About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Thursday, September 29, 2011

WAJASIRIAMALI WATAKIWA KUTUMIA FURSA ZILIZOPO KUKUZA SHUGHULI ZAO

                    Na Stephano Mango,Songea
WAJASIRIAMALI wa mkoa wa Ruvuma wametakiwa kutumia rasilimali zilizopo mkoani humo katika shughuli zao ili ziweze kuwasaidia kuondokana na umasikini miongoni mwa jamii zinazowazunguka

Wito huo umetolewa jana kwenye viwanja vya NSSF na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Thomas Oley Sabaya wakati wa uzinduzi wa  mradi wa utafutaji wa masoko na uuzaji wa bidhaa kwa kutumia gari ya dhahabu iliyotolewa kwa wajasiriamali wa mkoa wa Ruvuma kwa ushirikiano wa Chemba ya Wafanyabiashara,Wenye Viwanda na Kilimo(TCCIA) na Wakorea chini ya mradi wa KOICA

Sabaya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Songea alisema kuwa Mkoa wa Ruvuma una hali ya hewa nzuri ambayo unaweza kuifanyia shughuli yoyote ile ya kijasiliamali hivyo wananchi wanapaswa waitumie fursa hiyo vizuri katika kukuza uchumi wao na wa jamii yote kiujumla

Alisema kuwa imebainika kuwa wajasiliamali ni muhimu sana katika kukuza uchumi endelevu wa nchi lakini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi ambazo tunapaswa kuziondoa ili waweze kuchangia kikamilifu uchumi wan chi yao

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Meneja wa Programu ya Wakorea wa Kujitolea Hwang,Jin Yun(Jenne) alisema kuwa mradi huo ni ushirikiano kati ya KOICA na TCCIA Ruvuma wenye dhumuni la kuimarisha mfumo wa utafutaji wa masoko na uuzaji bidhaa kwa kutumia gari katika mkoa wa Ruvuma

Jin Yung alisema kuwa KOICA kupitia Programu ya Korea ya marafiki wa kujitolea wa dunia ambao husambazwa sehemu mbalimbali husaidia kuijengea uwezo miradi midogo iliyopo kwenye taasisi wanazofanyia kazi

‘Katika mradi huu Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini kupitia Shirika la Kimataifa la maendeleo la Korea(KOICA) imetoa msaada wa dola za Kimarekani 29,550 ambapo TCCIA Mkoa wa Ruvuma imechangia dola za Kimarekani 650 katika kukamilisha mradi huu pia napenda kuushukuru uongozi wa TCCIA kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Jaehong Cho kwani bila yeye tusingeweza kufanikisha mradi huu”alisema Jin Yung

Awali Mwenyekiti wa TCCIA mkoa wa Ruvuma Mays Mkwembe akitoa utangulizi wa uzinduzi huo alisema kuwa kwa kushirikiana na KOICA tulifanikiwa kuibua mradi huu ambao unazinduriwa ukiwa na lengo la kuwasaidia wajasiliamali katika nyanza ya usafirishaji na uuzaji bidhaa mbalimbali ili ziwafikie wateja kwa urahisi na kwa muda muafaka

Mkwembe alisema kuwa mradi huu utasaidia kutatua changamoto zinazowakabili wajasiriamali kama vile tatizo la usafiri wa bidhaa kwa gharama kubwa pia bila kuwa na gari ya uhakika,tatizo la kutafuta masoko,kuvumisha na kutangaza bidhaa zao

Alifafanua kuwa kazi ya gari la dhahabu itakuwa ni usafirishaji wa bidhaa hadi kwenye soko ambapo muuzaji anahitaji,kuuza bidhaa mbalimbali katika gari,kutangaza na uvumishaji wa bidhaa mahali popote,maonyesho ya bidhaa kupitia gari,kutangaza shughuli mbalimbali za biashara,kukodisha gari kwa shuguli mbalimbali

