About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Monday, January 2, 2012

WATU 312 WAFA KWA UGONJWA WA MALARIA WILAYANI TUNDURU



Na Augustino Chindiye,Tunduru
JUMLA ya Watu 312 ikiwa ni sawa na asilimia 44% ya vifo 709 vilivyo tokea Wilayani Tunduru katika kipindi cha mwaka 2010/2011 vilisababishwa na ugonjwa hatari wa Malaria.

Hayo yamebainishwa jana na Mratibu wa Malaria wa Wilaya hiyo Hussen Mrope wakati akiongea na Mawakala wa kubadilisha tabia kwa jamii katika mapambano ya Malaria (CCA) katika Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Sky way Mjini hapa na kuongeza kuwa  ukubwa wa tatizo la ugonjwa wa takwimu za ugonjwa huo zinaonesha kuwa pia wagonjwa 183839 ikiwa ni sawa na asilimia 44 % ya  wagonjwa 4170439 ya wagonjwa waliopata huduma za nje yaani OPD na kurejea majumbani mwao.

Akizungumzia ukubwa wa tatizo la ugonjwa huo Wilayani humo Mrope alisema kuwa jumla ya wagonjwa 15130  sawa na asilimia 30 % ya  wagonjwa 17094 ya wagonjwa waliolazwa katika Vituo vya afya, Zahanati na Hospitali waligundulika kuwa na ugonjwa huo

Baada  ya Afisa huyo kueleza tatizo hilo wajumbe hao wakabainisha changamoto mbali mbali na kuiomba Serikali ya Wilaya hiyo kutekeleza wajibu wao na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wa maduka ya vyakula ambao pia wamekuwa wakiuza Madawa ya Binadamu zikiwemo dawa zinazo tibu Malaria.

Sambamba na ombi hilo pia wajumbe hao wakatumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi hao kufuatilia kero mbali mbali ikiwemo matatizo ya upandishwaji wa bidhaa yakiwemo Madawa ya Binadamu ikiwemo Dawa mseto bila kujali kuwa dawa hiyo imelipiwa ruzuku na  Serikali na inatakiwa kuuzwa kwa bei isiyo zidi Tsh.1000 kwa Dozi ya Mkubwa na Tsh.500 kwa Dozi ya Mtoto.    

Hakimu Kolowa mhamasishaji kutoka katika kata ya Mtina na Hasan Kamtande wa Kata ya Mchoteka ni miomngoni mwa wajumbe waliopaza sauti zao na  kufichua Siri hiyo na kuongeza kuwa endapo hali hiyo haitadhibitiwa mapema jamii kubwa hasa wanaoishi Vijijini wapo katika hatari ya kupata madhara makubwa yatakayogharimu uhai wa Binadamu

Wakifafanua taarifa hiyo wajumbe hao walisema kuwa pamoja na jamii kujenga mazoea ya kupata huduma hiyo katika maduka hayo yaliyopo karibu na makazi yao lakini mazingira ya utunzaji wa madawa hayo hauendani na mazingira yanayotakiwa kutimizwa katika utunzaji wake pamoja na wauzaji wake kutokuwa na elimu juu ya utoaji wa Dawa hizo na utunzaji wake. 

Alipotakiwa kuzungumzia tatizo hilo Mratibu wa Malaria wa Wilaya ya Tunduru Hussein Mrope mbali na kukiri kuwepo kwa tukio hilo alieleza kuwa mbali na wahamasishaji hao kupewa jukumu la kuijulisha jamii juu ya matumizi sahihi ya Dawa mseto yenye Nembo ya Jani aliahidi kuwapatia vitambulisho ambavyo watawapatia mamlaka ya kuanza kuwakamata wafanyabiashara hao.

Awali akifungua mkutano wa magunzo hayo Mwenyekiti wa Shirika lisilo kuwa la Kiserikali (HEDEFO) lililo pewa mamlaka ya kuratibu mapambano ya janga hilo Saidi Mkandu aliwataka wamiliki wa Ngos na Cbos kupendana na kutimiza wajibu wao katika kuihudumia jamii.

Aidha kupitia hotuba hiyo Mkandu alisema kuwa mradi huo wa Miaka miwili unatekelezwa katika Mikoa 9 ya Tanzania Bara chini ya mwamvuli wa ufadhili wa HEALTH FOCUS na Wizara ya Afya na ustawi wa jamii baada ya Mikoa hiyo ukiwemo Mkoa wa Ruvuma kubainika kuwepo kwa maambukizi makubwa ya ugonjwa huo.     

Nae Mratibu wa Mradi huo kutoka katika shirika hilo Nahoda Ameir katika maelezo yake aliwataka Wajumbe hao wa mabadiliko ya tabia kuitangaza Dawa mseto yenye nembo ya Jani kuwa inapatikana katika Hospitali, Zahanati ,Vituo vya afya na katika maduka yote ya dawa kwa bei nafuu ili kuwavutia wananchi na kuwafanya wapenda kuitumia.

Wakijibu kero ya Dawa hizo kuuzwa kwa bei ya juu kwa niaba ya wauzaji wa Maduka ya Dawa muhimu Wilayani humo  Geofrey Nguru ,Yosepha Makita na Lukas Chanangula mbali na kukiri kuuza Dawa hizo kwa bei za juu walidai kuwa hali hiyo imekuwa ikisababishwa na wao kununua madawa hayo kwa bei kubwa.

Walisema endapo hivi sasa watapata dawa hizo zilizo lipiwa ruzuku na Serikali kwa bei nafuu wao wapo tayari kuziuza kwa bei rahisi kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi.

Akifunga mkutano huo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Hospitali ya Serikali ya Wilaya ya Tunduru Dkt. Goerge Chiwangu alisema kuwa mbali na jamii kupatiwa elimu ya kupambana na ugonjwa huo lakini idara yake imekuwa ikikabiliwa na tatizo la kutibu malaria sugu kutoka kwa wateja wake ambayo chanzo chake ni kukaidi maelekezo ya wataalamu na kuacha kumaliza dozi.

 Mwisho