MKUU WA WILAYA YA TUNDURU JUMA MADAHA
Na. Augustino Chindiye Tunduru
WAKULIMA wa Kata za, Namasakata, Mtina na Misechela wamelalamika ucheleweshwaji wa mbolea na mbegu za ruzuku kutoka kwa mawakala waliopewa idhini ya kusambaza pembejeo hizo ili kuwawezesha kupanda mazao yao kwa wakati.
Kero hiyo ilibainishwa na wakulima wa vijiji vyote vilivyopo katika kata hizo wakati wakiongea na Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini Alhaji Mtutura Abdalah Mtutura alipofanya ziara ya kuwashukuru kwa kumchagua na kuwa mwakilishi wao Bungeni katika kipindi cha miaka mitano.
Kilio hicho ambacho kilithibitishwa na madiwani wa Kata hizo Saidi Njalanjala wa Kata ya Misechela, Mahamudu Katomondo wa Kata ya Mtina na wa Kata ya Namsakata Masache Masache walimweleza Mbunge huyo kuwa kitendo cha ucheleweshwaji wa pembejeo hizo kinavunja ari ya wakulima katika maandalizi ya kilimo katika msimu huu.
Akijibu malalamiko hayo Mbunge huyo aliwataka wakulima hao kuendelea na maandalizi ya mashamba yao na kuahidi kulifutilia tatizo hilo kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi baada ya kurejea Tunduru mjini.
Aidha Mtutura aliwahimiza wakulima hao kuzingatia maelekezo yanayo tolewa na wataalamu wa kilimo ili kulima kilimo chenye tija na akatumia nafasi hiyo kukemea tabia ya baadhi ya wakulima hao kufanya shughuli zao katika vyanzo vya mito hali iliyosababisha mito ya Vijiji vya Mchengamoto na Amani ambayo ilikuwa ikitiririsha maji muda wote kukauka.
Akizungumzia tatizo la ucheleweshwaji wa usambazaji wa mbolea kwa Wakulima Mwenyekiti wa kamati ya Pembejeo wa Wilaya ya Tunduru, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Madaha alisema kuwa tayari kamati yake imekwisha chukua hatua za kuwasimamisha uwakala mawakala watatu kati ya mawakala sita waliokuwa wamepitishwa na kamati hiyo baada ya kushindwa kutekeleza makubaliano yao .
Madaha aliwataja mawakala hao kuwa ni Halima Luambano,Joseph Kalaliche na Crispini Mumba baada ya kubaini kushindwa kupeleka pembejeo hizo wala kuweka katika maduka yao hali iliyo onesha kuwa mawakala hao walilenga kuchakachua Vocha kutoka kwa wakulima.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo hivi sasa kamati hiyo imebakiwa na mawakala watatu Zubery Namahala, Ally Chimwala, na Augustino Lukosi ambao tayari wamekwisha anza kusambaza Pembejeo hizo katika vijiji vyote ili kuwawezesha wakulima kupata huduma hiyo bila usumbufu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na afisa Kilimo wa Wilaya ya Tuinduru Chiza Marando alisema kuwa jumla ya wakulima 23046 wamepangwa kunufaika kupitia mpango wa mbolea ya Ruzuku huku mahitaji ya wakulima wa wilaya hiyo yakiwa ni tani 4375 za Mbolea za kupandia na kukuzia na tani 595 za mbegu.
Akiongea kwa niaba ya mawakala waliofutiwa uwakala wao Crispin Mumba mbali na kukiri kuwepo kwa tukio hilo alisema kuwa yeye na mawakala wenzake waliamua kuachana na biashara hiyo baada ya kubaini kuwa Biashara hiyo katika msimu huu haina faida kwa wafanyabiashara wenye mitaji midogo.
Alisema katika msimu huu Bei elekezi ni Tsh.70500/= kwa mfuko mmoja wa Mbolea na kwamba katika bei hiyo wakala amewekewa Tsh. 500 kama faida yake katika kila mfuko atakao uuza wakati huo huo yeye atakabiliwa na gharama za uchukuzi, kulipa kodi ya chumba cha kuhifandhia mzigo wake, malipo au ujila wa Mlinzi na Mtumishi pamoja na gharama za kushusha na kupakia.
Mwisho.