 Mwenyekiti huyo alisema kuwa taasisi ya TCCIA ilianzishwa mwaka 1998 mkoani Ruvuma ambapo hadi sasa TCCIA iko katika mikoa yote 21 ya Tanzania Bara na kwamba ipo mbele katika kukuza na kuendeleza sekta binafsi katika mkoa wa Ruvuma

Mkwembe alisema kuwa kazi kubwa ya taasisi hiyo ni pamoja na utetezi na ushawishi katika kujenga mazingira vutivu ya kuendeleza sekta binafsi,kujenga mazingira ya mahusiano na majadiliano na Serikali katika kuendeleza dhana ya ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma

Alizitaja kazi nyingine kuwa ni utoaji wa taarifa za masoko na biashara mbalimbali kwa kupitia kituo cha taarifa,kutoa mafunzo mbalimbali ya kuendeleza biashara na ujasiriamali,utoaji wa hati ya uasili wa bidhaa
MWISHO




 Viongozi wa ngazi mbalimbali wa TCCIA Ruvuma wakifuatilia hotuba zilizokuwa zikitolewa kwenye uzinduzi huo
 Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Thomas Oley Sabaya akisikiliza hotuba iliyokuwa inatolewa na Meneja wa Programu ya Wakorea wa Kujitolea Hwang,Jin Yung(Jenne)katikati,wa kwanza kushoto ni Mtaalamu wa Masoko wa Kujitolea Jaehong Cho ambaye alikuwa mkalimani wa lugha ya Kikorea kwenda kiswahili
Afisa Biashara Mkoa wa Ruvuma Nehemia Jemes akipita mbele ya kikundi cha ngoma kilichotumbuiza wakati wa uzinduzi wa gari ya dhahabu

UZINDUZI WA MRADI WA UTAFUTAJI WA MASOKO NA UUZAJI BIDHAA NI MKOMBOZI WA WAJASILIAMALI

 Kikundi cha Mletere kikitumbuiza wageni na Wajasiriamali mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo ya uzinduzi wa gari ya dhahabu jana
 Wageni mbalimbali wakifuatilia kwa umakini hafla hiyo muhimu kwa wajasiliamali jana

Bidhaa ambazo zinazalishwa Tanzania na wajasiliamali wake zikiwa zimepangwa vizuri kwenye shelfu maalumu ili kuwawezesha washiriki kuangaria na kuzinunua ikiwa ni fahari kununua bidhaa zinazotengenezwa na wajasiliamali wa ndani

HALI TETE NDANI YA CCM,VIJANA WA CCM SONGEA WATISHIA KUKIMBILIA UPINZANI


                       Na Joseph Mwambije,Songea

VIJANA wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM) Mkoani  Ruvuma wamekitaka Chama hicho  kurejesha nguvu iliyokuwa nayo miaka ya 70 enzi ya Mwalimu Nyerere ya kuwachukulia hatua Viongozi wa Serikali wanaojihusisha na ufisadi vinginevyo watakihama na kwenda Upinzani.
 
Walitishia kukihama Chama hicho hivi karibuni kwenye Mkutano ulioitishwa kwa ajili ya kupata maoni yao ya namna ya kurejesha heshima yake na kujua  kwa nini Vijana wanakichukia Chama hicho kilichoshika dola.
 
Walitoa  kauli za kukitahadharisha Chama hicho mbele ya wajumbe wawili wa Baraza la vijana wa CCM  Taifa  ambao pia ni wajumbe wa kamati ya watu nane inayozunguka Nchi nzima kuchukua maoni ya vijana na kuyafanyia kazi kwa lengo la kurejesha heshima ya Chama hicho.
 
Mmoja wa Vijana hao ambaye anatoka kwenye kundi la vijana wasomi Razalo Komba alisema shida kubwa inayokipata Chama hicho inatokana namna ya watendaji wabovu wa Serikali ambao wanatumia vibaya madaraka yao ndani ya Serikali na kuwatendea vibaya wananchi.
 
