About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Saturday, September 24, 2011

VIONGOZI WA CHADEMA KUUNGURUMA VIWANJA VYA SOKO LA SAMAKI KUPINGA UCHAKACHUAJI WA UMEYA SONGEA

Joyce Joliga,Songea

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kesho kinatarajia kufanya mkutano mkubwa wa hadhara ili kuwajulisha wananchi vurugu zilizotokea jana wakati wa uchaguzi wa Meya wa manispaa ya Songea na kusababisha uchaguzi kuvurugika kutokana na madai ya kuwepo kwa wizi wa kura.

Akizungumza na mwandishi wa mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ na Mwenyekiti wa chama hicho mkoa Joseph Fuime amesema, mkutano huo unatarajiwa kufanyika kesho majira ya saa 9 alasili hadi saa 12:00 katika  uwanja wa soko la Samaki lililopo karibu na shule ya Msingi Mfaranyaki .

Amesema,tayari kila kitu kimeshakamilika na wamepata vibali vya kufanya mkutano huo ambapo viongozi mbali mbali watahudhuria  akiwemo Mbunge wa jimbo la Mbozi Magharibi Silinde pamoja na wakili wa kujitegemea Edson Mbogoro.

Aidha,Fuime ametoa wito kwa wananchi wa Manispaa ya Songea kujitokeza kwa wingi kuhudhuria mkutano huo na tayari mambo yote yamekwenda vizuri na wanatarajia kuwa wananchi watafahamu kila kitu kilichojitokeza kutokana na vurugu hizo.

Kwa Upande wake Katibu wa Chadema Jimbo la Songea Paul Masumbuko amesema,chama kimesikitishwa na vitendo vya vurugu vilivyofanywa wakati wa uchaguzi huo na kueleza kuwa wanaungana mkono na Madiwani wao kutomtambua Mgombea wa umeya ikiwa ni pamoja na kutojishugulisha na shuguli zozote hadi uchaguzi utakaporudiwa.

"Kwanza kwa niaba ya chama  tunapenda kuwapongeza Madiwani wa CCM kwa kuungana na wenzao wa  Chadema ambao wapo  7 katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea wakati madiwani wa Ccm wapo 20 ambapo kwenye uchaguzi wa leo walikuwepo 19"lakini kwa kuonyesha kuwa hawamkubali mgombea wao wamempigia kura za hapana hiyo ndiyo demokrasia ya kweli ", alisema Masumbuko

 Amesema, kitendo kilichofanywa na Madiwani wa CCM kuungana na wenzao wa Chadema kimeonyesha ukomavu mkubwa wa demokrasia na kinapaswa kupongezwa kwa nguvu zote kwani upinzani si kupingana kwa kila kitu bali inapotokea maslahi ya wananchi ni vema waungane na kuonyesha uzalendo mkubwa kwa nchi na wananchi waliowachagua.

Katika tamko lililosomwa  jana na Madiwani wa Chadema  kwa niaba ya madiwani wenzake wa Chadema kwenye ukumbi wa Saccos ya halmashauri hiyo Diwani wa kata ya Bombamabili Kenny Mpangara alisema kuwa mazingira yote ya zoezi la uchaguzi yameonekana na utata kwa maslahi binafsi na kudai kuwa Madiwani wa Chadema watasusia vikao vyote vya halmashauri mpaka Meya mpya atakapopatikana .

Kwa upande wao Madiwani wa Chama cha Mapinduzi wakitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari na kusomwa na Diwani wa kata ya Lilambo Yobo Mapunda lilisema kitendo walichofanya Madiwani wa Chadema cha kufanya fujo na kutaka kuwapiga wengine ni kitendo kibaya sana katika kukuza demokrasia na kwamba CCm inamtambua Mstahiki Meya kuwa ni Charles Mhagama
MWISHO.

