Wednesday, August 15, 2012
MADHEHEBU YA KIKRISTO WAITAKA SERIKALI KUZUIA VIBALI VYA MIHADHARA NCHINI
Na Steven Augustino, Tunduru
VIONGOZI wa madhehebu ya Dini Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma wameiomba serikali kuingilia kati na kuzuia vibali vya Mihadhara na makongamano ya kidini yanayo chochea na kukashifu imani za madhehebu mengeni zikiwa ni juhudi za kulinda amani ya nchi yetu.
Wito huo umetolewa na Ujumbe wa Viongozi wa Madhehebu ya dini za kikristo wilayani humo wakati wakiongea na Mkuu wa Wilaya hiyo Chande Nalicho katika kikao kilicho fanyika katika Ukumbi wa mapumziko ya Ikulu ndogo mjini hapa.
Wakifafanua taarifa hiyo kwa nyakati tofauti, mwenyekiti wa viongozi wa madhehebu hayo Fr. Mathias Nkhoma wa kanisa la Anglikana, fr. Bosco Chinguile wa kanisa katoliki na Mchungaji Mwanja Mangoni wa kanisa la Bibilia walisema kuwa mtindo wa serikali kuachilia vitendo vya
Mihadhara inayo kashfu madhehebu ya Dini zingine kinaweza kuhahatarisha tunu ya amani yetu.
Walisema ili kudhibiti hali hiyo inafaa sasa vyombo vya usalama kuanza kuchukua hatua za kisheria kwa watu ambao wamekuwa wakitumia majukwaa ya mihadhara, mikutano na makongamano ya kidini kuwachochea chuki waumini wa dini nyingine zikiwa ni juhudi za Serikali kulinda amani hiyo inayotishiwa kutoweka miongoni mwa wananchi wake kwa chuki za
mwamvuli wa itikadi za kidini.
Nao Mchungaji kiongozi wa kanisa la biblia Tanzania Hosea Lupondo, Rev.Stephano Milinga wa Kanisa la Pentekoste, Rev. Mussa Mandingo wa kanisa la Upendo, Rev. Helman Ponera (EAGT), Rev. Emmanuel Kanduru (TAG) na Mch.Anderson Kasembe wa CAG Church walisema kuwa kauli hiyo wameitoa kufuatia uwajibikaji mdogo wa Serikali udhaifu uliotumiwa na baadhi ya viongozi wa Dini nyingine kusambaza madukani na mitaani Kanda, CD na DVD zinazo kashfu dini nyingine hasa zinazo chokonoa Ukristo.
Walisema wanaposoma alama za nyakati wanagundua kuwepo kwa viashiria vya kuzuka kwa uvunjifu wa amani hasa pale dini nyingine inapo tumia uzembe wa usimamizi wa sheria na kuacha waumini hao kutamba na kutumia lugha za kuudhi hasa pale wanapofikia hatua za kugusa waziwazi vipengele nyeti vya imani za waumini wa kikristo kuwa hailengi kuwepo
kwa mahusiano miongoni mwao.
Katika taarifa hiyo viongozi hao walibainisha baadhi ya maneno nyeti ambayo yamekuwa yakisemwa mara kwa mara na viongozi wa Dini nyingine kuwa ni pamoja na “ Yesu ni Mwislamu, makafiri wa kwanza ni Wakristo, Ukristo umeenzishwa na Paulo, Wakristo ndio wanaoruhusu ndoa za jinsia moja, wakristo ndio freemason na mengine mengi kama kivutio kwa waumi wake, na wakapendekeza kwa kuyataka madhehebu hayo kutumia majukwaa
hayo kueneza uzuri wa Dini yao kwa kutumia Vitabu vyake ili kuwavutia waumini wake.
Viongozi wengine waliokemea uchochezi huo kwa dini za kikrsto na majina ya makanisa yao kwenye mabano ni Mch. Geofrey Japhet (Tabernacle), Rev. Madaraka Bukuku, ( Moravian) Mch. Gerod Makota (F.G.B.F) na Mch.Yotham Mtanga wa KKKT ambao pamoja na mambo mengine waliahidi kutoa ushirikiano kwa kuwahamasisha waumini wao kushiriki
kikamilifu katika mazoezi ya Sensa na utoaji wa maoni yatakayo tumika wakati wa kuandika katiba mpya.
Awali akisoma taarifa ya Viongozi hao Katibu wa Ujumbe wa Viongozi hao Fr.Dominic Mkapa alisema kuwa maamuzi hayo yalipitishwa na waumini wa Kikristo yaliyotolewa katika kongamano la pamoja la kutathimini hali ya vitendo hivyo lililofanyika katika Viwanja vya kanisa la Biblia Tanzani Agosti 10 mwaka huu na kubaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali na kutoa mapendekezo hayo kuwa ni njia bora ya kuleta ustawi na maendeleo kwa watu wote.
Akiongea katika mkutano huo Mkuu wa Wilaya hiyo Chande Nalicho pamoja na kukiri kuwepo kwa vitendo hivyo aliahidi kutoa ushirikiano kwa viongozi hao na kuahidi kuzifanyia kazi kero hizo kwa kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Mwisho
Subscribe to:
Posts (Atom)