About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Sunday, January 2, 2011

MASHUJAA WA VITA VYA MAJIMAJI WAKINYONGWA

Viongozi wa Kabila la Wangoni na Askari Waliokuwa Mstari wa mbele katika mapigano ya vita vya Majimaji Wakinyongwa Tarehe 27/02/1906 na Jumla  yao walionyongwa walikuwa 67  ambapo 66 walizikwa kwenye Kaburi moja ambalo walilichimba wenyewe bila kujua kuwa watakuja kuzikwa wenyewe na Mwingine ambaye ni Nduna Songea Mbano alizikwa kwenye Kaburi la Peke yake.

UJENZI WA MNARA WA MASHUJAA WALIONYONGWA NA WAJERUMANI NI KIELELEZO MUHIMU CHA KUWAENZI



Na, Stephano Mango, Songea

ENEO waliponyongwa viongozi na askari 67 walioshiriki kupigana vita vya Majimaji februari 27,1906 linatarajiwa kujengwa mnara wa kumbukumbu ili kuweka alama ya kudumu na wananchi waweze kupatambua na kupaenzi kikamilifu.

Philip Maligissu ambaye ni Mhifadhi kiongozi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea,akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake hivi karibuni anasema, eneo hilo ni muhimu sana kwa historia ya nchi yetu ambalo lipo nyuma ya ukumbi wa Songea Club  hivyo ni lazima uwekwe alama ya kudumu itakayotambulika kiurahisi na kuvuta hisia za mawazo ya watanzania wengi kwenda kupatembelea.

Alisema kuwa mnara huo unatarajiwa kuwa kumbukumbu muhimu na adhimu ya mashujaa wa vita vya majimaji,askari wanaopigana vita vya kagera na kufa kwa ajali njiani kwenye mlima wa Lukumburu wakiwa wanarudi nyumbani baada ya ushindi na  mashijaa waliopigana vita ya pili ya dunia.

Alieleza kuwa eneo hilo ni kumbukumbu muhimu katika historia,utamaduni na utalii ambapo ujenzi wa mnara utakapokamilika utawekwa majina ya mashujaa hao kwenye vibao vya shaba ili watu waweze kusoma na kuwaelewa wapiganaji hao.

Maligissu alibainisha kuwa kutawekwa fensi nzuri fupi na imara itakayowawezesha watu kuingia kwa utaratibu maalumu na kufanya shughuli za utalii na kupata elimu stahiki ya kihistoria na kuhusu uhuru wa mtanzania na mwafrika kwa kutumia vielelezo halisi.

Binafsi nakubariana na wazo la kujenga mnara katika eneo hilo,kwani historia ya mapambano ya kupinga utawala wa wakoloni na uhuru wa nchi yetu haiwezi kukamilika bila kuwataja mashujaa wa vita ya majimaji waliopoteza uhai wao kwa kuitetea nchi na hadhi yao kuanzia Julai 1905 hadi Agosti 1907.

Jina hilo la vita vya majimaji lilitokana na imani ya matumizi ya dawa iliyochanganywa na maji,punje za mahindi na mtama zilizosadikika kuwa zingempa mpiganaji kinga ya kutodhurika kwa shambulio la risasi za Wajerumani chini ya uhamasishaji wa mganga kinjekitile ngwale.

Vita hivyo vilidumu kwa miaka miwili kuanzia 1905 hadi 1907 na waanzilishi wa mwanzo wa vita hivyo walikuwa machifu na Mganga wa jadi katika jamii ya  wangindo na wamatumbi.

Baadaye vuguvugu hilo lilienea kwenye jamii nyingi ikijumuisha jamii za wamatumbi,wangindo,wamwera,wapogoro,wandendeule,wabena,wasangu,wangoni na nyingine,

Inaeleweka wazi kuwa toka mwanzo wakoloni kutoka ujerumani walijawa na shauku ya kunyonya raslimali kutoka makoloni yao ndio maana walilazimisha jamii za watu walioishi katika kuenea waliyoyachukua kuja tawala kwa nguvu,kushiriki katika uanzishaji wa mashamaba  ya mazao waliyoyahitaji katika viwanda vyao huko ulaya.