MADIWANI WATISHIA KUJIUDHURU NYADHIFA ZAO MCHAKATO WA UMEYA SONGEA

Na Mwandishi Wetu,Songea
HALI ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea mjini mkoani Ruvuma ni tete kutokana na madiwani wake saba kutishia kurudisha kadi za chama hicho na kujiuzulu nafasi zao zote ndani ya chama ikiwemo na udiwani kwa kile kilichodaiwa kumpigia kura za hapana mgombea wa unafasi wazi ya umeya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Wakizungumza na waandishi wa habari jana kwa nyakati tofauti madiwani hao walisema kuwa wao kwa pamoja wameitwa kwenye kamati ya maadili ya chama hicho ili waweze kuhojiwa kwanini waliamua kukisaliti chama na kuungana na madiwani saba wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) na kumpigia kura za hapana mgombea wa nafasi ya umeya aliyepitishwa na Ccm Charles Mhagama katika uchaguzi uliofanyika jana na kuishia na vurugu kubwa kwa kurushiana makonde na matusi ya mwilini
Walisema kuwa ni kweli  walimpigia kura za hapana ili uchaguzi uitishwe upya kwa sababu mgombea wa chama chao hatoshi kushika wadhifa huo kwani kuna mambo mengi ambayo ameshindwa kuonyesha uongozi wenye umahili na kwamba Chadema wenye madiwani saba hawakusimamisha mgombea
“Ndani ya chama viongozi walilazimisha na akafanikiwa kupenya kwenye mchakato wa ndani nasi tukasema wamezoea kutuburuza kwa kutulazimisha kupitisha viongozi wanao taka wao kwa maslahi ya wachache sasa awamu hii tunawaonyesha nguvu zetu kwa kumpigia kura za hapana ili wahaibike vizuri mbele za watu wengi”walisema madiwani hao ambao hawakutaka majina yao yatajwe
Walisema kuwa kumpigia kura za hapana diwani mwenzangu wa Ccm kwenye uchaguzi wowote ule sio dhambi ila kumpigia kura za ndiyo diwani wa Chadema ndio ingekuwa dhambi kwa mujibu wa demokrasia mfu zilizopo ndani ya Ccm sasa tunashangaa kuitwa kwenye kikao cha maadili leo
“Tupo tayari kwa lolote ili wananchi wapime ubabe uliopo ndani ya Ccm kwani wao ndio waliotuchagua hivyo tunapaswa kushirikiana nao katika kulisukuma gurudumu la maendeleo na sio kuwadhurumu rasilimali zao na kuwasababishia ufukara mkubwa miongoni mwao
Juzi ulifanyika uchaguzi wa nafasi wazi ya Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambapo Chadema hawakusimamisha mgombea kwa madai kuwa mchakato mzima wa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki na kwamba Ccm walimsimamisha Diwani wa kata ya Matogoro Charles Mhagama
Katika uchaguzi huo uliotawala na vulugu za kila aina wajumbe waliopiga kura walikuwa 26 hivyo  kwa mujibu wa mtangaza matokeo Naibu Meya Mariam Dizumba kuwa Mhagama alipigiwa kura za ndiyo 14 na hapana 12 ndipo madiwani walipoanza kutaka uhesabuji ufanyike upya kwa uwazi kwa maana wanamashaka makubwa na utangazaji wa matokeo ambapo uchaguzi huo haukumalizika

Akizungumza na mtandao huu Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Alfonce Siwale alikiri kuwaita madiwani wote kwenye kikao cha maadili ili waweze kuhojiwa kuhusiana na zoezi zima la uchaguzi wa kuziba nafasi wazi ya umeya na kuongeza kuwa kama madiwani wanataka kujiudhuru nafasi zao itakuwa ni busara kwani mtu mzima alazimishwi jambo
MWISHO



NI AIBU NA FEDHEHA VULUGU ZA UCHAGUZI WA UMEYA SONGEA ! JE NANI WA KULAUMIWA?


 Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Emmanuel Nchimbi
 Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Songea Mjini Nachoa Zakaria
 Naibu Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mariam Dizumba

