KATIKA miaka saba aliyokaa madarakani, Rais Jakaya Kikwete anajivunia mambo kadhaa mbele ya Watanzania. Kwanza, “ameua” chama chake. Pili, amedhoofisha Bunge. Tatu, amethubutu kuiweka mahakama mfukoni mwa serikali. Nne, ameonyesha ubabe uliokithiri kwa “kuziba midomo” ya vyombo vya habari. Amebakiza nini? Niliwahi kusema huko nyuma kwamba Watanzania walidanganywa na tabasamu la JK mwaka 2005. Wapo pia waliozuzuka kwa utanashati wake. Wengine walikumbwa na wimbi kali la mkakati wa wanamtandao. Wapo pia waliomshabikia kwa sababu ya ushawishi wa fedha. Leo watu hawa wanasikitikia au wanafurahia uamuzi wao? Waliomwingiza JK madarakani CCM kikiwa imara; waliomkabidhi uenyekiti wa chama hicho kikitambia ushindi wa kishindo; leo wanajivuna kwa yaliyokipata CCM kwa miaka saba mfululizo? Je, chini ya Kikwete, wana CCM wana jeuri tena ya kuzungumzia ushindi wa kishindo huko tuendako? Wale waliomkabidhi serikali ikiwa na hazina imara; ambayo hata yeye alikiri hadharani kwamba ameachiwa mahali pazuri la kuanzia; leo wanapomsikia yeye na mawaziri wake wakilalama kwamba serikali haina pesa, wanamwelewa? Nani ametafuna hazina yetu? Wanaokumbuka jeuri ya Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta; wakatafakari jinsi alivyoingia kwa mbwembwe na kuondoka kwa kishindo cha aibu iliyoasisiwa na watu wake wale wale waliomwingiza; wanapopima utendaji wa spika aliyepita na wa huyu aliyepo; wanajivuna kwamba Bunge linafanya kazi yake iliyokusudiwa? Katika mazingira ambamo spika amejigeuza sehemu ya serikali; kwa jinsi anavyoitetea na kuilinda bungeni kuliko hata waziri mkuu; katika mazingira ambamo spika naye anashiriki katika vikao vya chama na serikali vya kunusuru chama au serikali katika masuala mazito, hata yenye kashfa; nani anakataa kwamba waliomwingiza na kumwondoa Sitta, na baadaye kumweka Anne Makinda walikuwa na malengo machafu? Bahati nzuri, katika utendaji wa Makinda, Watanzania wameanza kuelewa maana ya hoja yetu ya siku nyingi, kwamba spika wa Bunge asitokane na chama cha siasa; au akitokana na chama, mara tu baada ya kushika wadhifa huo, ajivue uanachama, awe kiongozi huru. Si hayo tu. Hata mfumo wetu wa mahakama umeingiliwa na serikali. Nimewahi kuhoji staili ya sasa ya jinsi serikali kutumia mahakama kuzima madai nyeti ya wafanyakazi wake. Ilianza kuzitumia kuzima madai ya wafanyakazi wa serikali. Juzi juzi ilizitumia tena kuzima madai ya madaktari. Sasa imezitumia kuzima madai ya walimu. Mahakama haikutoa “haki” kwa watumishi hao; bali imewatisha kwa kuwalazimisha kuripoti sehemu zao za kazi. Serikali haikutimiza madai yao. Tatizo limebaki pale pale! Wao na wananchi wanaendelea kulalamika. Serikali ya namna hii itadumu? Hata kama madaktari wote wanakuwa kazini; hata kama walimu wote wataingia madarasani; tuna uhakika gani na ubora wa huduma zinazotolewa? Tuna uhakika gani na umakini wao kazini? Huu ni uthibitisho mwingine kwamba serikali ndiyo inayoua mifumo ya afya na elimu. Wakubwa hawajali kwa sababu wakiugua