POLISI WAMKAMATA DIWANI NA WAZUIA MAANDAMANO SONGEA
Na,Stephano Mango,Songea
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma liliwakamata na kuwahoji zaidi ya masaa matatu wakazi wawili wa Kata ya Mshangano na Diwani wa kata hiyo kupitia Chama cha Mapinduzi(CCM)kwa tuhuma za kutangaza maandamano ya amani ya wananchi wa kata hiyo wakidai kupimiwa ardhi yao na Kampuni ya Ardhi Plan na kumtaka Waziri mkuu Mizengo Pinda kuwatimua kazi Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea na Afisa Mipango Miji wa Manispaa hiyo ambao wameonyesha dhahili kutaka kuwadhulumu maeneo yao
Wakazi hao waliokamatwa na polisi ni Suzo Luoga ambaye alikuwa ni dereva wa gari ya matangazo lenye namba za usajili T 295 AJS aina ya Chesar mark II,Joseph Haule ambaye alikuwa mtangazaji na Faustine Mhagama ambaye ni Diwani wa kata hiyo ambao wote walikamatwa wakiwa kwenye gari hilo ambalo lilikuwa linapita kwenye mitaa ya kata hiyo kuwatangazia uwepo wa maandamano makubwa
Mmoja wa watuhumiwa hao Haule ambaye alikuwa mtangazaji alisema kuwa kazi hiyo alipewa na viongozi ambao wenyeviti wa serikali ya mitaa ya Namanyigu,Mshangano na Mitendewawa na kwamba shughuli hiyo ya utangazaji ilisimamiwa kikamilifu na Diwani wa kata lengo kuhakikisha ujumbe unawafikia wakazi wote wa kata hiyo
Naye wa Kata hiyo Mhagama akizungumza na mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ jana alikili kukamatwa na alidai kuwa yeye pamoja na wenzake walikamatwa na Polisi majira ya saa tatu usiku huko katika eneo la Mshangano na waliamriwa kuingia kwenye gari la Polisi wakiwa chini ya ulinzi mkali na kupelekwa kwenye kituo kikubwa cha Polisi
Alisema kuwa mara baada ya kufikishwa kituoni hapo waliamliwa kuvuliwa viatu,mkanda na kuanza kupekuliwa na kasha kuwekwa mahabusu ambapo baadae alifika Kaimu Mkuu wa Polisi wa Wilaya akiwa ameongozana na Askari Kanzu wawili ambao walianza kuwahoji hadi saa tano na nusu usiku ndipo walipoambiwa wawatafute watu wa kuwadhamini ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea James Makene pamoja na Diwani wa Viti maalum Rehema Milinga walifika kituoni hapo na kuwadhamini
Kwa upande wake Makene ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Matarawe aliuambia mtandao huu kuwa kitendo cha kuwakamata Diwani na wenzake ni uonevu mkubwa na kinyume na utawala bora kwa kuwa Serikali ya Kata ya Mshangano ilipeleka barua ya kuomba kibali cha maandamano toka tarehe 19.8.2011 ambapo mpaka wanakamatwa walikuwa hawajapewa barua wala maelezo ya aina yoyote jambo ambalo liliashiria kukubaliwa ingawa baada ya kuwaweka mahabusu ndipo wakapewa barua ya maelekezo jambo ambalo limeleta utata mkubwa wa uadilifu wa jeshi hilo
Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alisema kuwa wananchi wa kata ya Mshangano waliomba kibali cha kutaka kufanya maandamano makubwa ya amani lakini katika barua yao ilionyesha mapungufu mengi ikiwa ni pamoja na kutoeleza tarehe,muda na njia ambayo maandamano yatapita
Kamuhada alisema kuwa tayari Serikali ya Kata ilipewa barua ya maelekezo na Jeshi la Polisi yenye kumbukumbu namba.SOA.3.6/65 ya tarehe 25.8.2011 ambayo ilipokelewa na Diwani wa kata hiyo majira ya saa tatu usiku
MWISHO