Alisema kuwa wapinzani wameijengea chuki inayotokana na Viongozi wa juu wa Serikali kushindwa kutimiza wajibu wao na kufanya mambo kana kwamba hakuna utawala wa sheria hivyo wanajiona wao ni Miungu watu wanaoweza kufanya chochote bila kuguswa.
 
‘Kwa jinsi mambo yanavyokwenda inaonyesha dhahiri kwamba CCM haiwapendi wasomi na udhaifu huo wapinzani wameutumia na kuwateka wasomi na hivi sasa inaungwa mkono na wasomi wengi ambao wana uzalendo na Nchi yao ambao wanaona mambo yanakwenda ndivyo sivyo,kama mambo yatakwenda hivi yanavyokwenda hata mimi nitahamia  Upinzani’alisema.
 
Kijana mwingine  Amoni Mtega alisema Chama hicho kimepoteza mvuto mbele ya watu kwa kuwa kinashindwa kujibu hoja za Wapinzani hivyo akakitaka kujibu hoja hizo tena kwa wakati huku akisisitiza kwamba kwa kushindwa kuzijibu hoja hata kama ni za uongo wananchi wanayaaamini yanayosemwa.
 
Alisema kuwa vijana wamedharauliwa na kunyimwa fursa za maendeleo na ndio sababu wanakimbilia kwenye vyama vya upinzani ambavyo wanaviona kuwa mkombozi wao mpya badala ya Chama cha CCM.
 
Akizungumza mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo Joseph Mkilikiti  alisema maoni hayo watayafikisha kwenye Baraza kuu Taifa ambalo litapeleka kwenye uongozi wa juu wa Chama hicho ili yaweze  kufanyiwa kazi.

Mkutano huo ulitonosha vidonda vya makundi ya uchaguzi wa mwaka jana kati ya kambi za Oliver Mhaiki na ya Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Emanuel Nchimbi baada ya Vijana  wa kambi ya Nchimbi ambao walitokea upinzani kumsifia Mbunge huyo na kumponda Mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa CCM Songea Mjini Vikta Ngonyani ambaye hakuwa kambi ya Mbunge huyo kwamba hajasoma,hafanyi ziara kuwatembelea vijana na kwamba hawezi kukabiliana na siasa za sasa.
 
Akifunga mkutano huo huku akionekana kujibu hoja za vijana hao Mwenyekiti huyo wa vijana wa CCM Songea mjini alisema kuwa inashangazwa na maneno ya vijana hao kuwa bado hawajui taratibu za chama hicho kwani waliingia na kukuta ziara zimeshafanyika  hivyo amewataka watulie iliwajifunze na siku zijazo watapata uongozi ndani ya chama hicho.
 
Alisema vijana hao ndio waliosababishan CCM kupoteza Kata tano za Mjini kwa kuwa Mbunge alikuwa akiwatumia kufanya kampeni na badala ya kuomba kura wao walikuwa wakiwatukana wapiga kura hivyo wapiga kura waliwaadhibu kwa kuwachagua madiwani wa CHADEMA.
       MWISHO.  

CHADEMA KUMPINGA MEYA ANAYEDAIWA KUCHAKACHUA MATOKEO YA KITI HICHO TUKUFU

Na  Joseph Mwambije,Songea
CHAMA cha demokrasia na maendeleo(CHADEMA)Mkoani Ruvuma kimepanga kufanya maandamano makubwa ya kupinga uchaguzi wa Meya wa Manispaa ya Songea ulio mwezesha Charles Mhagama kuwa Mstahiki Meya anayedaiwa kuchaguliwa kwa kura za ndiyo 12 na za hapana 14 na kuweka kambi kwenye viwanja vya Manispaa.
 
Hayo yamebainishwa juzi na Mwenyekiti wa Chama hicho wa Mkoa wa Ruvuma Bw. Joseph Fuime wakati akiwahutubia maelfu ya wananchi wa Songea kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya msingi mfaranyaki.
 
Alisema kuwa sababu kubwa ya kufanya maandamano hayo ni kupinga uchaguzi huo uliofanyika bila kufuata taratibu na kwamba licha ya kuwa Halmashauri ya Manispaa Songea kuwa maskini lakini wamemchagua Meya aliyedai kuwa ni mwizi.
 
