About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Monday, December 5, 2011

ROA NA HARAKATI ZA KUHAMASISHA MIFUKO YA JAMII YA WATOTO WAISHIO MAZINGIRA HATARISHI KATIKA JAMII ZETU

                         Mwenyekiti wa ROA Methew Ngarimanayo
Watoto wakionyesha vipaji vyao wakati wa mahafari ya darasa la Saba katika Shule ya Msingi Sabasaba iliyopo mjini Songea

Na Stephano Mango,Songea

MCHANGO wa asasi zisizo za kiserikali ni mkubwa sana katika jamii na Taifa kwa ujumla hasa katika harakati za kupinga ujinga,maradhi na umasikini unaowakabili wananchi wengi
 
Asasi hizo zimekuwa zikitoa huduma za kijamii katika makundi ya watu mbalimbali hasa pale Serikali inapokuwa imeelemewa na mzigo wa matatizo yaliyopo katika jamii husika
 
Kwa msingi huo pamoja na mambo mengine ndio iliopelekea Serikali kuruhusu kuanzishwa kwa asasi hizo ili waweze kushirikiana nazo kutatua kero mbalimbali zilizopo kwenye jamii kuanzia ngazi ya mitaa,vitongoji,kata hadi Taifa
 
Baadhi ya asasi zimekuwa zikifanya kazi kubwa ya kulea watoto yatima,wanaoishi katika mazingira hatarishi,kuhamasisha wananchi kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi,kutunza mazingira na namna ya kupambana na umasikini kwa kuanzisha miradi midogo midogo kwa njia ya vikundi vya uzalishaji mali
 
Katika harakati za kutokomeza umasikini,baadhi ya asasi hizo zimekuwa zikiwajengea uwezo wananchi kwa kuwapatia mafunzo juu ya usimamizi na uendeshaji wa shughuli za kiuchumi na kuwapatia mitaji ya kuanzia ili waweze kujikomboa na umasikini
 
Mara nyingi asasi hizo ili ziweze kuendelea kuendesha shughuli zake hutegemea misaada ya kifedha kutoka kwa wahisani mbalimbali wa ndani na wa nje kwa ustawi wa jamii wanazozishughulikia
 
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Mwenyekiti wa Shirika lisilo la Kiserikali la Ruvuma Orphans Association (ROA)  Mathew Ngalimanayo alisema kuwa shirika hilo lilinzishwa Aprili mwaka 1999 na kusajiliwa rasmi Aprili 6 mwaka 2001 na kwamba lengo kubwa la kuanzishwa kwa Shirika hilo ni kushughulikia changamoto wanazokabiliana nazo watoto yatima na watoto waishio katika mazingira hatarishi.
 
Ngarimanayo alisema kuwa lengo jingine ni kuvijengea uwezo vikundi mbalimbali vya wajasiriamali ili viweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kushiriki kikamilifu katika michakato mbalimbali ya maendeleo
 
Ikiwa ni pamoja na kutekeleza,kufuatilia na kutathimini utekelezaji wa sera mbalimbali za maendeleo na shughuli zinazofanywa na wadau mbalimbali ikiwemo serikali katika ngazi zote za utawala na utendaji

Alisema kuwa shirika hilo pia lilianzishwa kushughulikia changamoto ziletwazo na ugonjwa hatari wa Ukimwi katika jamii  kwa kushirikiana na Serikali,na wadau wengine wa maendeleo katika kufanikisha hilo katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu kwa kushirikiana na timu ya watoa huduma kwa wagonjwa majumbani limefanikiwa kuwatambua wagonjwa 516 kati ya hao wagonjwa 489 wamepatiwa huduma na wagonjwa 268 wanaendelea kupata huduma katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea na Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambapo jumla ya Tsh. 13,456 zimetumika kugharamia mahitaji ya wagonjwa hao pamoja na mafunzo ya namna ya kuishi na wagonjwa hao

“Tumefanikiwa kuwahudumia wagonjwa 489 kati ya wagonjwa 516 waliotambuliwa ambapo wagonjwa 29 wamepata nguvu na wanaendelea vizuri na shughuli zao za kila siku na wagonjwa 268 wanaendelea kuhudumiwa majumbani na pia Roa imefanikiwa kuwapatia huduma watoto yatima 234 walioko katika mfumo wa Elimu kwa kulipa karo zao,kuwapatia sare,viatu,madaftari na mikoba pamoja na huduma ya afya”.

