Diwani wa Kata ya Lituhi Adam Mhaiki
Na Gideon Mwakanosya,Nyasa
WANANCHI wa kata ya Lituhi Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma wameanzisha umoja wa wakulima wa kilimo cha umwagiliaji ambacho kitaweza kuwakomboa katika kuondokana na njaa na tatizo la umaskini miongoni mwa jamii
Akizungumza na Mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ jana Diwani wa Kata ya Lituhu Adam Mhaiki alisema kuwa hatua ya wananchi wa kata hiyo ya kuunda umoja huo imekuja baada ya kuona Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Chakula kuleta ushawishi mkubwa wa kuwa na mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika maeneo mbalimbali ya Vijiji vilivyo kandokando y a mto Ruhuhu kwa Wilaya ya Ludewa na Nyasa
Mhaiki alisema kuwa hatua za awali za upimaji wa maeneo ya kilimo cha umwagiliaji tayari zimekwisha fanyika ambapo ukubwa wa eneo hilo lililopimwa ni hekari 2800 na kwamba wakulima waliounda umoja huo ni wa Vijiji vya Mwela Mpya,Nkaya,Kihulu na lituhi
Alieleza kuwa mradi huo ukikamilika unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya mpunga,mahindi,vitunguu,nyanya na mbongambonga na kwamba kwa sasa jitihada zinafanywa kwa kushirikiana na Serikali ya Wilaya ya Mbinga na Wilaya ya Ludewa Mkoani Iringa ambako kuna wananchi wa kata ya Ngerenge kutafuta fedha ambazo zitaweza kusaidia kujenga miundombinu imara ya kilimo cha umwagiliaji katika maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kujenga daraja la kuunganisha wakulima wa wilaya ya Nyasa na Ludewa badala ya kutegemea kivuko kibovu kilichopo eneo la mto Ruhuhu ambacho kwa kipindi cha kiangazi huwa hakifanyi kazi kutokana na uhaba wa maji
Alieleza zaidi kuwa pia mradi huo ukikamilika utaweza kuinua hali za maisha za wananchi wa vijiji hivyo na taifa kwa ujumla kwa kupunguza umaskini wa kipato na njaa kwenye kaya nyingi katika maeneo hayo kwani kwa muda mrefu wananchi wa kata hizo wamekuwa wakitegemea kilimo cha mihogo na shughuli za uvuvi kwa kutumia vitendea kazi duni
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi Kapteni John Komba aliiomba Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Chakula kuhakikisha mradi huo mkubwa unakamilika mapema ili kuondoa kero kubwa ya wananchi wa maeneo hayo
Komba alisema wananchi wamehamasika kujiunga kwenye umoja wa wakulima ili waweze kupata nguvu ya pamoja ya mikopo na misaada kutoka kwenye mfuko wa jimbo ambao kazi yake kubwa ni kuwasaidia wananchi kwenye vikundi vya ujasiliamali ili waweze kupata ustawi katika maisha yao
Mwisho