About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Thursday, June 7, 2012

MBATIA ATAKIWA KUPIMA UENYEKITI WAKE


Na Asha Bani

CHAMA cha Sauti ya Umma (SAU), kimemshukia Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia, kikidai kuwa anatumiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mwenyekiti wa SAU, Paul Kyara, alitoa kauli hiyo jana katika taarifa yake aliyoituma kwenye vyombo vya habari, akisema kuwa Mbatia anapaswa kuutafakari upya uenyekiti wake baada ya kukubali uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete kuwa mbunge.

Kauli ya Kyara inakuja siku mbili baada ya Katibu Mwenezi wa NCCR Mageuzi, Moses Machali, kumtaka Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (CHADEMA), kuomba radhi kutokana na matamshi yake kuwa uteuzi wa Mbatia ni dhahili anatumiwa na CCM.

Kyara alisema kauli ya Machali kama alitumwa na mwenyekiti wake, basi inalenga kuua upinzani na inaongeza ushahidi wa NCCR kutumiwa na CCM na pia kuharibu mahusiano mazuri yaliyowekwa baina ya chama hicho na CHADEMA hadi kufikia muafaka wa Mbatia kufuta kesi ya uchaguzi katika Jimbo la Kawe dhidi ya Halima Mdee.

“Kama Mbatia alifuta kesi hiyo bila hila ni bora akawa na hofu ya Mungu ili kuepuka vitisho na malumbano, ni vema akatazama upya athari za kukubali uteuzi wa Mwenyekiti wa CCM huku yeye akibakia kama Mwenyekiti wa NCCR,” alisema.
Kwa mujibu wa Kyara, hilo linaondoa uhuru wa kutoa mawazo ya kuipinga CCM na hata uwezekano wa wananchi kumwamini kama mpinzani wa kweli.

“Mimi ninamshauri Mbatia afikirie kuachia ngazi kwenye nafasi ya uenyekiti wa taifa kama ilivyokuwa kwa Juma Duni Haji alivyoondoka katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu CUF mara baada ya kuteuliwa kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema Kyara.

Alisema endapo Mbatia atafumbia macho jambo hilo, yatamkuta kama yaliyomkuta Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad, ambaye ameendelea na nafasi yake ya ukatibu mkuu wa CUF na kushindwa kuikosoa serikali na kukipotezea mwelekeo chama chake.
“Mbatia na chama chake wanatakiwa kumpongeza Wenje kwa kueleza ukweli maana kuendelea kupingana naye ni kupambana na nguvu ya umma,” alisisitiza.