Alifafanua kuwa kwa kipindi hicho watoto waishio kwenye mazingira hatarishi waliofikiwa na huduma ya elimu ni watoto 234 ikiwa watoto wa shule ya msingi 145,watoto wa sekondari 84,watoto wa elimu ya juu 3 na watoto wa shule za ufundi 2 ambapo jumla ya Tsh 15,630,500/= zimetumika kugharamia mahitaji ya kielimu ya watoto wao
Alieleza kuwa hakuna taasisi ama kikundi chochote cha watu kinachoweza kumaliza changamoto,kero,na matatizo yanayohusiana na Vvu/Ukimwi na watoto waishio katika mazingira hatarishi bali kwa wadau wote kuungana na kushughulikia jambo hilo kwa kushirikiana hivyo ni vema kila mdau akatimiza wajibu wake kadri ya uwezo na nafsi yake 

Amezitaja changamoto wanazokutana nazo kuwa ni ukosefu wa fedha za kutosha wa kuendeshea shughuli za shirika hilo kadiri ya malengo na mipango iliyopo,mwitiko hasi wa baadhi ya wananchi na watendaji wa Serikali kuhusu dhana ya mifuko ya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi
Ngarimanayo alieleza kuwa kutokana hilo Roa kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la The foundation for civil society la Jijini Dar es Saam limefanikiwa kuhamasisha wananchi wa mitaa na kata katika Manispaa ya Songea na Halmashauri ya Wilaya ya Songea kufungua na kuiendesha mifuko ya kusaidia watoto yatima na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwenye maeneo yao.
 
Alisema wamefanikiwa kuwakumbusha wananchi juu ya wajibu wao wa kimsingi wa ulinzi,matunzo na malezi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa kila mtaa kuwa na kamati ya kuratibu na kusimamia masuala ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuanzisha mfuko maalumu wa kila mtaa wa kuhudumia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na watu wa makundi mbalimbali katika kata hizo wamehamasishwa juu ya masuala ya Vvu/ Ukimwi na kuendesha zoezi la upimaji Vvu/Ukimwi kwa hiyari.

Alifafanua kuwa suala la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ni bomu kubwa ambalo linazinyemelea familia zetu na taifa kwa ujumla hivyo kila mwananchi anatakiwa aamke na kutambua kuwa watoto hao wanaongezeka siku hadi siku katika jamii zetu ni jukumu la wadau wote kuwahudumia kwa kuwapa mahitaji muhimu ya kibinadamu
“Kila mdau popote alipo aliangalie suala hilo na achukue hatua stahiki ya kupunguza wimbi hilo kwani kwasasa takwimu za watoto hao mkoani Ruvuma imefika jumla ya watoto 32,532 ambapo sababu zinazosababisha hali hiyo ni pamoja na mimba za utotoni,kuzaa nje ya ndoa,umasikini wa kipato katika familia,mifarakano ya wanandoa,magonjwa mbalimbali,ajali za barabarani na maafa mengine “alisema Ngarimanayo
Alisema kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii mwaka 2006 na 2008 ilifanya zoezi la utambuzi wa watoto hao katika Wilaya za Mkoa wa Ruvuma na wakaweka utaratibu ambao wananchi walipaswa kuchukua na kuhakikisha watoto hao wanasaidiwa katika jamii wanamoishi
Alieleza zaidi kuwa katika ngazi za mitaa,Kata,Wilaya viliwekwa vyombo ambavyo vinaweza kukaa na kujadili kwa kina masuala ya watoto hao na kuweka mikakati ya kumaliza tatizo hilo kwa kutumia Kamati za Ukimwi kuanzia ngazi ya mitaa hadi Wilaya kwani Kamati hizo zingekuwa zinafanya kazi yake kikamilifu tatizo la watoto hao lingekwisha
Ameitaja mipango ya shirika hilo ya baadaye kuwa ni kuendelea kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuanzisha mifuko ya jamii ya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi,kugharamia gharama za masomo kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapatia karo,sare za shule,vifaa vya darasani na gharama zingine zinazohusiana na masuala ya elimu na kujenga uelewa kwa jamii juu ya haki na wajibu wa watoto yatima na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Katika hilo Serikali inatakiwa kusimamia kikamilifu mpango wa mifuko ya jamii ya kusimamia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi ili waweze kusaidiwa na jamii wanamoishi kwa kutumia kamati maalumu ya kuratibu watoto hao kuanzia ngazi ya mitaa hadi Wilaya ili kuweza kuleta ustawi na maendeleo ya watoto hao na hilo linawezekana endapo kila moja akitimiza wajibu wake
Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana 0755-335051
www.stephanomango.blogspot.com

AKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUKUTWA NA MENO YA TEMBO

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda
Na Gideon Mwakanosya, Songea

JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma linamshikiria Fundi magali wa Kampuni ya Sumry Mjini Songea Ally Makumba (42) Mkazi wa Bombambili Manispaa ya Songea akikabiliwa na tuhuma za kukutwa na Vipande 12 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 2.23 ambayo thamani yake ni shilingi milioni 2 na 45 elfu mia tatu kumi na mbili kwenye buti la basi la Kampuni ya Sumry lilikuwa likijiandaa kwa safari ya kutoka Songea kwenda Jijini Da es Salaam.

Akizungumza na mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com jana Ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amesema kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 29 mwaka huu majira ya saa 11 alfajiri huko kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi cha Mjini Songea.

Kamuhanda amefafanua kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio askari Polisi ambao walikuwa doria kwenye eneo la Kituo Kikuu cha basi walipata taarifa toka kwa Raia mwema kuwa kwenye basi la Sumry linalotarajiwa kuondoka kwenda Jijini Dar es Salaam kuna mtu ameweka mzigo ambao uko ndani ya begi ambalo ndani yake kuna meno ya tembo.

Ameeleza zaidi kuwa baada ya Polisi hao kupata taarifa kutoka kwa raia wema walikwenda kwenye eneo ambako basi hilo limeegeshwa huku abiria wakijiandaa kuingia kwa safari ya kuelekea Jijini Dar es Salaam na kuanza kufanya ukaguzi ambapo baadae walifanikiwa kulikuta begi kwenye buti ambayo ndani yake kulikuwa kuna vipande 12 vya meno ya tembo yenye uzito wa kilo 2.23 na thamani yake ni Milioni 2.45312 .

Amesema kuwa baada ya kulibaini begi hilo  Polisi walianza kupeleleza kuwa mzigo huo  ulikuwa umewekwa na nani au abiria gani na badea walifanikiwa kumkamata fundi Magali wa Kampuni hiyo ambaye anadai kuwa alikuwa ameuweka mzigo huo muda mfupi tu kabla ya askari kukamata meno ya tembo kwenye basi hilo lente namba za usajili T777BVD ambalo lililazimishwa kwenda kwenye Kituo Kikuu cha Polisi kwaajili ya Upelelezi zaidi.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Kamuhanda Polisi inaendelea kufanya upelelezi zaidi wa kina ili kubaini tukio hili na kwamba utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.

