About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Monday, July 4, 2011

UWAJIBIKAJI WA HALMASHAURI NI NGUZO MUHIMU KWA MAENDELEO NCHINI
Na Stephano Mango,Songea
HALMASHAURI ya Wilaya ya Songea ni moja kati ya Halmashauri tano za mkoa wa Ruvuma ambayo ilianzishwa julai 1,mwaka 2002 chini ya sheria namba 7 ya Serikali za mitaa ya mwaka 1982

Eneo la mamlaka ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea ni kilometa za mraba 16,727.143 ambapo inakadiliwa kuwa na jumla ya watu 188,368 ikiwa wanaume 96,465 na wanawake 91,903 ambao wanaishi katika Vijiji 63 vyenye kufanya kata 17 na Tarafa 3

Halmashauri hiyo ina Madiwani 23 kati ya hao 17 ni wa kuchaguliwa, 5 wawakilishi Viti Maalum na 1 kwa nafasi yake Mbunge na kwamba Halmashauri ina maeneo matatu ya mamalaka ambayo ni Serikali za Vijiji,Kamati ya Maendeleo ya Kata(WDC)  na Baraza la Madiwani ambalo ndilo mamlaka ya juu kabisa katika Halmashauri hiyo

Akizungumza na gazeti hili Ofisini kwake hivi karibuni  Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Anna Mbogo alisema kuwa Halmashauri ina jumla ya watumishi 1,673 kati ya watumishi 1,932 wanaotakiwa kuwepo kwani kwa sasa inaupungufu wa watumishi 257 wa fani mbalimbali

Mbogo alisema kuwa upungufu mkubwa upo katika sekta ya elimu ambayo inaupungufu wa wa Walimu 142 ikifuatiwa na sekta ya afya watumishi 61,utawala 28,maji 9,kilimo 8,ujenzi 6 na mifugo 5

Alisema kuwa katika suala la uchumi Halmashauri hiyo inategemea zaidi kilimo kwani wakazi wengi wa Halmashauri hiyo wanapata riziki zao kutokana na shughuli za kilimo na kwamba mapato ya Halmashauri kwa asilimia 90% hutoka kwenye sekta hiyo

Alifafanua kuwa Halmashauri imekuwa ikitekeleza shughuli zake kwa kuzingatia maelekezo na ahadi zilizomo katika Ilani ya uchaguzi ya chama tawala ambapo imegusa mambo mengi muhimu

Alisema kuwa pia wamekuwa wakitekeleza malengo ya Mpango wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini(MKUKUTA) ambayo ni Kukuza Uchumi,Kuimarisha huduma za Jamii,Uwajibikaji na Utawala bora,Kushirikisha jamii katika hatua zote za kuboresha hali zao za maisha kwa kuinua mapato yao,ya Halmashauri na Taifa kiujumla

Alieleza kuwa asilimia 90% ya ardhi katika Halmashauri hiyo inafaa kwa kilimo ambapo mazao ya chakula yamekuwa yakistawi vizuri kama vile mahindi,maharage,mpunga,viazi vitamu na mihogo na kwa mazao ya biashara yanayolimwa na kustawi vizuri ni kama vile tumbaku,korosho,kahawa,karanga,ufuta na nazi

Alisema kuwa kilimo cha umwagiliaji kwa zao la mpunga kinaendelea kupewa kipaumbele hasa baada ya zao la tumbaku kuwa na utata katika soko ambapo upanuzi,uboreshaji na uendelezaji wa shughuli za kilimo ndio njia inayoweza kukuza uchumi na kuondoa umasikini katika Halmashauri yetu

Alikiielezea sekta ya mifugo alisema kuwa Halmashauri ina jumla ya ng’ombe 33,123,mbuzi 57,089,nguruwe 27,159,sungura 496,bata 8,618,mbwa 5918,paka 294,punda 326 na kuku 225,908 kati ya hao kuku wa kienyeji ni 217,609 na wakisasa ni 8,299 ambapo jitihada zinaendelea kuongeza mifugo na mazao yake

