About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Tuesday, November 1, 2011

AUAWA KWA MTWANGIO WA NAFAKA AKICHEZA MUZIKI UKUMBINI

                    Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda
Na Gideon Mwakanosya,Songea
MKAZI mmoja wa Kijiji cha Ruanda kilichopo katika Wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma Afred Milinga (27) amekufa papo hapo baada ya kupigwa kichwani na mchi wa kutwangia nafaka na Festo Mahundi (21) wakati wakiwa kwenye ukumbi wa starehe wakicheza disko.

Akizungumza na Mwandishi wa habari wa mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ Gideon Mwakanosya jana ofisini kwake Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma  Naftan Mantamba alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi usiku majira ya saa 2.30 huko kwenye ukumbi wa starehe kijijini hapo.

Alisema kuwa inadaiwa kuwa kabla ya tukio hilo Milinga aliondoka nyumbani kwake na alielekea kwenye kilabu cha pombe za kienyeji ambako baadae alikwenda kwenye ukumbi wa starehe na alifanikiwa kuingia ukumbini humo ambamo alimkuta Mahundi.

Alieleza zaidi kuwa wakiwa kwenye ukumbi huo walianza kuzozana kati ya milinga na Mahundi ambako Mahundi baadae alitoka nje ya ukumbi huo hadi kwenye nyumba ya jirani ambako alichukuwa mchi wa kutwangia nafaka kisha aliingia nao ukumbini na kumpiganao kichwani Milinga na kumsababishia kifo papo hapo.

Mantamba alisema kuwa baada ya kutokea kwa tukio hilo Mahundi alikimbia na kutokomea kusikojulikana lakini baada ya muda Polisi walipopata taarifa ya tukio hilo walifanikiwa kumkamata Mahundi akijiandaa kutaka kukimbia kuelekea kijiji cha Lituhi.

Hata hivyo Mantamba alieleza kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliotokea kati ya Milinga na Mahundi uliotokea kwenye ukumbi wa starehe ambako kulikuwa na disko na kwamba mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani mara tu upelelezi utakapo kamilika.

WANAFUNZI SEKONDARI WAANDAMA KUSHINIKIZA KUREJESHWA KWA MKUU WAO WA SHULE

                      Afisa Elimu Mkoa wa Ruvuma Paulina Mkonongo

Na Steven Chindiye,Tunduru
ZAIDI ya Wanafunzi 500 wa Shule ya Sekondari ya Kutwa Mataka wametishia kutoingia madarasani hadi uongozi wa Halmasahuri ya Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma watakapofanya mabadiliko ya kumrejesha Shuleni hapo aliyekuwa Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Johnes Liombo.

Msimamo huo umetolewa na wanafunzi hao wakati wakiongea na uongozi wa Halmashauri hiyo baada ya uongozi huo  kupokea maandamano ya  amani yaliyofanywa na wanafunzi hao kwa nia ya kupinga uhamisho wa mwalimu huyo.

Sambamba na msimamo huo wanafunzi hao, wakiwemo wanafunzi  wa kidato cha Pili wanaotarajia kufanya Mtihani wa Taifa hivi karibuni walidai kuwa endapo mgogoro huo hautapatiwa ufumbuzi mapema nao hawataingia katika chumba cha mtihani huo.

Akisoma taaria ya wanafunzi hao kaka Mkuu wa shule hiyo Rajab Said alisema kuwa wanafunzi hao wamechukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa uhamisho wa Mwalimu Liombo ambaye amekaa miezi mitatu katika Shule yao ni wa uonevu na kwamba kitendo hicho hakiitakii mema Shule yao.

Alisema mwl. Liombo  ni mwalimu wa msaada kutokana na tabia yake ya kujituma katika ufundishaji na kwamba wanafunzi  wote wanaamini kuwa endapo angeendelea kubakia katika shule hiyo wanafunzi wote wangepiga hatua kitaaluma.

Akijibu kero hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mwl. Rashid Mandoa ambaye alikuwa akisaidiwa na baadhi ya wakuu wa Idara mbalimbali na kuwaomba wanafunzi hao warudi shuleni kwa ajili ya kuendelea na masomo na kuwataka waliwataka wanafunzi hao kutokubali kutumiwa ama kufanya maandamano kwa maslahi ya watu.
“kweli nimeamini kuwa wanafunzi wa Mataka Sekondari hawana nidhamu” alisema Mwl. Mandoa na kuongeza  kuwa endapo wanafunzi hao wangekuwa na nidhamu walipaswa kufuata taratibu za kuonana na uongozi kwa kufuata taratibu zinazotakiwa na sio kufanya maandamano kama walivyo fanya.

Aidha Mwl.Mandoa aliwahakikishia wanafunzi hao kuwa uhamisho wa mwalimu Liyombo ni wa kawaida kama wanavyohamishwa watumishi wengine wa Halmashauri hiyo

Nae Afisa Elimu wa Shule za Sekondari wa Wilaya hiyo Mwl. Alli Mtamila katika maelezo yake pamoja na mambo mengine aliwataka wanafunzi hao kurejea Shuleni kwa madai kuwa idara yake inafuatilia tatizo hilo na kulitafutia ufumbuzi ombi ambalo lilikataliwa na wanafunzi hao na kuwafanya watawanyike kurejea majumbani mwao.  

Akiongea kwa niaba ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo Fadhili Makanjila alisema kuwa kitendo cha uhamisho huo kimewakatisha tamaa wazazi na wanafunzi kwa katika kipindi cha Mwalimu Liombo kulikuwa na mikakati mizuli ya kuiinua kitaaluma shule hiyo.

