Diwani Mstaafu wa Kata ya Bombambili Golden Sanga( Sanga One)
Na Stephano Mango, Songea
KADA wa Chama cha Mapinduzi(Ccm) Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Golden Sanga (Sanga One) ametangaza nia ya kugombea Uwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Songea katika uchaguzi ambao unatarajiwa kufanyika mapema mwezi Septemba mwaka huu
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea Golden Sanga alisema kuwa ameamua kugombea nafasi hiyo ili kuweza kurudisha heshima ya Chama cha Mapinduzi mjini hapa
Sanga alisema kuwa kila kukicha mvuto wa Ccm miongoni mwa jamii umekuwa ukipungua kutokana na matendo maovu yasiyokuwa ya kimaadili yanayofanywa na Viongozi wa chama hicho ambayo yamekuwa yakiwakatisha tamaa wananchi na wanachama wa chama hicho
Alieleza kuwa kutokana na hali hiyo kumesababisha kata 6 kati ya 21 kuchukuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Urais wa mwaka 2010
Alieleza zaidi kuwa amejipanga kikamilifu kwa kushirikiana na viongozi wenzake watakaochaguliwa kushika nafasi mbalimbali ndani ya chama katika uchaguzi unaoendelea kufanyika mwaka huu ili kuweza kukijenga chama na kuleta ushindi stahiki katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa 2015
Kwa mujibu wa taarifa ya Chama cha Mapinduzi Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuwa wagombea wana haki ya kutangaza nia za kugombea nafasi wanazozitaka ndani ya chama ambapo kwa nafasi ya uwenyekiti wa Wilaya fomu zinatolewa agosti 1 na kurudishwa ndani ya siku mbili ambapo uchaguzi unatarajiwa kufanyika mapema septemba
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa waliotangaza nia hadi sasa ni Gerald Mhenga ambaye ni Katibu wa mipango na uchumi wa Ccm Wilaya ya Songea na Golden Sanga ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho ikiwemo udiwani wa kata ya Bombambili katika halmashauri hiyo
MWISHO