About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Thursday, February 23, 2012

ASKARI WANNE WAHOJIWA KWA KUSABABISHA MAUAJI YA WATU WATATU

 KAMANDA WA POLISI MKOA WA RUVUMA MICHAEL KAMUHANDA
 ASKARI WAKITULIZA GHASIA JANA
Mmoja wa marehemu aliyeuawa kwa kupigwa risasi na Polisi

Na, Stephano Mango ,Songea

VURUGU zilizojitokeza wakati wa maandano ya amani ya wananchi wenye hasira kali katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma zimesababisha hasara kubwa ya mali zenye thamani ambayo haikufahamika mara moja na kwamba katika sakata hilo Askari  Polisi wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuwapiga risasi za moto watu wawili ambao wamefariki kwenye maandamano hayo

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alisema kuwa hali ya mji kwa sasa hivi ni tulivu na hatua mbalimbali za kiusalama zinaendelea kuimarishwa ili wananchi waendelee na shughuli zao za kila siku

Kamuhanda alisema kuwa kwenye vurugu hizo watu 54 walikamatwa na wamefikishwa Mahakamani kujibu tuhuma za kufanya maandamano bila kibali na kusababisha uvunjifu wa amani katika maeneo mbalimbali ya mji wa Songea na vitongoji vyake

Alisema kuwa Askari Polisi waliohusika na kupiga risasi raia kwa sasa wanahojiwa na Jeshi hilo ili kupata uhalali wa kutumia risasi za moto katika tukio la maandamano yaliyofanyika jana na kwamba ikidhibitika kuwa walifanya uzembe watachukuliwa hatua za kisheria

Alieleza zaidi kuwa wananchi wakiwa kwenye maandamano hayo walivamia Ofisi za Chama cha Mapinduzi Manispaa ya Songea  na Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Vijijini walipiga mawe milango na kisha kuchoma bendera na kuleta hasara za mali nyingine za chama hicho, walivamia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Songea na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,walivamia  Ikulu ndogo walipiga mawe, walivamia Kituo cha Polisi na kupiga mawe na kuharibu baadhi ya magari ya wananchi

Alieleza kuwa waandamanaji walirusha mawe hovyo na kuwajeruhi wananchi wenzao, kufunga barabara kwa kutumia mawe makubwa, magogo na kuchoma mataili moto ili gari zinazoingia na kutoka nje ya mji zisiweze kuendelea na safari zake pia waandamanaji walivamia gari la Polisi na kuanza kurusha mawe na kusababisha Askari waanze kujihami kwa kurusha mabomu ya machozi

Alifafanua kuwa fujo hizo zinadaiwa kuwa zimetokana kwa sababu wananchi wamekuwa wakilalamikia matukio mfululizo wa mauaji mbalimbali likiwemo la mwendesha Pikipiki aliyeuawa februari 22 mwaka huu majira ya 2 asubuhi huko katika eneo la mto Matarawe, kuwa Jeshi la Polisi halichukui hatua ya kuwadhibiti wauaji hao

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Oley Sabaya alisema kuwa baada ya kutokea matukio hayo ameitisha viongozi wa Serikali za mitaa ya yote na kuwapa maagizo kuwa kuanzia sasa ulinzi shirikishi unatakiwa kuanza kwa kasi zaidi na kwamba kama kunawatu wanajihusisha na mambo ya uhalifu wajisalimishe haraka kwenye vyombo vya dola badala kusubiri wakamatwe

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amelaani kitendo kilichotokea juzi ambacho amesema sio cha kawaida hivyo kufuatia tukio hilo ameunda tume huru ya watu nane ambayo itafanya kazi ya siku saba ya kuchunguza kwa kina juu ya hali iliyojitokeza juzi mjini Songea na ripoti inapaswa kuwasilishwa arahamisi ijayo asubuhi ofisini kwake na kwamba hiyo tume inahusisha vyombo vyote vya dola

Baadhi ya wananchi wameiomba Serikali ichukue hatua za haraka kudhitibi hali iliyojitokeza juzi ambapo watu wawili waliuawa kwa kupigwa risasi na Polisi wakati wa wenye hasira kali walipokuwa wakipita mitaani kufanya vurugu huku wakidai kuwa Jeshi la Polisi limeshindwa kufanya kazi na mwingine kufa baada ya kutumbukia kwenye shimo na Pikipiki wakati wa vurugu hizo

