MKUU WA MKOA WA RUVUMA SAID MWAMBUNGU
Na Gideon Mwakanosya, Songea
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amewaonya wafanyabiashara wanaouza saruji Mkoani humo kuacha mara moja tabia ya kuuza bidhaa hiyo kwa ulanguzi ambapo Wakazi wa maeneo mbalimbali wamekuwa wakilalamikia bidhaa hiyo kuuzwa kati ya shilingi 25,000 na 28,000 kwa mfuko wa saruji wenye ujazo wa kilo 50 badala ya shilingi 15,000 bei ambayo ni elekezi toka kwa Kiwanda cha saruji Mbeya na amewapa siku tatu walanguzi wa bidhaa hiyo kuacha mara moja.
Akizungumza na mwandishi wa mtandao huu wa www.stephanomango.blogspot.com ofisini kwake hivi karibuni Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa Serikali haitakubalia kamwe kuona baadhi ya Wafanyabiashara wakiwa wanauza saruji kwa bei kubwa ambayo Mwananchi wa kipato cha chini hawezi kuimudu.
Alisema kuwa kutokana na kuwepo malalamiko mengi toka kwa Wananchi kuwa bei ya Saruji imekuwa ni kubwa alilazimika yeye mwenyewe kufanya ziara ya ghafla kwenye baadhi ya maduka yanayouza Saruji na kukuta bidhaa hiyo ikiwa imewekwa lebo ya bei ya shilingi 28,000 kwa mfuko mmoja wenye ujazo wa kilo 50.
Alieleza zaidi kuwa baada ya kubaini kuwepo kwa tatizo hilo amewaagiza wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha kuwa Mawakala wa Saruji Mkoani humo kuhakikisha kuwa wanauza mfuko mmoja wa Saruji wenye ujazo wa kilo 50 kati ya shilingi 15,000 hadi 17,000 badala ya bei waliyokuwa wakiendelea kuwalangua wananchi.
“Ndugu Mwandishi nimefanya mawasiliano ya moja kwa moja kwenye Kiwanda cha Saruji Mbeya ambako nimewauliza ni kwanini bei ya Saruji imepanda ghafla,wamenijibu kwamba wao hawajapandisha bei na uzalishaji wa bidhaa hiyo haujashuka na wala gharama za uzalishaji hazijapanda” Alisema Rc Mwambungu.
Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na mtandao huu kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa umebaini kuwa bei ya Saruji imepanda tangu Agosti mwaka huu ambapo imekuwa ikiuzwa kati ya shilingi 25,000 hadi 28,000 kwa mfuko wa kilo 50.
Uchunguzi huo pia umebaini kuwa bidhaa hiyo imekuwa ikisafirishwa kutoka Mbeya hadi Makambako ambako baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wakiinunua kisha kuileta Ruvuma kuiuza kwa bei ya ulanguzi ambayo tayari imekuwa ikilalamikiwa na Wakazi wakiwemo Wakandarasi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya Wananchi waliiomba Serikali ione umuhimu wa kuchukua hatua za haraka za kuudhibiti mfumuko wa bei ya saruji Mkoani Ruvuma ambao umesababisha watu wengi waliokuwa wakiendelea na shughuli za ujenzi kusitisha kutokana na bidhaa hiyo kuuzwa kwa bei kubwa.
Kwa upande wake Mkuu wa ghala la kuhifadhia Saruji ya Kiwanda cha Saruji Mbeya tawi la Songea aliyejitambulisha kwa jina moja la Kagambi alipoulizwa na mtandao huu juu ya tatizo la uhaba wa bidhaa hiyo alisema kuwa ni zaidi ya miezi miwili hajapokea Saruji toka Mbeya na ghala lake lipo tupu na alikataa kuendelea kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa yeye si msemaji labda kuwasiliana na Meneja mauzo wa Kanda ndiye anayeweza kujua ni kwanini Saruji imeadimika.
Mtandao huu ulifanya jitihada ya kumtafuta Meneja mauzo wa Saruji Kanda ya Iringa kwa njia ya simu ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Maguu, alisema kuwa zaidi ya miezi miwili Saruji imeadimika lakini hawezi kusema lolote kwa madai kuwa yeye siyo msemaji wa Kiwanda.
Hata hivyo mtandao huu ulifanikiwa kuwasiliana kwa njia ya simu na Meneja mauzo wa Kiwanda hicho cha Saruji kilichopo Halmashauri ya Jiji la Mbeya aliyejitambulisha kwa jina la Mwakasege na kumtaka atoe ufafanuzi ni kwanini kuna tatizo la uhaba wa bidhaa inayozalishwa na Kiwanda chake ambapo alisema kuwa Kiwanda cha Saruji bado kina bidhaa hiyo nyingi lakini tatizo kubwa linalowakabili ni magari makubwa ya kusafirishia Saruji kwenda kwenye maghala ya mawakala.
Mwakasege alisema kuwa kwa Mkoa wa Ruvuma tangu octoba 6 mwaka huu Kiwanda kimeshindwa kupeleka saruji kutokana na ukosefu wa magari kusafirisha Saruji kwenda Songea lakini kuna mpango ambao umebuniwa na kiwanda ambao utaweza kupunguza tatizo hilo lililojitokeza.
Aliubainisha mpango huo waliobuni kuwa ni kwa vile Mkoa wa Ruvuma una machimbo ya makaa ya mawe katika Kijiji cha Mngaka kilichopo kata ya Ruanda Wilaya ya Mbinga ambayo yanahitajika sana kwenye kiwanda cha Saruji Mbeya hivyo magari yatakayokuwa yakienda kubeba makaa ya mawe yatakuwa yakibeba Saruji toka Kiwandani na kuipeleka Songea ambako kuna ghala kubwa la kuhifadhia Saruji hiyo ya kiwanda kisha wafanyabiashara watakuwa wakiinunua bidhaa hiyo kwenye depot ya Songea.
Alifafanua kuwa Malori hayo makubwa yatakuwa yakitoka Mbeya yakiwa yamesheheni saruji na wakati wa kurudi yatakuwa yakisheheni makaa ya mawe toka Mngaka Ruanda Mbinga hivyo hakutakuwa na shida tena ya uhaba wa Saruji endapo mpango huo utaenda kama ulivyopangwa
MWISHO