‘Tuna majosho 18,yanayofanya kazi ni 6,yasiyofanya kazi ni 12,pia kuna josho la kupuliza 1(Spray race) ambalo linafanya kazi na majosho 6 yanajengwa sasa na kwamba tuna machinjio ya kati(Min Abattoiirs) katika mji mdogo wa Madaba ambayo inafanya kazi”alisema Mbogo

Alisema kuwa katika sekta ya Maliasili Halmashauri ina misitu ya hifadhi 9 ambapo misitu 6 ni ya Serikali kuu ambayo ni Wino,Msitu wa nishati Songea,Chabruma,Machinjioni,Igawisenga na East-West Matogoro na misitu ya hifadhi inayomilikiwa na Halmashauri ni mitatu nayo ni Maposeni,Gumbiro na Lihanje

Alifafanua kuwa shughuli za uwindaji zitaendelea kupewa kipaumbele kwa kuanzisha vitalu zaidi na kwamba lengo la upandaji wa miti katika mwaka 2010/2011 ilikuwa ni kupanda miti1,500,000 ambapo hadi kufikia mei 2011 jumla ya miti 750,00 imeoteshwa na upandaji wa miti hiyo unaendelea ili kufikia lengo kusudiwa

Mbogo alieleza kuwa katika mpango wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini Halmashauri imekuwa ikiziangalia kwa umakini vyama vya ushirika vya mazao 8,chama kikuu cha ushirika 1,vyama vya akiba na mikopo vya kata 12 ambapo Saccos hizo zinajumla ya wanachama 11,795,hisa zao ni Shs. 167,918,850,akiba na amana jumla ya Shs.997,860,024 na kwamba Saccos hizo zimeweza kutoa mikopo yenye jumla ya Shs.2,262,831,160

Alifafanua kuwa pamoja na Saccos 12 za kata pia wafanyakazi wa Halmashauri wana Saccos 2 na makundi maalumu(wanawake) 1 ambazo zinajumla ya wanachama 2,597,hisa za Shs 70,204,490,akiba na amana ya Shs 773,808,775 ambapo mikopo iliyotolewa kwa mwaka 2010/2011 ni jumla ya Shs 1,806,100,366

Alisema kuwa kwa upande wa sekta ya ardhi Halmashauri inaendelea kupunguza kero za migogoro ya ardhi kwa kuelimisha wananchi sheria ya ardhi namba 5 ya vijiji ya mwaka 1999 ,pia inaendelea kuandaa matumizi bora ya ardhi katika vijiji

Alieleza zaidi kuwa Halmashauri ina jumla ya barabara zenye urefu wa kilometa 531 ambazo ni za changarawe na udongo ambapo kwa msimu wa 2010/2011 barabara nyingi ziliharibika na mvua lakini zimetengenezwa kwa kushirikiana na wananchi na sasa zinapitika vizuri

Kwa upande wa sekta ya elimu,Mbogo alisema kuwa Halmashauri inajumla ya walimu 771 wanaofundisha wanafunzi 43,642(msingi 37,161,na awali 6,481) ambapo shule za msingi zipo 94,pia kuna upungufu wa walimu 200 kwa kigezo cha uwiano wa Mwalimu 1 wanafunzi 45 pia kuna vyumba vya madarasa 709 kati ya mahitaji ya vyumba 982 ambapo nyumba za walimu zipo 360 kati ya nyumba 969 zinazohitajika na kwamba mikakati mbalimbali inaendelea kufanywa kutatua tatizo hilo

Akielezea elimu ya Sekondari alisema kuwa kuna jumla ya shule 26 kati ya hizo sekondari 23 za Serikali,3 zinamilikiwa na madhehebu ya dini na watu binafsi nako pia kuna changamoto mbalimbali ambazo zinaendelea kuwekewa mikakati ya kuboresha zaidi
Akizungumzia sekta ya afya alisema kuwa Wilaya ina Hospital 1 inayomilikiwa na Misheni,vituo vya afya vya Serikali 2 ambavyo ni Muhukuru na Madaba,Zahanati 36 kati ya hizo 13 zinamilikiwa na Misheni na 23 zinamilikiwa na Halmashauri