‘Wamemchagulia Meya aliyehusika na uuzaji wa greda kwa shilingi milioni18,ununuzi wa gari  bovu la Zimamoto kwa shilingi milioni 350 ambalo halifanyi kazi na huu ni mpango wa Wabunge kuweka watu wao ili waibe fedha’alisema na kuongeza
 
‘Mlifanya makosa makubwa kumchagua Nchimbi(Emanuel Nchimbi) na mngemchagua Mbogoro(Edson Mbogoro) kuwa  Mbunge wenu  tusingepata Meya mwizi na kama ingekuwa enzi ya Nyerere Nchimbi angejiuzulu anamtka Meya huyo ili amtumie kujinufaisha na tunatamka kuwa huyo si Meya wa wananchi ni Meya wa Mbunge na atapopita mitaani mumzomee’alisema.
 
Alimshambulia Mbunge wa jimbo la Songea Mjini  Emmanuel Nchimbi kuwa hana nia njema na wananchi wake na kwamba watakuwa tayari kutoa ushahidi kuwa kura ziliibwa na hivyo watapambana kwa kutumia  akili na busara na watashinda.
 
Alisema kuwa kabla ya kufanya maandamano hayo watazunguka kata 21 za Manispa ya Songea kufanya mikutano ya kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwenye  maandamano na kuanda vyakula na taa na kisha kuvigeuza viwanja vya Manispaa kuwa Viwanja vilivyomng’oa  madarakani aliyekuwa Rais wa Misri.
 
Hata hivyo  Bw. Mhagama alipoulizwa kuhusu tuhuma za kuhusika na ununuzi wa gari bovu la Zimamoto,uuzaji wa greda alisema yeye hausiki na tuhuma hizo kwa kuwa magari hayo yalinunuliwa saba Nchi nzima na kwamba greda liliuzwa kwa kufuata sheria zote.
 
Naye  katibu wa Jimbo la Songea Mjini Bw. Masumbuko Paul alisema kuwa Wabunge wa Mkoa wa Ruvuma wamekuwa mzigo kwa wananchi wao kwa kushindwa kuwatatulia matatizo yao kama tatizo kubwa la umeme na ajira kwa wananchi,alisema kuwa siku za CCM kukaa madarakani zinahesabika.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Songea Mjini Idd Abdalah alilaani kukihusisha CHADEMA na udini,ukabila  na urangi na kuwataka Waislamu kuondoa dhana hiyo na kuungana kuiondoa CCM madarakani huku akiwapongeza madiwani wa CCM waliopiga kura za hapana kwa Mhagama.
Mwisho
 




MGODI WA MAKAA YA MAWE WA NGAKA KUZALISHA UMEME MEGAWATTS 120

Na Joseph Mwambije,Songea
 
MGODI wa Makaa ya mawe wa Ngaka uliopo katika kijiji cha Ruanda , wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma utaanza kuzalisha Umeme kiasi cha megawatts 120 katika kipindi cha miaka miwili kuanzia sasa baada ya Kampuni ya TANCOAL Energy inayomiliki Mgodi huo kupata leseni ya biashara hiyo.
 
Shughuli za uchimbaji wa Makaa ya Mawe zilizozinduliwa rasmi hivi karibuni  na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Cyril Chami aliyeambatana na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo la Taifa NDC Dkt.Chrisant  Mzindakaya.
 
Mgodi huo wa Makaa ya mawe wa Ngaka, unamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania yenye asilimia 30, na kampuni ya Intra Energy ya Australia yenye hisa asilimia 70.
 
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri huyo wa Viwanda na Biashara  alisema mradi huo utaleta ukombozi mkubwa kwa Tanzania ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya kukosekana kwa nishati ya umeme wa kutosha.
 
“Ukikosa umeme maana yake viwanda haviwezi kufanya kazi, ajira zinapungua, wafanyabiashara wanaathirika na shughuli zingine za uzalishaji mali zinakwama” Alisema Dkt Chami.
 