Mgombea wa nafasi ya Umeya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Charles Mhagama
Na Mwandishi Wetu
MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamerushiana makonde baada ya Naibu Meya wa Halmashauri hiyo Mariam Dizumba kudaiwa kuiba kura zilizopigwa na madiwani hao ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi ya Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo aliofariki dunia miezi michache iliyopita
Katika uchaguzi huo ulioanza kwa marumbano makubwa yaliyodumu kwa zaidi ya dakika 20 kati ya madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) na Madiwani wa Chama cha Mapinduzi ambao walikuwa wanajadili namna uchaguzi huo utakavyokuwa  huru na haki kutokana na Chadema kutosimamisha mgombea na Ccm kusimamisha mgombea
Kutokana na hali hiyo Msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Nachoa Zakaria alitoa ufafanuzi wa kanuni za uchaguzi wa nafasi hiyo ambapo aliwataka madiwani kupiga kura za ndio au hapana na kwamba wapigakura halali waliojiorodhesha walikuwa ni Madiwani 26 akiwemo na Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Emmanuel Nchimbi
Baada ya hali hiyo kutulia Msimamizi wa uchaguzi Zakaria aliita orodha ya wajumbe na kuwataka wachukue karatasi za kupigia kula ambapo madiwani wote walipiga kura na kuitwa wahesabu kura waweze kuzihesabu kura hizo
Zoezi la kuhesabu kura lilipomalizika Naibu Meya wa Halmashauri hiyo Mariam Dizumba alilisimama na kuanza kutangaza matokeo kwa kudai kuwa Mgombea Umeya wa Halmashauri hiyo Charles Mhagama amepigiwa kura za ndio 14 na kura za hapana 12
Dizumba alisema kuwa kutokana na matokeo hayo namtangaza Diwani wa kata ya Matogoro Charles Mhagama kuwa ndiye Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuanzia sasa
“Naomba Msimamizi wa uchaguzi umuite Diwani Mhagama aweze kuvaa joho la Umeya na kukalia kiti chake”alisema Dizumba
Baada ya Msimamizi wa uchaguzi  Zakaria kumuita Diwani Mhagama na kumtaka avue joho la Udiwani na kuvaa joho la Umeya ndipo baadhi ya madiwani walipomtaka Msimamizi wa uchaguzi azihesabu upya kura hizo ili madiwani wote wazione
“Naomba msimamizi usitishe zoezi la kumtaka Diwani Mhagama akalie kiti cha Umeya kwa sababu kuna mashaka makubwa na zoezi la utangazaji wa matokeo yake hivyo zihesabiwe kura upya na madiwani wote wazione”alisema Diwani wa kata ya Mfaranyaki Seneta Yatembo
Jambo ambalo Msimamizi wa uchaguzi alionekana kupata kigugumizi nalo na kumsababisha Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Nchimbi kuingilia mgogoro huo na kupelekea kuharibu hali ya hewa na kuanza kurushiana lugha za matusi miongoni mwa madiwani
Wakati mgogoro huo ukiendelea Diwani wa Viti Maalum Chadema Rhoda Komba akaanza kuwaita madiwani wenzake  ili waweze kumuona Naibu Meya Mariam Dizumba alivyokuwa anaiba kura zilizopigwa za hapana kutoka kwenye sanduku la kura na kuchukua kura za ndiyo kutoka kwenye mkoba wake na kuziweka ndani ya sanduku la kura
Hali hiyo ilisababisha vurugu kubwa na kumfanya Mbunge Dkt Nchimbi akimbie na sanduku la kura kuelekea nje ya ukumbi kabla ya kunyanganywa na kutakiwa kurirudisha ndani na Madiwani wakiongozwa na Madiwani wa Chadema
Wakati Madiwani wanamnyang’anya sanduku la kura Dkt Nchimbi ndipo Naibu Meya Mariam Dizumba alipata mpenyo wa kukimbia na kufanikiwa kuingia ndani ya gari na kutokomea kusikojulikana na kufanya madiwani kuvua majoho na kuondoka zao huku wakimzomea Dkt Nchimbi na kurusha maneno ya matusi
Baada ya tafrani hiyo Madiwani wa Chadema waliitisha kikao na waandishi wa habari na kutoa tamko la kutomtambua Charles Mhagama kuwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo na kwamba wameiomba tume ya uchaguzi ione umuhimu wa kuitisha uchaguzi mwingine
“Akisoma tamko hilo kwa niaba ya madiwani wenzake kwenye ukumbi wa Saccos ya halmashauri hiyo Diwani wa kata ya Bombamabili Kenny Mpangara alisema kuwa mazingira yote ya zoezi la uchaguzi yameonekana na utata kwa maslahi binafsi na kudai kuwa Madiwani wa Chadema watasusia vikao vyote vya halmashauri mpaka Meya mpya atakapopatikana
"Madiwani wa Chadema wapo 7 katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea wakati madiwani wa Ccm wapo 20 ambapo kwenye uchaguzi wa leo walikuwepo 19"alisema Mpangara
Kwa upande wao Madiwani wa Chama cha Mapinduzi wakitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari na kusomwa na Diwani wa kata ya Lilambo Yobo Mapunda lilisema kitendo walichofanya Madiwani wa Chadema cha kufanya fujo na kutaka kuwapiga wengine ni kitendo kibaya sana katika kukuza demokrasia na kwamba Ccm inamtambua Mstahiki Meya Charles Mhagama
Akizungumza na waandishi wa habari Msimamizi wa uchaguzi Nachoa Zakaria kuhusiana na kitendo cha Naibu Meya Mariam Dizumba kutangaza matokeo badala ya Msimamizi wa uchaguzi alisema kuwa kwenye vikao vya baraza la madiwani Mkurugenzi ni katibu wa vikao na kwamba Naibu Meya ndiye alikuwa sahihi kutangaza matokeo hayo
MWISHO