Na Stephano Mango, Namtumbo
HALMASHAURI ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma ambayo ina shule 30 za Sekondari zikiwemo Shule 24 za Serikali na Shule za Binafsi 6 inakabiliwa na tatizo kubwa la upungufu wa Walimu wa masomo ya Sayansi na Lugha na kusababisha Wanafunzi wa Shule hizo kushindwa kumudu masomo ipasavyo wakiwa kwenye Shule hizo.
Akizungumza na Mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com jana Ofisini kwake Kaimu Afisa Elimu wa Shule za Sekondari wa Wilaya ya Namtumbo Lydia Herbert alisema kuwa Halmashauri hiyo yenye jumla ya Wanafunzi wa Sekondari 7871 wakiwemo wavulana 4671 na wasichana 3193 ina uhaba mkubwa wa walimu wa Masomo ya Sayansi na Lugha.
Herbert alisema kuwa mpaka sasa Halmashauri hiyo ina walimu 208 wa Shule za Sekondari ambao hawawezi kukidhi haja ya wanafunzi waliopo kwenye Shule za Sekondari Wilayani humo na kwamba kutokana na hali hiyo kuna upungufu wa walimu 32 wa masomo ya sayansi na lugha.
Alieleza zaidi kuwa hali ya miundo mbinu katika shule za Sekondari zilizopo katika Wilaya hiyo ilikuwa inahitajika kuwa na vyumba vya madarasa 285 lakini vyumba vya madarasa vilivyopo kwasasa ni 164 na kufanya kuwepo tatizo kubwa la vyumba vya madarasa kwenye Shule hizo.
Alibainisha zaidi kuwa katika Shule hizo za Sekondari Wilayani humo zinahitajika maabara 115 lakini maabara zilizopo ni 3 tatu ambazo zipo katika Shule mbili za binafsi na Shule moja ya Serikali na walimu wa Shule hizo wanakabiliwa na tatizo kubwa la nyumba za kuishi ambapo nyumba za walimu zinazohitajika ni 384 na nyumba zilizopo ni 84 tu ,.
Alisema katika Shule hizo za Sekondari Wilayani humo kuna changamoto kubwa zinazojitokeza mara kwa mara ambaapo ni utoro wa wanafunzi wa kike na wakiume uliokithiri na mimba za utotoni ambapo wanafunzi 22 walibainika kuwa ni wajawazito katika kipindi cha January hadi October mwaka huu.
Ameitaja mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto hizo kuwa ni kuwaelimisha wananchi wa Wilaya ya Namtumbo juu ya umuhimu wa elimu kupitia mikutano ya ndani na ya hadhara ili waweze kuelewa kuwa wazazi wa wanafunzi hao wanapaswa kuchangia ujenzi wa madarasa,madawati na kujenga nyumba z akuishi walimu.
Mikakati mingine ni kuboresha miundo mbinu ya Shule za Sekondari Wilayani humo ili kuwa na Mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia kwa kujenga nyumba za walimu,vyumba vya madarasa pamoja na maabara kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
Kaimu Afisa Elimu huyo Herbert ameiomba Serikali kupitia Wizara za Elimu Utamaduni na Ufundi na Wizara ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (TAMISEMI ) kuona umuhimu wa kuwaletea walimu wengi zaidi wa masomo ya sayansi ambao wataweza kuziba mapengo mengi ya walimu katika Shule za Sekondari Wilayani humo