Vita vilipoanza katika vilima vya matumbi,kaskazini magharibi mwa kilwa julai  1905 na sababu kubwa ilikuwa ni wananchi kupinga vitendo viovu hasa vya kulazimisha kulima mazao ya biashara,kulipa kodi na unyanyasaji mwingine waliofanyiwa na mfumo wa utawala wa wajerumani.

Kwa muda wa miaka miwili wajerumani walishuhudia waafrika wakiwadhihirishia kwamba  dhana waliyokuwa nayo ya kuona Afrika ni bara la giza haikuwa sahihi hata kidogo.

Walilazimishwa kujua kwamba Afrika ina watu wenye dhamira,utashi na uwezo wa kutetea utu, uhuru na heshima yao,jambo lililowalazimisha wajerumani kuongeza wapiganaji kabla ya ushindi ili kukabiliana na mashambulizi ya mashujaa wa Afrika wa kusini  mashariki mwa Tanzania bara.

Wajerumani kwa juhudi kubwa na kwa kutumia bunduki na mbinu nyingine nyingi ikiwemo kuchoma moto mashamba na  maghala ya kuhifadhia chakula ya waafrika ili kudhoofisha uwezo wa kushambuliwa

Baada ya vita kusambaa askari na viongozi 67 walioshiriki vita walikamatwa na kufungwa jela na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa Februari 27 mwaka 1906.

Tarehe hiyo ilikuwa ni siku ya masikitiko makubwa kwa watu wa Ruvuma na Taifa kiujumla kwani watu 67 walinyongwa na kuzikwa katika kabuli moja lililochimbwa na wao wenyewe walipokuwa wafungwa bila kujua kuwa ndilo litatumika kuwazika wenyewe isipokuwa kiongozi wao Nduna Songea Mbano ndiye aliyezikwa kwenye kaburi la peke yake.

Mashujaa 66 walinyongwa na kuzikwa kwenye kaburi moja akiwemo chifu Mputa Gama na wasaidizi wake (nduna) kumi na mbili (12)  akiwemo nduna Songea mbano  ambaye alikuwa maarufu kuliko chifu mputa Gama alinyongwa na kuzikwa katika kaburi lake.

Akizungumzia tukio la kunyongwa mashujaa wa vita hivyo Makamu Mwenyekiti wa Baraza la mila na Desturi la Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea,Ally Songea Mbano ambaye pia ni Mjukuu wa Nduna Songea Mbano aliyepewa heshima ya jina lake litumike katika kuuita mji wa Songea

Anasema kwa masikitiko kuwa unyongaji ulifanyika kwa awamu tatu yaani Februari 27, machi 20 na Aprili 12,1906 katika eneo la Songea Club lililopo kata ya Mjini Manispaa ya Songea na kwamba siku ya kunyongwa watu wengi walikusanywa na walisimamishwa mahali ambapo waliweza kuwaona wanyongaji na waliokuwa wakinyongwa

Anasema  kuwa ilifanya vile ili kujenga hofu miongoni mwa jamii za waafrika ili kuwa vunja moyo wa ushupavu na ujeuli hasa pale watakapokuwa wanapewa amri mbalimbali za wakoloni wa kijerumani.

Katika eneo ambalo mnara unatarajiwa kujengwa kuna nguzo kubwa mbili zilizosimikwa pande mbili ambazo kwa mujibu wa Mbano,nguzo hizo zilishikilia mnyororo uliofungwa vitanzi vinne na kwamba chini ya nguzo hizo kulikuwa na ubao uliowekwa juu ya nguzo fupi nne.