 Wananchi hao ambao ni wakazi wa maeneo ya Mfaranyaki, Majengo, Bombambili na Mjini ambao wameomba majina yao yahifadhiwe walisema kuwa hali iliyojitokeza juzi haikuwa ya kawaida hivyo ni vyema Serikali ikatafuta njia muafaka ya kudhibiti chanzo cha vurugu badala ya kujishughulisha na kuzuia maandamano ya amani ya wananchi na kwamba thamani yake haikuweza kufahamika mara moja

MWISHO

MTOTO MCHANGA AOKOTWA NA MSAMALIA MWEMA AKILIA MSITUNI

Na,Steven Augustino,Tunduru

MTOTO mchanga anayekadiliwa kuwa na umri wa wiki moja au mbili kameokotwa baada ya kutelekezwa na mama yake mzazi na kukomea kusiko julikana

Taarifa kutoka kwa msamalia mwema aliyemuokota kichanga hicho Halima
Chalamanda alisema kuwa kabla ya tukio hilo alisikia Sauti ikitokea
katika vichaka vya Msitu uliokuwa kambi iliyofungwa ya Jeshi la Wananchi wa JWTZ wakati akielekea Shambani katika kijiji cha Namsalau.

Alisema kuwa baada ya kusikiliza kwa makini aligundua kuwa sauti ya kitoto
hicho ikitokea vichakani  hali iliyo msukuma kuingia katika msitu huo na kumkuta akiwa peke yake na kuamua kumchukua.

Chalamanda aliendelea kufafanua kuwa baada ya kumuokota mtoto huyo alichukua uamuzi wa kumpeleka katika Kituo kikuu cha Polisi kilichopo Mjini hapa na baadae akaelekezwa kumpeleka katika Hospitali ya Serikali ya Wilaya hiyo kwa ajili ya uchunguzi.

Akizungumzia hali ya  Mtoto huyo, Mganga wa Hospitali ya Serikali ya Wilaya hiyo Dkt. Goerge Chiwangu alisema kuwa hali ya mtoto huyo ilikuwa ni dhaifu sana lakini baada ya Msamalia huyo ambaye pia
analea Mtoto mchanga kumsaidia kwa kumnyonyesha Maziwa na kupatiwa hudumu za matibabu hali yake imeendelea kuimarika.

Alisema baada ya uchunguzi pia maafisa tabibu waligundua kuwepo kwa vidonda sehemu mbalimbali za mwili wake vilivyo sababishwa na  kukaa polini kwa muda mrefu hali iliyo wafanya wadudu kuanza kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake.

Dkt. Chiwangu alieendelea kueleza kuwa kutokana na mtoto huyo kukosa mtu ayemtambua ofisi yake kwa kusaidiana na idara ya Ustawi wa Jamii
Wilayani humo wanampango wa kumpeleka katika Kituo cha Kulelea Watoto
Yatima kilichopo katika Hospitali ya Missioni ya Mbesa ili alelewe
huko na Watoto wengine.

Wakiongea kwa nyakati tofauti Afisa ustawi wa jamii wa Wilaya hiyo
Alto Philipo na Mlezi wa Watoto yatima Katika Kituo cha Mbesa Mchungaji Ignas Nchimbi walisema kuwa hilo ni tukio la kwanza la mama kutupa mtoto mchanga Wilayani humo toka Kituo cha kulelea Watoto yatima kifunguliwe mwaka 1960.

Akizungumzia hali ya Watoto wanao lelewa katika kitu hicho Mchungaji Nchimbi alisema kuwa kituo hicho chenye Watoto 27, kichanga hicho kitakuwa cha 28 na kwamba hali ya kituo ni nzuri.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda mbali na kuthibitisha kuwepo kwa tukio hilo amesema kuwa jeshi hilo linaendelea na uchunguzi na kwamba sheria itafuta mkondo wake endapo mtuhumiwa atabainika.

Mwisho