 Makanjila aliitaja miongoni mwa mikakati hiyo kuwa ni pamoja na Mkuu huyo kuwa na mipango shirikishi tofauti na walimu wengine na akatolea mfano mpango wa kuwaweka wanafunzi wa kidato cha pili katika KAMBI ambalo wanafunzi hao walikuwa wakipatiwa masomo ya ziada nyakati za usiku ikiwa ni mikakati ya kuwa andaa  na  mithani ijayo

WANACHAMA 130 WA NEW MUUNGANO SACCOS WAPATIWA ELIMU YA UJASILIAMALI NA USHIRIKA

Na Gideon Mwakanosya,Songea
CHAMA cha akiba na Mikopo cha New  Muungano SACCOS kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kimetoa mafunzo kwa wanachama wake 130 ya elimu ya ujasiliamali na elimu ya ushirika ili kuwasaidia wajasiliamali hao kufanya kazi kwa umahili zaidi.
Akifungua mafunzo hayo ya siku mbili Katibu wa New Muungano SACCOS  Biatha Komba kwenye ukumbi wa shule ya msingi Mfaranyaki alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwasaidia wanachama wake kujua elimu ya ushirika na ujasiliamali ili wanapokopa mikopo yao waitumie kwa matumizi sahihi kama walivyoomba.

Komba alisema kuwa pia wananchama wake ni lazima wajue sheria ,kanuni na misingi ya ushirika ili wanapofanya kazi zao za kila siku wasipatwe na usumbufu wa aina yeyote katika mitaji,na masoko kwa biashara wanazofanya.

Aliainisha changamoto ambazo zinaikabili chama hicho kuwa ni pamoja na mfumuko mkubwa wa taasisi zisizo rasmi za kifedha ambazo zimekuwa zikifanya kazi ya kukopesha wafanyabiashara na wafanyakazi wakiwemo walimu fedha, vitendea kazi vya kisasa kama kompyuta,fotokopi mashine pamoja na usafiri kwaajiri ya kuwafuata wanachama na kupeleka fedha benki.

Kwa upande wake Afisa Tawala wa Tarafa ya Songea Magharibi Blanka Luambano ambaye ndio alikuwa mgeni rasmi aliupongeza mradi wa SELF  kwa kuifadhiri SACCOS hiyo ambayo imeonekana kuwa ni msaada mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Songea.

Alisema kuwa New Muungano SACCOS ni miongoni mwa taasisi chache za fedha ambazo zimejikita zaidi katika kusaidia kuondoa umasikini kwa wafanyabiashara wadogo na kwamba kwa muda wote imekuwa ikiwahimiza wanachama wake kukopa fedha kwaajiri ya kukuza biashara zao wanazozifanya kila siku.

Semina hiyo ya siku mbili ambayo washiriki wake ni kutoka kata 13 zilizopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambayo imefadhiriwa mradi wa kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo (SELF) ambao uko chini ya Wizara ya fedha inatarajiwa kuwa na mada za uongozi wa utawala bora,ujasiliamali, sheria na kanuni za vyama vya ushirika

DC MJENGWA ACHARUKA UCHOMAJI MOTO OVYO WILAYANI MBINGA

                     Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Kanali Edmund Mjengwa
Na Cresencia Kapinga,Mbinga
SERIKALI wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma imeagiza kuwachukulia hatua kali za kisheria viongozi wa kijiji na kata wakiwamo Madiwani pamoja na makatibu tarafa ,ambao maeneo yao yatakumbwa na uchomwaji moto bila wahusika kuchukuliwa hatua yoyote.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Kanali Mstaafu Edmund Mjengwa kwenye kikao cha baraza la Madiwani  kilichofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa  jumba la maendeleo uliopo wilayani humo.

Kanali Mjengwa alisema kuwa ipo tabia ya viongozi kama vile Watendaji wa Vijiji na kata pamoja na Madiwani wao ambao wamekuwa wakiona matukio ya uchomaji moto kwenye maeneo yao lakini hakuna hatua wanazozichukuwa.

"Naagiza ya kwamba kuanzia sasa tukio la moto likitokea kijijini kwako na zisipochukuliwa hatua za kuuzima,viongozi wa eneo husika watakuwa wa kwanza kuchukuliwa hatua za kisheria vinginevyo muhusika afikishwe katika vyombo vya sheria ili sheria ichukuwe mkondo wake" alisema Kanali Mjengwa.

Aidha amewaagiza Madiwani wa Wilaya hiyo kuwaelimisha Wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwani imeonekana wananchi wengi hawajui umuhimu wake hivyo kufanya vitendo vya ukataji wa miti na uchomaji moto kuwa ni vya kawaida na ni sehemu ya maisha yao ya kila siku pasipo kujua athari zake.

Pia amewaagiza makatibu tarafa wote wa wilaya hiyo kuwachukulia hatua watu wote ambao wamejenga kwenye vyanzo vya maji ili kuvinusuru vyanzo hivyo kukauka na kusababisha wananchi waingie kwenye janga la ukosefu wa maji kutokana na watu kufanya makazi kwenye vyanzo hivyo.

 Alisema kiutaalamu maeneo ya vyanzo vya maji hayapaswi kuwekwa makazi ya watu kwani yanaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo magonjwa ya mlipuko na kukauka kwa vyanzo hivyo kutokana na baadhi ya watu wengine kulima kwenye vyanzo hivyo bila kujari hathari ambayo inaweza kutokea hapo baadae.