hawatibiwi katika hospitali zetu; na watoto wao hawasomei katika shule zetu. Viongozi wasiojali wananchi kwa kiwango hiki, wanaweza kutushawishi kwamba wana uzalendo na nchi hii? Wanaweza kuaminika kwa kauli zozote wanazotoa? Tabia hii ya serikali ya JK ndiyo imewafanya wananchi wakose imani na uongozi wake. Siku hizi serikali haiaminiki kwa Watanzania. Kwa miaka saba aliyokaa madarakani, wananchi wameanza kuona mwisho wa utawala wa CCM. Haya ni maandalizi ya anguko la watawala, na mwanzo wa zama mpya chini ya utawala mpya, na mfumo mpya. Na wana CCM ambao bado wana mishipa hai ya kisiasa, wanalitambua hili na wanatafuta jinsi ya kujinusuru, hata kama itabidi kukitosa chama chao cha sasa. Baadhi yao wamewahi kuniambia kwamba, kwa jinsi wanavyotazama mambo ndani ya CCM, Rais Kikwete amefika mwisho wa safari yake ndefu. Amepata alichotafuta kwa muda mrefu. Ameridhika. Hajali kama serikali inadhoofika, na haiaminiki. Hajali kama chama chake kinakufa. Baadhi yao wanasema wameanza kutafuta mahali pa kuponea kisiasa, na kumwacha “afe na chama chake.” Lakini, wapo pia wanaoamini kwamba JK hapendi kuangusha serikali wala kuua chama chake, bali analazimishwa na mambo mawili – uwezo wake mdogo kimenejimenti, na hitaji la wakati, baada ya miaka 50 na ushei ya utawala ule ule. Hizi ni dalili za serikali inayoanguka. Tatizo ni kwamba inataka kuanguka na kila mtu, na kila kitu. Ndiyo maana haitaki kuona mahakama zikiwa huru; Bunge likifanya kazi yake kwa uhuru na uaminifu; na vyombo vya habari vikiwa huru. Ni ajabu kwamba serikali, ambayo nayo inamiliki vyombo vya habari, yenye idara za habari kila wizara, yenye wataalamu kila eneo; badala ya kujibu hoja zinazoibuliwa na vyombo vya habari visivyo vya serikali, inakimbilia kuvifungia au kuvifuta. Woga! Ni aibu kwamba serikali inayojitapa inazingatia utawala wa sheria, inashindwa kutumia mahakama kudai haki dhidi ya vyombo vya habari; au hata kuvipeleka mbele ya Baraza la Habari; badala yake inatumia mabavu ya sheria kandamizi kuvifungia na kuvifuta. Woga! Inaweza kuvifungia sasa. Inaweza kupenyeza fikra chafu hata miongoni mwa wahariri wa vyombo hivi kuwagawa, ili wakose msimamo wa pamoja wanaponyanyaswa na serikali. Lakini, ukweli ni kwamba vyombo hivi vinavyofutwa vina nguvu na ushawishi kwa umma, na vinaaminika kuliko serikali yenyewe, hata huko kifungoni vilikofungiwa. Na bahati mbaya ni kwamba serikali haijui kuwa kadiri inavyojitahidi kuvifungia au kuvifuta, pole pole inaandaa mazingira ya kujifungia na kujifuta. Mara zote, mwisho wa serikali za kibabe ni mbaya. Bahati mbaya zaidi, serikali inafungia vyombo vya habari, lakini haiwezi kufunga wala kufuta mawasiliano ya umma, hasa katika zama hizi zenye njia nyingi sana za kuwasiliana. Na kadiri serikali inavyozidi kuwa katili, ndivyo umma unavyozidi kuamini kila kibaya kinachosemwa dhidi ya serikali yao. Inaweza kukanusha tuhuma kupitia kwa waziri, waziri mkuu, au rais wa nchi. Lakini siku hizi nani anamwamini waziri mkuu au rais? |