About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Friday, September 13, 2013





 Mkurugenzi  Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania ( TGNP) U ssu Mallya

Na,Alpius Mchucha—Namtumbo

BAADHI ya wanawake wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,wamesema wangetamani  siku moja kuona katika katiba ijayo kunakuwa na kipengele maalum cha kuwabana wanaume wanaowakashifu wanawake kwa kutaja sehemu za siri za wanawake hao kwani tabia hiyo imekuwa ikiwadhalilisha sana kwa jamii na kuwavunjia heshima na utu wao.

Wakizungumza katika mdahalo wa siku moja jana uliowakutanisha wanawake zaidi ya 50 kutoka katika vijiji mbalimbali  vya wilaya hiyo wanawake hao walisema,wameshachoshwa na matusi yanayotolewa na wanaume ambayo yanataja sehemu za mwili wa mwamke hivyo ni lazima  kutafuta njia ya kukomesha kwakuwa matusi hayo yamewafanya kuonekana kama siyo watu wanaotoa mchango kwa jamii na  nchi.

Mdahalo huo wenye lengo la kujadili,kubadilishana uzoefu, kujifunza masuala ya  kijinsia na elimu ya uraia uliandaliwa kwa pamoja na shirika lisilokuwa la kiserikali la Oxfam na mradi wa kuwawezesha vijana wa Restless Devolopment ulifanyika katika ukumbi wa Parokia mjini Namtumbo.

Mmoja wa wanawake hao Christina Kuhimini alisema, sasa wameshachoshwa na  udhalilishaji dhidi yao  hivyo kuiomba serikali kutokuwa na huruma na watu hao  wasiokuwa na hata  chembe ya aibu ambao kila kukicha wanatafuta maneno mapya ya  kuwakashifu wanawake licha ya kutambua kuwa bila ya  mwanamke  basi hata wanaume hao wasingeweza kutokea hapa Duniani kwa kile alichoeleza kuwa hakuna binadamu anayeweza kuzaliwa na mwaume bila ya kuwa na mwanamke.

“bahati mbaya sana muda wa kutoa maoni kwa ajili ya katiba mpya umekwisha,lakini kupitia vyombo vya habari vilivyopo hapa leo naomba  sana watufikishie ujumbe wetu sisi wanawake wa Namtumbo tumechoshwa sana na matusi yanayotolewa na wanaume kila siku,tena ni mibaba mizima nayo utoa lugha za kuwakashifu wanawake ambao hawana hatia yeyote,ili siyo jambo jema hata kidogo ni baya linalowadhalilisha wanawake”alisema.

Aliongeza kuwa,  tabia hiyo  ya matusi licha ya kutaja maumbile ya ndani ya mwanamke lakini kwa bahati mbaya sana imekuwa ikiwarithisha watoto wadogo wanaohitajki kusikia au kufundishwa matendo  mazuri kutoka kwa watu wazima,lakini cha kushangaza hakuna hatua inayochukuliwa hivyo kuendelea kuota mizizi na kuonekana kama jambo la kawaida.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtandao wa polisi wanawake  na mratibu wa dawati la jinsia mkoani hapa Mrakibu wa jeshi la  polisi Anna Tembo alisema tatizo kubwa lililopo ni  wazazi kushindwa kuwafundisha maadili mema watoto wao tangu wakiwa wadogo hivyo kujikuta wakiiga tabia mbaya za mitaani ambazo hazina misingi bora kwao.

Pia amewataka wanawake kubadilika na kuanza kujitambua kwa kutojihusisha katika matukio yanayowafedhehesha ambayo yanawafanya kuonekana vituko kwa jamii ya kistaarabu na ambayo kwa kiasi Fulani yanawapa kiburi wanaume kufanya watakalo kwa wanawake.

Tembo alieleza kuwa,wanawake wengi wanafanya matukio   ambayo ndiyo yanayowapa hamasa wanaume kufikiria kuwa mwanamke ni chombo cha kutumika vibaya badala ya pambo ndani ya nyumba na kuendelea kuwafanyia unyama wa kila aina akina mama.

Alitaja uvaaji wa nguo fupi,  zinazobana na zinazoonesha maumbile yao,kucheza shoo nyakati za usiku katika sehemu za starehe,kujiuza, na hata ukatili kwa watoto navyo ni sababu kubwa ya kudhalilika kwao.
                 MWISHO