Aidha Waziri huyo aliongeza kuwa Wizara yake itaunga mkono juhudi za kufanikisha mradi huo kwa kuwa inaamini utakua mkombozi wa Taifa katika kipindi kifupi kijacho.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TANCOAL Energy Bw. Graeme Robertson alisema kwa sasa mradi huo unazalisha tani 30,000 za makaa ya mawe kwa mwezi sawa na tani 360,000 kwa mwaka ambazo huzisambaza katika viwanda vya hapa nchini ikiwemo viwanda vya saruji vya Mbeya na Tanga.
 
Bw. Robertson alisema kwa kuanzia TANCOAL Energy itazalisha megawatts 120 za umeme katika kipindi cha miaka miwili kuanzia sasa, lakini uzalishaji huo utakua ukiongezeka hadi kufikia megawatts 2,000 kwa kuwa eneo hilo la Ngaka lina hifadhi kubwa ya makaa ya mawe inayozidi tani milioni 250 na kwamba utafiti unaoendelea unaonesha eneo hilo linaweza kuwa na hifadhi kubwa zaidi.
 
Aliongeza kuwa katika utekelezaji wa Mradi huo kampuni hiyo licha ya kuinufaisha Tanzania kwa nishati ya kutosha ya umeme, pia itahakikisha inaisaidia jamii kwa kutoa ajira na kununua bidhaa za kilimo zinazozalishwa na wananchi
 
Naye Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la Maendeleo la Taifa NDC Dkt.  Mzindakaya aliwaondoa shaka watanzania, akisema mradi huo una manufaa makubwa zaidi kwa Tanzania kuliko kwa mwekezaji.
 
Alisema kuwa Tanzania pamoja na kunufaika na umiliki wa kampuni ya TANCOAL Energy kwa asilimia 30 pia itanufaika na matokeo ya kuwepo kwa umeme wa kutosha ambao utaihakikishia ustawi wa viwanda, biashara na kilimo.
 
Mzindakaya pia alisema haina sababu kwa Taifa kulaumiana kwa kuchelewa kuitumia rasilimali hiyo na badala yake viongozi wachukue hatua ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
 
Mbunge huyo Mstaafu aliongeza kuwa wapo baadhi ya wanasiasa ambao wamekua wakinung’unika na kulaumu wakati wao wenyewe hawachukui hatua zozote za kuwasaidia wananchi.
 
“Hata huu mradi sio watu wote watauunga mkono, wapo watakaoupinga lakini sisi NDC tutasonga mbele” Alitamba Dkt Mzindakaya na kuongeza kuwa NDC na bodi yake hawawezi kuingia mkataba wa kijinga.
 
Katika hatua nyingine Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt Chami amekanusha vikali uvumi ulioenezwa kuwa Mradi wa Makaa ya mawe wa Ngaka unapanga kujenga mitambo ya kuzalisha umeme katika wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya badala ya Mbinga Mkoani Ruvuma.
 
Chami alisema uvumi huo hauna ukweli wowote na kwamba, mitambo hiyo itajengwa katika makutano ya Mto Ruhuhu na Mto Ngaka yaliyopo jirani na yanapochimbwa makaa hayo wilayani Mbinga.
 
Pamoja na kuzindua uchimbaji wa makaa hayo ya mawe alisema pia alikabidhi vyeti kwa wanafunzi wa shule ya msingi Mtunduwalo ambao wamefuzu majaribio ya kujifunza kazi za makaa ya mawe na pia amezindua madarasa matatu ya shule hiyo ya msingi ambayo yamejengwa kwa ufadhili wa kampuni ya TANCOAL Energy.
 
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la  Mbinga mashariki Bw. Gaudence Kayombo ambaye amekua chimbuko la Mradi huo alielezea furaha yake ya kuanzishwa kwa mradi huo na kutoa wito kwa wananchi wake kujipanga kuuza bidhaa za kilimo kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo pamoja na kuchangamkia fursa ya ajira
Mwisho