KAMA kawaida yake, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, jana aliibuka mbele ya waandishi wa habari akizungumzia mauaji ya mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi, aliyeuawa na Jeshi la Polisi juzi mkoani Iringa wakati akitimiza majukumu yake.
Tendwa ambaye ni mlezi wa vyama vya siasa mwenye jukumu la kuvisimamia, kuvishauri na kuhakikisha vinatendewa haki na kufanya shughuli zao katika mazingira sawa ya ushindani, alitumia muda mwingi kutupa lawama kwa chama cha CHADEMA kuhusu vurugu hizo.
Katika kuonesha kuwa Tendwa anacheza ngoma asiyoijua mdundo wake, alitumia muda mwingi kurejea hadithi zake za vitisho vya kuifutia usajili CHADEMA, akidai kushangazwa na operesheni zake mikoani wakati huu ambapo hakuna uchaguzi.
Kwanza, tunampongeza Tendwa kwa kujitokeza hadharani na kuzungumza hicho alichoona kinampendeza yeye na wale waliomteua, maana pamoja na kuchelewa kutoa maonyo hayo kwa polisi na CHADEMA, bado ameendelea kudhihirisha kuwa hatambui wajibu wake.
Tunasema hivyo kwa ushahidi kuwa kazi ya ofisi yake haionekani kuvisaidia vyama vya siasa, hasa vya upinzani na badala yake Tendwa amekuwa kinara wa kuvitisha na kutosikiliza malalamiko yao.
Mathalani katika vurugu zilizozushwa na polisi kwenye maandamano ya CHADEMA mkoani Arusha Januari 5, mwaka jana, kisha mkoani Mwanza, Msajili huyu hakuonekana kusema lolote hadi Rais Jakaya Kikwete alipohutubia taifa na kuwatisha CHADEMA ndipo kesho yake naye akaibuka na vitisho.
Kama hiyo haitoshi, katika uchaguzi mdogo wa Igunga ambao matokeo yake yametenguliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, miongoni mwa mambo yaliyomuengua Dk. Dalali Kafumu, yalilalamikiwa sana na wapinzani kwenye kampeni kuwa CCM inacheza rafu lakini Tenda alikaa kimya na matokeo yake yameonekana.
Ni Tendwa huyu aliyeibuka kwenye kampeni za uchaguzi mdogo Arumeru Mashariki na kuwatisha CHADEMA kuwa wasimtumie aliyekuwa mbunge wao wa Arusha Mjini, Godbless Lema, katika kampeni hizo akidai wazee wa jamii ya Kishiri walimwambia watamdhuru.
Tunachelea kuamini kuwa ikiwa Msajili mwenye jukumu la kusimamia amani na utulivu anapofikia hatua ya kuzua uongo kama huo, tena kipindi cha uchaguzi halafu akashindwa kuthibitisha madai ya kauli zake, leo tutamshaangaje akiibuka na kuwasingizia CHADEMA kwa lolote ilhali ukweli wa vurugu za kisiasa unajulikana?
Ofisi ya Tendwa imezuia vyama kufanya shughuli za kisiasa kama mikutano na maandamano wakati huu wa sensa na vyama vyote vimetii lakini CCM inaendelea na mchakato wa uchaguzi wake wa ndani kwa wagombea kuchukua na kurudisha fomu kwa maandamano bila kuonywa, ila CHADEMA wanaofungua tawi wanatishiwa kufutwa kuwa wanachochea vurugu.
Tangu kuanza tena kwa mfumo wa vyama vingi nchini, Ofisi ya Msajili imekuwa na kasoro nyingi sana katika ustawi wa demokrasia ya upinzani, maana hata mtangulizi wa Tendwa, Jaji George Lindi, naye alipwaya ingawa huyu wa sasa amezidisha ushabiki kiasi cha kujikuta akicheza ngoma asiyoijua.
Chanzo TAHARIRI, Tanzania Daima, Septemba 6,2012