Alifafanua zaidi kuwa vituo hivyo vinatoa huduma kimgawanyo wa uwiano wa kitanda kwa wagonjwa 1:591,uwiano wa kituo cha afya kwa idadi ya watu 1:50,236,uwiano wa Zahanati kwa idadi ya watu1:5,494 pamoja na unafuu wa upatikanaji wa huduma za afya bado kuna changamoto nyingi katika magonjwa ya malaria,kuharisha,kifua kikuu,HIV/UKIMWI

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema kwa upande wa sekta ya maji wananchi 114,500 sawa na asilimia 60% ya wakazi wote wa Halmashauri ya Songea wanapata maji safi ambapo mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano wa wananchi,Serikali kuu, Halmashauri na wahisani na kwamba juhudi za kusambaza maji kwa wakazi waliobaki zinaendelea

Alisema kuwa katika mpango wa maendeleo ya vijana kuna jumla ya vikundi 100 vimepata mafunzo ya ujasiliamali yatakayo wawezesha kujiajiri katika sekta binafsi,vikundi 6 zimepata mkopo wa Shs.23,089,750 na mtandao wa vijana wenye lengo la kujenga umoja kati yao,elimu ya Ukimwi,madawa ya kulevya na kupambana na umasikini umesajiliwa

Alisema kuwa kwa upande wa utawala bora vikao vyote vya kisheria katika ngazi zote vimekuwa vikifanyika,uwazi na uwajibikaji katika mapokezi ya fedha na matumizi yake limefanyika kwani wananchi wamekuwa wakishirikishwa kwa ukaribu sana

Alifafanua kuwa mapato ya Halmashauri hutokana na ruzuku ya Serikali kuu na vyanzo vyake vya ndani ambavyo ni ushuru wa mazao,masoko,magulio na mapato mengine ambapo kwa mwaka 2010/2011 Halmashauri ilikasimia kukusanya Shs 10,145,866,000 kutokana na fidia ya vyanzo vya mapato,ruzuku ya mishahara na ruzuku ya matumizi ya kawaida

“Hadi mei 31,2011 Halmashauri ilikuwa imekusanya Shs 7,776,727,211.84 sawa na asilimia 76.65% ya mapato yote na ili kuongeza mapato zaidi kwa mwaka wa 2011/2012 Halmashauri imejipanga kutekeleza mikakati mingi”alisema Mbongo

Alisema kuwa miongoni mwa mikakati hiyo ni kupitia upya mikataba ya mawakala kwa kuwawekea malengo ya ukusanyaji ushuru na kuboresha mfumo wa kuwasimamia mawakala hao,kutungwa kwa sheria ndogo katika kila chanzo,timu ya mapato  kuwajibika kuratibu shughuli zote,mfumo wa motisha kwa wakusanyaji mapato wazuri utadumishwa ili kuleta ushindani na mikakati mingine mingi

Alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2010/2011 Halmashauri iliomba kuidhinishiwa kutumia Tshs 4,684,201,400 ambapo hadi mei 31 zilipokelewa Shs 3,347,542,178.30 ikiwa ni sawa na asilimia 71.5% ya fedha iliyokusudiwa na kwamba katika kipindi hicho Halmashauri ilitumia Shs 2,336,884,172.83 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo sawa na asilimia 49.9%

Ni wazi kuwa endapo Halmashauri nchini zikiwajibika kikamilifu katika kusimamia miradi ya maendeleo wananchi watakuwa na imani na serikali yao na malalamiko yatapungua kwa kiasi kikubwa na kufanya amani tuliyonayo iendelee kustawi

Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana kwa 0755-335051
Baruapepe;stephano12mango@yahoo.com


Mratibu wa Kampeni ya Ushindi ni Lazima Martha Lunyerere akipita mbele ya watazamaji katika uwanja wa majimaji wakati timu zikichezwa