“Basi waliwafunga wafungwa wa nne toka kwenye mnyororo ule mkubwa na wakasimamishwa juu ya ule ubao uliotegeshwa wakawapachika zile kamba zilizoning’inia kila mmoja na kamba yake huku wakiwa wamefungwa kamba mikono yote miwili ili wasiweze kujimudu kujitikisa na nyuso zao zilikuwa zimefungwa vitambaa nyekundu ili wasiweze kuona” anasema Mbano.

Anasema kuwa walisitiliwa maumbile yao kwa vitambaa vidogo kwenye sehemu zao za siri kabla ya askari kufyatua ubao na ndipo miili ya Mashujaa hao ikabaki ikining’inia kwenye vitanzi mpaka  walipokata roho

Baada ya Mashujaa kukata roho katika mateso makali, wauaji hao waliondoa miili hiyo na kuweka kando kwani walikuwa wakiwanyonga  wanne kwa wakati mmoja ambapo kwa siku ya kwanza Februari 27 walinyongwa watu 40 na  machi 20 walinyongwa watu 26 na Aprili 12 . 1906 alinyongwa Jemedari Nduna Songea Mbano.

Anabainisha kuwa maiti za Mashujaa walionyongwa kwa siku moja zililazwa katika kaburi hilo kubwa kiubavu bila sanda na kufukiwa kidogo ili kutoa nafasi kwa maiti wengine wa siku nyingine kuzikwa na kwamba walioongezeka kunyongwa walilazwa juu ya wale wa kwanza na kufukiwa katika kaburi hilo moja kubwa na kuongeza kuwa kati ya Mashujaa hao kulikuwa na wa imani tofauti  kwani walikuwepo wapagani,wakristo na waislamu.

Anasema kuwa Aprili 12 .1906 Nduna Songea  Mbano alidai na yeye anyongwe kama ndugu zake na wajerumani walimnyonga na kumzika kwenye kaburi la pekee yake ambalo lipo kwenye eneo la Makumbusho ya Taifa ya  majimaji Songea katika eneo la  Mahenge,Manispaa ya Songea.

Anasema hiyo ilitokea kwa sababu Nduna Songea Mbano alikuwa ndiye jemedali mkuu wa jeshi la wangoni na alikuwa hodari asiyeogopa  lolote kwa hiyo wajerumani walitaka abakie ili wamtumie kwa malengo yao jambo ambalo hawakufanikiwa.

Mzee Mbano anasema kuwa Mashujaa walionyongwa  vitanzini walikuwa 67, waliokufa gerezani kabla ya kunyongwa walikuwa wawili na waliopigwa risasi ili kuonyesha nguvu ya risasi walikuwa watano na kufanya jumla ya mashujaa 74 waliouwawa kikatili.

Ingawa inakadiliwa kuwa watu 75,000 walipoteza maisha yao ukanda wa kusini mwa Tanznaia baada ya vita ambapo katika eneo la Ruvuma inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 1000 walipoteza maisha yao.

Ni wazi kuwa vita vya Majimaji vilikuwa na madhara makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa watu wa mikoa ya kusini mashariki mwa Tanzania bara kwani kulitokea vifo vilivyosababishwa na  mapigano,upungufu wa chakula, watu kushindwa kufanya kazi kutokana na kukimbia makazi yao, ulimwaji wa mashamba na maghala ya kuhifadhia chakula uliofanywa na wajerumani ili kudhoofisha uwezo wa kushambuliwa wajerumani nao walipata madhala  kwani wapiganaji wao waliuawa na wapiganaji wazalendo na walilazimika kuongeza wapiganaji kukabiliana na mashambulizi kabla ya ushindi.

Vita vya Majimaji ni kumbukumbu muhimu katika historia ya Tanzania na kwamba Mashujaa wa vita hivyo wanastahili kuheshimika kwa kuwa walitetea utu, heshima na haki za binadamu na kielelezo halisi cha watanzania kukataa kutawaliwa na wakoloni kwani machifu na wapiganaji wengine wa vita hivyo Nduna songea mbano na wenzake wanastahili kukumbukwa.