MWISHO

VIONGOZI WA DINI WAOMBWA KUZUIA KUFUNGISHA NDOA KWA WATU WASIOPIMA VIRUSI VYA UKIMWI

Na Steven Augustino, Tunduru

SERIKALI imewataka Viongozi wa Dini waliopewa mamlaka ya kubariki Ndoa kuachana na tabia za kufungisha ndoa kwa waumini wao ambao wataenda kuomba kupatiwa huduma hiyo huku wakiwa hawajapima virusi vya Ukimwi,

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Madaha wakati akiongea na wananchi waliojitokeza katika Maadhimisho ya siku ya Kutafakari mikakati ya kupambana na janga la Ukimwi yaliyofanyika Kiwilaya Katika Kijiji cha Makande kilichopo katika Tarafa ya Lukumbule Wilayani humo.

Pamoja na agizo hilo pia Madaha aliwataka Wazazi na Walezi kuto
ziachia Televisheni na Mitandao ya Kompyuta iwalelee Watoto wao bali wao wenyewe watimize wajibu wao katika utoaji wa malezi yenye maadaili yanayo endana na maudhui ya ki Africa na kuwaepusha watoto wao kupata Mimba za utotoni na Virusi vya Ukimwi .

Akifafanua hotuba hiyo Madaha alisema kuwa endapo Mashekhe na
Mapadre watasimamia kwa vitendo wataisaidia jamii kujenga tabia za kupima afya zao kwa hiari ili kujitambua na kupanga mikakati ya maisha bila kuwa na mashaka.

Sambamba na maagizo hayo Dc, Madaha pia alitumia nafasi hiyo kutoa elimu ya Ukimwi kwa kuwataka Makungwi na Manyakanga kuachana na tabia za kutoa masomo yasiyo endana na maadili zikiwa ni juhudi za mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Aliseam hivi sasa makungwi na manyakanga hao wamekuwa wakitoa elimu inayowapatia udadasi hasa watoto wa kike na kuwataka kwenda kujaribisha kwa vitendo hali ambayo imekuwa iki wasababishia madhara makubwa yakiwemo ya kupata Mimba na maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi.

Akizungumzia msimamo wa Serikali juu ya mapambano hayo Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Jalia Msangi alisema kuwa ingawa msimamo wake hauendani na maadili ya Dini aliwahimiza
wananchi kuvaa na kutumia kinga mbadala iliyoidhinishwa na wataalamu wa Afya ili kujikinga na maambuikizi mapya ya VVU na Ukimwi.

Alisema katika kukabiliana na Janga hilo Halmashauri yake imekuwa ikiongeza juhudi za kughalamia utoaji wa elimu Sekondari kwa Watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu 461 pamoja na kutoa huduma kwa Wajane na Wagane 20 kuanzia mwaka 2009.

Awali akisoma Risala ya maadhimisho hayo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Tunduru Dkt. Alex Kazula, Mganga kutoka kitengo cha Ushauri nasaha Dkt. Modestus Ponera  alisema kuwa baada ya Serikali kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za Upimaji wa VVU na UKIMWI watu wengi zaidi wamekuwa wakijitokeza ili kupatiwa huduma hiyo.

Dkt. Ponera aliendelea kueleza kuwa pamoja na kuwepo kwa juhudi hizo idara yake imekuwa ikikabiriwa na changamoto kubwa ya jamii kutobadilitabia za kuachana na ngono zisizo salama, na akaongeza kuwa baada ya idara yake kutoa elimu ya kuachana na Unyanyapaa idadi ya Wagonjwa ambao huenda kupatiwa huduma ya tiba na matunzo imeongezeka kutoka wateja 52 mwaka 2005 hadi wateja 2935 mwaka huu.

Nje ya Ukumbi wa maadhimisho hayo nikakutana na kundi la vijana wa uhamasishaji wa kupima afya kwa hiari la Jipange Pambana na Ukimwi(JIPAU) ambapo Mratibu wa kundi hilo Mchungaji Simoni Magonga akaeleza kuwa hivi sasa Shirika lake limefanikiwa kufungua matawi katika vijiji vyote vya Wilaya hiyo zikiwa ni juhudi za kuisaidia Serikali katika mapambano hayo