kumkomoa Nchimbi wakaamua kumpigia kura diwani huyo ili wakamuumbue kwenye uchaguzi wa jumla ambao ungevipambanisha Chadema na CCM kwa kumpigia kura za hapana au maarufu kwa kura za maruhani.
Hata hivyo Katibu wa CCM Songea mjini Alphonce Siwale alipoulizwa kuhusiana na ushawishi wa Nchimbi wa kumtaka Mhagama awe Meya alisema kama alituma ujumbe wa simu wa kuwataka madiwani wa CCM kumchagua diwani huyo alisema alifanya hivyo kwa ushawishi wake binafsi.
Katika uchaguzi uliofanyika 23 Septemba mwaka huu Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) hakikusimamisha mgombea hivyo kukatokea majadiliano ni jinsi gani uchaguzi utakuwa huru na wa haki kwa kuwa Chadema hawakusimamisha mgombea.
Kutokana na hali hiyo ndipo Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Nachoa Zakaria ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo alisimama na kutoa ufafanuzi wa kanuni za uchaguzi wa nafasi hiyo na kusema wanatakiwa kupiga kura za ndiyo kama wanamtaka mgombea huyo na ikiwa hawamtaki basi wanatakiwa kupiga kura za hapana.
Sipendi nirudie yale yaliyoandikwa na wenzagu lakini napenda kujadili muktadha mzima uliozunguka tukio hilo na ni nani alisababisha kama vile Chemsha bongo ya yai na kifaranga cha kuku nini kilianza.
Katika uchaguzi huo ni wazi kabisa kanuni zilivunjwa baada ya kubainika kuwa Charles Mhagama alipigiwa kura za Hapana 14 na za ndiyo 12 na waswahili husema kwa nini tuandikie mate wakati wino upo?hivyo basi kama uchaguzi ule ulikuwa huru na wa haki na kanuni hazikuvunjwa basi kura zingehesabiwa tena kabla ya Naibu Meya kuiba kura na kuziweka kwenye kipima joto chake kidogo na kukificha sehemu zake za siri.
Baada ya kupigwa kura na kuhesabiwa hadharani Msimamizi wa uchaguzi Nachoa alimwonyesha matokea Dizumba ndipo alipotaka kusoma alionyesha mstuko mbele ya madiwani na kumuonyesha Nchimbi ambaye alimuamuru kuyasoma kwa kuyapindua na alipoyasoma madiwani wakataka kura zirudiwe kuhesabiwa kwa madai alichokitangaza hakikuwa na ukweli.
Hapo ndipo kulitokea vurumai kubwa na ndipo Naibu Meya huyo alipopigwa mtama na diwani wa Kata ya Mjini kupitia Chadema Joseph Fuime na kuanguka chini kisha kuinuka kukimbilia nje na kura alizokwapua na hapo ndipo diwani huyo alipomwendea Nchimbi na kumwambia ni aibu kwake kusimamia wizi wa kura.
‘Ni aibu kubwa kwa Waziri kama wewe kusimamia wizi wa kura na hapa huwezi kunifanya chochote kwa kuwa Uwaziri wako ni nje ya ukumbi huu na tukiwa ndani humu wewe ni diwani kama mimi na utambue kuwa Songea wamechoka na tabia yako ya kuwachagulia viongozi’alisema diwani huyo huku akiwa amemkodolea macho Nchimbi ambaye alikuwa akinon’gonezana jambo na diwani wa Matarawe James Makene.
Wakati akitoka nje ndipo alipopokewa na watu waliokuwa nje ya ukumbi huo ambao walikuwa wakimwimbia Nchimbi mwizi wetu na yeye alionekana akizungukazunguka akichezea simu asijue la kufanya hadi pale alipokuja dereva wake na gari na kumpakia na kisha kuondoka eneo hilo ambalo lilikuwa lina vurumai kubwa.
Baada ya Naibu Meya kutoka nje ya ukumbi alikimbilia kwenye gari moja na kuingia huku akifuatwa na madiwani wawili wa Chadema ambao walikuwa wakimzuia asikimbie na kura,katika sakata hilo Kada wa CCM Hamis Abdalah Ally alitaka kumgonga na gari diwani wa Mfaranyaki(CHADEMA) Salumu Mfamaji ambaye alikuwa mbele ya gari hiyo.Kada huyo wa CCM alifanikiwe kumkimbiza Naibu Meya huyo ili asiweze kupigwa.
Baada ya tukio hilo maneno yalizagaa mitaani kwamba Nchimbi ametishia kuwanyang’anya kadi madiwani saba wanaodaiwa kupiga kura za hapana dhidi ya mgombea pekee wa Chama chake,jambo ambalo lilijadiliwa na wachunguzi wa masuala ya siasa kwamba wanawezaje kuwanyang’anya kadi madiwani hao wakati kura ni siri ya mtu na wao wamewajuaje?.