Pamoja na jamii nyingine zilizopambana na wakoloni wakiongozwa na  machifu kama vile Mkwawa wa wahehe, Mangi sina wa Moshi, Abushiri na Bwana heri wa Pangani na viongozi waliongoza harakati za kudai uhuru kutoka kwa  waingereza

Mashujaa wa harakati za kudai uhuru  ni wale wote walioshiriki bila kuyumbishwa na hila za wakoloni kuhamamisha wananchi kuondoa utawala wa kigeni mpaka Taifa letu lilipopata uhuru mwaka 1961 Tanzania bara,na mapinduzi ya Zanzibar yaliyoondoa utawala wa kisultani Tanzanaia visiwani  mwaka 1964.

Orodha ya Mashujaa wa vita vya Majimaji ni kubwa ambapo baadhi ya majina yao yamehifadhiwa katika orodha ya walionyongwa baada ya kukamatwa na kufungwa na wajerumani.

Miaka zaidi ya mia moja  baada ya vita vya Majimaji watanzania wamejifunza mengi na kujenga upendo miongoni mwao na mahusiano mazuri na mataifa mengine ingawa ni wazi kuwa machungu ya vita hivyo bado hayajasahaulika

Lakini utamaduni mpya umejengeka miongoni mwa watanzania wa kushirikiana na kuheshimiana bila kujali kabila,rangi na asili ya mtu anakotoka huu ni ukomavu mkubwa uliojengwa na Mashujaa wetu hivyo ujenzi wa mnara wa Mashujaa hao ni muhimu kwa kizazi kilichopo na kijacho kwani ni kielelezo muhimu cha kuwaenzi, kuwaheshimu na kuwathamini wazee hao

Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana simu 0755-335051
Barua pepe;stephano12mango@yahoo.com.

KABURI LA NDUNA SONGEA MBANO

Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea Phillip Maligissu Akionyesha Kaburi alilozikwa Nduna Songea MbanoAmbalo Lipo kwenye Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea

NDUNA SONGEA MBANO KIONGOZI SHUJAA WA WANGONI ANAYESTAHILI KUENZIWA DAIMA.




Na Stephano Mango, Songea.

HUWEZI kuilezea na kuikamilisha historia ya vita ya Majimaji na ukombozi wa nchi yetu bila kumtaja shujaa wa kabila la wangoni Nduna Songea Mbano ambaye jina lake lilipewa hadhi ya kuuita mji wa Songea kutoka kwenye jina la Ndonde mwaka 1906.

Kiongozi huyo alikuwa ni miongoni mwa wasaidizi ( Nduna) 12 wa Chifu wa kabila la wangoni (Nkosi) chifu Mputa bin Gwezerapasi Gama.

Ambapo wasaidizi wake wengine walikuwa ni Mgendera Mawaso Gama, Kohongo Magagura, Mputa Mkuzo Gama, Magodi Mbamba Mbano, Mtekateka Muyamuya Tawete, Fratela Fusi Gama.

Manduna wengiwe ni Maji ya kuhanga Komba, Zimanimoto Gama, Mpambalyoto Soko Msalawani, Mtepa Hawaya Gama na Nduna Mkomanile ambaye alikuwa ni mwanamke pekee kuwa nduna.

Nduna Songea Mbano alikuwa ni maarufu kuliko manduna wenzake na hata chifu Mputa Gama alikuwa anamtegemea sana katika kuwaongoza Manduna wenzake na wapiganaji wa vita ya Majimaji kiujumla.

Mhifadhi kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Maji maji Songea Philipo Maligissu akizungumzia maisha ya Nduna Songea Mbano katika viwanja vya Makumbusho hayo,alisema kuwa Songea Mbano akiwa miongoni mwa manduna alitokea kuwa maarufu sana ukilinganisha na wenzake 11  ambapo sifa kubwa iliyo mpa umaarufu ili kuwa ni ueledi na ushadi wake wa kuandaa mikakati ya kivita, na maamuzi mazito yasiyoteteleka na kuyasimamia maamuzi hayo kikamilifu.

Kwa umakini mkubwa Nduna Songea Mbano aliweza kufanya kile alichokuwa akikiamini na uthibitisho wa jambo hilo ulianza kujitokeza julai 12, mwaka 1897 katika viwanja vya Bomani kwa mkuu wa Wilaya wa wajerumani luteni Engelhardt.

Maligissu anasema kuwa kwa rekodi zilizopo zinaonyesha kuwa tarehe hiyo Nduna Songea Mbano alionekana kuwa ni mtu wa kipekee katika idadi ya Manduna 11 ambao walikuwa wasaidizi wa chifu Mputa Gama kwa kitendo chake cha kubisha wazi wazi tamko la utawala mpya wa wajerumani la kutaka wangoni wakomeshe biashara ya utumwa.

Siku hiyo ilikuwa ni siku rasmi ambayo utawala wa kikoloni ulikuwa unaanzishwa katika mji wa Songea wakati huo ulikuwa unaitwa Ndonde na Mkoa wa Ruvuma kiujumla chini ya Luteni Engelhardt wa Jeshi la Kijerumani ambaye alikuwa ndiye Mkuu wa Jeshi kwa kanda ya Kusini.

Wajerumani walipofika kuanzisha makoloni yao katika maeneo ya ukanda wa kusini walikutana na msuguano mkubwa kutoka kwenye tawala za kiafrika hususani tawala za wangoni.

Maligissu anasema kuwa wangoni walikuwa na tabia ya kwenda mikoa ya Lindi na Mtwara kuvamia na kuchukua mateka na kuwaleta Songea kuwafanyisha shughuli mbalimbali katika maeneo yao ya utawala.

Tabia hiyo ya wangoni iliwachukiza sana wajerumani kwani wajerumani walikuwa wanaheshimu sana makubaliano yaliyofikiwa kutoka kwenye mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 hadi 1885.

Katika mkutano huo moja ya makubaliano yaliyofikiwa ni pamoja na kila nchi yenye koloni barani Afrika ni lazima ikomeshe biashara ya utumwa na kwa kuwa wajerumani walikuwa wamejiimarisha sana katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Hivyo walipokuja Ruvuma wakatoa tamko kwa wangoni kuwa hairuhusiwi na haitaruhusiwa tena kwenda Lindi,Mtwara na maeneo mengine kuchukua mateka na kwamba mateka wote waliochukuliwa na wangoni waachiwe huru.

Baada ya wajerumani kutoa tamko hilo ndipo Nduna Songea Mbano alipojitokeza waziwazi na kusimama kujibu hoja iliyotolewa na wajerumani kuhusiana na tamko hilo.

Nduna Songea Mbano alisema kuwa utawala wa kabila la wangoni hauwezi kutekeleza tamko hilo na kwamba msimamo wao ni kutoutambua utawala mpya wa kijerumani na tamko lao.

Aliendelea kusema kuwa ujio wa utawala wa wajerumani na kutoa tamko hilo kwa wangoni  una lengo la kudhoofisha utawala wa Machifu na Manduna katika maeneo yao kwa kufuata kanuni zao za kimila na kitamaduni.

Kuanzia hapo wajerumani walimuona Nduna Songea Mbano kuwa ni mtu hatari sana katika utawala wao mpya na walimuweka alama maalumu na kuanza kumfuatilia nyendo zake.

Kwa sababu alionekana kuwa kiongozi shupavu na mwenye misimamo mikali na anayezingatia heshima na utu wa kabila lake bila kuyumbishwa.