Siku ya pili baada ya tukio hilo Nchimbi ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Songea Mjini na Waziri wa habari utamaduni na michezo alipigiwa simu na mwandishi wa habari wa Gazeti la Majira Joseph Mwambije ili kutaka kujua kama kweli aliwatisha madiwani hao kuwanya’nganya kadi alisema hawezi kufanya hivyo kwa kuwa kanuni na taratibu za Chama hicho anazijua.
Lakini pia alisema kuwa waandishi ni wajinga na wapumbavu kwa kuwa wameandika habari za uongo kuwa yeye amekimbia na sanduku la kura.
Septemba 25 mwaka huu aliitisha mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea na kutoa tamko la kukanusha kuwa yeye hakukimbia na sanduku la kura akiyatuhumu magazeti matatu ya kila siku kwa kumuandika habari za kumchafulia jina.
Ama kwa hakika Nchimbi amechanganyikiwa na tukio lile limemchanganya pengine na kupunguza kasi yake ya mbio za Urais wa mwaka 2015 kwani yeye katika tamko lake anayatuhumu magazeti yaliyoandika habari hiyo Septemba 23 lakini ukweli ni kwamba siku hiyo ndiyo kilifanyika kikao cha Baraza la madiwani na hakuna gazeti lililoandika habari hiyo siku hiyo bali magazeti yaliripoti habari za tukio hilo Septemba 24 mwaka huu.
Harakati za Waziri huyo kijana kukanusha tuhuma hizo zitaishia kumuumbua zaidi ikiwa picha za video zitaonyeshwa kwenye halaiki ya watu kwa kuwa yeye Nchimbi anasema hakuna diwani aliyetoka nje ya ukumbi huo na kura lakini kama hakuna diwani aliyetoka nje ya ukumbi na kura,Mariam Dizumba kwa nini alitoka ndani ya ukumbi akikimbia na kwanini alipigwa ngwala na kudondoka na kwa nini aliondoka wakati kikao hakijafungwa?
Pia katika tamko lake anasema Meya aliyechaguliwa alifunga mkutano lakini ukweli ni kwamba mkutano au kikao hicho hakikufungwa hivyo kiliparaganyika baada ya utaratibu mzima na kanuni za uchaguzi huo kuvurugwa kwa kuwa aliyetakiwa kutangaza matokeo hayo ni Mkurugenzi wa Manispaa na si Naibu Meya ambaye ni mpigakura kwenye uchaguzi huo na pia ana maslahi.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanahoji ni kwa nini CCM Songea Mjini imetoa mapendekezo ya kuwafukuza uanachama madiwani watano kati ya saba waliopiga kura za hapana dhidi ya Mhagama wakati mwaka 2007 hawakumchukulia hatua Mariam Dizumba ambaye alipiga kura ya hapana kwa Elizabeti Ngongi ambaye alishinda unaibu meya kwenye uchaguzi wa mwaka huo na akaenda mahakamani kuzuia uchaguzi huo.
Katika sakata la mwaka huo Manispaa hiyo ilikaa bila Naibu Meya kwa miezi mitano hadi pale nafasi hiyo alipopewa Mariam Dizumba ambaye alishindwa na ndipo akaamua kufuta kesi sasa madiwani hao watano na huyu aliyekishtaki Chama chake,Mkurugenzi na Elizabeti Ngongi yupi mwenye kosa kubwa?
Anaendelea kusema katika tamko lake’mkutano huu wa madiwani ulirekodiwa kwa picha za video,mikanda ya picha hizo ipo inaweza kupatikana kwa ushahidi’anasema.Lakini picha hizo za video zinaonyesha akizomewa kwa kuitwa mwizi wa kura na huku akielezwa kuwa ni aibu kwake kusimamia wizi wa kura na kama alionyeshwa picha hizo basi alionyeshwa sehemu tu ya picha za tukio.
Lakini ni katika mkutano huo ndipo alipobanwa na waandishi wa habari athibitishe ujinga na upumbavu wao na ikiwa atashindwa kufanya hivyo afute kauli yake na atoe ufafanuzi kuhusu madai yake kwamba habari hizo zimeandikwa na mtu mmoja na kwamba katika tukio hilo amemdhalilisha Rais kwa nini asijiuzulu kwa kumdhalilisha Rais aliyemteua?
Nchimbi alishindwa kuyajibu maswali hayo na kupandwa na jazba na kutoa maelezo ambayo hayahusiani na maswali aliyoulizwa na kushusha heshima yake.
Wakati hali ikiwa hivyo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na maendeleo(CHADEMA)Mkoa wa Ruvuma Joseph Fuime anasema kuwa kwa tukio lile ingekuwa enzi ya Mwalimu Nyerere Nchimbi angejiuzulu.
Akihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Shule ya msingi mfaranyaki maarufu kama Soko la samaki Fuime alisema ni aibu kwa Manispaa ya Songea ambayo ni maskini kumchagua Meya aliyedai kuwa ni mwizi aliyehusika na uuzaji wa greda kwa shilingi milioni 18, na ununuzi wa gari bovu la Zimamoto kwa shilingi milioni 350 ambapo Mhagama alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo alisema greda liliuzwa kwa kufuata sheria zote na kuhusu gari bovu la Zimamoto halimuhusu kwani magari hayo yalinunuliwa saba Nchi nzima.
Alisema huo ni mpango wa wabunge kuwaweka watu wao kwenye nafasi za uongozi ili waibe fedha na kwamba walifanya makosa kumchagua Nchimbi na wangemchagua aliyekuwa mgombea wa Chadema Edson Mbogoro asingewaletea Meya mwizi.’Anamtaka Meya huyo ili ajinufaishe na mimi nasema Charles Mhagama atakuwa Meya wa Mbunge si wa madiwani na akipita mitaani mumzomee Meya huyo’alisema.
Alisema hiyo ni aibu kwa Rais aliyemteua na kwamba Chama Chake kimejipanga kuzunguka kata zote 21 kueleza ubaya wa Nchimbi na mwenendo mzima wa uchaguzi wa Meya na kueleza kuwa Manispaa hiyo haina Meya hivyo baada ya mikutano hiyo watafanya maandamano makubwa ya kupinga uchaguzi huo na kumpinga Meya huyo na kuvigeuza viwanja vya manipsaa hiyo kuwa Tahariri Squere ambavyo vilim’ngoa madarakani aliyekuwa Rais wa Misri Hosni Mubarak.
Hivyo basi ili kunusuru vurugu zitakazotokea kwenye maandamano yanayotarajiwa kufanyika ni wazi basi inatakiwa kurudia uchaguzi kwa kuwa uchaguzi uliofanyika ulikiuka utaratibu na CCM wana wasiwasi gani kurudia uchaguzi?Hapa ndipo Intelejensia ya Polisi inapaswa kufanya kazi kunusuru hali ya hewa ili yasije yakatokea mauaji kama yale yaliyotokea Arusha.
Mapendekezo ya CCM Wilaya ya Songea kufukuza madiwani waliopiga kura za hapana kwa mgombea wa Chama hicho yamepokelewa na Chama hicho Mkoa wa Ruvuma ili yaweze kutolewa maamuzi na Katibu wa Chama hicho Mkoa huo Emmanuel Mteming'ombe amesema Kamati ya maadili ya Chama hicho imewahoji madiwani hao ambao anasema kwenye Kamati ya siasa Wilaya hawakusikilizwa na kamati ya siasa Mkoa itatoa uamuzi wa kuwafukuza au kutowafukuza.
Hata hivyo wachunguzi wa mambo wa siasa wanasema madiwani hao hawatafukuzwa na kamati hiyo kwa kuwa ni kiongozi mmoja pekee na genge lake ndiye anayeshinikiza wafukuzwe na kwamba hawajafanya kosa linalofanya wafukuzwe na ikiwa watafukuzwa kwa upepo wa siasa Songea upande wa chama hicho si mzuri na kata hizo zinaweza kudondokea upinzani.
Hivi karibuni CCM Wilaya ya Songea mjini iliitisha kikao na madiwani wake kwa ajili ya kusafisha hali ya kisiasa ambayo imechafuka lakini hakikuweza kufanyika kutokana na madiwani kukisusia kwa kile kinachodaiwa kuwa ni mgomo wa kudumu kushinikiza kujiuzulu kwa Meya huyo anayedaiwa kupitishwa kwa mizengwe huku nguvu ya kigogo mmoja ikitajwa kuhusika.
Lakini pia katika kikao hicho madiwani waliopendekezwa kufukuzwa waliitwa na walifika wakiwa na kadi zao mfukoni tayari kwa kuzikabidhi ikiwa wataambiwa watoke kwenye Chama hicho.
Katibu wa CCM wa Wilaya ya Songea mijini Alphonce Siwale alipohojiwa kuhusu kuitishwa kwa kikao hicho alithibitisha kukiitisha na kusema kuwa kilishindikana kufanyika kutokana na mahudhurio hafifu ya madiwani ambao hawakufika hata nusu.
Alisema kuwa madiwani wengi walishindwa kuhudhuria kikao hicho kwa kuwa walikuwa safarini na kwamba kitafanyika tena kitakapopangwa na kilipaswa kusafisha hali ya hewa iliyochafuka kutokana na uchaguzi wa Meya.
Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa anapaswa kumuondoa Nchimbi kwenye nafasi ya Uwaziri wa habari,utamaduni na michezo kwani kwa tukio lile alimdhalilisha na aibu ile itamfuata Nchimbi kokote atakakokwenda iwe Dares salaam,Dodoma,Mbeya na Songea hivyo basi aibu ya Nchimbi ni aibu ya Kikwete aliyemteua.
MWISHO