Alionekana kuwa ni mtu wa pekee mwenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi katika mazingira yoyote kwa kushirikiana na wananchi wake ambao walikuwa wana mheshimu sana na kumsikiliza.

Maligissu anaeleza kuwa Nduna Songea Mbano alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwaunganisha wananchi wake na kuwa na umoja, upendo na mshikamano na kwamba alikuwa akiwaelekeza jambo wanalifanya kwa umakini na kwa ukamilifu.

Anaendelea kusema kuwa kuanzia hapo Nduna Songea Mbano aliendelea kujizolea umaarufu mkubwa na wajerumani baada ya kuona hivyo na kitendo cha nduna Songea kutamka kuwa yupo tayari kwa lolote lile na hawezi kukubali kuona tawala za kiafrka zinadharauliwa na wakoloni kwa namna yeyote ile.

Waliamua kuwaalika Machifu na Manduna wote Julai 13 mwaka 1897 Bomani kwa mkuu wa Wilaya wa kwanza katika nchi ya ungoni ambaye pia mkuu wa jeshi la wajerumani katika nchi ya ungoni Luteni Engelhardt na kuwaambia kuwa mtu yoyote katika eneo lake atakaye kaidi amri yeyote  kutoka kwa uongozi mpya wa wajerumani basi atapigwa risasi, kunyongwa hadi kufa au kufungwa maisha .

Siku hiyohiyo Machifu na Manduna walichukuliwa hadi juu ya mlima wa shabaha wa chandamari uliopo katikati ya mji wa Songea na kuwaonyesha nguvu ya risasi inavyoweza kufanya kazi katika mwili wa binadamu na kwamba silaha za kijadi na kimila za wangoni haziwezi kufua dafu mbele ya silaha hizo.

Licha ya wajerumani kutoa  mkwara na vitisho vingi Nduna Songea Mbano aliendelea kushikilia msimamo wake wa awali wa kuchukia utawala wa wajerumani na kuutetea utawala wa kiafrika mpaka vilipo kuja kutokea vita vya Majimaji.

Nduna Songea Mbano alitoa ushindani mkubwa sana katika vita hivyo na alionyesha ustadi mkubwa kwenye mapigano na katika sehemu zote ambazo wajerumani walipigana wameandika kuwa hawakupata ushindi mkubwa kama waliopata katika Mkoa wa Ruvuma zamani nchi ya ungoni.

Ambapo viongozi wao hawa kuwa wanafiki kwani walijitoa kikwe likweli kusaka ukombozi wa kweli na hadhi ya tamaduni zao mpaka dakika ya mwisho, ndio maana idadi ya watu walionyongwa katika historia ya nchi yetu walitoka katika himaya ya Nduna Songea Mbano na ushahidi upo wazi kuwa watu 67 walihukumiwa kunyongwa hadi kufa akiwemo Nduna Songea Mbano.

Katika kuonyesha kuwa Nduna Songea Mbano alikuwa na uwezo wa kufanya mambo kwa uweledi mkubwa bila kusaliti dhamira yake kuanzia mwaka 1897 alianza kuandaa jeshi lake la kupambana na utawala wa wajerumani.

Akaanza kuchukua watu wake na kuwapeleka juu ya mlima wa chandamari, kufanya nao mkutano na kutoa mafunzo ya kivita na kuwaelekeza kwa nini wanawachukia wajerumani.

Katika mlima huo ndipo alipoeleza kwa kina madhara ya kuukubali utawala wa wajerumani na kutoa ahadi kwa wananchi wake ya kuwaondoa wajerumani kwa lazima na kwamba alisema kuwa eneo hilo ni lao na wamekuwa wakiishi siku zote chini ya utawala wao sasa inakuwaje waletewe utawala mpya wakati hawahuitaji.

Chokochoko hizo zilizaa vita vya Majimaji na wakati mapigano yakiendelea wajerumani walianza kumtafuta Nduna Songea Mbano ili wamkamate na kufanya nae mazungumzo ya maridhiano.

Kumbe Songea Mbano alikuwa amejificha kwenye pango kubwa lililopo kwenye mlima wa chandamari na usiku hukutana na askari wake nje ya pango hilo na kuwapa mafunzo zaidi ya kivita.

Maligissu anaeleza kuwa Nduna Songea Mbano alikuwa anaishi na Ndugu zake katika eneo la Mateka lililopo katika eneo la Manispaa ya Songea na wakati wa vita ndipo Songea Mbano alikuwa anajifisha katika pango hilo ili wasimkamate mpaka atakapotimiza malengo yake.

Wajerumani walipoona wanaendelea kupata madhara makubwa kutokana na vita hivyo waliamua kuwakamata ndugu na familia yake, chifu Mputa Gama na Manduna wengine na kuwafunga gerezani kwa lengo la kumdhoofisha Nduna Songea Mbano.

Baada ya wajerumani kumdhoofisha Nduna Songea Mbano alipata taarifa zote na akaamua kutoka kwenye pango hilo na kwenda kwa wajerumani na kutaka watu wake waachiwe ili mapigano yaendelee.

Ndipo naye alipokamatwa na kuwekwa gerezani na kwamba utawala wa wajerumani waliamua kuwa hukumu wafugwa hao kunyogwa hadi kufa akiwemo chifu wa kabila la Wangoni.

Wafungwa hao waliamuliwa kuchimba shimo kubwa bila kujua kuwa shimo hilo ndilo litakalotumika kuwa kaburi lao na ilipofika siku ya kunyongwa walinyongwa kwa zamu siku mbili na maiti zao kwenda kuwekwa kwenye kaburi hilo hadi walipofikia 66 ndipo walizikwa kwa pamoja kwenye kaburi hilo.

Nduna Songea Mbano walimuacha ili aweze kuwasaidia kufikisha malengo yao kwa wananchi kwani waliamini kuwa yeye ni kiongozi jasiri na anayependwa na watu wake na kusikilizwa vizuri.

Toka siku hiyo walipomuacha bila kumnyonga Nduna Songea Mbano aliwasumbua sana wajerumani na kutaka naye anyongwe kama ndugu zake kwani haoni sababu ya yeye kuishi wakati ndugu zake wamekufa na kusema kama hawataki kumnyonga basi hataki kula wala kunywa  chochote mpaka afe.

Ndipo wajerumani walipoamua kumnyonga na kumzika katika kaburi la pekee yake wakiamini kuwa ni mtu wa pekee mwenye ushujaa na maamuzi mazito na misimamo isiyoyumba na walimuenzi kwa kubadilisha jina la mji wa Ndonde na kuubatiza jina la Songea ambapo mpaka sasa linatumika kuuita mji huo wenye hazina kubwa ya historia na utalii wa kitamaduni

Kila mmoja wetu hana budi kujiuliza ni mafundisho yepi anaweza kuyapata katika historia ya nchi yetu na mchango mkubwa alioutoa Nduna Songea Mbano na je kizazi kilichopo tunao ule moyo wa ushujaa , uzalendo heshima na usawa kama ilivyo kuwa kwa mababu zetu basi inatupasa tutimize wajibu wetu kikamilifu ili vizazi vijavyo viweze kunufaika na uwepo wetu duniani.


Mwandishi wa makala hii
Anapatikana kwa simu namba  - 0755 – 335051

STEPHANO MANGO

Mwandishi wa Habari wa Kujitegemea Songea  Stephano Mango akiwa anatafakari Jambo nje ya Hotel ya Ok 92 ilyopo Songea Mjini

WAANDISHI WA HABARI

Mwenye Miwani Ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi wa IPP Media Gideoni Mwakanosya akiwa na Mwandishi wa Kujitegemea Stephano Mango Wakiwa Nje ya Chuo Cha EASY TECH. COMPUTER TRAINING CENTRE Kilichopo Songea Mjini.